Gharama ya Uhariri

Suala ambalo waandishi wengi hupenda kulifahamu ni kuhusiana na gharama ya uhariri ambayo anapaswa kulipia mswada wake ili uweze kuhaririwa. Huu ni ufafanuzi mfupi kuhusiana sababu za kutofautiana gharama kutoka mhariri mmoja hadi mwingine. Zifuatazo ni miongoni mwa sababu hizo;

1. Ukubwa wa kazi
Kuna wahariri ambao huangalia idadi ya kurasa za mswada, na wengine huangalia jumla ya idadi ya maneno ili kupanga gharama ya uhariri. Wahariri hawa huweza kuwa na gharama tofauti. Wahariri wengine hulipwa kwa saa (muda) mfano kila saa moja ya uhariri hugharimu shilingi elfu 10.

2. Uzoefu wa mhariri
Wahariri wenye uzoefu mkubwa wa kazi ya uhariri aghalabu gharama zao za uhariri huwa kubwa, na ubora wa kazi zao huwa wa hali ya juu ukilinganisha na wahariri wenye uzoefu mdogo, ambao wachache kati yao huweza kutoka kazi zenye ubora wa hali ya juu.

3. Haraka ya mwandishi
Mwandishi ambaye huhitaji uhariri wa haraka (express) hupaswa kutoa kiasi kikubwa cha pesa ukilinganisha na mwandishi ambaye yupo tayari kusubiri kazi yake ihaririwe hata kwa miezi 6. Kadri muda wa uhariri unavyokuwa mdogo ndivyo gharama ya uhariri huongezeka.

4. Ugumu wa kazi
Kazi nyepesi kuhariri huweza kuwa na gharama ndogo ukilinganisha na kazi ambazo humhitaji mhariri kuwekeza akili yake nyingi kuishughulikia kazi husika. Kabla kazi kuwasilishwa kwa mhariri ni muhimu iwe imepitiwa na watu makini walau wawili au watatu ili kupunguza makosa madogo madogo, hii hupunguza gharama ya uhariri pamoja na muda wa uhariri.

5. Uchipukizi au ukongwe wa mwandishi
Waandishi chipukizi huhitaji msaada mkubwa wa kuboresha kazi zao kuliko waandishi wakongwe hivyo kuhariri kazi zao huwa ni gharama kubwa zaidi. Mhariri anaweza kuhariri kazi ya mwandishi chipukizi na kuirudisha kwa mwandishi kwa marekebisho hata zaidi ya mara tatu (kazi moja huweza kuchukua muda mwingi wa mwandishi na mhariri), hii huwa tofauti na waandishi wenye uzoefu wa kutosha ambao aghalabu kazi zao hurudishwa walau mara moja tu kwa marekebisho.

Kwa huduma bora ya uhariri kwa gharama nafuu usisite kuwasiliana nasi.

(+225) 715 001 818 | 787 001 819

info@uhariri.com