Kisima cha Giningi
Tangu mwaka 1968 mwandishi Mohammed S. Abdullah anaandika riwaya hii hadi sasa, kumekuwa na ongezeko kubwa la waganga matapeli, labda kwa kuwa kile alichoshauri hakikufanyiwa kazi.
Ni vyema serikali ikatazama kwa macho mawili, ushauri wa waandishi wa vitabu ili kuzidi kujenga taifa imara.
Tuache hayo, twende sasa kwenye Kisima cha Giningi.
Kama unatamani kuifahamu vizuri Giningi na mauzauza yanayodhaniwa kuwepo huko, nenda kamsome Profesa Said A. Mohammed (SAM) katika tamthiliya ya ‘Kivuli Kinaishi’, huko utakutana na Bi Kirembwe, na mambo ya unga wa ndele.
Sasa basi, kama jina la kitabu lisemavyo ‘Kisima cha Giningi’.
Riwaya inaanza Bwana Msa anapokea barua ya wito kutoka kwa rafiki yake (Spekta Seif), kutoka Giningi Police Station, bila hiyana anamuaga Nujum tayari kwa safari ya kwenda kumsabahi rafiki yake, ambaye hawajaonana muda mrefu tangu kuisha kadhia ya ‘Mzimu wa Watu wa Kale’.
Kufika tu Giningi kwa mwenyeji wake, Sajin Paolo anampa taarifa fupi bosi wake (Spekta Seif), mbele ya Bwana Msa.
“Yule bwana aliyeripoti jana kanzu yake imeibiwa uwanjani pake juu ya kamba, amefika stesheni leo. Anasema kanzu yake imerudishwa pale pale juu ya kamba uwanjani pake, lakini anasema imekatwa, vipande vitatu vimetolewa, viwili mikononi na kimoja shingoni, na kanzu yote inanukia mafusho mabaya sana kama ilifukizwa kwa mavi ya punda makavu.”
Mambo ya ushirikina yameanza.
****
Yule bwana aliyeibiwa kanzu akaenda tena polisi, akawaambia polisi kuwa Fundi Mangungu kasema kanzu ile asiivae tena, ampelekee hela yeye atajua cha kufanya, hakuishia hapo akatia nia ya kwenda kwa Shehe Haji kusoma halbadiri.
Mambo mazito.
Hili halijaisha polisi, linakuja la Mwana wa Giningi kuibiwa dhahabu na pesa zake. Kwenye maongezi yake naye akamtaja Fundi Mangungu, yaani kashapita kwa mganga kushughulikiwa kesi yake.
Aisee! Ile damu ya ushushushu ya Bwana Msa ikaanza kuchemka, kama volkano juu ya kilele cha mlima Kilimanjaro. Huku kiko yake ipo mkononi inafuka moshi.
Anajitosa mzimamzima kufuatilia kadhia ya Mwana wa Giningi kuibiwa, ndipo anakutana ana kwa ana na Fundi Mangungu, mganga anayeaminika kwa kuloga na kuagua.
Tangu utotoni mwake Bwana Msa alitokea kuwachukia waganga kwa uwongo wao, siku moja akiwa angali mtoto alienda chooni kwa lengo la kujisaidia, pale kwenye tundu la choo akakuta mdudu, kwa utoto wake anaogopa kujisaidia pale. Badala yake akachukua kifuu cha nazi na kujisaidia, kisha akachukua kifuu kingine akafunika…
Siku mbili tatu zikapita, mama yake akaenda sehemu ya kuhifadhia vifuu, kwa bahati mbaya akafunua kifuu kile kile chenye kinyesi.
Tobaaa! Mama yangu mzazi…
Stendi ya kwanza ya mama yule ikawa kwa mganga, mganga alimwambia mambo mengi ya uongo yaliyozua uhasama baina ya ndugu na kujizolea pesa za bure, kwa ujanjaujanja tu. Hali ile haikumfurahisha mwenye kinyesi chake, Bwana Msa.
Yeye ndiye aliyekuwa anafahamu vizuri ule uchafu ulifikaje mle, aliyosema mganga yalikuwa tofauti kabisa, mbingu na ardhi.
*****
Bwana Msa kwa mganga sasa.
Fundi Mangungu akasema, “mimi nilioteshwa usingizini leo usiku kuwa utakuja wewe leo… Basi sinyanyui mkono wangu kufanya chochote hadi unipe shilingi mbili,”
Bwana Msa akatoa noti ya shilingi tano, “chukua zako mbili, urudishe zangu tatu,”
“Aa, mimi sina senti moja hapa nilipo. Lakini wewe nipe hizo shilingi tano, mbili za kutazamia na tatu zitakuwa za dawa,”
“Ulijuaje fundi, kuwa nitahitaji dawa nawe hata hujanitazamia?” Bwana Msa aliuliza.
Ikawa vuta n’kuvute mganga anataka zote tano, huku Bwana Msa hataki kutoa zote tano. Wakamalizana kwa Bwana Msa kutoa shilingi 2 ya chenji aliyokuwa nayo mfukoni.
Haya ikaja kwenye shida iliyomleta sasa. Mganga akamuuliza lililomleta mteja wake, Bwana Msa akaangalia pajani kwa mganga akamwona nzi.
Akamwambia mganga, “nzi huyu akiruka kutoka pajani pako, atatua wapi pengine?? Kwa hakika hasa, fundi, hii ndiyo haja yangu iliyonileta kwako.”
Mganga akahamaki.
Mbilinge haikuwa ndogo. Ikawa kama tapeli kakutana na jambazi.
Mganga akacheka vibaya sana, kutoa jibu la swali aliloulizwa.
Baada ya kuhenyeshwa na Bwana Msa, yule mganga mwongo anayecheza na saikolojia za wateja wake akawa mpole kupindukia, maji yamemfika shingoni.
“Sasa wewe watakaje,” Aliuliza Fundi Mangungu kutaka suluhu.
“Nataka uwache kudanganya watu na kuwanyang’anya pesa zao kwa hadaa… Na sasa hivi ni bora unipe pesa zangu ulizozifutika kiunoni kwako mbio mbio. Nipe shilingi zangu mbili upesi upesi kama ulivyozipokea.”
Kutaka kuepusha shari, Fundi Mangungu, kwa mara ya kwanza katika tarehe ya kazi yake ya uganga, alirudisha pesa zilizokwisha kuingia mkononi mwake, na kubatilisha ule msemo maarufu, “Kiendacho kwa mganga hakirudi”.
*****
Waganga matapeli wapo wengi bwana, tujihadhari. Tukiacha mbali habari za waganga matapeli, pia wahariri matapeli wapo. Usisite kuwasiliana nasi kwa huduma bora ya uhariri, isiyo na utapeli.
Kalunga Matovolwa.
0715001818
0787001819