Usomaji Prufu

Usomaji Prufu hufanyika baada ya mswada kuhaririwa kabla ya kuchapishwa kuwa kitabu, ni ukweli usiopingika kuwa wahariri ni binadamu nao pia hufanya makosa. Lengo la Usomaji Prufu ni kuondoa makosa ambayo yalisahauliwa na mhariri au yalisababishwa wakati wa uhariri. Tuangalie kidogo baadhi ya makosa ambayo hushughulikiwa wakati wa usomaji prufu.

Makosa ya upatanisho wa kisarufi ambayo hujitokeza katika kazi nyingi huchunguzwa kwa kina aghalabu makosa hayo hujitokeza katika uhusiano uliopo baina ya nomino (majina) au kiwakilishi chake na vitenzi, hasa katika matumizi ya viambishi vya O-rejeshi vinavyoambikwa katika vitenzi kutoendana na nomino zinazohusiana na vitenzi hivyo. Mfano;  Risasi iliomkwaruza (badala ya kuandika Risasi iliyomkwaruza), gari iliyokuwa (badala ya kuandika gari lililokuwa),mtoto aliekuja (badala ya kuandika mtoto aliyekuja) n.k

Makosa ya kimofolojia, katika lugha kila neno huwa lina namna ambayo tahajia za neno hilo zinapaswa kuwa, katika usomaji prufu makosa hayo hubainika na kusahihishwa, aghalabu makosa hayo huwa katika maumbo ya umoja na wingi wa maneno, ambapo kuna baadhi ya maneno ambayo maumbo yake ya umoja na wingi huwa sawa lakini watumiaji wa lugha huyaandika kimakosa kwa mfano;  wingi wa polisi ni polisi (na si mapolisi), wingi wa askari ni askari (na si maaskari), magari mawili (na si gari mbili) n.k

Makosa mengine ni kuunganisha maneno yanayopaswa kutenganishwa kama vile kwanini? (sahihi ni kwa nini?), mbali mbali (sahihi ni mbalimbali). Na kutenganisha maneno yanayopaswa kuunganishwa mfano pale pale (sahihi ni palepale), ovyo ovyo (sahihi ni ovyoovyo).

Makosa haya na mengine mengi huwa tunayashughulikia katika usomaji prufu wetu, karibu sana kwa huduma hii ili tuifanye kazi yako bora kuwa bora zaidi.

Kwa nini Usomaji prufu?

Ukiwa kama mwandishi wapaswa kufahamu umuhimu wake baada ya uhariri.

Ukamilifu

Kwa hakika hakuna binadamu aliyemkamilifu, hata wahariri muda mwingine huingiza au husahau kutoa baadhi ya makosa katika uhariri wao, hivyo ni lazima apatikane mtaalamu wa mwisho kuipitia kazi kabla ya kuchapishwa

Utofauti

Baada ya mhariri kupitia mswada wako ni lazima kazi iende kwa msomaji prufu, ili ipate mapitio tofauti na ya awali, si vyema kazi moja kufanyiwa uhariri na usomaji prufu na mtu mmoja, hii hupelekea uchujufu wa kazi.

(+225) 715 001 818 | 787 001 819

info@uhariri.com