">

Sarafu ya Gavana

Wilbard Makene

Boniphace alikunja mkono na kisha kuuelekeza upande wa kushoto wa kichwa. Spika ya simu alilengesha vizuri sikioni. Alimeza mate kulainisha koromeo lake, kisha akasema, “Ameshafika ila amekuta mlango wa mbele umetiwa kufuli. Amegonga kengele bila mafanikio.”

Kabla hajajibiwa simuni, Boniphace alichungulia nje ili kuhakikisha hakuna anayemsikia wala kumwona. Alipojiridhisha, akarudisha uso ndani. Makwapa yake yalilowa jasho kwa hofu, moyo ulimwenda mbio, miguu iliyokuwa imeachia breki za gari ilikuwa ikitetemeka kama mcheza kiduku.

Kiyoyozi cha gari hakikufua dafu kuzituliza tezi za jasho kutoa taka. Boniphace alijitahidi kuficha kilichoendelea ndani ya akili yake, lakini mwili ulimsaliti; kila kiungo cha mwili, kuanzia utosini hadi kidole cha mwisho cha mguuni, vilidhihirisha wazi kile kilichokuwa kikiendelea kichwani mwake.

“Sina hakika na usalama eneo hili,” Boniphace alindelea kuongea huku akimwangalia bosi wake, Gavana wa Benki Kuu ya Weusi Kusini.

Boniphace alikuwa amemaliza kumshusha kwenye gari Gavana aliyekuwa ametoka kazini. Kiutaratibu na kulingana na mafunzo aliyopewa, Boniphace alitakiwa kuhakikisha bosi wake anaingia ndani akiwa salama kabla ya yeye kuondoa gari. Aliendelea kumtazama Gavana akitembea hadi alipoufikia mlango. Gavana aligonga kengele mara kadhaa bila kufunguliwa.

Boniphace, akiwa yu-ndani ya gari na simu sikioni, aliendelea kuzungumza, “Mimi mwenyewe sina hakika na usalama wangu mahali hapa.”

Mtu aliyekuwa akizungumza naye simuni akajibu, “Acha woga, endelea kufanya kazi. Kila kitu kitakuwa sawia. Maelekezo mengine nitakupa baadaye.”

Simu ikakatwa.

Boniphace alitoa mkono sikioni, na kuuelekeza mfuko wake wambele. Aliiachia simu itulie iserereke kuelekea ukingo wa mfuko.

Baada ya Boniphace kuuondoa mkono wenye simu sikioni, na kuiweka simu kwenye mfuko wa suruali yake, alirudisha macho kule mlangoni alikosimama Gavana. Bado mlango ulikuwa haujafunguliwa.

Hali hiyo ilimtatiza Boniphace, hakujua kama ni hali ya kawaida tu hivyo anaweza kuondoka. Ni hali tatanishi hivyo anapaswa kwenda kutoa msaada.

Laiti angelijua, asingeliendelea kupoteza muda kwenye gari.

….