Turufu ya Mwisho

Hamisi Kibari

Aliporejea Tanzania baada ya miaka saba, alikuwa na matumaini makubwa ya kumkuta mdogo wake akiendelea na shule vyema na kisha kuondoka naye kwenda kuishi Marekani. Hakuamini alichokuta mdogo wake kafanyiwa na hatari ya kifo iliyokuwa inamkabili. Licha ya kupambana ili kumwokoa, akajikuta katikati ya machozi.

Alipoamua kumweka ndani babu yake, akajikuta matatani zaidi. Akaamua kugombea ubunge ambao uligeuka kuwa kaa la moto lakini hakurudi nyuma… Hizi ni kurasa zinazokuhakikishia kwamba wanawake wanaweza!

 

Mh! Hatunaye tena duniani

BAADA ya kuweka mizigo yake sawia kwenye hoteli aliyofikia katikati ya mji wa Dodoma, masanduku mawili makubwa na begi, Marina alitoka akiwa na mkoba wake mdogo tayari kumtafuta rafiki yake kipenzi, Stella. Huyu ni mmoja wa watu wawili aliokuwa akiwaza sana njia nzima kukutana nao tangu alipoanza safari ya kutoka New York, Marekani kuja Tanzania, wa kwanza akiwa mdogo wake.

Kwa vile hakuwa na haja ya kujimwagia maji wala kula kwa sababu alikuwa ameshiba, hakuona sababu ya kuchelewa kumtafuta Stella. Alitoka nje na kusimama kwa muda akishangaa mabadiliko makubwa yaliyokuwa yamefikiwa katika mji wa Dodoma. Aliita teksi pale nje ya hoteli alikofikia na kumtaka dereva ampeleke mtaa wa Makole.

Miaka saba ni mingi, lakini aliamini hata kama Stella atakuwa amehama anaweza kupata taarifa zake kwenye nyumba aliyomwacha akiishi, pale Makole, nyumba ambayo hata yeye alipata kuishi pia. Pamoja na mabadiliko ya mji aliyoyaona toka amewasili Dodoma, maeneo ya katikati ya mji yalikuwa hayajabadilika sana kiasi cha kumpoteza.

Baada ya kutua na ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma mchana huo akitoka Dar es Salaam alikolala kwa siku moja akitokea Marekani, Marina hakupanga kwenda kijijini kwao, Mtakuja, Mayamaya, siku hiyo hiyo ili kupata muda wa kuongea na rafiki yake, Stella.

Pamoja na shauku kubwa aliyokuwa nayo ya kumwona mdogo wake, Marina alitaka jioni hiyo na hata siku ya pili yake ikiwezekana kuwa na rafiki yake kipenzi, Stella, wakiongea mengi na kukumbushana ya zamani baada ya kuachana kwa muda mrefu. Alitaka pia ajue anachokifanya kwa sasa na kuona namna ya kumsaidia. Mambo mengi yalikuwa kichwani mwake kuhusu namna ya kumsaidia Stella kama angemkuta kama alivyomwacha; je amfungulie duka la vipodozi, mgahawa, saluni ya kisasa ama chochote atakachotaka alimradi mtaji wake usiwe unavuka shilingi milioni 15.

 

Naam, hatimaye teksi ilisimama kwenye nyumba aliyomwelekeza dereva. Akashuka, akamlipa dereva ujira wake na kuchukua namba yake ya simu. “Nitakupigia uje unichukue unirudishe pale uliponitoa ama kunipeleka kwingine nikishamaliza mazungumzo yangu hapa… No, hebu tafadhali nisuburi kwanza pengine ninayemfuata hapa akawa keshahama.”

“Hamna taabu sister, isipokuwa ukumbuke nitakuchaji kidogo gharama za kusubiria,” akasema dereva. Bila shaka mwonekano wa binti huyo mrembo, pochi yake pamoja na mavazi yake nadhifu, suti ya kike ya rangi ya kahawia, viatu ambavyo dereva huyo alikuwa hajawahi kuviona na hata hoteli alimotokea vilionesha kwamba hawezi kukosa pesa ya kumwongezea kwa ajili ya kumsubiri. Kwa hakika mtu aliyemwona miaka saba iliyopita asingeweza kumtambua kwa jinsi alivyokuwa amebadilika.

“Usiwe na wasiwasi kaka,” alijibu Marina akigeuka kujongea kwenye mlango wa nyumba ya kizamani iliyokuwa imesimama mbele yake, nyumba ambayo takribani miaka saba au minane iliyopita aliishi akiwa na Stella.

Pale nje kwenye msingi wa nyumba hiyo hakukuwa na watu tofauti na alivyozoea zamani. Ilikuwa ni kawaida muda kama huo wa baada ya chakula cha mchana kwa kaya nyingi, mama mwenye nyumba na mabinti zake kukaa hadi baadhi yao watakapoanza matayarisho ya chakula cha usiku. Hata ile stuli aliyozoea kuiona mbele ya nyumba hiyo ikiwa na sinia la karanga alizokuwa akikaanga mama mwenye nyumba haikuwepo.

Marina aligonga mlango. Baada ya muda mlango ukafunguliwa. Alikuwa ni mama mwenye nyumba aliyekuja kufungua.

“Shikamoo mama. Habari za masiku,” alisalimia Marina akiachia tabasamu ikiwa ni mara ya kwanza kumwona mtu anayemfahamu tangu arejee Tanzania. Yule mama aliitikia huku akimwangalia usoni akitafakari yule ni nani. Marina akaona amwache tu yule dereva aondoke kwa sababu hata kama Stella alishahama nyumba hiyo alihitaji kuzungumza mawili matatu na mama huyo.

“Samahani kidogo mama. Nashukuru nimekukuta, ngoja kwanza nimuage huyu dereva,” alisema akigeuka kumfuata dereva teksi,  akamwambia aondoke na kwamba atampigia simu baada ya kumaliza kilichomleta katika nyumba hiyo.

“Karibu ndani mwanangu,” alisema mwanamke yule mtu mzima, Khadija binti Zubeir maarufu pale mtaani kama Mama Siwema, bado akijiuliza ni wapi alipomwona binti huyo mrembo.

Wakaongozana hadi sebuleni kwake, sebule ambayo Marina aligundua kwamba ilikuwa imezidi kuchakaa na hakuna kilichokuwa kimeongezeka. Mama yule mjane wa miaka takribani 15 akamkaribisha aketi kwenye kochi mojawapo lililokuwa na afadhali kidogo. Mengine yalikuwa yamechanika, sponji zake zikiwa nje huku lile kochi kubwa likiwa limevunjika.

Kulikuwa na meza kuukuu pembeni kidogo mwa sebule hiyo ambayo bila shaka ilitengenezwa kwa ajili ya kulia lakini ilikuwa haitumiki kwa ajili hiyo badala yake ilijaa makorokoro kibao.

“Hebu nikumbushe binti. Sura inaniijia halafu inatoka.”

“Mama umenisahau?”

“Yaani… uzee mwanangu. Ninajitahidi kukukumbuka bila mafanikio.”

“Haiwezekani Mama Siwema.”

“Kweli nimekusahau, macho nayo siku hizi sioni vizuri.”

“Ulishapima macho ili wakupe miwani?”

“Bado mwanangu, pesa nitapata wapi miye.”

“Basi nitakupa pesa, kesho ukapime. Siku nikija tena utaniambia gharama za miwani,” alisema akitoa shilingi 30,000 na kumpatia.

“Nashukuru sana mwanangu.”

“Mimi ni Marina, rafiki yake Stella mpangaji wako.”

“Ah! Marina, umebadilika sana. Umependeza. Kweli Ulaya si mchezo. Nasikia uliolewa Ulaya eh!”

“Si Ulaya, ni Marekani mama.”

“Ndo huko huko… Haya hebu niambie kuna habari gani mpya?”

“Hakuna jipya. Nimefika leo nikaona niwasalimie. Kwa kweli nimewakumbuka sana na nimefurahi sana kukuona.”

“Kweli ni siku nyingi. Miaka 10 sasa eh?”

“Siyo 10, ni miaka saba tu.”

“Hata hiyo mingi mwanangu.”

Yeah, vipi Stella, bado anaishi hapa?”

“Mh….” aliguna mama yule na kuinama huku uso wake ukibadilika. Alisita kidogo, akakohoa kisha akanyanyua tena uso. “Rafiki yako Stella hatunaye tena duniani. Alifariki dunia mwaka juzi… Lakini hadi anafariki alikuwa keshahama hapa. Alikuwa anaishi Kizota.”

Maneno yale yalimkata Marina moyoni mithili ya upanga mkali. Akajikuta anabubujikwa na machozi ghafla licha ya kuyazuia bila mafanikio kiasi cha Mama Siwema kuanza kibarua cha kumbembeleza ili kunyamaza.

Baada ya kutulia Mama Siwema hakutaka kumficha. Akamwambia kwamba rafiki yake alifariki dunia baada ya kuugua ugonjwa aliouita wa ‘kisasa’ akimaanisha Ukimwi.

“Lakini yule kilichomuua ni kutofuata masharti na uoga wa kupima. Unajua alianza kuugua hapa akaonesha kila dalili. Aliugua Kifua Kikuu na baadaye mkanda wa jeshi. Lakini mbishi wa kwenda hospitali, msiri na hataki kuwa muwazi. Mimi kama mtu mzima nilimwita, nikamweleza awaone watalaamu badala ya kudai anarogwa na wenzake na kuanza kwenda kwa waganga wa jadi lakini mwanangu wahenga walisema kweli, sikio la kufa halisikii dawa. Hakunisikia,” akasema Mama Siwema.

Akazidi kumwambia kwamba mke wa mdogo wake ambaye ni marehemu anaishi na ugonjwa huo kwa takriban miaka 15 sasa lakini ana afya njema na wala ukimwona huwezi kuamini kwamba ana tatizo hilo kwa sababu anafuata masharti na si msiri.

“Mdogo wangu ambaye ndiye alimletea huu ugonjwa alishakufa miaka mingi hata kabla rafiki yako hajaja kupanga hapa kwangu. Naye alikuwa kama huyo rafiki yako, anaogopa kupima na kuwa muwazi. Lakini wifi ni muwazi, hana wasiwasi  na ndio maana huwezi kujua kwamba anaishi na huu ugonjwa mpaka akwambie au uambiwe. Na siku hizi kaolewa na mwenzake anayeishi na ugonjwa huo. Maisha yao mazuri kabisa.”

Sitaki yawakute yaliyonikuta

 

AKIWA bado amegubikwa na huzuni kutokana na maneno aliyoambiwa kwamba Stella hayuko hai, Marina aliamua siku yake ya pili kuwa Dodoma kuzunguka madukani ili kuangalia mabadiliko yaliyopo na kuona kama kuna zawadi zozote za ziada anazoweza kumchukulia mdogo wake, mjomba wake, babu na bibi yake, mbali na alizotoka nazo Marekani.

Hakuona kitu cha maana sana zaidi ya nguo alizoongeza kwa ajili ya mdogo wake huku akiwa hana uhakika kama zingemtosha kwa kuwa alimwacha akiwa hajaanza shule na sasa aliamini yuko darasa la tano au la sita kama hawakumchelewesha. Akatembelea pia soko kuu la Dodoma ambako alinunua asali mbichi kwenye kidumu cha lita tano na kisha kurejea hotelini alikofikia.

Aliangalia saa yake. Ilikuwa inaelekea saa 10 alasiri. Akaona ule ulikuwa muda mwafaka wa kuondoka. Akampigia simu dereva teksi aje ampeleke Mayamaya.

“Niko hapa jirani tu dada. Nakuja,” alijibu dereva teksi ambaye tangu awasili Dodoma jana yake alikuwa akizunguka naye na kupenda huduma zake.

Alijikuta macho yake yakilowa machozi baada ya kumbukumbu za rafiki yake Stella kumwijia tena. Mengi aliyokuwa amepanga kufanya naye ikiwa ni pamoja na kwenda naye kijijini Mayamaya yaliyeyuka. Asubuhi hiyo alikwenda kuona kaburi lake akiwa ameandamana na mmoja wa watoto wa Mama Siwema, hatua iliyomthibitishia ukweli kwamba Stella kweli hakuwepo tena duniani.

Hatua hiyo ilimpa uzito wa kuondoka mapema kwenda kijijini kwao, akaona ni vyema aende jioni. Alitaka sasa aingie karibu na giza kijijini kwao.

Akiwa sasa amejilaza kitandani akimsubiri dereva teksi, alianza kukumbuka siku ya kwanza aliyokutana na Stella. Ilikuwa darasa la sita katika Shule ya Msingi Jamhuri ya mjini Dodoma baada ya mama yake kumhamisha kutoka Mayamaya kwa babu yake alikokuwa akisomea.

Alihamishwa kutokana na babu yake kutaka kumkeketa, jambo ambalo mama yake aliyekuwa akifanya kazi ya uhudumu katika Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), alikuwa akilipinga sana.

Mama yake ambaye pia ni marehemu alipojua mpango huo wa mwanawe kukeketwa alimfuata kijijini haraka na kuamua kuishi naye katika chumba kimoja alichokuwa amepanga. Mama huyo ambaye mshahara wake wa kima cha chini ulikuwa mdogo, sasa akawa anaishi na wanawe wawili; Marina na Celine ambaye alikuwa na umri wa takribani miaka mitatu. Watoto wote aliwazaa na wanaume tofauti na hadi mama huyo anafariki dunia, hakuwahi kumtajia Marina baba yake mzazi wala baba wa mdogo wake, Celine.

Kwenye shule mpya alikohamia ndiko alikutana na Stella waliyekuwa pia wakiishi jirani katika mtaa wa Changanyikeni na kujikuta wakiwa marafiki. Stella ambaye inaonekana alichelewa kuanza shule kama yeye Marina, alikuwa mkubwa kidogo kiumri kumzidi, wakipishana kwa mwaka mmoja na nusu na labda ndio maana akiwa darasa la tano tu akapewa ukiranja mkuu ama wenyewe wakimwita dada mkuu pale shuleni. Katika darasa lao, wao ndio walikuwa wakubwa zaidi kulinganisha na wenzao hali ambayo pia ilichangia urafiki wao.

Marina, akiwa amejilaza kitandani, huku machozi yakimbubujika, alimkumbuka pia marehemu mama yake aliyezidiwa sana kutokana na ugonjwa ambao wengi wanaamini kwamba ni wa ‘kisasa’, wakati yeye akisubiri majibu baada ya kuhitimu darasa la saba.

Mama yake alifariki dunia siku ambayo majibu ya mtihani wao wa darasa la saba yalitoka. Katika shule yao iliyokuwa ikilalamikiwa na wazazi kwa kutofaulisha watoto kwa wingi wakati huo, alikuwa msichana pekee miongoni mwa wanafunzi watano waliofaulu. Lakini kifo cha mama yake kikawa sababu ya kushindwa kuendelea na masomo.

Marina alikumbuka siku alizokuwa akimuuguza mama yake katika chumba kidogo cha kupanga, kwenye nyumba ambayo ilikuwa haina umeme. Mama yake alimsisitiza kwamba hata kama atafariki dunia, asithubutu yeye na mdogo wake kukubali kukeketwa.

“Mwanangu, naona kama sitapona ugonjwa huu. Endapo nitafariki dunia, mtarudi kwa babu yenu… Hakuna mwingine wa kuwalea hapa mjini. Lakini babu yenu akitaka kuwakeketa mkatae katakata… Mimi nimekeketwa lakini sitaki wanangu mfanyiwe hivyo abadani. Nimeona madhara yake na kwa kweli ni mila ya kipuuzi sana. Haifai, na inaweza kusababisha vifo. Mwenyewe nimeshuhudia hilo.”

Akakumbuka alipomuuliza kuhusu madhara ya kukeketwa kwa sababu aliona kama wasichana wenzake kijijini wanafurahia kukeketwa, akamjibu: “Madhara makubwa ni kusababisha kifo kama nilivyosema lakini unapata maumivu makali bila sababu, unabaki na kovu sehemu za siri ambalo limekuwa likiniletea shida sana wakati wa kuwazaa wewe na mdogo wako, halafu pale utakapoolewa, mwenzio atakuwa na kazi ya ziada ili kukuandaa mfanye tendo la ndoa. Lakini baya zaidi siku mumeo akikutana na mwanamke ambaye hajakeketwa anakukimbia. Baba wa mdogo wako alinikimbia kwa sababu hiyo. Hii ni mila ya ovyo ya kumkandamiza mwanamke na haina maana kabisa katika zama hizi.”

Alipomuuliza kuhusu baba yake, kwanza alikaa kimya, akabadilika sura na kukunja uso. Na hii haikuwa mara yake ya kwanza kuonesha kwamba hakulipenda swali hilo. Zilipita sekunde chache za ukimya kisha mama yake alimwambia asisumbuke kuulizia baba wa ovyo ambaye hajawahi hata kutaka kujua mtoto wake ana hali gani, anakula nini na anavaa nini. “Mwanangu, mimi ndiye baba yako, mimi ndiye mama yako, hakuna mwingine,” akamwambia kwa msisitizo.

Marina alizidi kutokwa machozi, kwani hadi wakati huo hakujua kinachoendelea kwa mdogo wake Celine huko kijijini. Pengine alishakeketwa. Alimwomba sana Mungu hilo lisiwe limetokea.

Marina akaendelea kukumbuka kauli za mwisho za mama yake akiwa amelala kwenye kitanda cha mauti. Machozi yalizidi kumtoka pale kitandani akasahau kabisa kwamba dereva teksi pengine alikuwa nje akimsubiri kumpeleka Mayamaya jioni hiyo.

“Lingine mwanangu, wewe ni binti mrembo kadiri ninavyokuona. Unazidi kuwa mwali na bila shaka wanaume wengi watakufuatafuata kwa tamaa zao tu za kishetani lakini hawana lolote. Watakuharibia maisha tu. Mimi mama yako nimejifunza mengi sana. Unaona ninawalea peke yangu kwa tabu, huku baba zenu wakinikimbia.

Hawana maana na hawana msaada baadhi ya wanaume. Mwanangu, mwanaume yeyote atakayekufuata, mwambie kama anakutaka, basi akuoe kwa taratibu zinazoeleweka, na si vinginevyo. Dunia pia imeharibika. Sitaki yawakute yaliyonikuta mimi. Kuna Ukimwi mwanangu. Nitazame mama yako ninavyoteseka,” Marina alizidi kukumbuka kauli za mama yake. Alikuwa akimwambia mambo mazito ambayo wakati huo hakuyatilia maanani sana kutokana na umri wake mdogo.

Baada ya mama yake kufariki dunia, Marina na mdogo wake, walilazimika kurejea Mayamaya, katika kijiji cha Mtakuja kwa babu yao ambako ndiko pia msiba ulifanyika. Wakati huo mdogo wake, Celine, alikuwa na umri wa miaka mitano.

 

Rudini kwa baba yenu

MARINA aliendelea kukumbuka namna alivyotoroka Mayamaya baada ya majogoo kuwika akiwa na mdogo wake huyo, Celine, siku ambayo alikuwa amepangiwa, yeye na mabinti wengine sita pale kijijini kupelekwa kwa ngariba ili kukeketwa baada ya jaribio la kwanza kutibuliwa na mama yake. Mdogo wake hakuwa miongoni mwa wale ambao walipaswa kukeketwa siku hiyo kwa vile alikuwa hajafikisha umri unaotakiwa, lakini akaamua kuondoka naye.

Babu yake alikuwa anatarajia baada ya Marina kukeketwa, amtafutie mchumba wa kumuoa bila kujali kwamba alikuwa hajafikisha umri unaofaa kuolewa. Kutokana na urembo aliokuwa nao, watu wa aina hiyo, wengi wakiwa watu wazima, walikuwa wameanza kujitokeza kutaka kuleta posa baada ya kusikia alikuwa keshamaliza darasa la saba na yuko kwenye mpango wa kukeketwa.

Pesa zilizomsaidia yeye na mdogo wake kutoroka kwa ajili ya kupanda magari alikuwa amepewa na rafiki mkubwa wa mama yake, Mwanaidi Jumanne, aliyekuwa amewatembelea kijijini hapo kuwajulia hali miezi mitano baada ya mama yao kufariki dunia.

Wakati akimsindikiza, ndipo mwanamke huyo akatoa shilingi 30,000 akampa imsaidie kununua vitu vidogo vidogo kama mafuta, sabuni, kandambili na nguo za ndani yeye na mdogo wake pamoja na taulo za kike za usafi kwa kuwa Mwanaidi alijua kwamba alishapevuka.

Katika kipindi hicho, Marina alikuwa na taarifa kwamba tayari shule ya bweni ya sekondari ya watoto wenye vipaji maalumu ya Msalato aliyokuwa anapaswa kwenda ilikuwa imeshafunguliwa takribani miezi mitatu na ushei iliyokuwa imepita na hivyo wanafunzi wenzake wa kidato cha kwanza walikuwa wakiendelea na masomo. Lakini babu yake, Mzee Nhonya Chilyawanhu, alikuwa amesema hana pesa za kuchezea kwa kusomesha mtoto wa kike.

“Marehemu mama yenu hakuwa amesoma zaidi ya darasa la saba lakini alipokwenda hapo mjini, akapata kibarua tena kwa msaada wa kijana wangu ambaye sasa ni mbunge akaanza kujifanya msomi, mtu wa kisasa anadharau hata mila zetu, sembuse wewe ukihitimu kidato cha nne si ndio utatupanda kichwani kabisa,” Marina alizidi kukumbuka maneno ya babu yake.

Alikumbuka alivyohangaika na mdogo wake usiku usiku, wakipita vichakani na sehemu za hatari huku wakati mwingine akilazimika kumbeba mgongoni hadi Mayamaya Madukani ambapo walisubiria usafiri wa kuwapeleka mjini.

Lengo lake lilikuwa ni kwenda kwa rafiki wa mama yake huyo, Mwanaidi, na kuona namna anavyoweza kumsaidia kuepuka kukeketwa. Kwa vile alikuwa hakumbuki vyema mahala alikokuwa akiishi, alikuwa amedhamiria kumfuata ofisini na kwa bahati siku hiyo ilikuwa ya kazi.

Saa tatu na dakika kadhaa asubuhi, Marina akiwa na mdogo wake walishuka kwenye lori la mkaa walilopanda baada ya kufika katikati ya mji wa Dodoma. Huo ndio ulikuwa usafiri maarufu wa eneo hilo wakati huo. Hakuna aliyekuwa anapeleka huko gari lake la maana kutokana na ubovu wa barabara.

Baada ya kuwasili mjini, Marina na mdogo wake wakaenda moja kwa moja hadi katika ofisi za Ustawishaji Makao Mkuu Dodoma (CDA), alikokuwa akifanya kazi mama yao kuonana na rafiki wa mama yao huyo, Mwanaidi.

Pale getini walikutana na mlinzi mwenye huruma ambaye aliwapa mahala pa kusubiria kwani aliwaambia Mwanaidi alikuwa amekwenda kunywa chai mtaa wa pili. Saa nne na nusu, Mwanaidi alikuwa anakutana na wageni wake. Alionyesha mshangao mkubwa kuwaona.

 “Mama sisi tumetoroka. Asubuhi hii babu alikuwa anipeleke kwa ngariba kukeketwa na marehemu mama alisema nisikubali katu kufanyiwa hivyo,” alisema Marina aliyechangamka baada ya kumwona Mwanaidi, rafiki mkubwa wa marehemu mama yao.

 “Loh, makubwa. Sasa…?”

 “Tumeona tuje kwako, mama, utusaidie.”

“Niwasaidie? Mimi nitawasaidiaje… Haiwezekani, rudini mara moja kwa babu yenu. Kwa nini unaogopa kukeketwa wakati ni mila yenu? Rudini kwa babu yenu nyie watoto,” alisema kwa hasira akitoa pesa kwenye pochi yake kwa ajili ya nauli.

Marina na mdogo wake walibaki wameshangaa. Huyo ni mwanamke aliyekuwa sawa na ndugu wa damu wa mama yao. Hakutaka hata kuwakaribisha nyumbani ama kuandamana nao hadi kijijini kuongea na babu yao.

“Haya, msije mkanizulia jambo. Rudini sasa hivi kijijini. Nikiwakuta kokote hapa mjini nitawaitia polisi,” alimaka mwanamke yule mrefu, mweupe ambaye asili yake ni Nzega, Tabora.

Marina alikumbuka namna walivyoondoka eneo hilo akiwa na mdogo wake akitafakari kuhusu kurejea Mayamaya ama la. Akaanza safari kuelekea pasipojulikana akiwa na mdogo wake ambaye alionekana amechoka sana na kutamani kulala kutokana na kuamka usiku.

Wakati akiendelea kuwaza akiwa pale kitandani, yule dereva wa teksi aliyekuwa ameshasubiri kwa muda nje ya hoteli hiyo alimgongea na kumshitua kutoka kwenye lindi la mawazo.

“Dada vipi? Kama hujawa tayari kuondoka niruhusu nikimbie maeneo ya stendi kuna mteja wangu mmoja ananipigia simu. Ninajua anakokwenda kama bado ngoja nimkimbize,” alisema, yule dereva akiwa nje ya mlango wa chumba alichokuwa amepanga Marina katika Hoteli ya Blue.

“Hapana tunaondoka sasa hivi. Ingia unisaidie haya masanduku.”

Dereva teksi alimpigia simu mteja wake na kumtaka atafute usafiri mwingine, kisha akaanza kubeba sanduku la kwanza ambalo lilikuwa zito sana na kulipeleka kwenye teksi, akarudia lingine pamoja na begi huku Marina akitumia nafasi hiyo kwenda kumuaga meneja wa hoteli hiyo aliyeonekana mtu mkarimu, aliyemsikia akiitwa kwa jina la Theonestina Nyaru.

Safari ya Mayamaya

SAFARI ya kwenda Mayamaya ilipoanza, Marina akajikuta muda mwingi macho yake yakiangaza huku na kule kutazama mabadiliko ya mji wa Dodoma. Majengo marefu yalikuwa yamezidi kuongezeka.

Baada ya kupita Shule ya Wasichana ya Msalato ambako alipaswa kusoma kama mama yake asingefariki dunia, akajikuta akizama tena kwenye lindi la mawazo juu ya marehemu Stella na maisha yake Dodoma kabla ya kuondoka miaka saba iliyopita.

Kukuta Stella amefariki dunia ni jambo lililomhuzunisha sana sawa na siku alivyofariki dunia mama yake. Hakuamini, na kuna wakati alikuwa anataka itokee miujiza habari zile zisiwe za kweli. Hadi alipoona kaburi ndipo akaamini Stella yuko dunia nyingine ya wafu.

Alikumbuka namna siku ya kwanza waliposhinda wakiranda randa katika jiji la Dodoma baada ya Mwanaidi kukataa kuwasaidia, wakitoka mtaa mmoja hadi mwingine huku baadhi ya maeneo wakifukuzwa kukaa. Ilipofika mchana, alinunua chakula kwa mama lishe mmoja kutokana na akiba kidogo ya pesa aliyokuwa nayo. Walipomaliza kula, Marina akamwomba mama lishe huyo kazi ya kumsaidia shughuli na mahala pa kulala yeye na mdogo wake. Mama huyo akamshangaa.

“Kwanza sina shida ya msichana mwingine hapa, nilio nao wananitosha… halafu mnatokea wapi hadi mtake kuja kulala kwangu. Nikikaribisha vijizi kwangu je?” Alihoji mama huyo.

Baadaye akawa kama amekumbuka kitu. Akamuuliza Marina kama alishawahi kufanya kazi za ndani kwa sababu kuna jirani yake ana mtoto mchanga na anatakiwa kuanza kazi baada ya kuelekea kumaliza likizo ya uzazi na hivyo anatafuta msichana wa kazi za ndani.

Marina akakubali kwamba yupo tayari kufanya kazi za ndani na hasa kama atafuatana na mdogo wake.

“Ninakuhakikishia tutafanya kazi vizuri sana nikisaidiana na mdogo wangu ingawa kiukweli sijawahi kufanya kazi za ndani.”

“Yaani ukafanye kazi za ndani na mdogo wako? Nani anaweza kukubali mzigo huo… Kama unataka kazi mrudishe mdogo wako nyumbani halafu uje hapa nikupeleke ukafanye kazi, nadhani jirani yangu atakuwa hajapata mtu,” akasema yule mama.

“Nyumbani ni mbali mama, tusaidie.”

“Mbona sikuelewielewi? Hebu niondokee hapa. Nisije nikampelekea jirani msichana wa ajabu,” akamaka yule mama.

Marina alijaribu kubembeleza lakini ikawa kama anachochea ghadhabu za mwanamke huyo ambaye sasa alitishia kuwaitia polisi. Akaondoka na mdogo wake bila kujua wanakoelekea. Ilipofika jioni hakujua watalala wapi. Akapata wazo la kwenda darasani kwenye shule ya msingi aliyosoma. Walipofika mlinzi akawafukuza.

Wakati akifikiria pa kwenda na mdogo wake huku giza likizidi kutanda, Marina akakumbuka kwamba siku moja kuna mgeni alikuja kwa mama yake akasema alifika Dodoma usiku kwa treni na kulala stesheni. Hivyo akaamua kwenda huko ambako walifanikiwa kulala kwenye jumba la wasafiri sakafuni yeye na mdogo wake hadi asubuhi.

* * *

Kulipopambazuka akalazimika kutoka pale stesheni na mdogo wake kwenda mitaani tena. Wakati wanatoka kula chakula cha mchana kwa mama lishe mwingine na mdogo wake na kuanza tena kuzunguka wakitafuta mahala pa kukaa ili kuvuta muda huku roho ikikataa kurejea Mayamaya, ndipo Marina akakutana na Stella njiani.

Stella alifurahi sana kumwona, na haraka haraka akawakaribisha kwa bashasha kwenye chumba chake alichoita ghetto, katika mtaa wa Makole kwa Mama Siwema.

“Marina, nilijua uko sekondari, si ulishinda wewe… Nikawa natamani siku moja nije Msalato kukuona. Hata jana nimekufikiria sana,” akakumbuka Stella alivyomuuliza baada ya kuwasili chumbani kwake.

Marina alishangaa kugundua kwamba binti mdogo kama Stella aliyekuwa amemaliza darasa la saba kiasi cha miezi takribani mitano iliyokuwa imepita alikuwa anaweza kumiliki chumba kile. Je, alikuwa amemudu vipi kununua kitanda, jiko na vifaa vichache kwa ajili ya kupikia? Akawa anajiuliza.

“Stella, hiki ni chumba chako… Unakimiliki wewe?” Alihoji.

“Ndiyo. Nina miezi mitatu sasa toka nipange hapa. Si unajua wakati ule nilikuwa nasomea kwa mjomba ambaye amehamia Mpwapwa? Mimi sikutaka kwenda huko nikaamua kubaki hapa hapa Dodoma baada ya kupata kibarua.”

Marina ambaye alikuwa na shauku ya kutaka kujua anachokifanya Stella kuendesha maisha yake alimsimulia sababu ya kuwa mjini pale yeye na mdogo wake na jinsi walivyolazimika kulala stesheni. Habari zile zilimshitua sana Stella na hasa kugundua kwamba babu yake alikataa kumsomesha Marina kwa sababu ambazo hazikumwingia akilini.

“Utakaa hapa kwangu na mdogo wako tukitafakari cha kufanya,” alisema Stella, maneno yaliyomtia faraja kubwa Marina.

“Nina shauku ya kutaka kujua unaendeshaje maisha yako rafiki yangu,” hatimaye alihoji Marina. Hata, hivyo Stella alikwepa kujibu swali lile na badala yake akaanzisha hadithi nyingine.

Dereva wa gari dogo alilokuwa amepanda alizidi kukanyaga mafuta kuelekea Mayamaya. Kwa upande wa Marina aliendelea kuzama kwenye lindi la mawazo dhidi ya Stella, mtu ambaye baada ya kuambiwa kwamba hayupo duniani, sasa mkanda mzima wa urafiki wao ulikuwa umefunika kabisa ubongo wake.

Marina alikumbuka siku ya kwanza aliyoishi nyumbani kwa Stella akiwa na mdogo wake bila matatizo yoyote. Alikumbuka pia siku ya pili yake kumtaka Stella amweleze kile anachokifanya hadi kumudu maisha, akila vizuri na kulipia chumba ikiwa ni pamoja na kujinunulia baadhi ya vitu ambavyo wakati ule kwa umaskini wa familia yake aliviona kama vitu vya thamani sana kwake lakini Stella alimtaka kuvuta subira kwamba angemfahamisha tu kadri ambavyo wangeendelea kuishi pale pamoja.

Vitu vilivyomkosha Marina ni pamoja na kitanda kipana cha kisasa cha mbao na godoro la sponji ambalo wote watatu walilala bila matatizo, jiko la mkaa, vyombo kama glasi, masufuria na vijiko vilikuwa vitu vya mtu ‘tajiri’ kulinganisha na pale kwa babu yake. Kingine kilichomfanya Marina kuona Stella kashamudu maisha ni kumiliki seti ya runinga ndogo. Chumba cha Stella chenye umeme pia kilikuwa bora kidogo kulinganisha na kile alichokuwa akiishi mama yake.

Chumba hicho kilichokuwa kwenye mabanda ya uani kwa Mama Siwema, kilionekana kwake ni kizuri sana kulinganisha kile walichokuwa wakilala kwa babu yao, kwenye nyumba ya kienyeji aina ya tembe na kilichokuwa na mwanga hafifu. Kwa babu yake, yeye na mdogo wake Celine walikuwa wakilalia kitanda cha zamani cha chuma na godoro la sufi.

Karibu vitu vyote vya maana vya marehemu mama yake ikiwa ni pamoja na kitanda cha kisasa na godoro lake vilichukuliwa na babu yao, wajomba zake wawili na mama yao mkubwa aliyekuwa ameolewa Singida. Yeye aliambulia vitu kama nguo na viatu. Mdogo wake, Celine hakumbuki kama aligawiwa chochote.

Marina aliendelea kukumbuka kwamba alikaa kwa wiki moja akiwa pale kwa Stella, yeye na mdogo wake bila kujua mwenyeji wao alikuwa anafanya kazi gani.

Alichogundua katika wiki hiyo ni kwamba, kila siku Stella alikuwa akiondoka saa tisa mchana baada ya kuupara na kuvaa nguo za kubana ama fupi ambazo Marina aliziona si za staha sana kwa sababu zilikuwa zikimchora umbo lake ama kumwacha nusu uchi na kurejea usiku wa manane, akiwa amelewa na wakati mwingine harejei kabisa hadi asubuhi. Hilo la kulewa lilimshitua sana Marina.

Hata hivyo, kila Stella alipokuwa akiondoka na kuahidi kurudi usiku mwingi alikuwa anahakikisha amewaachia chakula yeye na mdogo wake au kuwaachia pesa ya kwenda kula chakula kwa mama lishe. Maisha pale kwa Stella yalikuwa pengine mazuri kidogo kulinganisha na kwa babu yake, hasa kwa kuzingatia kwamba walikuwa na uhakika wa kupata milo mitatu kwa siku, kuanzia chai hadi chakula cha usiku. Kule Mayamaya ratiba ya chai ilikuwa hakuna.

Marina alikumbuka kwamba Jumatatu, wiki iliyofuata toka afike pale, Stella alirejea usiku wa manane kama kawaida yake na saa nne asubuhi alipoamka, alimwambia kwamba siku hiyo alikuwa ana mapumziko ya siku moja na kwamba siku iliyofuata angeanza kwenda kazini asubuhi kwa wiki nzima.

“Sasa nilikuwa ninafikiria kwamba, kwa vile Celine kwa umri wake si rahisi kukeketwa, tumrejeshe Mayamaya kwa babu halafu wewe utarejea hapa na kisha nitakutafutia kazi kama hii ninayofanya,” alisema Stella bila kumwambia aina ya kazi anayofanya.

Marina alifikiri kidogo, ilikuwa ni vigumu kumkatalia mwenyeji na mfadhili wake ingawa hakupenda kuona mdogo wake anarejea kijijini. Kwa vile suala la shule lilikuwa limetoweka, aliona ni busara sasa kufanya kazi ili asiendelee kuwa tegemezi kwa Stella. Alimwona Stella kama mtu ambaye ameshayaweza maisha. Pamoja na umri mdogo wa miaka 15 na ushei huku Stella akiwa na miaka takribani 17, alitamani na yeye kupanga chumba kama cha Stella na kisha kuishi na mdogo wake.

“Ni sawa, tunaweza kwenda leo kwa sababu nina wasiwasi pia kwamba, babu japo sikuwa na jinsi isipokuwa kutoroka, atakuwa anahangaika kututafuta. Hajui tuko wapi,” alijibu Marina.

Saa nne asubuhi siku hiyo, waliondoka kwenda Mayamaya na kufika kwenye saa tisa jioni kutokana na shida ya usafiri. Nusura babu yake ammeze Marina kwa kuwataabisha kumtafuta kila mahala, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa polisi. Babu huyo alisema kesho yake walipanga kwenda kutoa picha zao kwenye magazeti.

“Kama ulikimbilia kwa wanaume, ungeenda mwenyewe. Kwa nini ukaondoka na mtoto?” Akawa anafoka babu yake.

Marina aliweka wazi kwamba kilichomfanya akimbie ni kupinga kukeketwa, jambo ambalo lilimfanya babu huyo aanze kumweleza alichoita umuhimu wa kukeketwa katika jamii yao.

“Marina, utachekwa na kila mtu na utakosa mwanaume wa kukuoa. Mbaya zaidi utasababisha mikosi kwako mwenyewe na kwa sisi jamaa zako. Hilo halikubaliki katika jamii yetu,” alisema babu yule, lakini Marina aliendelea kushikilia msimamo wake kwamba hataki kitu hicho na pia hataki kuona mdogo wake anafanyiwa kitendo hicho kama alivyousiwa na mama yao. Babu yake akazidi kusisitiza kwamba ni lazima akeketwe, hata kama si mwaka huo basi mwaka unaofuata.

Kwa jinsi hali ilivyokuwa pale nyumbani kwa babu yake, Marina na Stella walilazimika kutoroka, Marina akidanganya kwenda kuoga kisimani na mgeni wake.

“Babu tunakwenda kuoga, na tunarejea sasa hivi. Rafiki yangu atalala hapa, ataondoka kesho,” alidanganya Marina akiwa ameshika ndoo, sabuni na dodoki.

Baada ya kuruhusiwa na babu yao kwa shingo upande Marina na Stella waliondoka na kutelekeza ndoo katika eneo la karibu na boma la babu yao ili iwe rahisi kuonekana na wao wakaenda zao kutafuta usafiri wa kuwarejesha mjini.

Wakati huo ilikuwa inaelekea saa 11 jioni, saa ambazo walijua magari ya kwenda mjini yalianza kuwa ya taabu. Kwa bahati walipofika kwenye barabara kuu, Mayamaya Madukani, walifanikiwa kupata gari la mkaa la kuwapeleka Dodoma mjini.

Silazii damu mabwege

SIKU iliyofuata asubuhi saa 12, Stella alimchukua Marina hadi katika hoteli moja ya mama wa Kisomali ambako Marina sasa aligundua kwamba Stella alikuwa mhudumu wa hoteli hiyo ambayo pia ilikuwa na baa na tayari Marina alikuwa ameshamwombea kazi ya uhudumu. 

“Mimi ni mhudumu tu hapa kwa upande wa mgahawa na baa, lakini mama anapenda mabinti warembo na wadogo kama wewe kwa sababu anaamini wanavutia pia biashara yake. Umeumbika Marina, hawezi kukukataa,” alisema Stella wakiwa wameketi akisubiri kumkutanisha na bosi wake aliyemwita mama ambaye ndiye mmiliki wa hoteli hiyo.

“Hataniona mdogo?” Aliuliza Marina ambaye kwa urefu wake ungeweza kudhani mkubwa lakini alikuwa bado binti mdogo, akiwa hajafikisha umri wa miaka 18 unaotambulika kama wa mtu mzima.

“Hapa kuna wadogo hata kuliko wewe, utawaona. Kwanza mtu akikuona urefu wako hawezi kujua kwamba hujafikisha umri wa miaka 18. Hata mimi mwenyewe ndio nakaribia kufikisha miaka 18 lakini naonekana mkubwa tu na wala hakuna anayeuliza umri wa mtu hapa. Na wewe sasa hivi hutakiwi kujiona mdogo. Mama anachoangalia hapa ni kama maziwa yameshatoka, bahati nzuri yanaonekana, kingine ni uzuri. Pia anaangalia shepu na uchapa kazi. Mimi sina wasiwasi na wewe kwa hayo,” alisema Stella.

Marina alizidi kugundua kwamba hoteli ile ya mama wa Kisomali pia ilikuwa na nyumba ya kulala wageni ambako Stella alimwambia kwamba kuna wahudumu wengine upande huo lakini yeye alikuwa amemwombea kazi pale upande wa hoteli na baa.

“Sasa mimi sina ujuzi wowote, atanikubali kweli?”

“Kwani mimi nina ujuzi gani? Hapa ninaona mama anahitaji wapishi waliosomea maana uandaaji wa mapishi mbalimbali huhitaji ujuzi kidogo lakini huku upande wa kugawa chakula na baa, anachohitaji mama ni mabinti warembo, mabinti wadogo kama wewe na mimi,” alijibu Stella na kuongeza kwamba kuna wasichana wawili walikuwa wameacha kazi wiki hiyo, mmoja akiwa ameolewa na mwingine kupata kazi kwingine alikoona kuna maslahi mazuri zaidi, kwa hiyo kulikuwa na pengo la wahudumu.

Maneno ya Stella yalikuwa kweli kwani yule mama wa Kisomali baada ya kumtia machoni alikubali kumpa kazi ya uhudumu kwa ujira wa kutwa bila kujali siku moja ya kupumzika kila wiki. Akamwambia baada ya miezi mitatu akionekana anafaa na kumchukua rasmi atamwongezea ujira.

Akamtaka aanze kazi baada ya siku mbili kama sare zake zitakuwa tayari. Lakini katika hizo siku mbili akamwambia alitakiwa kuja ili kufundishwa kazi. Mama yule wa Kisomali akaagiza apelekwe kwa fundi wake akampime na kumshonea sare haraka. Sasa Marina alijua kwamba kumbe baadhi ya nguo alizokuwa akivaa Stella ni sare za kazi.

Alipokwenda kupima sare za kazi alimwelekeza fundi nguo zisiwe za kubana sana na sketi ziwe ndefu na za heshima. Kisha akarudi hotelini ambako alikuta wateja wakiwa wamefurika, baadhi wakiwa wameegesha magari yao nje na kugundua kwamba mgahawa ule uliokuwa katikati ya mji wa Dodoma ulikuwa na wateja wengi. Alianza kupewa somo la maadili ya uhudumu na mama mwenye hoteli kisha akamkabidhi kwa meneja wake, ambaye alikuwa dada mtu mzima kiasi na kukaa naye akimwelekeza kazi kwa takribani saa mbili. Kisha alimwelekeza mahala pa kukaa awe akiangalia shughuli zinavyoendelea pale hotelini hadi mchana.

“Kesho utakuja saa kumi alasiri, utaangalia kazi za jioni hadi usiku hususan upande wa baa kwa sababu kuhudumia wanywaji ndio kazi kubwa usiku,” alisema yule Meneja.

Meneja pia alimwambia pale hotelini kuna vyumba kwa ajili ya wahudumu na ni ruksa kukaa kama hana mahala pa kuishi.

Baadaye usiku alipokuwa na Stella, baadhi ya mambo aliyohoji Marina kutoka kwa mwenyeji wake ni kutaka kujua kama mshahara alioambiwa ambao ulikuwa wastani wa shilingi 4,000 kwa siku  ungemwezesha kupanga chumba na kuishi na mdogo wake.

“Najua shilingi 120,000 unadhani  ni nyingi lakini ni kiasi kidogo sana kwa maisha ya hapa mjini. Hata hivyo, mimi wakati mwingine ninaweza nisiuguse hata miezi miwili mshahara wangu wa shilingi 180,000,” akajibu Stella.

Akafafanua kitu kilichoonekana kuwa na ukakasi kwa Marina kwamba alikuwa akipata pesa kwa wanaume na kwamba alikuwa anatembea na mume fulani wa mtu ambaye ndiye alikuwa akimchukua usiku mara kwa mara na kumwachia pesa ya kummalizia mahitaji yake.

“Huyo mwanaume ndiye wangu wa muda mrefu, na ndiye kanipangisha hapa. Anataka kunioa niwe mke wa pili lakini nasikia mkewe mkali sana. Hata hivyo, huwa silazi damu nikiona kuna bwege na pesa zake ananitaka,” akasema Stella maneno yaliyozidisha ukakasi kwake, hasa ikizingatiwa kwamba, pamoja na kuvunja ungo, Marina alikuwa hajawahi kumjua mwanaume.

Marina alikumbuka siku nyingine alipokuwa anakwenda kwenye kibarua chake akakutana na Mwanaidi Jumanne, aliyekuwa rafiki mkubwa wa mama yake. Bila shaka asubuhi hiyo alikuwa pia akielekea kazini kwake.

Marina alitaka kumkwepa lakini mama yule akawa keshamwona na kumwita: “Wewe Marina, bado unatangatanga humu mjini?”

“Shikamoo mama.”

“Sitaki shikamoo yako. Tangu siku ile hujarudi kwa babu yako?”

“Ndio mama.”

“Unafanya nini?”

“Kuna kibarua ninafanya.”

“Kibarua gani?”

“Ni mhudumu wa hotelini.”

“Mdogo wako yuko wapi?”

“Nilimrudisha kwa babu.”

“Wewe ndio ukaamua kuzamia mjini, siyo? Sasa ninataka urudi kwa babu yako. Utaishia kuwa changudoa… Achana na hicho kibarua. Siku nyingine nikikuona ninakurudisha ukiwa na pingu mkononi. Sitaki kukuona tena unatanga tanga mjini,” alifoka Mwanaidi, akasonya na kuondoka.

Marina akaendelea kumshangaa rafiki wa mama yake huyo huku akijiuliza kwa nini haoneshi kabisa upendo wakati zama za uhai wa mama yake walikuwa mithili ya kidole na upele kama si soksi na kiatu au ulimi na mate.   

Dereva alimshitua kutoka kwenye lindi la mawazo, baada ya kumuuliza waende uelekeo upi baada ya kufika pale Mayamaya Madukani.

Marina aliangalia nje. Kweli walikuwa Mayamaya Madukani ambako kutokana na kuzama katika kukumbuka mambo ya nyuma walifika bila kujua. Palikuwa pamebadilika kidogo. Kulikuwa na majengo kadhaa mapya yaliyopabadilisha japo kidogo. Kikubwa alishukuru pia kwamba sasa barabara kutoka Dodoma hadi Mayamaya Madukani ambao sasa aliona ukiwa mji kamili ilikuwa ya lami.

Dereva alimwambia kwamba kabla hawajaendelea, anataka aangalie tairi lake la kushoto kwa sababu gari lilikuwa likimvuta kwa upande huo. Alipokwenda kuangalia akagundua upepo ulikuwa umepungua sana.

“Dada naona kuna shida kwenye tairi, ngoja tutafute sehemu nirekebishe,” alisema na kutafuta sehemu ya kubadilisha tairi.

Alipata sehemu akaenda kubadilisha tairi. Marina akapata wasaa wa kushuka na kujinyoosha miguu huku akitafuta mahala pa kujisaidia.

 

 

Mambo yako makubwa

ILIWACHUKUA dakika 40 wakiwa pale Mayamaya Madukani ambapo palikuwa pamebadilika sana; nyumba za kisasa na maduka yakiwa yameongezeka, ndipo wakaanza safari ya kuelekea kijijini kwao, Mtakuja, umbali wa takribani kilometa tatu kutoka hapo madukani.

“Shika njia ile pale, mbele, kushoto,” Marina alimwelekeza dereva. Mwendo wa kutoka pale Mayamaya Madukani hadi kijijini kwao Mtakuja ulikuwa wa kasi ndogo kutokana na ubovu wa barabara.

Baada ya mwendo wa dakika tano kwenye barabara hiyo ya udongo ya kwenda kijijini kwao, dereva alianza kulalamikia ubovu wa barabara. “Dada, huku kweli tutafika salama?”

“Jitahidi. Tutafika. Gari huwa zinafika hata kipindi cha mvua.”

“Labda gari kubwa.”

“Hapana, hata gari ndogo. Twende tu taratibu, sina haraka,” alisema Marina.

“Huku mna mbunge jamani?” Alizidi kulalamika dereva baada ya kimya kifupi kupita. Marina hakujibu kwa sababu alikuwa ameanza kuzama tena kwenye kumbukumbu ya mambo yaliyopita, kabla ya kuondoka Dodoma kwenda Marekani. Alikumbuka namna alivyobughudhiwa na wanaume mara baada ya kuanza kazi ya uhudumu wa chakula katika mgahawa aliokuwa ametafutiwa  na rafiki yake, Stella.

Alishukuru pia kwamba walikuwa wamepangwa shifti tofauti na Stella kwani naye aligeuka kuwa mtu wa kumshawishi asiwaachie wanaume waliokuwa tayari kumtoa na kumpa pesa. Mpaka muda huo anaanza kazi pale hotelini, Stella hakujua kwamba Marina hakuwa amewahi kuguswa na mwanaume yeyote maishani mwake na ni jambo ambalo alikuwa hapendi hata kulisikia.

Kila mara alikumbuka maneno ya mama yake: “Lingine mwanangu, wewe ni binti mrembo kadri ninavyokuona. Unazidi kuwa mwali na bila shaka wanaume wengi watakufuatafuata kwa tamaa zao tu za kishetani lakini hawana lolote. Watakuharibia maisha tu. Mimi mama yako nimejifunza mengi sana. Unaona nimewalea peke yangu huku baba zenu wakinikimbia. Hawana maana na hawana msaada. Mwanangu, mwanaume yeyote atakayekufuata, mwambie kama anakutaka, basi akuoe kwa taratibu zinazoeleweka, na si vinginevyo. Dunia pia imeharibika. Kuna Ukimwi. Nitazame mama yako ninavyoteseka…”

Mwezi wa kwanza ulipoisha Marina alikumbuka namna alivyolipwa mshahara wake wa kwanza, shilingi 120,000. Kwake zilionekana ni pesa nyingi na hivyo aliamua kumsubiri rafiki yake, Stella ili amsadie matumizi ya hizo fedha. Alijua sehemu kubwa ingekwenda kwenye kuchangia chakula wanapokuwa nyumbani na mavazi, kwani hadi muda huo, takribani asilimia 70 ya nguo alizokuwa akivaa nje ya sare za kazi alikuwa amepewa na Stella.

Baadhi ya nguo alizopewa ni zile ambazo Stella alikuwa hazivai tena akiziona zimepauka, zimembana ama si za kileo na nyingine aliamua kumpa ili naye abadilike na kuonekana binti wa kisasa. Kuna hii siku alikataa kuandamana naye kwenda mjini kwa sababu eti amevaa nguo ambazo hazivutii. Ilikuwa ni baada ya Marina kukataa kuvaa sketi fupi ama suruali ya kubana aliyomtaka avae.

Alikumbuka tena siku nyingine ambayo Stella alimshurutisha waende usiku kwenye dansi baada ya bendi moja maarufu kutoka Dar es Salaam kutembelea Dodoma, na yeye akalazimika kuvaa sketi fupi ili asimuudhi Stella. Siku hiyo aliona taabu sana. Hakuwa na raha, kila mara alijiona yuko nusu uchi na kujaribu kuivuta ile sketi ifunike mapaja yake vizuri bila mafanikio.

Tofauti na Stella ambaye alikuwa akivaa sare anapofika hotelini na akitoka anavua na kuvaa sketi zake fupi ama suruali za kubana, Marina yeye alikuwa haoni sababu ya kutotoka nyumbani, pale Makole walikokuwa wakiishi, akiwa amevaa sare ya kazi na kurejea akiwa na vazi hilo hilo kila siku.

Marina akazidi kukumbuka namna alivyomudu kumaliza mwaka huku akizidi kupendwa sana na mama wa Kisomali kutokana na adabu na bidii ya kazi. Mama huyo aligundua pia kwamba Marina alikuwa mwepesi wa kujua mambo, msikivu, mwadilifu na alikuwa mzuri wa mahesabu hadi alipolazimika kujua mengi kumhusu na historia ya familia yake.

Marina akamsimulia kwamba alifaulu kwa alama za juu na kutakiwa kujiunga na shule ya watoto wenye vipaji maalumu lakini akakosa mtu wa kumsomesha baada ya mama yake kufariki dunia, tena siku ambayo matokeo yao ya kuhitimu darasa la saba yalitoka. Masimulizi yake kwa mama huyo wa Kisomali kwa sehemu fulani yalifanana na historia ya bosi wake kwani na yeye alikosana na wazazi wake kwa sababu ya kugoma kukeketwa.

Huku gari likizidi kwenda taratibu kwenye njia ambayo ilikuwa na mashimo mengi, Marina alikumbuka pia siku ya kwanza alipolazimika kuongea na mmoja wa wanaume aliyekuwa na kawaida ya kunywa na kula kwenye mgahawa wao, akija na gari lake la kifahari na kuliegesha. Ni mwanaume ambaye alisikia wenzake wakimsifia kuwa ana pesa nyingi lakini si mtu wa kupenda wanawake kama ilivyokuwa kwa vijana wengi wenye pesa.

Alisikia wahudumu wenzie wakisema kwamba mteja huyo aliyekuwa akifanya kazi kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), bosi wao alikuwa akimthamini sana, pengine kuliko mteja yeyote hadi kupikiwa chakula maalumu alichokuwa akiagiza. Ikawa inaelezwa kwamba alikuwa ni Mmarekani mweusi aliyekuwa anaongea Kiswahili cha kubabia baada ya kuishi Tanzania, huo ukiwa mwaka wake wa nne.

Siku hiyo, Marina alikuwa amejitwisha debe la unga wa mahindi akitokea sokoni ambako alikwenda kununua kwa vile angalau bei ilikuwa nzuri kulinganisha na maduka ya mtaani kwao.

Akiwa barabarani, yule kijana mrefu, alisimamisha gari pembeni mwa barabara, kisha akashusha vioo vya gari na kutoa kichwa dirishani na kumuuliza Marina anakokwenda. Kwanza Marina alitaka asihangaike naye wala kumsikiliza lakini alipomwangalia vizuri, akagundua kwamba ni yule Mmarekani mweusi anayeelezewa habari zake kama mteja asiyependa kuhangaika na mabinti.

“Ninaweza saidia wewe, binti? Nakufahamu wewe fanya kazi pale kwa hoteli?” Aliongea Kiswahili chake kwa taabu.

“Ndiyo, lakini acha tu kaka nitafika,” alijibu Marina.

Where are you going… oogh, wapi kwenda wewe?”

“Ninakwenda hapo Makole?”

“Makole bali… Let me saidia wewe, please. Mimi enda jia iyo,” alisema yule kijana.

Marina alikubali, akaingiza mahindi ndani ya gari lake kubwa lenye nembo ya WFP mlangoni, akaketi kiti cha nyuma. Yule mwanaume akaendesha gari, wote wakiwa kimya zaidi ya kumwelekeza mahala pa kukata hadi alipokuwa akiishi. Akateremka huku yule kijana naye akiteremka na kumsaidia kubeba unga ule uliokuwa kwenye kiroba hadi chumbani kwao, kule kwenye mabanda ya uani alikokuwa akiishi na Stella.

Stella ambaye pia alikuwepo akijiandaa kwenda kazini, alishangaa kumwona Marina kaja na Mmarekani huyo. Yeye mwenyewe alikuwa mmoja wa watu waliojipendekeza sana kwake bila mafanikio. Kilichomshangaza zaidi ni namna alivyomsaidia kubeba kiroba kile cha unga bila kujali kuchafuka.

Marina alimshukuru mwanaume yule kwa msaada wake. “Hapana jali, Marina… Bye,” alisema na kuondoka. Marina alishangaa pia kugundua kwamba kijana yule anafahamu hata jina lake.

“Mambo yako makubwa, Marina,” alisema Stella akiendelea kujipodoa.

“Nimekutana naye hapo barabarani baada ya kutoka sokoni akanikumbuka kwamba huwa ananiona pale kazini. Akanipa lifti,” akajibu Marina.

“Marina, usilaze damu. Mwanaume ana pesa huyo. Usimwachie kabisa,” akasema Stella ambaye kuna wakati alianza kumsimanga kwa kumnyonya kutokana na yeye kutoa sehemu kubwa ya mahitaji yao kwa kuwa alikuwa kama anajiuza kwa wanaume, kitu ambacho Marina aliapa kwamba hawezi kufanya.

“Nisimwachie vipi? Kanipa lifti tu kwa ukarimu wake, basi. Wala hakuna jambo jingine.”

“Hakikisha unakuwa naye karibu Marina. Ukitaka asali fuata nyuki, namna hii utamudu kweli kupanga chumba kisha uishi na mdogo wako? Kwa mshahara gani? Kumbuka nilikwambia anayenilipia chumba amechoka kunipeleka gesti. Anataka awe anakuja kwenye chumba anachokilipia,” alisema Stella maneno yaliyomchoma sana Marina yakimaanisha kwamba anatakiwa kumpisha na kupanga chumba chake.

“Nitamudu tu dada’ngu mpendwa, nipe tu hii miezi miwili niliyokuomba,” alisema Marina ambaye alikuwa keshachonga kitanda na godoro lake na vitu kadhaa vya muhimu kuanza kujitegemea. Kwa vile sehemu kubwa alikuwa akila kazini, hakuwa anakunywa pombe wala tamaa ya vitu hususan mavazi, Marina aliamini kiasi cha shilingi 180,000 alichokuwa akilipwa sasa baada ya kuongezewa ujira kingeweza kumtosha kuendesha maisha yeye na mdogo wake.

Hakutaka pia kuishi katika vyumba walivyokuwa wakiishi baadhi ya wasichana wenzake pale hotelini kama bweni kwani mpango wake mkubwa ulikuwa ni kuishi na mdogo wake.

Siku chache baadaye, akiwa anatoka kazini kuelekea nyumbani baada ya kumaliza zamu yake, Marina alikutana tena na Mmarekani  huyo mweusi akishuka kwenye gari lake. Akamwita.

I was comin’ to see you. Naweza enda nawe mahala pengine ongea kudogo?”

“Hapana. Ninawahi nyumbani kaka. Asante sana,” alisema.

 “Marina, I want to talk to you, please,” alisema.

 “Kaka, mimi sijui Kiingereza… Nimechoka, ninawahi nyumbani.”

“Napeleka wewe nyumbani kwa gari muda yoyote.”

“Ninashukuru kwa ukarimu wako kama ulivyonisaidia siku ile kaka. Lakini leo sina mzigo wala sina haraka, asante sana,” alijibu na kuanza kuondoka. Alikumbuka tena maneno ya marehemu mama yake ya kumtaka ajihadhari na wanaume kwani wengi ni waharibifu tu kama walivyoharibu maisha yake. Alikuwa anawaogopa wanaume kama alivyokuwa akiogopa kukeketwa.

Yule mwanaume alijaribu kumwita akimsihi waongee kidogo lakini Marina wala hakugeuka nyuma. Akaenda zake.

 

Huyu bwana anakufaa

MARINA alikumbuka siku iliyofuata, baada ya kufika kazini, aliitwa faragha na mama wa Kisomali. Hali ile ilimshangaza kiasi, kwani hata  mahala walipokwenda kuongelea palikuwa maalumu, katika moja ya ofisi zake alikokuwa akifanyia mazungumzo na watu maalumu pia.

Kisha akamtaka Marina aagize chochote anachotaka na yeye atalipa. Marina alikataa. Kwa sababu walikuwa wakila chakula kinachobaki na siyo kuagiza chakula maalumu kama wateja.

“Marina, samahani nimekuita hapa ninataka nikupe ujumbe muhimu na maalumu sana kwako,” alianza yule mama mwenye asili ya Kisomali.

“Hamna taabu mama,” akajibu.

“Marina, toka nimekuwa na wasichana hapa, kwanza ninakiri wewe ni mrembo sana kuliko wasichana ambao nimekuwa nao hapa. Hata ukivaa gunia unapendeza tu mwanangu. Lakini kikubwa una tabia nzuri, unajituma sana. Wewe ni tofauti kabisa na rafiki yako, Stella. Nimekupenda Marina,” akaanza mama yule.

“Asante mama.”

“Lakini, siyo mimi tu ninayekupenda kwa ajili ya tabia yako, uchapakazi wako na haiba ya umbo na sura yako bali wapo wengi. Yupo kaka mmoja, ukimwona ni mweusi kama sisi lakini yeye ni raia wa Marekani, anaitwa Robertson Murray. Yeye kwa kifupi anataka kukuoa. Bado kijana mdogo sijui kama hata miaka 30 amefika,” alisema Mama wa Kisomali huku Marina akimtumbulia macho.

Akaendelaea: “Inabidi nienda moja kwa moja kwenye hoja. Ni kwamba, amekupenda sana na mimi nimemhakikishia kwamba katika wasichana ninaowajua, wewe ndiye unamfaa. Na nikiri tu kwamba hata mimi ningekuwa na kijana wa kiume ambaye yuko tayari kuoa, ningemwomba akuoe hata kama sisi Wasomali tunapenda sana kuoana sisi kwa sisi.”

Habari zile zilimshangaza Marina. Akabaki ameduwaa.

“Sikiliza Marina,” akaendelea mama wa Kisomali: “Mimi mwenyewe, baada ya kuona tabia zako, nilikuwa ninapanga nikuendeleze kielimu ili uje kuwa meneja wa hoteli yangu. Lakini kwa vile ninamheshimu sana huyu kijana, na kwa vile anazungumza suala zuri la kukuoa na si vinginevyo, nimemkubalia. Ninakushauri ukubali Marina. Huyu kaka ni kati ya wanaume waadilifu sana na mimi ninamheshimu sana,” alisema mama yule.

“Wazo la kuolewa sijawahi kuwa nalo kichwani mama, mimi bado mdogo. Kwa nini usinisomeshe mama kama unaweza ukaachana na huyo mwanaume?”

“Marina, huyu bwana amenihakikishia kwamba, kama unataka kusoma, yuko tayari kukusomesha. Kwa kifupi, muda wake wa kufanya kazi Tanzania umekaribia kuisha. Amewapenda Watanzania na angetamani kurejea kwao akiwa na mke wa Kitanzania. Hana mpango kabisa wa kuoa kwao Marekani na chaguo lake ni wewe.”

Marina alizidi kuchanganyikiwa. Hata hivyo, alikumbuka maneno haya ya mama yake: “Mwanangu, mwanaume yeyote atakayekufuata, mwambie kama anakutaka, basi akuoe kwa taratibu zinazoeleweka, na si vinginevyo…”

Akasema baada ya kukaa kimya kwa muda: “Nimekusikia mama. Nipe siku mbili hivi za kufikiria na ningependa kusikia pia ushauri wa Stella, halafu nitakujibu. Lakini mimi bado mdogo.”

Mama yule akamgeukia: “Marina, Stella anaweza asikupe ushauri mzuri. Sana sana atakuonea wivu kwa bahati uliyopata, kuolewa na mtu wa uhakika. Nisikilize mimi. Ingawa sina ujamaa na wewe na ningetamani huyu bwana amwoe binti yangu kama ningekuwa naye, lakini nimekupenda Marina na ninakuombea mazuri. Hakuna atakayekupa ushauri mwingine mzuri zaidi yangu. Usimsikilize Stella, nisikilize mimi. Ni wachache sana wanaopenda kuona maendeleo ya wenzao,” alisema mama yule.

 

Celine, are you sure?

GARI lile dogo sasa lilikuwa limeshaingia kijijini kwao, Mtakuja. Aliona nyumba ya babu yake ambaye ni mmoja wa wazee maarufu kijijini hapo mbele yao. Sasa alikumbuka jambo jingine muhimu alilosahau. Alishangaa kwamba safari yote kutoka Marekani, aliwaza kumwona Stella akifika Dodoma mjini na kisha kuwahi Mayamaya kuona familia yake, hususan mdogo wake, Celine, lakini akawa amemsahau huyu mama wa Kisomali.

Sasa alipanga, kwamba akae pale kijijini kwa siku mbili au tatu, kisha atakapokwenda mjini, amtafute mama huyu. Ni mama aliyewakutanisha na mumewe, akamshawishi hadi kukubali kuolewa na mwanaume pekee aliyekutana naye katika maisha yake tofauti na mabinti wengi wa siku hizi.

“Tunakwenda nyumba ile pale,” Marina alimwelekeza dereva teksi. Ama kwa hakika aligundua kwamba karibu safari nzima alikuwa kwenye dimbwi kubwa la mawazo, mkanda wa maisha yake kabla ya kuondoka Dodoma ukijirudia. Hata baadhi ya vitongoji na maeneo muhimu alipita bila kujua. Hakukumbuka namna walivyopita Veyula, Kambi ya JKT Makutupora, Mzakwe na maeneo mengine hadi Mayamaya.

Lakini alishukuru kwamba hatimaye alikuwa amefika kwenye asili  yake, mahala alikokulia, kijijini kwao Mtakuja. Ni mahala ambako, ingawa zamani aliona kama inachosha kuamka alfajiri kusaka maji visimani, kulima na kusaka kuni, lakini kumbe shughuli hizo zilikuwa burudani za aina yake ambazo hazipatikani Marekani. Maisha yale ya kijijini, kutafuna mihogo mibichi au karanga wenyewe wakiita mayowe, wakati wa msimu, kunywa maziwa na kula zabibu kutoka kwenye mti moja kwa moja yalikuwa na raha zake ambazo alikuwa amezikosa licha ya adha za kubeba maji kichwani.

Gari lilizidi kusogea karibu na boma la babu yake ambaye alimwacha akiwa Mwenyekiti wa kijiji cha Mtakuja na mlinzi wa mila za Kigogo ikiwemo ya kukeketa aliyokuwa akiipiga vita. Aliangalia saa yake, ilikuwa inaelekea saa 12:50 jioni. Jua lilikuwa linaendelea kuzama na kuruhusu taratibu giza la usiku kuanza kuchukua nafasi yake.

Hatimaye gari lilisimama upenuni mwa boma la babu yake. Mara akaona bibi yake akitokeza baada ya kusikia ngurumo ya gari. Bibi mtu alipomkaribia huku yeye akishuka ndani ya gari akamwona na kumtambua. Akaanza kuruka ruka huku akiwaita wengine na kupiga vigelegele. Marina alishangaa alivyomtambua haraka licha ya mwanga wa jua kuanza kupotea tofauti na mama Siwema, labda kwa vile damu ni nzito kuliko maji.

“Ni Marina. Njooni mumpokee,” aliita bibi yule. Alionekana bado ana nguvu. Marina alifurahi, akapiga hatua za haraka kumkumbatia bibi yake.

“Solowenyu bibi?” Alisalimia kwa Kigogo.

“Alenyenye Marina,”

“Milimonyi (mnaendeleaje na shughuli)?”

“Miswanu.”

Alirudi tena kumlipa ujira dereva na kuteremsha masanduku yake. “Dada, huniongezei kidogo pesa. Huoni jinsi barabara ilivyo mbovu? Mpaka kufika hapa lazima nitakuwa nimekata springi za gari kwa sababu mengine si mashimo bali mahandaki. Dereva mwingine angekataa kuja huku,” alisema yule dereva baada ya Marina kumlipa ujira waliokubaliana na kumwomba amsaidie kushusha mizigo.

Marina alitoa shilingi 3,000 bila kinyongo na kumwongezea. Akamsaidia kubeba begi na masanduku yake makubwa mawili aliyokuwa nayo hadi kwenye nyumba ya babu yake na tayari mjomba wake naye alishakuja pale kusaidia.

Baadaye aliagana na dereva wakikubaliana kwamba akiwa na shida angempigia simu. “Usije ukaacha kuja kwa sababu ya ubovu wa barabara nikikupigia simu tafadhali uje,” alisisitiza Marina.

“Sawa dada, lakini waambieni viongozi watengeneze barabara. Inatisha. Huu ni mwaka wa uchaguzi. Safari hii chagueni mbunge atakayewajali na kuibana serikali iwatengenezee barabara,” alisema dereva teksi yule. Hilo lilimkumbusha Marina kuhusu uchaguzi mkuu ambao alitamani kushiriki lakini pengine ungefanyika akiwa ameshaondoka kurudi Marekani.

Marina alifurahi kumwona babu yake, Mzee Nhonya Chilyawanhu akiwa na afya njema. Jioni hiyo akiwa ameketi upenuni mwa nyumba yake akisubiri mjukuu wake mwingine aliyekuwa akikoka moto wa kuota pale katikati ya boma lake.

Alipepesa macho na kugundua kwamba nyumba hiyo ya bati, kati ya nyumba chache kijijini hapo zenye bati, ilikuwa imeboreshwa kama alivyoagiza.

Wakati anaondoka kwenda Marekani, mumewe alikuwa ametoa kiasi cha shilingi milioni 10 ili kuboresha nyumba hiyo, ikiwa ni pamoja na kuiwekea madirisha na milango ya kisasa  na kuipiga lipu upya. Ilikuwa inavutia kiasi.

Katika ujio wake huo, Marina alikuwa amedhamiria kujenga nyumba hapo kwa babu yake ambamo angekuwa akifikia na mumewe au mdogo wake. Kadhalika alifikiria kununua nyumba ya wastani Dodoma mjini kama angebaki na pesa. Alipanga pia kuchimba kisima cha maji na ikiwezekana kufunga umeme-jua ili babu na familia yake wawe wakitumia.

Alishukuru kuona sasa Mayamaya Madukani kuna umeme lakini kijijini kwao ulikuwa haujafika.

“Karibu mjukuu wangu, karibu sana,” alisema babu yake ambaye pia bado alikuwa na nguvu. Pamoja na umri wake mkubwa akishika jembe hata vijana wadogo walikuwa hawamfikii eneo analoweza kulima kwa siku. Alikuwa mzee mchapa kazi, akimiliki mashamba kadhaa ya zabibu, mihogo na karanga na pia akifuga ng’ombe na mbuzi. Ndio maana ilikuwa ni nadra kaya yake kukumbwa na njaa, kama utalinganisha na familia zingine katika eneo hilo. Pale kijijini alikuwa ni kati ya wazee wenye kujiweza ambaye asingeshindwa kumsomesha Marina hata shule ya kulipia kama angetaka.

Marina alimkumbatia babu yake kwa furaha kisha akaketi kwenye kigoda pembeni mwake na ndugu wengine wakahamia mahala pale. Walikuwa na hamu ya kusikia mengi kutoka kwa Marina.

“Marina, yaani umekaa Ulaya umebadilika sana mjukuu wangu. Unaonekana kama mzungu,” alisema babu yake akimkodolea macho. Mwanga ulikuwa bado unaruhusu kumwona vizuri.

“Nashukuru kukukuta salama babu… Na wewe huzeeki,unazidi kuwa kijana. Ningekuwa sijaolewa ningempindua bibi unioe…” alisema kwa utani na kusababisha kicheko.

“Haya, Ulaya mnatunyima nini wenzetu?”

“Si Ulaya babu, ni Marekani… Huko maisha ni kawaida tu. Ila kikubwa hakuna kusinzia sinzia. Kazi mtindo mmoja. Watu wanafanya kazi usiku kucha.”

“Mbona hukuja na mumeo, ama umemwacha mjini (Dodoma)?”

“Hapana, yeye amebaki Marekani, ana shughuli nyingi. Safari nyingine nitakuja naye kwa sababu naye alikuwa na hamu ya kurudi Afrika. Unajua baadhi ya Wamarekani weusi kama yeye wanapenda huku kwa sababu wanajua ndiko asili yao. Hata hivyo, nimeacha akifuatilia mpango wa kurudi kufanya kazi huku Afrika ingawa inaweza isiwe hapa Tanzania.”

“Hebu nikumbushe jina la mumeo, anaitwa nani,  Murei?”

“Hapana babu, anaitwa Robertson Murray. Inatamkwa ‘Mari’.”

“Yaani majina yote wakakosa wakamwita Mali.”

“Siyo Mali ila Mari na unatamka kwa kuweka stress… yaani uzito kidogo kwenye ‘m’.”

“Kwa hiyo majina yenu yanafanana, wewe Marina, yeye Mari… Tuyaache hayo, tulishajiuliza sana. Mtoto huyu anakaa huko muda wote huu, miaka imekuwa mingi bila barua wala nini na simu zipo. Si ungekuwa unatupigia?” Aliuliza Mzee Chilyawanhu akichomoa simu yake kwenye mfuko wa shati na kumwonesha.

“Ni kweli babu, nilipoteza namba zote za simu na wakati ule nilikuwa bado mshamba wa hivi vitu na kumbuka simu zilikuwa hazijawa na muda mrefu toka zimeingia. Wewe mwenyewe babu hukuwa na simu. Sasa hivi nikirejea tena Marekani, nitafanya utaratibu wa kuwasiliana. Kwanza nilipokuwa Dar es Salaam nimekununulia simu nzuri zaidi ya hiyo. Nitakupa baadaye.”

“Na mimi umeninunulia simu?” Alihoji bibi yake.

“Nyanyizi, kwani bado tu huna simu?” Alihoji kwa kutaja jina la bibi yake ambalo pia ni jina lake yeye Marina alilopewa na mama yake kama la ukoo.

“Wewe mtoto, kwani uliniacha na simu?”

“Nilidhani babu keshakununulia. Basi usikonde, nitakununulia au utachukua ya mumeo kwa sababu yeye nimemletea mpya na ya kisasa. Mwenyekiti wa kijiji anatakiwa awe na simu ya kisasa. Babu si wewe bado mwenyekiti au ulishatoka?”

“Ndiyo,” mwaka jana wamenichagua tena.

“Hongera babu.”

“Kama Marina una simu nyingine hiyo itakuwa ya kwangu,” alidakia mjomba wake, Mazoya, aliyekuwa akiishi pale kwa baba yake na muda wote baada ya kusalimiana na mpwawe alikuwa kimya. Huyu ndiye aliyekuwa akimfuata mama yake kwa kuzaliwa.

Mjomba wake mkubwa, Charles Chilyawanhu, alikuwa akiishi Hombolo, kilometa kadhaa kutoka Mayamaya huku mama yake mkubwa akiishi Singida alikoolewa.

“Mjomba, nitakununulia simu… Lakini hapa bila umeme simu mnachaji wapi?” Alihoji Marina.

“Tunachaji kwa watu wenye betri na umeme-jua kwa shilingi 500 hadi simu ijae,” alijibu babu yake na kuongeza: “Enhe, hujaniletea mjukuu wa pili?”

“Nilikuwa ninasoma kwa hiyo sikutaka kuzaa kwanza. Sasa nimemaliza mambo ya shule ninaweza sasa kukutafutia mjukuu wa pili babu yangu,” alisema Marina.

“Unachelewa mjukuu wangu. Wenzako wengi hapa rika lako wana watoto, wengine hadi watoto watatu,” alisema babu yake.

Dakika chache huku giza likizidi kufukuza mwanga wa mchana majirani kadhaa walikuwa wameanza kumiminika pale kwa Mzee Chilyawanhu kumsalimia Marina. Inaonekana habari za ujio wake zilikuwa zimeanza kusambaa. Walikuwepo pia mabinti wawili aliosoma nao shule ya msingi kabla ya kuhamia mjini. Kama alivyosema babu yake, wote walikuwa na watoto, mmoja akiwa na wawili. Marina alifurahi sana kuwaona.

Giza lilizidi kuingia na wageni waliokuja kumsalimia walianza kuaga mmoja mmoja kurejea makwao. Kuna kitu kimoja muhimu alikuwa hajakiona hadi muda huo. Mdogo wake, Celine. Mwanzoni alihisi kwamba atakuwa amekwenda kuteka maji kisimani, lakini sasa takribani dakika 50 zilikuwa zimepita toka awasili bila kumwona. Kama mtu hakwenda kufua, ilimchukua dakika 30 kwenda katika kisima chochote cha karibu na kurudi.

“Mbona Celine sijamwona. Yuko kisimani?” Akaamua kuuliza.

Ulipita ukimya fulani bila jibu. Baadaye babu yake akamgeukia: “Yupo, utamwona tu baadaye.”

“Kwani yuko wapi, katumwa?”

“Una haraka gani Marina? Umeshafika nyumbani, utamwona tu mdogo wako. Yeye ndiye analea huu mji siku hizi. Ndiye ananitunza babu yako.”

“Lakini anaendeleaje na shule?”

“Shule anaendelea kama kawaida,” alijibu babu yake kwa kifupi.

Baadaye kikao hicho kilihamia kwenye eneo lililokuwa limekokwa moto. Marina alianza kuulizwa kuhusu maisha ya Marekani, vyakula wanavyokula na yeye akaanza kuwasimulia kwa kifupi na kwamba kule kazi inathaminiwa na inalipa vizuri kama mtu si goigoi.

“Hata mimi nilikuwa ninasoma muda wote tangu nifike Marekani na nilikuwa ninafanya kazi, ninatenga muda wa kumpikia mume wangu na siku nyingine yeye ndiye anapika,” akasema Marina.

“Marina, yaani mume wako ndiye anapika? Wewe ukiwa wapi kwa mfano?” Alihoji mjomba wake akionesha mshangao.

“Nikiwa nyumbani. Mbona ni kawaida tu kule mume na mke kushirikiana kazi. Hata babu hapa siku nyingine anapaswa kumsaidia bibi kutandika kitanda, kufua hata kufagia. Mimi kila nilipokuwa kwenye mitihani wakati nasoma mume wangu ndiye ananifulia nguo na kazi zote za nyumbani ikiwemo kudeki nyumba, kupika na kuosha vyombo.”

“Duh, hayo mambo usije ukaleta huku kwetu! Halafu, wewe una mume anafanya kazi. Kwa nini sasa ujitese tena kwa kufanya kazi huku pia unasoma?” Akahoji Mazoya.

“Ni kwa sababu kazi zipo na uwezo huo nilikuwa nao. Nina mahitaji mengi ambayo siwezi kila kitu kumtegemea mume wangu na pia ninajua umaskini tulio nao huku nyumbani. Lazima nitafute pesa na kuweka akiba,” alisema Marina. 

* * *

Muda ulizidi kwenda bila kumwona Celine. Ilikuwa inaelekea saa mbili usiku wakati chakula kilipotengwa pale nje kwenye kikome walipokuwa wakiota moto. Bado Marina alikuwa hajamwona mdogo wake.

“Jamani, kwani Celine kaenda wapi?” Akahoji tena.

“Si nimekwambia utamwona tu. Una haraka gani na umeshafika nyumbani?” Alijibu babu yake wakati akinawishwa mikono na mmoja wa wajukuu zake.

“Mdogo wako kalala, anajisikia vibaya. Maliza kula ukamsalimie,” aliingilia bibi yake.

“Nina hamu naye sana, ngoja nimjulie hali kwanza ndipo nitakuja kula. Isitoshe sina njaa sana. Nilikula tu jioni hii wakati ninajiandaa kuja huku, kwa hiyo bado nimeshiba… Tena kwenye mfuko wangu ule mdogo kuna chakula na matunda. Ngoja nitakuja nayo,” alisema akinyanyuka kwa sababu  alijua mabegi yake yalipelekwa kwenye banda la tembe alimokuwa amelala Celine.

Banda hilo ni la mama yake na ndilo alipanga kulivunja na kujenga pale nyumba ya kisasa ikiwa na sebule, vyumba viwili; chake na cha Celine, jiko, stoo na kila chumba kikiwa na choo cha ndani kwa ndani pamoja na choo cha jumla. Ramani yote alikuwa nayo kichwani.

Babu yake alimtaka ale kwanza chakula lakini Marina alikataa. Aliingia mlangoni kwenye banda lile la tembe likiwa giza huku hewa ya ndani ikiwa nzito kutokana na kuwa na madirisha madogo.

Alikumbuka jambo moja muhimu alilosahau kufanya, kununua taa za kuchaji mjini Dodoma. Aliwasha tochi ya simu yake ili kufukuza giza akapata mwanga kidogo.

“Celine,” aliita baada ya kusogea kwenye kitanda alichokuwa amelala mdogo wake.

“Abe,” sauti ya mtu aliyekuwa amelala kitandani iliitikia kwa mbali.

“Celine, hakuna taa humu?” Aliuliza Marina akisogelea kitanda.

“Haina mafuta,” Celine alijibu kwa shida akiwa kama mtu anayejilazimisha kuzungumza.

Marina alizidi kukaribia kitanda na kumwinamia mdogo wake akimmulika kwa kutumia mwanga wa tochi ya simu yake ya mkononi.

“Celine, nasikia unaumwa. Unasumbuliwa na nini mdogo wangu?”

“Naumwa… Nani?” Alijitahidi kujibu kwa shida binti yule.

“Ni mimi dada yako, Marina.”

“Marina! Dada naumwa…” alisema Celine akijaribu kunyanyuka bila mafanikio.

“Tulia tu usinyanyuke,” alimkataza huku akiketi kwenye kitanda.

Sasa macho yalianza kuzoea mwanga ule mdogo uliotokana na simu yake ya mkononi. Aliweza kuona sura ya mdogo wake. Alionekana yuko kwenye maumivu makali kisha akamsaidia kunyanyuka na kumketisha kitandani.

“Unasumbuliwa na nini, Celine?”

“Walinikeketa takribani wiki sasa. Damu zilikuwa zimegoma kukatika lakini baadaye zikakatika. Hata hivyo, kuanzia jana ninapata homa kali. Mwili hauna nguvu, ninasikia kizunguzungu na kichwa kinaniuma sana. Pia ninatapika. Sina hamu ya kula na ninasikia misuli inanibana na hata mdomo unavuta,” alisema kwa taabu.

Habari zile, kwamba Celine kakeketwa zilimshitua sana Marina. Alihisi kama anaishiwa nguvu. Matumbo yakamcheza, mwili ukapata ganzi. Kijasho chembemba kikaanza kumtoka.

“Celine, are you sure… Wamekukeketa?” Alihoji tena Marina kwa hamaki.

“Ndio dada. Babu alinilazimisha.”

Jibu lile lilizidi kumsononesha Marina. Alikumbuka wakati anaondoka namna alivyomsisitiza babu yake kutomkeketa Celine na yeye akakubali, na hasa kwa kuonekana kama alilainishwa na pesa ambazo mumewe alimpa kwa ajili ya kukarabatia nyumba na kuboresha choo.

Marina ambaye alikuwa amezidi kujua madhara ya kukeketwa mbali na aliyoambiwa na mama yake kama vile kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwemo ukimwi kama kisu kimoja kitatumika kwa watu wengi au kuugua pepopunda kutegemea aina ya kisu kilichotumika na mazingira ya kidonda, aliwaza na kugundua kwamba anatakiwa kuchukua hatua za haraka za kumtafutia matibabu mdogo wake.

“Enhe, umepewa dawa yoyote mpaka sasa?”

“Hapana… er ndio. Yule ngariba aliyenikeketa, jioni hii amenipa dawa lakini haijasaidia sana. Hali inazidi kuwa mbaya.”

“Dawa gani alikupa. Ya kienyeji?”

“Ndiyo… Nilaze dada. Najisikia viba… mmh,” alisema akishindwa kumalizia sentensi yake.

“Haya, ngoja tufanye utaratibu kukupeleka kwenye matibabu Mayamaya Madukani haraka… Lakini ngoja kwanza nikupe dawa za maumivu,” alisema Marina.

Alikwenda kwenye mkoba wake na kutoa dawa za maumivu alizotoka nazo Marekani kwa ajili ya dharura na pia akachomoa kwenye begi lake chupa moja ya maji kati ya tano alizokuwa amenunua Dodoma mjini ili Celine amezee dawa.

Marina alikuwa amejihami na maji hayo akihisi kwamba miaka mingi ya kujitenga na maji ya kisima yasiyochemshwa yangeweza kumletea matatizo tumboni kama akiyatumia.

Alimnyanyua tena mdogo wake pale kitandani na kumkalisha, akampa zile dawa kunywa. Celine alizinywa kwa taabu akisema taya lilikuwa linavuta na kumfanya ashindwe kupanua mdomo vizuri. Hata hivyo, kwa shida shida akafanikiwa kunywa zile dawa.

“Hizi dawa ni nzuri sana. Bila shaka muda mfupi ujao utajisikia nafuu kidogo lakini lazima tukupeleke hospitali,” alisema akimlaza tena kitandani mdogo wake huku machozi yakimtiririka kutokana na hali aliyokuwa nayo. 

 

 

Mila gani hizi zisizo na maana?

MARINA alitoka nje haraka akiwa amefura kwa hasira hadi pale alipokuwa ameketi babu yake akiendelea kula.

“Babu, mbona umefanya jambo nililokukataza sana… Imekuwaje mmemkeketa Celine?” Alihoji huku akitetemeka kwa hasira na kufuta machozi. Midomo ilikuwa ikimcheza. Babu yake aliendelea kula pale nje bila kumjibu. “Sijui kwa nini Mungu hakuniongoza nije mapema nikute hamjamfanyia mdogo wangu ujinga huu… Maskini mdogo wangu Celine…”

“Marina, kula kwanza tutaongea. Hatuwezi kutupa mila zetu, unasikia? Mimi ndiye mlinzi wa mila hapa kijijini halafu unataka kwangu ndiyo nioneshe mfano mbaya, siyo? Hata wewe unatakiwa kukeketwa ili mizimu itulie na wazee wenzangu wazidi kuniheshimu. Kwa mila zetu wewe bado mtoto hadi utakapokeketwa na hivyo Celine sasa ana heshima na ni mkubwa kuliko wewe,” alisema babu yake.

“Lakini babu, mila gani hizi zisizo na maana isipokuwa matatizo? Anyway maji yameshamwagika. Celine anatakiwa kupelekwa hospitalini, tena haraka sana.”

“Tatizo lake limeshajulikana na ameshapatiwa dawa. Atapona tu usiwe na wasiwasi,” alijibu bibi yake aliyekuwa pembeni mwa mumewe.

“Bibi, mtu katokwa damu nyingi na sasa ana homa kali na hana nguvu. Huyu anahitaji kuongezewa damu na maji na inawezekana amepata uambukizo au pengine ana malaria kali. Lazima tumpeleke kwenye matibabu haraka iwezekanavyo. Wapi tunaweza kupata usafiri hata wa pikipiki tumwahishe kwenye matibabu Mayamaya?”

“We mtoto, bibi yako keshakwambia kwamba keshapata dawa. Tulia atapata nafuu tu,” alisema kwa sauti ya ukali kidogo huku akimkazia macho.

“Kanambia kapata dawa lakini haijamsaidia. Huyu katokwa damu nyingi na bila shaka amepungukiwa damu na ndio maana analia kichwa kuuma, kizunguzungu na kuishiwa nguvu. Lazima apate tiba nzuri ikiwa ni pamoja na kuongezewa damu na maji haraka.”

“Unapoteza muda. Haya mambo tuachie sisi. Toka nizaliwe hadi nimefika umri huu, kumbukumbu zinaonesha kuna wanawake wachache sana, hata kumi hawafiki waliowahi kupata matatizo hadi kufariki dunia. Na hiyo ilitokana na uzembe tu wa wahusika au kushindwa kufuata masharti kwa mujibu wa mila zetu lakini wasingepoteza maisha. Kila kitu kimedhibitiwa kwa Celine, na hilo unalotaka kufanya ni kukiuka masharti. Mizimu yetu haiwezi kukubali,” alisema babu yake.

Marina aliona si rahisi kueleweka kwani hata kama kwa miaka na miaka walishafariki watu watatu pekee pale kijijini kutokana na kukeketwa, mdogo wake anaweza kuwa wa nne. Hakutaka hilo litokee abadani.

Alifikiria kumpigia simu dereva teksi aliyemleta akaona ni kuchelewa kumwahisha mdogo wake hospitali kwani kwa muda ule wa takribani saa nzima pengine alikuwa keshafika Dodoma mjini.

Alitoka haraka kusaka usafiri wa pikipiki au hata wa baiskeli kwa sababu alikuwa na uhakika kwamba hakukuwa na mtu mwenye gari katika kijiji kile ambacho umaskini wa kipato ulikuwa bado mkubwa.

Katika nyumba nne zenye pikipiki maarufu kama bodaboda pale kijijini alizoelekezwa na binamu yake, yaani binti wa mjomba wake Mazoya ambaye pia alikuwa akiitwa Nyanyizi, jina la bibi yake, hakufanikiwa kupata. Katika nyumba mbili alikuta pikipiki zikiwa mbovu, mbili zikiwa zimelala mjini kwa maana ya Mayamaya Madukani na moja mhusika alisema hawezi kutoka usiku ule kwani anajisikia vibaya.

Alitamani tena kumpigia simu yule dereva teksi lakini akaona aende mbali kidogo alikozidi kuelekezwa. Akawa anakwenda huku akikimbia. Aliuliza nyumba kadhaa hatimaye akafanikiwa kupata vijana wawili waliokuwa tayari kumpa usafiri wa pikipiki, mmoja wa kumbeba mgonjwa na mwingine wa kumbeba yeye.

Kwa bahati nzuri wote walikuwa wakimfahamu, mmoja aitwaye Chiwamba akiwa amesoma naye darasa moja katika shule ya msingi Mtakuja kabla hajahamishiwa Dodoma mjini. Yule mwingine alikuwa madarasa ya chini, Marina alikuwa hamkumbuki lakini yeye alisema anamfahamu.

Alienda haraka na vijana hao nyumbani hadi kwenye chumba alichokuwa amelala Celine ili wamkimbize kwenye zahanati iliyoko Mayamaya Madukani au Centre kama wao walivyokuwa wakiita.

Haraka haraka, huku wale vijana wakisubiri nje, aliingia ndani, akawasha simu yake ili kupata mwanga na kuelekea alikokuwa amelala Celine. Aliita wakati anakaribia kitanda lakini hakuitikiwa. Aliita tena huku akizidi kusogea karibu kabisa na kitanda, bado hakusikia sauti yenye kumwitika.

Akasimama upenuni mwa kitanda akiendelea kumwita mdogo wake lakini hakuna sauti iliyomjibu. Aliingiwa na wasiwasi mkubwa akihisi kama roho inataka kuchomokea utosini.

“Celine,” aliita akiinama kupeleka mkono kitandani ili kupapasa japo alishaona dalili kama vile pale kitandani hakukuwa na mtu.

Marina alipapasa godoro kwa mkono wake wa kulia, lakini hakuhisi uwepo wa mtu zaidi ya shuka iliyokuwa imejikunjakunja juu ya godoro lile gumu la sufi.

Hakutaka kuamini kwamba kitanda kile hakikuwa na mtu. Ni dakika zisizozidi 20 alimwacha mdogo wake huyo akilalamika kwa maumivu katika kitanda hicho. Alikumbuka tena kwamba kwa vile Celine alishindwa hata kunyanyuka na kukaa ili kusalimiana naye mpaka akawa analazimika kumsaidia kunyanyuka, hawezi peke yake kushuka juu ya kitanda kile na kutembea bila msaada wa mtu.

Alimulika kwa simu yake kila sehemu ya chumba taratibu macho yake yalianza kuzoea mwanga ule hafifu. Alijiridhisha kwamba hakukuwa na mtu kitandani wala sehemu nyingine kwenye kile chumba.

“Atakuwa amekwenda wapi huyu,” alijiuliza. Alipata wazo kwamba anaweza kuwa ameanguka chini ya kitanda. Alimulika kwa mwanga wa simu uvunguni lakini hakumwona Celine. Alitoka haraka na kwenda hadi pale alikokuwa ameketi babu yake na bibi akiwa amefura kwa hasira.

“Babu, Celine amekwenda wapi? Tunatakiwa kumpeleka hospitali haraka… Mmemficha wapi?” Aliuliza. Hakuna aliyemjibu.

Aligundua kitu kingine kwamba wakati anaondoka pale kwenye moto alikuwa amemwacha mjomba wake lakini mara hii hakuwepo. Aliuliza tena mahala aliko Celine, lakini hakuna aliyemjibu. Kila mtu aliendelea na shughuli zake na binamu yake, Nyanyizi, alipotaka kuzungumza kitu akakemewa na babu yake kunyamaza.

Aliamua kuvamia nyumba kubwa ya babu yake ambako alihisi wanaweza kuwa wamemhamishia Celine haraka haraka wakati yeye akienda kusaka usafiri. Tofauti na chumbani alikokuwa akilala, humu kwa babu yake kulikuwa na mwanga wa kutosha pale sebuleni ambako kulikuwa na taa ya chemli.

Alipepesa macho hakuona mtu. Akachukua ile taa na kuingia nayo chumbani kwa babu yake bila kujali. Alimulika kila sehemu hadi uvunguni lakini hakumwona Celine. Alitoka haraka na kwenda kwenye nyumba ya mjomba wake iliyokuwa inapakana na ya babu yake.

Kwa msaada wa taa ya chemli iliyokuwa imewashwa humo alimtafuta Celine huku akimwita kwa jina bila mafanikio. Akatoka na kwenda kwenye tembe nyingine walimokuwa wakilala watoto, hususan wajukuu pamoja na wageni. Humo pia hakumpata mdogo wake.

Roho ilizidi kumwenda mbio. Alirudi tena pale kwenye moto alikokuwa babu yake na kumwomba amsaidie kujua mahala Celine alipo. Alijaribu kueleza umuhimu wa kumwahisha hospitalini kwa sababu yawezekana amepungukiwa damu na kwamba hilo linaweza likagharimu maisha yake, lakini si babu wala bibi yake aliyemjibu.

Upande wa pili wale vijana wawili wakiwa na pikipiki zao walikuwa wakimsubiri. Alipata hisia kwamba Celine alikuwa amefichwa mahala na alihisi pia kwamba aliyefanya kazi hiyo ni mjomba wake ambaye hakuwepo hadi muda huo. 

“Nifanye nini miye sasa?” Alijikuta akijiuliza huku akihisi miguu ikielekea kukosa nguvu na kutamani kukaa. Kasi ya mapigo ya moyo ilizidi kuwa juu.

 

Kwenda hospitali ni lazima

AKIWA anaonekana kukata tamaa huku hasira zikiwa zimemjaa na kujilaumu kwa kuchelewa kuja Tanzania, Marina aliwafuata vijana waendesha bodaboda waliokuwa wakimsubiri kuwaeleza habari za mgonjwa aliyetaka wamsaidie kwenda hospitali kutoweka.

“Sijui nifanyeje. Inaniuma sana. Mdogo wangu naona wamemficha na sijui ni kwa nini na kwa faida ya nani. Mtanisaidiaje ndugu zangu kumtafuta huko walikomficha. Lazima apelekwe hospitali huyu. Katokwa na damu nyingi sana baada ya kukeketwa na ana homa kali,” alisema.

“Lazima wamfiche kwa sababu wanajua akifika hospitali ni kesi,” alidakia Chiwamba. Akaongeza: “Nafikiri watakuwa wamempeleka kwa yule bibi, Majimbi Uledi, kule bondeni.”

“Huyo bibi ni nani?” Alihoji Marina.

“Ni ngariba na pia ni mganga. Ndiye aliwakeketa, kwani humjui? Watu wanaokeketwa na kupata matatizo huwa wanapelekwa kwake,” alijibu Chiwamba. Marina aliomba wampeleke haraka kwa huyo bibi.

Wakati wanafika katika nyumba hiyo, Marina alimwona Mazoya akitoka mahala hapo ingawa yeye hakuwatambua. Ile ilimpa matumaini Marina kwamba inawezekana kweli Celine alikuwa kaletwa hapo kwa matibabu ya kienyeji. Waligonga hodi nyumbani kwa bibi huyo na binti mdogo alipofungua mlango, Marina hakusubiri kukaribishwa. Akaingia ndani huku wale vijana wawili wakimfuata nyuma.

Pale ndani walimkuta Celine akiwa amelazwa kwenye ngozi na yule bibi akiwa amemwinamia. Kuna kitu alikuwa akimpaka kichwani.

Kwa msaada wa mwanga wa kibatari kilichokuwa kimewashwa, pembeni waliona kikombe cha maji na chupa kadhaa za dawa za mitishamba. Marina alimsalimia yule ngariba ambaye alimkumbuka mara moja kwamba ni rafiki wa bibi yake Nyanyizi kwa muda mrefu na walikuwa wakilima jirani. Alikumbuka pia kwamba alipokuwa mdogo alikuwa akimletea dawa walizokuwa wakiita kwamba ni za chango. Bibi yule alisimama akionekana ameshituka kuwaona.

“Samahani, bibi, tumekuja kumchukua huyu mgonjwa wako sasa hivi,” alisema Marina baada ya kusalimiana, kujitambulisha na bibi yule akamkumbuka.

“Huyu mwacheni hapa alale, nimeshampa dawa, itamsaidia tu… Mjomba wako aliyemleta katoka hapa sasa hivi,” alijibu yule bibi.

“Hapana bibi. Huyu lazima tumwahishe kwenye matibabu na hatuna muda wa kuendelea kupoteza hapa,” alijibu Marina.

“Matibabu ndio nimeshaanza kumfanyia. Nilipoambiwa anaumwa tangu jana nilimpa dawa na nimeendelea kumpa dawa nyingine itamwongezea nguvu. Asubuhi ataamka mzima kabisa,” alijigamba yule bibi na kuongeza kwamba mjomba mtu alikuwa kahangaika kwa kumbeba Celine mgongoni hadi kumfikisha hapo kwake usiku huo.

Lakini Marina alipomwangalia mdogo wake alimwona kwamba alikuwa na hali mbaya zaidi na sasa akiwa hata hawezi kuongea. “Hapana bibi. Utatusamehe, huyu lazima tumpeleka hospitali sasa hivi… Kwenda hospitali ni lazima na wala siyo ombi,” alisisitiza Marina.

“We mtoto, hospitali?” Alimaka yule bibi. “Utawaambia nini watu wa serikali, unataka kumletea babu yako taabu?”

Marina hakutaka kumsikiliza. Alimwita Celine ambaye aliitikia kwa mbali. Alimweleza kwa ishara kwamba mataya yalikuwa yanavuta na mwili hauna nguvu, na kwamba bado alikuwa anasikia kizunguzungu.

Marina aliwaomba wale vijana kumbeba taratibu Celine hadi kwenye pikipiki. Yule bibi aliwazuia lakini Marina akiwa na hasira alimsukuma na kumtaka awaache wampeleke Celine kwenye matibabu ya uhakika. Nusura yule bibi ajibamize kwenye ukuta hadi Marina akajihisi vibaya kwamba alitumia nguvu kubwa zaidi kumsukuma bibi wa watu. Akamtaka radhi huku akisisitiza kwamba suala la kutompeleka hospitali halipo.

Haraka haraka wale vijana walitoka nje wakiwa wamembeba Celine na kumkalisha kwenye pikipiki mojawapo huku yule ngariba akiendelea kusisitiza wamwache. Marina alimwomba Celine ajikaze na kujishikilia kwenye pikipiki ili wamwahishe hospitali.

Kijana aliyekuwa na pikipiki hiyo alimweka kwa mbele karibu na tangi la mafuta na yeye akawa nyuma akiwa katikati ya mikono yake baada ya kuona mgonjwa huyo alikuwa hana uwezo wa kujishikilia mwenyewe. Marina alivua koti refu la baridi alilolivaa alipokwenda kumsalimia Celine na kumfunika mdogo wake.

“Tutakwenda taratibu hadi tutafika tu dada. Usiwe na wasiwasi,” alisema Chiwamba.

Marina aliona hakukuwa na namna kwani huko nyuma kabla ya ujio wa bodaboda wagonjwa walikuwa wakipelekwa kwenye matibabu Mayamaya kwa baiskeli au kwa miguu. Alikumbuka siku moja bibi yake aliumwa sana usiku wakalazimika kutoa kitanda cha chuma, kikageuzwa mithili ya machela kisha wakatafutwa wanaume takribani kumi pale kijijini waliombeba kumpeleka zahanati.

Saa tatu kasoro dakika chache usiku, walikuwa wanafika mbele ya zahanati ya Mayamaya na kukaribishwa na mlinzi. Wakaingia ndani, Celine akalazwa kwenye benchi.

Marina alimweleza yule mlinzi shida ya mgonjwa na kwamba alihitaji huduma haraka sana. Mlinzi akawaambia wasubiri akawaite wahusika.

“Si tulikwambia dada ni nadra usiku kuwakuta wahusika. Lakini huduma atapata ingawa niliwahi kusikia tabibu aliyeletwa hapa kwamba ni cha pombe,” alisema yule kijana mwingine na kuongeza kwamba kwa bahati nzuri tabibu huyo wa zahanati na hata muuguzi wanaishi hapohapo jirani na zahanati.

“Kwani zahanati hii ina watumishi wawili tu, tabibu na muuguzi?”

“Huwa wako wauguzi wawili lakini nasikia yule mama aliyekuwa hapa muda mrefu tangu sisi tukiwa watoto alistaafu kwa hiyo yuko mmoja tu,” alijibu Chiwamba. Marina pia alimkumbuka muuguzi huyo wa muda mrefu.

“Ninakumbuka wakati ninaondoka kulikuwa na mkakati wa kujenga kituo cha afya hapa kwa kuwa Mayamaya ilikuwa inazidi kupanuka kwa haraka. Bado tu hakijajengwa?”

“Kinajengwa lakini hakijakamilika,” alijibu Chiwamba.

Mmoja wa wale vijana alidai kwamba kiasi cha wiki mbili zilizopita, yupo mama alifikishwa hapo saa saba usiku akiwa na matatizo ya kujifungua, lakini kwa kuchelewa kukosa huduma, hata ile ya kwanza, alifia hapo na mwanae tumboni. Habari zile zilizidi kumsikitisha Marina. Ni habari ambazo ukimweleza mtu anayeishi Marekani anaweza hata asikuamini.

* * *

Dakika chache baadaye, muuguzi alikuwa anaingia pale kwenye zahanati na akaagiza mgonjwa alazwe kwenye kitanda katika chumba cha mapokezi. Wale vijana wakambeba Celine na kumlaza kwenye kitanda kilichokuwa kwenye zahanati hiyo.

Marina alisimulia kwa kifupi matatizo ya Celine ambayo yanatokana na kukeketwa na kikubwa alisema alitokwa damu nyingi na kwa muda mrefu na sasa ana homa kali na anasema misuli inamvuta.

“Bila shaka atahitaji kuongezewa maji na damu,” alisema Marina.

Yule muuguzi akionekana kusikitika, alisema kwamba zahanati ile ndogo haikuwa na lolote la kumsaidia mgonjwa kama yule.

“Nawashauri mwende hospitali kubwa, Dodoma… Na hapa Centre muda huu, saa tatu si rahisi kupata usafiri. Magari hapa yanakata kabisa saa mbili. Mngefika mapema mngeweza kubahatisha hata magari ya mkaa yanayotoka huku usiku usiku kukwepa kukamatwa yakawapeleka,” alisema.

Lakini aliongeza pia kwamba suala la kukeketwa lilitakiwa pia kuripotiwa polisi, wapate fomu ya polisi namba tatu ndipo waanze matibabu.

“Sikiliza dada, mgonjwa ana  hali mbaya na kinachotakiwa ni kuokoa maisha yake badala ya kuanzia polisi… Lakini tumesikia kuna tabibu hapa, yeye kwa nini asije naye kumwona mgonjwa?”

“Kwa hali ya mgonjwa nashauri tu mwende hospitali kubwa, Dodoma. Isitoshe sasa anaweza akawa keshaonja kidogo. Huo muziki kama unausikia unatoka mahala anakokunywa pombe kwa sababu nilipita pale muda mfupi uliopita nikamwona,” alijibu yule muuguzi. Toka wawasili hapo walikuwa wakisikia muziki wenye makelele si mbali sana na mahala hapo.

“Sasa tufanyeje dada’ngu?” Alihoji Marina.

“Si rahisi kupata usafiri hapa. Inabidi mlale tu hadi asubuhi na mapema mjaribu kubahatisha usafiri umpeleke hospitali. Hapa mimi nitampa vidonge tu kwa ajili ya kumpunguzia maumivu,” alisema yule muuguzi.

Marina akamjibu kwamba alikuwa keshampa dawa za maumivu na kumtajia aina ya dawa alizompa. Wakati Marina akitafakari hali ile huku akifikiria kuondoka na wale waendesha bodaboda kwenda nao mjini Dodoma, mdogo wake aliendelea kuguna kwa maumivu kuonesha kwamba alikuwa anajisikia vibaya sana pale kitandani.

Mara walisikia mlango wa zahanati ukigongwa na mtu akaingia huku akiuliza. “Nani yuko humu?” Yule muuguzi hakujibu. Akamwambia Marina kwa sauti ya chini kwamba huyo ni tabibu wa zahanati hiyo ambaye wananchi wa kawaida walimwita daktari.

“Neema, una wagonjwa. Wamekupa shilingi ngapi… Oh! Una binti mrembo hapa, I love you dear,” alisema tabibu yule mtu mzima kidogo akimgeukia Marina baada ya kumtia machoni.

“Bosi John, hawa wana mgonjwa anayehitaji huduma ya haraka. Hebu mwangalie,” alisema muuguzi.

Yule tabibu alimwangalia mgonjwa na kuuliza kama alishapewa dawa ya maumivu. Alipojibiwa kwamba tayari akashauri kwamba ni vyema awahishwe hospitali kubwa haraka.

“Leo mbunge kalala hapo kwa mama yake. Mkamwombe kama amekuja na dereva wake awape msaada. Siku hizi anajipendekeza kwa wananchi kwa vile uchaguzi unakaribia. Anaweza kutoa msaada,” alisema yule tabibu. Neema akaunga mkono. Akasema kwamba kwa sababu tarehe za uchaguzi zinaanza kusogea mbunge wao ameanza kujipendekeza kwa wananchi.

“Kwa vile ni suala la ugonjwa, kwake utakuwa ni mtaji wa kura. Majuzi kulikuwa na msiba hapa karibu kila kitu aligharimia yeye. Na siku hizi anakuja sana hapo kwao lakini akishachaguliwa anahamia mjini. Hatumuoni ng’o,” alisema muuguzi yule, Neema.

Marina alimwomba Neema amsindikize kwa mbunge na yule tabibu akabaki pale kuwasubiri huku akimwangalia mgonjwa. Marina alishukuru kwa ushauri wa tabibu yule licha ya mwanzo kukerwa na ulevi wake. Akaomba kijana mmoja kati ya wale wawili awasindikize kwenda kwa mbunge ambako hakukuwa mbali sana kutoka pale kwenye zahanati.

Walitoka haraka kuelekea kwao na mbunge wa jimbo la Mayamaya. Neema alirudia kumwambia Marina kwamba mbunge huyo kwa muda mrefu alikuwa amejisahau na sasa ndipo anahaha kuwa karibu na wapiga kura baada ya kuona uchaguzi umekaribia.

“Kuna kijana hapa msomi, kwa sasa ni mkurugenzi katika halmashauri fulani, nasikia ndiye watu wanamtaka na kwa kweli mimi huwa ninaona hakuna mbunge hapa. Ameshindwa hata kuibana serikali kuboresha hii zahanati na kumalizia ujenzi wa kituo cha afya. Na kimsingi kwa jinsi Mayamaya ilivyopanuka na sasa ni mji mdogo inahitaji hospitali kamili ambayo itakuwa inamhudumia hata mama yake. Hata kwenye zahanati tunahitaji wauguzi wawili zaidi na tabibu mwingine mmoja,” alisema Neema wakati wakielekea kwenye nyumba aliyosema ndiyo ya mbunge.

Aliongeza: “Kama alivyosema tabibu, endapo kaja na dereva wake atakubali tu kutoa msaada.”

“Anaitwa nani huyu mbunge?”

“Nyagani.”

“Ahaa! Bado ni mbunge. Nakumbuka uchaguzi fulani alikuwa anakuja kwa babu yangu kijijini Mtakuja ili amsaidie mambo ya kampeni. Babu yangu ndiye mwenyekiti wa kijiji.”

“Babu yako ni nani…”

“Chilyawanhu.”

“Namfahamu. Mzee mbishi sana yule, aking’ang’ania jambo lake ameng’ang’ana. Kama zamani alipewa kidonge cha Asprin cha rangi ya njano, leo ukimpa kidonge cheupe cha Asprin hiyo hiyo hakubali. Yuko tayari hata kupanda basi kwenda kununua Asprin ya njano Dodoma mjini akiamini ndiyo itamponyesha.”

“Kumbe unamfahamu vizuri babu. Vipi mbunge, anatatua kero zenu?”

“Hana analofanya. Tena wanasema ana bahati jimbo liligawanywa yeye akabaki huku Mayamaya vinginevyo asingeshinda uchaguzi uliopita. Kule alikuwa hakubaliki kabisa na inasemekana yeye aliweka ushawishi mkubwa bungeni jimbo kugawanywa baada ya kuona hakubaliki kule kwingine. Hata hivyo, jimbo lilikuwa kubwa sana.”

“Kwa hiyo anataka kugombea mara ya pili?”

“Hii itakuwa mara ya tatu.”

“Akiniamini akatupa gari nitashukuru kwani nitaweka mafuta na hata kumlipa ujira wowote atakaotaka kwa sababu ninaweza kuendesha gari. Cha msingi ni kuokoa maisha ya mdogo wangu,” alisema Marina. Kitu cha kwanza alichokifanya, hata kabla hawajaondoka na mumewe kwenda Marekani ilikuwa ni kujifunza kuendesha gari.

Akaendelea: “Ninahofia tu mgonjwa hawezi kujishikilia vizuri na hivyo inakuwa taabu kumbeba lakini tukikosa usafiri tutakwenda hivyo hivyo na pikipiki hospitali kubwa Dodoma mjini, au unasemaje kaka,” alisema Marina akimgeukia yule mwendesha bodaboda ambaye alijibu kwamba yeye na mwenzake wako tayari.

Nyumba iliyokuwa mbele yao katika barabara kuu ya kwenda Dodoma ilikuwa ni moja ya nyumba nzuri za eneo hilo na ambayo Marina alikumbuka kuiona wakati wanaelekea kijijini kwao. Ni nyumba ambayo haikuweko miaka saba iliyopita. Neema alimjibu kwamba mbunge huyo aliijenga mwishoni mwa kipindi chake cha kwanza cha ubunge.

Waligonga hodi getini na kufunguliwa na kijana mmoja wa kiume. Marina alipiga jicho pale uani na kuona gari aina Land Cruiser la mbunge huyo likiwa limeegeshwa.

Ilionekana walikuwa hawajalala. Marina aliangalia saa yake na kugundua kwamba ilikuwa inaelekea saa tatu na dakika tano usiku. Yule kijana aliwakaribisha ndani.

Waliingia sebuleni na kumkuta mbunge huyo akiwa ameketi na mama mmoja mtu mzima, Marina alihisi kwamba ndiye mama wa mbunge huyo. Neema, kama mwenyeji, alijitambulisha na kisha kumtambulisha mtu waliyekuwa wameandamana naye.

 “Wewe ni mjukuu wa Mzee Chilyawanhu?” Alihoji yule Mbunge.

“Ndiyo,” alijibu Marina.

“Mbona sikufahamu kwa sababu siku hizi ninakuja sana kwa babu yako,” alisema mbunge.

“Kwa takribani miaka saba sikuwepo nyumbani, lakini niliwahi kukuona miaka ya nyuma.”

“Ulikuwa wapi, Dar es Salaam?”

“Hapana… nilikuwa mbali tu na hapa Dodoma,” alijibu bila kutaka kusema kwamba alikuwa nje ya nchi.

“Wewe ni mtoto wa nani pale kwa Chilyawanhu?”

“Lucy…”

“Alaa, vizuri sana, nilikuwa namfahamu sana marehemu Lucy. Hata kazi CDA nilimtafutia mimi.”

Walimweleza shida yao akakubali kuwasaidia.

“Kumbe nyinyi ndio mlikuwa mnanishika miguu. Mimi ninaondoka sasa hivi kwenda mjini. Kwa hiyo nisubirini hapo nje nimalize mambo fulani na mama yangu, halafu tumwahishe mgonjwa hospitali,” alisema Mbunge, sentensi ambayo ilimpa faraja kubwa Marina ingawa alitamani mbunge anyanyuke muda ule ule waondoke.

“Tunashukuru sana. Yaani mimi ninaamini kama mdogo wangu atalala hivi mpaka asubuhi bila kupata msaada, tunaweza kumpoteza. Tumemwacha hata kuongea hawezi,” alisema Marina kisha wakanyanyuka huku Marina akitamani kumwambia wamalize maongezi yao haraka ili wawahi hospitali lakini akasita.