Utafiti

Utafiti ni msingi mkuu wa uandishi wa kazi ya kibunilizi, ambapo mtunzi anapaswa kufanya utafiti kabla ya kuandika kazi & wakati wa uandishi wa kazi yake. Msomaji wa kazi yoyote ya fasihi huvutwa na hadithi ambayo mtunzi wake ameonesha umakini katika vipengele mbalimbali ndani ya bunilizi yake. Kwa uzoefu wa kuhariri kazi mbalimbali za waandishi wa fasihi tutakubainishia baadhi ya maeneo makuu ambayo mtunzi anapaswa kuyafanyia kazi kama ifuatavyo.

1. Utafiti wa mandhari
Mtunzi wa kazi ya fasihi ni lazima afanye utafiti kuhusu maeneo anayotaraji wahusika wake watatokea, mathalani kama sehemu kubwa ya hadithi yako itakuwa imegusia mkoa wa Dodoma fanya utafiti kuhusu majina ya barabara, majina ya hoteli, baa, misikiti, makanisa unayotaraji kuyatumia au kuyataja. Kama kazi yako mhusika mkuu atafungwa gerezani kwa muda mrefu au hata mfupi ni muhimu kufanya utafiti kuhusu maisha ya gerezani kuhusiana na jinsi wanavyoamiliana, viongozi wa magereza na majukumu yao, adha wanazokabiliana nazo wafungwa, utaratibu wa kuwaona wafungwa au mahabusu n.k, , hebu twende mbali zaidi kuhusu suala la utafiti wa mandhari kwa kutoa mifano ya uhalisia wa kazi zilizofanyiwa utafiti wa mandhari.

“Stesheni ya Giningi ilikuwa kibanda kidogodogo cha matofali ya saruji, na juu yake kimeezekwa bati lenye rangi nyekundu. Pembeni huku na huku yamesimamishwa makalibu ya duara ya kukusanyia maji ya mvua, na chini yametiwa bulula”
Muhammed S. Abdullah – Kisima cha Giningi

Kazi nyingine ambazo waandishi wake wamefanya utafiti wa kutosha katika suala la mandhari ni kama vile Vipuli vya Figo iliyoandikwa na Profesa Emmanuel Mbogo, Mkimbizi iliyoandikwa na Hussein Tuwa, Mashimo ya Mfalme Sulemani iliyoandikwa na H. R. Haggard na riwaya ya Barua ndefu kama hii iliyotafsiriwa na Profesa C. Maganga.

2. Utafiti wa muda
Hii ni sehemu muhimu sana kufanyiwa utafiti wa kutosha hasa kama mwandishi hana uzoefu wa kutosha na eneo au kitu husika ambacho kimefungamanishwa na muda maalumu. Kwa mfano kama mwandishi hajawahi hata siku moja kupanda ndege kusafiri ndani au nje ya nchi anapaswa kuwa makini pale anapoweka muda maalumu katika eneo hilo laa sivyo atajikuta anazungumza kitu ambacho hakipo kabisa, hebu tuone mfano. 

“Bwana Kitwana Kadoda aliwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere dakika kumi na tano kabla ya ndege kuruka kuanza safari yake kuelekea Cape Town, akakata tiketi haraka na kuingia kwenye ile ndege kubwa aina ya Boeing”
Mfano wangu

Kwa taratibu za kusafiri uwanja wa ndege huwa ni tofauti na taratibu za usafiri wa magari yaendayo mikoani pale stendi ya mabasi ya Ubungo, dakika kumi na tano kabla ya ndege kuruka si kukata tiketi tu bali hata kuingia ndani ya ndege huwezi kuruhusiwa kutokana na utaratibu.  

3. Matumizi ya vitu
Eneo lingine la muhimu kufanyiwa utafiti ni katika matumizi ya vitu mbalimbali kama vile silaha, dawa, sumu n.k kulingana na mwegamo na mtiririko wa bunilizi yako. Kama uandishi wako umejikita katika ujasusi na upelelezi ni lazima ufanye utafiti wa kutosha katika matumizi ya silaha mbalimbali kama vile visu, bastola, waya, saa, kalamu na vitu vingine vinavyoweza kutumika kama silaha kulingana na muktadha husika hili litakusaidia kuendana na uhalisia wa matumizi ya silaha husika laa sivyo utajikuta umeandika kitu cha ajabu.

“John Mafuru alishika kwa makini bastola yake aina ya Chinese na kumshindilia yule gaidi risasi kumi na mbili zilizozama kila sehemu ya mwili wake”
Mfano wangu

Hapa kwa mtu anayeijua bastola aina ya Chinese atakushangaa sana, kwani bastola hii ina uwezo wa kubeba risasi nane tu.  Yaweza kuwa unazungumzia aina nyingine ya bastola na si Chinese.

4. Utafiti katika matumizi ya Lugha
Utafiti huu unategemea na aina ya hadithi unayoiandika imebeba wahusika wa aina gani? Kwa kigezo cha umri, kabila, kazi, jinsia, cheo, muda, n.k. Hapa jitahidi mhusika mtoto awe na lugha ya kitoto kama huifahamu kafanye utafiti walau kidogo, kama kazi yako mandhari yake imejikita Pwani au Bara ni vyema kujua matumizi ya lugha ya watu wa maeneo hayo kama wahusika wako watakuwa wametokea maeneo hayo na wana athari za lugha mama, kwa mfano baadhi ya jamii huchanganya matumizi ya herufi ‘r’ & ‘l’, ‘s’ & ‘th’, ‘z’ & ‘dh’. Tuangalie mfano wa utafiti wa lugha ya wafungwa gerezani.

“Oyaaa Santana hapa, nishapewa upepo na nyapara, kuanzia sasa hakuna mtu yoyote kuzungumza. Kama yeye siyo kiongozi humu. Wala hakuna kumokee! Hapa ni mwendo wa kimya hadi nyapara atengue cheo changu ”
Ibrahim Gama – Balaa

Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa mhusika askari avae lugha ya kiuaskari, mhusika mtoto avae lugha ya kitoto, labda kuwepo na mazingira tofauti yatakayopelekea ukiushi.

5. Utafiti wa masuala ya kitaaluma
Mara nyingi kazi ya kibunilizi hugusa maeneo mbalimbali ya kitaaluma kama vile sheria, afya, usalama, usafirishaji, ugavi na ununuzi. Ni nadra kukuta binadamu mmoja anafahamu kwa undani fani zaidi ya tatu na kuendelea kutokana na mifumo yetu ya elimu na watu wengi kupenda kubobea katika fani moja. Ni vyema mwandishi kufanya utafiti wa masuala madogo hasa yale ambayo hana uhakika nayo kuhusiana na taaluma fulani, kwa mfano kama katika kazi yako kuna mhusika atahukumiwa kunyongwa au hukumu nyingine yoyote basi tafiti walau sheria mbili tatu kuhusiana na hukumu hiyo, na ikitokea atakata rufaa basi chunguza taratibu za kukata rufaa zikoje.

“Ndio ni lazima kupata nakala ya hukumu pamoja na tuzo, yaani decree. Kisheria, huwezi kukata rufaa bila nakala ya hukumu…”
Hamis Kibari – Gereza la Kifo

Kila kada ya kitaaluma ina kaida zake zinazoiongoza katika ufanyaji wa mambo kwa usahihi, kama riwaya yako imegusia suala la utakatishaji fedha ni vyema kuwaona wanauchumi kukueleza namna suala hili linavyojitokeza, kama unahitaji kujua masuala ya kiusalama basi waone polisi au taasisi nyingine za kiusalama kwa ajili ya ushauri.

Baada ya kuona baadhi ya maeneo ambayo mwandishi anaweza kufanya utafiti wa kina ili kuboresha mswada wake, sasa tuangalie njia ambazo anaweza kuzitumia kufanya utafiti.

NJIA ZA KUFANYA UTAFITI

Zipo njia nyingi unazoweza kuzitumia kufahamu taarifa muhimu unazohitaji ikiwapo usomaji wa vitabu, kufanya mahojiano, kuangalia filamu mahususi n.k, katika sehemu hii tutagusia baadhi ya njia muhimu ambazo mwandishi anaweza kuzitumia katika kufanya utafiti wakati wa uandishi wa mswada wake.

1. Kufanya mahojiano
Kama unataka kufahamu kuhusu matumizi ya nusu kaputi basi mtu sahihi kumtafuta ni mtaalamu wa nusu kaputi kwani si kila daktari anafahamu namna inavyotumika na inavyofanya kazi katika mwili wa mwanadamu, kama unahitaji taarifa muhimu kuhusu wadunguaji (Snipers) basi tafuta mwanajeshi mwenye fani hiyo, hii itakusaidia kupata taarifa sahihi kutoka kwa mtu sahihi na muhimu zaidi taarifa hizo zinaweza kukusaidia hata katika ujenzi vitushi na wahusika wako.
Angalizo: Mosi watu wenye taaluma zao muda mwingine kuna usumbufu katika kuwapata chagua watu wawili watatu kisha anza kuwafuatilia ukiwa na subira na uvumilivu, pili ni vyema ukafahamu walau ABC ya kitu unachokwenda kuhoji ili kunogesha mahojiano yenu.

2. Nenda katika eneo husika
Msomaji wa kazi ya fasihi hujisikia raha sana pale ambapo mwandishi atataja sehemu ambayo anaifahamu vizuri, ukiwa mwandishi makini hupaswi kila mara kueleza mandhari ya kazi yako kwa juu juu tu, baadhi ya mandhari jaribu kuziwekea ufafanuzi wa kina kama waweza kufika sehemu ya Mandhari ya kazi yako fika katika sehemu hiyo kutafuta mawili matatu ikiwepo mandhari na taratibu za maisha ya sehemu hiyo au ofisi hiyo. Kama majambazi watakimbizwa basi jitahidi kutaja barabara walizopitia walau hata kwa uchache. Kama ukihitaji kutembelea ofisi au kampuni fulani basi andika barua ya kuomba kufanya hivyo yenye maelezo yenye kujitosheleza.

3. Usomaji wa vitabu
Usomaji wa vitabu na rejea nyingine ni katika vitu muhimu vinavyosaidia kupanua ufahamu, soma vitabu vingi kadri uwezavyo au kusikiliza vitabu vilivyowekwa katika mfumo wa sauti vinavyohusu suala ambalo umekusudia liwe kiini cha kitabu chako au ambalo litatumika kukuelekeza kwenye kiini cha kazi yako. Katika kufanya utafiti pia waweza soma makala mbalimbali kuhusu suala mahususi ulilolikusudia au kusoma katika vyanzo mbalimbali.
Ni vyema kubaini mwegamo wako wa uandishi yaani uandishi wako umeegamia katika mkondo wa kijasusi, kihistoria au mikondo mingine, ukishabaini penda kusoma kazi nyingi za mwegamo wako hasa za waandishi makini au wanaofanya vizuri sokoni kutoka ndani na nje ya nchi. Pia usisahau kusoma vitabu vya waandishi wengine wasio wa mkondo wako kwa lengo la kujifunza.

4. Kuangalia filamu, documentary na video mbalimbali.
Dunia imekuwa kama kijiji popote ulipo unaweza kupata taarifa uitakayo kupitia mtandao wa intaneti. Hivyo ni vyema kutenga muda kidogo kutafiti vitu unavyohitaji kupitia njia ya kuangalia, jambo kubwa na la msingi ni kuangalia kwa kutafuta taarifa mahususi. Kwa mfano unaweza kuandika katika mtandao wa YouTube ‘How to use AK 47’ kisha nenda kwenye taarifa mahususi achana na habari za ilitengenezwa lini na nani aliyeitengeneza (tafuta taarifa mahususi). Maarifa mengi katika mtandao yanapatikana kwa lugha ya kingereza hivyo usitafute ‘Jinsi ya kutumia AK 47’ tafuta taarifa mahususi kwa kutumia lugha ya Kiingereza.

5. Uliza wanaofahamu
Kama kuna jambo dogo linakutatiza ni vyema kuwauliza wanaofahamu kwani katika dunia hii kila mtu kuna analo fahamu yaweza kuwa vigumu kwa Juma Sembe kufahamu bei ya supu Tandale kuliko Athumani Mningo. Kama unashida ya kufahamu ni mwaka gani Azam TV ilianzishwa basi mtafute mtu anayeweza kukupa taarifa hiyo kwa usahihi wake laa sivyo utajikuta muda wa matukio ya kitabu chako hauendani na uhalisia wa yale unayoyazungumza. Mfano matukio ya kitabu chako yamejikita mwaka 2000 halafu unaiambia hadhira yako “John aliwasha king’amuzi cha Azam nakuanza kutafuta  stesheni aliyoikusudia…”, wakati mwaka 2000 hakukuwa na ving’amuzi.