Mkimbizi

Hussein Tuwa

Naitwa Tigga Mumba.Marafiki zangu walizoea kuniita Tigga-Mu…lakini sasa sina marafiki tena. Mimi ni mtafiti wa mambo ya kale…lakini nadhani niseme kuwa nilikuwa mtafiti wa mambo ya kale…Archaelogist.

Nilikuwa ni mtu mwenye matarajio makubwa kabisa katika maisha. Nikiwa na shahada yangu ya kwanza ya utafiti wa mambo ya kale kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, marafiki wachache lakini wazuri na wacheshi,mchumba mtanashati niliyekuwa natarajia kufunga naye ndoa itakayojaa upendo nikiwa na ndoto ya kuzaa naye watoto wawili: wa kwanza wa kike na wa pili wa kiume, pamoja na jamii yangu ndogo iliyojaa upendo. Sikuwa na sababu ya kukosa matarajio makubwa katika maisha.

Lakini vyote hivi vilikuja kutoweka ghafla katika tukio moja tu la kutisha na kuogopesha sana lililotokea katikati ya msitu mnene ulioko katikati ya nchi hii…siku moja nilikuwa msichana mmoja mcheshi wa miaka ishirini na saba, mrembo wa kuridhisha mwenye ndoto nyingi za mafanikio mbele yangu, siku iliyofuata  vyote hivi viligeuka na kuwa ndoto moja mbaya na ya kutisha sana. Ila tu mambo yaliyobadilisha matarajio na maisha yangu hayakuwa ndoto bali ni kweli kabisa!

Ni vigumu sana kuamini kuwa mambo yaliyonitokea…na yanayoendelea kunitokea, yananitokea mimi. Na kibaya zaidi ni kuwa pamoja na kuniwia vigumu sana mimi kuamini kuwa ninatokewa na mambo haya, bado najikuta kuwa ni mimi peke yangu ndiye ninayeamini ukweli wa matukio haya ya kutisha. Kwa sababu kila ninapokwenda, kila ninapojaribu kuelezea ukweli wa matukio haya, hakuna hata mmoja anayeniamini…na naishia kuwa mkimbizi ninayekimbia kwa woga na wasiwasi.

Na kama hiyo haitoshi, kibaya kuliko vyote ni kwamba kwa mtu niliyekuwa na marafiki, jamaa na hata mchumba wa dhati, najikuta kuwa nalazimika kukabiliana ma masahibu haya peke yangu.

Yote hii ni kwa sababu ya kushuhudia tukio moja la kutisha katikati ya msitu mnene.

Tukio lililonifanya niwe mkimbizi ndani ya nchi yangu…kwa sababu sasa sina mahala popote ambapo ninaweza kujihisi salama, sina mtu yeyote ambaye nitajihisi kuwa salama kwake, hakuna mazingira yoyote yanayoweza kunifanya nijihisi salama.

Mahala pekee ambapo nitajihisi salama ni pale nitakapokuwa peke yangu…na mtu pekee nitakayejihisi salama kuwa naye ni mimi mwenyewe! Na mpaka nitakapoipata hiyo sehemu ya peke yangu, nitabaki kuwa mkimbizi tu…peke yangu, mpweke!

Na hata hapa ninapoandika maelezo haya ya tukio la kutisha lililobadilisha kabisa maisha yangu na mtazamo wangu katika maisha kwa ujumla, niko peke yangu.

Nikiwa na mtu pekee ninayemuamini katika maisha yangu…Tigga Mumba.

Peke yangu.

Niliyejawa woga.

Nisiye na kwangu.

Mkimbizi…

SEHEMU YA KWANZA: MAUAJI

Ulikuwa ni msafara wa watu watano, watatu kati yao, pamoja na mimi mwenyewe, tukiwa ni waajiriwa wa Idara ya Makumbusho ya Taifa kitengo cha utafiti wa masalia ya kale. Wa nne alikuwa ni mpiga picha binafsi aliyeajiriwa kwa muda na Idara ya Makumbusho ya Taifa mahususi kwa shughuli iliyozaa msafara huu; wakati mtu wa tano alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyekuwa anafanya utafiti kwa ajili ya shahada yake ya pili pale Mlimani.

Alikuwa anafanya utafiti juu ya masalia adimu ya viumbe vya zama za mwisho za mawe nchini Tanzania, utafiti ambao ulisawiri kabisa dhumuni la msafara wetu.

Kutoka katika Idara ya Makumbusho ya Taifa alikuwepo mtafiti wa mambo ya kale mwandamizi (ambaye ni mimi), mtafiti mkuu wa mambo ya kale aliyeitwa Ibrahim Geresha,ambaye ndiye alikuwa mkuu wa msafara na mkuu wangu wa kazi; pamoja na dereva wetu ambaye tangu niajiriwe katika Idara ile ya Makumbusho ya Taifa nimekuwa nikimjua kwa jina moja tu la Beka.

Mpiga picha wetu katika msafara huu alikuwa anaitwa Gilbert Kyaro, ambaye alipendelea zaidi kuitwa Gil, na alikuwa akipenda sana kusikiliza na kuimba nyimbo za mwanamuziki wa zamani, Johnny Gil.Nadhani ndicho kitu kilichomfanya naye ajisikie kuitwa Gil.

Wakati gharama zote zilizotuhusu katika msafara huu zilikuwa zikilipwa na idara ya Makumbusho ya Taifa, zile za bwana Ubwa Mgaya, kama nilivyokuja kumjua jina lake hapo baadaye, zilikuwa zikilipwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama sehemu ya fungu lake la utafiti.

Wakati Toyota Landcruiser ikitupeleka kwa kasi kuelekea kwenye eneo la tukio, nilikuwa na matarajio kuwa na hii itakuwa ni safari nyingine ya kuvutia na kunufaisha kama nilivyozoea. Sikuwa na sababu ya kutarajia vinginevyo.

Nikiwa nimehitimu kwa mafanikio makubwa mafunzo yangu ya shahada ya kwanza ya Utafiti wa mambo ya kale (Bachelor’s Degree in Archaelogy) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka mmoja uliopita, nilijihisi kuwa mwenye bahati sana kuweza kuajiriwa na Idara hii ya Makumbusho ya Taifa kiasi cha mwezi mmoja tu baada ya kusherehekea kupata kwangu digrii hii adimu, nikiwa naelewa fika jinsi kazi zilivyokuwa ngumu kupatikana hapa nchini hata kwa wahitimu wa vyuo vikuu. Lakini nadhani hii ilitokana na fani niliyochagua kusomea, kwani ni fani ambayo haina upinzani mkubwa hasa hapa nchini.

Marafiki zangu wengi walinishangaa kutokana na uamuzi wangu wa kusomea fani hii, lakini kwa wakati ule nilikuwa nimo ndani ya penzi zito la Profesa mmoja kijana wa pale Chuo Kikuu ambaye alinishawishi kuchagua fani hiyo akidai kuwa ilikuwa ina nafasi nyingi za kwenda kujiendeleza nje ya nchi.

Nilipofika mwaka wa pili nikamfumania mpenzi wangu huyo nyumbani kwake, akifanya mapenzi na mwanafunzi mwenzangu ambaye nilikuwa nikiishi naye chumba kimoja pale chuoni, tena sakafuni jikoni kwake wakiwa kama walivyozaliwa. Nilichofanya ni kuwamwagia maji ya baridi kutoka kwenye jokofu lililokuwa pale jikoni na kuwaacha wakitapa tapa pale sakafuni nami nikashika hamsini zangu. Matokeo yake penzi la Profesa kijana likafa pamoja na ahadi ya kutoka nje ya nchi kwa masomo zaidi katika fani ya utafiti wa mambo ya kale.

Hapo tena ilikuwa haiwezekani kubadilisha masomo, hivyo nikaendelea tu na fani hiyo hiyo.

Baada ya kile kituko cha jikoni kwa Profesa kijana, nilibadilishana chumba na msichana mwingine.Nikahamia chumba kingine ambapo nililazimika kuishi na msichana wa kipemba aliyekuwa akiswali sala tano kila siku, kitu kilichoonekana kumkera yule msichana aliyekuwa akiishi naye awali.Kwangu hili halikuwa tatizo.

Lakini pamoja na upumbavu wake, Profesa kijana hakukosea, kwani nilipata ajira haraka sana baada ya kumaliza masomo yangu, na baada ya mwaka mmoja wa ajira kwenye Idara ya Makumbusho ya Taifa nimekuja kuona kuwa hii hasa ndiyo fani inayonifaa kwani iliniweka njiani muda mwingi kwa safari kuelekea sehemu mbalimbali nchini kufanya tafiti nyingi za mambo ya kale na kukusanya mabaki ya kale kwa kuchunguzwa kitaalamu zaidi makao makuu ya idara, Dar es Salaam.

Ila kilichonipendeza zaidi kwenye kazi yangu hii ni pesa. Kwanza mshahara niliokuwa nikipokea ulikuwa ni mzuri sana, hasa kwa mtu niliyetoka chuoni kama mimi, ambaye hapo nyuma nimekuwa nikishambuliwa na FFU mara kadhaa nikiwa katika maandamano na migomo kugombea kuongezewa posho isiyotosheleza chochote wakati nipo chuoni. Zaidi ya hapo kulikuwa kuna posho nyingi zinazotokana na safari kama hizi za kikazi, ambazo huwa tunaziita per diem.

Na hivyo wakati mabaki ya kiumbe kisichojulikana yalipogunduliwa wiki chache zilizopita katika msitu fulani huko Manyoni katikati ya kanda ya kati ya Tanzania, kwa mara nyingine tena nikajikuta nikiwa safarini.

Manyoni Expedition,  au ‘Msafara wa Manyoni’ kama msafara wetu huu ulivyojulikana, ulikuwa ni msafara wa awali, uliotarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja ambapo iwapo baada ya hapo ingethibitika kuwa kile kilichogundulika huko Manyoni ni kweli kilikuwa mabaki ya kiumbe hai wa kale, basi ungekuwa ni mradi mahususi ambao ungeweza kudumu kwa kadiri ya muda ambao ungehitajika kuukamilisha. Na ikifikia hapo ndipo ningekuwa nazivuna per diem kama sina akili vizuri na wakati huohuo nikifanya kazi ninayoipenda.

Nikiwa nimetulia ndani ya Toyota Land Cruiser kuelekea Manyoni kupitia Dodoma, nilijifariji kuwa baada ya misukosuko na maisha magumu niliyolazimika kupitia wakati nikitafuta digrii yangu pale Mlimani, sasa nilikuwa nafaidi nyakati nzuri kabisa katika maisha yangu.

Nyakati nzuri sana.

Nilisahau kabisa msemo tuliowahi kuambiwa na mhadhiri mmoja wakati tuko chuoni kuwa “Ni nyakati nzuri kabisa katika maisha ya binadamu ndizo zinazobadilika na kuwa nyakati mbaya kabisa bila ya kutarajia…”

It is always the very good times of one’s life that normally turns into one’s very bad times in no time

Ni kwamba kama mtu akiwa katika maisha mabovu hakuna kibovu zaidi kitakachomkuta zaidi ya hicho, lakini akiwa kwenye maisha mazuri ndio ataona mabadiliko pale hali hiyo itakapotoweka.Na kwa kawaida maisha mazuri huwa hayadumu. Kwa wakati ule nilimuelewa sana mhadhiri yule, halafu nikasahau kabisa juu ya ukweli ule.

Sikuwa na sababu ya kuukumbuka tena, kwani tayari nilikuwa nimeshaingia kwenye raha ya maisha mazuri…mpaka pale yalipokuja kunigeuka.

Tulisafiri kwa saa sita mpaka Dodoma, ambapo tulilala kwenye hoteli moja ya bei nafuu kubania pesa zetu za safari kwa makubaliano kuwa tungeaza sehemu ya pili ya safari yetu asubuhi ya siku iliyofuata ili kukwepa jua kali libabualo, la nusu jangwa.

Asubuhi ya siku iliyofuata, nikiwa msichana pekee kwenye msafara ule, nilijiweka vizuri kwenye kiti changu cha dirishani nyuma ya kiti cha dereva na safari yetu kuelekea Manyoni ikaanza. Nilipachika visikilizio masikioni na kuanza kusikiliza muziki wa Bongo Flava kutoka kwenye Walkman yangu ya CD na kuwaacha wasafiri wenzangu wakiburudika na muziki wao wa mayenu kutoka kwenye redio ya gari.

Kadiri safari ilipoendelea huku Land Cruiser ikienda kwa kasi kupitia kwenye njia za vumbi na kona nyingi kuelekea kwenye lengo la safari yetu nikabaini kuwa bwana Ubwa Mgaya wa Chuo Kikuu alikuwa akinitupia macho ya mara kwa mara, jambo ambalo lilianza kunikera.

Nikavaa miwani yangu ya jua na kuamua kuangalia nje ya dirisha.

Ilikuwa jioni sana tulipoingia Manyoni mjini.Tulikubaliana kupata malazi katika nyumba yoyote ya wageni tutakayoiona, ambayo ilitokea kuwa ni nyumba kubwa ya vyuma sita isiyokuwa na umeme, ikiwa na choo cha shimo ambacho pia hutumika kama bafu, na mama mwenye nyumba mcheshi sana. Ilibidi tufanye zamu kutumia choo na bafu na kwa msisitizo wa bwana Ubwa Mgaya nikapewa nafasi ya kuwa wa kwanza kutumia huduma hiyo. Nilipotoka bafuni nikajibwaga kitandani chumbani kwangu kwa lengo la kujipumzisha kabla ya kupata mlo wa jioni, lakini nilipofumbua macho ilikuwa alfajiri ya siku iliyofuata.

Kama jinsi taratibu zinavyotaka, tuliripoti ofisini kwa mkuu wa wilaya, ambaye alitokea kuwa ni mwanamke wa makamu mwenye sura ya kuvutia na tabasamu la kutia moyo. Kwa kuwa alikuwa ana taarifa ya ujio wetu, hatukupoteza muda pale ofisini kwake. Baada ya mkuu wa msafara bwana Ibrahim Geresha kututambulisha na mpiga picha wetu Gilbert “Gil” Kyaro kutupiga picha ya pamoja tukiwa na mkuu wa wilaya, tulipewa wenyeji wawili kutoka kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ambao ndio wangetuongoza kuelekea huko kulipoonekana hayo mabaki ya kiumbe cha kale kisichojulikana.

Kwa mara nyingine tena tukaingia kwenye Land Cruiser yetu na safari ya kuelekea msituni ikaanza, tukiwa tuna watu wawili zaidi na zana zetu za kazi zilizojumuisha mahema, machepeo maalum, vifaa vya kupikia, chakula cha kuweza kutosha kwa wiki nzima na mabegi yetu binafsi. Tukiwa njiani nilianza urafiki na mpiga picha wetu Gil huku nikibaini kuwa bwana Ubwa Mgaya sasa hakuwa akinitupia macho ya wizi tena bali alikuwa akinikodolea macho waziwazi kama mvulana ambaye amebaleghe halafu akamwona msichana wa ndoto zake.

Niliamua kutomtilia maanani na kujaribu kuelekeza akili yangu kwenye kazi iliyopo mbele yetu.

Laiti ningejua kilichokuwa kikitusubiri huko mbele…

--

Haikuwa mpaka siku yetu ya tatu kule msituni ndipo tulipofanikiwa kufanya ugunduzi tulioukusudia. Ugunduzi wa masalia ya kiumbe hicho cha kale yaligundulika umbali wa kilometa zipatazo mbili kutoka eneo ambalo masalia hayo yalionekana kwa mara ya kwanza na wachimba madini walioshindwa kufanikiwa kupata madini waliyoyakusudia na badala yake wakaambulia kufukua mabaki ya kiumbe hicho.

Zilikuwa ni siku tatu za kazi ngumu lakini ya kufurahisha, kwani tulikuwa tukicheka na kutaniana huku tukichimba na kutambaa ardhini tukipima aina za udongo na kulinganisha na aina ya mabaki yaliyogunduliwa hapo awali.

Tulichimbua aina mbalimbali za mifupa na kujaribu kuipima kitaalam kugundua aina ya kiumbe kilichobakiza mifupa hiyo.Wakati tukiwa katika harakati zetu hizo, Gil naye alikuwa katika harakati za kupiga picha vitu tulivyokuwa tunavichimbua kutoka ardhini na sisi wenyewe tukiwa katika pozi mbalimbali za kazi.

Alikuwa anatumia kamera ndogo aina ya Sony ambayo ilinivutia sana. Akanielekeza ni wapi ningeweza kuipata nami nikaweka dhamira kuwa nikirudi tu ustaarabuni nitainunua. Ilikuwa ni kamera iliyoweza kupiga picha za video na wakati huohuo kupiga picha za kawaida. Wakati wa kupiga picha za video, mtumiaji hakutakiwa kuiweka jichoni mwake muda wote, kwani ilikuwa ina kijiruninga kidogo pembeni ambacho mtumiaji aliweza kuwaona watu aliokuwa akiwapiga picha kupitia pale kwenye hicho kijiruninga. Kwa hakika ilinivutia sana na mara kadhaa nilipokuwa najipumzisha katikati ya kazi, Gil alikuwa akinielekeza namna ya kuitumia, na nilivutiwa zaidi na mikanda yake ya kurekodia picha za video ambayo ilikuwa midogo sana kuliko hata ile mikanda ya kaseti za redio.

Nyakati za jioni tulipenda kukaa kuzunguka moto na kupata mlo ambao mimi nilijitolea kuwa nawapikia wenzangu, na kuongea juu ya mambo mbalimbali kabla ya kila mtu kuingia kwenye hema lake kulala. Ni katika nyakati hizi za jioni baada ya kazi wakati siku moja bwana Ubwa Mgaya aliponiuliza iwapo nilikuwa nimeolewa, wakati huu ikiwa tumezoeana kidogo. Nilimjibu kwa kumwonesha pete yangu ya uchumba ambayo ilikuwa kidoleni mwangu.

“Oh! Aa-OkayI mean, Hongera sana…”  Alijibu kinyonge huku akionesha wazi kuwa alikuwa amekatishwa tamaa.

Nikamshukuru kana kwamba sikuelewa kitu.

--

Ilipofika siku ya nne ilikuwa tayari imethibitika kuwa ‘Manyoni Expedition’ ilikuwa imefanikiwa, kwani tuligundua mabaki mengi sana yaliyofanana na yale yaliyogundulika hapo awali ambayo hata hivyo hatukuwa na namna ya kujua ni ya kiumbe wa aina gani mpaka hapo tutakapoyafikisha Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi. Kwa hali hii, mapema siku iliyofuata tulianza kufungasha virago vyetu tayari kwa safari yetu ya kurudi Dar.

Hivyo, wakati wenzangu wanafungasha mahema na vifaa vyetu vya kazi na kupikia, nilimwomba Gil kamera yake ili nijifurahishe kwa kupiga picha mbalimbali za wanyama wadogowadogo pale porini ambao walikuwa wengi. Gil alitoa mkanda wa video aliokuwa amerekodi picha zetu za kazi na akaniwekea mkanda mwingine.

“Haya nenda kachezee huo.” Alisema kwa utani na sote tulicheka. Nilichukua ile kamera na kukimbia porini zaidi kutafuta wanyama wa kuwapiga picha.

“Msiniache jamani eenh!” Niliwapigia kelele wenzangu.

“We’ ukisikia honi ujue safari iko tayari!” Ibrahim Geresha alinipigia kelele. Nami nikamnyooshea ishara ya dole gumba kumuashiria kuwa nimemuelewa.

Nikaona kundi la tumbiri ambalo lilinivutia na nikaanza kuwapiga picha wakiruka kutoka tawi moja la mti kwenda lingine kwa kutumia ile kamera ya Gil. Mara nikaona digidigi wakikimbizana nami nikawageukia wao na kamera yangu. Nilikuwa najisikia raha sana. Muda si mrefu likapita kundi kubwa la nyani wakubwa sana ambao kidogo walinitisha kwani nilisikia kuwa nyani wa aina hii huwa wakiona mwanamke msituni lazima wambake. Hivyo nilijificha kwenye kichaka huku nikiwapiga picha za video hadi walipopotea.

Nilijitoa kutoka kwenye kichaka nilichokuwa nimejificha na kuanza kurudi kwa wenzangu taratibu huku nikiangaza huku na huko kutafuta viumbe vingine vya kuvutia wakati ghafla niliposikia mngurumo kama wa ndege kwa mbali lakini ukizidi kuja karibu kila sekunde.

Nilitazama juu lakini sikuona kitu kutokana na matawi ya miti yaliliyojishona sana juu yangu. Niliongeza mwendo kurudi kwa wenzangu, lakini ile sauti ilikuwa inaongezeka na hata kuanza kupeperusha matawi ya miti iliyokuwa karibu kwa upepo nami nikawa na hakika kabisa kuwa ule ulikuwa ni mngurumo wa helikopta. Nilitazama huku na huko nikijaribu kuitafuta ile helikopta bila mafanikio.

Nikaamua kukimbilia  kwa wenzangu lakini hapo ndipo ghafla nilipoona helikopta ikijitokeza juu ya uzio wa vilele vya miti iliyokuwa ikinikinga. Bila ya kujua ni kwa nini au ni kitu gani kilichonifanya nichukue hatua hiyo, nilijibanza haraka nyuma ya mti na kuanza kuitazama ile helikopta kubwa wakati ikizunguka kwa madaha mara mbili juu ya eneo lile kabla ya kuanza kuteremka taratibu na kwa makelele kwenye ukingo wa msitu ambako katika kuranda randa kwangu sikuweza kufika. Nilijiuliza ile helikopta itakuwa inatafuta nini kule porini katika muda ule. Kwa siku zote nne tulizokuwa tumepiga kambi pale msituni hatukuona harakati zozote za binadamu isipokuwa zile za kwetu tu, ambazo zilikuwa ni za muda tu, hivyo wote tulikubaliana kuwa eneo lile halikuwa na harakati nyingi zaidi ya zile za tumbiri na digidigi.

Niliitazama kwa makini zaidi ile helikopta. Ilikuwa ni sawa na zile za kijeshi ambazo huwa zina sehemu ya rubani yenye vioo wakati sehemu yake ya katikati iko wazi kiasi kwamba kama mtu hauko makini unaweza kuanguka kutoka huko juu.Ilikuwa ina rangi ya kijivu iliyochakaa na haikuwa na alama yoyote ya kuitambulisha iwapo ilikuwa ni helikopta ya polisi, jeshi au msalaba mwekundu.

Niligeukia kule ambako tulikuwa tumeweka kambi yetu.Nikasikia sauti za akina Ibrahim Geresha na Gil zikielekea kule ilipokuwa ile helikopta.Nilitazama tena kule ambako ile helikopta ilikuwa inatua lakini sasa ilikuwa imeshapotelea nyuma ya uzio wa ile miti mirefu. Mara nikamwona mmoja kati ya wale wenyeji wawili tuliopewa na ofisi ya mkuu wa wilaya akikimbia kuelekea kule ilipopotelea ile helikopta. Alinipita bila ya kuniona kiasi cha hatua kama ishirini hivi kushoto kwangu. Nilisita kidogo tu, kisha kutokea pale nilipokuwa, nikaanza kukimbia sambamba na yule mwenyeji kuelekea kule ilipokuwa ile helikopta huku nikijiuliza ni nini kilikuwa kinatokea.

Nilipofika kwenye ukingo wa ule msitu  niligundua kuwa palikuwa pana bonde dogo lililoishia kwenye ukanda wa michanga, kana kwamba zamani kulikuwa kunapita mto mpana lakini sasa umekauka. Na hata pale nilipokuwa nikilitazama lile dege kubwa likishuka kwa madaha, niliweza kuona watu wawili wakiwa wamekaa katika lile eneo la wazi wakiwa wamejifunga mikanda maalum ya kuwazuia wasianguke.

Lile dege lilitua ardhini huku likitimua vumbi, nami nikabaki nachungulia nikiwa kwenye ukingo wa msitu lakini nikichukua tahadhari ya kutoonekana..Nikiwa nimelalia tumbo pale kwenye ukingo wa msitu, nilijaribu kufinya macho ili nione vizuri kule kwenye helikopta, na kwa muda sikuona kitu kutokana na vumbi lililotimuliwa na upepo wa mapangaboi ya dege lile.

Kutoka pale nilipolala, ile helikopta ilikuwa umbali wa kama mita arobaini na kwa chini kidogo kiasi kwamba nilikuwa naitazama kutokea juu kidogo. Bado vumbi lilikuwa likitua taratibu sana hivyo kuona ilikuwa vigumu lakini tayari moyo ulikuwa umeanza kuniingia wasiwasi. Nilitazama kushoto kwangu ambapo nilitegemea kuwaona akina Ibrahim Geresha na Gil wakitokea lakini sikuwaona.Niligeuka tena kule kwenye ile helikopta na safari hii niliona watu wawili wakiwa wamevaa makoti marefu meusi wakiwa wamesimama nje ya ile helikopta wakiangaza huku na kule, wakati mtu mwingine wa tatu akiteremka kutoka kwenye ile helikopta.

Sikuweza kuwaona vizuri wale watu lakini mara moja niligundua kuwa yule aliyeteremka mwisho kutoka kwenye ile helikopta alikuwa akitembea kwa kuchechemea kidogo, kana kwamba alikuwa na ulemavu wa mguu mmoja, na akitembelea mkongojo..

Ni watu gani hawa?

Wale watu waliongea kwa muda kisha yule mwenye mguu mbovu alionekana kutoa amri fulani na wale wawili wa mwanzo walirudi ndani ya ile helikopta.Bado nikiwa na mawazo kuwa kulikuwa kuna jambo baya lililokuwa mbioni kutokea, niligeuka tena kushoto kwangu kujaribu kuwatazama wenzangu.

Hakuna mtu.

Nikageuka tena kwenye helikopta. Wale watu wawili walioingia tena kwenye ile helikopta walitoka wakiwa wanamburura mtu mwingine ambaye alikuwa kifua wazi! Wazo la kwanza kupita kichwani mwangu lilikuwa ni kwamba yule mtu aliyekuwa anabururwa alikuwa mgonjwa, lakini wazo hilo lilifutika haraka kichwani mwangu na nafasi yake ikachukuliwa na woga na hofu kubwa pale niliposhuhudia yule mtu aliyekuwa akibururwa akisukumwa ardhini kikatili na kugaragara vibaya sana kwenye

vumbi na michanga huku akitoa yowe ambalo nililisikia waziwazi kuwa ni la uchungu.

Nilitaka kupiga kelele lakini nilijizuia na kabla sijajua nifanye nini, moyo ulinilipuka na kihoro kikanitawala pale nilipowaona Ibrahim Geresha na Gilbert ‘Gil’ Kyaro wakiteremka kibonde kwa kasi kuelekea pale kwenye helikopta katika wakati ule ule ambapo lile tendo la kusukumwa ardhini yule mtu asiye na shati likitokea. Wote wawili walisimama ghafla walipoona tendo lile na kwa sekunde chache hakuna kilichotokea wakati wale watu wenye makoti marefu wakiwatazama akina Ibrahim na akina Ibrahim wakijaribu kuelewa walichokiona.

Mara wale watu waliwazingira wale wenzangu huku wakiwaongelesha na kuwanyooshea bastola! Mwili uliniisha nguvu. Sijawahi kuona bastola hata siku moja ukiachilia mbali kwenye sinema, kwa hiyo yaliyotokea pale chini yalikuwa ni mambo ya kutisha sana kwangu.

Sijui ni nini kilichoniongoza kufanya nilichokifanya, lakini sasa nikikaa na kufikiri, nadhani nilichokifanya kilitokea bila ya mwenyewe kufikiri.Ni jambo ambalo unaloweza kusema mtu kalifanya in a spur of a moment – tendo linalofanyika kutokana na hali fulani kwa wakati fulani bila ya mtendaji kupata muda wa kufikiri. Mara nyingi tendo kama hili huwa ni la athari kwa mtendaji, kama vile mtu anaweza kumpiga mtu na silaha fulani in a spur ofa moment bila ya kufikiri halafu akamuua,jambo ambalo kama angepata muda wa kulifikiria asingelifanya. Na jambo nililolifanya lilikuja kuniletea madhara na madhila makubwa sana maishani mwangu.

Nilipoona wale watu wamewaelekezea bastola akina Gil tu hapo hapo niliinua ile kamera iliyokuwa mikononi mwangu na kuanza kurekodi matukio yale. Hilo ndilo jambo nililolifanya na ambalo sijui ni kwa nini nililifanya, kwani wakati nalifanya nilikuwa nimetawaliwa na woga wa hali ya juu.

Sikuweza kusikia yaliyokuwa yakisemwa kule chini lakini kadiri nilivyokuwa nikiliangalia lile tukio kutoka kwenye kijiruninga kidogo cha kwenye ile kamera yenye nguvu, sikuwa na shaka hata kidogo juu ya kilichokuwa kinaelekea kuwatokea watafiti wenzangu kule chini na hapo hapo moyo ulininyong’onyea. Wale ni watu ninaowafahamu na walikuwa wanaelekea kuuawa na sikuwa na lolote nililoweza kufanya kuwasaidia bila ya mimi mwenyewe kujiongezea kwenye orodha ya watakaouawa.

Yule mtu mwenye mguu mbovu aliwasogelea akina Ibrahim taratibu wakati mwingine akiwalengeshea bastola, ilhali yule wa tatu akiwa amemkanyaga mgongoni yule mtu aliyebururwa kutoka kwenye helikopta aliyelala kifudifudi mchangani.

Kufikia hapa moyo wangu ulikuwa ukipiga kwa kasi sana na akili yangu ilikuwa ikizunguka bila mwelekeo maalum na sikupata wazo lolote la kusaidia katika hali ile.Nikabaki nakodolea macho kile kijiruninga cha kwenye kamera ya Gil nikishuhudia yaliyokuwa yakitendeka kule chini.Moyo ulikuwa unapiga kwa nguvu hadi nikahofia kuwa wale watu kule walipo wangenisikia na kuja kunikamata.

Na nilizidi kuchanganyikiwa nilipowafikiria wale watafiti wenzetu waliobaki kule kwenye kambi yetu pamoja na wale watu kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya. Hatimaye nilipata wazo kuwa kwa kuwa sikuwa na namna ya kuwaokoa Gil na Ibrahim pamoja na yule mtu asiye na shati pale chini ambao tayari walikuwa mikononi mwa wale watu wabaya, cha msingi ambacho ningeweza kufanya ni kujaribu kujiokoa mimi mwenyewe na wenzangu waliobaki kule kambini.

Nilikuwa nataka kujiinua ili nikimbie kule kambini kuwatahadharisha wenzangu wakati nilipomuona yule mwenyeji mmoja kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya akiteremka kibonde kwa kasi kuelekea pale walipokuwa akina Ibrahim.Naye akajikuta amezingirwa na wale watu wenye makoti marefu na nia mbaya.Nikaduwaa.

Sasaitakuwaje?

Moyo wangu ulinyong’onyea zaidi nilipogundua kuwa mwili wangu ulikuwa unatetemeka vibaya sana kiasi nilishindwa kujiinua kutoka pale chini. Nikabaki nimelala kiwetewete pale chini huku machozi yakinitoka, nikiwatazama wenzangu wakikusanywa kama kundi la kondoo na kupigishwa magoti huku mikono yao ikiwa imewekwa nyuma ya vichwa vyao.

Mtu mwenye mguu mbovu alikuwa akiwauliza maswali na Ibrahim Geresha alikuwa akijitahidi kujieleza ili aokoe maisha yake na ya wenzake. Lakini hata pale nilipokuwa naangalia matukio yale nilijua kuwa bidii zake hazitazaa matunda.Nilibonyeza kitufe kilichoandikwa ‘zoom’ kwenye ile kamera yenye nguvu na mara picha ilivutwa na nikaweza kuiona kama vile wale watu wote kule chini walikuwa kama hatua kumi tu kutoka nilipokuwa.Niliielekeza kamera ile usoni kwa yule mtu mwenye mguu mbovu aliyekuwa akiuliza maswali na hapo hapo nilishituka na kufumba macho nikidhani kuwa ameniona kwani wakati ule sura yakeilikuwa imegeuzwa moja kwa moja kule nilipokuwapo.Nilifumbua macho na kuanza kumtazama kwa makini. Haikuwa sura ya mtu mzuri hata kidogo. Huyu nilimhisi kuwa na umri mkubwa wa labda kuanzia miaka hamsini kwenda juu. Jicho lake la kulia lilikuwa kubwa kuliko la kushoto na hapo nikagundua kuwa lilikuwa ni jicho la bandia, kwani wakati mboni ya jicho lake la kushoto ilikuwa ikitembea huku na huko alipokuwa akiongea, lile la kulia lililokuwa na mboni yenye rangi tofauti, lilikuwa limetulia tu..

Jicho la mbuzi.

Nilijisikia baridi ikipita mwilini mwangu kwa kumtazama tu yule mtu mbaya.

Taratibu niliielekeza kamera kwa mtu wa pili kati ya wale waliokuwa wameteremka kutoka kwenye helikopta, ambaye bado alikuwa amewaelekezea akina Ibrahim bastola yake. Huyu naye hakuwa mtu mzuri. Alikuwa ana kidevu kilichochimbika na mdomo wake muda wote ulikuwa umebetuliwa mithili ya mtu aliyechefuliwa na kitu fulani.Alionekana kuwa na umri wa kati ya miaka thelathini na tano na arobaini na usoni mwake alikuwa amevaa miwani ya jua iliyoficha macho yake.

Nikaielekeza kamera yangu kwa yule mtu wa tatu ambaye alikuwa amemkanyaga yule mtu asiye na shati.

Ni nani yule?

Nilipouona uso wake kwenye kamera tu hapo hapo nilihisi ganzi ikinitambaa mwili mzima huku ubaridi mkali ukinitambaa kwenye uti wangu wa mgongo. Huyu mtu alikuwa ni muuaji wa kuzaliwa! Alikuwa ana macho ya kutisha kuliko yote niliyowahi kuyaona. Na hata pale nilipokuwa nikiutazama uso wake kupitia kwenye kijiruninga cha ile kamera ya Gil, macho yake yalinikumbusha macho ya nyoka mwenye sumu kali. Pamoja na kuogofya kwa macho yale yaliyojaa ukatili, nilijikuta nikiendelea kumtazama yule muuaji.

Niliweza kuona mdomo wake ukiongea kikatili kuwaeleza jambo akina Ibrahim,na ingawa sikuweza kusikia alikuwa akisema nini, hakukuwa na shaka kabisa kichwani mwangu kuwa aliyokuwa akiyaongea hayakuwa na wema kwa wenzangu hata kidogo.

Bila ya kujali jasho lililokuwa likinivuja kwa wingi usoni, niliteremsha kamera yangu kutoka usoni kwa Macho ya Nyoka mpaka kwa yule mtu aliyemkanyaga kwa mguu wake pale chini.

Sijawahi kuona mtu anayekufa maishani mwangu, lakini muda kamera ya Gil ilipouleta uso wa yule mtu kwenye kijiruninga chake kidogo nilijua mara moja kuwa nilikuwa nauangalia uso wa mtu anayekufa…uso wa mtu anayejua kuwa anakufa.

Uso wake ulikuwa umevimba na ukivuja damu vibaya, damu iliyochanganyika na michanga.Mwamba wa pua yake ulikuwa umevunjika na kulikuwa kuna jeraha kubwa lililotambaa kutokea kwenye paji la uso wake hadi chini ya jicho lake la kulia. Mdomo wake wa juu ulikuwa umevimba vibaya sana. Alikuwa akitiririkwa na machozi ya kukata tamaa. Kwa jinsi nilivyomuona, nilimkisia kuwa alikuwa na umri wa kati ya miaka thelathini na thelathini na tatu, si zaidi ya hapo. Alikuwa ni kijana mwenye sura nzuri ya kuvutia…hiyo ni kabla ya kukutana na hawa watu wenye makoti marefu: sasa hivi alikuwa mbali sana na mtu mwenye sura ya kuvutia, na nilimwonea huruma sana.

Pamoja na yote hayo,  kitu kilichonipa hisia kuwa nilikuwa natazama uso wa mtu anayekufa haikuwa ile sura yake iliyobondwa bondwa au mdomo uliovimba wala mwamba wa pua uliovunjika. La Hasha. Yalikuwa ni macho yake. Yalikuwa yanatazama kwa kukata tamaa na hayakuwa na ile nuru ya uhai ambayo binadamu huwa tunakuwa nayo, hata kama tunaumwa lakini hatuelekei kufa.

Mikono yake ilikuwa imetawanyika kila upande pale mchangani na miguu yake ilikuwa imefungwa pamoja kwa kamba. Suruali yake ya jeans ilikuwa imechafuka na kuchanika ovyo ilhali  miguuni hakuwa amevaa viatu.

Hawa watu wamemfanya nini huyu jamaa?

Au huyu jamaa kawakosea nini hawa watu?

Kwa muda akili yangu ilinizunguka na sikujua nifanye nini. Taratibu nilianza kuiweka kamera pembeni nikiwa nimekata tamaa, lakini mara nikahisi kitu kisicho cha kawaida. Nilihisi kana kwamba…kana kwamba… mnh,lakini haiwezekani!

Taratibu nikairudisha tena ile kamera usoni mwangu na kuielekeza kwa yule mtu aliyelala kifua wazi pale mchangani na hisia yangu ikathibitika.

Yule mtu anayekaribia kufa ameniona!

Moyo ulinipiga chogochemba na nikahisi kana kwamba kuna vipepeo wengi wamenasa ndani ya moyo wangu, wakiruka huku na kule kutafuta pa kutokea.

Yule jamaa ameniona!

Niliona wazi kutoka kwenye macho yake yaliyokata tamaa kuwa ameniona. Ilikuwa kana kwamba alikuwa anajaribu kuniambia kitu kwa macho yake…kama ananiomba kitu kwa macho yake!

Nilijua palepale kama ninavyojua sasa kuwa taswira ile ya macho ya yule mtu itabakia akilini mwangu kwa muda mrefu wa maisha yangu.

Tulitazamana.

“Usinitazame namna hiyo tafadhali… sina msaada wowote kwako!” Nilijikuta nikimnong’oneza kana kwamba atanisikia huku nikiiweka pembeni ile kamera na kulaza paji la uso wangu mkononi mwangu.

Anajaribu kunielewesha nini?.

Niliinua tena kamera na kumtazama yule mtu. Bado alikuwa anaangalia upande niliokuwepo.

“Sasa usifanye hivyo…! Utanikamatisha na mimi!” Nilinong’ona tena peke yangu na hapo hapo nilirudisha kamera kwa Macho ya Nyoka. Bado alikuwa ameelekeza uso wake kwa wale mateka wao, akiwa hana habari na yule mtu aliyemkanyaga pale chini, bila shaka kwa sababu alikuwa ana uhakika kuwa hakuwa na uwezo tena wa kujaribu kitu chochote. Nilikuwa narudisha kamera kwa yule mtu aliyefikwa na madhila mazito kabisa pale chini wakati ghafla niliposikia purukushani kutoka kule walipokuwa akina Ibrahim Geresha. Niliinua uso haraka na kushuhudia yule mwenyeji aliyekuwa akituongoza katika utafiti wetu akitimua mbio kutoka eneo lile.

“Mamaaa!” Nilijisemea mwenyewe kwa woga huku nikiinua kamera kuangalia kule alipokuwa akikimbilia yule mwenyeji na hapo hapo nilishuhudia yule mtu akitupa mikono yake hewani na kupiga yowe kubwa huku akipiga hatua tatu zaidi za kupepesuka hali doa kubwa jekundu likitokea kwenye mgongo wa fulana yake nyeupe iliyopauka.Alianguka chini kama mzigo na kufurukuta kidogo kisha akatulia.

Amekufa!

Yule mwenyeji aliyekuwa akituongoza kule msituni alishikwa woga na kuamua kutimua mbio akiamini kuwa anajiokoa lakini risasi kutoka kwenye bastola ya Macho ya Nyoka ilimpata katikati ya uti wa mgongo na kumuua pale pale.

Kwa mtu ambaye hajawahi kuona mtu akiuawa hata siku moja hilo lilikuwa ni jambo la kuogopesha sana kwangu. Mwili ulinifa ganzi na nikahisi kupoteza fahamu.

Kwa namna fulani niliweza kuendelea kuielekeza ile kamera kule walipokuwapo lakini mikono ilikuwa ikinitetemeka vibaya sana. Nilianza kubwabwaja peke yangu huku nikijitahidi kujizuia kulia kwa sauti. Machozi yalinitiririka huku nikijaribu kuendelea kuangalia yale yaliyokuwa yakitendeka kule chini.

Kule walipokuwa akina Ibrahim kulikuwa kuna kelele nyingi zilizotokana na mayowe ya wale wenzangu waliokumbwa na woga mkubwa kwa kumuona mwenzao akiuawa. Gil alijaribu kukimbia lakini nilimuona Ibrahim Geresha akimkamata mkono na kumvuta chini kwa nguvu huku naye akilala chini ilhali akiinua mikono yake juu. Gil naye alifanya hivyo hivyo huku akisema maneno ambayo sikuweza kuyasikia lakini niliweza kuona kuwa alikuwa amechanganyikiwa.

Wale watu wenye makoti marefu walikuwa wakitoa amri kwa makelele huku wakiwapiga mateke akina Ibrahim waliokuwa wamejilaza chini kifudifudi kujisalimisha.

Eeh, Mungu wangu…balaa gani hili tena!

Mara hiyo nikahisi mkojo ukinitoka,ukilowesha suruali yangu ya kodrai na kuchuruzika mchangani.

Oh! Shiit!

Niliiweka pembeni ile kamera na kutupa macho kule walipokuwa akina Ibrahim.Niliwaona wakiinuliwa kwa nguvu kutoka chini walipokuwa wamejilaza na kusukumwa kimabavu kuelekea kule walipotokea. Nilimtazama yule mtu aliyebururwa kutoka kwenye ile helikopta na nilimuona akifanya kitu ambacho sikukielewa. Haraka niliichukua tena ile kamera na kuielekeza kwake. Kwa kutumia mkono wake wa kushoto na kwa taabu sana, yule mtu alikuwa akiandika vitu fulani mchangani!

Eeh! Sasa hii ndio nini?

Sikuelewa kwa nini yule mtu alikuwa anafanya vile na nikaanza kumtilia mashaka iwapo alikuwa ana akili timamu muda ule, kwani nilisikia kuwa watu wakiwa wanakaribia kufa -na kwa hakika yule mtu alikuwa anakaribia kufa – huwa wanapoteza akili. Kwa sababu wakati mambo kama yale yanatokea mtu mwenye akili timamu huwezi kufikiria kuchora chora mchangani… isipokuwa kama akili yako si timamu.

Nilimtazama kwa makini kwa kutumia ile kamera. Alikuwa akinitazama bila ya kusema neno wala kufanya kitu kingine zaidi.Kwa mara nyingine tena nikapata hisia kuwa yule mtu alikuwa akinieleza kitu kwa macho yake.

Ni nini lakini?

Nilitazama kule walipokuwa wenzangu na nikaona kuwa walikuwa wakiongozwa kuelekea kule walipotokea huku wawili kati ya wale majambazi watatu wakiwafuata wakiwa wamewaelekezea bastola zao.

Macho ya Nyoka alibaki nyuma kwa muda na nilimuona akimwinamia yule mtu aliyekuwa amelala kifudifudi pale mchangani na kumkemea kwa muda mfupi kisha akampiga teke la mbavu kabla ya kukimbia kuwafuata wenzake waliokuwa wakiwaongoza akina Ibrahim kutoka eneo lile.

Nilihisi kuwa wale watu walikuwa wamewalazimisha akina Ibrahim wawapeleke pale tulipoweka kambi yetu, na nilijua kuwa kama hivyo ndivyo, basi walikuwa wana nia ya kuua watu wote watakaowakuta huko. Moyo ulinipiga kwa kasi na sikujua ni nini la kufanya. Nilijiinua kidogo na kujaribu kuchungulia vizuri zaidi. Wale watu walikuwa wametoweka kutoka eneo lile na kuingia msituni kuelekea ambapo nilihisi kuwa ni kule tulipoweka kambi yetu.

Akili yangu sasa ilikuwa ikijitahidi sana kuelewa mambo yaliyokuwa yakitokea pale msituni ili angalau nipate njia ya kujiokoa. Mambo hayakuonekana kuleta maana kwangu, kwani sikuelewa ni kwa nini wale majambaziwaamue kuondoka wote watatu na mateka wao wapya na kumwacha mateka wao waliyekuja naye pale bila ulinzi wowote.

Bila shaka walikuwa wamechagua eneo hili pweke katikati ya msitu ili waje kumuua halafu wamwache huku msituni akioza na kuliwa na fisi.Lakini kwanini ilikuwa ni lazima huyu mtu aje kuuawa huku msituni?

Kwa nini wasingemuua tu huko walipotoka halafu wakaja kuutupa mwili wake huku msituni? Tena wangeweza kumuua hata mle mle kwenye helikopta na kuja kuutupa tu mwili huku msituni. Kidogo hili lilileta maana kwani katika msitu huu, ingechukua muda mrefu sana kwa mwili wake kugundulika.Lakini sasa hili la kuja kumuulia huku msituni…

Kufikia hapa nilikuwa nalia kwa sauti kama mwehu huku midomo ikinitetemeka na machozi yakinimwagika mfululizo huku nikijitahidi kuyafuta bila mafanikio kwa mkono wa shati langu la drafti drafti lililokuwa na mikono mirefu.

Nilimgeukia yule mtu aliyelala pale mchangani akiugulia na nilishituka nilipoona kuwa alikuwa akijitahidi kusota kwa taabu sana kuelekea upande niliokuwepo. Sasa kaka yangu ukija huku si tutakamatwa wote…?

Alipoona kuwa namtazama, aliniinulia mkono wake mmoja kwa ishara ya kuniita. Moyo ulinipiga mshindo na woga ukanitawala.

Unataka nini…?

Nilitazama kule walipoelekea wale majambazi na mateka wao ambao ni watafiti wenzangu. Walikuwa wameshapotelea msituni. Nikamgeukia yule mtu aliyekuwa akigaragara pale mchangani. Alikuwa akizidi kuniashiria kwa taabu. Alijitahidi kujiinua kutoka pale chini lakini alianguka tena chini na kupiga ukelele hafifu wa maumivu. Alibaki akitweta pale chini huku akiwa amejiinamia, akiwa ametuliza paji la uso wake kwenye mkono wake uliolazwa mchangani. Nilimtazama huku nikiwa nimechanganyikiwa na machozi yakinitoka.

Lakini huu si muhali kaka yangu? Na usichana huu mi’ n’takusaidia vipi hapo…?

Yule mtu aliinua uso wake kunitazama kwa mara nyingine na safari hii niliingiwa na simanzi isiyo kifani kwani jamaa alikuwa analia waziwazi huku akiniangalia. Alipeleka mkono wake wa kushoto na kuanza kupigapiga chini pale alipoandika vitu ambavyo mpaka wakati ule sikuweza kuviona na hivyo sikuvielewa.

“What? you want me to see what you’ve written?” Nilijinong’onea mwenyewe kumuuliza yule mtu iwapo alikuwa anataka nione alichokiandika, nikijua wazi kuwa yule maskini ya Mungu alikuwa hanisikii. Na hata pale nilipokuwa nikijisemesha kwa kuchanganyikiwa, yule mtu alijaribu tena kujiinua lakini alishindwa na kuanguka tena mchangani huku akitoa mguno wa maumivu.

Mungu wangu! Huyu mtu anataka kuniambia kitu!

Nilisita.

Nilitazama kule walipoelekea wale majambazi. Kulikuwa kimya kabisa. Moyo ulinipiga kwa nguvu na matumbo yalininyonga. Nikamgeukia yule mtu pale chini, kisha nikatazama tena kule walipokuwa wamepotelea wale majambazi na akina Ibrahim.

Bado kimya.

Niliikwapua kamera ya Gil na kutoka mbio huku nikiwa nimeinamisha mwili wangu kutokea kiunoni kuelekea pale alipokuwa yule mtu aliyekuwa kwenye  mashaka mazito.

Nilipomfikia nilijikuta nikitoa mguno wa woga huku mwili ukinisisimka. Yule mtu alikuwa amechakaa vibaya sana kwa kumtazama kutokea karibu kuliko nilivyokuwa nikimwona nikiwa mbali.

Mwili wake ulikuwa una makovu mengi mabichi ambayo niliweza kuhisi kuwa yalitokana na kuchomwa kwa ncha ya sigara au kitu chenye moto.

“Oh! Mungu wangu! Mungu wangu! Mungu wangu…” Nilijikuta nikibwabwaja huku nikiutazama mwili wa yule mtu ulivyoharibiwa kwa mateso.

Zaidi ya vidonda vilivyotokana na kuchomwa kwa ncha ya sigara, pia mwili wake ulikuwa una majeraha yaliyotokana na kuchanjwa kwa kitu au vitu vyenye ncha kali, kama vile kisu kikali sana. Nilijaribu kumshika lakini nilishindwa kwani nilihisi kuwa kila nitakapomshika nitakuwa namtonesha. Miguu yake iliyokuwa imefungwa kamba ilikuwa ina majeraha makubwa sana yaliyokuwa yakivuja damu iliyolowesha ile suruali yake iliyochanika ovyo ovyo. Mguu wake wa kushoto ulikuwa una jeraha kwa nyuma ya paja lake wakati ule wa kulia ulikuwa una jeraha baya sana kwenye ugoko. Pamoja na kwamba sikuwa na uzoefu na majeraha ya aina ile, mara moja nilijua kuwa yalikuwa ni majeraha ya risasi.

Nilianza kutetemeka kwa kihoro na wasiwasi. Kwa hakika hawa watu walikuwa wamemtenda vibaya sana huyu kijana. Nilijaribu kumwinua nikashindwa kwani alikuwa mzito kuliko uwezo wangu. Alijitahidi kujigeuza na kulalia mgongo. Nililaza sikio langu kifuani mwake na kusikiliza mapigo ya moyo wake. Yalikuwa dhaifu sana.

“…the…bas…tard!” Yule mtu alisema kwa taabu na sauti yake ilikuwa ya chini sana.

“Usiongee! Tulia, nitakusaidia.” Nilimwambia kwa upole huku nikitupa macho ndani ya ile helikopta. Ilikuwa tupu.

Yule mtu alinikamata mkono wangu kwa nguvu na kunivutia kwake. Nilipatwa na woga na kumgeukia. Alipoona nimemgeukia, aliniashiria kwa kidole pale mchangani alipoandika kwa kidole chake. Nilitazama na kuona kuwa alikuwa ameandika namba ambazo sikuelewa zilimaanisha nini. Nilimtazama kwa mshangao na kutaka kumuuliza juu ya zile namba lakini alizidi kunisisitiza kwa macho yake huku akijitahidi kuongea bila ya mafanikio.Nilifikiri haraka haraka. Kwa vyovyote hizi nambazina maana kubwa kwake.Nilielekeza kamera ya Gil kwenye zile namba zilizoandikwa pale chini ili niweze kuzitazama vizuri baadaye.

“Sawa…nimeshaona! Hizi namba ni za nini? Na wewe ni nani…kwa nini wale watu wamekufanya hivi? Umewafanya nini? Ni nani wale?” Nilijikuta nikimvurumishia maswali yule mtu huku nikiangaza huku na huko kwa wasiwasi wa kukutwa na wale watu wabaya.

Badala ya kujibu yule mtu alikohoa kwa taabu na kubaki akitweta kama mtu aliyemaliza mbio ndefu…

Find the Bastard!” Yule mtu alisema kwa kimombo, akimaanisha ‘mtafute mwanaharamu’, au kitu kama hicho. Mara moja nikamuelewa kuwa alikuwa anamaanisha kuwa anataka niwatafute wale watu waliomfanyia unyama huu ili wawajibike.

Yes! Usiwe na wasiwasi nitahakikisha wanafikishwa mbele ya sheri—”

“…at the Rickshaw…!” Yule mtu alinikatisha kama vile sijaingilia kati kauli yake ya mwanzo. Sikumuelewa.Alikuwa akitweta sana kila baada ya kusema neno na nikaelewa kwamba kuongea kulikuwa kunampa taabu. Na alichokisema kilikuwa hakieleweki.

“Rickshaw? Rickshaw iko wapi ?” Nilimuuliza.

Kwa uelewa wangu Rickshaw ni aina ya mikokoteni inayotumika zaidi kule Taiwan na Thailand kubebea watalii.Hivyo neno lile katika mazingira yale halikuleta maana kabisa kwangu. Badala ya kunijibu yule mtu alianza kutapatapa huku akitupa kichwa chake huku na huko hali akigumia kwa taabu. Moyo ulinienda mbio na woga ukanizidi kwani nilihisi  kuwa yule mtu ndio alikuwa anaelekea kukata roho.

Na hata bado sijamjua!

“Wewe ni nani…ndugu zako ni nani?” Niliuliza haraka na kwa wasiwasi.

Get the key… the bastard!” Jamaa alikuwa anaongea kizungu tu.

Key…?What key…?”

At the Rickshaw…!”

I don’t understand!

Please…Go now!”

“Lakini bado sijaelewa…nataka kukusaidia! Au hujui Kiswahili? Can’t you speak Swahili?”

Find the bastard!” Yule mtu asiye na jina sasa alifoka, na hiyo ilionekana kummalizia kabisa nguvu zake hafifu. Alibaki akitweta kwa taabu huku akinitazama kwa macho ambayo kidogo yalionesha matumaini.

Nilichanganyikiwa na nikajikuta nikibubujikwa na machozi huku nikimtazama yule mtu kwa huzuni. Yeye alinitazama na kutoa kitu kama tabasamu dogo sana.

Okay…I can speak english… who are you? Who are those people…? Do you have any relatives….? I can help you…I want to help you!” Niliamua kurejea maswali yangu ya awali kwa kiingereza nikitaraji kuwa labda atanielewa zaidi kwa lugha ile.

Please Go…watakukuta!” Aliniambia kwa sauti hafifu, halafu alipeleka mkono wake na kufuta zile namba alizoziandika pale mchangani.

“Watakuua…wacha nijaribu kukusaidia…”

I don’t care…you go find the bastard!” Halafu alijitahidi kutabasamu tena lakini safari hii hakufanikiwa kwani alishikwa na kikohozi kikali na damu ikaanza kumtoka mdomoni. Nilimwinua kichwa chake ili damu isimpalie na kuanza kumfuta ile damu kwa mkono wa shati langu. Yule mtu alinishika mkono kwa nguvu na kunitolea macho.

“Ondoka hapa mwanamke…they will kill you!

Ah! Kumbe anafahamu Kiswahili.

“Lakini—”

“Onnn…do…kkka!”

“Akh! Sasa…Ah!” Sikujua niseme nini tena.Nilipagawa.

Huku machozi yakinibubujika niligeuka huku na kule. Hakukuwa na dalili yoyote kuwa wale wauaji wangerudi muda ule, lakini sikuwa na uhakika. Nilimgeukia tena yule jamaa.

“Sasa kaka yangu…sijaelewa chochote katika maelezo yako! Nataka nikusaidie, lakini na wewe lazima unirahisishie kazi hiyo…” Sikuweza kuendelea kwani yule mtu alikuwa ametulia kimya akiwa amefumba macho huku akihema kwa taabu. Hakuwa akitilia maanani kabisa maneno yangu. Nilimshika bega na kumtikisa, lakini hakukuwa na badiliko lolote.

“We’ kaka we’…hebu ongea kitu basi! Sasa uliniitia nini huku? Kwa nini hawa watu wanataka kukuua? Umewafanya nini…?”

Yule mtu aliendelea kubaki kimya bila kufumbua macho wala kutikisika. Hali ile ilizidi kunichanganya. Kabla sijaamua nifanye nini nikasikia vishindo vya miguu vikitokea kule msituni. Niligeuka haraka huku na huko nisione kitu.

Nilimtazama tena yule mtu kwa mara ya mwisho, kisha nikanyakua kamera yangu na kutoka mbio kurudi pale nilipokuwa nimejificha hapo mwanzo. Kiasi cha kama dakika mbili tu baadaye wale wauaji walirejea katika eneo lile, wakiwa peke yao bila ya wale wenzangu walioondoka nao awali. Moyo ulinilipuka nikijua kuwa ningezidi kuchelewa wale watu wangenikuta na sijui wangeamua kuniua kwa mtindo gani tu!

Huku moyo ukinipiga nilibaki nikichungulia kule alipokuwa yule mtu asiye na jinailhali akilini nikijiuliza ni kipi kilichowakuta wale wenzangu. Moja kwa moja Macho ya Nyoka alimwendea yule mtu,akamwinua kikatili na kumkalisha kitako huku miguu yake iliyofungwa kamba ikiwa imenyooshwa mbele.Yule mtu aliangukia ubavu pale mchangani. Macho ya Nyoka alimpiga teke la mbavu na kumtolea amri yule mwenzake aliyekuwa amevaa miwani, ambaye alimwinua tena yule mtu na kumshikilia pale chini.

Yule mtu mwenye mguu mbovu alimsogelea yule jamaa asiye na jina na kuanza kumsemesha au kumuuliza maswali fulani. Inaelekea yule jamaa aliamua kutojibu kwani mara ile ile Macho ya Nyoka alimshindilia ngumi kali ya uso na jamaa akatoa yowe kubwa na kuanguka mchangani. Haraka yule jambazi mwingine alimwinua na kumkalisha tena pale chini.

Macho ya Nyoka alitoa bastola na kumwekea mdomoni huku akimsemesha maneno ya kutisha. Kisha yule Kigulu alimsogelea na kumuuliza tena. Jamaa akatikisa kichwa kutoafikiana naye na hapo aliambulia kipigo kingine kutoka kwa Macho ya Nyoka. Aliulizwa tena, akatikisa kichwa tena kukataa. Macho ya Nyoka alimkaba koo kwa mkono wake wa kulia huku akimwekea mdomo wa bastola kwenye paji la uso na kumsemesha kwa ghadhabu.

Hapo niliinua tena ile kamera ya Gil na kuielekeza kule kwa lengo la kuona vizuri matukio yale ya kutisha. Na hata pale nilipokuwa naielekeza ile kamera upande ule, nilimshuhudia yule mtu akimcheka Macho ya Nyoka waziwazi usoni. Tendo lile lilimkera Macho ya Nyoka ambaye alianza kumvurumishia kipigo kikubwa yule mtu. Mateke, ngumi, makofi. Hatimaye yule Kigulu alimzuia Macho ya Nyoka na kumsukuma pembeni.

Macho ya Nyoka alipiga teke mchangani kwa hasira na kurusha michanga hewani. Alisogea pembeni na kuweka bastola yake kwenye mfuko wa koti lake refu.

Yule mtu asiye na jina alibaki akigaragara mchangani kwa uchungu na maumivu makubwa. Damu zilimtoka kwa wingi usoni na mdomoni wakati Kigulu akimkemea Macho ya Nyoka kabla ya kumwinua kichwa yule mtu asiye na jina na kumuuliza tena kitu alichokuwa akimuuliza hapo awali.

Kwani mnataka nini kutoka kwa huyo mtu ndugu zangu?

Yule jamaa badala ya kumjibu alimtemea mate usoni.

Kigulu aliruka nyuma kwa hasira na kujifuta mate kwa kiganja cha mkono wake huku akipepesuka . Muda huohuo yule jambazi mwingine aliyekuwa amevaa miwani ya jua alimrukia yule jamaa kwa teke kali la uso lililomrusha nyuma yule jamaa huku akipiga yowe na kuanguka chali mchangani.

Mungu wangu! Kwani si uwaambie tu wanachokitaka ndugu yangu? Watakuua hao…!

Machozi yalizidi kunibubujika kwa woga na huruma kwa yule mtu huku nikijaribu kufikiri nifanye nini kumsaidia yule masikini ya mungu,lakini kabla sijapata ufumbuzi niliona kitu ambacho sikukitegemea kabisa.

Yule mtu asiye na jina alimrushia mchanga machoni yule Kigulu na hapo hapo alijiinua mzimamzima kutoka pale mchangani hali bado miguu yake ikiwa imefungwa na kumrukia Macho ya Nyoka aliyekuwa amesimama pembeni bastola yake akiwa tayari ameiweka mfukoni.

Kigulu alirukaruka huku akijipangusa mchanga machoni wakati Macho ya Nyoka na yule jambazi mwingine walibaki wakiwa wameduwaa kwa nukta ya sekunde, jambo lililomwezesha yule mtu asiye na jina kumfikia Macho ya Nyoka na kumkamata koo kwa mikono yake yote miwili na wote wawili wakapiga mweleka mzito pale mchangani.Wale watu hawakutegemea kitendo kile na hivyo hawakuwa wamejiandaa na tukio kama lile.

Yule mwenye miwani na Kigulu walipiga kelele kwa pamoja na kukimbilia pale walipoanguka wale mahasimu wawili ambao walikuwa wakibiringishana mchangani. Macho ya Nyoka alikuwa akijitahidi kujikwamua kutoka mikononi mwa yule mtu aliyekuwa ukingoni mwa mauti, na yule mtu asiye na jina akizidi kumkaba koo bila shaka kwa nguvu zote alizobakiwa nazo kwa wakati ule.

Vumbi lilitimka na wote wawili wakapotelea kwenye vumbi lile. Hapo hapo yule mwenye miwani aliwafikia na kumrukia mgongoni yule mtu asiye na jina aliyekuwa juu ya Macho ya Nyoka na kujaribu kumnasua kutoka kwa mwenzao, lakini yule jamaa alikuwa amemkamata koo Macho ya Nyoka vizuri sana. Kilikuwa ni kitimtim kizito kilichodumu kwa dakika zipatazo mbili hivi.

Na mara ulisikika mlipuko mkubwa wa bastola.

Yule jamaa mwenye miwani aliruka na kujitupa pembeni, akainuka na kupiga mweleka tena, kisha akainuka na kupepesuka kabla ya kusimama wima. Kigulu alikuwa ameshajifuta michanga machoni na aliungana na yule jambazi mwingine aliyekuwa akitweta pale pembeni. Walibaki wakiwa wamesimama midomo wazi wakiwaangalia wale watu wawili waliolaliana pale chini nami nikiwa nimekaukwa koo kwa hofu iliyotokana na mambo niliyokuwa nikiyashuhudia pale msituni.

Nilibaki nikiwa nimeielekeza kamera yangu kwa wale mahasimu wawili waliolaliana pale mchangani.

Kwa kama dakika moja na nusu hivi hakukuwa na mtikisiko wowote kutoka kwenye ile miili miwili iliyolaliana, kisha niliona mwili wa yule mtu asiye na jina ukiinuka mzimamzima na kuangukia ubavu kando ya Macho ya Nyoka. Kisha kwa kihoro nilimuona  Macho ya Nyoka akijiinua kutoka pale mchangani na kusimama huku akipepesuka akiwa na bastola mkononi mwake, sehemu ya mbele ya koti lake refu ikiwa imetapakaa damu.

Nilipomtazama yule mtu asiye na jina pale chini, niliona jeraha kubwa kifuani mwake na damu nyingi ikibubujika kutoka kwenye jeraha lile.

Alikuwa amekufa.

Nilihisi mwili ukifa ganzi na nikaanza kulia upya kumsikitikia yule mtu aliyeuawa. Macho ya Nyoka alipoona ameelemewa na kabali ya yule mtu aliamua kumpiga risasi ya kifuani na kumuua pale pale. Kigulu alimjia juu Macho ya Nyoka.Alimfokea huku akitupa mikono yake hewani na kuunyooshea kidole ule mwili wa yule mtu aliyelala pale mchangani bila uhai. Hata yule mtu mwenye miwani naye alikuwa akifoka kwa nguvu huku akitupa tupa mikono yake hewani. Macho ya Nyoka naye akawa anawafokea wenzake huku akitikisa bastola yake na kumnyooshea mkono yule marehemu pale chini na kujishika koo.

Wakati nikiendelea kutazama mambo yale kupitia kwenye kijiruninga cha kamera ya Gil, nilishindwa kuelewa maana ya matukio yale na kuzidi kuchanganyikiwa.

Ina maana hawakutaka huyu mtu afe!?

Kwa hakika nilichanganyikiwa. Nikawakumbuka wenzangu kule kambini. Mungu wangu! Watakuwa wamewafanya nini wenzangu? Nitawakuta hai kweli…?

Wale wauaji watatu waliacha kugombezana na sasa walikuwa wakiongea taratibu huku yule Kigulu akitoa maelekezo. Macho ya Nyoka aliutazama mwili wa yule marehemu na kuutemea mate kwa ghadhabu.

Kigulu alimshika mabega na kumsukumia kule ilipokuwa ile helikopta yao, na wote wakaingia kwenye lile dege kubwa. Nilibaki nikiwa nimejibanza pale kichakani nikiishuhudia ile helikopta ikizungusha mapangaboi yake kwa muda kabla ya kunyanyuka kwa madaha kutoka pale mchangani na kuelea hewani. Ililala kulia kisha ikalala kushoto, na kwa sekunde kadhaa niliweza kumuona yule mtu mwenye miwani akiwa ameshika usukani wa ile helikopta, halafu ikalala tena kulia, ikapaa na kutoweka kutoka eneo lile, ikiuacha mwili wa yule mtu asiye na jina pale mchangani.

Sikusubiri zaidi.

Nilining’iniza mkanda wa ile kamera ya Gil begani na kutimua mbio kuelekea kule ilipokuwa kambi yetu huku nikiita majina ya wenzangu kwa kelele. Mara kadhaa nilijikuta nikianguka na kujiinua tena na kuendelea kukimbia bila kujali kuwa nilikuwa nikipamia miti ovyo na kujiumiza. Nikiwa kama niliyechomoka kwenye mdomo wa mauti,suala la kujipamia kwenye miti lilikuwa ni dogo sana kwangu kwa wakati ule.

Nilipofika kambini kwetu nilipiga mweleka mzito kwa mshituko na kubabaika. Wenzangu wote walikuwa wameuawa! Ni vigumu kuamini lakini ndivyo ilivyokuwa.Ilikuwa ni picha ya kutisha kuliko ile niliyoiona kule ilipokuwa ile helikopta.Huku nikitetemeka na kulia kwa sauti nilijiinua kutoka chini nilipoanguka na kuanza kuwakimbilia wenzangu mmoja baada ya mwingine huku nikiwaita kana kwamba wataitika.

Yalikuwa ni mauaji ya kutisha.

Ibrahim Geresha alikuwa amelala chali mbele ya hema lake huku akiwa ametumbua macho na amekenua meno kwa uchungu.Damu ilikuwa ikichuruzika kutoka kwenye tundu moja lililokuwa katikati ya paji lake la uso.Nilimkimbilia na kujibwaga ubavuni mwake.

“Mista Geresha!Mista Gereshaaa…!” Nilimuita huku nikiutikisa mwili wake kwa nguvu.Ingawa bado mwili wake ulikuwa na joto, Ibrahim Geresha alikuwa ameshakufa. Nililia kwa woga na kuchanganyikiwa kukubwa kabisa.

Niliinuka na kuanza kuangaza eneo lile lililokuwa kambi yetu ya utafiti. Ilitisha sana! Hatua chache kutoka pale alipoangukia bosi wangu Ibrahim Geresha niliuona mwili wa yule mwenyeji mwingine tuliyepewa na ofisi ya mkuu wa wilaya nao ukiwa umeanguka pale kwenye ile ardhi ya mawe ukiwa hauna uhai. Yeye alikuwa amelala kifudifudi huku akiwa na jeraha kubwa sana kisogoni ambalo sikuwa na shaka kuwa lilitokana na risasi.Alikuwa ametawanya mikono yake kila upande na mkono wake wa kulia ulikuwa umekusanya fungu la changarawe kwenye kiganja chake bila shaka kutokana na uchungu alioupata wakati roho ilipokuwa ikimtoka.

Nilikimbia kwa kupepesuka kutoka pale nilipokuwa nimesimama na kumuendea bwana Ubwa Mgaya huku nikiita jina lake bila ya matumaini. Alikuwa ameuawa vibaya sana, kwani bila shaka risasi ilimpata akiwa anajaribu kukimbilia ndani ya hema lake. Alikuwa ameshikilia mlingoti wa hema lile kwa mkono wake wa kulia, ambao kutokana na uzito wake uliangukia juu ya paa la gari letu lililokuwa karibu na hema lile. Mgaya akawa ananing’inia kwenye ile nguzo aliyoilalia kwa kiwiliwili chake huku turubai la hema lake likiufunika mwili wake. Kwa pale nilipokuwa, nilikuwa nikiuona uso wake ukiwa umetokeza kwenye turubai lililotapakaa damu nyingi sana naye akiwa ametumbua macho sio kwa uchungu bali kwa mshangao.Ingawa sikuona ni wapi hasa risasi iliyomuua bwana Ubwa Mgaya ilikuwa imeuingia mwili wake, kiasi cha damu kilichotapakaa kwenye lile turubai kilitosha kabisa kunithibitishia kuwa naye alikuwa marehemu. Nilianza kurudi nyuma taratibu huku nikiendelea kuukodolea macho uso wa marehemu Ubwa Mgaya.

“Nisaidieni jamaniiii! Watu nisaidieniii…Ooooh Mama yangu weee! Mambo gani tena haya jamaniii!” Nilikuwa nikilia kwa sauti huku nikimangamanga huku na huko pale msituni nisijue niende wapi. Harufu ya damu ilikuwa inanilevya na nilihisi kichefuchefu kikubwa sana.

Nilijibwaga chini na kubaki nikiwa nimepiga magoti huku nimezungukwa na maiti za watafiti wenzangu.

Nililia!Nililia sana na kwa muda mrefu.Na kila nilivyozidi kulia niliona haitoshi,kana kwamba kulia sana kungeniletea mtu wa kunisaidia.

Lakini bado kuna wenzangu wengine siwaoni! Ingawa nilikuwa niliamini  kuwa wenzangu wote walikuwa wameuawa, lakini taratibu akili yangu ilianza kufanya kazi huku nikiendelea kulia.Nilikuwa nimeona maiti za wenzangu watatu tu pale kwenye ile kambi yetu, na damu nyingi ikiwa imetapakaa eneo lote lile… lakini walitakiwa wawe zaidi ya watatu! Nilinyamaza kulia na kubaki nikigumia kipumbavu huku nikitembeza upya macho yangu  eneo lile.

Wako wapi Beka na Gil?

Niliinuka taratibu na kuanza kulizuru upya eneo lile huku nikizidi kupata matumaini kuwa kumbe kuna wenzangu waliofanikiwa kuokoka na mauaji yale ya kutisha.

“Giiiiill! Giiiiilll!” Nilianza kuita huku nikiangaza huku na huko kwa matumaini. Hatua chache kutoka pale ulipokuwa umelala mwili wa yule mwenyeji mmoja aliyekuwa akituongoza kule msituni niliona mchirizi mzito wa damu ukielekea kwenye kichaka kidogo kando kidogo ya ile kambi yetu. Nilianza kuufuata ule mchirizi huku moyo ukinienda mbio. Nilihisi kuwa huenda mmoja kati ya wale wenzangu wawili waliobakia atakuwa amefanikiwa kutoroka lakini amejeruhiwa. Ule mchirizi ulipita kando ya gari letu lililokuwa limepaki pale na kuelekea sehemu mbele ya gari lile. Nilizidi kuufuata huku nikiita majina ya Gil na Beka kwa zamu. Sikujua ni yupi hasa kati yao ambaye ningemkuta mwisho wa mchirizi ule.

Nilipotokeza mbele ya lile gari tu nilipata mshituko mkubwa na yowe la woga likanitoka. Hapo hapo nilianza kupiga kelele kwa kiwewe huku nikikimbia hatua kadhaa kutoka kwenye lile gari.

Beka alikuwa amelalia boneti la gari kwa ubavu wake huku mkono wake mmoja ukiwa umenyooshwa mbele juu ya lile boneti na kichwa chake akiwa amekilaza juu ya mkono ule. Miguu yake ilikuwa imetawanywa vibaya huku pale chini kukiwa kumetifuliwa na kuchimbwa chimbwa bila shaka kutokana na purukushani za miguu yake wakati akihangaika kushindana na roho yake wakati ikimtoka, kwani hakukuwa na shaka kuwa Beka alikuwa amekufa, na alikuwa amefikwa na umauti kwa uchungu mkubwa.

Kwa pale nilipokuwa Beka alikuwa amenigeuzia mgongo lakini niliweza kuona damu nyingi ikiwa imetapakaa kwenye lile boneti na kutiririka ardhini, ikilowesha suruali na viatu vyake.

Huku nikitetemeka na kulia kwa sauti, nilijilazimisha kuzunguka upande wa pili wa lile gari ili niweze kumuona Beka kwa mbele kuhakikisha iwapo kweli naye alikuwa amekufa. Nilichokiona kilinithibitishia hofu yangu na kuzidi kunitisha. Damu nyingi ilikuwa ikimtiririka kutoka kwenye jeraha la risasi lililokuwa chini kidogo ya jicho lake la kulia, ambapo mkono wake wa kulia ulikuwa umepashika kana kwamba alikuwa akijaribu kuizuia ile damu isizidi kutiririka. Aidha, alikuwa ana jeraha lingine la risasi ambalo ndilo lililotoa damu nyingi zaidi. Hili lilikuwa katikati ya shingo yake, sehemu ambapo shingo ile ilikuwa ikiungana na kiwiliwili chake.

Eee Mungu wangu! Mauaji yote ya nini haya lakini? Kuna aliyebaki kweli zaidi yangu…?

Hapo nikamkumbuka Gil.

Woga ukanizidi, kwani ingawa nilijua kuwa naye atakuwa ameuawa, nilijikuta nikiuogopa zaidi ukweli kwamba wenzangu wote watakuwa wameuawa kuliko kule kumwona na yeye akiwa ameuawa.Niliita jina lake kwa sauti ya kitetemeshi huku nikikimbia kumsaka katika eneo lile bila mafanikio.

Nilikimbia mpaka kwenye vichaka vya pale jirani, lakini nako pia hakukuwa na dalili yoyote kuwa Gil alipita huko. Hatimaye nikajiona nimechoka kwa kukimbia ovyo huku nikichosha mapafu yangu kwa kupiga kelele bila mafanikio.Nilijibwaga chini kwa kukata tamaa na kubaki nikiwa nimeduwaa pale chini nisijue la kufanya.

Akili yangu ilikuwa kama iliyokufa ganzi.Sikuweza kufikiri kitu.Sikuweza kuelewa kitu.Nilibaki nikiwa nimezubaa pale msituni kwa muda mrefu bila ya kujitambua. Tai walianza kushuka taratibu kutoka angani na kuizungukia ile miili ya wale wenzangu waliouawa. Jambo hili lilinikera na kunihuzunisha sana.Hawa ni binadamu na ni watu ninaowafahamu. Ni saa chache tu zilizopita nilikuwa nikiongea na kucheka nao kwa furaha. Nimekuwa nao safarini na kwenye eneo hili kwa wiki nzima. Sasa wameuawa sijui kwa sababu gani, halafu kama hiyo haitoshi, nashuhudia kwa macho yangu miili yao…mizoga yao…ikidonolewa na tai huku porini! Hii haiwezekani. Haiwezekani kabisa!

Nilikurupuka na kuwafukuza wale ndege wakubwa wenye kucha kali na zenye nguvu na midomo mikali kama mkasi kutoka kwenye miili ya wale marehemu wasio na hatia.

“Tokeni hapa! Kwenda ’ukoo! Mnadhani kila kitu ni cha kuliwa tu! Huuuuuush! Huuuuuush!” Niliwabwatia kwa hasira wale tai, ambao waliruka hewani kwa muda tu na nilipogeuka walirudi tena kuanza kuwadonoa tena wale wenzangu waliouawa.

Na hata pale nilipogeuka nilishuhudia kwa kihoro mmoja wa ile midege mikubwa na mibaya akinyofoa jicho la bwana Ubwa Mgaya na kuruka nalo hewani huku likivuja damu!

Nilihisi kichefu chefu kizito na nikatamani kufa.Kwa hasira niliwarudia tena na kuwafukuza kwa kelele huku nikitupa mikono hewani na kuwatupia mawe, lakini mchezo ukawa ni ule ule. Walishaona chakula na hawakuwa tayari kukiacha kwa kuniogopa mimi. Mwisho nikachoka kukimbizana nao. Nikajibwaga chini kwa kukata tamaa.Nilibaki nikiwatazama kwa huzuni wenzangu wakiliwa na ile midege mikubwa huku nikilia kwa huzuni.

Lazima nifanye kitu…siwezi kukaa hapa muda wote.

Niliinuka na kuliendea begi langu lililokuwa nje ya hema langu. Nilikumbuka kuwa begi langu nililiacha ndani ya hema lile kabla sijaenda kule msituni kuwapiga picha wanyama. Sasa mbona liko nje? Sikufikiri zaidi. Niliitumbukiza ile kamera ya Gil ndani ya begi lile, kisha nikalipachika mabegani mwangu na kulining’iniza mgongoni. Nikaliendea gari letu. Lazima nikatafute msaada, na nisingeweza kurudi wilayani peke yangu kwa miguu. Nilitumaini kuwa ufunguo ungekuwa ndani ya lile gari. Nilifungua mlango wa dereva na kichwa cha Gil kikaniangukia mapajani na kubaki kikining’inia nje ya mlango wa gari lile.

Nilipiga yowe kubwa la woga huku nikiruka nyuma na kupiga mweleka. Nilijiinua na kuanza kujisukuma nyuma huku nikipiga mayowe. Nilipiga mweleka mwingine.Nikabaki nikisota kurudi nyuma huku nikizidi kupiga kelele. Lilikuwa ni jambo ambalo sikulitegemea na la kutisha sana. Na hata pale nilipokuwa nikipiga kelele huku nikiukodolea macho uso wa Gil uliokuwa ukinitumbulia macho bila kuniona, kama vile alikuwa amelala kichwa chini miguu juu,nilikiri moyoni mwangu kuwa kwa hakika sasa nilikuwa nimeshindwa. Sikuwa na uwezo tena wa kuendelea kustahamili kushuhudia mambo haya.

Gil alikuwa ameuawa akiwa ndani ya gari, bila shaka akijaribu kutoroka kutoka eneo lile. Mwili wake ulikuwa umelala chali kwenye sakafu ya gari, kisogo chake kikiwa kimeegemea mlango wa dereva kwa ndani, ambapo nilipoufungua kichwa kile kiliangukia nje na kubaki kikining’inia wakati kiwiliwili chake kikibaki ndani ya gari.

This is a bloody massacre!

Nilijiinua na kuanza kutimua mbio. Nilikimbia bila ya kuwa na uelekeo maalum huku nikijitapikia mwili mzima, lakini sikujali wala sikusimama. Nilikimbia na kukimbia, huku nikijaribu kufuata alama za matairi ya gari letu zilizoachwa mle njiani wakati tukielekea kule kwenye eneo la kambi yetu,ambazo hata hivyo zilishatoweka kwa kiasi kikubwa.

Machozi yalinitiririka na kamasi zilinivuja lakini sikusimama. Niliendelea kukimbia kwa nguvu zangu zote. Mapafu yangu yalikuwa kama yanayowaka moto na nilitamani nikae chini nipate kupumua na kupumzika, lakini miguu yangu ilizidi kukimbia tu, ikinipelekesha kama gari bovu. Sikuweza kusimama. Ilikuwa ni mbio moja kwa moja. Akilini mwangu nilikuwa nina wazo moja tu, nalo ni kufika ofisini kwa mkuu wa wilaya.

Kwa wakati ule, huko ndiko mahala pekee nilipoweza kupaona kuwa pa usalama…

--

 

Baada ya kukimbia kwa muda mrefu, huku nikisimama njiani na kupumzika mara kadhaa hatimaye niliingia mjini. Sijui niliwezaje kukimbia mpaka Manyoni mjini, lakini nilifika. Akili yangu bado ilikuwa na wazo moja tu la kufika ofisini kwa mkuu wa wilaya na kutoa ripoti juu ya mauaji yale ya kinyama na hatimaye kupata msaada. Muda wote niliokuwa nikikimbia kutoka kule porini, picha za miili ya wale wenzangu wakiwa wameuawa, na yule mtu asiye na jina aliyeuawa na wale watu wabaya, zilikuwa zikinirudia akilini mwangu bila mpangilio.Na kadiri zilivyonirudia ndivyo nilivyozidi kutimua mabio.

Nilipojiona kuwa nimeshaingia mjini niliacha kukimbia na kuanza kutembea haraka haraka, lakini nilipoangalia saa yangu na kugundua kuwa ilikuwa ni saa tisa za alasiri, nikaingiwa na woga kuwa huenda nikakuta ofisi ya mkuu wa wilaya imefungwa na yule mama akawa amekwenda nyumbani.

Sikuwa na mtu hata mmoja anayenifahamu katika mji ule zaidi ya yule mkuu wa wilaya na baadhi ya watendaji wake. Na suala la yale mauaji halikuwa la kumweleza mtu akakuelewa kirahisi, hasa ukizingatia kuwa nilikuwa mgeni kabisa katika mji ule mdogo. Wazo hili lilinifanya nianze kutimua mbio katikati ya mji bila kujali watu waliokuwa wakinishangaa.

Nilipolifikia jengo la ofisi ya mkuu wa wilaya, ambalo wenyeji waliliita ‘wilayani’, nilipita moja kwa moja hadi mapokezi.

“Nahitaji kuonana na mkuu wa wilaya tafadhali!” Nilimwambia jamaa niliyemkuta pale mapokezi huku nikitweta.

Badala ya kunijibu jamaa alikuwa akinikodolea macho kama aliyeona jini. Binti tuliyemkuta pale mapokezi siku ile tuliyoripoti pale ofisini na wenzangu hakuwepo. Hili halikuwa jambo zuri kwangu, kwani nilikuwa nina hakika kama ningemkuta yule binti angenikumbuka na kunipunguzia kazi ya kujitambulisha upya.

Sasa yule jamaa aliinuka taratibu kutoka kwenye kiti chake na kuanza kurudi nyuma taratibu huku macho yakimtembea kwa woga ambao sikuuelewa ulitokana na nini.

“Kaka, ninaomba kuonana na mkuu wa wilaya tafadhali, ni muhimu…dharura!” Nilimwambia tena yule jamaa huku nikimkazia macho kuonesha msisitizo.

Jamaa alikuwa ananitazama kana kwamba nilikuwa mwehu, huku macho yake yakiangukia kifuani na eneo la tumbo langu na kunirudia tena usoni.

“We’ bwana bubu? I said I need to see the Goddamn District Commissioner  for God’s sake! It’s an emergency, can’t you understand?” Nilijikuta nikimfokea kwa kimombo kusisitiza haja yangu ya kuonana na mkuu wa wilaya huku nikipiga meza kwa kiganja cha mkono wangu. Watu wameuawa kama kuku huko halafu mtu ananikodolea mimacho kama hajawahi kuona mwanamke aliyesuka rasta akiwa amevaa suruali na shati!

“Kuna kichaa hukuu!” Jamaa alibwata huku akiruka nyuma hali ametumbua macho kwa woga mkubwa kabisa..

“Hah! Mi’ kichaa? Hebu nipeleke kwa DC halafu uone ka’a mi’ kichaa! Kuna balaa kubwa limetokea huko msituni…tulikuwa tunafanya utafi—” Nilimchachamalia, lakini hapo nilimuona yule dada niliyetarajia kumkuta pale mapokezi akiingia eneo lile kutoka kwenye chumba ambacho nilikijua kuwa kilikuwa ndio ofisi ya mkuu wa wilaya, akiwa amekumbatia mafaili.

Na wakati huohuo kwa pembe ya jicho langu niliona askari wawili wakiingia pale ofisini.

“Ah! Dada! Afadhali umetokea… ” Nilimdakia yule dada haraka haraka kabla sijatiwa mikononi mwa wale askari, nikaendelea, “…eem, si unanikumbuka mimi? Nilikuja na wenzangu…kwa ajili ya utafiti…? Kutoka Idara ya Makumbusho ya Taifa?”

Yule dada alinitumbulia macho kwa mshangao, kisha nikaona kuwa alinikumbuka.

Yee-ees…nakukumbuka…lakini mbona hivyo? Wengine wako wapi…?” Alisema huku akiweka yale mafaili mezani haraka na kunisogelea huku naye akiniangalia kifuani na kunitazama tena usoni kwa namna ya ajabu.

Hawa watu wanashangaa nini?

Niliwageukia wale askari, nikaona wamesimama bila maamuzi baada ya kuona kuwa yule dada ananifahamu. Bila shaka waligundua kuwa kumbe sikuwa kichaa kama alivyopayuka yule bwege niliyemkuta pale mapokezi.

“Ni balaa kubwa…” Nilianza kumueleza yule dada lakini sikumalizia sentesi yangu, badala yake nikafuata macho yake yaliyokuwa yamekodolea sehemu ya tumbo langu, huku nikimsikia yule jamaa niliyemkuta pale mapokezi akisema, “Huyu lazima ni chizi tu…”

Niliinamisha uso wangu na kujitazama tumboni na hapo hapo nilihisi mwili ukifa ganzi. Nikaelewa kwa nini hata yule bwege aliniona kichaa. Shati langu lilikuwa limefunguka vifungo vyote bila ya mimi kuwa na habari na hivyo nilibaki kidari wazi kabisa! Zaidi ya sidiria iliyoficha matiti yangu madogo, sikuwa na kitu kingine chochote chini ya shati lile ambalo sikuwa nimelichomekea ndani ya suruali yangu iliyosheheni vumbi.

Nilikuwa nimetapakaa jasho lililochanganyika na kamasi, nguo zangu zikiwa zimegandiwa na mabaki ya matapishi niliyojitapikia huku nikikimbia,vumbi likiwa limenitapakaa mwili mzima. Kwa hakika walikuwa na haki ya kunishangaa na kuniona kichaa.

Mtoto wa kike unatembea ovyo mitaani kidari wazi isipokuwa kwa sidiria tu hali shati chafu likipeperushwa hewani kwa upepo kama muhuni!

Ile kuonekana sidiria tu lilikuwa ni jambo la ajabu sanakatika mji kama ule, sasa ukichangia na jinsi nilivyochafuka, na jinsi nilivyokuwa nimetumbua macho kwa woga hali mirasta yangu ikiwa shaghalabaghala huko kichwani, lazima nionekane mwehu.

Shit!” Nilifunga vifungo vya shati langu haraka haraka huku nikitamka maneno ya kumtaka radhi yule dada. Na hata nilipokuwa nikihangaika kufunga vifungo vya shati langu lililotapakaa matapishi na damu, nilimuona yule dada akiinua macho yake kuwatazama wale askari na kuwatolea ishara fulani, kisha aligeuka na kuanza kurudi tena kule ofisini kwa mkuu wa wilaya.

Kabla sijajua la kufanya au la kusema, wale askari walinikamata kwa nyuma na kunisukumia ndani ya ofisi ile ambako yule dada alielekea.

Hey! Heeeey! What the…niacheni bwana! Nataka kuonana na mkuu wa wilaya!” Nilibwata kwa sauti huku nikijitikisa kutoka mikononi mwa wale askari bila mafanikio.

“Tulia bibie! Ndiko tunapoelekea!” Mmoja wa wale askari aliniambia kwa ukali. Sikuelewa ni nini kilikuwa kinatokea, lakini nilijua kuna tatizo. Kuna jambo halikuwa sawa.Niliingizwa ndani ya chumba ambamo mkuu wa wilaya alikuwamo.

Alikuwa ameketi kwa utulivu nyuma ya meza yake kubwa, lakini nyuma ya utulivu ule niliweza kuona kuwa yule mama alikuwa anajitahidi sana kuficha wasiwasi mkubwa.

Aliinuka kutoka kwenye kiti chake na kunielekeza niketi kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake. Niliketi nikiwa na wasiwasi mkubwa huku wale askari wawili wakisimama kila upande wa kiti nilichokalia wakati yule dada akifunga mlango kwa ndani na kubaki akiwa amesimama kando ya mlango ule.

“Asante Matilda…nadhani unaweza kwenda kupiga simu sasa.” Mkuu wa wilaya alimwambia yule dada ambaye alitoka huku akijibu kwa sauti ya chini “Yes madam.

“Binti…ni nini kimetokea? Mbona umekuwa hivyo?” Mkuu wa wilaya aliniuliza kwa upole kana kwamba alikuwa anaongea na mtoto mdogo.

“U…unanikumbuka mheshimiwa…? Naitwa Tigga…nilikuja na wenzangu hapa ofisini kwako siku chache zilizopita?” Nilimuuliza kwa mashaka huku nikiwatazama wale askari wawili kwa zamu. Walikuwa wameshikilia bunduki zao aina ya SMG mikononi mwao kana kwamba wako na mhalifu hatari sana. Nilimeza mate kwa woga na kumgeukia tena yule mkuu wa wilaya.

“Nakukumbuka binti…ni katika ile Manyoni Expedition…lakini mbona hivi? Kumetokea nini? Wenzako wako wapi?” Aliniuliza.

“Wote wameuawa…! Wenzangu wameuawa kinyama mheshimiwa. Mi’ nimefanikiwa kutoroka…inatisha sana!” Niliropoka.

Badala ya kuonekana kushtushwa na taarifa ile, yule mama aliketi kwenye kiti mbele yangu,akawatazama wale askari kisha akanigeukia.

But are you alright? Nadhani unahitaji matibabu…tukupeleke hospitali kwanza?” Aliniambia kwa kujali. Nilitikisa kichwa kwa nguvu.

“Mi’ niko salama kabisa mheshimiwa…ila wenzangu wote wameuawa nakwambia! Nd’o nimekuja kutoa taarifa na kuomba msaada. Wamewaua wote!” Nilimwambia kwa sauti iliyojaa kitetemeshi.

“Wameuawa? Nani amewaua?” Mkuu wa wilaya aliniuliza huku akinitazama kwa namna ambayo sikuielewa kama ilikuwa ni wasiwasi au huzuni.

“Macho ya Nyoka…na Kigulu…na mwenzao.” Nilimjibu, na hapo nikaona kuwa nilizidi kutoeleweka, huku ikinifunukia kuwa yule mama naye aliniona mwehu.

Ee Mungu wangu, hebu nisaidie kiumbe wako!

“Macho ya Nyoka? Binti, una uhakika na maneno yako? Ni nini hasa kilichotokea…hebu tulia utueleze kwa kituo.” Aliniambia.

Nikaanza kumuelezea mambo yaliyotokea kule msituni kwa kadiri nilivyoweza kuyakumbuka. Na kadiri nilivyokuwa nikimuelezea, ndivyo uzito wa matukio yale ulivyozidi kunielemea, nikaanza kububujikwa machozi.

Sijui ni kwa nini, lakini nilikuwa nikimuelezea matukio yale kama jinsi mimi nilivyoyaona, na sio kama jinsi mambo yalivyotokea kule msituni na jinsi mimi nilivyoyachukulia. Badala ya kumueleza kuwa niliona mtu akiteswa nami nikaanza kurekodi matukio yale kwa kamera ya Gil, nilimuelezea tu kuwa niliona jinsi wale watu watatu wakimtesa na kumuua yule mtu, na jinsi nilivyowakuta wenzangu wakiwa wameuawa kule msituni kwenye kambi yetu. Baada ya kumaliza maelezo yangu nilibaki nikilia kwa kwikwi huku nikiwa nimefunika uso wangu kwa viganja vya mikono yangu. Ofisi yote ilikuwa kimya.

“Pole sana binti…” Hatimaye yule mama aliniambia kwa sauti ya upole, na kuiacha kauli yake ikielea kana kwamba kuna la ziada alilotaka kuniambia. Niliinua uso wangu na kujifuta machozi kwa mkono wa shati langu chafu.

“…na nataka nikujulishe kuwa kuanzia sasa uko chini ya ulinzi mpaka hapo maelezo yako yatakapofanyiwa uchunguzi wa kina.” Alimalizia.

“Hah?” Nilimaka kwa mshituko huku nikiinuka kutoka pale kitini, lakinimikono yenye nguvu ya wale askari ilinikamata mabega na kunikalisha tena kitini.

“Mama! Yaani huniamini? Kwa nini niwe chini ya ulinzi? Mimi ni mfanyakazi wa Idara ya Makumbusho ya Taifa, na wewe unajua hilo…mbona sielewi?” Nilimuuliza kwa jazba huku nikijaribu kuinuka, na kwa mara nyingine nikidhibitiwa pale kitini na wale askari..

“Taarifa zako zote tunazo, Tigga…au nikuite Sylvia?” Yule mama alinijibu huku akinikazia macho makali. Hili lilinishangaza, na nikashindwa kulielewa kabisa.

Eh! Haya makubwa!

“Mbona sikuelewi mheshimiwa? Kwa nini uniite Sylvia? Mi’ naitwa Tigga! Tigga Mumba! Na ni taarifa gani za kwangu ambazo mnazo?” Nilimuuliza yule mheshimiwa huku moyo ukinienda mbio na akili ikinizunguka.

Badala ya kunijibu, yule mama alinikabidhi karatasi iliyokuwa juu ya meza yake. Bila ya kuelewa, niliipokea ile karatasi huku mikono ikinitetemeka na kuanza kuisoma. Yaliyoandikwa kwenye ile karatasi yalibadilisha kabisa mtiririko wa maisha yangu. Yalikuwa ni mambo ya ajabu na ya uongo usio kifani. Moyo ulinilipuka na ukaanza kunienda mbio mara dufu. Akili ilinizunguka na nikashindwa kabisa kuelewa ni nini maana ya mambo yale.

This is ridiculous!

Nilikuwa natazama karatasi iliyokuwa ina picha yangu ya ukubwa wa pasipoti kwenye kona ya kulia na maelezo chini yake. Ile picha sio kama ilikuwa imebandikwa, bali ilikuwa imetolewa kivuli moja kwa moja kwenye ile karatasi. Ilikuwa ni sura yangu bila shaka.

Maelezo yaliyokuwa kwenye karatasi ile yalinielezea kuwa mimi nilikuwa naitwa Sylvia Mwamkonda, nikiwa na umri wa miaka ishirini na saba, umri ambao ni wa kweli kabisa na hata tarehe yangu ya kuzaliwa iliyotajwa pale ilikuwa ni sawa kabisa!

Yale maelezo yalikuwa yanamtahadharisha Mkuu wa wilaya ya Manyoni kuwa mtu huyo aitwaye Sylvia Mwamkonda (yaani mimi) ni hatari sana kwani anasumbuliwa na ugonjwa wa Paranoid Schizophrenia, ambao ni ugonjwa mbaya sana wa akili unaoweza kumpelekea kufanya vitendo vya hatari vinavyoweza kuhatarisha maisha yake na ya wengine watakaokuwa jirani naye.

Kutokana na ugonjwa huu hatari wa akili, mtajwa hapo juu (yaani Sylvia, ambaye ndiye mimi) ametokea kuwa hatari kwa wengine na kwake yeye mwenyewe. Kwa hali hiyo basi,anatakiwa awekwe kwenye hospitali maalum za wagonjwa wa akili kwa matibabu na kwa usalama wake na wa wengine.

Kwa mujibu wa maelezo ya barua ile iliyotoka Idara ya Makumbusho ya Taifa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo (jina na saini yake vyote ni sahihi kabisa kama jinsi mimi nilivyovijua) ni kwamba Idara ya Makumbusho ya Taifa imegundua juu ya ugonjwa huu wa Sylvia (ambaye ni mimi) baada ya kupokea ripoti ya daktari aliyemfanyia uchunguzi baada ya uongozi wa Idara hiyo kumpeleka kwa matibabu wakati alipoanza kuonesha dalili za ugonjwa huo.

Barua ilieleza kuwa bahati mbaya walipokea ripoti hiyo wakati Sylvia akiwa tayari ameshatumwa kuelekea Manyoni kikazi pamoja na wenzake. Kwa hali hiyo basi, Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho ya Taifa, kwa kupitia barua ile, alikuwa anaiomba ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni kumweka chini ya ulinzi mara moja mtu huyo anayeitwa Sylvia mara tu atakapoonekana popote pale katika wilaya ile kwa usalama wake na hasa wa watafiti wenzake aliotumwa pamoja nao kikazi huko Manyoni,na raia wengine wasio na hatia ambao wanaweza kudhuriwa naye.

Mwisho, barua ile ilimuagiza mkuu wa wilaya apige namba ya simu iliyokuwamo kwenye waraka ule mara moja pindi atakapofanikiwa kumuweka chini ya ulinzi mtu huyo hatari aitwaye Sylvia Mwamkonda. Ile namba haikuwa miongoni mwa namba za Idara ya Makumbusho ya Taifa nilizozijua.

Ni nini kinatokea hapa?

Nakala ya barua ile ilikuwa imepelekwa kwa wakuu wa vituo kadhaa vya polisi jijini Dar es Salaam, Dodoma na pale Manyoni. Pia nakala ya barua ile ilikuwa imepelekwa kwa mganga mkuu, hospitali ya wagonjwa wa akili ya Mirembe. Akili ilinicheza.

Paranoid Schizophrenia!

Sikuamini kama mambo yale yalikuwa yanatokea kweli. Nilimtazama yule mkuu wa wilaya kwa hasira.

Is this some kind of a joke?” Nilimuuliza iwapo ule ulikuwa ni utani wa aina fulani, lakini badala ya kunijibu yule mama aliendelea kunitazama kwa utulivu. Niliitazama tena ile karatasi. Niligundua kuwa ilikuwa imetumwa kwa njia ya fax siku ileile, kiasi cha saa moja tu iliyopita. Tatizo namba ya fax iliyotumika kutumia ujumbe ule haikuonekana pale juu ya karatasi.

These guys are really good! Yaani wameweza kughushi vitu kama hivi?

“Huu ni uzushi mtupu, Mheshimiwa!” Nilimwambia kwa jazba, na bado yule mama alizidi kunitazama tu bila ya kunijibu. Nilivuta pumzi nyingi na kuzishusha kwa utulivu.

“Mheshimiwa, sijui ni kwa nini umeletewa ujumbe huu, lakini nakuhakikishia kuwa huu ni uzushi na uongo mtupu! Mimi sio Sylvia, mimi naitwa Tigga Mumba kama nilivyotambulishwa kwako na bwana Ibrahim Geresha…marehemu Ibrahim Geresha, siku ile tulipokuja hapa ofisini kwako kwa mara ya kwanza. Nadhani kuna kitu kinafanyika ambacho bado hatujakielewa hapa…” Nilijitahidi kumweleza kwa utulivu ili nisizidi kuonekana kichaa.

“Sasa hapa sio mahala pake msichana. Utaenda kutoa maelezo kwenye vyombo vinavyohusika…wewe ni mgonjwa na unahitaji msaada wa kitaalam, hapa unashikiliwa kwa usalama wako tu, na si vinginevyo…”

“Mimi sio mgonjwa bwana! Nakwambia hii ni njama tu…sijui ni kwa nini, lakini nakuhakikishia kuwa hii ni ghilba kubwa kabisa! Naomba unisaidie mheshimiwa…wenzangu wameuawa, bila shaka na mi’ ningeuawa huko…bila msaada wako nitafanyaje mimi?” Nililalamika kwa kuomboleza.

“Na hilo ndilo haswa tunalopaswa tujiulize Sylvia…”

“Mimi sio Sylvia jamani!” Nilimkatisha yule mheshimiwa huku nikifoka na kunyanyuka kutoka pale kwenye kiti.

Mmoja wa wale askari aliruka mbele yangu na kuninyooshea mtutu wa bunduki yake.

“Kaa chini mwanamke!” Alinikemea, nami nilimtazama kwa hasira huku nikiketi.Aliendelea kunielekezea ile bunduki nikiwa nimeketi pale kitini.

“…tunapaswa tujiulize kwa makini sana Sylvia ni kwa nini katika watu wote waliouawa, tena wote ni wanaume, uokoke wewe tu Sylvia, mtoto wa kike…lazima tujiulize sana juu ya hilo.” Mkuu wa wilaya aliendelea kunieleza huku akinitazama kwa makini. Ilikuwa kana kwamba anajaribu kunichokoza makusudi… au anayepoteza muda makusudi kwa kuniongelesha namna ile.

Kwa nini?

Nilikumbuka kuwa wakati mimi nilipoingizwa mle ofisini mwake mkuu wa wilaya alimuagiza yule dada akapige simu…

“Khah! Unamaanisha nini sasa…?” Nilimuuliza kwa mshangao.

“Labda ulinusurika na kifo kwa sababu ulishindwa kujiua mwenyewe Sylvia…”

Whaaaat?” Niliropoka kwa sauti, nikataka kuendelea, “Yaani—”

“Wewe ni mgonjwa Sylvia…Paranoid Schizophrenia ni ugonjwa hatari sana, unaweza kuwaua wenzako bila kujijua halafu ukaamini kuwa watu walikuja kuwaua na wewe ukafanikiwa kutoroka…vitu hivi vipo…”

Nilibaki nikimkodolea macho yule mama hali nikiwa mdomo wazi. Na hata pale nilipokuwa nikimkodolea yule mama, nilijua kuwa nilikuwa nimenasa. Sasa naonekana mimi ndiye niliyeua! Hii sio kweli…haiwezekani!

“How do you know all this? Just from this piece of rubbish?” Nilimuuliza kwa kebehi huku nikimpungia ile barua, nikihoji amewezaje kujua mambo yote yale, na iwapo ameyajua kutokana na ile barua ya kughushi ambayo niliifananisha na takataka tu.

“Hapana Sylvia, baada ya kupata hii taarifa nilipiga hiyo namba ya simu nikaongea na dokta wako, dokta Martin Lundi…”

“Dokta wangu? Hivi nyie watu mnapata wapi ujingaujinga wa aina hii? Mimi sina dokta yoyote na ndio kwanza leo nalisikia hilo jina…”

“Ni vigumu sana kwako kuelewa Sylvia…”

“Mimi sio Sylvia jamani mbona sieleweki?” Nilimkatisha yule mama kwa ukali.

Alinitazama kama jinsi ambavyo wewe unavyoweza kumtazama mtu unayemjua kuwa ni mgonjwa wa akili, lakini yeye mwenyewe akawa anakuhakikishia kuwa yeye ndiye daktari bingwa wa magonjwa ya akili. Kwa kweli nilichanganyikiwa. Nilijaribu kufikiri haraka sana ni jinsi gani nitafanikiwa kuifuta imani ile potofu  iliyomkolea ubongoni yule mama kuwa mimi ni mwehu.

Sikupata namna, na badala yake nikaanza kujihisi  kuwa ndiyo ninaigiwa rasmi na wazimu.

Nifanyeje sasa Mungu wangu?

Mara nilipata wazo. Nitawahakikishia kuwa huu ni uongo mtupu kwa kuwapa ushahidi kuwa mimi sio Sylvia bali ni Tigga. Nilianza kulivua begi langu kutoka mgongoni kwangu haraka. Lakini kama umeme wale askari walinibana mikono hali yule mwingine akiniwekea mdomo wa bunduki yake kifuani.

“Tulia kama ulivyo! Ukileta ujanja tutakupiga risasi!” Mmoja wa wale askari alifoka.

“Nataka niwaoneshe uthibitisho tu kuwa mimi sio Sylvia bali ni Tigga!” Nilibwata huku nikiuweka chini mkoba wangu.

Walibaki wakinitazama. Nilianza kuinama na kupeleka mikono yangu ndani ya lile begi lakini walinizuia tena. Nilimtazama mkuu wa wilaya.

“Mama, naomba nitoe kitambulisho na pasipoti yangu…vitathibitisha kuwa mimi ni Tigga Mumba na sio Sylvia-sijui-nani-sijui-huko kama wanavyodai hao walioandika hiyo barua…” Nilimwambia.

Mkuu wa wilaya alinitazama kwa mashaka.Nilimuona akijishauri iwapo anikubalie au la.

“Sasa ukinizuia utajuaje kuwa ni kweli unaniweka chini ya ulinzi kama Sylvia-sijui-nani-sijui au Tigga Mumba?” Nilimuuliza.

“Askari atafanya hiyo kazi, wewe tulia kama ulivyo.” Mkuu wa wilaya aliniambia huku akimwamrisha kwa kichwa mmoja wa wale askari aupekue mkoba wangu.

Na hapo nikaliona kosa langu.

Vipi wakiikuta ile kamera halafu wakaamua kuuchukua ule mkanda wenye ushahidi? Mungu wangu! Sasa nitakuwa na uthibitisho gani juu ya kutohusika kwangu na mauaji yale?

Askari alianza kulipekua lile begi langu. Kwa moyo uliopiga kwa nguvu nilishuhudia akiitoa ile kamera na kuiweka juu ya meza bila ya kusema lolote. Nilimtazama mkuu wa wilaya. Naye hakuwa akiitilia maanani ile kamera, ila macho yake yalikuwa yakiangalia kwa makini kila kitu kilichokuwa kikitolewa kwenye begi lile.

Lilikuwa ni begi dogo, na ndani yake nilikuwa nimeweka nguo zangu za ndani, leso za kujifutia jasho, pedi za hedhi, miwani yangu ya jua, pamoja na simu yangu ya kiganjani ambayo ilikuwa imeshaishiwa chaji, pamoja na chaja yake.

Pia kulikuwa na walkman yangu ya CD, CD mbalimbali za muziki pamoja na kitambulisho changu cha kazi, kadi ya benki, pasipoti, kijitabu kidogo cha anuani pamoja na albamu ndogo ya picha ambayo mara nyingi huwa nasafiri nayo kwa ajili ya kujikumbusha picha za ndugu na mama yangu pindi nikiwa mpweke safarini.Zaidi ya hapo, kulikuwa kuna pesa kiasi cha shilingi laki nne hivi, sehemu ya matunda ya per diem za safari, fadhila za Idara ya Makumbusho ya Taifa.

Yule askari alitoa kitu kimoja baada ya kingine na kuviweka juu ya meza ya mkuu wa wilaya, akifinya sura yake pale alipolazimika kuzishika nguo zangu za ndani, hasa zile pedi za hedhi. Alitoa vitu vyote na kudai kuwa amemaliza, nami nikamtazama kwa mshangao.

“Mbona sijaona pasipoti na vitambulisho vyangu?” Nilimuuliza huku nikianza kuinuka. . “Kwa sababu havimo na havikuwemo toka mwanzo!” Mkuu wa wilaya alinijibu huku yule askari mwingine alinikalisha tena kitini kimabavu.

What do you mean kwa sababu havimo?”Nilifoka kwa hamaniko, kisha nikamgeukia yule askari aliyekuwa amelipekua lile begi na kumbwatia, “Hebu angalia vizuri wewe…!” Yule mama alionekana kuwa ametosheka kwamba nilikuwa nasema uongo na kwamba mimi kwa hakika ni Sylvia-nani-sijui kama ilivyoelezwa kwenye ile barua feki.

“Hakuna uthibitisho wowote kwenye begi lako Msichana, kwa hiyo acha kupoteza muda wetu.” Alisema kwa hasira.

“Haiwezekani! Kunatakiwa kuwe na kitambulisho changu cha kazi humo…kinaonesha kuwa mimi ni Tigga Mumba!” Nilimaka kwa kitetemeshi.

Na hata pale nilipokuwa nikiongea maneno yale, yule askari alilikung’uta kwa nguvu lile begi, na hakuna kitu zaidi kilichotoka.

“Hakuna.” Yule askari alisema kana kwamba anaijibu ile kauli yangu.

Akaligeuza lile begi nje ndani na kulikung’uta tena.

Hamna kitu.

Nilichanganyikiwa!

“Hah! Yaani…kikadi changu cha benki…?”

“Hakuna!” Mkuu wa wilaya alinijibu kwa kukatisha tamaa.

“Na pasipoti yangu…?”

“Hakuna!”

“Simu yangu ya mkononi…?”

Yule mama alinitazama na kutikisa kichwa kwa kukatisha tamaa huku akibetua midomo yake.

Oh! Mungu wangu, balaa gani hili sasa?

“Kulikuwa pia kuna albamu yangu ya picha humo…”

“Haimo!” Mkuu wa wilaya alinijibu huku akipekua lile rundo la nguo zangu za ndani pale juu ya meza, kisha akatupia macho yake kwenye ile kamera ya Gil pale mezani kwa muda.

Nilibana pumzi huku nikimtazama kwa wasiwasi.

Alihamishia macho yake kwenye ile walkman yangu, nikashusha pumzi ndefu, kisha akatazama zile CD chache za muziki kando yake. Akahamishia macho yake kwenye zile pesa zangu zilizokuwa zimefungwa vizuri kwa mpira maalum yaani rubber band, kando yake ikiwapo ile miwani yangu ya jua. Akanitulizia macho.

“Una lolote zaidi la kutueleza Sylvia?”

Sikuwa na jibu. Akili ilikuwa ikinizunguka kwa kasi sana na nilihisi kizunguzungu.

Sasa vitu vyangu vingine vitakuwa vimekwenda wapi?

Nilikumbuka kuwa nililikuta begi langu nje ya hema langu kule msituni, wakati nililiacha ndani. Nikaelewa.

“Watakuwa wamevichukua wale wauaji…” Nilisema kwa sauti hafifu. Nilikuwa nikijisemea mwenyewe, lakini wote mle ndani walinisikia.

“Mh! We’ binti acha kufanya mchezo na mimi, umesikia? Ni wauaji gani hao wa kufikirika unaotuambia?” Mkuu wa wilaya alinikemea kwa hasira.

“Kigulu na Macho ya Nyoka?” Yule askari mmoja aliniuliza kwa kejeli. Niliona kuwa hapa tayari nilikuwa nimethibitika kuwa mgonjwa wa akili.

Paranoid Schizophrenia!

Nilimtazama, nikajaribu kusema kitu nikashindwa.

Niseme nini?

Nilikuwa nimekwama. Niliamua kunyamaza kusubiri hatima yangu huku akili ikinizunguka. Lakini kitu kimoja nilichokuwa na uhakika nacho ni kuwa pale hapakuwa mahala pa kuutoa ule ushahidi wa mkanda wa video niliokuwa nao. Sijui ni kwa nini, lakini hivyo ndivyo nilivyohisi na ndivyo nilivyoamua.

Yule askari mwingine alianza kuvikusanya vile vitu vyangu na kuvirudisha tena ndani ya lile begi langu. Nilimtazama huku moyo ukinidunda akiitumbukiza tena ile kamera ndani ya begi.Nilishusha pumzi.Alipolifikia lile burungutu langu la pesa alisita kwa muda, kama aliyekuwa akijishauri iwapo azirudishe kwenye begi langu au azihamishie mfukoni mwake. Nilimtumbulia macho kwa hasira naye akaamua kuzirudisha kwenye begi langu. Na hapo yule dada aliyeitwa Matilda alirudi mle ofisini.

“Dokta Martin Lundi amefika Mheshimiwa.” Alimwambia mkuu wa wilaya na moyo ukaanza kunienda mbio. Mkuu wa wilaya aliagiza aingie ndani nami nikaukodolea macho mlango kumtazama huyo daktari wangu Martin Lundi.

Watu watatu waliingia ndani haraka haraka. Wote walikuwa wamevaa makoti marefu meupe juu ya nguo zao za kawaida, na hapakuwa na shaka kuwa walikuwa wauguzi au madaktari. Moyo ulinilipuka na nikataka kupiga yowe lakini sauti ikakwama ghafla. Nilikuwa nikimkodolea macho mmoja wa wale watu watatu walioingia ambaye alionekana kuwa ndiye kiongozi wa jopo lile la matabibu.

Mkuu wa wilaya alisimama na yule daktari aliyeonekana kuwa ndiye kiongozi alikwenda moja kwa moja hadi kwa mkuu wa wilaya na kumpa mkono huku akijitambulisha.

“Naitwa Martin Lundi…Dokta Martin Lundi, tuliongea kwenye simu.”

“Nimefurahi kuonana nawe Dokta, nadhani mgonjwa wako ndiye huyu?” Mkuu wa wilaya alimwambia huku akinioneshea kwa kidole.

Yule mtu alinigeukia na uso wake ulifanya tabasamu dogo kama jinsi ambavyo madaktari wengi wanavyofanya pindi wakianza kuongea na wagonjwa wao.

Hallo Sylvia, unajisikiaje leo?” Aliniuliza taratibu huku akinisogelea, na hapo ndipo nilipopata nguvu ya kuongea, baada ya muda wote kuwa nimepigwa na bumbuwazi, kwani yule mtu aliyejiita dokta Martin Lundi alikuwa ndiye yule muuaji wa tatu, ambaye alikuwa akiendesha ile helikopta kule msituni!

“Ndiye huyu! Huyu ni mmoja wa wale wauaji mheshimiwa! Usimruhusu anishike!” Niliruka ghafla kutoka kwenye kiti changu na kumkimbilia yule mkuu wa wilaya huku nikimkwepa yule muuaji huku nikipayuka.

Kilichofuatia hapo ni kizaazaa kizito.

Wale askari hawakutegemea tendo lile hivyo niliweza kumfikia mkuu wa wilaya ambaye alipiga yowe kubwa la woga, bila shaka kichwani mwake akiamini kuwa nilikuwa ni mgonjwa wa akili hatari na muuaji.

Haraka sana mmoja wa wale wasaidizi wa yule jamaa aliyejiita Dokta Martin Lundi alinirukia na kunikamata mkono. Nilimzaba kofi la uso na kuanza kuuendea mlango kwa kasi lakini wale askari walizinduka. Walinielekezea bunduki zao huku wakifoka kuwa nikae chini haraka.

Nilisimama huku nikitetemeka, nikimtazama yule jamaa aliyejiita Martin Lundi.Ingawa kule msituni alikuwa amevaa miwani ya jua na koti refu jeusi, na sasa alikuwa amevaa miwani ya macho na chini ya lile koti lake refu jeupe alikuwa amevaa shati na tai, bado niliweza kumtambua vizuri sana.

“Huyu ni moja wa wale wauaji Mkuu!” Nilibwata tena huku nikimnyooshea kidole.

Na hata pale nilipokuwa nikipiga mayowe kuwa yeye ni mmoja wa wauaji, niliushuhudia uso wake ukionesha mshangao wa hali ya juu ambao haraka ukawa woga mkubwa, kisha hapo hapo hisia zote zile zikafutika haraka sana usoni mwake.

Alimgeukia mkuu wa wilaya na kujaribu kufafanua huku akitabasamu.

“Ah! Paranoid Schizophrenia…kila mtu anamuimagine kuwa ni adui…ndilo jambo baya zaidi katika ugonjwa wa Sylvia…” Alimwambia, akimaanisha kuwa ule ugonjwa ulikuwa unanifanya nimfikirie kila mtu kuwa ni adui, akiwemo yeye mwenyewe. Na nilipomtazama mkuu wa wilaya niliona kuwa alikuwa ametishika sana na ile purukushani fupi na wakati huohuo maelezo ya yule daktari bandia yakionekana kuleta maana sana kwake.

“Acha uongo wako wewe! Mimi sio Sylvia na we’ unajua hilo! Nyie ndio mmemuua yule mtu kule msituni…” Nilimkemea yule jamaa huku wale wenzake wawili wakinishika kwa nguvu kutokea nyuma na wale askari wakinielekezea bunduki zao. Kwa mara nyingine tena uso wa yule jamaa ulionekana kushtushwa na maneno yangu.

“Ooo, Sylvia, Sylvia…usiwe na wasiwasi.Sasa hivi nitakupa dawa yako na utajisikia vizuri…” Aliniambia huku akinisogelea taratibu.

“Mimi siyo Sylvia wewe, Fala nini? Mimi ni Tigga Mumba na we’ sikujui na wala hatujawahi kujuana hata siku moja!” Nilimpigia kelele huku nikijikukurusha kutoka mikononi mwa wale wasaidizi wake bila mafanikio.

Yule jamaa alimgeukia tena mkuu wa wilaya na kujaribu kufafanua tena hali ile.

Actually hii ni dalili mojawapo ya ugonjwa huu, mgonjwa kujiamini kuwa yeye ni mtu fulani tofauti na utambulisho wake halisi…eeenh, hali hii kitaalamu tunaiita echolaliaandechopraxia…inaweza kumfanya mgonjwa hata afikie kuiga mwendo, sauti au tabia ya mtu fulani na kuamini kuwa yeye ndiye huyo mtu.”

Duh! The guy is really good!

Nilielewa kilichokuwa kinafanyika pale. Yule jamaa alikuwa anatumia kila jambo nililokuwa nikilifanya kujaribu kuthibitisha ukweli wa maelezo yangu na kumbainisha kuwa yeye ni miongoni mwa wauaji, kuwa ni njia ya yeye kuthibitisha kuwa kweli mimi nilikuwa mgonjwa wa akili.

Na mkuu wa wilaya pamoja na wale askari walionekana kuamini kila kitu alichokuwa akikieleza, nami nilizidi kuonekana kichaa.

“Mnh!(nilisonya), eti ekolalia and ekopraksha! We’ acha uongo wewe!” Nilimkemea yule mtu muongo aliyejiita dokta Martin Lundi, lakini bado niliona kuwa maneno yake ndiyo yaliyoaminika kuliko lolote nililosema na nitakalosema.

Yule mtu alimuashiria mmoja wa vibaraka wake ambaye alifungua mkoba waliokuja nao na kutoa sindano na kichupa kidogo kilichokuwa na dawa ya majimaji.Nilijua kuwa walitaka kunidunga sindano ya kunidhuru, wakijidai ni dawa kutokana na hayo maradhi waliyonipakazia.

Oh, Mungu wangu! Hii itakuwa sindano ya sumu tu…nifanyeje?

Mtu aliyejiita Martin Lundi aliipokea ile sindano kutoka kwa yule kibaraka wake na kujitia kuangalia kiwango cha dawa kilichowekwa ndani ya bomba la ile sindano.

Niliamua kubadilisha mtindo.

“Mheshimiwa usimwamini hata kidogo huyu mtu. Huyu ni muuaji…yeye na wenzake wawili ndio waliofanya mauaji ya kinyama kule msituni…yaani ukimwachia tu anichukue hapa basi jiandae kuokota maiti yangu katika msitu wa jirani.These guys are killers!” Nilimwambia yule mkuu wa wilaya kwa kuomboleza huku nikijitahidi kuiweka sauti yangu chini ili nisionekane mwehu.

Lakini mkuu wa wilaya alikuwa haambiwi hivyo.

“Wewe ni mgonjwa Sylvia na unahitaji tiba.” Aliniambia kwa msisitizo.

Nilitikisa kichwa kwa kukata tamaa. Nilitazama mazingira yalivyokuwa mle ndani. Wale askari wawili walikuwa wamesimama mbele yangu kiasi cha hatua za mtu mzima zipatazo kumi hivi wakiwa wameninyooshea bunduki zao.

Kushoto kwangu alikuwa amesimama Dokta Martin Lundi muongo, ilhaliMkuu wa wilaya alikuwa amesimama mbele ya meza yake iliyokuwa kulia kwangu. Wale vibaraka wa Martin Lundi muongo walikuwa wamenishika mikono yangu, mmoja kila upande wangu wakiwa kwa nyuma yangu.

Lazima nifanye kitu haraka!

“Mkuu huyu jamaa sio daktari wala nini… muuaji tu huyu, na nakuhakikishia utakuwa na damu yangu mikononi mwako ukimruhusu atoke na mimi hapa kwako mheshimiwa…hebu mwambie akupe kitambulisho chake kama kweli yeye ni daktari, mwongo mkubwa huyu!” Nilimwambia yule mama huku nikimtazama yule mtu aliyejiita Martin Lundi. Hapo hapo yule jamaa alitoa kitambulisho kutoka mfukoni mwake na kupiga hatua moja huku akinyoosha mkono wake kumpa mkuu wa wilaya kile kitambulisho.

“Sylvia ni mgonjwa sana, na nadhani itabidi nimchome sindano yake hapa hapa…” Alisema huku akimkabidhi kitambulisho mkuu wa wilaya ambaye alisogea na kunyoosha mkono wake kukipokea.

Na hilo ndilo nililolitarajia, na ndiyo nafasi niliyokuwa nikiisubiri. Sikufanya makosa.

Wakati waliposogeleana kupeana kitambulisho, kwa sababu nilijua kuwa jamaa atakuwa amejiandaa na kila kitu kuthibitisha kuwa kweli yeye ni Dokta Martin Lundi, wote wawili walijikuta wako mbele yangu na wakati huohuo wakinikinga kutoka kwa wale askari wawili waliokuwa wameninyooshea bunduki zao. Mkuu wa wilaya alikuwa karibu sana nami kiasi kwamba kama nisingekuwa nimeshikwa mikono na wale wasaidizi wa yule mtu aliyejiita Martin Lundi, ningeweza kumshika.

Huku bado mikono yangu ikiwa imeshikwa na wale vibaraka wa Martin Lundi,nilijirusha juu kwa nguvu nikitanguliza miguu yangu na kumbana mkuu wa wilaya kiunoni kwa miguu yangu.

Yule mama alipiga ukelele wa woga na wale jamaa waliokuwa wamenishika walivutwa mbele kunifuata hali mikono yangu ikiwaponyoka. Mkuu wa wilaya alipiga mweleka sakafuni nami nikawa nimembana kwa nguvu kwa miguu yangu hivyo wote tukaenda chini kwa kishindo.

Nilisikia wale askari wakipiga kelele na dokta Martin Lundi akiropoka neno ambalo sikulielewa. Wakati huohuo wale jamaa waliokuwa wamenishika nao wakilalama kila mmoja kinamna yake.

Vyote hivyo sikuvitilia maanani, akili yangu ilikuwa kwa mkuu wa wilaya. Haraka sana nilijiinua huku nikiwa bado nimembana kiunoni kwa miguu yangu na kumtia kabali kwa mkono wangu wa kulia hali nikijiinua kutoka pale sakafuni kwa mkono wangu wa kushoto na nikimbururia pembeni yule mama aliyekuwa akipiga mayowe kwa woga. Nilijua kuwa wale vibaraka wa Martin Lundi muongo walikuwa nyuma yangu hivyo wangeweza kunivamia. Nilimwinua yule mama kwa nguvu na kuyumba naye hadi kando ya meza yake.

Iilikuwa ni tendo la haraka na lisilotarajiwa na wote mle ndani. Wale askari kutahamaki nilikuwa tayari nimemdhibiti mkuu wa wilaya vizuri sana. Martin Lundi alianza kunisogelea.

“Hatua nyingine moja tu namvunja shingo huyu bi kizee wenu hapa!” Nilimkemea kwa hasira. Nilikuwa nimembana kwa kabali kali sana yule mama na nilikuwa nimemuweka mbele yangu kama ngao.

Martin Lundi alisimama na kuwageukia wale vibaraka wake, ambao ndio walikuwa wanajizoa zoa kutoka sakafuni. Wale askari walinielekezea bunduki zao huku wakitweta kwa wasiwasi.

“Mwache mheshimiwa sasa hivi msichana ama sivyo tunakupiga risasi!” Mmoja wao alifoka, nami nikamcheka kwa dharau.

“Wacha ujinga wewe! Utanipiga risasi hapa bila ya kumuanza huyu bi kizee kwanza?”

“Sylvia, haina haja ya kufanya fujo, eeenh? Naomba umwachie mhe—” Martin Lundi alianza kunisemesha kwa sauti ya kubembeleza kana kwamba anaongea na kichaa kweli, na sikusubiri amalize.

“Hebu ninyamazie mimi huko! Unadhani unaweza kunihadaa kama ulivyomhadaa huyu mama hapa?”

Alinichefua!

“Ah! Hebu tumia akili msichana, unadhani utajiokoa vipi hapo wakati umezingirwa na askari?” Martin Lundi muongo aliniambia kwa hasira, akipoteza ule utulivu wake wa bandia.

“Haaa-Loh! We’ mwehu nini? Umesahau kuwa mimi ni mgonjwa wa akili? ParanoidSchizo-nini sijui huko…?Sasa tangu lini mgonjwa wa akili akatumia akili?” Nilimjibu kwa kebehi huku akili yangu ikifanya kazi haraka haraka. Yule jamaa alikosa jibu alibaki akinikodolea macho.

Nilipeleka mkono wangu wa kushoto na kunyakua begi langu lililokuwa juu ya ile meza ya mkuu wa wilaya.

“Waambie mbwa koko wako wateremshe bunduki zao chini mama!” Nilimnong’oneza yule mkuu wa wilaya huku nikining’iniza begi langu begani.

“Unafanya kosa kubwa sana we mtoto…” Alisema kwa taabu yule mama.

“Si kazi yako!We’ si umeamini kuwa mimi mwehu? Kwa hiyo usipoteze muda wako na wangu kumpa mwehu ushauri…do it!” Nilimnong’oneza huku nikijua kwamba ndio nilikuwa najithibitishia shutuma za wazimu.

Mkuu wa wilaya aliwaashiria wale askari waweke chini silaha zao. Wale askari walisita. Nikazidi kumkaba. Yule mama alitoa sauti za kukoroma kutokana na kabali ile. Bado akili ilikuwa ikinitembea.

Baada ya hapa halafu nini sasa…?

“Weka chini silaha askari!” Nilifoka huku nikiongeza nguvu kwenye ile kabali. Bila shaka macho yalimtoka pima yule mheshimiwa kwani niliwaona wale askari wakimkodolea macho kwa woga. Nililegeza kabali.

“Tupa chini!” Mkuu wa wilaya aliropoka na kuanza kukohoa kwa taabu.

“Hapana!” Martin Lundi muongo aliropoka, lakini wale askari walishapata amri ya mkuu wao wa kazi. Walizitupa chini zile bunduki na kubaki wakinitazama kwa hasira.

“Vizuri…sasa nyote rudini nyuma, na muegemee ukuta ule!” Nilifoka huku nikiwatazama wale askari, Martin Lundi muongo na vibaraka wake. Hakuna aliyetikisika. Walibaki wakinitazama.Moyo ulikuwa ukinidunda kwa nguvu sana.

“Hamnielewi?” Nilifoka, lakiniwale watu mle ndani hawakutikisika.Walibaki wakinitazama kwa hasira. Bila shaka waliona kuwa tayari wameshadhalilishwa na mtoto wa kike kiasi cha kutosha na hivyo hawakutaka kuendelea kudhalilika zaidi, liwalo na liwe.

Sasa itakuwaje?

Muda huo mlango ulifunguliwa.Matilda aliingia mle ndani na hapo hapo akaachia mdomo wazi kwa butwaa.Wale askari wakamgeukia, na kwa sekunde mbili hivi hakuna kilichotokea, kisha nilifanya lililostahili.

Kwa nguvu nilimsukuma yule mkuu wa wilaya kwa wale askari huku nikizirukia zile bunduki pale sakafuni.

Matilda alipiga kelele na kurudi mbio kule alipotoka. Wale askari nao waliruka kuziwahi bunduki zao. Wakapamiana na mkuu wa wilaya na wote wakaenda chini kwa kishindo. Kwa kona ya jicho langu nilimuona Martin Lundi muongo akipeleka mkono wake kwenye mfuko wa ndani wa koti lake. Nikaiwahi bunduki moja na kuikanyaga nyingine kwa mguu wangu.

“Wote tulia hivyo hivyo!” Nilifoka huku nikiwa nimeishika ile SMG vizuri sana mikononi mwangu na kuizungusha mle ndani ili kila mtu aone kuwa nilikuwa nina bunduki mkononi, na kuituliza kwa Martin Lundi muongo aliyeganda  akiwa ametumbukiza mkono wake ndani ya koti lake.

“Toa hiyo bastola yako na uitupe chini wewe!” Nilimfokea kwa ukali. Alibaki akinitumbulia macho. Alizidi kunikera.

“Haraka!” Nilifoka kwa hasira na bila kujua nilibonyeza kifyatulio na ile bunduki iliachia mfululizo wa risasi huku ikitoa kelele kubwa.

Hekaheka iliyotokea hapo ilikuwa si mchezo.

Mkuu wa wilaya alilia kama mjinga, wale askari walipiga kelele ovyo. Martin Lundi aliruka huku akipiga yowe kubwa. Risasi zilichimba sakafu hatua chache kutoka miguuni mwake, hali wale vibaraka wake wawili wakijitupa chini kuokoa maisha yao. Na mimi mwenyewe yowe lilinitoka.

Sikuwa nimekusudia kufyatua risasi, wala sikujua ni jinsi gani ya kutumia bunduki ile. Nilijua nimeua mtu, lakini niliona wote bado wazima.

“We kichaa nini? Utaua watu hapa!” Mmoja wa wale askari alibwata akiwa pale chini, huku vilio vya mkuu wa wilaya vikizidi kutawala.

“Kumbe na wewe pia hujui kuwa mimi ni kichaa kama mimi eenh?” Nilimjibu yule askari bila kumtazama, macho yangu yakiwa kwa yule muuaji aliyejiita Martin Lundi.

Tulitazamana. Hasira niliyoiona katika machonimwake ilitosha kabisa kuniambia kuwa nilikuwa natazamana na muuaji.

“Mara ya pili risasi zinaweza zikakupitia na wewe…tupa bastola yako chini!” Nilimfokea.

“Ee mtoto wee! Huyo daktari bastola aitoe wapi lakini…?” Mkuu wa wilaya alilalama akiwa amekaa sakafuni pamoja na askari wake. Na hata pale alipokuwa akisema hivyo, Martin Lundi alitoa bastola yake na kuitupa chini. Kwa pembe ya jicho langu niliona mdomo wa mkuu wa wilaya ukidondoka na kubaki wazi kwa butwaa baada ya kuona kumbe ‘daktari’ wake alikuwa ana bastola. Sikupoteza muda kumsuta, kwani alishajionea mwenyewe.

Niliipiga teke ile bastola ikapotelea uvunguni mwa kabati la vitabu lililokuwemo mle ofisini. Niliipiga teke na ile bunduki nyingine nayo ikapotelea kulekule uvunguni mwa lile kabati.

Huku nikiwa nimewaelekezea bunduki wale watu, nilirudi nyumanyuma kuelekea mlangoni, nilitoka na kuwakuta Matilda na yule bwege niyemkuta pale mapokezi wakihangaika kupiga simu.

“Wacha!” Niliwafokea na wote waliruka na kuanza kurudi nyuma wakiwa wamenyoosha mikono yao juu. Nilisikia purukushani kutokea kule nilipowaacha mkuu wa wilaya wenzake. Haraka niliwafungia kwa nje kwa komeo, nikaisogelea ile simu na kuung’oa waya wake kwa nguvu huku wale watu wawili wakinitumbulia macho kwa woga.

Nikatoka mbio nje ya jengo lile.

Gari la kubebea wagonjwa lilikuwa limepaki mlangoni mwa jengo lile na dereva aliyekuwa amekaa nyuma ya usukani naye alikuwa amevaa koti jeupe kama wale wenzake niliowaacha ndani.

Nilimuwahi kabla hajataharuki na kumwekea mtutu wa SMG shingoni kupitia dirishani. “Toka!” Nilimfokea huku nikifungua mlango wa lile gari. Nilishaona kuwa ufunguo ulikuwa umechomekwa mahala pake. Jamaa alishituka na sikumpa muda zaidi. Nilimvuta kwa nguvu na kumbwaga chini. Raia wachache waliokuwa wakipita na kuzagaa nje ya jengo lile walipigwa butwaa huku wengine wakipiga kelele za woga.

Sikuwajali.

Nilirukia ndani ya lile gari na kuondoka nalo kwa kasi huku nikitimua vumbi na kuitupa nje ile bunduki.

Kupitia kwenye kioo cha pembeni, nilimuona Martin Lundi muongo akitoka mbio nje ya ofisi ile huku akinitupia risasi kwa bastola yake akifuatiwa na wale askari. Nilikunja kona na kuingia kwenye barabara ya vumbi iliyoelekea nje ya mji.

Sikuamini kuwa niliweza kumkaba yule mama namna ile na kuwatoroka wale watu wabaya.

Mungu wangu!Sasa nimekuwa mtu wa aina gani mimi?

Huku nikitokwa na machozi kwa woga, nilikanyaga mafuta na kuzidi kutokomea kwa kasi pasina kujua mbio zangu zingeishia wapi.

SEHEMU YA PILI:

Treni ya reli ya kati iliingia stesheni ya Dar es salaam kwa mbwembwe na vishindo, huku ikipuliza honi yake kali kuwajulisha wananchi waliokuja kupokea ndugu na jamaa zao kuwa ilikuwa imeingia jijini.

Nilijichanganya na abiria wengine kutoka daraja la tatu ambamo ndimo nilipokuwa nikisafiria na kutoka kuelekea nje ya stesheni ile Iliyokuwa na msongamano mkubwa wa watu, kila mtu akihangaika na mzigo au mizigo yake huku wachukuzi wakikimbia huku na huko kutafuta watu wa kuwabebea mizigo.

Wakati huohuo wasafiri wenzangu wakihangaika kutafuta wenyeji wao hali na wenyeji nao wakiwa katika hali hiyo hiyo. Kelele za kila aina zilitawala eneo lote lile. Watoto wadogo walilia ovyo wakiogopa kelele na hekaheka za watu waliojazana na waliokuwa wakipita kuelekea huku na huko ndani ya stesheni ile kubwa ya treni nchini.

 Na ni mchanganyiko na mvurugano huu ndio nilioutaka, kwani uliniwezesha kutoka pale stesheni na kujichanganya mjini kama wasafiri wengine bila ya kugundulika mara moja. Ilikuwa ni saa kumi na nusu za jioni siku ya tatu tangu yalipotokea yale mauaji ya kutisha kule msituni.

Nilikuwa nimevaa gauni refu la maua maua ambalo juu yake nilikuwa nimevaa jaketi zito kama jinsi wengi wa wasafiri waliokuwa wakitokea mikoa ya kanda ya ziwa na kati walivyokuwa wamevaa kutokana na hali ya baridi ya maeneo hayo,na ingawa Dar hakukuwa na mazingira ya baridi kulazimisha watu kuvaa makoti au majaketi, niliendelea kulivaa jaketi lile kwani lilinifanya nionekane kuwa ni msafiri kutoka mikoani kama wengine.

Kichwani nilikuwa nimejifunga kilemba kilichofunika kabisa nywele zangu za rasta, na miguuni nilikuwa nimevaa viatu vyepesi vya kamba vilivyoshika miguu yangu vizuri sana. Begi langu dogo la kuning’iniza mgongoni,likiwa na vitu vyangu vichache vilivyobakia pamoja na ile kamera ya marehemu Gil, nilikuwa nimeliweka ndani ya mfuko wa plastiki na juu yake nilikuwa nimesokomeza doti ya kanga.

Usoni sikuwa nimevaa ile miwani yangu ya jua ingawa nilitamani sana kufanya hivyo ili nisijulikane kirahisi. Nilijua kwamba, kama kuna wanaonitafuta; wawe polisi au wale wauaji, kwa vyovyote vile wangetegemea nivae miwani ili nisijulikane.

Nilichofany a nilipaka wanja mzito kwenye nyusi zangu, ambazo kwa kawaida ni nyembamba na fupi, kuzunguka juu ya macho yangu na kuleta picha kuwa nilikuwa na nyusi ndefu zilizotambaa juu ya macho yangu kutoka kona moja ya jicho hadi nyingine. Pia nilipaka wanja kwenye kope zangu za chini. Kwa mtu aliyenijua vizuri, ingemchukua muda kunitambua kwani kwa kawaida huwa sina kabisa mazoea ya kupaka wanja namna ile.

Nilionekana wa kuja hasa.

Huku bado nikiwa na wasiwasi na moyo ukinienda mbio, nilitembea haraka kutoka eneo lile la stesheni. Niliangaza huku na huko, nikitegemea kusikia sauti kali ikiniita kutokea nyuma yangu, ambapo nilikuwa tayari kutimua mbio.

Lakini sikusikia mtu yeyote akiniita.

Nilivuka barabara na kukata kushoto kuelekea kwenye mnara wa saa ambapo kulikuwa kuna teksi zilizokuwa zikisubiri abiria. Niliingia kwenye moja ya teksi zile na kumwamrisha dereva anipeleke Sinza, nyumbani kwa mchumba wangu, Kelvin.

Nilijua kuwa kufikia sasa nilikuwa natafutwa na wale watu wabaya pamoja na polisi, kwani kizaazaa nilichozusha kule Manyoni kwa mkuu wa wilaya kisingeweza kuachiwa kipite hivi hivi. Yule ni mwakilishi wa rais katika wilaya ile, na kitendo cha kumgaragaza sakafuni na kumkaba namna ile kilikuwa ni kosa kubwa sana. Na kama hivyo ndivyo, kwa vyovyote vile wanaonisaka wangeanzia nyumbani kwangu Upanga nilipokuwa nimepanga, na kwa mama yangu Tabata, hivyo  wangekuwa wakinisubiri huko.

Ndio maana niliamua kwenda kwa mchumba wangu, ambaye nilijua angekuwa na msaada mkubwa kwangu katika janga hili kuliko mama yangu au dada yangu ambao wote walikuwa ni wanawake kama mimi.

Nilitulia kwenye kiti cha nyuma ndani ya ile teksi huku nikiwa nimeukumbatia mfuko wangu wa rambo na kuanza kutafakari matukio ya saa arobaini na nane zilizopita, kuanzia pale nilipotoroka kibabe kutoka kwenye ile ofisi ya mkuu wa mkoa…

 

 

--

Baada ya mwendo mrefu na wa kasi nikiwa na lile gari la kubebea wagonjwa nililoliteka kutoka kwa mmoja wa vibaraka wa dokta Martin Lundi muongo, nilifika kwenye njia panda. Njia moja niliielewa kuwa ilikuwa inaelekea Dodoma mjini na nyingine sikujua ilikuwa ikielekea wapi. Nilifuata ile njia nyingine kwa kiasi cha kama nusu kilometa hivi na kulitelekeza lile gari kando ya barabara.

Niliteremka na kuanza kukimbia kwa miguu kurudi kule kwenye njia panda nikitumia njia ya msituni sambamba na ile barabara. Kwa mbali nilianza kusikia ving’ora vya magari ya polisi na nikajua kuwa msako ulikuwa umeanza.

Baada ya kukimbia kwa muda niliweza kuiona ile njia panda kwa mbali na nilisimama ghafla. Nilijizamisha msituni zaidi na kuanza kutembea taratibu na kwa tahadhari huku moyo ukinidunda. Kutokea kule msituni nilipokuwapo, niliweza kuona magari yapatayo matatu ya polisi yakiwa yamesimama njia panda. Nilizidi kusogea kwa tahadhari kubwa.

Nje ya magari yale kulikuwa kuna kundi la askari waliokuwa wakiangaza huku na huko. Bila shaka walikuwa wakijaribu kung’amua ni njia ipi niliyochukua kati ya zile mbili. Nilizidi kunyata kuelekea kule walipokuwapo ili niweze kuona kilichokuwa kikiendelea. Wale askari walikuwa wakiongea na mwanamke mmoja aliyejitanda kanga akiwa amebeba mtoto mgongoni. Nilikumbuka kumpita kwa kasi huyo mama hatua chache kabla ya kuifikia ile njia panda.

Yule mama alionyesha kidole chake kuelekeza kule kwenye ile njia niliyoelekea na lile gari. Wale askari walionekana kubishana naye kwa muda, lakini yule mama alikuwa akizidi kuionesha ile njia niliyoelekea huku akitikisa kichwa kwa msisitizo. Wale askari waliparamia magari yao kwa pupa na kuondoka kwa kasi kuelekea kule nilipolitelekeza lile gari, huku wakiacha gari moja na askari wawili pale kwenye njia panda.

Nilijua kuwa kwa pale nilikuwa nimewapoteza, hivyo nilizidi kuambaa na msitu ule sambamba na ile barabara iliyoelekea Dodoma mjini.

Mwendo mfupi baadaye niliona lori la mkaa likiwa limepaki upande wa pili wa ile barabara. Kwa jinsi lilivyokuwa limepaki, ni kwamba lilikuwa likielekea maeneo ya Dodoma mjini. Moyo ulianza kunipiga kwa kasi. Nilijificha nyuma ya miti na kuchungulia.

 Dereva na utingo wa lile gari walikuwa wakihangaika kubadilisha tairi lililokuwa limepata pancha. Ingawa nilitamani kwenda kuwaomba msaada, niliogopa kufanya hivyo kwa hofu ya kutiwa mbaroni na kukabidhiwa kwenye vyombo vya dola au kufanyiwa uhuni tu na wale watu, kwani mtoto wa kike kuomba msaada kwenye njia pweke kama ile ilikuwa ni kujitafutia kubakwa tu.

Niligundua kuwa tairi lililokuwa na matatizo lilikuwa la mbele upande wa kushoto. Kwa hali ile wale watu walikuwa upande wa pili wa gari lile na hawakuweza kuniona,kwani hata mimi nilikuwa nawaona miguu na mikono yao tu wakihangaika kufunga hilo tairi.

Nilitazama  kulia na kushoto. Kulikuwa kimya, utingo alitoka na kulitupia lile tairi lililopasuka kule nyuma ya gari kulikokuwa na magunia ya mkaa, kisha akarudi tena kule alipokuwapo dereva wake.Nilibana nyuma ya miti kando ya ile barabara na kusubiri. Ile barabara ilikuwa kimya sana, na hakukuwa na gari hata moja lililopita. Wale jamaa walipomaliza waliingia kwenye lori lao na kuanza kuondoka kwa mwendo mdogo kama nilivyotarajia kutokana na uchakavu wa lile gari na mzigo ililobebeshwa. Nilichomoka mbio huku nikivuka ile barabara, nilidandia lile lori na kujilaza kule nyuma kwenye magunia ya mkaa bila ya kujali masizi yaliyonitapakaa.

Nilisafiri na lile lori hadi kijiji kimoja ambapo ndipo lilipokuwa likielekea. Niliwachungulia dereva na utingo wake wakiingia kwenye mgahawa uliokuwa eneo la sokoni ambapo ndipo tuliposimamia. Niliteremka bila kuonekana na kujichanganya mle sokoni huku nikijikung’uta masizi ya mkaa kutoka kwenye lile lori.

Nilijua kuwa nguo zangu zilikuwa zinatisha, hivyo nilinunua nguo za mtumba zilizokuwa zikiuzwa pale sokoni. Kwa bei ya jioni nilipata gauni na jaketi kwa shilingi elfu moja na mia tano. Nikanunua na kilemba kwa ajili ya kuficha rasta zangu ambazo nilijua zilikuwa ni alama kubwa ya kunitambulisha kwa polisi na hata wale wauaji niliowatoroka. Nikanunua na viatu vya chini ambavyo ingekuwa rahisi kwangu kukimbia pindi ikibidi. Nilirudi kule kwenye ule mgahawa kama mtu nisiye na hofu yoyote na kupita moja kwa moja mpaka sehemu ya vyoo.

Nikiwa kule chooni nilinawa uso na sehemu muhimu za mwili wangu na kubadilisha nguo, nikiziweka nguo zangu nilizotoka nazo kule kwa mkuu wa wilaya ndani ya mfuko wa nailoni niliokuwa nimebebea zile nilizonunua pale mtumbani. Nilitokea mlango wa nyuma wa ule mgahawa na kurudi kule sokoni nikiwa mtu mwingine kabisa, mfuko wangu uliokuwa na nguo zangu za zamani nikiutumbukiza kwenye pipa la taka lililokuwa nyuma ya ule mgahawa.

Kutoka pale sokoni nilisafiri kwa lori lingine lililokuwa limewabeba wachuuzi waliokuwa wakifanya biashara zao pale sokoni kwa nauli ya shilingi elfu moja hadi Dodoma mjini ambapo tulipofika ilikuwa saa mbili za usiku.

Kwa muda ule hakukuwa na usafiri wowote wa kuweza kunifikisha Dar, hivyo nikabaki nikitembea ovyo mjini nisijue pa kwenda na wakati huohuo nisiweze kutulia popote kwa hofu kuwa polisi walikuwa wakinisaka na huenda wakanikuta na kunitia mbaroni. Nilijua kuwa nikisubiri hadi asubuhi itakuwa hatari kwani kwa vyovyote wabaya wangu walikuwa wanategemea kuwa ningejaribu kutafuta usafiri wa kurudi Dar, na hivyo wangenivizia kituo cha mabasi.

Nilipata wazo la kudandia malori ya mizigo ambayo huwa yanasafiri usiku, lakini pia niliona kuwa hilo lilikuwa gumu kutokana na kwamba nisingeweza kujificha kwenye lori la mtu mpaka Dar bila kugundulika kama nilivyofanya hapo mwanzo. Na hata kama ningesafiri kwa makubaliano na dereva kwa malipo maalum, bado kulikuwa kuna uwezekano wa kuwekwa vizuizi njiani ili kukagua magari yote yatokayo nje ya mkoa ule ili kunikamata. Mambo niliyomfanyia mkuu wa wilaya yalikuwa mabaya sana, na lazima polisi walikuwa wakinisaka kwa nguvu sana.

Ndipo nilipopata wazo la kutumia treni. Nilipitia kwenye kibanda cha urembo na kununua wanja na kuelekea stesheni ya treni ya Dodoma huku nikiombea nikute kuna treni. Bahati bado ilikuwa yangu kwani nilikuta treni ndio inapakia na abiria walikuwa wakiliparamia kwa fujo lile gari refu la chuma. Bila kuzubaa nami nilijitosa ndani ya gari lile bila tiketi, nikijua kuwa mkaguzi akinikuta nikiwa ndani na safari imeshaanza, hatakuwa na la kufanya. Na nilijiamini kwa kuwa nilikuwa nina pesa.

Nilipita hadi kwenye mabehewa ya daraja la tatu, nikaingia bafuni ambapo kwa kutumia kioo kilichokuwapo kule bafuni, nilijipaka wanja na kujifunga kilemba changu vizuri. Nilipojitizama, nilikubali kuwa nilikuwa nimebadilika.

Nilibana kwenye kiti cha dirishani kwenye kona nyuma kabisa ya behewa lile, lakini mwenyewe alipotokea, niliinuka na kuketi juu ya ndoo ya plastiki ya mmoja wa wasafiri waliorundikana pamoja nami ndani ya behewa lile. Na hapo ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa nina njaa kali sana. Nilinunua mapande ya viazi vya kuchemsha na chupa ya maji kupitia dirishani na kuanza kula kwa pupa, bila ya kujali kuwa nilikuwa nakula katikati ya kundi la watu.

Msafiri kafiri.

Wachuuzi wa vitu vidogo walikuwa wakipita huku na huko kule nje ya behewa kana kwamba haikuwa usiku. Nilinunua machungwa kwa ajili ya kula wakati safari ikianza, kisha nikamtuma yule muuza machungwa anitafutie mchuuzi wa visu. Nikanunua na kisu kidogo kwa ajili ya kumenyea machungwa yangu nikiwa safarini. Baridi ilianza kunishambulia ingawa nilikuwa nimevaa jaketi. Nikanunua doti ya kanga kutoka kwa mchuuzi aliyekuwa akipitisha biashara hiyo kule nje, na kujifunika miguuni.

Baada ya muda treni ilipuliza honi yake kali na safari ikaanza. Nilipiga mbwewe kwa shibe na kuegemea dirishani huku nikitafakari matukio yaliyonitokea siku ile. Mwili wote ulikuwa ukiniuma na miguu niliihisi ikipwita na kuvuta kutokana na kukimbia kwa muda mrefu. Nilikuwa nanuka jasho na nywele zangu zilitoa harufu. Nilijiweka sawa pale kwenye ndoo niliyokalia na kujiegemeza zaidi kwenye kona ya behewa lile.

Muda si mrefu nilipitiwa na usingizi mzito. Mpaka nilipokuja kushtushwa na ile honi kali ya treni wakati ikiingia Dar es Salaam…

--

Kelvin alikuwa amepanga chumba kimoja kilichoingiliana na bafu yaani master bedroom, na sebule, huko maeneo ya Sinza. Aliingia chumbani kwake kutokea bafuni alipokuwa akioga,akiwa na bukta tu. Alikuwa ameinamisha kichwa chake akijifuta maji kwa taulo, na alipoinua kichwa alitoa mguno mkubwa wa mshituko, macho yakimtoka pima. Alirudi mbio kule bafuni, lakini aliteleza na kupiga mweleka. Aliinuka haraka na kubaki akiwa ameegemea ukuta huku akitumbua macho ya woga mkubwa.

Aka!

Nilipoingia nilipita moja kwa moja chumbani kama kawaida yangu, ambapo niliposikia maji yakimwagika bafuni, niliamua kumsubiri pale chumbani.

Niliinuka haraka na kumsogelea.

“Kelvin! Kelvin! It’s me…Tigga…” Nilimwambia huku nikizidi kumsogelea.

“Tigga…?” Kelvin aliuliza kwa mshangao huku akinitazama kana kwamba hajawahi kuniona hata siku moja. “Ni wewe? Mbona hivyo…?”

“Ndiyo Kev…ni mimi…” Nilimjibu, halafu nikakumbuka jinsi nilivyojishindilia miwanja na nguo nilizovaa. Nilitoa kile kilemba nilichokuwa nimejifunga kichwani na rasta zangu zikamwagika kichwani kama zinavyotakiwa. Nikavua jaketi langu la mtumba na kubaki na lile gauni refu. Kelvin alinitazama na nikaona kuwa sasa amenitambua vizuri. Lakini bado alionekana kuwa ana mashaka. Ni nini tena?

“Oh! Tigga! Umerudi?” Alisema na kubaki akiwa amesimama palepale alipokuwa huku akinitazama kwa namna ya ajabu. “U… umeingiaje…?”

“Mlango ulikuwa wazi Kev, niligonga sikupata jibu…nikaingia.” Nilimjibu huku nikimtazama mchumba wangu kwa makini. Niliona kuwa hakuwa na furaha kuniona kama nilivyotarajia, na nikashindwa kuelewa ni kwa sababu gani.

“Sasa…huo wanja…?” Aliuliza kwa mshangao. Nilijikuta nikitabasamu pamoja na matatizo yangu.  

“Oh! Huu? Ni hadithi ndefu Kev…naomba niingie bafuni kwanza.” Nilimwambia huku nikielekea kule alipokuwa usawa wa kuelekeabafuni. Kelvin alisogea pembeni kwa woga kunipisha, na alikuwa akinitazama kwa namna ya ajabu.

Ni nini kinatokea hapa?

Nilisita.

Nilijikuta nikirudi na kuuchukua ule mfuko wangu wa nailoni uliokuwa na lile begi langu niliouacha juu ya kitanda na kwenda nao bafuni huku nami nikimtazama Kelvin kwa mshangao.

Nilitumia muda mrefu kuliko kawaida yangu kule bafuni, na nilipotoka nilikuwa nikijisikia murua zaidi. Kelvin, akiwa ameshavaa suruali yake ya mazoezi na fulana mchinjo, alikuwa amesimama nyuma ya dirisha akimalizia kuongea na simu. Aligeuka nilipoingia na kuja kuketi kitandani, akiitupia ile simu kando yake pale kitandani na kunitazama.

Kwa kawaida huwa naweka baadhi ya nguo zangu pale kwa Kelvin kwani mara kwa mara huwa tunalala wote pale kwake. Hivyo nilibadili nguo na kuvaa suruali yangu ya jeans na kijitop changu chekundu kilichoishia juu kidogo ya kitovu, na juu yake nikamalizia na koti la jeans. Nilipojitazama kwenye kioo nilijiona kuwa kweli nilikuwa nimerudi kuwa Tigga Mumba ninayejijua na ambaye Kev, kama nilivyozoea kumwita kwa mkato, alimzoea.

Lakini bado nilikuwa na wasiwasi mkubwa, sikuwa na amani kabisa. Na nilikuwa na wasiwasi kuwa baada ya mambo niliyoyaona na niliyoyafanya kule Manyoni, maisha yangu hayatakuwa kama zamani tena. Nilihisi joto sana. Niliiendea swichi ya kuwashia feni lililokuwa likining’inia darini mle ndani ili nipate upepo, lakini Kelvin alinishtua kwa kunipigia kelele.

No Tigga! Usiwashe!”

Nilishituka! Niliruka nyuma na kusimama nikimkodolea macho Kelvin kwa mshangao.

“Ni nini? Nataka kuwasha feni…”

“Ina shoti hiyo Tigga. Yaani ukifyatua tu hiyo swichi, taa zote zinazimika nyumba nzima. Mpaka waje wapande juu ya dari huko sijui wachokonoe vitu gani ndio uwake.”

“Ah! Umenishitua! Tangu lini?” Nilimuuliza huku bado moyo ukinienda mbio.

“Leo ni ya nne. Yaani nyumba yote inakuwa kiza Tigga. Kuanzia huko kwa mwenye nyumba hadi huku kwangu.”

Nilishusha pumzi na kubaki nikiwa nimesimama katikati ya kile chumba.

Kelvin alinitazama kwa wasiwasi.

“Tigga, uko…okay…?Mbona umekuja kiajabu ajabu?” Aliniuliza.

Nilimtazama kwa muda mpenzi wangu yule.

Kwani ni kitu gani tena mpenzi? Leo hakuna busu kama kawaida, hakuna kukumbatiana kama kawaida, hakuna kunisifia jinsi nilivyotoka bomba,angalau baada ya kutoka bafuni, kama kawaida yako…why?

Lakini sikumuuliza maswali hayo yaliyopita kichwani mwangu, bali nilibaki nikimtazama tu. Nilitamani nimfuate pale kitandani alipokuwa ameketi nimkumbatie, nipate liwazo nililolihitaji sana wakati ule. Lakini sikufanya hivyo.Sikujua nianzie wapi. Niliketi kando yake pale kitandani na kumgeukia.

“Kiajabu vipi Kev?”

“Nguo ulizovaa…wanja…what’s happening? Umenitisha sana.”

“Hukunitambua?”

“Aah, hapana…ila, ndio… kwanza sikukutambua…” Alijibu na kunitazama, kisha akatazama pembeni.

Hapana Kev, ulinitambua, ila uliniogopa.Sana tu. Kwa nini?

“Mnh! Kelvin, nimekutwa na matatizo makubwa na ya kutisha…” Nilimwambia huku nikimtazama kwa makini.

“Ni matatizo gani mpenzi…kwa jinsi ulivyokuja, ni dhahiri kuna tatizo. What happened?” Aliniuliza huku akinitazama kwa mashaka.

Nikamuelezea mambo yote yaliyotokea kule msituni, na yaliyotokea kule kwa mkuu wa wilaya hadi jinsi nilivyofanikiwa kutoroka na kulazimika kusafiri mpaka Dar nikiwa nimejipaka wanja kishamba namna ile na nikiwa nimevaa nguo zilizokuwa bado zinanuka harufu ya mitumba ambazo hazikuwa katika mtindo wangu wa mavazi kabisa.

Nilimueleza kwa sababu nilikuwa nataka nipate mtu japo mmoja atakayeniamini. Kwa namna fulani hilo kwangu lilikuwa ni jambo la muhimu sana. Katika mazingira ya kawaida, Kelvin angekuwa ni mtu wa kwanza ambaye ningetegemea aniamini katika hili, ukitoa mama yangu na dada yangu. Lakini mazingira hayakuwa ya kawaida.

Muda wote niliokuwa nikimuelezea matukio yale ambayo mimi niliamini kuwa ni ya kutisha na yaliyoweza kumtisha na kumshitua yeyote nitakayemsimulia, Kelvin alikuwa amejiinamia akichezea vidole vyake akitazama sakafu. Na baada ya kumaliza maelezo yangu, bado Kelvin alikuwa amejiinamia akichezea vidole vyake akitazama sakafu.

“Pole sana Tigga…” Hatimaye aliinua uso wake na kuniambia, lakini bado alionekana kuwa alikuwa anaficha kitu fulani.

Nilimtazama na kuitikia pole yake kwa kichwa huku nikiuma mdomo wangu kwa uchungu. Kelvin alikuwa ananificha kitu. Nilitazama pembeni. Kitu kikubwa kilichonishangaza ni kwamba hata nilipomueleza Kelvin kuwa nilikuwa nimepiga picha za video tukio la kuuawa kwa yule mtu asiye na jina kule msituni, bado hakuonesha udadisi wa kutaka kuona ushahidi ule. Kwa nini?

Machozi yalianza kunitoka taratibu.

Nilikimbilia kwa mkuu wa wilaya nikitegemea msaada, matokeo yake nikakutana na balaa lingine kubwa zaidi, lililoashiria kuwa huenda mimi ndiye muuaji.

Sasa nimekimbilia kwa mpenzi wangu…mchumba wangu, nikitegemea kueleweka na kuliwazwa na kupewa msaada wa mawazo jinsi ya kukabiliana na balaa hili.Lakini nako nakuta mazingira tofauti.

Eeh! Mungu wangu…

That’s all you can say Kelvin?” Nilimuuliza kwa uchungu huku bado nikitazama pembeni, nikimaanisha kuwa baada ya kusikia mambo yaliyonikuta, hana la kusema zaidi ya kuniambia pole sana. Aliinuka na kuja kuchutama mbele yangu, akiweka mikono yake juu ya mapaja yangu. Niliinamisha kichwa changu na kumtazama.

“Tigga my dear,najua ni vigumu sana kwako kuelewa, lakini…lakini…unahitaji msaada wa kitaalamu Tigga…” Aliniambia kwa upole.

SAY WHAAT!” Niliropoka kwa mshangao huku nikisimama na kumtazama kana kwamba alikuwa kichaa.

“Ndio Tigga, unahitaji matibabu…na kama unajali mapenzi na maisha yetu pamoja, nakuomba sana ukubali kupatiwa matibabu…” Kelvin aliniambia kwa upole huku akinitazama usoni.

Hii ni kali zaidi!

Uchungu niliousikia haukuwa na kifani. Akili yangu ilikuwa kama iliyokufa ganzi. Nilimtazama Kelvin kwa mshangao, na sikuweza kummaliza.

“Na wewe pia Kelvin? Yaani na wewe huniamini? Hata baada ya kusikia matatizo yaliyonipata bado unadiriki kuniambia kuwa nahitaji matibabu? Nitibiwe nini sasa Kelvin?” Nilimuuliza kwa uchungu huku nikitiririkwa na machozi.

“Tigga…”

“Kelvin! Yaani…Kelvin! Unataka kuniambia kuwa unaamini mimi ni mgonjwa wa akili…? Kwamba nimewaua wenzangu wote kule msituni na…na…Ooh! My God! Hii haiwezekani, hii haiwezekani kabisa!” Nilishindwa kuendelea, maneno yalinikwama kooni. Moyo uliniuma. Yaani ilikuwa kama kuna ndoana iliyounasa moyo wangu na ikiuvuta kwa nguvu.

Nilimtazama yule mtu niliyempenda kwa moyo wangu wote kiasi cha kufunga naye uchumba, na nikashindwa kuelewa kilichokuwa kinatokea.

“Tigga jaribu kuelewa…najua kuwa kwako hili ni jambo gumu kulikubali, lakini—”

“Unaweka mapenzi na maisha yetu pamoja at ransom Kelvin kwa ajili ya kutosheleza imani kuwa mimi nina wazimu kweli?” Nilimkatisha kwa uchungu, nikimaanisha kuwa anaweka rehani maisha yetu pamoja kutegemeana na kukubali kwangu kufanyiwa hayo matibabu ya ugonjwa wa akili nisiokuwa nao.

“Tigga…”

“Unachoniambia Kelvin ni kuwa unaamini kwamba mimi, Tigga, mchumba wako, nina ugonjwa wa akili, sio?”

“Tigga dear, ingawa hilo linaonekana ni jambo baya, lakini ndilo jambo pekee linaloleta maana, mchumba!”

“Hah! Wait a minute Kelvin,” Nilimwambia na kumkazia macho huku nikishusha sauti na kumuuliza, “Unataka kuniambia kuwa mimi kuwa mgonjwa wa akili ndilo jambo pekee linaloleta maana?”

“Ndio Tigga! Otherwise haitaleta maana hata kidogo! Mambo uliyoyafanya huko Manyoni kwa mkuu wa wilaya?Tigga ninayemjua mimi hawezi kuyafanya asilani!” Kelvin alinijibu kwa msisitizo uliochanganyika na wasiwasi.

“Aakh! Pale nilikuwaunder pressure Kelvin! Nilikuwa najaribu kuokoa maisha yangu!” Nilimjibu kwa jazba nikisisitiza kuwa nilifanya mambo yale kwa sababu nilikuwa kwenye shinikizo kubwa la kujaribu kuokoa maisha yangu.

And that is the problem Man! Paranoid Schizophrenia is all about uncontrolled pressures Tigga!” Kelvin alinijibu kwa hamasa huku akisisitiza maneno yake kwa mikono, akimaanisha kuwa ule ugonjwa unaosemekana kuwa ninao unahusiana na kushindwa kudhibiti mashinikizo.

Nilichoka!

Kelvin alionekana kuamini kila alilokuwa akilisema. Kama jinsi yule mkuu wa wilaya alivyoonekana kuamini kila aliloelezwa na yule dokta wa uongo.
“We’ unajua nini kuhusu hiyo Paranoid Schizo…Schizo…shit Kelvin! You can’t be serious!Wale watu walikuwa wanasema mimi naitwa Sylvia-vitu gani–tusijui huko, halafu unaniambia nidhibiti mashinikizo!” Nilimfokea kwa hasira.

Alinitazama kwa huzuni.

Alijaribu kusema neno akaghairi. Akatupa mikono yake hewani kwa kukata tamaa na kwenda kusimama nyuma ya dirisha. Alijishika kichwa kwa mikono yake yote miwili na kurudi tena hadi pale alipokuwa amesimama awali. Alinitazama, akataka kuongea tena akaghairi. Akaenda kuketi kwenye kochi moja na pekee lililokuwamo mle chumbani na kujiinamia akiwa amejishika kichwa.

Nilimtazama kwa muda mrefu huku moyo ukiniuma sana.

Why do you believe them so, Kelvin?” Hatimaye nilimuuliza kwa sauti ya kunong’ona iliyojaa majonzi na kukata tamaa, nikihoji kwa nini alikuwa akiwaamini wale wazushi kwa kiasi kile.

Yeye  aliinua uso wake na kunitazama kwa muda.

You wanna know why?” Aliniuliza huku akiinuka na kwenda kwenye kabati la nguo na kutoa karatasi moja kutoka kwenye droo ndogo ya kabati lile.

This is why!” Aliniambia huku akinikabidhi ile karatasi.

Nilimtazama kwa mshangao huku nikiipokea ile karatasi kwa mikono yenye kutetema. Kelvin alirudi na kuketi kwenye lile kochi na kujiinamia kama alivyokuwa hapo mwanzo.Niliisoma ile karatasi na akili ikanizunguka. Nilimtazama Kelvin kwa mshangao na kuisoma tena ile karatasi.

Sasa huu ni mchezo!

Ilikuwa ni karatasi ile ile niliyopewa na mkuu wa wilaya kule Manyoni. Ikiwa na kivuli cha sura yangu kwenye kona yake ya kulia, na yale maelezo ya uongo yaliyokuwa yakielezea jinsi nilivyokuwa mtu hatari kutokana na ule ugonjwa wa akili niliosingiziwa. Yaani ilikuwa ni karatasi ile ile isipokuwa kitu kimoja tu.

Wakati ile karatasi niliyoiona kule kwa mkuu wa wilaya ilikuwa ikinitambulisha kwa jina la Sylvia – nani-sijui huko, hii niliyopewa na Kelvin hivi sasa ilikuwa ikinitambulisha kwa jina langu halisi, yaani Tigga Mumba!

Hii ni nini sasa jamani…?Hivi kwa nini hawa jamaa wamekazania kunichanganya akili yangu namna hii?Kwa kweli nilizidi kuchanganyikiwa. Sikuelewa kabisa ni nini maana ya jambo lile. Lakini nadhani lililonichanganya zaidi ni vipi ile karatasi ilifika kwa Kelvin. Kelvin anahusika vipi na sakata hili la ajabu. Nilipagawa.

Nilimtazama Kelvin kwa muda bila ya kujua niseme nini, naye alikuwa akinitazama kama mtu aliyekuwa anasubiri kuona nitafanya nini baada ya kuisoma ile karatasi.

“K-K-Ke-Kelvin, umeipata wapi hii karatasi?” Nilimuuliza kwa sauti ya kutetemeka. Badala ya kunijibu, yeye alibaki akinitazama tu, nami nikazidi kuchanganyikiwa.

“Kelvin, hii taarifa ndiyo niliyopewa kule kwa mkuu wa wilaya…lakini kule ilikuwa ikinitambulisha kwa jina Sylvia…where did you get this?” Nilimwambia na kumuuliza.

“Hiyo ni nakala ya karatasi uliyooneshwa kule Manyoni, Tigga. Walichosema ni kwamba baada ya kuoneshwa hiyo karatasi, ukaanza kupiga kelele na kudai kuwa wewe ni Sylvia Mwamkonda na sio Tigga Mumba.Walipozidi kukusaili ndipo ulipojaribu kumteka mkuu wa wilaya Tigga…na walipokushindwa nguvu ndipo ulipotoroka na kukimbia…” Kelvin alinijibu huku akinitazama machoni. Nilipigwa na butwaa.

“Walichosema? Ni kina nani hao waliosema hivyo Kelvin!

“Polisi…na Dokta Lundi.”

“Dokta Lundi! Dokta Martin Lundi? Alikuja hapa?”

“Walikuja ofisini…kisha tukaja wote mpaka hapa.Ndio wakanieleza mambo yaliyotokea huko…”

“Wamekujuaje wewe…?” Nilimuuliza kwa mshangao na kuchanganyikiwa.

Kelvin alibetua mabega yake. “Ile ni serikali Tigga…wana njia zao…” Aliniambia. Nilifumbua mdomo, sikujua nataka kusema nini, hivyo nikaufumba. Nilitembea kutoka kona moja ya chumba hadi nyingine na kurudi. Kisha nikakumbuka.

Ni ile albamu waliyoiba kutoka kwenye mkoba wangu kule msituni!

Mle ndani kulikuwa kuna picha nyingi nilizopiga na Kelvin, tukiwa katika mikao ya mapenzi na hata baadhi ya picha tulizopiga wakati wa sherehe yetu ya kufunga uchumba. Na kuna picha kadhaa ambapo Kelvin alikuwa amevaa fulana zilizokuwa na nembo ya kampuni aliyokuwa akifanyia kazi.Eh! Mungu wangu! Wamefika hadi huku! Kunitafuta mimi…ili waniue na mimi!

“Li-lini…?” Niliinua uso wangu na kumuuliza huku akili ikinizunguka.

“Jana Dear…niliwabishia sana Tigga, lakini ushahidi wa maelezo waliyonipa…haupingiki.Ndio maana nakuomba ukubali kufanyiwa matibabu…kwa sababu yote uliyoyafanya mpaka sasa si kosa lako…”

“Sikufanya kitu chochote zaidi ya kuokoa maisha yangu Kelvin! Kwa nini hutaki kuniamini? Wale ni watu wabaya sana Kelvin…yaani wamekuja mpaka hapa halafu wewe bado unawaamini hata baada ya kukuambia kuwa nina ushahidi wa mkanda wa video unaoonesha  tukio zima la kuuawa kwa yule mtu asiye na jina kule msituni!”

“Kwa mujibu wa maelekezo ya Dokta Lundi, hivyo vyote vinaweza kuwa ni vitu unavyofikiria tu kichwani mwako Tigga, lakini havipo.Kitendo cha kujaribu kumteka nyara mkuu wa wilaya tu kinathibitisha jinsi unavyohitaji msaada wa kitabibu!” Kelvin alizidi kutetea hoja zile za uongo. Na ndio alizidi kunichanganya.

“Kwa hiyio na huo mkanda wa video ninaousema nao nimeufikiria tu kichwani mwangu lakini haupo?” Nilimuuliza.

Alitupa mikono hewani kwa kuchanganyikiwa.

“Hilo la mkanda wa video nd’o nalisikia kwako, Tigga… ninachojua ni kwamba baada ya kusikia ushahidi wa akina Lundi nimeshawishika kukubaliana nao kwa maslahi yako Tigga.” Aliniambia kwa mashaka.

“Ulichoambiwa ni uongo na uzushi mkubwa niliopata kuusikia maishani mwangu! Hakuna cha dokta Lundi wala nini…yule mtu ni muuaji, na nakushangaa kuwa unaweza kuamini utumbo kama huo,Kelvin. What’s the matter with you Kev?” Nilimuuliza kwa jazba huku nikimtazama kwa makini, lakini bado Kelvin alionekana kabisa kuwa alikuwa haniamini.

Kwa hakika haya mambo sasa yalikuwa yanaelekea kunishinda. Ni nini hii? Haiwezekani!

“Kelvin, ile karatasi niliyoiona Manyoni ilinitambulisha kuwa mimi ni Sylvia Mwamkonda, na ni wao ndio waliokuwa wakiniita mimi Sylvia, nami nikawa nasisitiza kuwa mimi ni Tigga na sio Sylvia! Sasa tena wewe unaniambia eti wamekwambia kuwa ni mimi ndiye niliyekuwa nalikana jina la Tigga na kung’ang’ania jina la Sylvia? This is preposterous Kelvin!” Nilimwambia na hata pale nilipokuwa nikimwambia maneno yale, na jinsi nilivyousoma uso wake alipokuwa akinitazama, wazo lilinijia.

Ndio maana aliponiona alishituka sana hadi akapiga mweleka! Sio kwa kuwa hakunitambua kutokana na wanja na mavazi niliyovaa, bali kwa hofu kuwa ameingiliwa na mwehu na muuaji…Mungu wangu!

“Sawa bwana…naona kuwa umeamua kuwaamini hao watu…lakini nakuhakikishia kuwa hiyo karatasi waliyokuonesha imeghushiwa kama ile waliyonionesha mimi kule Manyoni. Na n’nashangaa kuwa baada ya kusikia maelezo yangu bado hutaki kulielewa hilo.”  Nilimwambia kwa unyonge huku akilini nikijaribu kutafuta la kufanya baada ya kujitokeza kwa hali ile.Hata huyu mchumba wangu mwenyewe niliyemtegemea naye ametekwa na laghai za wale wauaji. Nilipiga mwayo. Nilijihisi mchovu na njaa iliniuma. Kelvin alinitazama kwa huruma.

Sasa kama unanihurumia kwa nini huniamini? Kwa nini hutaki kunisaidia? Au ni kweli nina matatizo ya akili mimi?

“Sio hivyo tu Tigga, maelezo ya Dokta Lundi, hiyo karatasi, mambo uliyoyafanya kule kwa mkuu wa wilaya, pamoja na maelezo ya kwenye gazeti…”

“Gazeti? Gazeti gani? Maelezo gani?” Nilimkatisha kwa jazba. Lakini Kelvin hakunijibu maswali yangu na badala yake aliendelea na maelezo yake.

“…vyote hivyo vinanifanya nisiamini moja kwa moja kuwa huhitaji msaada wa kitabibu Tigga. Lakini kama huna matatizo hayo yanayosemwa kuwa unayo, njia pekee ya kuthibitisha hivyo ni kufanyiwa uchunguzi wa kitaalam ili kuthibitisha ukweli au uongo wa maelezo yao hayo.” Kelvin alisema.

“Kitu ambacho hujui Kelvin ni kuwa hao watu sio madaktari, na kwamba hawanitaki kwa uchunguzi bali kwa kuniua ili kuficha ushahidi kuwa kuna mtu aliyewaona wakiua mtu msituni na baadaye kuwaangamiza wengine wengi kule porini…mi’ siwezi kujipeleka kichwa kichwa tu kwenye  mtego wao wakati nimeshaona mambo wanayoweza kuwafanyia binadamu wenzao bwana!” Nilimchachamalia.

Kelvin aliinuka na kuchukua gazeti lililokuwa juu ya meza kando ya kitanda na kunitupia.

“Hebu soma hilo gazeti Tigga, mi’ naenda kukuletea chakula, kwani naona kuwa una njaa.” Aliniambia na kuelekea jikoni, ambalo lilikuwa kando ya ile sebule yake. Nililichukua lile gazeti na kupekua kurasa zake haraka haraka nikitafuta habari inayoelekea kuhusiana na maelezo ya Kelvin huku moyo ukinienda mbio.

Lilikuwa ni gazeti litokalo kila siku kwa lugha ya kiingereza ambalo katika ukurasa wake wa habari za ndani ya nchi (local news) kulikuwa kuna kichwa cha habari kilichosomeka “Massacre at an expedition site.”, kikimaanisha “Mauaji ya kinyama kwenye eneo la utafiti.”

Habari iliyofuatia kichwa cha habari kile, ilielezea juu ya kuuawa kwa watafiti wa mambo ya kale wanne na wenyeji wawili katika msitu mmoja huko Manyoni. Iliendelea kuelezea dhumuni la utafiti ule na kuwaorodhesha waliouwa ambao ni wale wenzangu pamoja na majina ya wale wenyeji wawili waliotoka kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya.

Zaidi ya hapo ilielezea kuwa polisi ilikuwa ikimsaka mwanamke anayejulikana kwa jina la Tigga Mumba, ambaye alikuwa ni sehemu ya ule msafara wa wale watafiti waliouawa na ambaye ametoweka kutoka kwenye eneo la utafiti na hajulikani aliko. Habari ilizidi kubainisha kuwa mwanamke huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili ujulikanao kama Paranoid Schizophrenia, ambao inasadikiwa kuwa huenda ndio uliomsukuma kuwaua watafiti wenzake na kutoweka.

Habari ile iliendelea kutoa maelezo marefu juu ya ugonjwa ule, huku ukielezea mambo ambayo mtu anayesumbuliwa na ugonjwa huo anaweza kuyafanya, ikiwemo kukana utambulisho wake na kujiamini kuwa ni mtu mwingine kabisa, kumuona kila mtu ni adui anayefaa kuuawa ili kuokoa wananchi wengine na kuamini vitu vingi vya kufikirika.

Aidha habari iliendelea kuelezea juu ya tukio la mwanamke mmoja aliyejaribu kumteka nyara mkuu wa wilaya ya Manyoni siku hiyohiyo ya tukio, na kudokeza kuwa inaaminika kuwa mwanamke huyo ndiye huyo aliyefanya mauaji ya kule msituni, ambaye mwandishi alimsema kuwa ni hatari sana na kuiasa jamii iwe macho na kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi mahala popote atakapoonekana.

Habari ilimalizia kwa kuainisha kuwa iwapo msichana huyo atapatikana na kuthibitika kuwa alikuwa ameathirika na ugonjwa huo wa akili atapatiwa matibabu katika hospitali ya wagonjwa wa akili na hatowajibika kwa matendo aliyofanya akiwa katika hali ya ugonjwa ule adimu.

Nilimaliza kusoma habari ile na kubaki nikiwa nimepigwa butwaa.

Ile habari ilikuwa ni uongo mtupu!

Ilieleza kuwa watu waliouawa kule msituni walikuwa sita na kuwataja majina yao, kitu ambacho si kweli. Kwa uelewa wangu, watu waliouawa ni saba. Mbona hawakumtaja yule mtu asiye na jina? Lakini pia nilielewa ni kwa nini hata Kelvin aliamini maelezo yale, kwani ni wazi kuwa ile habari ilikuwa imeandikwa kwa nia ya kunichafulia kabisa jina na muonekano wangu mbele ya jamii, hasa kwa watu wanaonifahamu na ambao wangeweza kunisikiliza na kuamini upande wangu wa maelezo  juu ya mambo niliyoyaona kule msituni.

Kile kipande cha mwisho cha habari ile ndicho hasa kilikuwa kinaonesha ni jinsi gani habari ile ilivyokuwa ya kupikwa na kupotosha.

Eti nikigundulika kuwa ni mgonjwa wa akili sitawajibika kwa matendo yangu! (niliguna). Yaani wanachodhani ni kwamba nitajisalimisha mwenyewe na kudai kuwa ni mgonjwa wa akili ili nisiwajibishwe! (nilisonya). Wana wazimu kweli kweli!

Niliirudia tena ile habari na kuangalia jina la mwandishi wa habari ile.

Na mwandishi wetu.

Nilitabasamu huku nikitikisa kichwa kwa huzuni. Na mwandishi wetu. Nani? Hakuna jina!Mungu wangu! Hawa watu wana uwezo namna gani? Yaani wameweza hata kueneza wayatakayo kupitia kwenye gazeti muhimu kama hili!

Sasa tayari wameshamteka mawazo Kelvin, sijui nitakimbilia kwa nani tena!

Niliwafikiria mama yangu na dada yangu. Sijui na wao wameshatembelewa na Dokta Lundi? Lakini nilikuwa nina imani kuwa hawatamuamini hata kidogo. Nilichukua simu ya Kelvin huku nikisikia mabakuli yakigongana kule jikoni na kuanza kutafuta namba ya mama yangu ambayo nilijua kuwa ilikuwa imehifadhiwa kwenye kumbukumbu za simu ile. Ilikuwa ni simu aina tofauti na ile ya kwangu, hivyo sikuwa na mazoea nayo. Nilibonyeza kitufe nilichodhani kitanifikisha kwenye kumbukumbu za namba za simu za watu mbalimbali zilizohifadhiwa kwenye simu ile.

Call register.

Siyo hapa! Nilibonyeza tena.

Missed Calls.

Akh! Siyo hapa. Nilibonyeza tena ili nirudi kwenye sehemu iliyoonesha namba za simu.

Received Calls.

Nilibonyeza tena, bado nikihangaika kurudi kwenye sehemu iliyoonesha namba za simu.

Dialled Numbers.

Bado tu! Niliamua kubadilisha kitufe, na kubonyeza kingine. Moyo ulinilipuka na nikazidi kuchanganyikiwa. Kwenye ile simu kulitokea maneno:

Dialled 1

Kisha chini yake kulitokea namba ya simu.

Ilikuwa ni namba ya simu yangu.

Ilimaanisha kuwa simu ya Kelvin ilitumika kunipigia simu kwenye namba yangu.Nilikunja uso kwa kutoelewa. Nilibonyeza sehemu iliyosema Options, halafu nikabonyeza sehemu iliyosema Time of Call. Kwenye simu ilitokea tarehe ilipopigwa ile simu na muda ilipopigwa.

Ilikuwa ni siku ile ile.

Na muda ilipopigwa simu ile ulikuwa ni katika wakati ule mimi nilipokuwa bafuni!

What is this?

Sikuwa na shaka kuwa simu yangu ilikuwa imechukuliwa na wale wauaji. Sasa vipi Kelvin apige namba yangu wakati ule mimi nikiwa naoga bafuni kwake?

Nikabonyeza kitufe kilichosema Back, na kurudi tena pale ilipokuwa inaonekana namba yangu kama ni namba iliyopigiwa kwa kutumia  ile simu ya Kelvin.

Kwa kidole kinachotetemeka kikabonyeza kitufe kinachoashiria kupiga simu na kupeleka simu ile sikioni mwangu taratibu.

Ilikuwa inaita.

Nilisikiliza huku moyo ukinipiga sana, na nilikuwa nataka kuikata wakati niliposikia ile simu ikipokelewa upande wa pili!

It’s Okay Kelvin, tunakuja. Endelea kumkawiza hapo hapo…” Sauti ya kiume iliyopokea simu yangu iliongea, na buibui mwenye miguu ya baridi sana alinitambaa mgongoni.

Ilikuwa ni sauti ya Dokta Martin Lundi.

Nilihisi chumba kikisogea nami nikapepesuka kwa kizunguzungu cha ghafla. Nilijibwaga kitandani na kubaki nikiwa nimekaa nikiikodolea macho ile simu.

Niliishiwa nguvu kabisa na mwili ulinifa ganzi. Nilielewa ni nini maana ya jambo lile lakini bado ilikuwa vigumu sana kuamini.

Ah! Yaani kumbe muda ule nilipotoka bafuni na kumkuta Kelvin akimalizia kuongea na simu alikuwa akiongea na  muongo Martin Lundi aliyekuwa anatumia simu yangu!

Muda huo Kelvin aliingia mle chumbani akisukuma kijitoroli cha kuandalia chakula kikiwa na boksi la Kellog’s Corn Flakes, bakuli la kulia pamoja,  kijiko na glasi ya maziwa. Ule ulikuwa ni mlo nilioupenda sana na nadhani ndio maana Kelvin aliamua kuniandalia. Niliirudisha pale kitandani ile simu taratibu huku nikimtazama usoni yule mwanamume niliyempenda kwa kiasi kikubwa kabisa.

Why Kelvin?

“Kula flakes kwanza, mchumba, halafu ukiona unahitaji kula zaidi itabidi tutoke tukapate mlo wa maana hoteli.” Aliniambia huku akinitupia lile tabasamu lake nililolipenda sana na kuniita kwa jina alilopenda kulitumia akitaka kuonesha upendo.

Mchumba.

Nilibaki nikimtazama huku akili ikinizunguka vibaya sana. Yaani nimeacha kwenda kwa mama yangu nimekuja kwake, kumbe yeye…

Siyo siri, iliniuma sana.

Mara nilijisikia nimeshiba na hamu yote ya kula ikaniisha. Niliinuka na kusimama nikimtazama Kelvin kwa kutoamini, yeye akijishughulisha kunichanganyia maziwa na zile corn flakes. Na nilipokuwa nikimuangalia nilijikuta nikipandwa na ghadhabu za hali ya juu kiasi midomo ikaanza kunitetemeka. Machozi yalianza kunitiririka bila ya kupenda.

Inanibidi niondoke harakakabla sijafanya jambo la kijinga!

Kelvin alinigeukia na kutaka kusema kitu, bila shaka kunialika ule mlo aliouandaa, lakini alikunja uso kwa mshangao na wasiwasi baada ya kuniona nikimtazama huku nikitiririkwa na machozi.

Honey? Mbona unalia…kuna nini tena?” Aliniuliza huku akinisogelea na akionesha kujali kwa hali ya juu. Alijaribu kunishika na kunivutia kwake kuniliwaza na hapo ndipo alipozidi kunikera.

“Usiniguse Kelvin! Niache!” Nilimfokea kwa hasira.

Aliruka hatua chache nyuma na kunitazama kwa mshangao, sura yake ikionesha hofu kubwa, kama jinsi ilivyokuwa pale aliponiona kwa mara ya kwanza mle ndani alipokuwa anatoka bafuni.

“Tti-Ti-Tigga…ni nini…?” Aliuliza huku akizidi kunitazama kwa mshangao.

Sikuweza kumjibu. Nilibaki nikimtazama kwa fadhaa na hasira. Nilichomoa pete ya uchumba iliyokuwa kidoleni kwangu na kumnyooshea mkono wangu ukiwa umekunja ngumi, ile pete ikiwa ndani yake. Kelvin alipokea mkono ule huku bado akiwa na mshangao mkubwa.

“Ni nini kwani… ?” Aliuliza huku akifungua kiganja chake na alipoiona ile pete aliinua uso na kunitazama akionekana kuwa hakuelewa kabisa maana ya tendo lile.

“Khah! Tigga! Ni vipi—” Aliuliza kwa kuchanganyikiwa.

“Naondoka Kelvin. Na sitakuwa na haja tena na hiyo pete yako!” Nilimwambia huku nikiuendea ule mfuko wangu wa nailoni. Kelvin alinizuia kwa kunishika mabega na kunigeuza ili tutazamane.

What’s the meaning of this, Tigga?” Alinifokea kwa kimombo akimaanisha kuwa anataka nimueleweshe maana ya kitendo kile.

Nilimsukuma kwa nguvu na kumkemea kwa ukali.

It means uchumba umekwisha Kelvin, that’s what it means!”

Alinitazama kwa mshangao mkubwa sana, na hata pale alipokuwa akinitazama, niliweza kuona kuwa kwa hakika sasa nilimthibitishia kwamba nilikuwa mwehu. Paranoid Schizophrenia.

Potelea mbali.

“Ah! Tigga, lakini…kwa nini?”

“Usipoteze muda wangu Kelvin…kwani we’ uko tayari kuoa kichaa?” Nilimuuliza huku nikiuchukua ule mfuko wangu wa nailoni na kutoa lile begi languliliokuwa ndani yake.

“Tigga, hebu kaa basi tuongee…huwezi kuvunja uchumba kienyeji namna hii…”

“Nimeshauvunja Kelvin na niache niende zangu!” Nilimjibu huku nikivaa viatu vyangu vya kamba.

“Hapana Tigga, huwezi kuondoka saa hizi…hebu ngoja tuelewane.”Aliniambia kwa sauti ya kitetemeshi. Nilimtazama kwa muda, kisha nikachukua begi langu.

“Unataka kunikawiza ili rafiki yako Martin Lundi anikute kama alivyokuagiza, Kelvin?”Nilimwmbia huku nikielekea bafuni.

Kauli ile ilimchanganya vibaya sana. Alinitazama kana kwamba ndio kwanza ananiona. Alijaribu kufungua kinywa akakosa la kusema. Akatupa mikono juu kwa kukosa la kufanya.

“U-Unasemaje? Kwa nini unasema hivyo…?” Alijilazimisha kuuliza.

Nilisimama nje ya mlango wa kuingia bafuni na kumtazama kwa muda. Nilisikia uchungu sana kuona kuwa bado alikuwa anajaribu kunidanganya.

“Umeingiwa na nini Kelvin? Kwa taarifa yako najua kuwa ulimpigia simu Martin Lundi wakati niko bafuni, yeye akitumia simu yangu. Na najua kuwa hivi sasa yuko njiani kuja hapa kunikamata na hatimaye kuniua!” Nilimjibu kwa hasira huku nikimtazama moja kwa moja usoni.

Jamaa alihamanika vibaya sana. Kwa hakika aliona kuwa uongo wake umegundulika. Tulitazamana kwa muda, kabla sijamuuliza kwa uchungu.

“Kwa nini lakini Kelvin?”

“Nimefanya hivyo kwa faida yako Tigga! Niamini tafadhali!” Alinijibu huku akiniangalia kwa kuomboleza.Nilimtazama kwa dharau na kebehi.

“Kwa faida yangu?”

“Ndio Tigga…unahitaji matibabu Tigga, na Dokta Lundi ana nia ya kukutibu mpenzi…”

“Wakati nimeshakwambia kuwa huyo Dokta Lundi wako ni muongo na muuaji Kelvin? Na wakati nimekwambia kuwa nina ushahidi wa mkanda wa video unaoonesha jinsi alivyoshirikiana na wenzake kumuua mtu kule msituni, na sina shaka kabisa kuwa yeye na wenzake ndio waliowaua watafiti wenzangu kule porini Kelvin? Eti kwa faida yangu! Unan’chekesha!”Nilimkemea kwa hasira.

Alikosa la kusema. Alinitazama kwa kukata tamaa na kuchanganyikiwa. Niligeuka kuelekea kule bafuni, lakini Kelvin alinisemesha.

“Sasa ndio unavunja uchumba Tigga kweli?”

Nilimgeukia na kumtazama kwa dharau ambayo sijawahi kudhani kuwa ningepata kuionesha kwake maishani mwangu.

“Umesaliti upendo wangu na umesaliti imani yangu kwako Kelvin. Umeamua kumuamini dokta Lundi muongo hata baada ya kusikia maelezo yangu, Kelvin. Na sasa umeshayaweka maisha yangu hatarini kwa upuuzi wako!” Nilimjibu na kugeuka haraka kuingia kule bafuni.

“Lakini Tigga…”

“Mimi naondoka Kelvin!” Nilimpigia kelele bila ya kugeuka wakati nikiingia kule bafuni.

“Ni kweli kabisa Tigga…lakini utaondoka na mimi!”

Mwili ulinifa ganzi na nilisimama ghafla, kwani ile ilikuwa ni sauti ya dokta Martin Lundi. Nilitoka mbio kule bafuni na kurudi pale chumbani kwa Kelvin.

Dokta Martin Lundi muongo alikuwa amesimama ndani ya chumba kile akiwa na wafuasi wake wengine wawili, tofauti na wale aliokuwa nao kule Manyoni siku mbili zilizopita. Ingawa alikuwa amevaa nguo tofauti, bado juu ya nguo zile alikuwa amevaa lile koti lake refu jeupe lililomfanya aonekane tabibu.

Hallow Tigga…” Alinisemesha huku akitabasamu na akinitazama kwa makini.

Sikuwa na la kusema. Nilimeza funda kubwa la mate na kutembeza macho yangu mle ndani. Nilikuwa nimenasa. Hakukuwa na namna yoyote ya kutoroka kutoka mle ndani. Nilimtazama Kelvin.

“Ah! Dokta Lundi… umefika hatimaye…” Alimuongelesha yule mtu aliyejiita Dokta Martin Lundi, ambaye badala ya kumjibu, alinikazia macho yake ya kuogofya na kuniuliza.

“Oke Tigga, ni ushahidi gani huo unaodai kuwa unao?”

Nilibaki nikimkodolea macho kwa mshangao. Nikamtazama Kelvin, naye alionekana kushangaa tu. Alimtazama yule muuaji aliyeamini kuwa ni tabibu, kisha akanitazama, na akamtazama tena yule muuaji.

“Eeh…dokta, sijui mnatarajia kufanyia wapi hayo matibabu…” Kelvin alimuuliza Martin Lundi muongo kwa mashaka kidogo.

“Huyo sio daktari Kelvin! Ni muuaji huyo!” Nilibwatuka kwa hasira.

Dokta Lundi alitoa tabasamu lake baya kabla ya kusema, “Tigga, Tigga, Tigga…usiwe na wasiwasi, nitakupatia dawa sasa hivi na utajisikia vizuri tu…”

Ingawa nilikuwa nimejawa na woga usio kifani, nilijikuta nikimbetulia midomo kwa kukereka.

“Kwa hiyo sasa nimekuwa Tigga na sio Sylvia tena, eenh? Hivi unadhani unamlaghai nani hapa wewe?” Nilimhoji.

Yule dokta laghai alijitia kutikisa kichwa kwa huzuni huku akinitazama kwa makini. Kelvin alionekana kutoelewa afanye nini. Dokta Lundi alinisogelea taratibu huku wale watu wake wawili wakijizatiti mlangoni ili nisijaribu kutimua mabio. Na kwa hakika nilikuwa nimekwama. Nilijilazimisha kufikiria namna ya kujiokoa sikufanikiwa. Niliufikiria ule mkanda wa video na nikahisi kizunguzungu. Ikiwa watafanikiwa kunipokonya ule ushahidi, basi nimekwisha.

“Mnh! Paranoid Schizo—” Dokta Lundi alianza kusema uongo wake huku akinisogelea lakini sikumpa nafasi.

“Toka huko na uzushi wako hapa! Hakuna cha Paranoid Schizo…-nini wala nini hapa! Uongo mtupu! Na wewe unajua hilo! Mimi ni mtu mwenye akili timamu!Nimewaona mkiua mtu kule porini, na najua kuwa ninyi ndio mliowaua wenzangu kule msituni…sasa mnanitaka na mimi ili mniue kuniziba mdomo kwa kujitia eti ni madaktari, kwenden’ zenu huko!” Nilimbwatukia kwa kelele huku nikirudi nyuma.

Dokta Lundi alighadhibika na kunitolea macho.

“We’ Tigga—” Alianza kunikemea, lakini nilimkatisha tena.

“Utawadanganya hao hao lakini sio mimi…kaa mbali nami!” Nilimwambia huku nikimwoneshea Kelvin aliyekuwa akizidi kushangaa.

Sijui ilikuwaje hata nikapendana na jitu bwege kama hili!

“Tigga ana ushahidi kuwa mliua mtu Dokta…nadhani labda tungehakikisha juu ya hilo kabla hamjamchukua…” Kelvin aliropoka kwa kitetemeshi.

“Sawa kabisa Kelvin…Tigga, hebu tuoneshe huo ushahidi wako!” Dokta Lundi aliniambia huku akizidi kunisogelea na uso wake ukionesha mashaka, kana kwamba anajishauri iwapo aamini kuwa inawezekana nikawa kweli nina kitu kama hicho au la. Nilitazama huku na huko sikuona pa kukimbilia.

“Ah! Tangu lini mwehu…Paranoid Schizo-nini sijui huko, akawa na ushahidi wa kumtia wasiwasi mtu mwenye akili timamu kama wewe dokta? Mi’ si mwehu bwana? Then why are you so worried about my evidence, eenh?” Nilimuuliza huku nikizidi kurudi nyuma, nikimaanisha kwa nini ushahidi wangu uwatie hofu wakati wanajua kabisa kuwa mimi ni mwehu.

Niligota ukutani.

Dokta Lundi alitoa amri na kwa hatua moja kubwa mmoja wa wale vibaraka wake alinirukia pale nilipokuwa. Nilipiga yowe huku nikiruka pembeni lakini yule jamaa alikuwa mwepesi. Alinidaka na kunikamata mikono yangu kwa nguvu. Nilimpiga teke la ugoko, akaguna kwa maumivu huku akiiachia mikono yangu, nami nikamtandika kofi la uso. Kelvin aliropoka neno na Dokta Lundi akamfokea. Yule jamaa alinichapa kofi kali sana la uso lililonipeleka chali kitandani kwa Kelvin na kunigaragaza mpaka upande wa pili wa kile kitanda, huku begi langulikianguka sakafuni.

Nilijiinua huku nikisikia kizunguzungu kutoka kule ubavuni mwa kitanda huku nikihisi damu ukinichuruzika kutoka puani kutokana na kofi lile. Nilibebwa mzima mzima na wale wasaidizi wa Martin Lundi na kuketishwa kwenye kochi lililokuwa mle ndani. Nilitoa ulimi wangu kuramba eneo nililohisi kuwa lina damu juu ya mdomo wangu na nikahisi ladha ya chumvichumvi.

“Heey! Sasa mbona mnampiga? Hivi ndivyo mnavyowahudumia wagonjwa nyie?” Kelvin aliwafokea wale watu na kumtazama Dokta Lundi ambaye alikuwa akinitazama kwa hasira bila ya kusema neno.

“Dokta! Ongea na watu wako bwana! Hawawezi kumfanya hivi mchumba wangu hata kama ni mgonjwa wa akili…”

“Mimi sio mchumba wako Kelvin, na wala sio mgonjwa wa akili! Haya ndio uliyoyataka, sasa unalalama nini? Kwa nini hukutaka kuniamini tangu mwanz—”

“Kelele!” Dokta Lundi alifoka.

“Ebbo! Yaani mnakuja kunitolea amri nyumbani kwangu? Haiwez–AAAH!.” Kelvin alianza kumaka, lakini Dokta Lundi alimchapa kofi la uso lililompeleka mpaka ukutani.

“Shut Up!

Na hapo hapo mmoja wa wale wasaidizi wa Martin Lundi alimrukia pale ukutani na kumbana mikono yake kwa nyuma. Ikawa sote tumedhibitiwa na wale wasaidizi wa Martin Lundi.

Nilimtazama Kelvin kwa kukata tamaa. Alibaki akitembeza macho huku na huko asijue afanye nini.

“Unasema ulituona tukiua mtu?” Martin Lundi aliniuliza nikiwa nimebanwa na yule msaidizi wake pale kwenye kiti. Sikumjibu. Alinipiga kofi la shavu lililotawanya vimulimuli machoni mwangu. Kelvin aliropoka kitu, lakini sikuelewa ni kitu gani. Nilimtazama yule muuaji kwa ghadhabu.

“Ndio, nimewaona! Wewe pamoja na mwenzako mwenye mguu mbovu na mwingine mwenye macho kama nyoka! Mlikuja na helikopta na wewe ndio ulikuwa ukiendesha, uongo?” Nilimtemea yale maneno kwa hasira.

Jamaa alinitazama bila ya kusema neno lakini niliona kuwa uso wake ulibadilika na aliamini kuwa nilikuwa nasema kweli.

“Uongo?” Nilimuuliza tena.

Nilipigwa kofi lingine kali la uso lililonitandazia maumivu makali, na nililia kwa uchungu.Lakini sikukata tamaa.

“Kwa nini mlimuua yule mtu, Lundi? Au na yeye alikataa kukubali kuwa ni mgonjwa wa akili kama mimi?” Nilizidi kumkemea kwa hasira yule muuaji muongo.

“Hah! Ni kweli hayo maneno Dokta?” Kelvin aliropoka  kutoka kule alipokuwa ameshikiliwa na yule kibaraka mwingine. Dokta Lundi alimwendea kwa kasi na kumtandika ngumi ya uso huku akimkemea.

“Hebu nyamaza wewe!”

Alinirudia pale nilipokuwa nimeshikiliwa kwenye kiti na kuniuliza.

“Na unasema kuwa una ushahidi wa tukio hilo?”

“Kwa hiyo ni kweli?” Kelvin aliuliza kwa kihoro huku akimkodolea macho yule daktari bandia, damu ikimchuruzika kutoka kwenye kona ya mdomo wake.

“Nina ushahidi wa mkanda wa video!” Nilimtemea tena maneno kwa hasira huku nikimsogezea uso wangu kwa kumsuta. Hapo hapo alinibamiza kofi lingine kali la uso na kunidaka koo kabla sijataharuki.

Kelvin alijikurupusha kutoka kule alipokuwa ameshikwa lakini niliona kuwa yule mtu aliyemshika alikuwa amemzidi nguvu. Alianza kupiga kelele lakini haraka jamaa alimbana koo na kumzuia kupiga kelele.

“Nautaka huo ushahidi sasa hivi!” Dokta Lundi muongo aliniambia kwa hasira. Nilimtazama kwa kiburi bila ya kusema neno. Alizidi kunitazama kwa ghadhabu nami nikamrudishia mtazamo wa ghadhabu.

“Au unadanganya wewe? Huna cha ushahidi wala nini…!” Aliniambia huku bado akiwa amenikaba.

“Mimi sio muongo kama wewe babu! Lakini kwa kukuridhisha tu, tufanye ninakudanganya na wala sijawaona mkishuhudia wakati bastola ya Macho ya Nyoka ilipoutoa uhai wa yule mtu kule msituni, na wala sina ushahidi wowote juu ya yote hayo!” Nilimjibu.

Dokta Martin Lundi alichanganyikiwa wazi wazi kwa jibu lile. Alinitazama halafu akamgeukia Kelvin, kisha akanitazama tena.

“We’ unao ushahidi wewe!Uko wapi?” Alisema na kuniuliza kwa jazba. Nilimchekea mbele ya uso wake bila ya kumjibu. Yule kibaraka wake alinibamiza kofi la kisogoni, na hapo hapo Dokta Lundi aliniinua na kunibamiza ukutani huku bado akiwa amenikaba koo.

“Tuoneshe huo mkanda sasa hivi!” Alinifokea.

Sikumjibu.

Alimuamrisha yule msaidizi wake anikamate, naye akaunyakua ule mkoba wangu na kumimina vitu vyote vilivyokuwa ndani yake juu ya kitanda. Aliiona ile video kamera ya Gil. Aliokota kile kisu kidogo nilichonunua kwenye treni na kukitazama, kisha akanitazama.

“Unatembea na visu mwanamke? Kwa hakika wewe ni muuaji!” Alisema kwa kebehi. Kisha aliichukua ile kamera na kuanza kuitazama taratibu, akiigeuza huku na huko. Moyo ulikuwa ukinidunda vibaya sana na watu wote mle ndani walibaki kimya. Nilimtazama Kelvin na nikamuona akiikodolea macho ile kamera kana kwamba ilikuwa ndio tegemeo pekee la kuokoa maisha yake. Muda huu yule jamaa aliyekuwa amemkaba alikuwa amelegeza kabali, naye akaropoka.

“Kumbe ni kweli…!”

Akili ilikuwa ikinitembea haraka sana. Niliangaza mle ndani nikitazama uwezekano wa kujiokoa na kuona kuwa ulikuwa mdogo sana.

Mtu aliyejiita Dokta Martin Lundi alifungua sehemu ya kuingizia mkanda kwenye ile kamera na kutazama ndani yake, na wote mle ndani wakawa wanamtazama yeye.

Hamna mkanda!

Aliinua uso wake kwa ghadhabu na kunitazama.

“Hamna mkanda wa video humu!” Aliniambia kwa ghadhabu.

“Ulitegemea nini Dokta Martin Lundi?” Nilimuuliza kwa kejeli.

“Kwa hiyo hamna ushahidi wa mkanda?” Aliniuliza.

“Sijui, we’ si ndio dokta bwana! Unajua kila kitu. Hadi umeweza kujua kuwa mimi ni mwehu bila hata ya mi’ mwenyewe kujua…” Nilitoa majibu ya kejeli huku akilini nikitafuta namna ya kujiokoa.

Dokta Lundi alipekua kwenye rundo la vitu vilivyotoka kwenye mkoba wangu akitafuta mkanda wa video asiupate. Alitoa bastola na kunigeukia kwa ghadhabu. Kelvin aliguna kwa woga baada ya kuona ile bastola.

Where is the tape?” Aliniuliza kwa hasira. Nilijua pale nikizidisha jeuri yule mtu angeweza kuniua kweli. Njia pekee ilikuwa ni kuendelea kumfanya yeye auhitaji ule mkanda kutoka kwangu.

“Mkanda ninao na nimeuficha…” Nilipigwa kofi lingine na kujipigiza kisogo changu ukutani. Yowe la uchungu lilinitoka.

“Umeuficha wapi mwanamke?”

“Nimeukabidhi kwa wakili, akiwa na maelekezo kuwa auwasilishe kwenye vyombo vya dola na vituo vya televisheni iwapo nitashindwa kuwasiliana naye kwa siku mbili mfululizo, au nitakapofikwa na umauti kwa namna yoyote ile.” Nilimjibu kwa kujiamini huku nikimtazama usoni.

Jamaa alichanganyikiwa.

“Muongo mkubwa! Where is the tape?” Alibwata akisisitiza nimwambie ni wapi ulipo ule mkanda wa video huku akiniwekea bastola yake kwenye paji la uso.

“Mimi sio muongo kama wewe! Huo ndio ukweli, kama huamini basi…fanya utakalo!”

“N’takuua wewe!”

“Kwani hiyo si ndio kazi yako? Nimeshuhudia kwa macho yangu kule porini, na wakili wangu ameshuhudia hilo kupitia kwenye ule mkanda wa video niliomkabidhi.”

Kelvin alicharuka.

“Kumbe nyie ni wauaji! Niacheni! Niacheni!” Alijikurukupusha na kumsukuma yule mtu aliyemkamata. Jamaa alipambana naye kwa muda na kufanikiwa kumbwaga chini na kumbana sakafuni.

“Hapana. Huo mkanda uko humu humu ndani…” Martin Lundi alisema, na kumgeukia yule kibaraka aliyekuwa amenishika mimi, “…hebu pekua humu ndani mpaka uupate!” Aliamrisha. Kiza kilikuwa kimeanza kuingia, na yule jamaa aliwasha taa za mle ndani na kuanza kupekua.

Alipekua kila mahali huku Kelvin akilalamika akiwa amebanwa sakafuni jinsi vitu vyake vilivyokuwa vikitupwa tupwa ovyo mle ndani. Jamaa alipekua kila mahali. Kabati lilichambuliwa ovyoovyo, chini ya kitanda, bafuni, akatoka na kuingia jikoni, sebuleni.

Alirudi bila mafanikio.

“Mkanda uko wapi we’ binti?” Martin Lundi aliuliza

“Kama nilivyokuambia. Kwa wakili wangu.”

Alitikisa kichwa kwa masikitiko.

“Twende kwa wakili wako!” Aliniamrisha.

“Mnh! We’ unadhani mi’ mwehu kama unavyonipakazia?Itabidi uniue kwanza ndio nikupeleke huko kwa wakili wangu, na ukiniua taarifa zitatapakaa kwenye vyombo vya habari kama mvua!”

Alinipiga kofi kali la mdomo. Na wakati huohuo Kelvin alipata upenyo, kwani alimtupa pembeni yule jamaa aliyekuwa amembana pale chini na kusimama. Jamaa alijitahidi kumkamata tena lakini Kelvin alimwahi na kumsukumia teke la kifuani lililomtupa ukutani. Kisha akamrukia Dokta Lundi huku akipiga kelele za ghadhabu. Dokta Lundi aligeuka akitanguliza bastola yake, nami niliruka pembeni na kufyatua ile swichi ya kuwashia feni.

Mlio wa bastola ulivuma ndani ya kile chumba na kiza kikatawala ghafla kikiambatana na yowe la uchungu kutoka kwa Kelvin. Nilijitupa sakafuni na kujibiringisha chini ya kitanda wakati wale wauaji wakipiga kelele za kuchanganyikiwa.

“Washa taa!” Dokta Lundi alibwata, lakini mmoja wa watu wake alipiga kelele kuwa ni kiza nyumba yote.

“Pumbavu! Yuko wapi mwanamke!”

Nilisikia Kelvin akilia kwa maumivu na nikaingiwa na woga mkubwa. Bila shaka alikuwa amejeruhiwa kwa risasi kutoka kwenye  bastola ya Dokta Lundi.

Oh! Mungu, Ni mabalaa mpaka lini sasa?

Na mara nilisikia kelele kutokea kule nje.

“Kelvin! Kelvin! Fungua! Sasa mbona umefyatua hiyo swichi tena?”

Ilikuwa ni sauti kutokea nje ya nyumba! Ndicho kitu nilichokuwa nakitarajia. Nikiwa nimejilaza uvunguni mwa kitanda nilinyamaza kimya nikisikiliza. Ilikuwa ni hekaheka mle ndani wakati wale wauaji wakikimbia ovyo huku na kule.

Twendeni! Kuna watu wanakuja…Shit!”

“Sasa huyu mwanamke?”

“Tutampata tu…Let’s Go!”

Nilisikia vishindo vyao vikitoka nje ya chumba, na huko sebuleni nilisikia kelele nyingine, bila shaka walikutana na watu waliokuwa wanaingia sebuleni kwa Kelvin kuja kujaribu kurekebisha hitilafu ya umeme.

“Heyy! Nyie nani…”

“Toka!”

“Yallaaaa! Wezii!”

Ohh! Shiit! Let’s Gooooooo!”

Nilisikia vishindo na mikikimikiki huko nje, na wakati huohuo Kelvin alizidi kulia mle ndani. Nilitoka kule uvunguni na kumuendea pale niliposikia sauti yake ikitokea.

“Kelvin! Kelvin…? Vipi?” Nilimsogelea huku nikipapasa kutokana na kiza.

“Wamenipiga risasi! Nakufa Tigga… sa…sama…hani kwa kuto…kuamini!”

“Aaaah! Kelvin! Nyamaza ngoja nitafute msaada…”

“Nenda Tigga! Wata…rudi! Mi’ nakufaaaa!”

Hii nini tena sasa?

Nilisikia mlipuko wa bastola huko nje na nikaruka kwa mshituko huku yowe likinitoka. Watu walipiga mayowe huko nje.

“Nenda Tigga!”

Nilikurupuka bila ya kujijua. Nilikimbilia kwenye kitanda cha Kelvin na kutoa tochi niliyojua kuwa huwa inakaa kwenye droo ya kando ya kitanda kile. Niliwasha ile tochi,nikakusanya vitu vyangu haraka haraka na kuvitia kwenye mkoba wangu, pamoja na ile kamera ya Gil.

Nilikimbilia bafuni kwa Kelvin nikiwa na ile tochi mkononi. Niliichukua sabuni kubwa aina ya Geisha ambayo Kelvin hupenda kuogea na kuitumbukiza kwenye ule mkoba wangu na kurudi mbio kule chumbani. Kelvin alikuwa akigaragara pale sakafuni huku damu ikimvuja ingawa sikuweza kujua jeraha lilikuwa wapi hasa.

Huko nje nilisikia gari likitia moto na kuondoka kwa kasi. Nilimuinamia Kelvin na kutaka kumsemesha, lakini alinihimiza niondoke.

Go Tigga…watu watajaa sasa hivi!”

Na hata aliposema maneno yale, nilianza kusikia ving’ora vya magari ya polisi kwa mbali.

Iam so sorry dear!” Nilisema kwa sauti ya chini na kuiacha ile tochi ikiwaka mle ndani kando yake, nami nikatoka mbio nje ya nyumba ile huku nikitiririkwa na machozi nikiwa na begi langu mgongoni.

SEHEMU YA TATU:

Nilikurupuka kutoka usingizini huku nikipiga yowe kubwa. Niliketi kitandani na kuangaza huku na huko ndani ya chumba ambacho kilikuwa kigeni kwangu. Jasho lilikuwa likinitoka na koo lilinikauka. Ilikuwa ni ndoto ya kutisha iliyojumuisha matukio ya kuogofya niliyoyaona kule msituni siku si nyingi zilizopita ambayo ilinifanya nikurupuke namna ile kutoka usingizini. Kwa sekunde kadhaa nilizidi kuduwaa pale kitandani bila ya kujua nilikuwa wapi na nilifikaje mahala pale, kisha nikakumbuka. Niliteremka kutoka kitandani na kuelekea juu ya meza iliyokuwamo mle ndani na kuchukua chupa ya maji ya Uhai na kuyabugia kwa pupa. Nilirudi na kuketi kitandani na kuitafakari ile ndoto.

Niliota matukio ya kule msituni na jinsi nilivyokuwa nikihangaika kuifukuza ile midege iliyokuwa ikiwadonoa wale wenzangu waliouawa kule msituni, na nilipokuwa nikiwafukuza, mmoja wa midege ile alikuwa ameng’ang’ana kuudonoa uso wa bwana Ubwa Mgaya, ila nilipomsogelea, bwana Ubwa Mgaya aligeuka na kuwa Kelvin.

Oh! Mungu wangu!

Nilimfikiria Kelvin na moyo ulianza kunipiga kwa nguvu. Sijui ana hali gani huko aliko! Bila shaka atakuwa amekufa, kwani nilimwacha bila msaada wowote…

Lakini kwa nini hukutaka kuniamini Kelvin?

Nilipotoka mbio pale nyumbani kwa Kelvin sikuwa na uelekeo maalum na sikujua nilikuwa nakimbilia wapi. Ila kitu kilichonisaidia ni kuwa kule nje kulikuwa kuna mtafaruku mkubwa uliotokana na ule mlipuko wa risasi kutoka kwenye bastola ya wale wauaji niliofanikiwa kuwakurupusha kwa kutawanya kiza katika nyumba ile. Nilitoka mbio kwa muda mfupi na nilipopotelea mtaa wa pili tu nilianza kutembea haraka haraka huku nikilia peke yangu kwa kwikwi. Kiza kilikuwa kimeingia na eneo la Sinza ndio lilikuwa linaamka. Watu walikuwa wamejaa katika mabaa mengi yaliyotapakaa eneo lile huku muziki ukisikika kutoka kila kona.

Nilikuwa nimechanganyikiwa vibaya sana, na nilijaribu kufikiri ni kitu gani nilitakiwa kufanya lakini ilikuwa vigumu sana kubaini. Akili ilikuwa imekufa ganzi. Nilijilazimisha kuogopa suala la Kelvin kupigwa risasi na wale wauaji, lakini cha ajabu nilijikuta siogopi kabisa. Hisia zote zilikuwa zimekufa ganzi.

Nilizidi kukata mitaa ya Sinza bila ya kujijua hadi nilipojihisi kuchoka. Niliangallia saa yangu ikaniambia muda ulikuwa ni saa tatu kasoro robo za usiku.

Sasa niende wapi Mungu wangu saa hizi!

Nilijua kuwa kwa hali iliyofikia, nilitakiwa kuripoti kituo chochote cha polisi kujisalimisha na kupata msaada. Lakini kila nilipokumbuka maelezo ya Kelvin kuwa Dokta Lundi alifika ofisini na hatimaye nyumbani kwake akiwa na askari wa jeshi la polisi, niliingiwa woga na wasiwasi mkubwa iwapo huko nitapata msaada ninaouhitaji. Kwa kadiri nilivyoelewa, pamoja na kuwa nawindwa kwa nguvu sana na wale wauaji wabaya, pia nilikuwa natafutwa na polisi sio tu kwa kile kimuhemuhe nilichozusha kule kwa mkuu wa wilaya, bali pia kama mhusika wa yale mauaji yasiyo na maana kule msituni. Kwenda kituo cha polisi kwa sasa ni sawa na kujipeleka mwenyewe kwa Pilato. Nilidhani kuwa njia salama kwangu ni kwenda kwa mtu mkubwa kabisa katika jeshi la polisi nikiwa na ule ushahidi wangu wa mkanda wa video, vinginevyo ule mkanda unaweza ukapotelea mikononi mwa Dokta Martin Lundi muongo, na huo ndio utakuwa mwisho wangu.

Sasa niende wapi?

Suala la kwenda nyumbani kwangu halikuwepo kabisa, kwani bila shaka kama wale watu wabaya walikuwa wameamua kunifuatilia kwa nguvu kiasi kile, basi huko ndio wangekuwa wamepiga kambi kabisa.

Nilifikiria kwenda nyumbani kwa mama yangu Tabata, lakini nilihisi kuwa nako ningemkuta Dokta Lundi na vibaraka wake wakinisubiri. Nilifikiria kwenda kwa mmoja kati ya marafiki zangu wachache, lakini sikulipenda kabisa wazo la kumgongea mtu usiku kama ule na kumpelekea mashaka yangu. Nilikimbilia kwa Kelvin na matokeo nimeyaona, sasa itakuwaje nikienda kwa mmoja wa hao marafiki zangu halafu Dokta Lundi akaniibukia huko huko? Ingawa unaweza kuona kuwa nilikuwa nampa huyu Martin Lundi uwezo mkubwa wa kimungu wa kuweza kunifikia mahala popote niwapo, lakini kwa wakati ule akili yangu ilikuwa imeingiwa na woga mkubwa kabisa. Nilikuwa nimegubikwa wasiwasi wa hali ya juu.

Paranoid?

Niliamua kupitisha usiku ule wa mashaka kwenye nyumba ya wageni, ambamo baada ya kujitahidi kupata usingizi kwa shida, nilijikuta nikikurupushwa na ndoto ile ya kutisha.

Mwili ulinisisimka.

Ndani ya masaa sabini na mawili mlolongo mzima wa maisha yangu ulikuwa umebadilika kwa namna ya ajabu kabisa. Ndani ya muda huo, maisha yangu yaliyokuwa yamepambwa na ndoto nzuri sana za mafanikio na matarajio makubwa, yaligeuka na kuwa ndoto moja ya kutisha sana iliyogubikwa mashaka mazito. Ndani ya masaa hayo nilikuwa nimevunja uchumba kama masihara, na bila shaka mtu aliyekuwa mchumba wangu alikuwa amepoteza maisha.

Kwa nini?

It is  always the very good times of one’s life that normally turns into one’s very bad times in no time

Nilianza kulia upya.

Nililia kwa unyonge na upweke. Nililia kwa kusikitikia maisha yangu yaliyoharibiwa bila sababu. Niliwalilia wenzangu niliokuwa nao kule msituni, waliouawa bila hatia.

Nilimlilia Kelvin.

Nililia sana na kwa muda mrefu. Kisha nilijilaza kitandani, huku nikijihisi mchovu kuliko kawaida.

Nilipitiwa na usingizi.

Lakini muda si mrefu baadaye nilishtushwa na vishindo na kelele nje ya chumba changu. Nilikurupuka nikiwa makini ghafla. Nje ya chumba kile nilisikia kelele za watu waliokuwa wakifoka na kushurutisha wapangaji wengine wafungue milango yao. Nilihamanika vibaya sana. Niliangaza huku na huko ndani ya chumba kile nisione pa kukimbilia. Kile chumba kilikuwa ni kama kile cha Kelvin, kikiwa na bafu lake kwa ndani, ila mlango wa kutokea ulikuwa ni mmoja tu. Nilinyakua koti langu la jinzi na kulivaa haraka haraka na kuanza kuvuta viatu vyangu kutoka chini ya kitanda huku moyo ukinienda mbio wakati niliposikia mlango wa chumba changu ukigongwa kwa nguvu.

“Nani?” Niliuliza kwa sauti ya kitetemeshi huku nikihangaika kuvaa viatu.

“Polisi! Fungua!” Sauti kali ilijibu kutoka nje ya mlango ule na kuamrisha.

Mungu wangu, nimenyakwa! Nilienda haraka mpaka pale mlangoni, nikiacha kuvaa viatu na kuuliza kwa mashaka.

“Mnataka nini…?”

Mlango ulipigwa ngumi kwa nguvu.

“Hebu fungua mlango mwanamke…! Upesiiii, Ebbo!”

Nilifungua mlango haraka kwa woga na nilijikuta nikisukumiwa ndani kwa nguvu na askari wawili wakiingia mle ndani, mmoja akiwa mwanamke. Nilirudi nyuma na kubaki nikiwakodolea macho kwa woga. Yule askari wa kiume alipita moja kwa moja hadi kule bafuni na kukagua huku na huko, na kurudi pale chumbani. Yule wa kike aliliendea kabati la nguo la mle ndani na kulifungua. Hakukuta kitu, hivyo akarudi na kusimama mbele yangu.

“Ni… niwasaidie nini afande…” Niliuliza kwa wasiwasi. Badala ya kunijibu wale askari walikuwa wakinitazama huku nyuso zao zikificha hisia zozote ambazo ningeweza kuzisoma, kisha yule mwanaume aliongea.

“Uko peke yako humu?”

“Ndiyo…”

“Mwanamke peke yako gesti?” Yule mwanamke alidakia. Hili sikulijibu.

“Wewe ni nani, na kwa nini uko hapa saa hizi?” Yule askari wa kiume aliniuliza. Sikusita, nilitoa jibu hapo hapo.

“Naitwa Mwajabu, nimelala hapa gesti kwa sababu sina mwenyeji hapa mjini nami ni msafiri…”

“Ukilala ndio huwa unavaa nguo namna hii? Je ukioga?” Yule askari wa kike aliniuliza.

“Nimevaa nguo baada ya nyie kuanza kunigongea… ndio maana nilichelewa kufungua mlango.” Nilimjibu.

“Una kitambulisho?”

“Sina.” Walitazamana, kisha wakaniamrisha nitoke nje. Huko nilikuta askari wengine wapatao wanne, mmoja kati yao akiwa mwanamke. Wapangaji wengine walikuwa wamesimamishwa nje ya milango ya vyumba vyao, nami nikaamriwa nisimame mbele ya mlango wangu. Nikiwa nimejawa wasiwasi na udadisi, niliwatazama wale wapangaji wengine waliotolewa vyumbani mwao. Wengi wao walikuwa wawili wawili,yaani mume na mke, na walikuwa wakilalamika kwa kuingiliwa faragha yao, hasa wanaume ambao bila shaka walikuwa pale kwa kujiiba wakisaliti ndoa zao.

Nilimgeukia yule askari wa kike.

“Afande kwani kuna nini… mbona mnadhalilisha watu namna hii?”

“Huu ni msako wa machangudoa… na wewe ni mmoja wao kwa hiyo usijitie kutoelewa hapa!”

Eh! Kwanza kichaa… Paranoid Schizophrenia… sasa changudoa! Ni nini hiki?

“Hah! Mi’ sio changudoa… mi’ ni msafiri…”

“Wasafiri huwa hawakai kwenye vijigesti vya vichochoroni kama hivi, halafu huwa wanatembea na vitambulisho. Tulia hapo tuelekee kituoni sasa hivi!” Alinijibu yule askari wa kike halafu akawaendea wale askari wengine na kuanza kuwaeleza vitu ambavyo sikuweza kuvielewa huku akinioneshea kidole. Wawili kati ya wale askari niliowakuta pale kwenye korido nje ya chumba changu walinisogelea taratibu huku wakinitazama kwa makini. Kwa namna fulani nilihisi kuwa pale mimi ndio nilikuwa kusudio la msako ule, ila nilishindwa kuelewa ni vipi walijua kuwa nipo kwenye ile gesti, ambayo kwa hakika ilikuwa vichochoroni. Na kama hivyo ndivyo, basi kwa hakika lile kundi la Dokta Martin Lundi lilikuwa hatari sana. Na kama haikuwa njama ya Martin Lundi muongo, basi ilimaanisha kuwa ule ulikuwa ni msako wa polisi kweli, ambao kwa vyovyote mwisho wake ilikuwa ni kupelekwa kituoni tu. Sikuwa na shaka hata kidogo kuwa iwapo nitafikishwa kituoni tu, basi nitakuwa kwenye mashaka mazito.

Mungu wangu, hivi nitaweza kuondokana na balaa hili mimi?

“Enhe, msichana, mbona uko hapa gesti peke yako?” Mmoja wa wale askari wengine, mwanaume aliniuliza. Nilitaka nimuulize iwapo hilo lilikuwa ni kosa, lakini kabla sijajibu, yule askari mwingine wa kike alidakia. Nilimhisi kuwa na umri wa kati ya miaka thelathini na tatu au na tano. Alikuwa na sura ya kuvutia, na yale mavazi yake ya kiaskari yalimkaa vizuri sana, hasa suruali yake ambayo ilionesha jinsi alivyojaaliwa makalio mazuri ya kuvutia.

“Na usituletee habari ya kuwa eti umsafiri… msafiri huna hata mzigo?”

Nilibaki nikiwakodolea macho wale askari nisijue la kuwaeleza. Na wakati bado naendelea kushangaa, yule askari mwanamke alinisukumia tena chumbani mwangu na kufunga mlango kwa ndani, akimuacha yule mwenzake kule nje. Bila ya kunitazama alitembeza macho mle chumbani na kuniuliza. “Umesema unaitwa nani?”

“Mwajabu…”

Aliliendea kabati la nguo la mle ndani na kulifungua kwa kutumia fimbo yake na kuchungulia ndani bila ya kushika kitu. Hakukuwa na kitu. “Unasema we’ ni msafiri… unatokea wapi na unaelekea wapi?” Aliuliza tena bila ya kunitazama huku akielekea kule bafuni.

“Natokea Mkuranga… naenda Zanzibar…” Jibu lilinitoka kana kwamba nilikuwa nasema ukweli. Yule askari aliguna na kurudi kando ya kitanda changu. Akiendelea kutonitazama, alilisukuma kwa fimbo yake begi langu dogo lililokuwa pale kitandani, kisha alilichukua na kukung’uta vilivyokuwamo ndani yake pale kitandani.

“Zanzibar unaenda kufanya nini?” Aliniuliza huku akipekua vile vitu vilivyomwagika pale kitandani. Aliinua ile kamera ya Gil na kuitazama kwa makini.

“Ku… kununua nguo za biashara…”

Aliifungua ile kamera sehemu ya kuwekea kaseti na kuchungulia ndani. Ilikuwa tupu. Nilikuwa nikitazama kila kitendo chake kwa makini huku moyo ukinienda mbio. Yule askari wa kike aliiweka kitandani ile kamera, na kuanza kupekua vitu vyangu vingine kwa muda na kwa utaratibu wa hali ya juu. Nilizidi kupata wasiwasi kwani huyu askari alionekana kuwa anajua anachofanya na sio anayebahatisha tu ambaye ningeweza kumlaghai kirahisi. Aliinua tena ile kamera na kuitazama kwa makini, huku akiigeuza huku na huko. Hatimaye aliiweka kitandani na kunitazama usoni kwa mara ya kwanza tangu aingie mle ndani.

Ok, sasa mchezo basi Tigga, where is the tape?” Aliniuliza huku akiwa amenikazia macho kiaskari hasa, akimaanisha nimweleze ni wapi ulipo ule mkanda wa video wenye ushahidi wa mauaji ya yule mtu asiye na jina kule msituni.

Mshituko nilioupata kwa swali lile ulikuwa mkubwa sana. Niliruka kana kwamba nimepigwa kofi na kubaki nikimkodolea macho yule mwanamke aliyevaa mavazi ya kiaskari, kana kwamba nilikuwa nimeona jini.

Mimi nilijitambulisha kwake kwa jina la Mwajabu, sasa yeye ameniita kwa jina langu halisi na anajua juu ya ule mkanda wa video! Kwa hiyo muda wote ule alikuwa akijua kila kitu!

Hii ni njama ya Dokta Martin Lundi muongo! Oh, My God! Sasa nitapata wazimu!

Nilimtazama kwa kihoro yule mwanamke.

Hii ni babu kubwa! Na huyu naye ni mwenzao?

“Mbo… mbona sikuelewi Afa… nde?” Nilijitutumua kumuuliza huku nikirudi nyuma kwa woga.

“Usinitanie mimi wewe! Lete huo mkanda sasa hivi!” Yule askari alinifokea na hapo hapo alinitolea bastola na kuniwekea usoni. Sikumjibu kitu. Nilibaki nikiukodolea macho mdomo wa ile bastola huku moyo ukinienda mbio. Tulibaki tukitazamana kwa muda huku yule askari akinihemea usoni kwa hasira. Alipoona bado namkodolea macho bila kumjibu, alinidaka koo na kunisukumia kitandani.

“Tunajua kuwa unao huo mkanda… tunautaka… na nakuahidi kuwa tutayafanya maisha yako yawe mabaya sana hapa duniani mpaka utautoa!” Alinifokea kwa sauti ya chini huku akinitomasa puani kwa mdomo wa ile bastola yake.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa hawa watu kujidhihirisha kwangu, nami sikuweza kuiachia nafasi hii, ingawa nilikuwa nimetishika vibaya sana.

“Kwani nyie ni kina nani? Wewe sio askari… ni mmoja wao!. Mnataka nini kutoka kwangu?”

“Kauli ya kijinga na swali la kijinga! Mimi sio askari wakati unaniona kuwa ni askari? Unauliza tunataka nini wakati nimekwambia tunautaka huo mkanda! Mjinga sana wewe!”

“Nyinyi?Nyie ni kina nani?”

“Si kazi yako kujua… where is the tape Goddamn it?” Yule askari wa kike alinijibu kwa ghadhabu huku akisisitiza nimpatie ule mkanda wa video. Aliniudhi.

“Mnh! Mi’ naona wewe ndio mjinga. Sasa nikikupa huo mkanda halafu mimi hatima yangu itakuwa nini?” Nilimuuliza kwa kebehi. Alinibamiza kofi kali sana la ghafla na macho yalinichomachoma kwa machozi machanga. Nikiwa sijawahi kupata kipigo cha aina yoyote ile kwa miaka mingi sana, vipigo nilivyopata siku ile viliniuma sana. Kwanza Dokta Lundi na vibaraka wake kule kwa Kelvin, halafu huyu mwanamke mwenye mavazi ya kiaskari.

“Mi’ n’takuua ukinichezea we’ mtoto, lete huo mkanda…”Alinikemea kwa sauti ya chini huku akinididimizia bastola yake kooni.

“Sina mimi huo mkanda!… kwani rafiki yako Martin Lundi muongo hajakueleza?”

Yule askari alisonya kwa hasira na kuikoki bastola yake huku akiididimiza kwa nguvu katikati ya koo langu na kuniambia kwa ghadhabu. “Usicheze na serikali Tigga… sisi tuko kila mahali, huwezi kutukwepa. Salama yako ni kutoa ushirikiano unaohitajika…”

No! Wewe sio askari na wala nyie… sijui ni watu gani, lakini nyie sio serikali… serikali haiko hivyo…”

The tape Tigga! Nautaka huo mkanda wa video sasa hivi!”

“Suala hilo nilishalimaliza kwa rafiki yako Martin Lundi muongo… kanda iko kwa wakili wangu!” Nilimkemea huku nikimsogezea uso wangu kwa kiburi. Yule askari alitoa sauti ya kukereka kwa jibu lile na kutaka kusema neno lakini ghadhabu zilimkaba kooni hivyo alibaki akinitumbulia macho kwa hasira, akijaribu kuamua achukue hatua gani badala ya kunilipua kwa ile bastola yake. Tulitazamana, na katika muda ule niliona kuwa yule dada alikuwa tayari kunilipua kwa risasi, kwani jibu langu lilimghadhibisha vibaya sana. Nilishuhudia midomo ikimcheza kwa hasira na macho yakimwiva.

Nilibaki nikimtazama kwa woga mkubwa na wasiwasi usio kifani. Bado shavu lilikuwa likinichonyota kutokana na kofi lake kali. Tulibaki tukitazamana kwa muda mrefu,hakuna mmoja kati yetu aliyesema neno.

Na mara yule askari wa kiume aliita kutokea nje ya chumba changu akimhimiza yule mwanadada waondoke nami pamoja na wale wapangaji wengine walioshindwa kujieleza vizuri kule nje kuelekea kituoni.

“Dakika moja afande!” Yule mwanadada askari alimjibu kwa sauti huku bado akiwa ananitazama usoni kwa macho ya ghadhabu. Hatimaye alishusha pumzi ndefu, na huku akilegeza mdidimizo wa bastola yake shingoni kwangu alinong’ona kwa hasira.

“Unafanya kosa kubwa sana Tigga, na utajuta kwalo!”

Kisha alisonya na kuiweka bastola yake kwenye mkoba wake na kuelekea mlangoni kwa mwendo wa haraka akiniacha nikiwa nimeduwaa mle chumbani nikimtazama huku nikijitahidi kumeza mate bila mafanikio. Alipofika mlangoni nilimsikia yule askari wa kiume alimuuliza juu yangu. Yule mwanadada aliyevaa mavazi ya kiaskari alisimama mlangoni na kunitazama kwa muda, kisha akamjibu huku bado akiwa ananitazama.

“Hana matatizo huyu… ni msafiri anayeelekea Zanzibar. Lets get out of here!” Kisha alifunga mlango taratibu na kutoweka.

Nilibaki nikiwa nimeduwaa.

Heh! Hawa watu… ni watu gani hawa? Kwa nini wanakuwa na uwezo wa kunifuatilia namna hii? Na vipi wanakuwa na namna ya kujiingiza kwenye nyanja za kiserikali namna hii? Hivi yule mwanamke ni askari kweli au bandia?

Yaani kichwa kilinizunguka kwa maswali hayo kwa muda mrefu nikiwa nimekaa pale kitandani bila ya kupata dalili ya uelewa. Lakini swali kubwa zaidi lililobaki kichwani mwangu lilikuwa moja tu: kwa nini yule dada askari hakunikamata na kunipeleka kituoni?

Naam. Kwa hakika hili kwangu lilikuwa ni a hundred dollar question, kama wamarekani wanavyopenda kusema. Kwa nini yule dada asinikamate na kuniweka chini ya ulinzi? Kwani baada ya kituko kile, sikuwa na shaka kuwa alikuwa ana taarifa zote za tafrani niliyoizusha na kizaazaa nilichoacha kule Manyoni kwa mkuu wa wilaya.

Sasa kwa nini ameniacha?

Kadiri nilivyozidi kujiuliza maswali hayo, ndivyo taratibu nilipoanza kupata mwanga.

Nilijishawishi kuwa wale watu wanaonisakama hawakuwa wakifanya hivyo ili wanitie kwenye mikono halali ya sheria, bali walikuwa wananitaka kwa sababu yao binafsi, ambayo ni kuupata ule mkanda wenye ushahidi wa madhambi yao niliojinadi kuwa ninao.

Kitu kingine ambacho kilijitokeza ni kwamba wale watu… watu gani…? walikuwa na uwezo wa kutumia mamlaka za nyanja mbalimbali za kiserikali kwa maslahi yao.

Sasa hii ilibadilisha lile swali langu la msingi: hawa watu ni akina nani?

Niliwaza na kuwazua lakini bado niliishia kujiongezea maswali mengi yasiyo na majibu. Lakini kitu kimoja kilibaki akilini mwangu. Ule mkanda wa video ndio ulikuwa salama yangu, kwani nilikuwa na hakika kabisa kuwa wale watu hawashindwi kabisa kuniua, lakini hawatoweza kufanya hivyo mpaka waupate ule mkanda. Kabla ya hapo hawatathubutu kuniua, labda wajithibitishie kuwa hakuna mtu mwingine yeyote anayejua juu ya mambo yaliyomo ndani ya mkanda ule zaidi yangu. Lakini hilo wazo halikunipa amani hata kidogo, hasa nilipomkumbuka yule mtu niliyempachika jina la Macho ya Nyoka. Yule jamaa ni kichaa, angeweza kuniua wakati wowote, kama jinsi alivyomuua yule mtu asiye na jina kule msituni.

Nilikumbuka maneno makali ya yule askari wa kike aliyetoka mle chumbani muda si mrefu uliopita.

“… na nakuahidi kuwa tutayafanya maisha yako yawe mabaya sana hapa duniani mpaka utautoa!”

Kufikia hapa niliamua kuwa sina ujanja bali niendelee kukimbia tu mpaka nipate mtu nitakayeweza kumuamini na kumpa ule mkanda na ambaye ataweza kunisaidia, kwani lile suala sikuwa na uwezo wa kupambana nalo peke yangu.

Lakini ni nani wa kunisaidia? Na ni nani wa kumuamini?

Mambo yaliyonikuta kwa Mkuu wa Wilaya na kwa Kelvin yalinifanya nizidi kujiona kuwa bado niko peke yangu, nisiye na kimbilio.

Na yote hii ni kwa ajili ya mambo niliyoyaona na ambayo sasa yako kwenye ule mkanda wa video. Sikusubiri zaidi.

Nilikurupuka ghafla na kuanza kukusanya vitu vyangu vilivyotawanywa ovyo pale kitandani na kuvishindilia kwenye begi langu. Niliichukua ile sabuni aina ya Geisha niliyoichukua bafuni kwa Kelvin na kwa kutumia kile kisu changu kidogo, nilifuatisha mchinjo mwembamba sana nilioukata kuuzunguka mgongo wa ile sabuni wakati nilipokuwa nimejifungia bafuni kwa Kelvin kabIa ya kuanza kuoga, na kuitenganisha ile sabuni kwa ubapa na kubaki na vipande viwili mithili ya silesi mbili za mkate. Katikati ya kila ubapa wa ile sabuni kwa ndani nilikuwa nimechimba kwa kisu kiasi cha kuweza kuzamisha ile kaseti ndogo kabisa ya video. Kwa mikono iliyotetemeka na huku moyo ukinipiga kwa nguvu, niliitoa ile kaseti ambayo hapo awali nilikuwa nimeizungushia nailoni ya sabuni kabla ya kuizamisha kwenye kishimo nilichochimba kwenye moja ya bapa mbili za ile sabuni niliyoikata kistadi na kuibananisha tena kwa maji kidogo na kuuficha ule mchinjo kwa rojo zito la sabuni ile baada ya kuiloweka na kukauka.

Ile kaseti ilionekana safi na salama, wala haikuonekana kuathirika na kificho kile kilichoiokoa kutoka kuangukia mikononi mwa dokta Martin Lundi na kuendelea kuiokoa tena kutoka kuangukia mikononi mwa yule askari wa kike aliyeahidi kuyafanya maisha yangu yawe mabaya mpaka atakapoitia mkononi ile kaseti.

Kwa kutaka kuhakikisha, niliingiza kwenye ile kamera ya marehemu Gil na kuirudisha mwanzo kidogo, kisha nikabonyeza sehemu iliyoandikwa ‘play’.

Kwenye kile kijiruninga kidogo cha kamera ile, nilimuona tena yule mtu asiye na jina akimg’ang’ania koo Macho ya Nyoka…

Niliizima na kutumbukiza ile kamera pamoja na ile kaseti ndani ya mkoba wangu.

Nilivaa viatu vyangu na kutoka haraka mle ndani bila kujali kuwa ulikuwa usiku.

Kwa wakati ule jambo la muhimu kwangu lilikuwa ni kuwa mbali na eneo lile kwa kadiri iwezekanavyo.

--

Nilipitisha sehemu iliyobaki ya usiku ule Club Billicanas, ambako nilijichimbia kwenye kona pweke ndani ya ukumbi ule na kuduwaa nikiangalia jinsi vijana wenzagu wakijirusha na kufurahi pamoja na wapendwa na marafiki zao. Baada ya kukurupuka kutoka pale kwenye ile gesti, sikuwa na kimbilio lolote la haraka nililoweza kulifikiria kwa wakati ule. Ingawa nilibahatika kupata watanashati kadhaa waliojitokeza kutaka kucheza nami na wengine hata kujaribu kunitongoza, sikuwa na hamu kabisa ya kujipumbaza na furaha zile, hivyo niliwakatalia kistaarabu na kuendelea kukaa kimya peke yangu ndani ya ukumbi ule.

Akili yangu ilikuwa imepigwa na bumbuwazi kwa jinsi mambo yalivyozidi kuniendea vibaya, kwani nilijiona nikizidi kudidimia katika dimbwi la uadui na tuhuma zisizo na msingi, bila ya matumaini ya kujinasua kutoka katika dimbwi lile. Na ilionekana kuwa kadiri mambo yalivyozidi kusonga mbele, ndivyo ule mtandao dhalimu wa akina Martin Lundi ulivyozidi kupanuka.

Angalau pale ndani ya ule ukumbi maarufu wa starehe sikuwa na wasiwasi wa kukurupushwa na vibaraka wa yule mtu anayejiita Martin Lundi, au wana usalama ambao nao nilikuwa na imani kuwa walikuwa wakinisaka. Nilikuwa na hakika kabisa kuwa katika mawazo yao wasingetarajia kabisa kwamba katika mazingira kama niliyokuwa nayo ningeweza hata kufikiria kwenda sehemu kama Club Billicanas.

Na kuanzia hapo niliamua kuwa salama yangu ilitegemea katika kufanya yale ambayo wao hawayatarajii.

Wao.

Nilimfikiria yule mwanadada aliyevaa mavazi ya kiaskari aliyeacha kuniweka chini ya ulinzi muda mfupi uliopita…

Wao ni nani? Who are these people?

Alfajiri kulipopambazuka nilitoka pamoja na washabiki wengine wa starehe waliokesha pale ukumbini na kuchukua teksi mpaka nyumbani kwa mama yangu Tabata, nyumba ambayo tuliachiwa na marehemu baba yetu.

Niliondoka pale nyumbani baada ya kuanza kazi na kwenda kupanga nyumba ya msajili maeneo ya Upanga ili niweze kujitegemea, nikimwacha mama na dada yangu wakiishi pale nyumbani. Kwa kuwa naye hakuwa ameolewa, na  kipato cha ajira yake hakikumuwezesha kupanga nyumba na kujitegemea kama mimi, dada yangu aliendelea kuishi na mama pale nyumbani.

Ilikuwa ni saa kumi na mbili kasoro robo wakati mama aliponifungulia mlango nami nikaingia ndani ya nyumba ile niliyolelewa tangu utoto wangu. Mama alionekana wazi kuwa ameshitushwa na ujio wangu, na mara nilipoingia ndani alifunga mlango haraka na kuniongoza hadi chumbani kwake ambako tulikumbatiana kwa nguvu huku sote tukibubujikwa na machozi kimyakimya. Nilimuuliza iwapo Koku, dada yangu alikuwepo nyumbani. Aliniambia kuwa alikuwa ameshatoka kwenda kazini. Koku alikuwa ni nesi wa hospitali ya wilaya ya Temeke. Nilibaki nikiangaza mle ndani huku nikitokwa na machozi. Kwa namna fulani nilihisi amani kwa kuwepo tu pale nyumbani na mama yangu.

“Oh! Tigga mwanangu! Ni nini tena kimekukuta mwanangu?” Mama alilalamika kwa sauti ya chini huku akibubujikwa na machozi. Sikuweza kujibu. Sasa nilikuwa nikilia kwa nguvu nikiwa nimemkumbatia mama yangu. Hapa nilikuwa nimepata liwazo nililokuwa nikilihitaji sana tangu nikutane na mtihani huu mgumu kabisa katika maisha yangu.

“Matatizo makubwa yamenikuta mama…” Nilibwabwaja kwa simanzi. Nilitaka kumueleza juu ya Kelvin, lakini jibu lake lilinishitua.

“Najua mwanangu… pole sana. Lakini unahitaji kitu cha kula… na mapumziko.”

“Unajua…?” Nilimuuliza huku nikimtazama kwa mashaka. Tulitazamana, na niliona kuwa alikuwa akinitazama kwa huzuni kubwa…

“Walikuja hapa… wakanieleza kila kitu…” Alinifafanulia huku akiniketisha kitandani kwake.

Hapo nilikuwa makini kupita kawaida. Walikuja hapa… wakanieleza kila kitu…

“Nani walikuja mama? Dokta Lundi? Dokta Martin Lundi alikuja hapa?”

“Ndio mwanangu… Dokta Lundi alikuja, akanieleza yote yaliyotokea…”

Nilimtazama mama yangu na nikahisi moyo ukiniisha nguvu. Kwa jinsi mama alivyokuwa akiongea, niliona kuwa lolote ambalo alikuwa ameelezwa na huyu mtu anayejiita Martin Lundi, alikuwa amelielewa vizuri sana na hakuwa na shaka nalo kabisa.

Eh! Mungu wangu!

Sikuwa na shaka hata kidogo kuwa Martin Lundi muongo atakuwa ameleta uongo na fitna zake kwa mama yangu, lakini nilikuwa na hakika kabisa kuwa mama asingeweza kumkubalia ule uongo wake kirahisi. Lakini kilichonishangaza ni kuona kuwa mama alikuwa anaongea kana kwamba alikuwa amemuamini! Nilimeza funda la mate, ambayo niliyahisi machungu kuliko kawaida.

“A… alikuja na polisi…?” Nilimuuliza mama kwa wasiwasi. Mama alinitazama kwa mshangao mkubwa sana. Kana kwamba alikuwa anamshangaa mtu mwenye wazimu.

“Polisi? Kwa nini aje na polisi? Hapana, alikuja na madaktari wenzake…”

Nilibaki mdomo wazi. Kwa hiyo hapa hakuja na askari. Ni uongo gani uliotumia kwa mama yangu Martin Lundi?

“Na akakueleza kila kitu…?”

Yes, my love. I am so sorry for you, lakini usiwe na wasiwasi, mama yako hatokuacha peke yako. Na nitahakikisha kila kitu kinakuwa sawasawa.”

How, mama? Utahakikishaje kuwa kila kitu kinakuwa sawa…? Kwani umeelezwa nini na Dokta Lundi? Yule ni muongo sana mama, isije ikawa…”

“Usiwe na wasiwasi mwanangu… mimi nitakuwa na wewe kila hatua mpaka mwisho.”

Nilichoka! Nilitaka kumuuliza alikuwa anamaanisha nini kwa kauli ile, lakini hakunipa nafasi. Aliinuka kwenda kunitayarishia chai nami nikaingia bafuni na ule mkoba wangu ambako nilioga haraka haraka na kupiga mswaki kwa kutumia kidole na kusukutua kwa dawa ya meno. Niliogopa hata ile kuwaza tu kuwa na mama naye atakuwa amekolezwa ule ujinga wa Dokta Lundi. Nilitaka kuamini kuwa alikuwa upande wangu na aliazimia kunisaidia mpaka mwisho wa mkasa huu.

Lakini hivyo ndivyo alivyokuwa akimaanisha kwa kauli yake ile?

Au alikuwa anamaanisha vinginevyo?

Nilipotoka nilimfuata mama jikoni ambako alikuwa akimalizia kukaanga mayai. Nilikunywa chai kulekule jikoni huku akilini nikiwa najaribu kutafakari ni nini maana ya yale maneno ya mama. Baada ya kunywa ile chai na kushiba kisawasawa, nilianza kujihisi usingizi mzito. Nilikumbuka kuwa sikuwa nimepata muda wa kulala sawasawa tangu niingie hapa jijini kutoka kule Manyoni ambapo balaa lote hili lilipoanzia. Nilijilazimisha kupingana na usingizi ule na kumkabili tena mama yangu.

“Mama… umesema Dokta Lundi amekueleza kila kitu… amekueleza nini?” Hatimaye nilimuuliza mama yangu. Alinitazama kwa muda, kisha alishusha pumzi kabla ya kunijibu taratibu.

“Amenieleza kuhusu… kuhusu yaliyotokea kule msituni Tigga. Lakini amenihakikishia kabisa kuwa yote yaliyotokea kule si jukumu lako! Niliogopa sana mwanangu, lakini Dokta Lundi is such a humble man… (ni mtu mkarimu sana…) ameahidi kukusaidia kwa kadiri ya uwezo wake…”

Mwili ulinifa ganzi na nikahisi ile nyumba ikizunguka. Yaani mama alikuwa anaamini kuwa Dokta Lundi ni mtu mzuri mwenye nia ya kunisaidia!

Sikuamini.

“Mama! Unataka kuniambia kuwa umeamini aliyokueleza Dokta Lundi?” Nilimuuliza kwa jazba huku nikiinuka kutoka kwenye kiti nilichokuwa nimekalia na kumsogelea huku nikimtazama kwa makini. Mama alinitazama kwa mashaka huku akijishughulisha kusogeza vile vyombo nilivyokuwa nikilia pale mezani.

“Sasa kwa nini nisimuamini Tigga mwanangu? Yule ni mtu mwenye nia ya kusai…”

“Yule ni mtu mwenye nia ya kuniua mama! Na usimruhusu kabisa aje karibu na wewe, atakudhuru! Dokta Martin Lundi ni muuaji mama, na mimi nimemuona kwa macho yangu akishirikiana na wenzake kumtesa na hatimaye kumuua mtu kule msituni.” Nilimkatisha mama yangu kwa hasira.

Kwa nini watu wanapenda kumuamini Martin Lundi muongo?

“Hapana Tigga… hayo yote yamo katika fikira zako tu mwanangu… ni kutokana na…”

Paranoid Schizophrenia?” Nilimkatisha mama yangu kwa uchungu, kabla hajamalizia ile kauli yake, na kuendelea; ”Hivyo ndivyo Dokta Lundi alivyokueleza mama? Kuwa hayo mambo ni fikira zilizojengeka bila msingi kichwani mwangu kutokana na huo ugonjwa unaosemekana kuwa ninao?”

“Tigga mwanangu, usiifanye hii hali iwe ngumu kuliko inavyohitajika…”

Nilitoa sauti ya kukata tamaa na kutikisa kichwa kwa masikitiko makubwa.

“Mama! Hivi kuna historia ya wazimu katika familia yetu? Kuna mtu yeyote… babu au bibi fulani huko nyuma, aidha upande wako au wa baba ambaye alipata kuugua wazimu?” Nilimuuliza kwa jazba. Mama alibaki akinitazama tu huku akivisogeza sogeza vile vyombo bila uelekeo maalum. Lile swali lilionekana kuwa lilimchanganya kidogo na niliona wazi kuwa wazo hilo halijawahi kumpitia kichwani mwake hata kidogo.

“Ennh, mama, hebu nieleze hilo… sijawahi kusikia hata siku moja… au mlituficha?” Nilizidi kumsukumia maswali.

“Hakuna Tigga, lakini…”

“Unaona? Mi’ najua magonjwa kama hayo yana namna ya kurithishwa katika familia, au nakosea?”

Mama hakunijibu. Niliona alikuwa amechanganyikiwa na nilimwonea huruma sana.

Nilihisi chuki ya hali ya juu kwa yule mjinga anayejiita Dokta Lundi kwa kutufikisha katika hatua hii mimi na mama yangu. Lakini kwa nini mama asiuone uongo huu? Mimi ni mwanae for God’s sake!

Nilimsogelea na kumuambia kwa kuomboleza: “Mama. Naomba uniamini mimi mwanao. Dokta Lundi ni muongo tena muongo mkubwa sana! Na wala sidhani kama ni dokta kweli yule. Anachofanya ni kupita akinipakazia uzushi wa ugonjwa huo wa uongo ili kuninyima nafasi ya kusikilizwa na kuaminika mahala popote nitakapokwenda. Na hiyo ni kutokana na mambo niliyoyaona kule msituni na ambayo nina ushahidi usiopingika… ushahidi ambao utamuathiri sana huyo Dokta Lundi na wenzake!”

Niliona kabisa kuwa hali ile ilikuwa ikimchanganya vibaya sana mama yangu, na nilizidi kumuonea huruma lakini ilibidi nimueleweshe.

“Mama, mi’ n’na ushahidi wa kuthibitisha kuwa Dokta Lundi si mtu mwema kama anavyotaka wewe umuone…”

“Amenionesha picha za kule msituni Tigga…watu wameuawa Tigga! Kama kuku…! Inatisha sana!” Alisema kwa sauti ya chini huku akilengwa na machozi.

“Na akakuambia kuwa ni mimi ndiye niliyewaua wale watu?” Nilimuuliza mama kwa uchungu. Hakunijibu, lakini katika macho yake niliona kuwa nilikuwa nimeuliza jibu. Iliniuma sana.

Mama! How can you believe such rubbish?” Nilibwata huku nikitupa mikono yangu hewani,nikimuuliza ni vipi anaweza kuamini upuuzi kama ule, kisha nikaendelea kwa sauti ya chini huku nikisisitiza kauli yangu kwa mikono yangu.

“Mama… ni yeye pamoja na wenzake watatu ndio waliofanya yale mauaji kule msituni! Na hakuna mtu yeyote anayejua hilo isipokuwa mimi. Huoni kuwa anafanya kusudi kunipakazia ugonjwa huo ili taarifa nitakazotoa dhidi yake na wenzake zitiliwe mashaka na kila mtu? Si unaona jinsi wewe mwenyewe unavyoshindwa kuniamini? Hivi ndivyo anavyotaka, na ndivyo inavyokuwa kila mahali niendapo mama! How can you believe him mama?” Nilimueleza kwa hisia kali huku nikihoji uhalali wa mama yangu kuamini uongo wa Martin Lundi kirahisi namna ile. Na hata pale nilipokuwa nikiongea maneno yale, nilijihisi uchovu na usingizi mzito. Nilipiga mwayo mrefu na kujibwaga tena kwenye kiti. Mama alinisogelea na kunipapasa kichwani.

“Pole sana Tigga. Unaonekana una usingizi, kwa nini usijipumzishe kidogo halafu tutaongelea hili jambo baadaye?” Aliniambia kwa upole. Na hii ndio tabia ya mama yangu ambayo toka utotoni mwangu nilikuwa siipendi. Akiwa na jambo lake basi yuko radhi mliahirishe kwa muda kuliko kukubaliana na wazo lingine, akitumaini kuwa baada ya muda utakuwa umeelewa ‘ujinga’ wako na kukubaliana na mawazo yake.

Sasa mimi sina muda wa kupoteza namna hiyo mama!

Nilimtazama mama yangu kwa kukata tamaa, na mwayo mwingine ukanitoka. Sikuwa nimepata usingizi wa kutosha usiku uliopita. Lakini huu sio wakati wa kulala! Dokta Lundi akitokea…

“Tafadhali usimruhusu Dokta Lundi anikamate mama… please!” Nilimwambia kwa sauti ya chini huku nikihisi macho yalikuwa mazito kuliko kawaida.

“Mi’ nakutakia yaliyo mema kwako mwanangu, na si vinginevyo.” Mama alijibu, lakini kauli ile haikunipa amani hata kidogo.Nilijilazimisha kuinuka na kwenda kujilaza kwenye kochi refu lililokuwa pale sebuleni huku nikiwa nimeukumbatia mkoba wangu. Mama alinishauri nikalale chumbani, lakini sikukubali, nilimwambia kuwa nataka kujipumzisha kwa dakika chache tu.

Nadhani nilisinzia kwa dakika chache sana, kisha nikahisi nikipambana na usingizi ule mzito, nikijitahidi usinielemee.

Lazima niamke! Lazima niamke!

Wazo hilo lilikuwa likinijia tena na tena ilhali usingizi ukizidi kunielemea. Kwa mbali nilisikia sauti ya mama yangu ikinisemesha. Niliinuka ghafla na kutazama kila upande, lakini nilikuwa peke yangu pale sebuleni. Ilikuwa ndoto? Hapana, nilisikia sauti ya mama ikitokea sehemu ndani ya nyumba ile. Alikuwa akiongea na nani? Aliniambia kuwa Koku alikuwa ameshaenda kazini, sasa huyo anayeongea naye ni nani? Niliinuka taratibu na kuelekea kule niliposikia sauti yake ikitokea.

Nilimkuta akiwa katika chumba cha kulia chakula. Alikuwa amekaa kwenye kiti akiwa amenigeuzia mgongo na alikuwa anaongea na simu, na alikuwa akimbembeleza kitu fulani huyo aliyekuwa akiongea naye. Nilisimama kando ya mlango wa kuingilia kule alipokuwepo na kujaribu kusikiliza maongezi yale huku moyo ukinienda mbio.

“… nataka nijue ni wapi hayo matibabu yatakapofanyika na mimi nataka niwepo…”

Usingizi ulinikauka mara moja, nikazidi kusikiliza.

“… yeye yupo hapa, lakini lazima na mimi niwepo…”

Moyo ulinilipuka na kuongeza mapigo.

Mama alikuwa anaongea na Dokta Martin Lundi!

Nilichanganyikiwa.

Haraka nilirudi kule sebuleni na kulinyakua lile begi langu dogo. Nilitembea haraka kuelekea mlango wa nyuma wa nyumba ile, na nilipopita tena kwenye ule mlango wa kuingia chumba cha kulia chakula, mama alikuwa ameshamaliza kuongea na simu.

“U… unaenda wapi Tigga… usingizi umeisha mara hii?” Aliniuliza huku akinisogelea. Moyo uliniuma kuliko kawaida. Sikuweza kumtazama.

“Na… naenda kulala chumbani…” Nilimjibu bila kumtazama na bila kupunguza mwendo wangu. Mwisho wa korido kabla ya kuufikia mlango wa nyuma wa nyumba ile kulikuwa kuna chumba cha wageni. Nilipokifikia nilisimama nje ya mlango wa chumba kile na kumgeukia mama yangu. Alikuwa amesimama akinitazama.

“Ennh… naomba uniamshe ifikapo saa saba…” Nilimwambia kwa sauti ya chini huku nikifungua mlango wa kile chumba.

“Sawa mama…” Alinijibu, kisha akanisogelea kwa hatua za haraka, nami nikamsubiri huku nikitazama sakafuni. Alinikumbatia kidogo na kunibusu kwenye paji la uso.

“Lala unono mwanangu… yote yatakwisha tu, muamini mama yako.”

Sikujua nimjibu nini, lakini machozi yalinitiririka nami nikageuza uso wangu ili asione jinsi nilivyoumia. Niliingia ndani ya kile chumba na kusimama nyuma ya mlango kwa ndani nikisikilizia mienendo ya kule nje huku moyo ukinipiga sana. Hakuna kilichotokea, kisha nikasikia maji yakimwagika jikoni na vyombo vikigongana. Nikahisi mama alikuwa akiosha vyombo jikoni.

No time to waste!

Nilitoka nje ya chumba kile taratibu na kufungua mlango wa kutokea nyuma ya nyumba ile taratibu mno. Nilitoka nyuma ya nyumba yetu na kuruka michongoma iliyofanya uzio wa kuizunguka nyumba ile na kutokea mtaa wa pili.

Huku nikitiririkwa na machozi, nilitembea kwa mwendo wa kasi kuelekea nisikokujua.

Nilikimbilia kwa Kelvin, nikakutana na usaliti nisioutegemea na roho iliniuma sana. Lakini hili la kukuta usaliti kama ule kwa mama yangu liliniuma zaidi. Sasa nitakimbilia wapi? Kwa nini hawa akina Martin Lundi wanakuwa na uwezo wa kuwarubuni watu mpaka wanafikia hatua ya kunigeuka namna hii?

Au inawezekana ikawa ni kweli mimi nina huo ugonjwa ninaosemekana kuwa ninao na mambo yote ninayoamini kuwa nimeyaona ni fikira zangu tu zenye maradhi?

Lakini nilipopapasa begi langu na kuigusa ile kamera ya marehemu Gil, nilipata hakika kuwa niliyoyaona yalikuwa ni kweli tupu.

Sasa ni nini hii?

Hata mama yangu! Oh, My God!

Ama kwa hakika sasa nilikuwa peke yangu, nisiye na kimbilio.

Ili iweje sasa?

Nilijua kuwa mama alifanya vile akiwa na imani, kuwa ananisaidia, kwamba anafanya kwa faida yangu.

Lakini sivyo mama! Martin Lundi ni muongo na muuaji! Nitawezaje kusema hadi niaminike?

Nilikuwa nikiwaza mambo hayo na mengi mengine huku nikipotelea mitaa ya nyuma kutoka ule uliokuwamo nyumba yetu. Sikuwa na uelekeo maalum, na kwa wakati ule sikujali. Jambo pekee nililojali kwa wakati ule ni kujiweka mbali na mikono ya yule mtu mbaya anayejiita Martin Lundi, na kundi lake.

Bila ya kujua nilikuwa nimezunguka na kufuata mtaa uliotokea mwanzoni mwa ule mtaa ambao nyumba yetu ilikuwepo. Nikiwa nimesimama mwanzoni mwa mtaa ule, niligeuka kutazama upande ilipokuwepo nyumba yetu ambapo ni katikati ya ule mtaa. Nilishuhudia kwa kihoro magari matatu yakisimama kwa kasi na vishindo nje ya nyumba yetu na watu wakiremka na kukimbilia nyumbani kwetu, huku wengine wakiizingira nyumba ile kwa nje. Nilidhani nilimuona Dokta Lundi miongoni mwao. Lakini kwa umbali ule sikuweza kuwa na uhakika. Niliongeza hatua na kupotea eneo lile nikimwomba Mwenyezi Mungu amsaidie mama yangu.

SEHEMU YA NNE

Siwezi kuelezea jinsi nilivyoumizwa na kitendo cha mama yangu kuamuakumuamini yule shetani anayejiita Martin Lundi na kupuuzia kabisa utetezi wangu. Kwa kweli hakuna maneno ambayo ninaweza kuyatumia hata yakatosha kuonesha ni kiasi gani jambo lile lilikuwa limeniumiza, kwani ilikuwa ni kupita kiasi.

Ni kweli nilipogundua kuwa Kelvin aliamua kunisaliti kwa shetani Martin Lundi hata baada ya kusikia maelezo yangu, niliumia hata nikahisi kuna ndoano iliyokuwa ikiuvuta moyo wangu kwa nguvu kubwa; lakini kuumia nilikoumia kutokana na hali iliyotokea pale kwa mama yangu, kulikuwa ni zaidi ya hivyo.

Hata hivyo, sikuwa na la kufanya. Lililotokea lilikuwa limeshatokea, na aliyelifanya alikuwa ni mama yangu. Angalau kwa Kelvin niliweza kuvunja uchumba na kuachana naye, lakini huyu alikuwa mama yangu, aliyenizaa kwa uchungu mwingi. Sasa vipi mtu kama Martin Lundi ameweza kumrubuni, kumlaghai na kumshawishi hata akaweza kumuamini yeye na akashindwa kuamini maelezo ya mwanaye aliyemzaa kwa uchungu mkubwa?

Nilishindwa kuelewa, na nilizidi kuchanganyikiwa iliponibainikia kuwa hata ningefanya nini, nisingeweza kumfuta asiwe mama yangu kama jinsi nilivyoweza kumfuta Kelvin kutoka maishani mwangu (sijui yu hali gani huko aliko). Hivyo nilimwomba Mwenyezi Mungu amnusuru mama yangu na ghadhabu za Dokta Lundi pindi atakapofika pale nyumbani na kukuta nimewatoroka kwa mara nyingine tena, wakati yeye alishampigia simu na kumhakikishia kuwa nilikuwepo pale nyumbani.

Baada ya kuwashuhudia kwa mbali akina Martin Lundi wakiizingira nyumba yetu, nilielekea moja kwa moja kituo cha basi na kupanda basi nililolikuta likipakia abiria pale kituoni bila ya kujali lilikuwa likielekea wapi, lengo likiwa ni kupotea kabisa eneo lile. Na njia nzima wakati basi lile likifanya safari yake ambayo nilikuja kuelewa baadaye kuwa lilikuwa likielekea Posta, nilikuwa ni mtu niliyepigwa bumbuwazi. Woga ulinitawala kupita kiasi kwani sasa ilikuwa imenifunukia waziwazi kichwani mwangu kwamba katika janga hili nilikuwa peke yangu.

Nilikwangua akili kutafuta hatua muafaka ya kuchukua, lakini niliambulia ukungu tu. Nilifikiria kumfuata dada yangu Koku kazini kwake, lakini nililifuta haraka wazo hilo, kwani nilijua kuwa asingeweza kunisaidia lolote katika mazingira yale.

Nilijua iwapo mama ameamua kuchukua msimamo aliouchukua kwenye suala lile, hakuna shaka kabisa kuwa na yeye atakuwa na mtazamo ule ule.

Nilidhani kuwa Koku angeweza kusaidia kwa kumbana Dokta Lundi kwa maswali ya kitaalamu juu ya ule ugonjwa anaonipakazia na hatimaye kubainisha uongo wake, lakini kama angefanya hivyo, basi hata mama angekuwa na mtazamo tofauti. Lakini pia nilikumbuka kuwa Koku alikuwa ni nesi wa kawaida tu.Yumkini akawa hana uwezo na utaalamu wa kuuelewa ugonjwa ule kama jinsi alivyouelewa Dokta Martin Lundi muongo.

Sasa nifanye nini…?

Niliamua kwenda ofisini kwangu, katika jumba la Makumbusho ya Taifa. Huenda huko ningepata baadhi ya majibu ya maswali yangu. Kwani si huko ndipo iliposemekana kuwa ile barua ya uongo iliyopelekwa kwa mkuu wa wilaya ilikuwa imetokea? Sasa niliona kuwa iwapo nilikuwa nashutumiwa kwa mambo yasiyo na msingi, nilipaswa kwenda kutafuta majibu kwenye kiini cha shutuma hizo. Shutuma za kuwa nilikuwa mgonjwa wa akili zilikuwa ni nzito na mbaya sana. Nilijua kuwa ile barua ilikuwa imeghushiwa, na hata uwepo wake hautambuliki kule ofisini kwetu. Njia pekee ya kujithibishia hilo ni kwenda ofisini. Si hivyo tu, bali pia nilijua kuwa vyovyote iwavyo, iliniwajibikia kuripoti pale ofisini baada ya kutoka kwenye ile safari iliyozaa balaa niliyotumwa na ofisi. Sikujua ningekutana na nini huko nilipoazimia kwenda, lakini nilienda.

Niliingia kwenye jengo la ofisi yetu na kuelekea moja kwa moja ofisini kwa afisa utumishi, ambaye ndiye mwangalizi wa masuala yote ya wafanyakazi na ajira zao, lakini kabla sijaifikia ofisi yake niliwahiwa kwenye korido na baadhi ya wafanyakazi wenzangu ambao walinizingira kwa maswali kemkemu kuhusu matukio ya huko msituni.

Wapo walionipa pole, wapo walioulizia ilikuwaje hadi wenzangu wakaangamia kule porini, wakati wengine waliniambia kuwa kwa kujipeleka pale ofisini nilikuwa nimejitia kwenye mtego na kunishauri niondoke haraka, ilhali wengine wakionesha wazi kuwa walikuwa wakiniogopa.

Sikuweza kujibu swali hata moja, kwani yalikuwa yakija bila mpangilio maalum, nami nikaanza kuingiwa uoga na kuujutia uamuzi wangu wa kwenda pale ofisini. Niligundua kuwa habari zangu zilikuwa zimefika pale ofisini, na kwamba kwa ujumla ilieleweka kuwa sikuwa mtu salama tena kuwa karibu naye. Hili nililibaini kutokana na hali iliyojitokeza pindi nilipoingia pale ofisini, kwani wenzangu walikuwa wakiniuliza maswali yale na kunipa pole huku wakinitazama kwa wasiwasi, na muda wote walikuwa kikundi, hakuna hata mtu mmoja aliyekuwa tayari kukaa na mimi peke yake.

Nikiwa nimezingirwa na wale wafanyakazi wenzangu pale kwenye korido, nilimuona Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho akitoka nje ya ofisini kwake, iliyokuwa kwenye ghorofa ya kwanza, na kuchungulia pale chini nilipokuwa nimezongwa na walei wenzangu. Tulitazamana kwa muda, kisha alirudi ofisini kwake na kufunga mlango.

Hatimaye nilifanikiwa kujichomoa kutoka kwenye lile kundi la wafanyakazi wenzangu na kuingia ofisini kwa afisa utumishi.

“Heey! Tigga! Karibu mrembo… karibu…” Suleiman Kondo, afisa wetu wa utumishi alinikaribisha huku akiweka chini simu aliyokuwa akiongea nayo muda mfupi kabla ya ujio wangu, huku akiuinua mwili wake mkubwa na mzito na kusimama kwa heshima yangu.

Hili ni jambo ambalo halijawahi kutokea.

Hata siku moja Suleiman hajawahi kunikaribisha kwa kusimama, leo vipi hadi kusimama? Nilitembeza macho haraka mle ndani na kugundua kuwa ile simu aliyokuwa akiongea nayo ilikuwa ni ile niliyoijua kuwa huwa ina mawasiliano ya moja kwa moja na ofisi ya Mkurugenzi.

“Nimekuja kuripoti Suleiman… na kuleta taarifa za maafa yaliyotokea huko Manyoni.” Nilimwambia.

Ok… karibu na pole sana Tigga. Tumepatwa na msiba mkubwa… wenzetu wametutoka… what happened out there, Tigga?” Suleiman alisema kwa huzuni huku akinitazama usoni, na kunitupia swali lililonitaka nimweleze kilichotokea kule msituni.

Sikufanya haraka kumjibu bali akilini mwangu nilikuwa nikijaribu kuisoma hali ya mle ndani iwapo ilikuwa na maslahi nami au bado nilikuwa nakabiliwa na vikwazo kutoka kwa watu wangu. Niliketi kwenye kiti mbele ya meza yake na kwa mara nyingine Suleiman alitaka kujua kilichojiri kule Manyoni. Na badala ya kumjibu swali lake, nilimuuliza swali langu la msingi.

“Suleiman… hivi kuna barua yoyote iliyotoka hapa ofisini kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Manyoni wakati tukiwa kule?”

Suleiman alionekana kutoelewa maana ya swali lile, lakini niliona kuwa hakuwa akielewa lolote juu ya kuwepo kwa barua hiyo.

“Si kuna barua iliyotoka hapa ambayo mlipewa kwa ajili ya kuiwasilisha kwa Mkuu wa wilaya baada ya kufika huko?” Alinijibu kwa swali.

“Hiyo naijua… ninamaanisha iwapo kuna barua nyingine iliyotumwa kwa fax kutokea hapa ofisini kwenda kule kwa mkuu wa wilaya wakati sisi tuko kule.” Nilimfafaniulia huku nikimtazama kwa makini.

“Hakuna. Ni wapi umepata mawazo hayo, na ni nani aliyeandika barua hiyo?” Alinijibu kwa uhakika kabisa na kunihoji zaidi.

“Nimeiona hiyo barua kwa mkuu wa wilaya na imesainiwa na Mkurugenzi mwenyewe… nimeiona saini yake kabisa!” Nilimjibu kwa uhakika.

“Hakuna, haiwezekani. Barua zote za Mkurugenzi huwa nazitayarisha mimi, sekretari wake anazitaipu kwa kompyuta, na yeye anasaini tu… huo ndio utaratibu, na hakuna barua yoyote iliyotoka hapa kwenda Manyoni baada ya nyie kuondoka.” Suleiman alinijibu, nami nilimuelewa, kwani huo ndio utaratibu uliokuwepo pale ofisini.

Kwa hiyo ile barua ya akina Martin Lundi ilikuwa imeghushiwa.

“Hebu nieleze ni nini hasa kilichotokea huko Manyoni Tigga? Kwa sababu hapa wamekuja wana usalama wakikusaka kuhusiana na mauaji ya wenzetu kule msituni, na kuna tuhuma nyingine za ajabu sana za wewe kufanya fujo ofisini ya mkuu wa wilaya… infact, wamesema kabisa kuwa wewe ni fugitive from justice, sasa hiyo ni hali mbaya sana Tigga… na inatuweka sisi kama waajiri wako kwenye wakati mgumu sana.” Jamaa aliniuliza na kunieleza kwa kirefu.

Nilimtazama Suleiman kwa muda nisijue la kumueleza, kwani yale maneno yake yalinitisha sana, ingawa taarifa yake haikuwa ngeni kabisa akilini mwangu.

Fugitive from Justice.

Nililitafakari lile neno na mwili ukanisisimka.

Mkimbizi kutoka kwenye mikono ya sheria.

“Naona ni bora nikitoa maelezo ya safari yetu na mambo yaliyotokea kwa Mkurugenzi, Suleiman… nadhani na wewe utahitajika uwepo.” Nilimwambia huku nikiinuka.

Alionekana kusita kidogo, kisha akaafikiana nami, lakini kwa mashaka. Sikuelewa ni kwa nini alisita, ila niliona kuwa sikuhitajika kutumia muda mwingi sana pale ofisini. Niliazimia kuwa baada ya kutoa maelezo yangu kwa Mkurugenzi, nichukue likizo ili nipate muda wa kuzidi kutafuta namna ya kukabiliana na mtihani huu ulionikabili, na kujaribu kutafuta ukweli wa matukio yale ya ajabu.

Tulipoingia ofisini kwa Mkurugenzi tu nilihisi kuwa nilikuwa nimeingia kwenye matatizo, kwani moja kwa moja niliona kuwa yule mzee wa makamu ambaye tulizoea kumwita ‘mkuu’ tukimaanisha mkuu wa idara, alikuwa ameshadhamiria kunituhumu, bila shaka akiwa na taarifa za mambo niliyofanya kule Manyoni, na zile taarifa potofu zilizotoka kwenye gazeti siku chache zilizopita. Baada ya kumuamkia aliniuliza iwapo ndio siku ile nilikuwa nimeingia kutoka Manyoni, nikamjibu kuwa niliingia jijini jioni ya siku moja iliyopita. Yule mzee ambaye huwa tunamuogopa sana kutokana na mtindo wake wa uongozi ambao ni wa ukali na amri, alimwita katibu muhtasi wake na kuniambia nitoe maelezo ya safari yangu na mambo yote yaliyotokea huko Manyoni, wakati yule katibu muhtasi wake akinukuu maelezo yangu kwenye kompyuta.

Nilieleza mkasa wote wa safari yetu na mambo yote yaliyotokea kule Manyoni tangu pale nilipoishuhudia ile helikopta ikitua kule msituni, jinsi akina Ibrahim Geresha walivyowekwa chini ya ulinzi na wale watu wabaya ambao mmoja wao hivi sasa nilimjua kwa jina la Martin Lundi. Wote walikuwa kimya kabisa wakisikiliza maelezo yangu, nami nilikuwa makini sana kwa kutoeleza mambo niliyoongea na yule mtu asiye na jina kule msituni wakati wale wauaji walipoondoka na wenzangu.

Nikawaelezea jinsi nilivyorudi kule kambini kwetu na kuwakuta wenzangu wakiwa wameuawa na kudonolewa na ile midege mibaya. Hapa nilishindwa kujizuia, na machozi yalinitoka upya, na mara kadhaa nililazimika kushindwa kuendelea na maelezo yangu nikielemewa na kwikwi, na niliona hata yule katibu muhtasi wa kamishna naye alikuwa akitiririkwa na machozi.

Nilielezea jinsi nilivyolikuta begi langu nje ya hema na jinsi nilivyoweza kufika hadi ofisini kwa mkuu wa wilaya, na mambo yaliyotokea huko.

Hapa niliona kuwa Kamishna alizidisha umakini, na nikaelezea juu ya ile barua iliyotumwa kwa fax kwa mkuu wa wilaya ikisemekana kuwa imetokea pale ofisini.

“Hakuna barua ya aina hiyo msichana! Huo ni uzushi sasa!” Hapo Kamishna aliingilia kati kwa ukali. Nilimtazama kwa kutoelewa.

“Uzushi kivipi mkuu…? Kwamba hiyo barua haikuwepo, au unadhani kuwa mimi ninazusha juu ya kuwepo kwa barua hiyo?” Nilimuuliza kwa mashaka.

“Uzushi! Hakukuwa na barua ya aina hiyo iliyotoka hapa ofisini kwenda huko kwa mkuu wa wilaya… labda wewe unataka kutuchanganya tu kwa kuleta hadithi za barua za ajabu ajabu…”

“Aaah! Mkuu! Ni wewe ndiye uliyesaini ile barua, na sehemu ya maelezo yangu yaliyotolewa kwenye ile barua yalikuwa ni yale yanayoweza kupatikana kwenye faili langu la ajira hapa ofisini!” Nilimjibu kwa jazba, kisha nikaendelea kuwaeleza jinsi nilivyokana maelezo ya ile barua kule kwa mkuu wa wilaya.

“Hakukuwa na barua ya aina hiyo!” Kamishna alizidi kusisitiza, kisha akaendelea, “Unaweza kutuonesha hiyo barua?”

Nilimjibu kuwa niliiacha palepale kwa mkuu wa wilaya, na nikamwambia kuwa nina imani itakuwepo kwa mkuu wa wilaya iwapo wataamua kuifuatilia, kwani kule walikuwa wameamini kabisa kuwa ilikuwa imetokea pale ofisini.

Mkuu alinitazama kwa muda huku nikiona wazi kuwa alikuwa haniamini. Kisha bila ya kusema neno aliniashiria niendelee na maelezo yangu.

Nilieleza kisa chote hadi kufikia pale nilipoingia ofisini asubuhi ile.

Baada ya hapo ofisi yote ilibaki kimya. Kamishna alinitazama kwa muda mrefu wakati yule binti aliyekuwa akinukuu maelezo yangu akitoa nakala ya yale maelezo na kumkabidhi. Aliyatazama kwa muda kisha akanipa na kuniambia niyapitie iwapo yalikuwa ni sawa na vile nilivyoeleza. Nilisoma maelezo yale yaliyofikia kurasa saba, na kutoa marekebisho machache ambayo yule dada aliyarekebisha kwenye kompyuta yake na kutoa nakala nyingine ambayo ilikuwa sawa.

Kwa makusudi kabisa nilikuwa nimeacha kuelezea juu kuwepo kwa mkanda wa video uliokuwa una ushahidi wa yale mauaji ya kule msituni.

Niliweka saini yangu chini ya maelezo yale. Kisha Suleiman Kondo naye alisaini kama shahidi aliyekuwepo wakati nikitoa maelezo yale, na Kamishna naye akafanya hivyo hivyo. Yule dada aliambiwa arudi ofisini kwake na kuendelea na kazi zake.

Kilichofuatia ni mahojiano marefu baina yangu na Kamishna ambayo kwa ufupi yalikuwa yanahitaji kuelewa mtazamo wangu juu ya suala lile. Kwa nini yale mauaji yatokee, kwa nini wale wauaji waghushi ile barua iliyokuwa ikinitangazia mimi ule ugonjwa wa akili, na kwa nini mkuu wa wilaya alionekana kuwaamini zaidi wale madaktari badala yangu.

Sikuwa na majibu ya kuwatosheleza juu ya mengi ya maswali yao, kwani mimi mwenyewe nilikuwa natafuta majibu kwa maswali hayo hayo, ila jibu kubwa nililowapa lilikuwa ni juu ya sababu nilizodhani kuwa ziliwafanya wanipakazie ule ugonjwa wa uongo. Niliwaambia kuwa walifanya kusudi kunipakazia ugonjwa ule  ili taarifa nitakazotoa dhidi yao kuhusu mambo niliyoona wakiyafanya kule msituni zitiliwe mashaka na kila mtu.

Swali kubwa kabisa aliloniuliza mkuu wangu wa kazi ni kwa nini muda wote tangu mambo yale yalipojitokeza sikuenda kuripoti polisi. Hili kwake lilikuwa ni jambo la muhimu sana, na alishindwa kuelewa kuwa kama sikuwa na matatizo, kwa nini nilishindwa kwenda polisi.

“Mkuu wale watu tayari walishaonesha kuwa wana namna ya kuingiliana na vyombo vya dola kwa maslahi yao! Nilishindwa kwenda polisi kienyeji tu bila ya kuwa na uhakika wa hali nitakayoikuta huko…” Nilijaribu kumwelewesha lakini niliona kuwa suala lile lilikuwa gumu kueleweka.

Sikuweza kuwaeleza kuwa nilishindwa kwenda polisi kwa sababu nilikuwa nahofia usalama wa ule mkanda wa video wenye ushahidi, kuwa huenda ungeangukia mikononi mwa askari mwenye uhusiano na wale wauaji. Kwa usalama wangu, sikuwaeleza kabisa juu ya kuwepo kwa huo mkanda tangu mwanzo, sasa wangeelewa vipi? Ilikuwa ni hali ngumu.

“Tigga, samahani sana binti, lakini lazima nikueleze kuwa hii taarifa yako ni ngumu sana kuiamini… mimi binafsi naiona kama masimulizi ya filamu ya kubuni tu.” Hatimaye Mkurugenzi aliniambia, huku Suleiman Kondo naye akitikisa kichwa kuafikiana naye.

“Sasa nifanyeje wakuu wangu? Maana mi’ nimekuja kwenu kutafuta msaada…” Nilisema huku nikiwatazama kwa zamu, na badala ya kunijibu, Mkurugenzi aliinuka na kuingia chooni, ambacho kilikuwa kimejengwa humo humo ndani ya ofisi yake.

Kama Masterbedroom ya Kelvin…

Tulibaki na Suleiman Kondo mle ofisini. Niliajaribu kumdadisi juu ya hatua iliyopaswa kufuatwa kwa mujibu wa kanuni za ajira, lakini Suleiman alionekana kuwa na mashaka sana na kuongea lolote na mimi tukiwa peke yetu. Nilianza kujiuliza kwa nini, lakini mara nilipata jibu lililotembeza ganzi moyoni.

Mkurugenzi alitoka kule chooni na kuingia tena pale ofisini akiwa amefuatiwa na afisa wa jeshi la polisi!

“Ni wajibu wangu kukukabidhi kwenye mikono ya sheria Tigga, sehemu pekee ambayo suala lako linaweza kushughulikiwa ipasavyo.” Mkurugenzi aliniambia huku akimtanguliza yule afisa wa polisi.

Mate yalinikauka na nikapigwa na butwaa. Nilimtazama kwa mshangao, kisha nikamtazama yule askari na kumgeukia Suleiman Kondo ambaye alinitazama kidogo na kuinamisha kichwa. Nilimtazama tena yule afisa wa jeshi la polisi. Alikuwa amevaa mavazi wanayovaa askari wa ngazi za juu kwenye jeshi la polisi. Alikuwa mrefu na nilimhisi kuwa alikuwa katika umri wa kati wa ujana.

Nikahamishia macho yangu kwa Mkurugenzi.

“Mkurugenzi…” Nilianza kuongea kwa sauti ya kukwaruza huku nikiinuka  kutoka  kitini na moyo ukinipiga vibaya sana. Hapo hapo  yule afisa wa polisi alipiga hatua kubwa na kuwahi kusimama mlangoni, akinizuia nisitoke mle ndani.

Nilikuwa nimenaswa, na hata wazo hilo liliponijia, akili yangu ilienda kwenye ule mkanda wa video uliokuwa kwenye begi lililokuwa begani kwangu.

“Sina la kukueleza Tigga, na naomba uelewe kuwa hapa natimiza wajibu wangu. Na kwa mujibu wa sheria za kazi, kuanzia muda utakaokuwa chini ya ulinzi, ajira yako itasimama mpaka hapo sheria itakapoamua vinginevyo. Suleiman atakupatia barua rasmi kukuarifu juu ya hilo na taratibu nyingine za kisheria.” Mkurugenzi aliniambia kwa upole lakini kwa mkazo usioyumba.

“Lakini… lakini… si mmepata maelezo yangu? Kwa nini tena nikamatwe…?”

“Tigga Mumba?” Yule askari aliongea kwa mara ya kwanza.

Nilimgeukia huku macho yakiwa yamenitoka pima na kumtazama kwa makini.

Hivi huyu ni askari wa kweli au ni miongoni mwa wale wanaomsaidia Martin Lundi muongo?

Alikuwa ana sura ya kuvutia hasa, na tofauti na askari wengi, yeye alikuwa amechonga ndevu zake vizuri katika ile staili ya Timberland ambayo mabrazameni wengi huwa wanaipenda.

Sasa askari gani ananyoa ndevu kwa staili ya timberland?

Nilimkumbuka yule askari wa kike aliyeacha kunikamata kule gesti usiku uliopita.

“Mkurugenzi! Hu… huyu si askari wa kweli! Anaweza kuwa miongoni mwao! Usimruhusu anichuku…”

“Kuanzia sasa nakuweka chini ya ulinzi kwa kosa la kutoroka mikono halali ya sheria ambayo ilikutaka uisaidie polisi kwenye suala la mauaji yaliyotokea Manyoni.” Yule afisa alinieleza kwa ukakamavu bila ya kujali pingamizi langu.

“Lini? Lini nilitoroka mikono ya sheria? Huo ni uongo! Uongo mkubwa…” Nilibwata huku nikihaha mle ndani ilhali yule askari akiwa amedhibiti njia yangu ya kutorokea.

“Pia nakuweka chini ya ulinzi kwa kosa la kufanya vurugu zilizomsababishia mkuu wa wilaya ya Manyoni maumivu makali wakati ukiwa katika harakati za kuikimbia mikono ya sheria huko Manyoni.” Aliendelea kunisomea makosa yangu yule afisa wa polisi ambaye kwa hakika nilimuona kuwa ni muongo tu kama wale wengine.

Miguu iliniisha nguvu. Nikajibweteka kitini.

Yule askari alininyanyua kwa nguvu kutoka pale kwenye kiti na kuniongoza nje ya ofisi akiwa amenishika mkono wangu kwa nguvu, juu kidogo ya kiwiko changu.

Oh! Mungu wangu, huu ndio mwisho wangu!

 

 

--

Aliniongoza kuziteremka ngazi kuelekea ghorofa ya chini ambako  kulikuwa kuna mlango wa kutokea nje ya jengo lile. Pale ngazini tulipishana na binti mmoja wa kampuni ya ufagizi iliyoitwa WE KLEEN OFFICE CLEANERS ambayo ilikuwa ina mkataba wa kufanya usafi na ufagizi katika ofisi yetu.

Nilijiona kama niliyekuwa ndotoni na sikuwa na ujanja. Mkono ulionikamata ulikuwa imara na wenye nguvu, na niliongozana na yule askari huku nikijaribu bila mafanikio kuilazimisha akili yangu inishauri juu ya namna ya kujikomboa kutoka kwenye mtego ule.

Wafanyakazi wenzangu walikuwa wakinichungulia kutoka kwenye milango ya vyumba vya ofisi zao kwa wasiwasi uliochanganyika na udaku.

Nilizungusha macho na kumtazama tena yule askari aliyenikamata.

Mimi ni mrefu kuliko wasichana wengi, lakini huyu bwana alikuwa mrefu zaidi kwani niliona kuwa kichwa changu kilikuwa kinaishia juu kidogo ya bega lake. Nilipata harufu ya marashi ghali ya kiume ikitokea kwenye mavazi yake ya kiaskari, na hapo nikaji hakikishia kabisa kwamba yule mtu hakuwa askari wa kweli, na hata kama alikuwa ni afisa wa kweli, basi alikuwa ni miongoni mwa wafuasi wa Martin Lundi, na si vinginevyo.

Nifanye nini, Mungu wangu?

Tulipofika mwisho wa zile ngazi tulikata kushoto ambapo aliniongoza kufuata kijikorido kidogo kilichoelekea kwenye mlango mdogo wa dharura ambao ulitokea moja kwa moja kwenye sehemu ya kuegeshea magari ndani ya uzio wa jumba la makumbusho.

Mbele yetu, upande wa pili wa ile korido mfanyakazi mwingine wa ile kampuni ya kufanya usafi pale ofisini alikuwa ameinama akipiga deki. Kwa pale tulipokuwa, niliweza kuona tu yale maandishi makubwa kwenye mgongo wa fulana yake yaliyokuwa yakiitambulisha ile kampuni ya usafi na ufagizi.

Na hata pale tulipochukua uelekeo wa ule mlango mdogo wa dharura, naye aliinuka akiwa amebeba ndoo yake ya maji pamoja na mifagio  maalum ya kupigia deki, akasogea mbele zaidi ya ile korido na kuanza kuipiga deki ile korido kutokea kule kwenye ule mlango kutufuta.

Tulizidi kuelekea kule mlangoni huku yule afisa akianza kuchomoa pingu kutoka kwenye mfuko wa suruali, nami nikaingiwa na woga maradufu. Sijawahi kufungwa pingu hata siku moja maishani mwangu, na sio siri, pingu bora uisikie tu watu wakiitaja, lakini kuiona kwa macho inatisha si mchezo. Nilianza kutetemeka huku miguu nikiihisi mizito kuliko kawaida.

“Tembea vizuri mwanamke…!” Yule afisa alinikemea huku akinivuta mkono wangu kwa mkono wake mmoja hali ule mwingine ukiweka pingu yake sawa. Na hapo hapo wote tulishitushwa na kishindo kikubwa. Yule mfagizi alikuwa akiinua ndoo yake ili kutupisha, lakini ghafla ile ndoo ilimponyoka na kuanguka sakafuni kwa kelele kubwa huku ikimwaga na kurusha maji kila upande, akilowanisha miguu ya suruali yangu na ya yule askari.

Niliruka kwa mshituko huku nikitoa sauti ya woga hali yule afisa wa polisi akiropoka neno la kulaani kitendo kile naye akiruka pembeni. Bila kuniachia aliinamisha uso  kutazama jinsi suruali yake ilivyotota maji, kisha akauinua kwa hasira iliyomuelekea yule mfagizi.

Sote wawili tuliachia midomo wazi kwa butwaa.

Macho ya Nyoka alikuwa ametupa ile mifagio yake na sasa alikuwa ametuelekezea bastola kubwa iliyotisha huku akiwa amekenua meno kwa ghadhabu. Yule afisa wa polisi alinigeukia kwa hasira na mshangao. Akaona jinsi nami nilivyohamanika, nami nikaona ule mshangao ukimyeyuka na hasira ikimtawala, kisha akamgeukia tena yule mtu mwenye bastola mbele yetu.

Nilichoka!

Yaani kumbe muda wote ule nilikuwa nikimtazama Macho ya Nyoka na sikumjua. Nilipeleka macho kwenye ile fulana nyeupe aliyovaa, ikiwa na maandishi WE KLEEN OFFICE CLEANERS kifuani, na suruali ya jinzi nyeusi ambayo ndio sare wanazovaa wale wafanyakazi wa ile kampuni ya usafi na ufagizi.

Eeh! Hawa watu ni kiboko!

“Wewe ni nani… na unataka nini…? Mimi ni afisa wa ngazi ya juu wa polisi, na nakuamuru uweke chini hiyo silaha yako upe…” Yule afisa wa polisi alianza kumwambia yule muuaji huku akiwa ameinua mikono yake usawa wa mabega yake kuonesha kuwa hakuwa na silaha, akiachia ile pingu yake ianguke sakafuni.

.

“Kimya!” Macho ya Nyoka alimkatisha kijeuri, na nikaona yule afisa akifinyamacho kwa umakini.

“Sitojali iwapo ni afisa wa ngazi ya mbinguni au ya ardhini! Usipotii maelekezo yangu nakuua sasa hivi!” Macho ya Nyoka alimfokea, na niliona  kuwa alikuwa hatanii. Sikuwa na shaka kabisa kuwa mimi ndiye niliyekuwa nikitakiwa pale, na si yule askari. Bila kujijua nilijikuta nikijificha mgongoni kwa yule afisa wa jeshi la polisi huku nikijiuliza kuwa iwapo naye alikuwa ni mfuasi wa Martin Lundi, vipi tena Macho ya Nyoka amtishie bastola? Nilipata wazo kuwa muda wote Macho ya Nyoka alikuwa akinisubiri pale ofisini akijifanya naye ni mfagizi akijua kuwa kuna siku ningetokea. Bahati leo nimetokea na kukutwa na huyu askari, kwani sasa ilinijia wazi kuwa yule mtu alikuwa ni askari wa kweli.

Ok… haina haja ya kugombana. Unataka nini…?” Yule askari alimuuliza Macho ya Nyoka kwa tahadhari kubwa huku akimtazama usoni.

“Namtaka huyo mwanamke, na sitaki uniingilie, kwani sitasita kukuua!” Macho ya Nyoka alifoka.

“Hapana! Usimkubalie! Ni muuaji huyo…” Niliropoka kwa woga huku nikimng’ang’ania mgongoni yule askari.

“Kelele malaya wee…Kuja hapa! Upesi!” Macho ya Nyoka alinikemea huku akiniashiria nimfuate kwa ile bastola yake.

“Sijui unamtakia nini huyu binti, lakini najua kuwa unafanya kosa kubwa sana. Huyu binti yuko chini ya ulinzi, na we’ unataka kumtorosha… mna uhusiano gani?” Yule afisa alimuuliza kwa utulivu huku nikiuhisi mwili wake ukikakamaa.

“Sina uhusiano naye wowote! Huyo ni muuaji… namjua sana! Ndiye aliyeua… anataka kuniua!” Niliropoka kwa jazba kumwambia yule askari huku nikimtazama Macho ya Nyoka kwa hofu kubwa. Nilijaribu kugeuka  nyuma yetu kuona iwapo akina Suleiman waliweza kutuona, lakini tulikuwa tumeshapinda kona na hivyo watu wote waliokuwa ule upande wa vyumba vya ofisi hawakuweza kutuona.

Tulikuwa tumenasa wenyewe kwenye kona ya muuaji.

“Afande kaa chini! Msichana njoo kwangu… haraka!” Macho ya Nyoka aliamrisha huku akiukaza ule mkono uliokuwa umetuelekezea bastola hali macho yake ya kuogofya yakitoa mng’ao wa chuki kubwa.

Sikuwa na shaka kabisa kuwa tukizidi kubisha tu ataua mtu.

Huyu ni muuaji wa kuzaliwa hasa…

Na nilipokuwa nikimtazama, nilipata hisia isiyo shaka kabisa kuwa alikuwa anatafuta sababu tu ya kuua mtu pale.

“Mimi chini sikai, utafanyaje?” Yule askari alimuuliza kwa sauti ya upole sana, kana kwamba alikuwa anaongea jambo la kawaida kwa mtu asiye hatari, nami nikazidiwa na woga.

“Hah! Atakuua huyo afande! Atatuua sote…” Niliropoka kwa woga, na hapo nilishitukia kitu kama upepo tu kikipita kwa kasi mbele ya macho yangu, na bastola ya Macho ya Nyoka ikisambaratika sakafuni kwa kelele, kwani yule afisa alirusha teke lililoipangusa kama mzaha ile bastola kutoka mkononi mwake.

Mimi na Macho ya Nyoka tulizubaa kwa kama sekunde hivi wakati akili zikijaribu kuelewa kilichotokea, kisha Macho ya Nyoka alikurupuka ghafla huku akinguruma kwa ghadhabu kuirukia bastola yake iliyotupwa sakafuni, na hapo hapo yule afisa wa polisi alimrukia na kumshindilia soli ya kiatu chake kifuani. Macho ya Nyoka alitupwa na kujibabatiza ukutani wakati yule askari  akajitupa pembeni kuiwahi ile bastola ya yule muuaji.

Macho ya Nyoka alijiinua haraka na kujirusha miguuni kwa yule afande kabla hajaifikia ile bastola, na wote wawili wakapiga mweleka mzito pale sakafuni. Sasa na mimi ndipo nilipozinduka na kuanza kupiga kelele, nikiwa nimejibanza kwenye kona ya ile korido huku macho yakiwa yamenitoka pima nikishuhudia wale wanaume wakigaragazana sakafuni, kila mmoja akijaribu kumzuia mwenzake asiiwahi ile bastola. Kwa pale nilipokuwa niliona kuwa Macho ya Nyoka alikuwa amemlalia juu yule askari huku akinyoosha mkono wake kuiwahi ile bastola, wakati yule askari akiuvuta mkono wa Macho ya Nyoka usiifikie ile bastola huku wakati huohuo akijaribu kutoa bastola yake iliyokuwa kiunoni mwake kwa mkono wake mwingine, lakini mguu wa Macho ya Nyoka ulikuwa umeubana ule mkono hivyo akawa hawezi kufanikisha lengo lake.

Na hapo ikanijia kumbukumbu ya lile tukio la kule msituni baina ya Macho ya Nyoka na yule mtu asiye na jina. Tukio lililoishia kwa yule mtu kupoteza maisha yake. Kumbukumbu ile iliniletea woga mkubwa na nikahofia kushuhudia tena tukio kama lile.

Kwa nini kifo kinifuate kila mahali?

Nilikurupuka kutoka kwenye kona ya ile korido nilipokuwa nimejibanza na kujaribu kuwaruka wale jamaa ili niiwahi ile bastola, na wakati huohuo yule muuaji alijiinua akijaribu kuinuka na miguu yangu ikampamia kwenye ubavu wake nami nikapiga mweleka mkubwa huku nikiachia yowe la woga.

Nilijiinua kwa kupepesuka na kuegemea ukuta huku macho yakinitembea.

Macho ya Nyoka alikuwa ameshainuka akiwa ameikamata tena ile bastola yake na sasa ilikuwa ikimwelekea usoni yule askari ambaye alibaki akiwa amepiga goti pale sakafuni huku akitweta, akimtazama kwa hasira. Niliona kuwa alikuwa hana ujanja. Macho ya Nyoka hakutaka kuongea zaidi. Na niliona kuwa alikuwa ameghadhibika kupita kawaida. Akili yake ilikuwa imemwelekea yule askari na kwa muda ule alikuwa hana habari na mimi. Alifyatua kitunza usalama cha ile bastola huku uso wake ukimbadilika.

Alikuwa ameazimia kuua!

Niliinyakua ile ndoo ya bati aliyokuwa akipigia deki na kumpiga nayo kichwani kwa nguvu zangu zote huku nikitoa ukelele wa hasira iliyochanganyika na woga.

Macho ya Nyoka alitoa mguno hafifu na miguu ikamlegea huku bastola ikimtoka mkononi, damu ikimchuruzika kutoka upande wa kichwa chake pale pigo langu lilipotua.

Haraka sana yule afisa wa polisi aliruka na kumshindilia ngumi ya taya iliyompeleka chini mzimamzima, na wakati huohuo kelele za wafanyakazi wenzangu pale ofisini zilinijia huku wengine wakianza kuja eneo lile mbio wakiwa wamejaa udadisi mkubwa.

Nilibaki nikitazama kwa woga wakati yule afisa wa polisi akimnyanyua Macho ya Nyoka aliyepumbazwa na mapigo yale na kumbandika ile pingu iliyokuwa inifunge mimi kwenye mkono wake mmoja.

Akamgeuza kwa nguvu kimgongomgongo ili amfuge na ule mkono wa pili kwa nyuma, na hilo lilikuwa kosa.

Macho ya Nyoka aligeuka na pigo zito ambalo mpaka sasa siwezi kuelewa kama lilikuwa ni ngumi, teke au kiwiko cha mkono. Nilichoona ni yule afisa wa polisi akijipinda na kupepesuka huku akitoa yowe la maumivu.. Hapo hapo Macho ya Nyoka aliruka na kumtandika teke la kichwa lililomsukumiza ukutani kwa kishindo yule askari.

Nilipiga kelele na hapo hapo wale wafanyakazi wenzangu pamoja na wale wafanyakazi wengine wa ile kampuni ya usafi walitimua mbio kurudi walipotoka, kila mmoja akipiga kelele kivyake.

Macho ya Nyoka aliruka hatua mbili za nyumanyuma na kunigeukia kwa ghadhabu huku akininyooshea kidole kwa hasira bila ya kusema neno, na katika macho yale, niliona ahadi isiyotamkwa ya kifo cha mateso makubwa kutoka kwake,kisha aligeuka na kutimua mbio kutoka nje ya jengo lile kutumia ule mlango wa dharura tuliokuwa tukiuelekea hapo awali.

 “Don’t Move!” Yule afisa wa polisi alinifokea huku akininyooshea kidole na akiikwapua ile bastola ya Macho ya Nyoka na kutoka mbio kumfuata yule muuaji, akimpigia kelele asimame.

Sikuzubaa.

Nililiweka sawa begi langu mgongoni na kutimua mbio kuelekea upande wa lango kuu la kuingilia na kutokea ndani ya jengo lile, nikipuuzia kabisa ile amri ya yule afisa wa polisi. Mazingira yalikuwa hayaeleweki, nami sikuwa tayari kuhatarisha usalama wangu zaidi katika mazingira kama yale.

Suleiman Kondo alinipigia kelele nisikimbie lakini sikumjali. Niliendelea kutimua mbio.

“Mkamateni huyooo!” Nilimsikia akipiga kelele na nikaona wafanyakazi wenzangu pamoja na baadhi ya wale wafanyakazi wa ile kampuni ya usafi ambayo Macho ya Nyoka alifanikiwa kujipenyeza ili aweze kunivizia pale ofisini wakitanda mbele yangu na kunizibia njia.

“Tigga don’t run! Hii ni kwa usalama wako!” Suleiman Kondo alinipigia kelele huku akihangaika kunikimbilia kwa taabu kutokana na mwili wake mzito, akinisihi kwa kimombo, kuwa nisikimbie.

Nilipagawa.

Niligeuka na kutaka kurudi kule nilipotokea, nikaona baadhi ya wafanyakazi wakiwa wamefanya ukuta. Nilichanganyikiwa, jasho likinivuja na moyo ukinienda kasi kuliko ilivyowahi kutokea. Nilikuwa kama chui aliyezingirwa na wawindaji wenye ghadhabu. Nilimgeukia Suleiman Kondo, nikaona alikuwa ameungana na Mkurugenzi wakinikodolea macho.

“Tigga! Usifanye tena kosa hilo… uko chini ya ulinzi! Utazidi kujiwekea mazingira mazito!” Suleiman alinipigia kelele. Na hata pale Suleiman alipomalizia kauli yake nilisikia mlipuko mkubwa wa bastola kutokea kule  ambako yule afisa wa jeshi la polisi alikuwa akikimbizana na Macho ya Nyoka. Vilio vya woga vilitawala mle ndani kutoka kwa wafanyakazi wenzangu.

Sikutaka kusubiri kujua ni nani aliyepigwa risasi kati ya yule askari na yule muuaji niliyempachika jina la Macho ya Nyoka. Nilikwapua mtungi mkubwa wa maua uliokuwa pale kwenye korido kama sehemu ya mapambo ya ofisi, na kwa nguvu zangu zote niliutupia kwenye dirisha kubwa la kioo lililokuwa karibu yangu na kulipasua vibaya, likiacha uwazi mpana sehemu iliyokuwa na kioo.

Kelele zilitawala mle ndani nami nikajitupa nje ya dirisha lile na kuangukia nje ya jengo ambako nilijiinua haraka na kutoka mbio. Nilijipenyeza kwenye uzio wa nyuma ya jengo lile uliofanywa kwa aina ya miti kama michongoma na kutokea kwenye eneo la wazi lililokuwa limetapakaa majani yaliyokuwa yakitunzwa vizuri.

Nilizidi kutimua mbio huku akili ikinizunguka bila ya kujua ni kwa nini niliamua kufanya vile na nini ingekuwa matokeo yake, lakini sikujali.

Nilichojali kwa wakati ule ni kujiweka mbali na eneo lile ambalo lilishaingia walakini kuhusiana na usalama wangu. Nilikimbia na kujipenyeza kwenye uzio mwingine wa miti na kutokea kwenye mtaa mmoja mfupi  uliokuwa kimya sana. Nilihaha kwa muda, nikitazama  kulia na kushoto, kisha nikachomoka kasi kuelekea kushoto kwangu na kukutana na barabara nyingine ya lami, ambayo baada ya kuifuata nikakutana na njia panda.

Nilitimua mabio kuelekea kulia huku magari yakinipigia honi na nikisikia misuguano ya matairi lamini wakati yakifunga breki kwa ghafla. Sikugeuka nyuma wala sikupunguza mwendo. Nilikuwa natoka kasi kweli kweli. Niliibukia kwenye  eneo nililolifahamu ambapo nililiona jengo la International House likiwa kulia kwangu. Nikakunja kushoto kwenye makutano ya ile barabara niliyotoka nayo na ile ya kuelekea kwenye lile jengo la International House na hoteli ya Holiday Inn.

Nikaanza kutembea kwa mwendo wa haraka huku nikikimbia kidogo kidogo, nikichukua uelekeo wa jengo la PPF Tower. Jasho lilikuwa likinitirika vibaya sana na sidhani kama nina haja ya kukwambia jinsi moyo ulivyokuwa ukinipiga. Miguu ilikuwa ikinitetemeka na nikahisi maumivu kwenye sehemu ya juu ya mkono wangu wa kulia. Nilipojitazama nikaona kuwa nilikuwa nimejichanja na kipande cha kioo pale niliporuka dirishani. Kioo kilichana mkono wa lile koti langu gumu la jinzi  na kunichana, japo kwa kiasi kikubwa kabisa lile koti lilipunguza makali ya kile kioo na hivyo kupunguza ukubwa wa lile jeraha lililokuwa likichuruzika damu kidogo, lakini hilo nililiona kuwa ni suala dogo sana.

Nilikaza mwendo huku kitembeza macho kila upande, nikitaraji kusikia mtu akinipigia ukelele kuwa nisimame au akiwapigia kelele wapitanjia wengine kuwa wanikamate. Niliongeza kasi kuelekea barabara kubwa ya Azikiwe. Hatua kadhaa mbele yangu niliona daladala kubwa aina ya Isuzu Journey likisimama kwenye makutano ya ile barabara niliyokuwapo na ile ya Azikiwe kuelekea Posta ya zamani, na kondakta akinipigia kelele akiniuliza iwapo nilikuwa ni msafiri. Kwa rangi ya mstari wa lile basi, niliona kuwa lilikuwa ni lenye kufanya safari za Mwananyamala-Posta. Kwa wakati ule, basi lolote lingekuwa mwafaka kwangu, hivyo sikufikiri zaidi. Nilimpungia mkono anisubiri huku nikiongeza mbio.

Nililiparamia lile basi kwa pupa nalo likaondoka kwa kasi eneo lile kuelekea maeneo ya Posta ya zamani, huku yule kondakta akishangilia na kurukaruka mlangoni, nami nikijibwaga kwenye kiti nikitweta huku nikijifuta jasho kwa mkono wa koti langu.

Tulipofika eneo la Posta ya zamani nilipatwa na kihoro baada ya kuona tukisimamishwa na askari wa usalama barabarani. Niliangaza huku na huko. Nikaona magari yote yaliyokuwa pale barabarani yalikuwa yamesimama, yakifanya foleni kubwa. Nilichanganyikiwa vibaya sana. Niliinuka na kutaka kuteremka, lakini konda alinizuia, akiniuliza iwapo nilikuwa nataka kuwalipisha faini kwa kuteremsha abiria sehemu isiyo kituo, tena mbele ya wanausalama ambao mwenyewe aliwaita “yangeyange”.

Niliketi kwenye kiti huku akili ikinizunguka. Ina maana huu ni msako kwa ajili yangu, au…?

Nilitoa kichwa nje ya dirisha na kutazama kule mbele tulipokuwa tukielekea. Mwili ulinifa ganzi niliposhuhudia askari wa jeshi la polisi zaidi ya sita waliobeba bunduki aina ya SMG wakiwa wametanda mbele ya barabara, baina yao wakiwamo askari wa usalama barabarani.

Nimekwisha!

Nilimgeukia konda.

“Ni… ni kitu gani? Kuna nini mbona tumesimamishwa?”  Nilimuuliza kwa sauti ambayo nilishindwa kuamini kuwa ni yangu.

Konda alinitazama kwa muda kabla ya kuniuliza.

“Anti vipi…? Una haraka sana nini?”

Nilimtazama kidogo kisha nikapeleka uso wangu pembeni, asije akanishika sura halafu akaja kuniletea matatizo hapo baadaye.

“Hao ni wenye nchi wanapita dada’aangu, eeeh!” Yule konda aliniambia baada ya kuona kuwa sikumjibu hapo awali, kisha akaongezea. “Hii ndio Bongo dada’angu, Ooo! Namna hii mtu hata umpe nini hakubali kuachia madaraka. We’ watu wote tunasimamishwa ili mkuu apite bwana! Hata ingekuwa mimi siachii ngazi mwanangu!” Abiria waliangua kicheko nami nikabaki nimeduwaa huku nikihisi moyo ukinipiga kwa nguvu. Kwa hakika nilikuwa nimeshikwa na woga mkubwa.

Kumbe ni msafara wa kiserikali tu!

Nilishusha pumzi za faraja kwani nilijua iwapo ule ungekuwa kweli ni msako kwa ajili yangu basi nisingekuwa na namna ya kujiokoa. Muda si mrefu ving’ora vilisikika na msafara mrefu wa magari ya kifahari ambayo hayakuwa na shaka kuwa ni ya serikali ulipita, nasi tukaruhusiwa kuendelea na safari yetu muda mfupi baadaye. Nilitahamaki kuona lile basi likikunja kuelekea maeneo ya Feri badala ya kule Posta ya zamani kama nilivyotarajia. Kumbe lilikuwa ni basi la Mwananyamala-Kivukoni. Hii ilikuwa ni mbaya kwangu, kwani nilitaka nipotee lile eneo la mjini haraka iwezekanavyo. Sasa hii ya kuelekea Kivukoni tena si ndio ninazidi kujizamisha ndani ya mji kabisa? Nilitaka kumpigia kelele konda aniteremshe, lakini nikachelea kuonekana kituko bila sababu.

Niliamua kutulia kufuata safari ya lile basi.

Potelea mbali!

Nilipofika Kivukoni niliteremka baada ya kuona lile basi lilikuwa linaendelea kusubiri abiria wajae ndio lianze safari yake ya kuelekea Mwananyamala. Niliamua kutafuta basi lolote litakalonitoa kule katikati ya mji na kunirudisha uswahilini ambako ningeweza kupotea kirahisi, ingawa sikuwa na wazo la wapi nielekee hasa. Nilianza kuangaza huku na huko pale kituoni nikitafuta basi lolote ambalo lilikuwa liko tayari kuondoka eneo lile lakini hapo nilipatwa na mshituko mkubwa nilipoona umma wa watu ukinijia mbio kana kwamba walikuwa wanakimbiza mwizi.

Moyo ulinilipuka na woga ukanitawala.

Ni nini tena? Wamenijuaje?

Nilianza kukimbia kidogo kidogo huku akili ikinizunguka kwa woga na mwili ukiniingia baridi.

Lakini mbona wananikimbiza kimyakimya? Au…?

Na hata pale nilipokuwa nikijitahidi kukimbia kwa wasiwasi na woga mkubwa, nilishuhudia wale watu wakinipita bila hata kunijali na badala yake wakiendelea kutimua mbio kuelekea mbele.

What is happening…?

Niliendelea kukimbia miongoni mwao huku nikiangaza huku na huko, nikijaribu kuwatazama wakimbiaji wenzangu kwa mshangao nisijue kinachoendelea, halafu nikaelewa.

Wanakimbilia pantoni!

Kama mwehu nami nikakaza msuli na kutimua mbio kwa nguvu zangu zote kulikimbilia lile pantoni. Nililiwahi nikiwa miongoni mwa watu wa mwisho kabisa, na muda si mrefu lile pantoni likauacha ukingo wa bahari na kuanza safari ya kuelekea Kigamboni. Nilijiegesha kwenye kona moja mle ndani na kujikunyata nikilitazama jiji la Dar es Salaam likirudi nyuma taratibu wakati lile pantoni likikata maji kuelekea upande wa pili wa bahari ya Hindi.

Mwili wote ulikuwa ukiniuma na miguu ilikuwa ikinipwita kuliko kawaida. Nilitoa kitambaa changu cha kichwa na kujifunga kichwani, nikizificha kabisa zile nywele zangu za rasta.

Niliteremka upande wa pili wa bahari na kujiunga na msururu mrefu wa wasafiri wenzangu kuelekea katikati ya kitongoji kile cha Kigamboni. Sikuweza kabisa kuiruhusu akili yangu iyatafakari matukio ya asubuhi ile, kwani nilihisi kuwa ningeweza kulipuka wazimu ghafla.

Nilipitia kwenye maduka ya pale karibu na kipando cha pantoni na kununua nguo za kubadili, kwani zile nguo zangu zilikuwa zimeanza kutoa harufu ya jasho, na pia nilijua kuwa kufikia muda ule nguo nilizovaa zilikuwa zimeshajulikana, hivyo polisi wangekuwa wanamsaka mwanamke aliyevaa suruali na koti la jinzi, kijitopu chekundu kwa ndani, hali akiwa amesuka nywele katika mtindo wa rasta.

Kwa kuwa bado nilikuwa nina pesa za kutosha, nilinunua nguo kadhaa za kubadili na kuongeza begi lingine dogo ambamo niliweka zile nguo zangu mpya. Niliingia duka la dawa na kununua dawa ya kidonda, bandeji, mswaki na dawa ya meno.

Kisha nikakodi teksi na kumwambia dereva anipeleke kwenye nyumba nzuri ya wageni iliyotulia. Alinipeleka kwenye nyumba moja ya wageni ambayo niliafikiana naye kuwa ilikuwa imetulia.

Nikijiandikisha kwa jina la Nuru bint Shaweji, nilikodi chumba cha self contained kwa muda wa siku tatu. Kazi yangu nilijiandikisha kama mwanafunzi wa chuo cha elimu ya sayansi ya bahari cha Zanzibar. Sababu ya ujio wangu pale Kigamboni ikiwa ni kuandika juu wa mwenendo wa pwani ya Kigamboni. Maelezo yote haya nilijua kuwa ni upuuzi na uongo mtupu, lakini ilikuwa ni vigumu kwa yule jamaa wa mapokezi, ambaye alionekana kuwa hakwenda shule kiasi cha kuweza kuelewa mambo kama yale, kuyatilia maanani na kuyafuatilia.

Nilijifungia chumbani kwangu na kuelekea moja kwa moja bafuni ambako nilioga kwa muda mrefu. Kisha niliosha na kufunga kidonda changu, kabla ya kujibwaga kitandani na kuchapa usingizi mzito.

SEHEMU YA TANO:

Jambazi lauawa na pingu mkononi.

Kilikuwa ni kichwa cha habari kilichochukua uzito wa juu kabisa kwenye moja ya magazeti ya kila siku yanayotoka jioni.

Moyo ulinilipuka na kuanza kunienda mbio, huku nikishuhudia lile gazeti likitetemeka mikononi mwangu wakati nikikodolea kwa kutoamini kichwa kile cha habari.

Ilikuwa ni majira ya saa moja ya usiku wakati nikiwa napata mlo wa usiku kwenye mgahawa wa ile nyumba ya wageni wakati nilipoona kile kichwa cha habari kutoka kwenye moja ya magazeti yaliyokuwa yakitembezwa na kijana mmoja ndani ya mgahawa ule. Nilinunua haraka lile gazeti huku hamu ya kula ikiniisha. Niliinamia sahani yangu ya chakula na kukichezeachezea kwa muda kile chakula, kisha nikarudi chumbani kwangu upesi na kuanza kuisoma tena habari ile.

Macho ya Nyoka ameuawa!

“Haiwezekani! Haiwezekani auawe kirahisi namna hii! Macho ya Nyoka! Labda ungeniambia Dokta Martin Lundi, ningeweza kuamini, lakini sio Macho ya Nyoka!” Nilikuwa najisemea peke yangu mle ndani huku nikitikisa kichwa kuipinga a habari ile huku nikiiona waziwazi kwa macho yangu pale gazetini.

Lakini gazeti ndivyo lilivyoandika!

Hapana bwana, kwangu hilo lilikuwa haliwezekani kabisa. Yule mtu ni muuaji wa kuzaliwa. Yaani yeye ndiye mwenye kazi ya kuua watu, sasa iweje tena yeye ndio auawe kirahisi namna hii?

Sio Kweli. Hii ni mbinu yao tu ya kutaka kunilaghai ili nijiamini kuwa niko salama halafu wanikamate kirahisi. Macho ya Nyoka ndiye mtu niliyemuhofia kuliko wote miongoni mwa wale wauaji niliowaona kule msituni, na nilishapata hisia kuwa kama sitanusurika na maisha yangu katika kindumbwendubwe hiki, basi ni Macho ya Nyoka ndiye atakayeniua. Sasa tena hii habari…? Macho ya Nyoka afe? Hapana, sio kweli.

Sikuamini.

Nilikumbuka yale macho yake jinsi yalivyoniahidi kifo pale aliponitazama kwa chuki huku akininyooshea kidole kabla hajatimua mbio kumkimbia yule afisa wa polisi, pingu ikimning’inia kwenye  mkono mmoja.

Macho ya Nyoka aliniahidi kifo cha mateso makubwa kwa macho tu na nikaelewa bila shaka yoyote ni nini alikuwa akiniahidi! Yaani hakutamka hata neno moja! Macho tu, na ujumbe ukanifika!

Eti sasa amekufa!

Niliukumbuka ule mlipuko wa bastola niliosikia ukitokea kule nje walipokuwa wakikimbizana, baada ya yule afisa wa polisi kuniamuru nisiondoke wakati akimfuata mbio yule muuaji. Nami nikaamua kutimua mbio kutoka eneo lile bila ya kujali kelele za Suleiman Kondo kuwa nisikimbie.Pamoja na kuona kuwa kile kilichosemekana kutokea kuwa hakiwezekani, sikuweza kujizuia kuisoma ile habari iliyoandikwa gazetini kuhusu tukio lile lililotokea asubuhi ya siku ile pale ofisini kwetu.

Na hata nilipomaliza kuisoma kwa mara ya pili, bado nilibaki mdomo wazi na kujiuliza iwapo nilitakiwa niiamini au nisiiamini habari ile.

Kwa mujibu wa gazeti lile, ni kwamba jambazi hilo ambalo bado jina lake halijatambulika, liliuawa katika mapambano na polisi baada ya kufanikisha kutoroka kwa mwanamke ambaye alikuwa ametiwa mbaroni na polisi kuhusiana na mauaji ya kutatanisha ya watafiti wa Idara ya Makumbusho ya Taifa pamoja na watu wengine huko Manyoni.

Kutokana na maelezo ya gazeti lile, nilielewa kuwa Macho ya Nyoka alipokuwa akikimbizwa na yule askari, aliamua kusimama ili apambane naye, ambapo alitoa bastola (hii itakuwa nyingine, ambayo bila shaka alikuwa nayo – kwani ile bastola yake ndiyo aliyokuwa akiitumia yule askari baada ya kuangushwa chini katika mapambano), lakini kabla hajaitumia, yule askari alimuwahi kwa risasi ya mguu, na alipozidi kujaribu kumtupia risasi ndipo yule askari alipompiga risasi nyingine(sikumbuki kusikia mlipuko wa pili wa bastola, lakini wakati huo mimi ndio nilikuwa nimehamanika nikitafuta namna ya kutokomea kutoka eneo lile) iliyompata kifuani na kumuua.

Just like that…!

Yaani hivi hivi tu!

Baada ya hapo gazeti lilielezea tena habari za yale mauaji ya Manyoni, na kutaja kuwa mwanamke aliyetoroka katika tukio lile bado anatafutwa na polisi na kutaja jina langu halisi, huku likinukuu taarifa ya polisi kuwa mwananchi yeyote atakayeniona au kuwa na habari zozote za mahala ninapoweza kupatikana, atoe taarifa katika kituo chochote cha polisi kitakachokuwa karibu naye.

Kwa kuwarahisishia kazi wananchi, wasifu wangu wote ulielezwa gazetini, ikiongezewa na taarifa ya nguo nilizokuwa nimevaa siku ile pamoja na mtindo wa nywele niliokuwa nimeusuka. Nilishukuru mungu kuwa ingawa nilipoingia pale kwenye ile nyumba ya wageni nilikuwa nimevaa zile jinzi zangu, nywele zangu za rasta nilikuwa nimezifunga ndani ya kilemba ambacho hadi muda ule nilipokuwa nakula pale kwenye mgahawa bado kilikuwa kichwani mwangu, na nilikuwa nimebadilisha nguo.

Zaidi ya hapo, picha yangu yenye ukubwa wa pasipoti iliwekwa pale gazetini, picha ambayo sikuwa na shaka ilitoka kule  kazini kwangu. Ni picha ambayo niliipiga siku chache baada ya kumaliza masomo yangu Chuo Kikuu, niliyoiwasilisha pale ofisini wakati naanza kazi kwa ajili ya kuwekwa kwenye faili langu binafsi la ajira.

Kwenye  picha ile nilikuwa naonekana mdogo zaidi, mwembamba zaidi, na zaidi ya hapo nilikuwa nimekata nywele zangu na kuziacha ndogo ndogo sana, ikiwa si siku nyingi tangu nitoke kwenye msiba wa baba yetu, ambapo kutokana na msiba ule, nilinyoa nywele zote.

Haikuwa picha ya kunitia shaka sana, lakini niliogopa kupita kiasi, kwani sasa jina langu lilikuwa hadharani, na wajihi wangu ulikuwa gazetini kwa kila mwenye macho kuuona.

Nitakimbilia wapi sasa?

Bila hata kufikiri zaidi nililitupa pembeni lile gazeti na kuanza kufumua zile rasta.

Hivi ni kwa nini haya mambo yanatokea?Ndilo swali lililokuwa likijirudia tena na tena kichwani mwangu tangu nilipoamka kutoka kwenye ule usingizi mzito ndani ya ile nyumba ya wageni. Na baada ya kusoma zile habari za kwenye lile gazeti, nilijikuta nikizidi kujiuliza lile swali. Na kila nilipojiuliza swali lile,nilijikuta nikijiuliza swali lingine kubwa na gumu zaidi. Kwa nini mambo yale yanikute mimi katika watu wote?

Kwa kweli wakati natimua mabio baada ya tukio la pale ofisini, nilikuwa na hakika kabisa kuwa nilikuwa nachukua uamuzi pekee wa busara katika mazingira yale. Lakini kila nilivyozidi kuyatafakari upya matukio yote yaliyotokea pale ofisini siku ile, nilipata hisia kuwa yule afisa wa jeshi la polisi alikuwa ni askari wa kweli, na kwamba hata kama alikuwa ana nia ya kunikamata kwa makosa yale aliyonitamkia pale ofisini kwa Mkurugenzi, kuibuka kwa Macho ya Nyoka kwa namna alivyotuibukia na matendo yaliyofuatia, kungeweza kabisa kumbadilisha mawazo na labda angeweza kuwa ndiye mtu wa kunisaidia, hasa nikizingatia kuwa yule alikuwa ni afisa wa ngazi ya juu kwenye jeshi la polisi.

Lakini kwa wakati ule ningeyajuaje hayo? Ningeweza kuyachezea bahati nasibu maisha yangu? Hapana, bora nilivyokimbia.

Nilivyozidi kulitafakari tukio la pale ofisini na uamuzi niliochukua, ilinifunukia wazi kuwa sasa nilikuwa naendeshwa na hisia zaidi kuliko kitu kingine chochote. Kwamba, ujumla wa matukio yote yaliyonikuta huko nyuma hadi kufikia sasa, umepelekea hisia zangu zote kufikia hatua ambapo zilikuwa zinaanza kutekeleza matendo ya kujihami na kujiokoa kwanza, halafu kutafakari juu ya hatua hizo baadaye. Baada ya matukio ya kule kwa mkuu wa wilaya nilipokimbilia kutafuta msaada, na yale ya kule kwa Kelvin na nyumbani kwa mama yangu, nilikuwa nimejitosheleza fika akilini mwangu kuwa sehemu pekee yenye usalama kwangu ni pale nitakapokuwa peke yangu. Na kwamba kila nitakayemdhania kuwa huenda akawa na msaada kwangu, anaondokea kuwa upande wao.

Wao.

Wao ni akina nani?

Na yule afisa wa polisi naye…?

Macho ya Nyoka alikuwa tayari kabisa kumuua yule askari…sasa amekufa yeye!

Kwa hakika nilijua kuwa kama sikuchukua uamuzi wa haraka na kumbamiza Macho ya Nyoka kwa ile ndoo, bila shaka ningemshuhudia yule askari akiuawa mbele ya macho yangu.

Nilijishawishi kuwa kwa wakati ule, nilikuwa nimechukua uamuzi wa busara sana kukimbia kutoka eneo lile, kwani kwa mambo niliyoyashuhudia kutoka kwa akina Martin Lundi, isingekuwa ajabu kabisa kukuta kuwa yule askari na Macho ya Nyoka walikuwa kitu kimoja, na walikuwa wanajifanya kutupiana mateke mbele yangu ili nijenge imani kwa yule askari wapate kunichukua kirahisi.

Lakini sasa nilielewa vinginevyo.

Kwa hakika yule alikuwa ni askari wa kweli, lakini hata kama ningebaki pale ofisini kama alivyoamrisha, angenielewa na kunisaidia? Au ndio ingekuwa kama yale ya kule kwa mkuu wa wilaya?

Kadiri nilivyoitafakari ile hali huku nikiendelea kujifumua zile rasta, ilinijia wazi kuwa ingawa kifo cha Macho ya Nyoka kilitakiwa kiwe faraja kwangu, bado hakikuleta unafuu wowote kwangu, kwani bado nilikuwa natafutwa na akina Martin Lundi. Tena sasa baada ya kifo cha mwenzao na kuelezwa gazetini kwa mazingira yaliyopelekea kifo chake, nilijua kuwa watazidisha bidii za kunisaka kwani nilikuwa nina hakika kabisa kuwa hawakutaka kabisa nitiwe mbaroni na polisi wasio upande wao ili waweze kuupata na kuupoteza ule ushahidi nilio nao, ambao ulikuwa una madhara makubwa sana kwao.

Na kama hiyo haitoshi, polisi nao kwa upande wao walikuwa wanaendelea kunisaka. Sasa sijui kwa nini gazeti liliandika kuwa Macho ya Nyoka alikuwa amekuja kunitorosha, wakati yule afisa aliona wazi kuwa yule muuaji hakuwa na nia ya kunitorosha kwa urafiki baina yetu bali kwa sababu nyingine tu. Vyovyote itakavyokuwa, mbele ya yule afisa wa polisi na jeshi lake, bado nilikuwa mkimbizi kutoka kwenye mikono ya sheria, tena niliyekaidi amri ya kutotoroka niliyopewa na yule afisa wakati akimfukuza yule muuaji.

Yule afisa wa polisi akiendelea kuniwinda basi ajue kuwa anaweza kuendelea kuniwinda kwa sababu niliokoa maisha yake…

 

--

 

 

Kwa siku mbili mfululizo sikutoka nje ya chumba changu zaidi ya kwenda kula kwenye ule mgahawa wa ile nyumba ya wageni na kurudi tena chumbani. Hizi zilikuwa ni siku mbili za kutathmini yale matukio yaliyonitokea na jinsi nitakavyokabiliana nayo.

Siku yangu ya kuondoka ilipofika, niliongeza siku nyingine tatu, nikidai kuwa nilikuwa sijamaliza utafiti wangu. Wakati huu nilikuwa nimeshanunua madaftari na makaratasi pamoja na kalamu kadhaa ili kweli nionekane mwanafunzi niliye kwenye utafiti. Na ili nisijiletee mashaka, nilikuwa nikitoka nje na kwenda kuzubaa pwani iliyokuwa karibu na ile nyumba ya wageni, na mara nyingine nikitembea tu mle mjini, huku mara zote nilizotoka, nikihakikisha kuwa nilikuwa nina madaftari yaliyoonekana wazi kwenye mkoba wangu.

Katika kipindi hiki, nilitumia muda wangu mwingi kadiri nilivyoweza kuangalia televisheni iliyokuwamo mle chumbani, hasa taarifa za habari ili nijue iwapo kuna habari zaidi juu yangu katika vyombo vya habari na kama zipo, zimetolewa kwa mtazamo gani.

Aidha nilikuwa nikinunua magazeti kila siku nilipotoka kwenda kupata kiamsha kinywa na kuyasoma kwa makini kutafuta habari zozote zilizohusiana na matukio niliyokumbana nayo. Lakini habari ile ilionekana kufifia kabisa magazetini na kwenye vyombo vingine vya habari.

Kama mvua iliyonyesha ghafla wakati wa kiangazi, halafu ikapotea na kukiacha kiangazi kiendelee kutawala.

Hali hii ilinitia wasiwasi sana, kwani haikuniingia akilini kabisa kuwa baada ya taarifa kama ile, na taarifa zangu zikiambatana na picha yangu kutolewa gazetini, mambo yawe kimya kiasi kile. Nami nilizidi kuchoka kukaa katika ile hali ya wasiwasi na kujificha, nikipita nikijibandika majina yasiyo yangu kwa woga wa kukutwa na watu wa Dokta Lundi au wanausalama.

Na kadiri nilivyokuwa nikiendelea kujificha kwenye ile nyumba ya wageni, nilikuwa nazidiwa na hamu na dukuduku la kutaka kujua hali ya mama yangu ikoje hasa baada ya kukutana na Dokta Lundi siku ile nilipowatoroka pale nyumbani. Nilitamani pia kumpigia simu dada yangu labda angenipa habari zozote lakini nilishindwa kutokana na woga kuwa huenda namba ya simu nitakayotumia ikafuatiliwa na kugundulika kuwa nimepiga kutokea Kigamboni halafu wakaniibukia kule nilikojificha.. Nilishindwa pia kutafuta habari za Kelvin kwa sababu hiyo hiyo, ingawa nilikuwa na shauku kubwa ya kuijua hatima yake.

“Lakini kwa nini niendelee kuishi kikimbizi namna hii?” Nilijisemea peke yangu nikiwa mle chumbani mwangu na kusonya kwa hasira na kuchanganyikiwa. Niliinuka kutoka kitandani nilipokuwa nimejilaza na kwenda kusimama nikiegemea ukuta huku nikiwa nimetumbukiza mikono yangu kwenye mifuko ya suruali ya michezo niliyokuwa nimeivaa.

“Na nitaendelea kuwindwa namna hii mpaka lini?” Nilijisemea tena kwa hasira na kutoa msonyo mwingine mkali. Nilitembea mle ndani huku nikiwa nimezamisha mikono yangu mifukoni nikiitafakari hali ile.

“Halafu kibaya ni kwamba hao wanaoniwinda wananijua fika, lakini mimi siwajui…naona watu wananikimbiza, wanaua watu, wanawarubuni ndugu na jamaa zangu, …lakini wao ni akina nani…?Sijui!” Niliguna na kujibwaga tena kitandani kwa kukata tamaa.

Muda ulikuwa ni kama saa kumi na mbili za jioni na kwa mbali nilisikia sauti ya adhana ikiwakumbusha waislamu kwenda msikitini kwa sala ya jioni.

“Kwani tatizo ni nini hasa …? Kwa nini yale mauaji yalitokea kule msituni? Kwa nini ilikuwa muhimu kwa Dokta Lundi kunipakazia mambo ya uongo namna ile…?”

Niliinuka na kuliendea begi langu.Nikaitoa ile kamera ya Gil, na kwa mara ya kwanza tangu nitoke kule Manyoni nilikaa chini na kuutazama upya ule mkanda tangu mwanzo hadi mwisho, nikilirudia upya lile tukio la kule msituni.

Nilipomaliza kutazama yale mambo ya ajabu niliyoyarekodi kule msituni nilijikuta nikibubujikwa na machozi bila kupenda. Lakini pia kulitazama tena lile tukio kuliniletea mwanga mpya kwenye  uelewa wangu wa tukio lile na nikajikuta nikiurudisha nyuma na kuuangalia upya kutokea mwanzo hadi mwisho huku nikitafakari matukio mengine yaliyonitokea ambayo hayakuwamo mle kwenye ule mkanda.

Niligundua kuwa kumbe wale wauaji, akina Martin Lundi, wote walikuwa wamevaa glovu mikononi mwao, kitu ambacho sikuwa nimekibaini  hapo mwanzo.

Ina maana walikuwa wamedhamiria kutoacha ushahidi wowote wa kuhusika kwao aidha na kifo cha yule mtu, au tukio zima la kule msituni.

Nilirudia ile sehemu nilipokuwa naongea na yule mtu asiye na jina kule msituni, ambapo hapa nadhani nilirekodi bila ya kujijua, kwani ile kamera ilikuwa imeelekea ardhini kwenye mchanga, na ilichorekodi kilikuwa ni yale mazungumzo yaliyotokea baina yetu tu pale mchangani. Na nilipokuwa nikitazama ule mkanda ukionesha michanga tu ya pale alipokuwa amelala yule mtu na sehemu kidogo ya bega na mkono wake, nilikuwa nayasikia upya yale maongezi kutoka kwenye ile kamera.

“Usiongee! Tulia, nitakusaidia”Nilijisikia.

Ikasikika miguno ya yule mtu, kisha nikaona zile namba ambazo yule mtu aliziandika mchangani na kunisisitizia nizitazame.

Niliusimamisha ule mkanda na kukimbilia kalamu na kijitabu kidogo kilichokuwa mezani, nikarudi pale nilipoiacha ile kamera na kuinakili ile namba huku moyo ukinienda mbio.

Nikaendelea kuutazama ule mkanda.

Sawa…nimeshaona! Hizi namba ni za nini? Na wewe ni nani…kwa nini wale watu wamekufanya hivi? Umewafanya nini? Ni nani wale?” Nilijisikia nikimuuliza kwa wahka.

Ikasikika sauti ya yule mtu akikohoa kwa taabu, ikifuatiwa na pumzi zake akitweta kama mtu aliyemaliza mbio ndefu.

“Find the Bastard!”Alisema kwa shida.

“Yes! Usiwe na wasiwasi nitahakikisha wanafikishwa mbele ya sheri—”

“…at the Rickshaw…!”. Alinikatisha.

“Rickshaw? Rickshaw iko wapi ?” Sauti yangu ilimuuliza.

Niliisimamisha tena ile kaseti na kuandika tena kwenye kijitabu changu:

Bastard.

Rickshaw.

Nikaendelea kuutazama ule mkanda.

Zilifuatia sauti za yule mtu akigumia kwa taabu, nami kumbukumbu zangu zikanionesha picha ya yule mtu alipokuwa akitapatapa huku akitupa kichwa chake huku na huko na nikakumbuka jinsi nilivyopandwa na woga nilipodhani kuwa ndio alikuwa anakata roho.

“Wewe ni nani…ndugu zako ni nani?” Sauti yangu iliuliza.

Niliusimamisha ule mkanda na kuandika kwenye kijitabu changu:

Wewe ni nani? – No answer. Mr. Who?Mr. Nani? Question Mark! =Mr. Q?

Nikabonyeza sehemu inayotakiwa na ule mkanda ukaendelea.

“Get the key… the bastard!”Sauti yake ilisema kwa kutweta.

“Key…? What key…?”Sauti yangu iliuliza kwa kutoelewa.

Niliisimamisha ile kaseti na kuandika tena kwenye kijitabu changu:

Key – Ufunguo. ???

Nikaendelea kuutazama ule mkanda.

“At the Rickshaw…!” Alitweta zaidi.

“I don’t understand!” Nilimwambia kwa kutoelewa.

“Please…Go now!” Sauti yake ilifoka.

“Lakini bado sijaelewa…nataka kukusaidia! Au hujui Kiswahili…? Can’t you speak Swahili?” Nilijisikia nikimsihi.

“Find the bastard!” Ile sauti ilinisisitiza.Niliisimamisha tena na kuandika kwenye kijitabu changu:

Find the Bastard! – Mtafute Mwanaharamu? (M. Lundi&wenzake???)

Nilibaki kimya kwa muda mrefu huku nikitafakari wakati picha ya tukio lile ikinijia akilini na nikakumbuka jinsi yule mtu alivyonitazama huku akitoa kitu kama tabasamu dogo sana baada ya kuniambia yale maneno.

Now why did you smile like that Mr. Q, eenh?” Nilijisemea mwenyewe kwa sauti ya chini, nikimuuliza yule marehemu huko aliko kwa nini alitabasamu namna ile baada ya kunieleza maneno yale.

Nilikaa nikitafakari kwa muda mrefu sana, huku nikichorachora vitu visivyoeleweka kwenye kile kijitabu changu kabla ya kuendelea kuuangalia ule mkanda.

Okay…I can speak english… who are you? Who are those people…? Do you have any relatives…? I can help you…I want to help you!” Nilikuwa nikimbembeleza anipe taarifa zaidi kumhusu.

Please Go…watakukuta!”. Niliusikia msisitizo ulioubeba woga aliokuwa nao, kwenye ile sauti.

“Watakuua…wacha nijaribu kukusaidia.” Nilijisikia nikimsihi huku sauti yangu yangu ikitetema.

“I don’t care…you go find the bastard!” Sauti yake ilinijibu kwa ukali.

Hapa niliusimamisha tena ule mkanda na kuandika kwenye kijitabu changu:

Mr.Q hajali kama angeuawa?? Anachojali = Find the Bastard!!!!

Who is the Bastard? – M. Lundi, Kigulu,Macho ya Nyoka(Dead?) au kuna kitu kingine?

Hapa nilitafakari tena kwa muda mrefu, na ingawa sehemu hii yote ya mkanda nilikuwa nimerekodi sauti tu, wakati picha ikionesha michanga tu ya pale mchangani alipokuwa amelala yule mtu asiye na jina(nilishampachika jina la Mr.Q), bado niliikumbuka vizuri sana sura yake ilivyokuwa pale alipomaliza kusema yale maneno na jinsi alivyojitahidi kutabasamu tena halafu akazidiwa na kikohozi kikali na damu ikaanza kumtoka mdomoni.

Hapa mkanda ulisimama kabisa kurekodi na hakukuwa na picha wala sauti yoyote, nami nikakumbuka kuwa ni wakati huu ndipo nilipomwinua kichwa chake ili damu isimpalie na kuanza kumfuta ile damu kwa mkono wa shati langu.

Nilikumbuka waziwazi kuwa nilipofanya vile, yule mtu alinishika mkono kwa nguvu na kunitolea macho huku akinisisitizia kuwa niondoke eneo lile haraka kabla wale wauaji hawajanikuta na kuniua.

Na kweli masikini, nilipoondoka na kumwacha pale, wale wauaji walirudi na kumkuta akiwa anagaragara pale mchangani.

Nililia kwa uchungu baada ya kuona ni jinsi gani yule mtu alivyonisisitiza niokoe maisha yangu ingawa alijua kuwa yeye angekufa muda wowote.

“Lakini kwa nini uliniita? Hukutaka nikuokoe, bali ulitaka kunieleza kitu…?” Nilimuuliza kwa fadhaa yule marehemu huko aliko huku nikibubujikwa machozi na nikihisi donge kubwa likinikaba kooni.

“Sasa mbona hukunieleza kitu chochote cha maana, Mr. Q?” Nilimuuliza tena kwa uchungu huku nikiendelea kububujikwa na machozi.

Nilitazama vitu nilivyoandika kwenye kile kijitabu changu.

Hakukuwa na kilichokamilika kwenye maandiko yale, ambacho kiliniwezesha kujua ni nini yule mtu alitaka kunieleza. Kwa muda mrefu nilibaki nikikodolea macho vitu nilivyoandika kwenye ule ukurasa wa kile kijitabu changu, bila ya kupata jibu la moja kwa moja.

456718

Bastard.

Rickshaw.

Wewe ni nani? – No answer. Mr. Who? Mr. Nani? Question Mark! = Mr. Q?

Key – Ufunguo.???

Find the Bastard! – Mtafute Mwanaharamu?(M. Lundi&wenzake???)

Mr. Q hajali kama angeuawa?? Anachojali = Find the Bastard!!!!

Who is the Bastard? – M. Lundi, Kigulu, Macho ya Nyoka (Dead?) au kuna kitu kingine?

 

Nilidhani ningeweza kupata mwelekeo fulani kutoka kwenye ule mlolongo wa vitu nilivyoandika kutokanana kauli za yule mtu aliyeuawa msituni. Nilihitaji kutafakari zaidi.

Hatimaye niliamua kuendelea kuutazama ule mkanda na nilipoifikia sehemu ambapo yule mtu niliyembatiza jina la Mr. Q alimrukia Macho ya Nyoka na kuanza kupambana naye, niliusimamisha tena ule mkanda na kubaki nikiikodolea macho kwa mshangao mkubwa ile picha iliyoganda pale kwenye runinga ya ile kamera huku akili ikinizunguka.

Kitu nilichokiona pale, ingawa nilishakiona kwa macho yangu kule msituni, na nikakiona tena kwenye ule mkanda nilipoutazama mara ya kwanza, kilinishitua na kuniletea mtazamo mpya kabisa katika suala zima la mkasa huu ulioniangukia.

Ilikuwa ni vigumu kuamini, lakini ndivyo ilivyoelekea.

Niliirudisha tena ile sehemu na kuiangalia upya.

Ni kweli kabisa nilichogundua, na hata pale ugunduzi ule ulipojithibitisha akilini mwangu, nilijikuta nikishikwa na butwaa nisijue la kusema.

Mr. Q alimrukia Macho ya Nyoka makusudi ili auawe!

Naam! Ndivyo haswa.

Nilihisi mwili ukinisisimka na vipele vya baridi vikinichipuka mwilini.

Kwa nini Mr. Q aamue kufanya vile? Kwani bila shaka alijua kuwa katika wale watu watatu, ni Macho ya Nyoka pekee ndiye aliyekuwa anaelekea kuua bila hata ya sababu, hivyo akaamua kumpa sababu ya kumuua.Na ndivyo ilivyotokea!

Nilifikiria maana ya kitendo kile  huku maswali yakinielemea.

Kwa nini aamue vile?

Kwa nini aamue vile wakati ule, na si wakati wowote kabla ya hapo?

Kutokana na tukio lile kama jinsi nilivyojikumbusha kwa kuutazama tena ule mkanda, ni kwamba yule mtu aliteswa sana kabla ya kufikishwa pale msituni, na kama aliteswa, lazima kuna sababu ya kuteswa huko.

Nilikumbuka kuwa kuna wakati kabla ya yule mtu kumrukia Macho ya Nyoka na hatimaye kuuawa, alimtemea mate Kigulu ambaye alikuwa akimuuliza kitu fulani, na kisha akamtupia mchanga usoni, na wakati Kigulu anajipangusa mchanga, yeye alimrukia Macho ya Nyoka.

Ambaye wakati huo alikuwa pembeni kabisa tena na bastola yake alikuwa ameiweka mfukoni baada ya kukemewa na wenzake alipokuwa akimtishia Mr. Q kwa bastola ile.

Hii ilimaanisha kitu kimoja tu…

Yule mtu alikuwa anawachokoza kusudi ili wamuue!

Kwa nini?

Nilikaa muda mrefu nikitafakari juu ya hilo, na hatimaye nilipopata jibu ubaridi ulinitambaa mwilini huku nikihisi kijasho kikinitoka.

Mr.Q aliamua kufanya vile kwa sababu alikuwa ameshanieleza kila kitu alichotaka na ndio maana akaona afe na siri yake badala ya kuitoa kwa wale wauaji.

Duh! Si mchezo!

Sasa ni siri gani hiyo lakini?

Jibu lilikuwa kwenye yale maneno aliyokuwa akiniambia, na si kwingine.

Nilijikuta nikikirudia kile kijitabu changu na kutazama vile vitu nilivyoviandika kwa umakini mpya. Na nilipokuwa nikitazama vile vitu nilivyoandika, nilipitisha uamuzi kuwa sasa muda wa kuendelea kuwindwa na akina Martin Lundi ulikuwa umekwisha. Na badala yake ulikuwa umefika muda wa mimi kuanza kuwawinda wao.

Windo lawa mwindaji, mwindaji awa windo.

 

--

 

Usiku ule sikulala. Sikutaka hata kula.

Kwa muda mrefu nilikuwa nikiutazama ule mkanda kwa kuurudia tena na tena nikijaribu kutafuta ugunduzi mpya kutoka kwenye vile nilivyovirekodindani ya ule mkanda. Mkanda ambao niliurekodi bila ya kupanga wala kufikiri, in a spur of a moment, lakini sasa umetokea kuwa muhimu sana katika mustakabali mzima wa maisha yangu.

Na kila nilipoutazama ule mkanda, hasa ile sehemu ya mwisho, nilizidi kujihakikishia kuwa ugunduzi wangu kuwa Mr. Q aliamua kumrukia Macho ya Nyoka makusudi ili auawe,ulikuwa sahihi.

Na alifanya vile baada ya kuwa amenieleza kila kitu alichotaka kunieleza.

Ndio maana alikuwa akiniita kwa bidii sana pale alipoachwa peke yake kule msituni.

Na ndio sababu alipokwisha nitajia The Rickshaw na kuniachia ile namba aliyoniandikia pale mchangani, na kunipa maagizo kuhusu The Bastard, alitoa tabasamu la faraja. Kwa wakati ule sikuelewa ni kwa nini alifanya vile, lakini sasa nilielewa. Kila nilipotafakari hali ile, nilizidi kumshangaa na kumwonea huruma yule mtu niliyempachika jina la Mr. Q. Kwa hakika alikuwa na ujasiri wa hali ya juu, kwani kwa hali niliyomkuta nayo, haikuwa na shaka kabisa kwangu kuwa alikuwa ameteswa sana kabla ya kufikishwa pale msituni ili atoe siri aliyokuwa nayo kwa wale wauaji. Na kwa jinsi mambo yalivyojitokeza pale msituni, ni kwamba hakuwatajia hiyo siri, na ndio maana Macho ya Nyoka aliponaswa na mtego wa Mr. Q na kumuua, wale wenzake, Martin Lundi muongo na yule Kigulu mwenye jicho la bandia walimkemea na kumfokea sana, kwani Macho ya Nyoka alikuwa amemsaidia Mr. Q kufa na siri yake.

Na ilipogundulika kuwa mimi nilikuwepo eneo lile, nikawa windo lao kuu kwa nia ya kutaka kufuta ushahidi wowote kuwa kuna mtu aliwaona wakiwa kule msituni. Lakini ilipowafunukia kuwa niliwaona wakimuua yule mtu, na kwamba nina ushahidi wa tukio lile kwenye mkanda wa video, umuhimu wangu kwao ukaongezeka maradufu.

Na sasa nadhani mimi ninayajua mambo aliyokuwa anayajua Mr. Q ambayo wao walishindwa kuyapata kutoka kwake pamoja na mateso waliyompa, kwani Mr. Q hakutakiwa kufa kabla ya kuwatajia hilo walilokuwa wakilitaka.

Nasema nadhani naijua siri aliyokufa nayo Mr. Q kwa sababu bado sijaweza kuung’amua ujumbe uliojificha kwenye yale maneno machache aliyonieleza kabla ya kufa kwake.

Jambo moja nililokuwa nina hakika nalo ni kwamba na mimi sikutakiwa kufa mpaka wale watu waupate ule mkanda wa video niliokuwa nao.

 

--

 

 

Asubuhi ya siku iliyofuata nilitoka na kuingia katikati ya jiji kwa mara ya kwanza tangu nikimbilie kule Kigamboni. Katika mawazo ya wale wauaji, haikuwajia kabisa kuwa ningekimbilia eneo kama lile, na bila shaka walikuwa wamenisaka sana jijini na sasa walikuwa wamebaki wamepigwa butwaa, wakijiuliza nimewezaje kuyeyuka kiajabu kama vile.

Nilikuwa nimekata nywele zangu katika mtindo wa Bob Cut, ambao ulinibadilisha sana muonekano wangu. Zaidi ya hapo, nilikuwa nimevaa suruali nyeusi ya kitambaa laini iliyonikaa vyema, na shati jeusi la kitambaa kizito lililokatwa katika mtindo wa koti, ndani yake nilivaa blauzi nyepesi ya kitamba cheupe, na hivyo kuonekana kuwa nimevaa suti nyeusi, huku miguuni nikiwa na vile vile viatu vyangu vya kamba vilivyoniwezesha kukimbia kwa urahisi pindi itakapolazimu kufanya hivyo. Nilikamilisha muonekano wangu kwa kubandika ile miwani yangu ya jua.

Kwa mtu yeyote ambaye angeonesha hamu ya kutaka kunijua, basi wazo ambalo angekutana nalo ni kwamba nilikuwa ni wakili miongoni mwa mawakili aidha wa serikali au wa kujitegemea, ambao huwa wanavaa nguo nyeusi na nyeupe kama vile.

Huku nikiwa nasumbuliwa na wazo kuwa laki zangu nne nilizotoka nazo kule Manyoni zilikuwa zinaniishia kwa kasi, nilisafiri kwa basi mpaka maeneo ya Makongo, huko nilitafuta kibanda cha simu za kulipia na kuanza kujaribu kupiga simu huku moyo ukinienda mbio.

Nilianza kuipiga ile namba iliyoandikwa mchangani na Mr. Q kule msituni, kwani mawazo yangu yalinituma kuwa ile ilikuwa ni namba ya simu. Na kama ingekuwa hivyo, basi ilikuwa ni namba ya muhimu sana katika ufumbuzi wa kadhia ile iliyoniangukia, kwani nilikumbuka jinsi Mr. Q alivyokuwa akijitahidi kuiandika ile namba kwa taabu pale mchangani, nami nikamdhania alikuwa amerukwa na akili kutokana na kukaribia kifo.

Lakini sasa nilielewa kuwa alikuwa anaelewa anachofanya, na alitaka mimi niione ile namba.

Niliipiga ile namba kwa mtandao wa Vodacom, lakini nikapata ujumbe kutoka kwenye mtambo kuwa ile namba haikuwapo katika mtandao wao. Nikaijaribu tena kwa mtandao mwingine, nako nikapata jibu kama lile. Wasiwasi ulianza kunipanda, na nikajaribu namba ile kwa mitandao mingine ya simu za kiganjani nchini , nakote mambo yakawa ni yale yale.

Mungu wangu, sasa itakuwaje?

Nilichanganyikiwa na nikabaki nikiwa nimeduwaa. Kama ile haikuwa namba ya simu, basi itakuwa ni namba ya nini?

Bado nilikuwa naamini  kuwa ile namba ilikuwa ni kiungo muhimu kwenye  uteguzi  wa kitendawili chote kilicholizunguka lile tukio la kule msituni. Sasa nifanye nini? Yaani usumbufu wote huu uwe ni bure kweli?

Nilikuwa nimekwenda kupigia simu kule Makongo nikiwa na matarajio kuwa endapo ile namba ilikuwa ya simu, hasa zile za kiganjani na ina uhusiano na akina Martin Lundi, basi ingekuwa rahisi sana kwa wale wauaji kunifuatilia na kujua kuwa nilikuwa nimepiga simu kutokea Makongo. Hivyo wao wangenisaka kwa nguvu zote maeneo ya Makongo, wakati mimi ningekuwa mafichoni kwangu Kigamboni. Lakini sasa haikuwa hivyo. Ile namba haikuwa ya simu.

Angalau haikuwa namba ya simu ya Kiganjani.

Nilijiambia kuwa huenda ikawa ni namba ya simu ya waya ya TTCL, lakini nilikumbuka kuwa namba zote za TTCL hapa jijini zilikuwa na tarakimu saba, na zilipangwa kutokana na eneo. Kwa mfano namba za Tabata anapoishi mama yangu zilikuwa zinaanzia na tarakimu 280xxxx wakati zile za maeneo ya barabara ya Nyerere zilikuwa zikianzia na tarakimu 286xxxx.

Lakini ile namba niliyoachiwa na Mr. Q ilikuwa na tarakimu sita, kwa hiyo kama ni hivyo basi ingekuwa ni namba ya mikoani. Sasa ni mkoa gani? Itanibidi nijue namba za utambulisho za mikoa yote ili niweze kuipiga ile namba na huenda nikabahatisha ikaita katika mkoa mmoja.

Niliondoka eneo lile na kuchukua basi hadi Kariakoo ambapo nilielekea moja kwa moja hadi kwenye kituo cha huduma kwa wateja cha kampuni ya simu za waya ya TTCL. Niliingia ndani ya ile ofisi na kukiendea kimoja kati ya vitabu vingi vya simu vilivyokuwa mle ndani na kufunua ukurasa ulioonesha namba za utambulisho, yaani area code, za mikoa yote ya Tanzania. Niliuchana ule ukurasa kwa uficho mkubwa na kuusokomeza kwenye mfuko wa suruali yangu bila ya kuonwa na mtu yeyote, kisha nikaiendea kaunta ya mle ndani na kununua kadi ya kupigia simu yenye thamani ya Shilingi elfu kumi na kutoka nje.

Kituo changu kilichofuata kilikuwa ni kwenye vibanda vya kupigia simu za kadi vilivyokuwa katika eneo la Telephone House, katikati ya jiji, kwani sikutaka kubaki eneo moja kwa zaidi ya nusu saa, nikihofia kukutwa na wale wauaji au wana usalama waliokuwa makini na ile picha yangu iliyotolewa gazetini siku chache zilizopita.

Nilianza kuipiga ile namba kwa kutumia area code za mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani, na kila mara ujumbe nilioupata ulikuwa ni ule ule.

Karibu TTCL.Namba uliyopiga haitumiki. Kwa maelezo ya namba zinazotumika, tafadhali piga namba 1-3-5

Nilichanganyikiwa. Matumaini niliyojijengea kutoka kwenye ile namba yaliyeyuka. Nilianza kujiondoa eneo lile kwa unyonge pasina uelekeo maalum, lakini hatua chache mbele wazo likanijia na nikarudi haraka pale kwenye vile kibanda cha simu za kadi. Nilikumbuka kuwa namba za jijini Dar zilikuwa na tarakimu saba baada ya kubadilishwa kutoka kwenye mfumo wa zamani wa tarakimu sita na tano, ambapo zile zilizokuwa na tarakimu sita, zilibadilishwa kwa kuongezewa tarakimu 2 mbele ya ile namba ya zamani.

Nikiwa na tumaini jipya niliipiga tena ile namba huku nikitanguliza ile tarakimu 2, lakini bado nilikutana na ujumbe ule ule kuwa ile ilikuwa ni namba isiyotumika.

Hapa nilikubali kushindwa. Ile namba haikuwa ya simu.

Ilikuwa ni namba ya nini basi?

Sasa nilikuwa nimebaki na vitu vingine viwili kichwani mwangu:

The Bastard na The Richshaw.

Je, baada ya kushindwa kuwawinda akina Martin Lundi kwa kuitumia ile namba, nitaweza kutumia miongozo ile miwili iliyobaki kunifikisha waliko na kwenye siri ya tukio zima la kule msituni?

Nilidhani kuwa The Bastard halikuwa jambo kubwa sana kwani bila shaka Mr. Q aliposema vile alikuwa akimaanisha Martin Lundi na wenzake, kwani ule walioufanya pale msituni si uanaharamu?

Ila sasa hii The Rickshaw…

“Mr. Q, kwa nini umeniachia mtihani mgumu namna hii?” Nilijisemea kwa huzuni huku nikiondoka eneo lile.

Kutokana na wahka wa kuifuatilia ile namba nikiamini kuwa ni ya simu, nilisahau kabisa kununua magazeti ya siku ile, hivyo nilinunua magazeti na kutafuta hoteli ya karibu ili nipate mlo. Niliyasoma yale magazeti nikiwa pale hotelini huku nikidonoadonoa chakula nilichoagiza. Yale magazeti hayakuwa na habari yoyote kuhusiana na mkasa ulionisibu.

Habari iliyochukua uzito wa juu kabisa kwenye magazeti yote yale ilikuwa ni kuhusu kifo cha ghafla cha Jaji mkuu wa mahakama ya kimataifa dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Niliisoma habari ile taratibu huku nikiendelea kula chakula changu na akili yangu ikirukaruka mara kwa mara ikijaribu kutafuta hatua mwafaka ya kuchukua baada ya kushindwa kutegua kitendawili cha ile namba niliyoachiwa na Mr. Q. Niligundua kuwa kitu kilichoifanya taarifa ya kifo cha yule jaji  ichukue uzito wa juu ni habari iliyoambatana nayo kwamba mtanzania alitarajiwa kushika nafasi yake.

Hii hata mimi ilinivutia, kuona kuwa jumuiya ya kimataifa imeweza kutupa heshima sio tu ya kuifanya mahakama ile muhimu kuwa na makao yake hapa nchini kwetu, bali pia kutoa nafasi kwa mtanzania kuongoza mahakama hiyo ya kimataifa.

Kwa mujibu wa maelezo ya magazeti, Mtanzania anayetarajiwa kuchukua nafasi ya Jaji aliyefariki, alikuwa ni kaimu wa jaji huyo raia wa New Zealand aliyekuwa na msimamo mkali dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994.

Ingawa historia ya mtanzania aliyetarajiwa kuwa jaji mpya wa mahakama ya kimataifa dhidi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ilielezwa kwa kifupi kwenye  magazeti yale,sikuifuatilia zaidi kwa sababu hata huyo jaji mwenyewe mtarajiwa nilikuwa sijawahi kumsikia kabla ya hapo.

Nililipia chakula changu na kuondoka, nikiyaacha yale magazeti pale mezani.

Nilipotoka tu nje ya ile hoteli nilimuona rafiki yangu mpenzi, Aulelia Mushi, ambaye tulisoma wote chuo kikuu na sasa alikuwa ameajiriwa na shirika la Umoja wa Mataifa la UNDP. Hata baada ya kuanza kazi, tulikuwa tukiendelea kuwasiliana na kukutana mara kwa mara.

Lakini tangu nikutane na masahibu haya sikuwa nimeweza kuwasiliana naye hata kidogo, na nilihofia kukimbilia kwake kwa kuhofia kumpelekea akina Martin Lundi huko na kumwachia matatizo. Na nilipomuona akitembea hatua chache mbele yangu, sikuwa na shaka kabisa kuwa alikuwa ni yeye na moyo ulinilipuka kwa furaha kuwa hatimaye nimekutana na mtu wa karibu nitakayeweza kuongea naye.

Kwa hakika alikuwa ni yeye, na ingawa alikuwa amenitangulia mbele yangu nami nilimuona kutokea mgongoni, nilimjua kwa hakika kabisa kuwa ndiye.

“Aulelia!” Niliita kwa sauti huku nikiongeza mwendo nimfikie.

Aulelia alisimama ghafla na kugeuka.Niliona akinitazama kwa mashaka na hatua zake zilisita, kama ambaye anajiuliza iwapo anayemuona ni mimi kweli au ananifananisha, huku sura yake ikionesha kitu kama mshituko.

“Heey! Aulelia! Mambo?” Nilimchangamkia huku nikiongeza hatua kumsogelea na nikimtanulia mikono yangu kumkumbatia kama ilivyo kawaida yetu.

Kwa mshangao wa hali ya juu nilimshuhudia akiruka nyuma kunikwepa huku kunitazama kwa namna ya ajabu. Nilibaki nikimkodolea macho.

“He! We’ vipi? Mbona sikujui?” Aliniambia huku akinitazama kana kwamba nina wazimu.

“Hunijui? Ni mimi! Tigga! Yaani inawezekana ukawa umenisahau?” Nilimuuliza kwa mshangao.

Aulelia aligeuka na kuanza kuondoka kwa mwendo wa haraka bila ya kunijibu.

Heh! Hii tena mpya! Huyu ni Aulelia kabisa, sasa vipi anasema hanijui?

Nilimkimbilia na kumshika mkono huku nikimsemesha, nikiwa makini kuwa watu walikuwa wameanza kutushangaa pale barabarani.

“Aulelia! Wewe si Aulelia wewe? Kwa nini unasema hunijui?” Nilimuuliza huku nikimchungulia usoni kwa makini.

Aliuvuta mkono wake kutoka mkononi mwangu..

“Hebu niache!We’ vipi? Mi’ sikujui, naona umenifananisha!” Alisema kwa hasira huku akitazama mbele na akiendelea kutembea haraka. Hakutaka kabisa kunitazama machoni.

“Kama we’ si Aulelia mbona uligeuka nilipokuita? Kwa nini unafanya hivyo?”

Yule dada ambaye sasa nilishindwa kumfikiria kuwa ni Aulelia niliyemjua ingawa nilijua fika kuwa ni yeye, alinitazama kwa woga na wasiwasi huku nikiona akilengwa na machozi.

“Mimi ni Aulelia kweli, lakini wewe sikujui! Na naomba usinicheleweshe!” Alinijibu kisha aliondoka kwa mwendo wa haraka akiniacha nikiwa nimepigwa na butwaa.

Hii ni nini tena?

Nilimtazama yule mtu ambaye tulikuwa pamoja kwa muda mwingi wakati tukiwa chuoni na nilishindwa kuelewa ni nini maana ya tukio lile. Na hata pale nilipokuwa nikimkodolea macho, nilimshuhudia akifungua mlango wa gari lake ambalo nililijua fika hadi namba na kuondoka eneo lile kwa kasi, lakini wakati lile gari likinipita, Aulelia alinigeuzia uso wake kunitazama na nikaona alikuwa akibubujikwa na machozi.

Mungu wangu! Martin Lundi amemfikia na yeye!

Niliondoka eneo lile nikiwa nimezidi kuchanganyikiwa huku moyo ukiniuma vibaya sana kutokana na kitendo alichonifanyia Aulelia.

Kwa nini Aulelia, eenh? Why do you have to do this to me?

Sikuwa na shaka kuwa tabia ya Aulelia niliyoishuhudia muda mfupi uliopita ilitokana na yale mambo yaliyonikuta. Lakini Aulelia ni mtu mwenye uelewa wa hali ya juu, si kawaida yake kufanya kitu kama kile bila ya kuwa na uhakika nacho. Nilikuwa na imani kabisa kuwa hata kama angesikia taarifa kuwa nimekuwa kichaa ninayeua watu ovyo, Aulelia angetaka kuongea na mimi na kuelewa ni yepi hasa yaliyonisibu na kujihakikishia mwenyewe kuwa kweli nimekuwa mwehu, badala ya kunikana moja kwa moja kwa maneno ya kuambiwa tu au ya kusoma magazetini. Lazima kuna kitu zaidi.

Kitu gani?

Sikuwa na la kufanya zaidi ya kurejea kwenye eneo langu la maficho kule Kigamboni. Siku yangu ilikuwa imepotea bila mafanikio yoyote.

--

Safari yangu kurudi kwenye ile nyumba ya wageni kule Kigamboni ilikuwa kama ndoto. Sikumbuki chochote kilichotokea humo njiani, ila nilijikuta tu nimefika na kupitiliza moja kwa moja chumbani kwangu na kujifungia.

Usiku ule nilisumbuliwa zaidi na mawazo juu ya tabia aliyoonesha rafiki yangu kipenzi Aulelia Mushi nilipokutana naye pale mjini. Sikuwa na shaka hata kidogo kuwa yule ni yeye, kwani hata gari aliloondoka nalo lilikuwa ni lile ambalo mimi nililijua siku zote kuwa ni lake, hata namba za lile gari ni zile zile za gari lake.

Nikiwa nimejilaza kitandani nikiwaza juu ya mambo haya, nilisikia wahudumu wa ile nyumba ya wageni wakifungua chumba kilichokuwa kikitazamana na kile nilichokuwa nimepanga na kumkaribisha mpangaji mpya kwenye chumba hicho. Mawazo yangu yalirudi kwa rafiki yangu Aulelia Mushi.

Kwa nini amefanya vile?

Sikupata jibu la kunitosheleza.Nilibaki na uchungu mkubwa moyoni kwani tukio lile lilinikumbusha kuwa bado nilikuwa mkimbizi nisiye na kimbilio, na kwamba sehemu pekee inayonifaa ni pale nitakapokuwa peke yangu.

Zaidi ya hapo mawazo yangu yalisumbuliwa na tatizo la upungufu wa pesa uliokuwa unaelekea kunikumba. Kwa hali hii nitakimbilia kwa nani anipe pesa? Na bila pesa nilikuwa sina ujanja wa kukabiliana na vitimbi vya akina Martin Lundi muongo. Nitakimbilia kwenye nyumba gani ya wageni au hoteli bila ya pesa?

Hapo niliamini kuwa akina Martin Lundi walikuwa ni watu hatari sana wanaopangilia mambo yao kwa wigo mpana mno, kwani kwa kunichukulia kikadi changu cha benki, walihakikisha kuwa wamenizibia kabisa mianya ya kujipatia pesa na hivyo kuyafanya maisha yangu kuwa magumu sana.

Nilikumbuka maneno ya yule askari wa kike aliyeniibukia kule kwenye nyumba ya wageni maeneo ya Sinza.

…na nakuahidi kuwa tutayafanya maisha yako yawe mabaya sana hapa duniani mpaka utautoa!

Na ilielekea kuwa kweli.

Sijui kwa nini hawakuzichukua na zile pesa taslimu zilizokuwa kwenye begi langu kule msituni, labda kwa kuwa nilikuwa nimezishindilia chini kabisa ndani ya begi lile nao hawakuwa na muda wa kulipekua sana. Au labda hawakutarajia kwamba ningeweza kuwa na pesa kiasi kama kile porini namna ile.

Nilikumbuka kuwa marehemu Ibrahim Geresha alichukua pesa kidogo sana, na sehemu kubwa ya posho yake ya safari alimwachia mkewe kwa matumizi ya familia yake. Sasa mimi sikuwa na familia ya kuiachia pesa, hivyo nikaenda nazo msituni.

Na ndizo zilizonisaidia mpaka kufikia hapa. Ingawa bado nilikuwa nina pesa za kuniwezesha kujikimu kwa siku kadhaa zijazo, niliona ni bora ningeanza kufanya utaratibu wa kutafuta pesa mapema kabla hazijanikaukia kabisa. Niliikumbuka akaunti yangu kule benki. Nilikuwa na zaidi ya Milioni moja na nusu kwenye ile akaunti, lakini ndio sikuwa na namna ya kuzipata bila ya ile kadi yangu ya benki.

Njia ya kujitia kuwa kadi imepotea isingenisaidia kwani utaratibu niliujua wazi. Nilitakiwa nitoe ripoti polisi, nipewe RB ya upotevu wa kitambulisho cha benki, ndipo Benki wangeweza kunipatia kadi nyingine. Kinyume na hapo hakukuwa na namna.

Suala la kwenda polisi kutoa ripoti ya kupoteza kitambulisho cha benki lilikuwa haliwezekani kabisa, kwani huko kulikuwa ni kujipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa Mamba, kwani nisingeweza kwenda polisi kwa jina la Nuru Bint Shaweji.Nilitakiwa niende kwa jina langu halisi, Tigga Mumba, ambalo ndilo lililokuwa kwenye kadi yangu ya Benki na ambalo linatambulika kule benki. Na ambalo kufikia sasa sikuwa na shaka kabisa kuwa lilikuwa maarufu kwenye  vituo vyote vya polisi sio tu jijini, bali pia hata mikoani.

Sasa nifanyeje?

Niliamua kwenda benki siku iliyofuata na kubahatisha kutoa kiasi cha pesa kutoka kwenye akaunti yangu. Namba yangu ya akaunti nilikuwa naikumbuka kwa kichwa, na kulikuwa kuna dada ambaye nilikuwa nimezoeana naye sana pale benki, kwani mara nyingi nikienda kutoa pesa huwa namuachia na yeye bakshishi kidogo, hivyo kila mara niingiapo pale benki huwa akinichangamkia sana.

Nilitaraji kuwa zile bakshishi nilizokuwa nikizitoa kwake huenda zikanisaidia kupata pesa bila kulazimika kutoa kitambulisho changu cha benki.

Baada ya hapo ningemfuatilia rafiki yangu Aulelia Mushi ili nijue kiini cha ile tabia ya ajabu aliyonionesha pale tulipokutana. Huenda ningepata mwanga wa kuniangazia njia ya kunifikisha kwenye ufumbuzi wa mtihani ulionikuta.

Kwa muda ule nilisahau kabisa masuala ya The Rickshaw, The Bastard na TheKey.

 

--

“Eem…Samahani kidogo anti, lakini itabidi nipate kibali cha kukupatia pesa kutoka kwa bosi wangu, si unajua tena…mambo ya procedure?” Yule dada niliyekuwa nimetaraji kuwa angekuwa mwepesi kunielewa pale benki na kunipatia pesa bila usumbufu na vipingamizi aliniambia huku akitabasamu kijinga, uso wake ukionesha wazi kuwa hakuipenda kabisa hali ile.

“Aaah! Ni lazima ufanye hivyo? We’ si unanifahamu Anti? Na hiyo ndiyo akaunti yangu…mi’ nakuja hapa benki mara kibao tu kuchukua pesa kwa hiyo akaunti…” Nilimjibu huku nikianza kujutia uamuzi wangu wa kwenda pale  benki. Nilikuwa nimecheza bahati nasibu mbaya sana kwenda pale , kwani pia ingewezekana hata hapa benki wakawa wana habari zangu na hivyo kunifanya niwe nimejiingiza mwenyewe kwenye mdomo wa Mamba.

Lakini ningeishi vipi bila pesa?

“Akaunti iko sawa kabisa Anti, na mi’ nakujua vizuri na sina shaka na wewe…”

“Sasa tatizo ni nini?” Nilimkatisha kwa swali.

Nilipofika pale benki nilijaza fomu ya kuchukulia pesa na kufoleni kwenye dirisha alilokuwa yule dada niliyemkusudia tangu siku iliyopita. Aliponiuliza juu ya kadi yangu ya benki nilimwambia kuwa nilikuwa nimeisahau nyumbani kwa mama yangu Morogoro nilipoenda likizo na kwamba nilikuwa nimeagiza mtu aniletee, lakini kwa muda ule nilikuwa nina shida kubwa sana ya pesa na hivyo nikamwomba anisaidie.

Aliniuliza kuwa nilikuwa na uhakika kuwa sijaipoteza nami nikamhakikishia kabisa kuwa nilikuwa nimeisahau pamoja na baadhi vitu vyangu kule Morogoro na nimewasiliana nao wakanithibitishia kuwa ipo na italetwa.

Nilimuona akisita huku akijaribu kuamua iwapo adharau taratibu za kazi kwa muda na anisaidie. Niliona wazi kuwa akilini mwake alikuwa akizikumbuka zile bakshishi nilizokuwa nikimkatia kila nilipokuwa nikienda kuchukua pesa pale benki.

“Naomba unisaidie Anti, Please!” Nilimwambia kwa kuomboleza huku moyo ukinidunda.

Yule dada alisita kwa muda. Kisha nilimuona akianza kuigonga muhuri ile fomu yangu nami nikabana pumzi, lakini mara aliingia dada mwingine pale kwenye kaunta ya yule dada.

“Bosi anakuita…sasa hivi!” Alimwambia na kutoka.

Yule dada alinitazama na kutabasamu kisha akaniomba radhi na kuelekea sehemu ya ndani ya ile benki ambapo wateja hatukuweza kuona kilichokuwa kikitendeka. Nilibaki nikisubiri pale kwenye foleni huku moyo ukinienda mbio na wasiwasi ukinipanda. Nilisikia manung’uniko ya wateja waliokuwa nyuma yangu, kwani nilikuwa nimetumia muda mrefu na yule dada pale dirishani, lakini sikujali.

Baada ya muda yule dada aliyekuja kumwita mwenzake alinijia na kuniomba niongozane naye kuelekea sehemu ya ndani alikoelekea yule dada aliyekuwa akinihudumia.

Hapo machale yalinicheza na nikataka kutimua mbio, lakini sikuweza kufanya hivyo kwani mlangoni kulikuwa kuna askari mwenye silaha na zaidi ya hapo watu waliojaa mle ndani wangeweza kunikamata kwa urahisi sana.

“Ku…kuna nini, something wrong?” Nilimuuliza kwa wasiwasi iwapo kulikuwa kuna tatizo lolote huku nikiangaza huku na kule nikijaribu kumtafuta yule dada aliyekuwa akinihudumia hapo mwanzo.

“Hakuna tatizo la kukutisha dada yangu, ni kuweka taratibu sawa tu. Nifuate tafadhali.” Yule dada alinijibu huku akiongoza njia.

Nilihisi mwili ukiniisha nguvu huku kwa mara nyingine nikiujutia uamuzi wangu wa kwenda pale benki. Nilimfuata yule dada huku nikiwa nimeingiwa na woga wa ajabu, akilini mwangu nikijua fika kuwa huko niendako nilikuwa naenda kukutana tena na yule muuaji muongo, Martin Lundi.

Niliingizwa kwenye ofisi moja nzuri sana iliyokuwa nyuma ya ukuta wa zile kaunta za kuhudumia wateja ambamo ndani yake alikuwapo mtu mmoja mrefu na mtanashati sana aliyekuwa ameketi kwenye kiti kizuri sana nyuma ya meza kubwa na safi. Mlangoni mwa ofisi ile kulikuwa kumeandikwa “Branch Manager” nami moja kwa moja nikaelewa kuwa yule ndiye alikuwa meneja wa tawi lile la benki. Ubavuni mwa ile meza ya meneja, nilimuona yule dada aliyekuwa akinihudumia pale kaunta akiwa amesimama  huku ameinamisha uso.

Mnh!

Baada ya kunifikisha ndani ya ile ofisi yule dada aliyenileta aliondoka na kuniacha pamoja na wale niliowakuta mle ndani.

Nilibaki nikiwa nimesimama kizembe nikisubiri maelekezo, lakini yule bwana tuliyemkuta mle ndani alikuwa akinitazama tu bila ya kusema neno.

Yule dada aliyekuwa akinihudumia pale kaunta alikuwa amesimama kando ya ile meza huku ile fomu yangu niliyoijaza ilikuwa juu ya meza ya meneja wa tawi.

Kibao kidogo kilichokuwa juu ya meza ile kilimtambulisha yule bwana kama Dick Bwasha. Nilipotembeza macho mle ndani, niligundua kuwa kulia kwa meza ya yule meneja wa tawi, kulikuwa kuna vijiruninga vidogo ambavyo vilimwezesha kuona kila kilichokuwa kikitendeka kule kwenye kaunta za kuhudumia wateja. Nilimgeukia yule dada aliyekuwa akinihudumia pale kaunta na nikaona alikuwa amebadilika na uso umemsawajika vibaya sana. Alikuwa ametishika vibaya sana, nami nikaanza kugwaya nisijue nitafanyaje. Muda huo yule bwana alimwashiria yule dada atoke nje ya ile ofisi. Dada aliondoka haraka akiniacha peke yangu na yule mtu mle ndani.

Hatimaye yule meneja wa tawi aliniashiria niketi kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake nami nikatii.

“Ulikuwa unataka kumfukuzisha kazi yule binti bila ya sababu. Ukisahau kitambulisho chako cha benki unatakiwa urudi ukakifuate ndio uje benki kutoa pesa. Na ukikipoteza, unatoa ripoti polisi, unapewa RB, unakuja hapa, unatengenezewa kadi nyingine kisha unachukua pesa. Huo ndo utaratibu.” Dick Bwasha akiniambia huku akiwa ameninyanyulia nyusi na akinitazama usoni.

Uso wake ulikuwa umejaa jeuri na kila alipoongea alibetua midomo yake kana kwamba anayehisi  kichefuchefu. Hii iliutia dosari kubwa utanashati wake. Nilibaki nikimkodolea macho kwa muda kabla sijapata neno la kusema.

“Lakini nilikuwa nimeomba msaada tu! Nina shida sana ya pesa na kitambulisho nimekisahau nje ya mkoa, nisingeweza kurudi kukifuata mkoani wakati nimeshikwa na shida ya dharura.” Nilimjibu huku nikizidi kupata hofu ya kuendelea kubaki na yule mtu mwenye majivuno na kiburi kikubwa kabisa ndani ya chumba kile.

“Hilo halitawezekana!” Alinijibu kwa mkato huku akinibetulia midomo yake mibaya na kuniinulia nyusi zake nene kwa kiburi cha hali ya juu.

Nilimtazama kwa muda huku hasira zikinipanda.

Kwani imekuwaje? Mimi sikuona kama lile lilikuwa ni suala kubwa sana kiasi cha kuanza kujibizana na meneja wa tawi.

“Lakini kuna pesa zangu kwenye benki yako! Zaidi ya milioni na nusu, sasa unataka kuniambia kuwa siwezi kuchukua kilicho changu kwa vile tu…”

“Sio kwa utaratibu uliotaka kuutumia. Sisi tuna taratibu zetu bwana!”

“Sasa kwa nini umeagiza niletwe huku ofisini kwako? Kwa sababu nilitaraji nimeletwa huku ili nipate msaada ambao labda wale wahudumu wa kule kaunta hawana mamlaka nao!” Nilimjibu kwa swali la mshangao.

Yule bwana alinitazama kwa kiburi huku akitafuna tafuna kalamu yake na domo lake likifanya tabasamu la kuchukiza.

“Unataka msaada?” Aliniuliza huku akiendelea kutafunatafuna kalamu yake na akinitazama kwa macho ya matamanio, na kuendelea; “Itabidi nawe ukubali kusaidia.”

Alinichefua!

Yaani huyu bwana alikuwa anataka kutumia nafasi hii kuniletea mzuka wake wa ngono!

“Sikiliza Mista, nilitegemea tatizo langu lingeeleweka na kupatiwa ufumbuzi kwa taratibu zinazoeleweka. Sioni sababu ya kujirahisisha kwako kwa pesa yangu mwenyewe bwana! Kama we’ una mzuka wa ngono si ukatafute machangudoa waliojaa tele huko mitaani!” Nilimkemea kwa hasira, wakati yeye akinitazama tu huku akiendelea kunichekea, akitafuna tafuna kalamu yake.

Nilizidi kuchukia.

“Na nitahakikisha kuwa naifunga akaunti yangu na nahamia benki nyingine! Benki gani inakuwa na watendaji wasio na adabu hata kidogo!” Nilimwambia kwa ghadhabu.

“Mnnhu! Mi’ n’lidhani utaenda polisi kupeleka mashitaka ya unyanyasaji wa kijinsia!” Dick Bwasha aliniambia kwa kebehi huku akinitazama machoni ilhali sura yake ikiendeleza lile cheko lake la kebehi, na aliposema vile, alitilia msisitizo sana neno ‘polisi’.

Sikumuelewa.Tulibaki tukitazamana kwa muda, kisha nikaamua kuondoka. Nilipeleka mkono wangu kwa nia ya kuinyakua ile fomu yangu ya kuchukulia pesa iliyokuwa pale mezani huku nikiinuka. Lakini mkono wa Dick Bwasha ulichomoka ghafla na kuukamata mkono wangu, akinizuia nisiichukue ile fomu. Niliruka kwa mshituko huku nikiachia yowe la woga.

“Not so fast young lady!” Dick Bwasha alinikemea akimaanisha kuwa nisifanye haraka kuondoka, huku naye akisimama kutoka kwenye kiti chake na kunikunjia sura yake kwa ghadhabu, lile cheko lake la kejeli na mchezo-mchezo likiyeyuka kabisa usoni mwake.

“Hey! Niachie!” Nilimwambia kwa hasira huku nikijaribu kuunasua mkono wangu kutoka himayani  mwake. Dick Bwasha aliizunguka ile meza kwa wepesi wa ajabu na kuja hadi pale kwenye kiti nilichokuwa nimekalia hapo awali na kunikalisha huku akiniinamia na kunisemea karibu sana na sikio langu.

“Unataka msaada, n’takusaidia. Lakini na wewe lazima ukubali kunisaidia bibie, unasemaje?”

Mwili ulinifa ganzi. Huyu bwana ana wazimu au kitu gani?

Mista, mimi ni mtu mwenye heshima zangu. Naomba huo upuuzi wako uupeleke kwa wanaoweza kuuvumilia lakini sio kwangu! Naomba niende zangu.” Nilisema kwa utulivu wa hali ya juu huku nikitafuta kitu cha kumbamiza nacho ili niweze kutoka salama mle ndani. Nimekuja kujaribu kuchukua pesa kutoka kwenye akaunti yangu ili niweze kukabiliana na matatizo yangu, badala yake nakutana na mjinga mwenye mawazo ya ngono za kibeberu.

Haya mambo gani sasa!

Dick Bwasha alirudi nyuma ya meza yake na kutoa picha kutoka kwenye droo ya meza ile na kuitupia mbele yangu pale juu ya meza.

“Ukiitazama hiyo picha utagundua kuwa sina shida kabisa na hicho ki**** chako mwanamke!” Aliniambia taratibu huku akinitazama kwa ghadhabu, akizitamka nyeti zangu kama anayetamka takataka fulani tu hivi.

Sikuamini macho yangu.

Niliitazama ile picha bila kuishika, ikiwa imelala pale mezani na nilihisi kudharaulika na kudhalilika kusiko kifani. Ile picha ilimuonesha Dick Bwasha akiwa uchi wa mnyama juu ya kitanda. Pamoja naye, ilikuwapo mijimama miwili ambayo nayo ilikuwa kama ilivyozaliwa, hakukuwa na shaka kabisa na walichokuwa wanakifanya pale kitandani. Ilikuwa ni picha chafu sana na sikuelewa wale watu waliwezaje kupiga picha kama ile bila ya kuwa na wazimu kidogo. Na pia nilishindwa kabisa kumuelewa yule meneja wa tawi la ile benki niliyoiamini kunitunzia pesa zangu miaka yote ile.

“Kha! Sasa hii ndio nini?” Niliinua uso kwa mshangao na kumuuliza , huku akilini mwangu nikijithibitishia kuwa jamaa hakuwa mzima.

“Hiyo ni kukuonesha ni jinsi gani mawazo yako yalivyo potofu. Niliposema na wewe inabidi unisaidie sikuwa na maana hiyo iliyojengeka kichwani mwako!” Aliniambia huku akibenua midomo yake kwa kiburi kikubwa kabisa.

Kwa kweli alinichosha!

“Sasa…” Nilianza kumuuliza, lakini Dick Bwasha alipiga meza kwa nguvu kwa kiganja chake na kunikatisha.

“We want the tape Tigga!” Aliniambia kwa sauti ya msisitizo huku akiinua mwili wake na kunisogezea uso wake karibu sana na wangu, akinitazama kwa macho makali yenye kuogofya, akimaanisha kuwa wanautaka ule mkanda wa video niliokuwa nao.

Duh! Hii sikuitegemea kabisa, na mshituko nilioupata naona ulikuwa mkubwa kuliko yote niliyowahi kukutana nayo tangu kinyang’anyiro hiki kinikute.

Say whaaat!” Niliruka kwa mshituko huku nikiinuka kutoka kwenye kiti nilichokuwa nimekalia na kubaki nikiwa nimemkodolea macho yule mtu aliyekuwa mbele yangu huku nikishindwa kabisa kuuzuia mwili wangu usitetemeke.

Dick Bwasha aliendelea kunitazama kwa hasira bila kutetereka.

You give us the tape, we give your money back…and more.” Dick Bwasha aliongea taratibu huku akiendelea kunitazama, akimaanisha kuwa wataniruhusu kuchukua pesa zangu na kuniongeza za ziada, iwapo nitawapatia ule mkanda wa video wenye ushahidi dhidi ya akina Martin Lundi.

Niliinua mkono uliokuwa ukitetemeka na kumnyooshea kidole huku macho yakiwa yamenitoka pima.

“We…wewe…ni mmoja wao!” Nilisema kwa kitetemeshi.

Dick Bwasha hakunijibu, badala yake aliketi vizuri kwenye kiti chake na kuirudisha ile picha yake chafu kwenye droo ya meza yake.

“Mmoja wa akina nani Tigga?” Aliniuliza huku akiendelea kunitazama kwa makini. Sikuweza kumjibu. Nilibaki nikimkodolea macho kwa kihoro.

Yaani hawa akina Martin Lundi ndio wametanda kila mahali namna hi?

Inawezekana vipi hii lakini? Huyu mtu anahusikaje na suala zima la kule msituni? Mungu wangu! Sasa nitapambana na watu wangapi Tigga mie?

“Tunautaka huo mkanda Tigga, na tutakupa pesa zote uzitakazo.” Dick Bwasha alinizindua kutoka kwenye yale mawazo ya kuijutia nafsi yangu.

“Halafu hizo pesa nikazitumie ahera? Nyie si wauaji tu! Sina mkanda mie!” Nilimropokea kwa jazba huku nikianza kusota ukutani kuuelekea mlango. Dick Bwasha aliendelea kuketi tu kwenye kiti chake bila hata kutetereka.

“Huwezi kutukimbia Tigga. Bora ukubali ofa hii. Tulijua tu kuwa utakuja hapa, nami nilikuwa nakusubiri muda wote. Toa mkanda huo halafu tutakusahau na hutatuona tena.”

Ooh, Yeah? Sitawaona tena kwa sababu nitakuwa mfu sio?”

“Tukitaka kukuua Tigga tunakuua tu, wala hilo sio tatizo kwetu lakini hilo si lengo letu…”

“Nyinyi ni akina nani? Mna lengo gani na nchi hii? Maana mnachokifanya kinaelekea kuathiri taifa zima sasa! Haiwezekani muwepo katika kila nyanja muhimu kama hizi halafu muwe na sera kama hizo….”

“Sio suala la nchi hili mwanamke!” Dick Bwasha alifoka kwa hasira kali kuliko nilivyotarajia, na akabaki akinitazama kwa hasira huku akihema kwa nguvu, kisha akaendelea; “Ni suala dogo tu la mkanda wa video Tigga, sasa sijui kwa nini unataka kulikuza bila sababu!”

“Khah! Hilo suala dogo limeacha watu wameuawa kama kuku kwenye msituni fulani ndani ya nchi hii, huku mimi nikitangaziwa wazimu!”

“Wewe ni mgonjwa wa akili ati, Tigga… lazima ukubali hilo. Kuung’ang’ania kwako huo mkanda wa video ni sawa na kichaa kung’ang’ania bunduki. Ataua kila mtu, ndio maana sisi tunataka kukusaidia…”

Nilibaki nikimkodolea macho kwa mshangao. Hivi hawa jamaa ni kweli wanaamini kuwa mimi ni mwehu? Nilitaka kusema neno nikaghairi, sikuona sababu ya kuendelea kubishana na yule adui juu ya jambo lile.

“Siwezi kuendelea kusikiliza upuuzi huu. Mi’ naondoka, fanya utakalo!” Nilimwambia huku nikiuendea mlango kwa hatua za haraka.

“Nenda tu Tigga, na wala sitakuzuia. Lakini ujue kuwa tutayafanya maisha yako yawe magumu sana kiasi utajuta kwa ubishi wako!” Dick Bwasha aliniambia huku akinitazama kwa hasira.

Nilitoka nje ya ofisi yake na kupitiliza hadi pale kaunta ambako nilikuta watu wachache wakiwa wamepanga foleni wakiendelea kupata huduma kama kawaida, bila ya kujua mambo yaliyokuwa yakitokea nyuma ya zile kaunta, wala undani wa watendaji wakuu wa benki ile.

Ni wapi ambapo hawa watu hawapo?

Nilitoka nje ya ile benki nikipepesuka huku akili ikinizunguka. Nilivuka barabara bila ya kuangalia na nikashtukia nikipigiwa honi huku nikisikia msuguano wa matairi ya gari lamini. Niliruka kwa mshituko huku nikikoswakoswa kugongwa na gari lililokuwa linakuja kwa kasi. Nilichanganyikiwa nakurudi mbio kule nilipotokea, kumbe nako kulikuwa kuna gari lingine linakuja, nalo likanipigia honi kubwa huku likiserereka na kunikwepa.

Anti umepewa talaka nini?” Dereva wa lile gari la pili alitoa uso nje ya dirisha lake na kunipigia kelele kwa hasira,kisha akamalizia na tusi zito la nguoni.

Nilisikia kelele na mayowe ya watu wakizomea, lakini sikujali.

Nilizidi kuongeza mwendo, ingawa kwa wakati ule sikujua nilikuwa naenda wapi. Nilikuwa nimechanganyikiwa vibaya sana, na nilijiona kuwa sasa nilikuwa naelekea kabisa kwenye wazimu.

Nilipopata fahamu kidogo niligundua kuwa nilikuwa nimeshika usawa wa kuelekea kituo cha mabasi ya Kivukoni.

Hatua chache kutoka kwenye ile nyumba ya wageni niliyokuwa nimepanga kule Kigamboni nilipata na mshituko mwingine ambao sikuutegemea, baada ya kile kisanga cha kule benki kilichonivuruga akili.

Nikiwa kimya ndani ya teksi niliyokodi baada ya kuteremka kwenye pantoni nilimuona mwanamke akitoka kwenye ile nyumba ya wageni na kuliendea gari lililokuwa limeegeshwa upande wa pili wa barabara nje ya nyumba ile, na moyo ulinilipuka.Nilijikuta nikiketi wima kwenye kiti cha gari lile na kumtazama kwa makini wakati ile teksi niliyokuwamo ikizidi kulikaribia lile gari aliloliendea yule mwanamke.

Moyo ukinipiga nilimtazama kwa makini yule mwanamke kutokea nyuma ya miwani yangu myeusi.Alikuwa ni yule askari wa kike aliyeniachia kule kwenye nyumba ya wageni ya Sinza nilipokimbilia baada ya vurumai iliyotokea nyumbani kwa Kelvin!

Kihoro kilichoanza kutulia baada ya mshituko nilioupata kule benki kilinirudia upya, tena kwa kishindo kikubwa.Mwili uliingia baridi na nikahisi nikishindwa kupumua vizuri. Nilibaki nikimkodolea macho yule mwanadada.Safari hii alikuwa amevaa mavazi ya kiraia na alikuwa akiongea na mtu aliyekuwa ndani ya lile gari lililokuwa limepaki mbele ya ile nyumba ya wageni, upande wa pili wa barabara. Dereva wangu alianza kupunguza mwendo kwani tulikuwa tumeifikia kabisa ile nyumba ya wageni  niliyomwelekeza anipeleke.

“Twende mbele tu! Usisimame hapa!” Niliropoka kwa hofu huku nikijishughulisha kutoa pesa kwenye mfuko wa suruali yangu.

“Lakini Anti, gesti si hii hapa?” Yule dereva aliniuliza kwa mshangao.

“Endesha bwana! Naenda…naenda saluni kwanza…kule mbele!” Nilimfokea kwa kuchanganyikiwa, naye aliipita ile nyumba ya wageni kwa mwendo ule ule wa taratibu huku akinigeukia kwa mshangao. Nilijitia kuangusha baadhi ya sarafu na kuinama kuziokota huku nikilaani kitendo kile, lakini nia yangu hasa ilikuwa ni kuinama ili yule mwanamke asinione wakati gari letu likipita pale walipokuwa wamesimama.

Nikiwa ndani ya ile teksi niligeuka na kupitia kwenye kioo cha nyuma cha ile teksi nilimuona yule mwanamke akiingia ndani ya lile gari,ambalo  liliondoka eneo lile kwa mwendo wa kasi.

Shit!” Nililaani kitendo cha wale wauaji kugundua maficho yangu nikiwa nimechanganyikiwa na kugeukia  kule tulipokuwa tukielekea.

“Sasa nini tena Anti? Mbona hivyo?” Yule dereva alilalamika huku akinitazama kwa mshangao, akidhani nilikuwa nimemlaani yeye.

Nilimtaka radhi kuwa si yeye niliyemkusudia na kumwambia aniteremshe mbele ya saluni moja ya akina mama, jambo ambalo alilifanya kwa faraja kubwa, kwani bila shaka alishaniona kuwa ni mteja mkorofi.

“Heh! Sasa nitakimbilia wapi mimi?” Nilijisemea mwenyewe huku nikizubaa nje ya ile saluni, kishanikaelekea kwenye kioski kimoja kilichokuwa jirani yake na kuketi, nikiiangalia ile teksi ikitoweka.

Bila shaka utakuwa na hisia ni jinsi gani nilivyochanganyikiwa. Yaani baada ya msukosuko wa kule benki na vituko na vitisho vya yule mtu aliyeitwa Dick Bwasha, halafu nafika hapa kwenye maficho yangu nakuta kuwa kumbe yule mwanamke aliyeahidi kuyafanya maisha yangu yawe mabaya kabisa hapa duniani naye alikuwa amekwisha fika.

Ni wazi kuwa wale wauaji walifika pale kwenye ile nyumba ya wageni kunifuata mimi wakanikosa, sasa je, wameacha ujumbe gani pale kwenye ile nyumba ya wageni? Jambo la busara kuliko yote kwangu wakati ule lilikuwa ni kutokomea moja kwa moja, nisirudi tena kwenye ile nyumba ya wageni, kwani haikuwa salama tena kwangu, lakini nitafanyaje? Kulikuwa kuna vitu vyangu ndani ya ile nyumba ya wageni ambavyo nisingeweza kuondoka bila kuvichukua.

Hususan ule mkanda wa video.

Nilijua kuwa ilinilazimu kurudi  tu mule ndani, nikajionee mwenyewe kilichoandaliwa kwa ajili yangu na wale wauaji wabaya.

Hata hivyo, niliendelea kukaa kwa muda mrefu pale kwenye kioski nikitaraji kupata uamuzi mwingine tofauti na ule, lakini kila nilivyotafakari, pamoja na woga ulionikumba baada ya kumuona yule askari mbaya nje ya ile nyumba ya wageni, sikupata wazo lolote zuri zaidi ya kwenda tu kwenye ile nyumba ya wageni na kukusanya vitu vyangu ndio niondoke.

Iwapo nitakuta kuwa yule askari wa kike anayeshirikiana na akina Martin Lundi ameacha wenzake wanisubiri, basi nitapambana nao huko huko. Si nilishaamua kuwa muda wa kuanza kuwawinda ulikuwa umefika? Sasa hii ndiyo ilikuwa nafasi yangu. Nilijipa moyo huku nikiuona kabisa ujasiri ukinipungua kwa kasi, kwani kasi ya maadui zangu kunizidi kete ilikuwa ni kubwa mno.

Kwanza Dick Bwasha, halafu yule mwanadada askari…kisha nani tena? (Niliguna).

Nililipia soda niliyoagiza na kuondoka kuelekea kwenye ile nyumba ya wageni huku nikiomba Mungu anijaalie uwezo wa kukabiliana na mambo nitakayokutana nayo.

 

--

Niliingia ndani ya ile nyumba ya wageni nikiwa na wasiwasi mkubwa. Nilichukua ufunguo wangu pale kaunta nikitarajia kusikia ujumbe wowote wa ajabu ajabu kutoka kwa yule mhudumu lakini haikuwa hivyo. Nilianza kuelekea chumbani kwangu taratibu, kisha nikarudi na kumuuliza yule mhudumu.

“Nilimuona dada mmoja akitoka huku ndani muda mfupi uliopita…ni nani yule?”

“Dada mmoja makini hivi mwenye shepu moja bomba sana?” Yule mhudumu aliniuliza, akielezea maumbile ya yule mwanadada. Nilimwambia ndio huyo huyo huku nikikumbuka jinsi hata mimi nilivyoisifia shepu yake siku ile aliponiibukia kule Sinza akiwa amevaa mavazi yake ya kiaskari.

“Yule ni mpangaji mpya, ameingia jana usiku… yuko na buzi lake chumba namba 16.” Yule mhudumu alinijibu bila ya kuonesha kutiwa wasiwasi na maswali yangu juu ya yule mwanadada.

“Aaanh! Okay…” Nilimjibu huku nikigeuza na kuanza kuelekea chumbani kwangu hali uso wangu ukiwa umejikunja kwa kuitafakari taarifa ile, kwani chumba namba 16 kilikuwa kinatazamana na chumba changu.

Nilikumbuka kuwa usiku uliopita niliwasikia wahudumu wa ile nyumba ya wageni wakimkaribisha kwenye kile chumba yule ‘mpangaji’ mpya, wakati nikiwa nimezongwa na mawazo juu ya kitendo cha rafiki yangu Aulelia Mushi kunikana waziwazi hadharani na tatizo la pesa lililokuwa likielekea kunikabili.

…ameingia jana usiku, yuko na buzi lake chumba namba 16.

Yaani kumbe nilikuwa nimelala nyumba moja na adui yangu!

Moja kwa moja nilijua kuwa wale watu watakuwa walinifuata nikitokea mjini siku iliyopita, kwani baada ya kuchanganywa na tabia ya Aulelia, sikuwa makini kabisa wakati narudi huku mafichoni kwangu. Hivyo iliwezekana sana wao kunifuatilia bila ya mimi kujua.

Shit!

Nilifungua chumba changu nikiwa bado nimezongwa na wazo la kuwa wale watu wangeweza kunivamia usiku ule mle ndani na nisingekuwa na njia yoyote ya kujiokoa kwani sikuwa nimejiandaa kwa lolote, nikiwa na imani kabisa kuwa hakukuwa na mtu yeyote aliyeyajua yale maficho yangu.. Nilisukuma mlango lakini nilipoanza kuingia chumbani tu nilisimama ghafla huku nikiachia mguno wa fadhaa.

Niliingia na kusimama hatua chache ndani ya chumba kile, nikiistajabia hali niliyokuta.

Chumba changu kilikuwa kimechakuriwa vibaya sana. Yaani ilikuwa ni kazi ya haraka na isiyojali mpangilio uliokuwamo mle ndani kabla. Mashuka yote yalikuwa yametolewa kitandani na kutupwa chini kwenye zulia. Makochi yalikuwa yamepinduliwa juu chini na kuraruriwa kwa ghadhabu, mito na godoro vilikuwa vimechanwa kwa kisu au wembe mkali sana.

Kabati la nguo lilikuwa limefunguliwa na kuachwa wazi. Meza ndogo iliyokuwamo mle ndani ilikuwa imelalia ubavu kwenye kona moja ya kile chumba, madaftari na makaratasi yangu vikiwa vimesambaratishwa ovyo sakafuni, hali zulia likiwa limefunuliwa baadhi ya sehemu na kuachwa likiwa limekunjamana vibaya.

Mabegi yangu yalikuwa yamepekuliwa kwa umakini wa hali ya juu na nguo zangu zilikuwa zimetawanywa huku na huko mle ndani.

Niliitazama ile hali, na kutokana na mtawanyo ule wa vitu mle ndani, niliweza kuziona hasira za wale waliokuwa wakiifanya ile kazi, na nikapata hisia ya hali ambavyo ingekuwa iwapo wangenikuta mimi mwenyewe mle ndani.

Nilibaki nikiwa nimeduwaa huku hasira zikinipanda, kwani hakuna kitu kilichonikera kama mtu kuchezea nguo zangu za ndani. Na pale nilipokuwa nimesimama, niliziona nguo zangu za ndani zikiwa zimetupwa tupwa ovyo na hata zile pedi zangu za hedhi zikiwa zimechanwa chanwa kwa visu au viwembe na kutawanywa vibaya mle ndani.

Nikiilazimisha akili yangu ifanye kazi inavyotakiwa, nilianza kuisaka kamera yangu ambayo nilipoondoka niliiacha ndani ya kile kibegi changu kidogo, ambacho nilikitumbukiza ndani ya lile begi langu lingine kubwa kidogo nililonunua wakati nilipotia mguu wangu kwa mara ya kwanza pale Kigamboni.

Niliikuta chini ya kitanda, huku ile sehemu ya kuwekea mkanda ikiwa wazi.

Mkanda haukuwemo.

Nilitoka mbio na kuwaita wahudumu wa ile nyumba na kuwaonesha kituko kile, nikitaka kujua ni nani aliyehusika na kitendo kile.Kilichofuatia hapo ni vurumai ya hali ya juu.Kila mhudumu akidai kuwa yeye hakuhusika na tukio lile. Waliuliza iwapo wakaite polisi, nikawauliza kuwa wanataka hao polisi waje wamkamate nani kati yao, na wote wakagwaya.

Nilimuuliza yule mfagizi wa siku ile iwapo alipoingia kufagia chumba changu alikikuta katika hali ile, naye akaeleza kuwa hakikuwa kwenye hali ile na alikisafisha na kutandika kama kawaida kisha akakifunga, wakati huo mimi nilikuwa nimeshatoka.

“Ina maana hamkusikia kelele au vishindo vyovyote kutokea humu ndani?” Niliuliza kwa mshangao huku akili ikinichemka.

Walinijibu kuwa hawakusikia chochote, na kwamba mara nyingi muda wa katikati ya asubuhi wakishafanya usafi wao huwa wanakaa upande wa mbele wa ile nyumba, hivyo inawezekana kabisa wasisikie lolote lilikuwa likitokea kule vyumbani.

Niliwauliza iwapo waliwaona wale wapangaji wa chumba namba 16 wakitoka nje muda wowote katika siku ile baada ya mimi kutoka. Wakanijibu kuwa kwa mara ya kwanza wapangaji wa chumba namba 16 walitoka nje ya chumba chao muda mfupi kabla ya mimi kurejea, na kwamba hata usafi chumbani kwao hawakutaka ufanyike, wakidai kuwa walikuwa wanalala na chumba hakikuwa kichafu.

“Walipotoka muda mfupi uliopita, waliwaaga kuwa ndio wanaondoka moja kwa moja au walisema watarudi?” Niliwauliza, nao wakanijibu kuwa walikuwa wamelipia kwa muda wa siku mbili na kwamba walisema kuwa wangerudi.

Nilijua kuwa wale watu walikuwa ndio wameondoka na hawatarudi, lakini sikuwaambia hilo.

“Kwa hiyo Anti…kuna vitu vimeibiwa?” Mmoja wa wale wahudumu aliniuliza.

“We’ unaonaje, huu si wizi wa wazi huu?” Nilimgeukia kwa hasira na kumuuliza kwa ukali, halafu nikaanza kuokota vitu vyangu huku nikilaani kwa sauti kuwa nilikuwa nimekaa kwenye nyumba ya wageni isiyo na usalama hata kidogo.

Moyoni nilijua kuwa halikuwa kosa lao, kwani nilijua kuwa hata ningekuwa kwenye hoteli gani, au nyumba yoyote nyingine ya wageni, ilikuwa ni suala la wale wabaya wangu kujua nilipo  tu, halafu tukio kama lile lingetokea huko huko. Bahati yao mbaya ni kuwa nilikuwa nimeamua kuja kujificha kwenye nyumba yao ya wageni, na wale wabaya wangu wamenigundua.

Ingawa walijitetea sana kuwa tukio kama lile halijawahi kabisa kutokea pale kwao, lakini niliamua kuzidi kulaumu ili wasizidi kuniuliza maswali zaidi, kwani kama ingewajia akilini kuwa ule haukuwa wizi bali wale watu walikuwa wakitafuta kitu fulani mle ndani mwangu, lazima wangekimbilia kuita polisi, jambo ambalo sikulitaka kabisa kwa sababu zinazoeleweka.

Mmoja wa akina dada wahudumu wa mle ndani alianza kunisaidia, lakini nilimzuia na kuwaomba wote wanipishe mle ndani, nikiwaambia kuwa nilihitaji kuangalia vitu vyangu vizuri ili nijue ni vitu gani hasa vilivyoibwa.

Walitoka huku wakibwabwaja maneno ya kunipa pole na wakiulizana wao kwa wao ni jinsi gani tukio lile liliweza kutokea.

Nilijifungia mle ndani na kuanza kukusanya vitu vyangu haraka haraka, nikijua kuwa muda wowote wale wauaji wangeweza kurudi na kunitembezea ubabe wao, kwani wakishindwa kuupata ule mkanda kwa njia moja, lazima watatumia nyingine. Kufikia sasa vitisho vimeshindwa, ndio kisa wakaamua kutumia njia hii ya wizi, na iwapo na hii haitafanikiwa, basi kwa vyovyote watatumia ubabe.

Baada ya kukusanya nguo na baadhi ya vitu vyangu ambavyo havikuathirika na ule upekuzi ambao kwangu niliuona kuwa ni kuingiliwa undani wangu kusikofaa kabisa, nililifungua tena lile begi langu kubwa na kuweka vitu vyangu vilivyonusurika, nikiitumbukiza na ile kamera ambayo likuwa imevunjika kidogo kwenye pembe yake moja, bila shaka baada ya kupigizwa chini katika ile pekua pekua yao, nikijua kuwa kama si kile chumba kuwa na zulia zito, basi bila shaka ile kamera ingevunjika vibaya sana.

Nilipokamilisha hili nilikimbia upesi kule bafuni na kuchukua mswaki na baadhi ya vipodozi vyangu na nilikuwa narudi tena kwenye kile chumba changu cha kulala wakati niliposikia simu ikiita.

Nilipagawa.

Sikuwa na simu na muda wote katika kuokota vitu vyangu mle ndani sikuona kuwa kulikuwa kuna simu.

Hii ni nini sasa?

Nilianza kuisaka ile simu nikifuatilia sauti ilipokuwa ikitokea huku moyo ukinipiga na akili ikinitembea kwa kasi sana.

Ilikuwaje hata kukawa kuna simu mle ndani? Ni kwamba imesahauliwa na wale wavamizi walioondoka muda si mrefu, au wameiacha makusudi ili wanipigie wakitaka kuongea na mimi? Na kama ni hivyo, ina maana walijua kuwa hivi sasa nilikuwamo mle ndani? Au walikuwa wanabahatisha tu?

Niliikuta simu kwenye ua la plastiki lililokuwa limesimamishwa kwenye kona moja ya kile chumba  kama sehemu ya mapambo, ambapo simu ile iliwekwa kwenye kopo maalum lililobeba lile ua.

Nilipotoka mle ndani asubuhi ile, lile ua lilikuwa juu ya meza ndogo iliyokuwamo mle ndani, sehemu ambayo lilikuwa likiwekwa siku zote tangu nianze kuishi ndani ya chumba kile.

Ilikuwa ni ile simu yangu iliyotoweka kule msituni!

Niliichukua kwa mikono iliyojaa kitetemeshi na kuangalia namba iliyokuwa ikinipigia.Hakukuwa na namba yoyote iliyoonekana kwenye ile simu zaidi ya neno ‘Private Number Calling’.

Huyu ni nani?

Nilizidi kuitazama ile simu kwa mshangao huku moyo ukinipiga kwa nguvu, nikijishauri iwapo niipokee ile simu au vinginevyo.

Vipi iwapo ile simu ilikuwa imepigwa na wale wauaji wakinitegea niipokee ili watajue kuwa nipo mle ndani waje kunivamia?

Au ni kweli kuwa wameisahau, na huyo alikuwa ni mwenzao akijaribu kuwasiliana nao? Kama ni hivi, basi labda nikiipokea angalau nitaweza kuongea na mmoja wa wabaya wangu na labda nitaweza kumlaghai kuwa mimi ni yule askari wa kike na kuweza kujua sehemu ya mikakati yao.

Lakini ni kweli ile simu ilikuwa imesahauliwa?

Kwa nini itokee leo ghafla tu baada ya kupotea muda wote huo?

Hapana,haikuwa imesahauliwa.

Niliona wazi kuwa ile simu ilikuwa imewekwa pale makusudi, kama jinsi lile ua lilivyosogezwa kusudi kwenye kona ya chumba kile na si kwa bahati mbaya; kwani kwa uharibifu uliofanywa mle ndani, ningetarajia na lile ua nalo liwe limesambaratishwa vibaya sana.

Niliitupia kitandani ile simu na muda huohuo ikaacha kuita.

Haraka niliinua ile meza iliyokuwa imelalia ubavu mle ndani na kuisimamisha usawa wa feni kubwa lililokuwa likining’inia kwenye dari la mle ndani. Nilikimbilia kule lilipokuwapo kabati la nguo, lakini nilijikwaa kwenye mabegi yangu na kupiga mweleka mzito mle ndani. Nilitoa tusi kubwa na kuinuka, nikachomoa droo ya kabati lile na wakati huohuo ile simu ikaanza kuita tena.

Nilirudi na lile droo kubwa la kabati na kulilaza juu ya ile meza. Niliparamia na kusimama juu ya ile droo iliyokuwa juu ya ile meza na kupeleka mikono yangu kwenye moja ya mapanga matatu ya ile feni na kuipapasa sehemu ya mgongo wake iliyokuwa imeelekea kwenye dari.

Hamna kitu.

Niliizungusha kidogo ile feni na kupapasa pangaboi lingine. Nako hali ikawa kama ile ya mwanzo na nikahisi kitu kikiuchoma moyo wangu na hofu ikanijaa.

Niliizungusha tena ile feni na kukamata pangaboi la tatu na kuupapasa mgongo wake taratibu.

Vidole vyangu vilipapasa kitu nilichokitarajia.

Huku nikishusha pumzi ya faraja, niliushika ule mkanda mdogo wa video uliokuwa umeshikiliwa kwenye mgongo wa lile pangaboi kwa utepe wa gundi na kuibandua kutoka kwenye lile pangaboi.

Niliteremka na kuuweka ule mkanda ndani ya sidiria yangu, nikanyakua begi langu na kutoka haraka nje ya chumba kile nikiiacha ile simu ikiendelea kuita.

SEHEMU YA SABA:

Koku alinijia juu vibaya sana.

Aliponiona tu nikiingia ofisini kwake pale kwenye hospitali ya wilaya ya Temeke, aliangaza macho huku na huko, kisha akainuka na kulinyakua koti jeupe la manesi lililokuwa likining’inia nyuma ya mlango.

Alinitupia lile koti huku akiwa amekunja uso kwa hasira.

“Vaa hilo koti, upesi!” Aliniambia huku akiwa amekasirika.

Nilishangaa huku nikifanya kama alivyoniagiza, wakati yeye akiukwapua mtandio mweusi niliokuwa nimejitanda kichwani mwangu, kabla ya kunishika mkono na kuniongozea maeneo ya vyoo vya wanawake.

Niliacha aniongoze namna ile, sote tukiwa tumevaa yale makoti meupe yalituyofika hadi chini kidogo ya magoti, mimi bado nikiwa na ile miwani yangu ya jua usoni.

Aliniingiza kwenye chumba kimoja kidogo kilichokuwa kando ya vyoo vya wanawake ambacho baadaye nilielewa kuwa kilikuwa kinatumika na manesi wa kike kubadilishia nguo.

Akakomea mlango wa chumba kile kwa ndani na kunigeukia kwa hasira.

What’s the matter with you Tigga, eenh? Kwa nini umekuja hapa? Hujui kuwa unajihatarishia maisha yako! Mi’ n’lidhani wewe ni smart kumbe bwege namna hii? Umekuja kufanya nini hapa? Ondoka! Tena fanya uondoke upesi!” Alinitiririshia makemeo  kwa sauti kali ya kunong’ona huku nikiona kuwa alikuwa amechukia vibaya sana.

Nilibaki nikimkodolea macho dada yangu nisipate la kumweleza kwa wakati ule. Nilipotoka mbio kule Kigamboni, wazo lililonijia ni kwenda moja kwa moja hadi kazini kwa dada yangu. Sijui ni nini hasa kilichonipeleka kule, lakini nadhani nilihitaji sana kuonana na mtu yeyote kutoka kwenye jamii yangu, na sikuweza tena kwenda nyumbani kwa mama yangu.

Pia nilihitaji msaada wa pesa kutoka kwake.

“Nilihitaji kukuona Koku! Nimekutwa na matatizo makubwa na nimekuwa nikikimbia na kujificha peke yangu kwa muda mrefu…”

“Na hilo ndio lilikuwa jambo la busara zaidi kwako!” Koku alinikatisha kwa ukali.

“Najua! Vipi mama, yu hali gani?”

“Ah! Yuko salama.Hajambo. Lakini amelichukulia vibaya sana suala lako.Linamuumiza.”

Nilimtazama dada yangu yule, na machozi yalinilengalenga.Koku alikuwa akijitahidi kujikaza asiangue kilio na alipokuwa akinikemea niliona jinsi midomo ilivyokuwa ikimcheza. Tulibaki tukitazamana, kisha akanivuta na kunikumbatia kwa nguvu.

“Oooh! Tigga, pole sana mdogo wangu. Nimekuwa nikikuogopea sana kwa siku zote hizo ulizokuwa ukihangaika peke yako. Nina hamu sana ya kujua ni kipi kilichokutokea huko porini, lakini hapa mahala si salama kwako.”

“Ina maana unaamini kuwa mimi sio mwehu? Siye niliyeua kule msituni?’ Nilimuuliza huku nikijitoa mikononi mwake na nikijipangusa machozi. Koku alinitazama kwa huzuni kwa muda kabla ya kunijibu.

“Sio siri mdogo wangu, kwanza niliamini kabisa kuwa ulikuwa umefanya hayo mambo ya ajabu. Dr. Lundi ni mtu mwenye uwezo mkubwa sana wa kujieleza na akaaminika.Lakini baadaye nikaja kuelewa kuwa wale si watu wazuri pale walipoanza kunihoji juu yako. Maswali waliyouliza…” Aliniambia na kuiacha sentesi yake ikielea.

“Maswali gani?” Nilimuuliza kwa shauku.

“Ah! Walianza kuuliza maswali ambayo nilidhani wao kama madaktari hawakutakiwa kuuliza. Maswali ambayo yangetakiwa yaulizwe na polisi.Maswali kuhusu mkanda wa video, jinsi nilivyokuelewa tabia zako, marafiki zako…lakini…lakini zaidi ya hapo ni baada ya kuongea na Kelvin…yeye ndiye aliyenihakikishia kuwa wale ni watu wabaya.”

“Kelvin? You spoke to Kelvin?” Nilimuuliza kwa hamasa, nikaendelea, “Yu hali gani sasa?”

“Niliongea naye siku kadhaa baada ya lile tukio la pale nyumbani kwake, na hapo ni baada ya Dr. Lundi kuja kututembelea nyumbani na kutueleza juu ya habari zako. Baadaye nilipata habari za masahibu yaliyomkuta Kelvin na nikaenda kumtembelea hospitali ya Muhimbili. Akanieleza kila kitu, japo kwa taabu….”

“Ameumia sana?”

“Risasi ilimpata kifuani upande wa kulia, ikatokea mgongoni, na ndio salama yake, kwani ingeingilia upande wa kushoto tungezika.” Koku aliniambia lakini bado alionekana kuwa na wasiwasi mkubwa.

“Maskini Kelvin…sasa anaendeleaje?”

“Nilipoenda kumuona alikuwa ana hali mbaya, lakini alijitahidi sana kunielezea yaliyomkuta.Ndipo nilipoelewa kuwa Martin Lundi ni mtu mbaya na kwamba yote aliyotueleza juu yako ni uongo. Siku iliyofuatia tu hali yake ilibadilika ghafla, na sasa yuko chumba cha wagonjwa mahututi na hawezi hata kuongea, ni ajabu kabisa.”

“Ajabu… kivipi?”

“Ah! Nilipoenda kumtembelea kwa mara ya pili alishindwa kabisa kuongea, ila aliniashiria nimpe kalamu na karatasi, na nilipompa, aliniandikia kwa mkono uliotetemeka  sana,  kitu ambacho kilinitisha mno… na ndicho kilichofanya nisiende tena kumwona pale hospitali mpaka leo.” Koku alinieleza kwa kunong’ona nami nilipata msisimko mpya. .

“Alikuandikia nini Koku?” Nilimuuliza huku moyo ukinipiga kwa nguvu.

Dr. Lundi. Ondoka upesi!” Koku alinijibu.

Nilibaki mdomo wazi.

“Yaani hayo ndio maneno aliyokuandikia?” Nilimuuliza.

Koku aliafiki kwa kichwa huku akizidi kuonesha wasiwasi mkubwa.

“Mungu wangu! Ina maana…”

“Nadhani Dr. Lundi alimfanya kitu kibaya Kelvin pale hospitali Tigga. Nadhani kuna sindano au dawa fulani amempa…inamuua Kelvin taratibu Tigga.” Koku aliniambia kwa huzuni kubwa. Nilibaki hoi.

Niliegemea ukuta na kujishika paji la uso. Akilini mwangu nilikumbuka wakati yule mtu aliyejiita Martin Lundi akipokea sindano kutoka kwa mmoja wa vibaraka wake kule ofisini kwamkuu wa wilaya na kujitia kuangalia kiwango cha dawa kilichowekwa ndani ya bomba la ile sindano.

Mungu wangu! Haya ni mambo gani sasa?

Lakini ilileta maana.

Kama Kelvin ataishi na kuelezea juu ya tukio zima la kule nyumbani kwake siku ile, ingenitoa kabisa kwenye hizi shutuma za uongo, na wakati huohuo ingemuweka yule mtu anayejiita Dr. Lundi kwenye  wakati mgumu.

“Kwa hiyo ni nini kilifuatia baada ya hapo?”

“Baada ya hapo ndio sijaenda tena kwa Kelvin, lakini akina Lundi walianza kunifuata fuata sana hadi hapa kazini, wakitaka kujua iwapo niliongea lolote na Kelvin. Nimewaeleza kuwa Kelvin hakuweza kuongea lolote, lakini naona hawakuniamini.” Koku alinijibu.

Hii kali. Sasa na dada yangu tena ametiwa katika mkumbo?

Nilimuuliza iwapo alimwelezea mama juu ya mambo haya.Akaniambia kuwa hakumueleza mama kabisa, kwa sababu mama alionekana kumwamini sana Martin Lundi, hivyo aliamua kumuacha hivyo hivyo.

“Umefanya vizuri sana.”

“Na wewe umefanya kosa kubwa sana kuja hapa. Inabidi uondoke upesi sana.” Koku aliniambia kwa wasiwasi.

“Kwani bado wanaendelea kukufuata mpaka sasa?” Nilimuuliza.

Koku alinishika mabega na kunitazama usoni kwa macho ya kuomboleza.

“Huelewi Tigga. Hawa watu wamo humu hospitalini!

Say Whaat?”Nilimaka.

“Ndio Tigga. Watu wapya wamekuwa wakiletwa hapa ofisini kufanya kazi, na mmoja amewekwa moja kwa moja pale kwenye kitengo changu. Yaani kama leo ungewahi kufika kidogo tu ungemkuta…na sijui ingekuwaje Tigga. Ondoka na usije tena hapa!” Koku aliniambia kwa jazba.

Niliogopa kupita kiasi.

“Sasa…sasa unajuaje kuwa hao watu ni miongoni mwao?” Nilimuuliza.

Koku alitikisa kichwa kwa masikitiko na kukata tamaa.

“Yule mtu sio nesi Tigga. Hajui lolote juu ya unesi.Kazi yake kukaa tu pale na kupokea simu, can you believe that? Jamaa kazi yake ni kupokea simu tu! Sasa pale kwangu ni ofisi ya maopareta pale?” Aliniambia na kuniuliza.

Nilikubaliana naye.Kwa mara nyingine nilikubali kichwani mwangu kuwa hakika ule mtandao wa Dr. Martin Lundi ulikuwa mkali na ulizidi kunizingira. Ilinibidi niondoke pale haraka iwezekanavyo.

“Halafu na polisi nao wakaja na maswali juu yako.” Koku aliendelea kunipasha habari.

Nilimuinulia uso uliojaa maswali huku akili yangu ikienda kwa yule askari wa kike aliyekichambua chumba changu kwa vurugu kubwa kule kwenye ile nyumba ya wageni muda mfupi tu uliopita, akitafuta mkanda wa video wenye ushahidi wa kumuangamiza Martin Lundi na wenzake.

“Na wao wako upande wa Martin Lundi.” Nilijibu kwa masikitiko huku nikitikisa kichwa.

“Hapana. Huyu aliyekuja ni polisi kweli Tigga, tena wa ngazi ya juu tu, kutokana na mavazi yake na jinsi wale askari alioongozana nao walivyoonekana kumgwaya.”

Nikamakinika.

“Yukoje?” Nilimuuliza.

Koku alimuelezea haraka haraka yule askari aliyemjia na maswali juu yangu, na aliposema kuwa alikuwa amekata ndevu zake katika mtindo wa Timberland, nilipata uhakika kuwa alikuwa ni yule askari niliyemtoroka kule ofisini kwangu, katika jumba la makumbusho.

Aliyemuua Macho ya Nyoka.

“Alitaka nini?” Nilimuuliza.

Koku akaniambia kuwa yule askari aliwataka yeye na mama yangu waende kuutambua mwili wa mtu ambaye aliuawa wakati akijaribu kunitorosha mimi kutoka mikononi mwa polisi, akiwataka wamwambie iwapo waliwahi kuniona nikiwa na mtu huyo wakati wowote huko nyuma na katika mazingira gani.

“Mlienda? Mlimuona huyo mtu?” Niliuliza huku moyo ukinipiga sana, nikijua kuwa huyo mtu aliyetakiwa akatambuliwe alikuwa ni yule jambazi niliyempachika jina la Macho ya Nyoka.

“Tulipelekwa mpaka mochwari Muhimbili. Na tukamuona huyo mtu. Ni jambazi hasa, Tigga! Yaani hata katika kifo, unaona kabisa kuwa yule mtu alikuwa muuaji! Yale macho! Mama hakulala.”

“Kwa hiyo mlimuona kwa macho yenu kuwa amekufa?”

“Mimi ni nesi Tigga, na najua mtu akifa anakuwaje. Yule mtu alikuwa amekufa! of course tulimwambia yule askari kuwa hatujawahi kukuona ukiwa na mtu yule hata siku moja, nasi hatukuwa tumepata kumwona yule mtu kabla ya pale kwenye lile sanduku la barafu pale mochwari.”

“Kumbe kweli Macho ya Nyoka amekufa!” Nilijisemea mwenyewe kwa sauti, na Koku akanikazia macho.

“Unamjua yule mtu?”

“Hapana, ila nilikutana naye muda mfupi kabla yule askari hajamuua. Ni mfuasi wa Martin Lundi, na nilimuona kwa macho yangu akiua mtu kule msituni Koku. Ni mtu mbaya sana yule.Bora alivyokufa.”

“Mungu wangu, Tigga!” Koku alistaajabia taarifa ile.

“Kwa hiyo yule askari akachukua hatua gani baada ya hapo?” Nilimuuliza.

Koku aliguna kabla ya kunijibu.

“Achukue hatua gani nasi tulishamwambia kuwa yule mtu hatujawahi kumuona hata siku moja? Alichofanya ni kutueleza kuwa muda wowote utakapowasiliana na sisi tumjulishe, na tukushauri ujisalimishe. Akatuachia kadi yenye namba zake za simu ili tumpigie muda wowote tutakapopata habari kuhusu wewe.”

“Ooo? Kwa hiyo unadhani ni bora nijisalimishe? Au utamjulisha huyo askari kuwa nilikuja kuwasiliana na wewe?” Nilimuuliza dada yangu.

Swali laangu lilimuumiza sana.

“Wewe ni mdogo wangu Tigga.| Aliambia kwa hisia kali.

“Ni kweli dada… I am sorry. Niko kwenye wakati mgumu sana kwa kweli… sifikiri sawasawa…” Nilimtaka radhi.

“Sawa Tigga. Mi’ najua mambo mengi yanayosemwa juu yako sio ya kweli, na hili nilimweleza hata yule askari, pamoja na zile habari nilizozipata kutoka kwa Kelvin. Lakini hata kama ungekuwa umefanya hayo mambo elewa kuwa katu siwezi kukusaliti mdogo wangu.”

 “Dah, Koku…” Donge lilinikaba kooni. Machozi yakanichonyota machoni.

Koku alinishika mabega, akanitazama moja kwa moja machoni.

“Ila kiukweli nadhani ni bora ujisalimishe Tigga, na katika kufanya hivyo inabidi uwe makini sana unajisalimisha kwa nani. Nadhani yule askari ni mtu safi…anaonekana ana uelewa fulani.” Koku aliniambia.

Niliyatafakari  maneno yake kwa muda.

lngawa niliielewa busara ya ushauri wake, bado nilikuwa nina tatizo la kujua ni yupi hasa askari wa kumuendea. Je ni kweli yule afisa aliyemuua Macho ya Nyoka alielekea kuwa mwafaka? Sikuweza kupitisha uamuzi wowote kwa wakati ule, lakini hata mimi nilidhani kuwa kwenye kutafuta msaada wa kuaminika juu ya suala hili, labda ningeanza na yeye.

Tulibaki kimya kwa muda, kisha nikamwambia Koku shida yangu.

“Koku, nahitaji pesa. Unaweza kunipatia kiasi chochote? Nimeishiwa…” Aliniambia nimsubiri mle mle ndani akanitazamie kwenye pochi lake kule ofisini kwake, kwenye kitengo cha madawa.

Alitoka na kurudi muda mfupi baadaye akiwa amebeba maboksi matupu ambayo bila shaka yalikuwa yamewekewa chupa za dawa mbalimbali. Alinikabidhi kiasi cha pesa akiwa amekifumbata mkononi mwake, nami nilizipokea bila kuzihesabu na kuzishindilia mfukoni mwangu.

“Hiyo ni shilingi elfu hamsini. Nasikitika sina zaidi ya hapo.” Aliniambia.

Nilimshukuru sana na kumwahidi kumlipa iwapo nitatoka salama kwenye  msukosuko ule ulionikabili.

Aliniambia nisijali na kunieleza kuwa yule mtu aliyekuwa akifanya kazi ya kupokea simu pale ofisini kwake ambaye alimhisi kuwa ni mfuasi wa Martin Lundi alikuwa amerudi.

Hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kutokea nje ya jengo lile isipokuwa kupita pale mbele ya dirisha la ile ofisi ya Koku. Dada akanibebesha yale maboksi, akitumbukiza lile begi langu ndani ya boksi moja na kuniambia kuwa nitoke nje nikiwa nimebeba yale maboksi na kuyatumia kuficha uso wangu wakati nikipita mbele ya ofisi yake, labda nitafanikiwa kumpita yule mtu bila kutambulika, hasa kutokana na lile koti jeupe nililovaa juu ya nguo zangu.

Nilimshukuru dada yangu kwa mara nyingine tena, naye alinikumbatia kwa nguvu na kuniambia kuwa amefurahi sana kuniona na kwamba niwe makini.

Nikiwa nimebeba yale maboksi nikijitia  mmoja wa manesi wa hospitali ile, nilitembea haraka kuelekea nje ya jengo lile huku nikificha uso wangu nyuma ya yale maboksi. Nilipopita kwenye dirisha la ofisi ya Koku, nilichungulia juu ya uzio wa maboksi niliyokuwa nimeyabeba na kuzungusha macho yangu yaliyofichwa na ile miwani ya jua niliyovaa kuelekea ule upande ambao nilidhani ningeweza kumuona huyo mtu anayekaa kwa kazi ya kupokea simu tu mle ofisini kwa dada yangu.

Koku alikuwa sahihi.

Yule mtu alikuwa ni mmoja wa wale vibaraka wawili wa Martin Lundi alioniibukia nao kule ofisini kwa mkuu wa wilaya.

Aise!

Yule mtu hakunizingatia wala hakunitilia shaka.

Nilitoka nje ya lile jengo huku nikiwa na woga mkubwa. Niliyatupa yale maboksi kando ya mapipa ya taka, baada ya kutoa begi langu kutoka kwenye   moja ya yale maboksi. Nyuma ya jengo lile nililivua lile koti jeupe nililovaa juu ya nguo zangu na kulitupa nyuma ya maua.

Nilitazama kulia na kushoto, kabla ya kuvuka barabara na kutoweka kutoka eneo lile huku nikijifariji kuwa angalau nilikuwa nimepata mwanzo mzuri, kwani nilikuwa nimepata taarifa za muhimu sana kutoka kwa Koku.

--

Saa yangu iliniambia kuwa muda ulikuwa ni saa sita na robo mchana. Nilisimamisha teksi na kumwelekeza dereva anipeleke Kijitonyama, nyumbani kwa aliyekuwa rafiki yangu Aulelia Mushi. Kwa kadiri nilivyoelewa, Aulelia bado alikuwa hajaolewa na alikuwa akiishi peke yake na msichana wa kazi tu. Yeye alikuwa ana tabia ya kurudi nyumbani kula chakula cha mchana na kurudi tena kazini. Nilitaka nimkabili ili nijue nini kiini cha ile tabia yake ya ajabu, na huenda kwa kufanya hivyo ningepata mwanga mwingine kuhusu wale watu wabaya wanaoniwinda.

Nilimkuta msichana wake wa kazi ambaye alinikaribisha kwa mashaka huku akinieleza kuwa tajiri yake amemzuia kukaribisha wageni asiowajua. Huyu alikuwa msaidizi tofauti na yule niliyemjua mimi, lakini kwa hapa jijini wasaidizi wa ndani huwa wanabadilika kila mara.

Nilimwambia mimi ni dada wa tajiri yake na kwamba nimewasiliana naye kwa simu na kuwa yuko njiani anakuja. Nilikaribishwa sebuleni na kuketi nikisubiri huku moyo ukinipiga kwa nguvu.

Samahani Aulelia, lakini ni muhimu kwangu kujua ukweli.

Sikusubiri sana, kwani muda si mrefu nilisikia gari lake likiegeshwa nje ya nyumba na dakika kama tatu tu baadaye aliingia ndani huku akimpigia kelele msaidizi wake aende akashushe mizigo kutoka kwenye gari.

. Aulelia alisimama ghafla na uso ulimbadilika mara moja, ukichukua mtazamo wa woga uliochanganyika na chuki kubwa.

Nilisimama kutoka kwenye kochi nililokuwa nimekalia na kumtazama.

Tulitazamana.

“Toka nyumbani kwangu Tigga! Toka kabla sijakuitia polisi!” Hatimaye alinifokea kwa chuki na ghadhabu.

Nilimuinulia viganja vya mikono yangu kumwashiria kuwa sikuwa na silaha yoyote na kwamba sikuwa nikitaka shari.

“Nitaondoka Aulelia, lakini nataka maelezo ya kitendo chako cha kunikana vile mbele ya watu…kumbe unanifahamu kuwa mimi ni Tigga?Sasa kwa nini ulisema hunijui?” Nilimuuliza huku nikimsogelea taratibu.

Alinitazama kwa jeuri na kuniinulia kidevu kwa kiburi.

“Hilo ndilo lililokuleta au kuna lingine?” Aliniuliza.

Nilimtazama na sikuamini kama ni yeye kweli anaweza kuniongelesha kwa kiburi namna ile.

“Aulelia! Ni nini lakini kinatokea? Mimi nimekutwa na matatizo makubwa sana rafiki yangu. Nimeshuhudia maiti za wenzangu zikiwa zimetawanywa kama mizoga ya wadudu tu huko porini, nimekuja hapa mjini kila mtu ananigeuka, kuanzia Kelvin hadi mama yangu… hadi wewe! Sijui ni nini kinatokea…” Nilimwambia kwa hamaniko.

“Kwa hiyo umekuja kunimalizia na mimi? Unataka kutafuna moyo wangu na kunywa damu yangu? Ndicho kilichokuleta?” Aliniuliza kwa jeuri ile ile, huku sauti yake ikitetemeka.

Nilishangaa.

“Nini? Mbona sikuelewi Aulelia? Ni vitu gani hivyo unaniambia?”

“Habari zako zote ninazo Tigga, na nakuhakikishia kuwa mimi hutanipata kirahisi…tutapambana!” Alinijibu kibabe, na hapo hapo aliruka kwa wepesi wa ajabu na kunyakua  kisu kikubwa kutoka kwenye kabati la vyombo lililokuwa pale sebuleni.

Nilishangaa, lakini akili ilianza kufanya kazi haraka haraka wakati nikimtazama akinijia akiwa na kile kisu mkononi.

“Ondoka upesi nyumbani kwangu Tigga! Ondoka na usirudi tena!”

“Sitaondoka bila majibu Aulelia! Kama utaniua kwa hicho kisu basi uniue tu, lakini mimi sikuja kwa shari kwa sababu ushari si fani yangu, nawe unajua hilo.” Nilimwambia huku nikiwa bado nimemuinulia viganja vyangu.

Aliduwaa, kwani bila shaka alitaraji ningemjia juu na kujaribu kupambana naye.

“Tigga n’takuchoma kisu ujue! Ondoka nakwambia…!”

“Nichome tu Aulelia! Mimi nimekikwepa kifo mara kadhaa tangu nikutwe na mkasa huu unaouendeleza hapa. Lakini huko nilifanikiwa kukikwepa kifo kwa sababu nilikuwa najua kuwa  napambana na adui. Lakini wewe sio adui yangu Aulelia… wewe ni rafiki yangu. Natarajia msaada kutoka kwako na sio mapambano. Kwa hiyo kama unadhani kunichoma kisu ni salama zaidi kwangu Aulelia, nichome tu. Vinginevyo,  ninachotaka kutoka kwako ni majibu tu.” Nilimwambia kwa utaratibu huku nikimsogelea baada ya kuona kuwa yeye amesimama. Hili hakulitegemea,  na nikaona akitetereka katika msimamo wake.Machozi yakamlengalenga.

“Umeongea na mtu anayejiita Dr. Martin Lundi?” Nilimuuliza kwa upole.

Aliafiki kwa kichwa, na kutazama pembeni.

“Akakwambia kuwa mimi nina wazimu…Paranoid Schizophrenia?”

Aliafiki tena kwa kichwa,kisha  akajibweteka  kwenye kochi, akiachia kisu chake kikianguka sakafuni. Niliketi kando yake huku moyo ukinipiga.

“Ulimwamini Aulelia? Uliamini kuwa mimi nina wazimu?”

“What did you expect (Ulitegemea nini), Tigga, eenh? Yule ni daktari, mtaalamu…ananieleza mambo kama hayo… unategemea n’taacha kumuamini?” Aliniuliza kwa hamasa, akiyapuuzia machozi yalikuwa yakimtiririka.

“Yule sio mtaalamu lolote!Ni muuaji mkubwa! Nimeshuhudia kwa macho yangu akishirikiana na wenzake wawili kumtesa mtu na hatimaye kumuua!” Nilimwambia kwa kwa jazba. Niliona akichanganyikiwa, asijue iwapo aniamini au ndio aamini kuwa kweli mimi ni mwehu, kwani kwake Martin Lundi ni mtaalamu wakati  mimi nasema ni muuaji.

How could you believe him Aulelia? We’ unanijua mimi!” Nilimuuliza kwa shutuma.

“Sikumwamini wala sikumbishia Tigga! Nilichomwambia ni kwamba ni mimi ndiye nitakayeamua iwapo ni kweli Tigga ana wazimu au vinginevyo pale nitakapomuona kwa macho yangu mwenyewe! Ndivyo nilivyomwambia Tigga!” Alinijibu na kutazama pembeni huku akifuta machozi. Na hivyo ndivyo nilivyotegemea Aulelia angelichukulia suala lile.

“Sasa kama ulikuwa na mtazamo huo kwa nini ulinifanya vile pale tulipokutana?” Nilimuuliza.

“Habari zako zilizagaa kwenye magazeti Tigga, na hazikuwa habari nzuri. Halafu nikaanza kupokea meseji za simu…” Aliniambia

“Meseji za simu? What has that got to do with any of this?” Nilimuuliza kwa mshangao na kutoelewa, nikitaka kujua hizo meseji za simu zilihusika vipi na habari zile tulizokuwa tukiziongelea.

Alinitazama kwa muda kisha akageuka pembeni na kuchomoa simu yake ya kiganjani kutoka kwenye mfuko wa koti la la suti aliyokuwa amevaa. Alibofya bofya kwa muda kwenye ile simu kisha akanikabidhi bila ya kusema neno. Niliipokea ile simu huku nikimtazama kwa macho ya kuuliza, lakini bado alikuwa amegeukia pembeni.

Niliitazama ile simu.Nikaona alikuwa ameniwekea sehemu iliyoonesha ujumbe mfupi wa simu, nami nikaanza kuusoma. Ulikuwa ni ujumbe mbaya wa vitisho vikali sana, na matusi mazito ya nguoni ambao uliishia hivi:

Nina hamu na damu yako! Najisikia kukuua na kuutafuna moyo wako. Ole wako nikutie mikononi malaya mkubwa we!

Nilishangazwa na ujumbe ule na nikainua uso kumtazama Aulelia, nikaona alikuwa akinitazama kwa makini.

“Aulelia! Ni nini hii? Huu ujumbe umetoka wapi? Unahusu nini? Una ugomvi na huyu mtu? Ni nani huyu?” Nilimuuliza, lakini alizidi kunitazama kwa muda kabla ya kunijibu.

“Tazama mtumaji wa hiyo meseji ni nani”

Nilimtazama kwa mshangao, lakini nilitekeleza na ndipo kwa kihoro kikubwa nilipogundua  kuwa ule ujumbe ulikuwa umetumwa kutoka kwenye simu yangu!

Nilichoka!

Niliiweka kwenye kochi ile simu na kusimama nikimtazama Aulelia kwa mshangao mkubwa.

“Si… si… sikutuma mimi ujumbe huu!” Nilimwambia huku nikiinyooshea kidole ile simu. Yeye alizidi kunitazama bila ya kusema neno.

“Simu yangu ilipotea kule msituni…na hadi hivi niongeavyo sinayo mimi! Nina hakika akina Martin Lundi waliichukua! Si nilikwambia? Wale ni watu wabaya sana!” Niliendelea kujieleza, lakini Aulelia aliichukua ile simu na kubofya tena kabla hajanikabidhi kwa mara nyingine.

Niliipokea huku nikimtazama kwa mashaka,kisha nikausoma ujumbe mwingine uliotumwa kwa Aulelia kutoka kwenye simu yangu.

Nimeshaua watu wengi na sasa najisikia kuutafuna moyo wako! Kaa chonjo, nakuja kukumaliza! Changudoa mkubwa we!

Loh!

Nilielewa kuwa ile ilikuwa ni njama ya Dokta Lundi ya kutaka kunifarakanisha na watu wangu wa karibu ambao walielekea kuniamini. Na sasa nilielewa sababu ya Aulelia kufanya mambo aliyofanya siku ile nilipokutana naye pale katikati ya jiji.

Machozi yalinibubujika bila kituo huku nikitikisa kichwa kwa masikitiko.

Ama hakika akina Lundi ni watu wenye mbinu sana. Nilikumbuka jinsi ile simu yangu ilivyoibuka ghafla tu kule kwenye chumba cha ile nyumba ya wageni kule Kigamboni. Ilikuwa ni baada tu ya lile tukio baina yangu na Aulelia siku ile. Kwa mara nyingine niliushukuru uamuzi wangu wa kuiacha kama ilivyo mle ndani siku ile na kuondoka zangu.

Hivi Aulelia angenielewa leo hii ninavyomwambia kuwa si miye niliyekuwa nikimtumia zile jumbe ogopeshi kama ningekuwa na ile simu leo hii?

Niliishia kugunia tu.

“Pole sana Aulelia, lakini mimi siye niliyetuma hizi meseji rafiki yangu. Why should I? Ni wazi hii ni mbinu ya Dokta Lundi kutaka kunifanya nionekane kichaa kwako!” Nilimwambia.

“Ni kweli Tigga. Niliamini kuwa umepata wazimu baada ya kuanza kupata hizo meseji kutoka kwako…lakini nadhani sasa naelewa kilichotokea. Kama unachosema ni kweli…”

“Tangu lini nikaanza tabia ya uongo? Ninachokwambia ni kweli ndugu yangu. Hawa watu wanataka kunichafua ili kila mtu apoteze imani na mimi…wewe ulitumiwa hizi meseji ili uamini kuwa mimi ni mwehu na upoteze kabisa imani na mimi!”

Aulelia aliniambia kuwa zile meseji zilikaribia kumtia yeye wazimu, kwani mara nyingine alikuwa akipigiwa simu usiku wa manane kwa ile namba yangu lakini akipokea hakuna anayeongea. Akanionesha ujumbe mwingine ambao ndio ulinichanganya zaidi.

Unatembea na mchumba wangu. Sasa nimegundua. Nimemuanza yeye halafu nakujia wewe! Nitainywa damu yako bila kuichemsha, Kimburu we!

Nilibaki mdomo wazi.

“Siku iliyofuata nilipata habari za mkasa uliomkuta Kelvin pale nyumbani kwake. Nilichanganyikiwa!” Aulelia aliniambia kwa huzuni.

Sikuwa na la kusema.

Angalau nilikuwa nimeelewa ni nini kilichotokea kwa rafiki yangu Aulelia. Nilijenga chuki kubwa kwa yule mtu aliyejiita Martin Lundi, kwani mambo aliyokuwa akinifanyia yalikuwa hayavumiliki.

Tulikumbatiana na rafiki yangu na kuombana radhi.

Nilimuelezea juu ya mkasa ulionikuta kule msituni kwa ufupi sana.Ingawa aliniomba sana niendelee kujificha pale kwake mpaka hapo mambo yatakapopoa, sikukubali. Nilimwambia kuwa ilikuwa ni salama zaidi kwake kama akiendelea kuwa mbali nami kwa kipindi hiki cha matatizo.

Nilichukua begi langu,tukaagana. Nilitoka nje ya nyumba yake kwa mlango wa nyuma, nikimuacha akibubujikwa na machozi.

Angalau nilikuwa nimefumbua ukweli fulani katika kitendawili hiki kilichonizunguka. Na nilikuwa nimevuna pointi moja muhimu dhidi ya Martin Lundi muongo.

--

 

Nilikutana na Kachiki kwa bahati mbaya sana.

Na nilipokutana naye sikuwa na hata chembe ya wazo kuwa yeye ndiye ambaye angenifunua macho kuhusu kile kitendawili cha pili nilichoachiwa na Mr.Q, The Rickshaw.

Niliondoka nyumbani kwa Aulelia pale Kijitonyama nikiwa mwingi wa furaha kuwa angalau nilikuwa nimefanikiwa kuzishinda fitna za Dokta Martin Lundi na kurudisha maelewano mazuri na rafiki yangu.

Aidha, nilikuwa nimefanikiwa kugundua njia aliyotumia yule mtu muongo,mfitinishaji na muuaji katika kunifarakanisha na watu wangu wa karibu, kama Aulelia.

Ndio maana walichukua simu yangu kule msituni!

Nilipanda basi la Kariakoo nikiwa na nia ya kutafuta hoteli itakayoniridhisha katikati ya jiji na kuanza kupanga mikakati mipya ya kukabiliana na akina Martin Lundi, nikiwa na nia ya kutafuta namna ya kujisalimisha kwenye vyombo vya dola nikiwa na ule ushahidi wangu.

Nilidhani kuwa kufikia sasa wale wabaya wangu walishajua kuwa huwa najificha kwenye nyumba za wageni zilizojiegesha nje kabisa ya jiji. Sasa mimi niliamua kuhamia kwenye hoteli iliyopo katikati ya jiji. Suala la pesa bado lilikuwa kikwazo, kwani nilijua elfu hamsini nilizoongezewa na Koku, zingetosha kwa malazi ya siku nne tu hotelini. Nikiongezea na pesa zangu zilizobakia, labda ningeweza kuishi kwa siku tano zaidi. Baada ya hapo nisingekuwa na ujanja.

Lakini bado nilikuwa na jukumu la kukamilisha kazi niliyoachiwa na Mr. Q, na siwezi kuishi vema na nafsi yangu kama sijawafikisha kwenye mikono ya sheria wale wauaji wengine waliomfikisha yule mtu kwenye kifo dhalili kama kile, kule msituni. Bila maziko ya kueleweka wala  jamaa zake kujua kuwa amefikwa na umauti.

Hivyo nilikuwa naomba Mungu anisaidie katika wiki mbili ambazo nitaweza kuishi hotelini niwe nimetimiza azma yangu ya kumlipizia kisasi yule mtu na kuwafikisha kwenye sheria akina Martin Lundi.

Labda kufikia muda huo nitakuwa nimeshawasambaratisha akina Martin Lundi, au nikawa nimepata namna ya kujisalimisha kwenye mikono halali ya sheria na kuukabidhi ule mkanda wenye ushahidi,kwenye mikono salama.

Lakini nitaweza?

Nikiwa nimezama kwenye mawazo yangu haya, ndipo niliposhitushwa na kelele za mabishano ndani ya daladala baina ya kondakta na dada mmoja aliyekuwa akidai kuwa ameibiwa pesa zake na hivyo hakuwa na nauli.

Kutokana na mavazi yake yaliyoleta hisia kuwa alikuwa changudoa, hata abiria wenzetu mle ndani walianza kumshutumu na kumtetea kondakta kiasi yule dada akaanza kuangua kilio. Kilio hakikumsaidia, maana Kondakta akawa anaongea masuala ya kupeleka basi polisi ili abiria wote tupekuliwe kumsaka mwizi aliyemuibia yule dada. Mzozo mpya ukaanza kutoka kwaabiria, wakiipinga hali ile.

Zogo likashamiri garini. Suala la kupelekwa kituo cha polisi kupekuliwa halikunikalia vyema kabisa akilini mwangu. Basi nilijitolea kumlipia yule dada na safari ikaendelea kwa amani. Lakini nilipoteremka Kariakoo, yule dada alinifuata tena na kuniomba nimsaidie nauli nyingine ili aendelee na safari yake ya Gongo la Mboto, kwani ni kweli alikuwa ameibiwa pesa zake zote.

Nikiwa na mashaka kuwa huenda yule dada alikuwa ni changudoa tu wa mjini anayetaka kunifanya bwege kwa kujitolea kwangu kumlipia nauli hapo mwanzo, nilianza kumhoji juu ya safari yake huku nikiendelea kutembea kuelekea kwenye maeneo niliyohisi yanaweza kuwa na hoteli ilhali yule dada akinifuata.

Ni hapo ndipo nilipogundua kuwa alikuwa anaitwa Kachiki, na kwamba alikuwa akifanya kazi ya uhudumu kwenye  baa moja iliyoitwa Uno Trabajo iliyoko maeneo ya Gongo la Mboto.

Nilikumbuka kuwa alipandia basi la Kariakoo maeneo ya Makumbusho, na nilipomuuliza kuwa ndipo alipokuwa akiishi, alinifahamisha kuwa yeye na wenzake wanaofanya kazi kwenye ile baa huwa wanalala palepale baa kwani mmiliki wa baa ile alikuwa amewajengea vyumba vya kulala, ila alienda kule Makumbusho kumfuatilia mwenzao ambaye aliondoka kazini siku mbili zilizopita na hakurejea, ambapo alipomkuta aligundua kuwa alikuwa ameamua kuacha kazi kienyeji tu baada ya kupata bwana wa kumweka ndani.Akaendelea kuIlaani tabia ile ya yule mwenzake ya kuamini wanaume wa mpito kiasi cha kuamua kuacha kazi, lakini kufikia hapa nikawa makini sana na ile taarifa yake.

“Yaani mnapewa na malazi hapo hapo Baa?” Nilimuuliza.

“Tena kila mtu na chumba chake bwana! Chakula tunakula hapo hapo, hata ukilipwa mshahara mdogo kuna tatizo gani? Kwa maisha ya hapa mjini Anti mtu ukipata pa kuweka ubavu bila kulipia kodi unataka nini tena zaidi?” Kachiki alisema kwa hamasa, nami nikawa nimeanza kulizungusha lile jambo kichwani mwangu.

Hizi pesa zitaniishia tu baada ya muda. Hivi sasa akina Martin Lundi watakuwa wananitafuta kwenye nyumba za wageni, na muda si mrefu msako wao utahamia kwenye mahoteli. Muda si muda watanikamata, kama jinsi walivyoniibukia kule Kigamboni. . Lakini hata siku moja wale watu wabaya hawatafikiria kunitafuta kwenye mabaa, labda nikutane nao kwa bahati mbaya tu wakiwa kwenye manywaji, jambo ambalo uwezekano wake ni moja kati ya mia moja.

Nilifanikiwa kumshawishi Kachiki anipeleke huko kwenye hiyo baa aliyokuwa akifanyia kazi ili aniunganishie hicho kibarua alichokiacha huyo rafiki yake. Alinishangaa kupita kiasi, kwani hakuamini kabisa kuwa mtu kama mimi naweza kuwa na shida ya kibarua cha ovyo kama jinsi yeye alivyokiona, kama kile.

Ilibidi niseme uongo wa kukata na shoka lakini nilifanikiwa, kwani nilimwambia kuwa pale nilikuwa naenda kutafuta nyumba ya wageni nilale kwani nilikuwa nimelaghaiwa na mwanaume aliyeniweka ndani kinyumba baada ya kunitorosha kwetu Kisiju, na kwamba  sasa amepata bibi mwingine na ameamua kunitelekeza kwenye nyumba ya kupanga kwa wiki nzima bila taarifa wala matumizi yoyote. Nikimpigia simu anasema yuko bize. Nikaamua kuondoka lakini baada ya kuuona mji, sikuwa tena na haja ya kurudi kwetu Kisiju.

Kachiki aliipokea ile hadithi yangu ya uongo kwa masikitiko makubwa hasa akiioanisha na lile tukio la yule rafiki yake aliyetoka kumfuatilia kule Makumbusho. Moja kwa moja alikubali kunipeleka kwenye ile baa aliyokuwa akifanyia kazi kuchukua nafasi ya huyo mwenzao aliyeacha kazi kama namna ya yeye kulipa fadhila yangu.

Ingawa kwa wakati ule niliona kuwa ile ilikuwa ni njia ya kujipatia mahala pa kujihifadhi kwa muda na wakati huohuo kujipatia kipato kidogo, lakini umuhimu wa uamuzi wangu wa kumsaidia yule dada na hatimaye kuamua kwenda kuomba kibarua kwenye ile baa aliyokuwa akifanyia kazi nilikuja kuuona baadaye.

--

Uno Trabajo ilikuwa ni baa ya aina yake.

Ilikuwa ni vigumu sana kuamini kuwa kule Gongo la Mboto kuliweza kuwa na baa kama ile, kwani ilikuwa katika kiwango cha kimataifa kabisa. Na kama alivyonieleza Kachiki, mmiliki wa ile baa aliwawekea wahudumu wake mazingira mazuri sana ya kazi, kwani pamoja na kuwapatia vyumba vya kulala nyuma ya ile baa, pia aliwapatia mahitaji kama sabuni, dawa za meno na matibabu.

Siku ile ile nilipata kibarua cha uhudumu wa baa kwa mshahara wa shilingi elfu ishirini kwa mwezi pamoja na mahitaji yote hayo muhimu,kwangu la msingi likiwa ni malazi na zile elfu ishirini. Nilipelekwa kwenye chumba changu kidogo lakini kisafi cha kuridhisha tu, kilichokuwa na kitanda kidogo cha futi tatu na mashuka yenye lebo ya ile baa.

Nilijifungia mle chumbani na kuanza kuweka vitu vyangu kwa mpangilio nilioutaka. Nilitoa lile burungutu la pesa nilizopewa na Koku na kuanza kuzipanga vizuri pamoja na pesa nyingine nilizokuwa nazo, na wakati nafanya hivyo niliona kitu kama kadi ndogo ikidondoka kutoka kwenye lile burungutu nililopewa na dada yangu.

Nilipoiokota niligundua kuwa ilikuwa ni kadi ya anuani, ambayo dada yangu aliifumbata pamoja na zile pesa wakati ananipa kule hospitali ya wilaya ya Temeke, nami bila kuangalia nikazishindilia mfukoni mwangu.

Niliisoma ile kadi na moyo ukanilipuka kisha ukaanza kunienda mbio.

John Vata

Assistant Commissioner of Police

Special Op.

 

Chini ya maelezo hayo zilifuatia namba za simu za waya, za kiganjani, anuani ya posta na ya barua pepe.

Nilikaa kitandani taratibu huku nikiendelea kuitazama ile kadi bila ya kuamini, nikijua wazi kuwa Koku alikuwa ameniwekea ile kadi makusudi, na kwa maana hiyo, lile jina nililoliona kwenye ile kadi ndilo lilikuwa la yule afisa wa polisi anayekata ndevu katika mtindo wa Timberland.

“Mungu wangu! Kumbe pale ofisini nilikuwa naongea na Kamishna msaidizi wa polisi!” Nilijisemea mwenyewe na kutazama tena lile jina lililoandikwa kwenye ile kadi.

John Vata.*

Sikuwa nimepata kulisikia lile jina mahala popote kabla ya pale. Nilijikuta nikitikisa kichwa na kutabasamu, nikistaajabia werevu wa dada yangu, kwani nilijua kuwa alikuwa amefanya vile makusudi kwa sababu alitaka nijisalimishe kwa yule askari ambaye yeye alimwamini.

Lakini mimi naweza kukuamini John Vata?

Na kwa nini afisa mkubwa kama yule afuatilie suala lile yeye mwenyewe? Mtu mwenye wadhifa kama ule alitakiwa atume vijana wake wafuatilie, kisha yeye aletewe taarifa tu ya maendeleo. Vipi aingie yeye mwenyewe kwenye upelelezi na hata kufikia hatua ya kupambana na muuaji kama Macho ya Nyoka namna ile?

Nilifikiria sana juu ya jambo lile, kisha nikapitisha uamuzi.

Baada ya kuweka vitu vyangu kwenye utaratibu nilioutaka mle ndani, nilitoka na kufunga mlango wa chumba changu kwa nje.Nikamfuata Kachiki aliyekuwa amejilaza chumbani mwake. Nilimuuliza ni muda gani tulikuwa tunaanza kazi akaniambia kuwa ni saa tisa mchana watu wakianza kutoka maofisini, ingawa kwa muda ule huduma ilikuwa ikitolewa lakini hakukuwa na wateja wengi hivyo tuliweza kupumzika tu na kwamba kuna zamu maalum huwa zinapangwa kwa kuhudumia muda ule wa kabla ya saa tisa.

Basi nilitoka, nikimwambia kuwa nilikuwa naenda kununua nguo za mitumba kwani niliona kuwa nguo zangu za kushindia zilikuwa haziendani kabisa na mazingira yale.

“Kweli shoga, maanake hizo suti zako na mazingira haya hata si mwake!” Alinijibu na sote tukacheka.Nikatoka, nikiwa na ule mkanda wangu wa video ndani ya sidiria yangu. Nilienda mpaka Kariakoo, huko nikatafuta kibanda cha simu na kuipiga ile namba ya simu ya kiganjani ya Kamishna Msaidizi wa polisi John Vata.Niliisikiliza ikiita huku moyo ukinienda mbio.

“John Vata!” Sauti niliyoikumbuka kuwa ni ya yule afisa wa polisi aliyenikamata pale ofisini kabla ya Macho ya Nyoka kutokea ilipokea ile simu.

“Tigga Mumba!”

Kimya kilitanda kwa muda, nikisikia yule afisa akihema upande wa pili wa ile simu.

“Uko wapi? Nahitaji kuongea na wewe…na ukumbuke kuwa bado uko chini ya ulinzi na—”

“Mimi ndiye niliyekupigia afande, hivyo naomba unisikilize!” Nilimkatisha.

“Unatakiwa ujisalimishe ndio uongee hayo unayotaka kuongea, sio kwenye simu namna hii…okay, unasemaje?”

“Niko tayari kujisalimisha afande, lakini nataka kwanza umtafute na umweke chini ya ulinzi mtu aitwaye Martin Lundi…Dokta Martin Lundi. Nitakapothibitisha kuwa huyo mtu amewekwa chini ya ulinzi nitajitokeza mahala popote utakapotaka, na nitakuja na ushahidi wa kukuonesha kuwa huyo ndiye mtu unayetakiwa umsake kwa mauaji ya kule msituni, na sio mimi. Tena nisikie na nione kwenye vyombo vya habari kuwa amekamatwa…magazeti, redio na televisheni…sio uniletee stori tu kuwa eti—”

“Tigga…”

“Sikiliza bwana! Sio uniletee habari tu kuwa tayari amekamatwa bila mimi kuona ushahidi wa hilo. Bila hivyo sijitokezi ng’o!”

“Tigga, unafanya kosa kubwa. Kwanza lazima uelewekuwa sisi hatushindwi kukutia mikononi—”

“Nyinyi ni ajkina nani?” Nilimkatisha, akili yangu ikirudi kwa yule askari wa kike aliyenicharaz amakofi kule Sinza, niliyemtoroka kule Kigamboni.

“Sisi jeshi la polisi, nani mwingine?” Alinikemea, na bila kusubiri nimjibu, akaendelea, “Kwa hivyo kukutia mbaroni nisuala la muda tu. Haklafu nataka ujue kwamba huwa sifanyi kazi kwa kupewa mashinikizo na watu wanaokimbia mikono ya sheria. Hivyo nakuhakikishia kuwa hata usipojitokeza, n’taendelea kukuwinda mpaka n’takutia mikononi tu…”

“Na ujue kuwa unaweza kuendelea kuniwinda na kujigamba namna hiyo kwa sababu mimi niliokoa maisha yako kutoka kwenye kifo kilichokuwa mikononi mwa yule muuaji aliyetaka kuniteka pale ofisini kwetu siku ile. Usisahau hilo kabisa!” Nilimjibu kwa hasira.

Alipiga kimya kwa muda na nikahisi alikuwa amechomwa na ukweli wa maneno yangu.

“Sasa utafanya ninavyokwambia au hutafanya?” Nilimuuliza baada ya kuona amekuwa kimya kwa muda mrefu.

“Sitoweza kumkamata Dr. Martin Lundi kwa kusikiliza uzushi wako tu mwanamke!Na kama huna la msingi kata simu na usubiri jinsi nitakavyokutia mbaroni!” Alinijibu kwa ile sauti yake ya utulivu mkubwa usioendana kabisa na mazingira ya mjadala ule, kwani pale alitakiwa awe mkali badala ya kuwa  mpole namna ile.

Kama jinsi alivyomjibu Macho ya Nyoka kwa upole wa hali ya juu kabla hajamshambulia kwa teke lililoipangusa bastola kutoka mikononi mwa yule muuaji.

Hapo nilijua kuwa John Vata alikuwa mtu hatari sana kupambana naye kwani anapochukia huwa anakuwa mpole. Nilianza kuogopa.

“Kwa nini unawahi kunishutumu kuwa ninazusha kabla hujafanya uchunguzi?”

“Martin Lundi unayemsema ni daktari bingwa na mzoefu wa muda mrefu, wa magonjwa ya akili. Ni mzee wa miaka sabini na tano, na sasa ni mstaafu anayesumbuliwa na maradhi ya kiharusi. Anaishi kwenye nyumba aliyojenga shambani kwake Kibaha, hivyo hawezi kuwa ndiye mtu unayemsema wewe kuwa eti alikuwa na wauaji wengine huko porini, eti ndiye  aliyeendesha helikopta baada ya mauaji ya kule msituni na kuwa eti ndiye anayekuwinda kwa nia ya kukuangamiza…”

What?”

“Oh,Yes! Kwa hiyo kata huo upuuzi na ujisalimishe mara moja!” Vata alinikoromea.

Nilibaki mdomo wazi. Huyu askari ameyajuaje yote haya nami sijawasilisha maelezo yoyote kwenye vyombo vya dola? Yaani yule mtu sio Martin Lundi?

“We’ binti upo? Sema ulipo ili nije tuonane, sisi wawili tu.Nadhani tunaweza kusaidiana katika hili.” Niliisikia sauti yake sikioni mwangu lakini akili yangu ilikuwa likizoni. Bado nilikuwa nimepigwa bumbuwazi.

“Um…Umeyajuaje yote hayo? Yule mtu sio Martin Lundi? Ina maana na nyie mlikuwa mnajua juu yake? Au na wewe ni mwenzao?” Niliropoka huku nikijitahidi kuisihi akili yangu irudi kazini.

“Habari zote hizo zilikuwa kwenye maelezo yako uliyoandika kwa mwajiri wako pale ofisini. Ulitakiwa na mwajiri wako uandike yale maelezo kwa maelekezo yangu. Na baada ya kupata maelezo yale nilianza kuyafuatilia na ndio nikagundua hayo kuhusu  huyo Martin Lundi wako.”

Nilikata simu.

Nilihisi dunia ikizunguka nami nikizunguka pamoja nayo. This is impossible!

Kwa hakika nilichanganyikiwa.

Nililipa pesa za muda nilioongea na kuondoka eneo lile haraka. Kwa mara nyingine tena Martin Lundi alikuwa amenizidi kete. Alitumia jina la uongo lakini la mtaalamu wa kweli wa magonjwa ya akili, aliyestaafu kazi muda mrefu.

Ama kwa hakika yule ni Martin Lundi wa uongo, ni muongo!

Sasa kama Dokta Martin Lundi halisi ni mzee wa miaka sabini na tano na mgonjwa wa kiharusi, yule mtu aliyekuwa kule msituni anayejiita Dokta Martin Lundi ni nani?

Nilitazama saa yangu nikaona saa tisa ilikuwa inakaribia sana, na bado nilikuwa sijanunua hizo nguo nilizodai kuwa naenda kununua. Lakini nilijua nilipanga kulitatua vipi tatizo hilo, hivyo nikakamata teksi na kwa mara ya kwanza tangu niingie jijini kutoka kule Manyoni kilipoanzia hiki kizaazaa, nilimwamrisha dereva anipeleke nyumbani kwangu pale Upanga, kwenye nyumba ya msajili.

Nilipanda ngazi kuelekea kwenye nyumba yangu iliyokuwa katika ghorofa ya pili ya jengo lile la msajili huku moyo ukinidunda na nikiwa makini sana. Wengi wa wapangaji wenzangu katika jumba lile walikuwa ni wahindi ambao sikuwa na mazoea nao, hivyo sikuwa na wasiwasi wa ule umbea wa mitaa yetu ya uswahilini, ambapo baada ya habari zangu kutangazwa kwenye redio na magazeti, muda huu ningekuwa natumbuliwa macho ya udaku na bila shaka baadhi ya majirani wangeshsanza kupiga simu polisi kuwaarifu juu ya uwepo wangu pale nyumbani.

Geti langu lilikuwa limefungwa vilevile kama nilivyoliacha.

Nilipanda kwenye ule mlango wa chuma uliozatiti usalama mbele ya mlango wangu wa mbele na kufungua tungi la kioo lililotakiwa liwe linaifunika taa iliyokuwa mbele ya mlango wangu, ambalo ndani yake hakukuwa na taa yoyote hivyo lilibaki limefungwa pale kwenye dari kama urembo tu.

Nililitoa lile tungi na kutumbukiza mkono wangu ndani yake nikatoa funguo zangu za nyumba, kisha nikalifunga tena pale kwenye dari.

Hii ilikuwa ni sehemu yangu ya kuficha funguo zangu miaka yote, na zaidi ya dada yangu Koku, hakuna mtu yeyote mwingine aliyeijua. Niliingia na kujifungia kwa ndani.

Niliitazama nyumba yangu kwa upendo mkubwa kwani nilikuwa nimeipamba kwa namna nilivyotaka, na ilikuwa vile vile. Bila kupoteza muda nilienda moja kwa moja hadi kwenye runinga yangu iliyokuwapo pale sebuleni na kuigeuza kule nyuma…

--

Baada ya muda niliingia chumbani na kuchagua baadhi ya nguo zangu za kushindia ambazo niliona zingeendana na mazingira ya kule kwenye kibarua changu kipya na kuziweka kwenye mfuko wa nailoni nilioupata mle ndani.

Niliiangalia nyumba yangu kwa mara ya mwisho na kufungua mlango ili niondoke,na hapo nikapatwa na mshituko mkubwa.

Nilikuwa natazamana uso kwa uso na yule askari wa kike niliyemtoroka kule Kigamboni, safari hii akiwa katika mavazi yake ya kiaskari.

Niliguna kwa mshituko huku mfuko wangu wa nguo ukinidondoka.Hapo hapo yule dada alinisukumia ndani kwa nguvu huku akinifuata mle ndani na kuufunga ule mlango kwa ndani.

Nilijiinua taratibu kutoka sakafuni nilipoangukia baada ya kusukumwa na yule dada na kumtazama kwa woga mkubwa huku nikijiuliza ni jinsi gani alijua kuwa nitakuwa pale muda ule.

“Unaenda mahali Tigga?” Aliniuliza huku akinisogelea taratibu hali macho yake yakionesha ghadhabu za hali ya juu.

Sikuweza kukusanya nguvu za kumjibu.

“Au ulidhani utaweza kutukimbia milele?” Aliniuliza tena kwa kebehi, na alipoona bado sina jibu, akaendelea, “Tulijua tu kuwa utakuja hapa kwako, kama tulivyojua kuwa ungekwenda kule ofisini kwako…ingawa kule ulitupotezea mwenzetu mmoja lakini bado tuko wengi na ni hatari kuliko hata yule uliyesababisha auawe.” Aliniambia kwa jeuri.

“Toka nyumbani kwangu! Huwezi kunitish-AAW!” Nilianza kumkemea lakini yule dada alinirukia na kunichapa kofi kali la uso lililonitawanyia maumivu uso mzima.

Kabla sijajua nijibu vipi pigo lile alinishindilia ngumi kama nne hivi za haraka haraka zilizotua bila mpangilio mwilini mwangu kuanzia kichwani hadi tumboni.

Nilijibwaga kwenye moja ya masofa yaliyokuwa pale sebuleni nikitweta kwa mapigo yale. Yule dada alinijia kasi,akanikwida shati langu,akaniinua kimabavu na kunibamiza kwa nguvu ukutani kabla ya kunishindilia ngumi nyingine ya tumbo.

Niliguna kwa maumivu na nikahisi fahamu zikinihama huku nikiingiwa na wazo iweje mwanamke mwenzangu aninyanyase namna ile.

“Nilikwambia kuwa utajuta Tigga! Sasa wakati ndio umefik—AAKH!”Nilimtwanga kichwa cha uso kabla hajamaliza tambo zake, akalia kwa uchungu huku akiyumba pembeni na mikono yake ikiniachia.

Nilimfuata mbio na kumshindilia teke la tumbo huku nikimtukana, naye akajipinda kwa uchungu.

Sikuishia hapo.Nikamtupia teke jingine lililokuwa linauendea uso wake, lakini alinidaka mguu na kunitupa kwa nguvu nami nikajibwaga sakafuni nikipigiza kichwa changu kwenye upande wa sofa mojawapo mle ndani.

Kabla sijainuka alinirukia pale chini na kuniwekea bastola kwenye paji la uso.

Where is the tape Tigga?” Alinikemea kwa hasira.

Badala ya kumjibu nilimtemea mate usoni naye akanichapa kofi kali la uso, kissha akalichana shati langu kwa hasira kiasi cha kuniacha nikiwa na sidiria tu, na kutumia kipande cha shati langu kujifutia yale mate.

“Usinichezee mimi wewe! Lete huo mkanda!” Alifoka.

“Kwani kule gesti mlipochanachana mito na kuvuruga chumba kizima hamkuupata?” Nilimuuliza kwa jeuri.

Akanipiga kichwani kwa kitako cha ile bastola yake na nikahisi maumivu makali.

“Na bahati yakohukuichukua ile simu tuliyokuachia kule gesti, kwani ungeichukua tungeweza kukufuata kila ulipoenda kwa kutumia mionzi maalum tuliyoitegesha kwenye ile simu.” (Akasonya).

“Hivi nyie mnadhani mimi ni mwehu kweli kama mlivyonipakazia?” Nilimuuliza kwa kujitutumua huku moyoni nikistaajabia jinsi wale watu walivyokuwa makini kwenye maovu yao.

“Usilete ujeuri usio na msingi Tigga, nipe huo mkanda sasa hivi!”

“Nilishawaambia kuwa mkanda uko kwa wakili wangu! Kwa hiyo mimi mkanda sina jamani mbona mnanisumbua hivi?” Nilimuuliza kwa jazba. Nikaambulia  kofi jingine kali sana.

“Wacha uongo!”

“Sasa si uniue tu basi halafu uone jinsi mkanda utakavyooneshwa kwenye vyombo vya habari na wakili wangu?”

Yule dada alichanganyikiwa.Alinitazama kwa hasira halafu akatazama pembeni, nami nikamtazama kwa makini.Nikaona kuwa kushindwa kwake kuupata ule mkanda kulikuwa kunamchanganya sana. Alinigeukia kwa hasira na kuanza kunipekua mwilini, akiutafuta ule mkanda. Alichanachana nguo zangu kwa hasira hadi ile sidiria yangu na kuniacha matiti nje.

Hakupata kitu.

“Sasa hii ndio nini lakini wewe? Hivi ni kipengele gani cha neno ‘sina mkanda’ ambacho kinakuwia ugumu kuelewa?” Nilimuuliza huku nikishindana naye kwenye kunipekua kwake. Nilipoona hanisikii nilimpiga kofi la uso, naye akanisukumia kwenye sofa lililokuwa pale sebuleni huku akinirukia na kunibana pale juu ya lile sofa lile.Akaudidimiza mdomo wa ile bastola yake utosini na kunitazama kwa macho yaliwiva kwa hasira huku akihema kwa ghadhabu. Kwa mara nyingine niliona kuwa yule dada alikuwa tayari kunilipua kwa ile bastola kama si kuhofia kuukosa kabisa ule mkanda wa video anaoutaka kwa kila hali. Kana kwamba kuupata ule mkanda lilikuwa ni jukumu binafsi kwake.

Kwa nini?

“Hivi ilikuwaje hata askari mzuri kama wewe ukajihusisha na watu wabaya kama wale lakini?” Nilimuuliza akiwa amenibana pale sofani.

“Si kazi yako kujua! Toa huo mkanda Tigga ama si hivyo mi’ n’takuua kweli!”

“Huwezi kuniua wewe!” Nilimbishia kwa jeuri huku nikimtazama usoni.

Alianza kunisemesha kitu lakini hapo hapo nilijiinua kwa nguvu na kumsukumiza pembeni nami niliukimbilia mlango ili nitoke mbio nimuache mle ndani, lakini alinidaka miguu na wote tukapiga mweleka mzito.

Alinibana pale sakafuni na kuirudisha bastola yake kwenye mkoba wake uliokuwa ukining’inia kiunoni na kuanza kunishindilia mangumi na makofi mengi huku akinitukana na kunikemea kuwa alikuwa anautaka ule mkanda.

Nilijitahidi kupambana naye lakini alinielemea vibaya sana na nikahisi nguvu zikiniishia.Nilijitutumua kwa nguvu zangu zote na kufanikiwa kumbwaga pembeni nami nikajiinua kujaribu kukimbia lakini alinirushia teke lililonisukuma hadi kwenye friji langu lililokuwa mle ndani nami nikaanguka tena sakafuni ilhali lile friji likifunguka na kuangusha chupa za maji ambazo zilipasuka na kumwaga maji sakafuni pamoja na baadhi ya vyakula vilivyokuwamo ndani ya ile friji, maji ya baridi yakinimwagikia na kutapakaa mle ndani.

Nililala pale  chini nikiwa nimeishiwa nguvu kabisa.

Yule askari wa kike aliniacha nikitweta pale sakafuni naye akautambalia  ule mfuko wangu wa nailoni niliokuwa nikijiandaa kutoka nao na kuanza kuupekua kwa pupa, akiutafuta ule mkanda wa video, bila ya kujali kuwa alikuwa amepiga magoti kwenye dimbwi la maji yaliyomwagika kutoka kwenye chupa zilizopasuka kutoka kwenye friji langu.

Nilipeleka mkono wangu na kukamata waya wa pasi uliokuwa umechomekwa kwenye swichi ya umeme ukutani hali ncha yake ya pili ikiwa kwenye pasi.

Ile pasi ilikuwa imelegea sehemu ambapo ule waya ulikuwa ukiingia kwenye ile pasi na mara kadhaa huwa inanitetemesha wakati nikiitumia. Niliung’oa ule waya kutoka kwenye ile pasi na huku nikiwa nimeushika hali zile ncha za kupitisha umeme zimetokeza nje, niliwasha ile swichi ya umeme na kuutupia ule waya pale kwenye lile dimbwi la maji hali mimi mwenyewe nikirukia juu ya kochi.

Yule dada alipigwa na shoti kubwa ya umeme ambayo hata mimi ilinitisha. Alitetemeshwa vibaya sana na ingawa alipanua kinywa kwa maumivu na kupiga ukelele, hakuna hata sauti iliyotoka. Alitupwa na ule umeme na kujipigiza kwenye mguu wa meza na kubaki akitupatupa miguu na mikono pale sakafuni. Nilikimbia na kuizima ile swichi na kubaki nikimtazama kwa woga.

Alikuwa amenyooka kama gogo pale sakafuni akiwa ametumbua macho bila ya fahamu.

Bila ya kujali iwapo nilikuwa nimemuua au la, nilikusanya vitu vyangu haraka haraka na kubadilisha zile nguo zangu zilizoraruriwa na yule askari mbaya.

Nilijifuta uso wangu kwa nguo zile na wakati huohuo nilibadili na kuvaa nguo katika zile nilizochagua kwa ajili ya kwenda nazo kule Gongo la Mboto. Kisha nilimburura yule askari mpaka nje ya mlango wa nyumba yangu na kuangaza huku na huko.

Kama jinsi nilivyotarajia, hakukua na mtu. Muda kama ule pale kwetu huwa kunakuwa kimya sana. Nilifunga mlango wangu kwa ufunguo na kumalizia kwa kulifunga na lile geti langu la chuma na kuuficha ule ufunguo wangu mahala palepale pa kila siku.

Niliuruka mwili wa yule askari na kuondoka haraka eneo lile.

Nje ya lile jengo nilikodi teksi na kumwamrisha dereva anipeleke sokoni Kariakoo.

Huko nilimpigia tena simu yule afisa wa polisi aliyeitwa John Vata.

“John Vata.”

“Tigga…” Nilisema huku nikihema na nikitazama  huku na kule.

“Tigga! Sasa mbona unakata simu kabla hatujamaliza kuongea? Uko wapi?”

“Sikiliza afande. Sasa hivi kuna askari mwenzenu ametaka kuniua nyumbani kwangu, na kama utawahi utamkuta pale nje ya nyumba yangu akiwa aidha hana fahamu au amekufa. Najua kufikia sasa utakuwa unapafahamu nyumbani kwangu.”

“Ndio, Upanga…nilishafika lakini nyumba ilikuwa imefungwa…”

“Wahi eneo hilo upesi. Huyo askari ndiye atakayekupa undani wa mambo yote haya, na yuko upande wa yule mtu anayejiita Martin Lundi. Mi’ n’takupigia tena kesho…”

No Tigga! Usikate! Nataka tu—”

Nilikata simu na kukodi teksi nyingine niliyoiamrisha inipeleke moja kwa moja hadi baa yaUno Trabajo  kule Gongo la Mboto.

Nikiwa kwenye kiti cha nyuma ndani ya ile teksi, mwili wote ulianza kunitetemeka na woga usio kifani ulinitawala.

--

Usiku ule sikulala vizuri.

Kwanza ni kutokana na kazi ngumu ya uhudumu wa baa ambayo sikuwa nimepata kuifanya hata siku moja, na sikutarajia kuwa ingefika siku ningelazimika kuifanya; na pili ni kutokana na mlolongo wa mawazo uliokuwa unagombania kuchukua nafasi ya usingizi..

Kachiki alinijia juu sana kwa kuchelewa kwangu kurudi pale baa alasiri ile, lakini halikuwa jambo lililoleta matatizo makubwa kutoka kwenye uongozi wa ile baa. Nilipopata nafasi ya kuweka ubavu kitandani ilikuwa ni saa nane za usiku na badala ya kulala nilikuwa nikisumbuliwa na wazo la yule askari wa kike mshirika wa mtu anayejiita Martin Lundi.

Itakuwaje iwapo nitakuwa nimemuua?

Je, yule mtu niliyetarajia anisaidie, Kamishna Msaidizi wa polisi John Vata atanielewa? Yaani huku kupambana na hawa wauaji kunanifanya na mimi sasa niwe muuaji? Kwa hiyo ndio tayari maisha yangu yamebadilika sasa, na sijui kama yatawezakurudi katika ile hali ya zamani.

Mawazo  hayo na kama hayo yalinisumbua sana usiku ule na kulipokucha tu niliamka na kusubiri kupambazuke ili nikampigie simu John Vata nipate kujua hatma ya yule mwanadada, na mustakabali wangu baada ya hapo.

Yeah Hallow!

“Eem-ah…Tigga hapa…”

“Sikiliza we’ binti, hivi unajua unaongea na kufanya mchezo na nani? Kwa nini hutaki kufanya—”

“Ulimkuta yule askari pale kwangu?”

“Unajua kuwa hakukuwa na mtu pale kwako, ndio maana nakuuliza kuwa unajua unafanya mchezo na nani?”

“Hakukuwa na mtu? Yaani hukumkuta nje ya mlango wangu?” Nilimuuliza huku nikifarijika moyoni kuwa kumbe yule dada hakufa. Ina maana alizinduka na kufanikiwa kuondoka kabla Kamishna Msaidizi John Vata hajamkuta.

“Hakukuwa na mtu na nyumba ilikuwa imefungwa vilevile!”

“Aaah… sasa basi…”

“Sasa mchezo basi! Hili suala la kusema kuna askari mwenzetu anashirikiana na huyo mtu anayejiita Martin Lundi sio la masihara, na nitahitaji uthibitishe hilo kwa ushahidi usiopingika, la si hivyo n’takutia kwenye matata mazito zaidi ya haya ambayo unayo hivi sasa!”

“Kwa hiyo huniamini Kamishna?”

“Siwezi kukuamini mpaka ujitokeze na nisikie maelezo yako!”

“Nilidhani maelezo yangu tayari unayo kupitia kwa mwajiri wangu? Unataka nini tena? Au ndiyo huyaamini?”

“Hayo maelezo ya kuwa mstaafu wa miaka sabini na tano kafanya mauaji halafu akarusha helikopta? Come on!” Alinijia juu.

“Sasa basi nakutaka umweke chini ya ulinzi mtu aitwaye Dick Bwasha. Ni meneja wa tawi la benki moja hapa jijini. Huyu naye ni mmoja wa hao watu waliofanya mauaji kule msituni…”

“Tulishapitia mchezo huo na sasa hatuuchezi tena! Jitokeze utueleze unalojua juu ya watu wote hao ndipo sisi tutaamua iwapo tuwaweke chini ya ulinzi wao au wewe…”

Nilitaka sana kujitokeza kwake na kupata msaada na ulinzi kutoka kwake, lakini bado ilikuwa vigumu kwangu kumuamini moja kwa moja, kwani kumbukumbu ya mambo yaliyonikuta mpaka sasa bado haikuniruhusu kuamini mtu yeyote kirahisi kama jinsi yule afisa wa polisi mtanashati alivyotaka. Na kibaya zaidi, tabia yake ya kutotaka kuniamini ilizidi kuniogopesha.

Kwa nini nimuamini wakati yeye haoneshi dalili za kutaka kuniamini?

“Fanya hivyo afande nami nitajitokeza. Nataka ujionee mwenyewe kuwa ni kweli hao watu ninaokutajia wapo, kisha tutaongea kwa undani zaidi na nitakupa vithibitisho vya kutosha.” Nilimwambia.

John Vata alibaki kimya kwa muda, kisha akauliza Dick Bwasha ni meneja wa tawi gani la benki nami nikamtajia, na kumsisitizia kuwa utaratibu ulikuwa ni ule ule. Nataka nihakikishe kwa yakini kabisa kuwa ni kweli huyo mtu amekamatwa.

“Kwa nini unafanya hivi wewe mwanamke?”

“Nataka kujua iwapo ninaweza kukuamini.”

“Unaitilia mashaka serikali?”

“Hata hao walionitumbukiza kwenye balaa hili nao walidai kuwa ni serikali.”

“Ni kina nani hao?”

“Kwa kweli sijui, ila ninachojua ni kwamba huyo mtu aliyejiita Martin Lundi ni mmoja wa viongozi wao na huyo Dick Bwasha niliyekutajia hivi punde ni mmoja wa vibaraka wao…mkamate Dick Bwasha afande, huenda akakufikisha kwa Martin Lundi muongo, nami nitajitokeza.” Nilimjibu na Kamishna Msaidiza John Vata alikaa kimya kwa muda kabla ya kuongea tena.

“We’ unanipigia simu kila unapotaka. Sasa mimi nikikuhitaji nitakupataje?”

“Nilidhani ulisema kuwa utaniwinda mpaka utanitia mbaroni, sasa imekuwaje tena?” Nilimjibu na kukata simu kabla hajaongea zaidi.

Nilirudi Uno Trabajo na kuchapa usingizi mzito.

--

Baada ya kusubiri kusikia habari za kukamatwa kwa Dick Bwasha kwa siku mbili bila mafanikio nilimpigia tena simu Kamishna Msaidizi John Vata. Nikiwa nimejawa ghadhabu kutokana na kutotekelezwa kwa maagizo yangu, nilijitambulisha kwake na kuanza kumshutumu juu ya suala la kutokamatwa kwa yule meneja wa benki anayeshirikiana na kundi la Martin Lundi muongo, naye kwa utulivu mkubwa alinipa jibu lililonikata maini.

Dick Bwasha is dead, Tigga!

Dick Bwasha is d-whaaaat?” Nilimuuliza kwa mshangao mkubwa.

“Huyo mtu uliyenielekeza nikamkamate kuwa ni mshirika wa mtu anayejiita Martin Lundi amekufa. Sasa nataka ujitokeze utoe maelezo juu ya mambo haya Tigga kwa sababu inaelekea kuwa kila unapopita unaacha kifo au vifo nyuma yako…halafu unasema mtu aitwaye Martin Lundi ndio muuaji!” Aliniambia kwa upole wa hali ya juu, na nikajua kuwa alikuwa ameghadhibika kwa kiwango cha juu.

Ina maana sasa naonekana kuwa namsingizia tu huyu mtu aitwaye Martin Lundi, ambaye kiutaratibu ni kwamba hayupo kwani Martin Lundi halisi ni mstaafu wa miaka sabini na tano.

Sikujua niseme nini, nilipigwa na butwaa.

Kwa mara nyingine tena Martin Lundi muongo alikuwa amenizidi kete!

Hivi ni siri gani hiyo waliyonayo hawa watu ambayo njia pekee ya kuificha ni kifo?

 “Tigga? Bado upo?”

Yeah…lakini…Dick Bwasha? It can’t be! How…I mean… amekufaje?”

“Nadhani wewe ndiye unaweza kutueleza kwa ufasaha juu ya hilo Tigga, sasa aidha ujitokeze mara moja au uache kabisa kunipigia simu namna hii. Mimi ni Kamishna msaidizi wa polisi ujue, sio mtu wa kufanyiwa mchezo namna hii!”

Niliogopa!

“Sifanyi mchezo afande! Lakini…

“Lakini nini?”

“Lakini si angalau umethibitisha kuwa huyo mtu Dick Bwasha yupo… alikuwepo kweli, right? Ina maana kuna ukweli kwenye ninayokueleza!”

“Unadhani hilo linakuvua tuhuma?”

“Sina tuhuma zozote mimi! Ni kwamba  hizi taarifa zinanitatanisha! Itakuwaje Dick Bwasha Afe? Na kwa nini unasema kuwa mimi ninaweza kuwaeleza kwa ufasaha juu ya kifo chake?” Nilikuwa nakaribia kuangua kilio kwenye simu.

“Wewe ndiye unasemekana kuwa ni mtu wa mwisho kuonana naye kabla hajakutwa akiwa amekufa ofisini mwake siku chache zilizopita, na mezani kwake kulikuwa kuna fomu uliyoijaza ya kuchukulia pesa pale benki…”

“Eeenh?”

Haya makubwa sasa!

“Niliondoka nikimwacha Dick Bwasha akiwa hai na jeuri kuliko kawaida afande! Kuna kitu kingine kimetokea baada ya mimi kutoka mle ofisini mwake…umewauliza vizuri wale wahudumu wa ile benki afande?”

“Unataka kunifundisha kazi sasa, eenh? Nakwambia jisalimishe kwangu mara moja wewe!” Aliniambia kwa ule utulivu wake wa kuogopesha.

“Akh! Sasa… hivi kweli kabisa inakuingia akilini kuwa kama ningekuwa nimemuua ningekutajia jina lake ukamsake? Seriously? Come on, man! Mi’ n’lidhani we’ ni mpelelezi makini!” Nilipayuka kwa kihoro huku nikiogopa ile hali iliyokuwa ikijitokeza, na badala ya kunijibu John Vata alikata simu.

Khah!Yaani amenikatia simu! Sikuamini masikio yangu.

Ina maana ameniona kuwa mimi ni muongo na bila shaka muuaji na ninataka kumchezea tu kwa sababu zangu binafsi.

Oh! Mungu wangu hii ni mbaya sana! Hii ni mbaya sana!

Nilimpigia tena, lakini ile simu ilibaki ikiita tu bila kupokelewa hadi ikakatika yenyewe, nami nikazidi kuhamanika.

Nikapiga tena, hali ikawa ni ile ile.

Please John Vata, pokea simu tafadhali!

Hatimaye ile simu ikakatika, na nilipopiga tena ile simu ikawa haipatikani.

Oh! My God! Nitafanyaje sasa Tigga miye…?

Niliondoka nikiwa niliyevurugikiwa na niliyehamanika kupita kiasi. Nilienda moja kwa moja hadi kwenye mgahawa uliokuwa jirani na ile benki niliyohifadhi pesa zangu. Niliketi kwenye kiti kilichokuwa kwenye kona na kuelekea mlangoni ambapo niliweza kumuona kila aliyeingia na kutoka kwenye ile benki.

Niliagiza chipsi kwa kuku na kusubiri kwa kufyonza juisi taratibu. Nilisubiri huku moyo ukinienda mbio na woga usio kifani ukinifanya nishindwe hata kuinua ile glasi ya juisi. Muda si mrefu niliona baadhi ya wafanyakazi wa ile benki wakianza kuingia mle mgahawani kupata mlo wa mchana nami nikamakinika nao. Hatimaye nilimuona yule dada niliyezoeana naye pale benki akiingia.Nikahama na juisi yangu hadi kwenye meza aliyoketi na kuketi mbele yake.

Tulitazamana.

“Ti…Unafanya nini hapa?” Aliniuliza kwa wasiwasi na kuanza kuangaza huku na huko ndani ya ule mgahawa.

“Nahitaji kuongea na wewe mara moja na naomba unisikilize na unijibu maswali yangu. Sina muda mrefu, itanilazimu niondoke mahala hapa.” Nilimwambia haraka, na kumtupia swali kabla hajasema neno lolote. “Ni kweli kuwa meneja Dick Bwasha amefariki?”

Yule dada aliafiki kwa kichwa huku bado akionekana kuwa na wasiwasi mwingi.

“Amekufa lini na amekufaje?”

Alinitazama kwa muda kisha akameza funda kubwa la mate.

“Siku ile ulipokuja kujaribu kuchukua pesa pale benki…” Alinijibu na kuendelea kunitazama kwa mashaka, nami niliendelea kumtazama nikitarajia maelezo zaidi kutoka kwake.

“Tulichoambiwa ni kwamba amepatwa na mshituko wa moyo…stroke…amekutwa akiwa ameegemea kiti chake kana kwamba amelala.” Aliendeleza jibu lake huku akinitazama kwa mashaka nami nikiwa nimemkazia macho kwa umakini.

“Ninasemekana kuwa mimi ndiye nilikuwa mtu wa mwisho kuonana naye na polisi wananishutumu kwa kifo chake…unajua nini kuhusu hilo?” Nilimuuliza nikiwa makini sana.

Akanieleza kuwa naye ndivyo alivyokuwa anajua na kwamba baada ya kuhojiwa na polisi amegundua kuwa kumbe nilikuwa nikitafutwa kwa mauaji ya kutisha tangu siku ile niliyokwenda pale benki na kujaribu kuchukua pesa kutoka kwenye akaunti yangu, jjambo alilodai kuwa nusura limtie na yeye kwenye matatizo kwa kushirikiana nami wakati akijua kuwa nilikuwa natafutwa kwa mauaji, ingawa ukweli ni kwamba yeye hakuwa akijua lolote juu ya hilo kwa wakati ule.

“Hayo yote sio ya kweli Anti, ila ni hadithi ndefu, muda hautoshi na hapa sio mahala pake.” Nilimwambia na kutulia kidogo, kisha nikamuuliza, “Ni nani hasa aliyetoa hiyo taarifa kwa polisi kuwa mimi ndiye nilikuwa wa mwisho kuonana na meneja Dick Bwasha? Na kuna uhakika gani juu ya hilo?”

“Mi’ nilikuacha naye mle ofisini, kisha ikaja amri kuwa asiruhusiwe mtu yeyote kuonana na meneja kwa siku ile…”

“Kwa hiyo wewe ndiye uliyewaeleza polisi kuwa mimi ndiye nilikuwa wa mwisho kuonana na Dick Bwasha?” Nilimuuliza kwa mshangao.

“Mi’ nilikuacha na Dick Bwasha ofisini, sijakuona ukitoka! Sasa ulitarajia niwaeleze nini polisi?” Yule dada aliniambia kwa msisitizo.

Nilitaka kumtupia swali iwapo aliweza kuona kila aliyeingia na kutoka benki wakati akiwa anahudumia wateja, lakini niliona akipepesa macho kwa mashaka, kana kwamba hakuwa na imani na kauli yake. Nilimkazia macho na kumsaili zaidi iwapo alikuwa na uhakika na maneno yake, akilini mwangu nikianza kupata mashaka iwapo naye hajarubuniwa na yule muongo ajiitaye Martin Lundi.

“Lakini walipokuja Agnes alikuwa ameshaondoka…na mi’ sikukumbuka kuwa siku iliyofuatia alikuwa anaanza likizo…” Yule dada alisema kwa wasiwasi, kama kwa kujitetea. Sikumuelewa, na nilipomuuliza zaidi aliniambia kuwa Agnes alikuwa ni yule dada mwingine aliyekuja kuniita na kunipeleka kule ofisini kwa Dick Bwasha na kutuacha naye mle ofisini. Yeye alikuwa ni sekretari wa meneja Dick Bwasha.

“Ah! Lakini nilipotoka Agnes alikuwepo pale kwenye meza yake nje ya ofisi ya Dick Bwasha!” Nilimwambia kwa msisitizo. Yule dada aliangalia pembeni, asijibu kitu.

“Sasa Agnes yuko wapi? Aliongea na polisi? Naye aliwaeleza nini?” Nilimuuliza kwa hamasa kubwa.

“Agnes hakuwepo wakati askari walipofika, siku ya tukio aliondoka mapema kwa sababu kesho yake alikuwa anaanza likizo…” Aliniambia.

Nilimtazama kwa huzuni iliyochanganyika na mshangao. Bila shaka aliiona huzuni iliyonigubika, akaendelea haraka, “Mi’ niligundua kuwa kuna mwanamke mwingine aliyeingia ofisini kwa Dick Bwasha baada ya wewe kutoka nilipoongea na Agnes kwa simu akiwa nyumbani kwake kumpasha habari za kifo cha Dick, lakini wakati huo nilikuwa nimeshaongea na polisi…”

“Hah! Yaani kumbe kuna mwanamke mwingine aliye….” Nilidakia kwa mshangao.

“Ndiyo, kwa mujibu wa maelezo ya Agnes. Alikuja mwanamke aliyevaa baibui na hijab kama mzanzibari, akinukia manukato ya udi kama jinsi akina mama wa kizanzibari wanavyonukia—” “Huyo mwanamke alionana na Dick Bwasha?” Nilimkatisha kwa pupa.

“Aliomba kuonana naye lakini Agnes alimwambia kuwa meneja haonani na mtu yeyote. Yule dada alitoa simu yake ya kiganjani na kumpigia Dick palepale. Dick alitoka na kumkaribisha ndani yeye mwenyewe.”

“Kwa hiyo mpaka hapo tu Dick alikuwa hai baada ya mimi kuondoka siku ile…”

“Sasa mimi hayo sikuyajua wakati naongea na wale askari dada’angu! Na kutokana na mshituko wa tukio lile, hakuna aliyekumbuka juu ya Agnes kwa kipindi kile!”

Okay…nini kilitokea baada ya yule dada wa kizanzibari kuingia ofisini kwa Dick Bwasha?”

“Kwa mujibu wa maelezo ya Agnes, alikaa huko ndani kwa muda, kisha alitoka na kumuambia Agnes kuwa meneja amesema kuwa asisumbuliwe tena. Ni baada ya huyo dada kuondoka ndipo Agnes alipoenda kuchukua barua yake ya likizo na kuondoka kimyakimya bila kumuaga bosi, akiamini kuwa alikuwa amelala kitini kwake. Kilichofuata ni wale wafagizi kumkuta Dick akiwa amekufa ofisini mwake. Muda huo benki ilikuwa imeshafungwa kwa siku ile na tulikuwa tumebaki sisi tu mle ndani…”

Hizi taarifa zilikuwa kali sana na nisingeweza kuziacha vilevile tu bila kuzifanyia kazi.

“Sasa rafiki yangu mimi nazidi kuhisiwa uuaji huko na wewe unakaa na taarifa kama hizi?”

“Sasa mi’ sikujua nifanye nini baada ya hapo…na jambo hilo limekuwa likinitisha sana…”

Nilichukua simu yake ya mkononi na kumpigia John Vata. Yule dada aliniuliza nilikuwa nafanya nini, nami nikamwambia kuwa nawapigia polisi ili wajue juu ya taarifa ile. Ingawa alijitahidi kupinga jambo lile, lakini sikujali. John Vata alipopokea ile simu nilijitambulisha na kumweleza juu ya ile taarifa kwa kifupi.

“We’ unajuaje mambo haya? Au bado unaendeleza mchezo wako wa kunitania? Nakuhakikishia kuwa—”

“Niko na huyo dada hapa niongeapo. Inaonekana hao vijana wako waliokuja kuchunguza juu ya kifo cha Dick Bwasha hawakuwa makini. Ndio maana hata mimi sina imani nao sana.”

“Nipe huyo dada niongee naye sasa hivi!”

“Sasa wewe ndio umpigie au umtembelee hapa benki, hii ni simu yake na tunammalizia muda wake wa maongezi!” Nilimjibu na kukata simu. Yule dada alikuwa ameogopa pasina kiasi, na alikuwa akilengwalengwa na machozi.

“Oh! Mungu wangu. Sasa itakuwaje…si nitaingia kwenye matatizo mimi?” Aliniuliza kwa wasiwasi mkubwa.

“Waeleze kama ulivyonieleza mimi. Usifiche chochote. Hutakuwa kwenye matatizo.” Nilimjibu na hapo hapo simu yake ikaanza kuita, naye alishituka na kuruka kama aliyetekenywa kwenye mbavu. Aliitazama ile simu ikiita kwa woga mkubwa.

“Pokea simu na uongee Anti…” Nilimwambia na nilipoona anazidi kuigwaya ile simu, niliipokea. Nilimsikia John Vata ikiongea simuni, nami nilimkabidhi yule dada ile simu, naye hakuwa na namnaAliiweka sikioni taratibu huku uso wake ukiwa na woga mkubwa.

Niliondoka haraka, nikimwacha akiongea na Kamishna Msaidizi John Vata.

 

--

 

Ni nani huyu mwanamke mwenye kuvaa baibui na kunukia udi?

Je, naye ni miongoni mwa wafuasi wa Martin Lundi muongo?(niliendelea kumwita hivyo kwa sababu sasa sikujua nimwite nani). Na kama ni hivyo, kwa nini amuue Dick Bwasha? Sikuamini kabisa maelezo ya kuwa Dick Bwasha kafa kwa mlipuko wa moyo. Hilo kwangu lilikuwa ni uongo mtupu. Niliamini kuwa akina Martin Lundi ndio waliomuu, kwani wale jamaa walikuwa wana uwezo wa kumuua mtu kwa njia yoyote waitakayo.

Nilikumbuka maelezo ya Koku juu ya mambo waliyomfanyia Kelvin, na sasa hawezi hata kuongea huko aliko, na inaelekea anakufa taratibu.

Ila kilichonishinda kuelewa ni kwa nini wamuue Dick Bwasha?

Au ndio adhabu yake kwa kushindwa kuuchukua ule mkanda wa video kutoka kwangu? Lakini kama ni hivyo mbona yule dada askari ameshindwa kuupata ule mkanda mara kadhaa na hajauawa?

Nilikuwa chumbani mwangu pale Uno Trabajo, nikiwa nimejilaza kitandani  nikitafakari mambo yaliyotokea siku ile.

“Yaani tayari Kamishna Msaidizi John Vata alishaniweka kwenye shutuma za kuhusika na kifo cha Dick Bwasha!” (Niliguna). Nilifikiria hali ingekuwaje kama nisingechukua jukumu la kumwendea yule dada wa pale benki na kumsaili juu ya kifo cha yule mtu jeuri aliyeitwa Dick Bwasha.

Na sasa huyu mwanamke anayevaa baibui…

Nilikumbuka maneno ya yule dada askari wakati aliponishtukiza pale nyumbani kwangu Upanga.

…ingawa kule ulitupotezea mwenzetu mmoja lakini bado tuko wengi na ni hatari kuliko hata yule uliyesababisha auawe.

Je, na huyu mwanamke mwenye baibui ndio miongoni mwa hao wenzao wengi ambao ni hatari kuliko yule muuaji niliyemwita Macho ya Nyoka?

Niliamua kwenda kumpigia tena simu Kamishna Msaidizi John Vata. Sikuwa na ujanja.

Nikiwa bado nasumbuliwa na mawazo yale, nilishitushwa na kishindo cha Kachiki aliyeingia chumbani kwangu kwa pupa akiwa amejawa hamasa kubwa.

“Nini wewe!” Nilimaka nikiwa nimeshituka sana.

“Mshikaji kuna dili la kwenda The Rickshaw, si mchezo!” Aliniambia huku akiwa ametoa macho na uso wake ukiwa umejawa bashasha.

The Rickshaw!

Niliinuka kutoka kitandani nikiwa makini mno.Nilimtazama kwa macho ya wasiwasi na kutoelewa.

 “Umesema The Rickshaw?” Nilimuuliza nikiwa wima na nikimsogelea taratibu, akilini mwangu nikianza kumhisi kuwa kumbe na yeye anahusika na akina Martin Lundi.

Yes! The Rickshaw mwanangu! Yiiiii-Hhaaa!” Alinijibu na kushangalia huku akiruka juu. Nilimkamata mabega kwa nguvu na kumkalisha kitandani.

“We’ unajua nini kuhusu hili neno The Rickshaw, eenh? Niambie upesi Kachiki na usinidanganye!” Nilimwambia kwa ukali huku nikimtikisa na moyo ukinienda mbio, akilini mwangu ikinijia picha ya yule mtu aliyeuawa kule msituni akinitamkia lile neno huku akitapatapa katika zile dakika za mwisho za uhai wake.Sasa leo Kachiki ananiambia kirahisi tu eti kuna dili la kwenda The Rickshaw! Tena kwa bashasha na furaha kubwa namna hii!.

Nilihisi msisimko wa ajabu.

Yaani wakati mimi nililihusisha lile neno na kifo cha kutisha kilichoambatana na vifo vya watu wengine wasio na hatia, yeye analizungumzia kwa bashasha namna ile!

Kachiki alinitazama kwa wasiwasi na mshangao kutokana na jinsi nilivyombadilikia ghafla baada ya kusikia neno lile.

“Aaah! Niachie bwana! Mbona hivyo?” Aliniambia huku akinikunjia uso na akiitoa mikono yangu kutoka mabegani mwake.

Niliona kuwa nilikuwa nimekurupuka kwa jazba kubwa bila sababu. Kachiki angeshindwa kunielewesha juu ya neno lile kwa mtindo ule. Nilijitahidi kutulia na kumweleza kwa upole ingawa moyoni sikuwa na upole wowote.

“Samahani Kachiki, lakini nimekuwa nikiitafuta sehemu hiyo iitwayo The Rickshaw kwa muda mrefu bila mafanikio. Sasa leo unaponiambia kuna dili la kwenda The Rickshaw nimepatwa na kiherehere kikubwa…”

Kachiki alinicheka kwa kebehi.

“Huwezi kupajua The Rickshaw hivi hivi tu Nuru!(Yeye ananifahamu kwa jina la Nuru Bint Shaweji) Huko huwa tunapelekwa tu na tunajikuta tumefika, lakini wewe mwenyewe ukitaka kujiendea tu hivi hivi huwezi kufika…mpaka upelekwe.” Alinijibu nami nikazidi kuvurugikiwa.

Mbona inakuwa kama simulizi ya Alfu lela-u-lela? Vipi nifike kwa kupelekwa tu na hata nikitaka kwenda mwenyewe nisipajue?

“Kachiki, huwa mnapelekwa? Mnapelekwa na nani? Na kwa nini kwenda huko kuwe ni “dili?” Kuna nini hapa Kachiki? Mbona sielewi?”

Alinicheka tena.

“Inasemekana Mzee Kazimoja ana hisa kwenye  hiyo The Rickshaw, na mara moja moja—”

“Mzee Kazimoja? Ndio nani huyo tena Kachiki? Mbona unanichanganya?”

“Aaah Nuru nawe! Mzee Kazimoja si ndio mwenye hii baa tunayofanyia kazi? Sijakwambia?”

Nilibaki kinywa wazi. Sikuwa nimetilia maanani kumjua mmiliki wa ile baa hapo kabla , na hata nilipoanza kazi, sikuwa nimeonana na huyo mmiliki bali nilionana na mwangalizi tu wa ile baa aliyekabidhiwa majukumu hayo.

Lakini hapo pia nilipata jibu la swali langu, kwa sababu tangu niliposikia jina la ile baa, nililiona kuwa si la kawaida, kwani kwa lugha ya kihispania, neno “Uno Trabajo” lilimaanisha “Kazi Moja” kwa kiswahili. Kumbe yule mmiliki alikuwa ameiita baa ile kwa kufuatisha jina lake kwa lugha ya kihispania.

“Enhe, umesema Mzee Kazimoja ana hisa The Rickshaw?”

“Ndiyo…”

“The Rickshaw ni nini?”

Ndipo aliponieleza mambo ambayo sikuyatarajia kabisa, na kama nisingekutana naye na nisingeambata naye hadi kwenye ile baa, hakika nisingeyajua asilani!

Aliniambia kuwa The Rickshaw ilikuwa ni kasino moja ya hali ya juu sana jijini, ambayo ndani yake kuna kila aina ya starehe, kuanzia kamari, madansi machafu,  hadi biashara ya ngono.

Mara moja moja huwa wanakuja wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali za magharibi kwa ajili ya kujistarehesha kwenye  ile kasino, na pindi wajapo hao wafanyabiashara, baadhi ya wahudumu wa ile baa ya Uno Trabajo huwa wanateuliwa na kupelekwa The Rickshaw kusaidia kutoa huduma kwani wahudumu wa huko huwa hawatoshi kwenye siku hizo. Na ni hapo ndipo kwenda The Rickshawkunapokuwa dili, kwani wale wafanyabiashara wa kizungu huwa wanatoa bakshishi nyingi na kama ikiwa bahati yako unaweza kuchukuliwa na kuburudika na mmoja wao na kujipatia pesa nyingi.

Kwa maelezo ya Kachiki, kuna mwenzao mmoja alifikia hatua ya kuchukuliwa kabisa na mmoja wa hao wafanyabiashara na kwenda naye Ulaya na mpaka muda ule alikuwa bado yuko huko.

Lakini kama hiyo haitoshi, mara tu wanaporudi kutoka huko huwa wanapewa malipo maalum na uongozi wa ile baa ya Uno Trabajo, malipo ambayo hufikia kiasi cha laki mbili hadi tatu, yakiwa na masharti ya kutosimulia yale waliyoyaona kule The Rickshaw

Hii taarifa ilikuwa mpya sana kwangu. Na hapo hapo niliazimia kufika huko The Rickshaw, kwani ile ilikuwa ni nafasi ambayo nisingeweza kuiachia hata kidogo.

“Mimi naujua sana mji wa Dar, Kachiki, lakini mbona hata siku moja sijawahi kuiona hiyo kasino iitwayo The Rickshaw?” Nilimuuliza.

“Sasa hapo ndipo hata mimi nilipochemsha, kwani mara ya kwanza nilipopelekwa huko, kesho yake nilitembelea karibu mji mzima nikijaribu kuitafuta ile kasino ili nikatafute namna ya kuhamia huko moja kwa moja. Sikuiona kabisa Nuru. Na si mimi tu, hata wenzangu pia walijaribu lakini wapi!” Aliniambia kwa masikitiko.

Sikumuelewa.

“Lakini si mlipelekwa? Inakuwaje tena mshindwe kupajua baada ya hapo?”

“Tunapelekwa tukiwa kwenye gari kama ki-hiace hivi, ambalo huwa halina madirisha kabisa, lina kiyoyozi cha nguvu humo ndani. Hivyo huwa hatujui tunapelekwa wapi, na tukifika huko, lile gari huingia mpaka ndani, tukiteremka huwa tayari tumo ndani. Tunaona tu neno ‘The Rickshaw’ mle ndani. Na mtindo huwa ni huohuo wakati wa kurudi. Tunateremkia kwenye mlango wa kuingizia vinywaji nyuma ya baa na kuingia ndani moja kwa moja” Kachiki alinieleza kwa kirefu.

Nilichoka!

Kwa vyovyote huko The Rickshaw kulikuwa kuna mambo mengi yasiyo sawa, ndio maana hata wale wahudumu wanaopelekwa huko walitakiwa wafike tu humo ndani bila ya kuijua njia.Kuna nini huko?

Ndio maana hata Mr. Q alikuwa amenisisitizia sana juu ya hii The Rickshaw.Ina maana alijua kuwa kulikuwa kuna jambo au mambo, yasiyo sawa…na huenda ndiyo sababu ya  kifo chake.Je, huko ndio makao makuu ya lile kundi la akina Martin Lundi muongo?

“Sasa mnaenda lini huko?” Nilimuuliza Kachiki kwa upole.

Alinijibu kuwa walitakiwa wapelekwe The Rickshawsiku iliyofuatia.

“Na mimi naweza kwenda? Nataka nikajionee na miye!” Nilimwambia huku moyo ukinidunda, nikijua kuwa jibu lake ndilo lingekuwa mwanzo wa majibu mengi yaliyokizunguka kisa hiki cha kutisha kilichonizunguka.

Kama kawaida yake, alinicheka.

“Wewe huwezi kwenda Nuru. Lazima uelewe kuwa hata sisi tunaopelekwa huko kwanza huwa tunasisitiziwa kuwa tutakayoyaona huko ni siri na tunatakiwa tuyaache huko huko! Halafu tunachukuliwa wale tu tuliokuwa hapa baa kwa muda mrefu, wewe bado mgeni huwezi kuchukuliwa bwana!”

Akili ilinizunguka. Nitafanyeje sasa?

Nilizidi kumhoji juu ya ile kasino iliyoitwa The Rickshaw lakini kufikia hapo alikuwa amechoka kujibu maswali yangu na kuamua kucheza muziki kwa furaha, akisubiria hiyo siku ya kupelekwa The Rickshaw. Nilimtazama kwa kukata tamaa, kisha nikamfukuza chumbani kwangu, nikimwambia nataka kulala.

“Usikonde shoga, nikirudi keshokutwa nitakukatia na wewe kidogodogo, si unajua tena?” Aliniambia wakati akitoka. Nilimsukuma nje na kufunga mlango wangu.

Mungu wangu! Kumbe The Rickshaw ni kasino ya hapa hapa jijini!

Ee Mr. Q, ni kipi ulichokiona huko The Rickshaw hata ikabidi uuawe?

Sikulala. Nilikuwa nikizunguka mle ndani nikiiwazia ile Kasino ya maajabu iliyoitwaThe Rickshaw. Iko wapi? Kuna nini huko? Nitafikaje? Ina uhusiano gani na yale mauaji ya kule msituni na wale akina Martin Lundi muongo?

Vyovyote iwavyo, lazima niwemo kwenye huo msafara wa kwenda The Rickshaw hiyo kesho. Nilidhamiria.

Na nilisahau kabisa kumpigia simu John Vata…

Kwa sababu ya Hakimiliki hadithi yetu itaishia hapa.

Uhariri.com

Kwa Huduma Bora Kabisa

Usalama

Kazi yako itafanywa na kuhifadhiwa kwa siri.

Muda

Kazi yako itakamilika ndani ya muda mfupi tuliokubaliana.

Gharama Nafuu

Pia tutakupa uhuru wa kulipa kwa awamu.

Wataalamu

Utahudumiwa na wataalamu wenye uzoefu wa kutosha.

Ushauri

Utakaokujenga kuwa mwandishi bora zaidi

Tutakufikia

Popote ulipo duniani. Tutakuhudumia kwa haraka.

Ushuhuda

Uhariri mnaoufanya ni wa kiwango cha juu sana, kwani humuacha mtunzi akiwa mwandishi bora zaidi kupitia ripoti zenye ushauri makini, mnazotoa kwenye kila uhariri.
Hussein Tuwa
Mwandishi wa riwaya ya Mkimbizi

(+225) 715 001 818 | 787 001 819