Kosa la Mwisho

Hussein Tuwa

Kimwaga alijichukia.
 
Alivyomfanyia mkewe, hapana… alivyomtenda mkewe… yeye mwenyewe hakuweza kujisamehe.
Sembuse mkewe?
 
Na hiki ndicho kilichozidi kumfanya ajichukie. Mainda alishamfumania mara chungu mzima, lakini mara zote hizo, alimsamehe huku akimsisitizia kuwa alikuwa akimpenda sana na hakutaka aendelee kupotea kwa kutopea kwenye ufuska.
 
Lakini yeye hakubadilika. Aliendeleza ufuska wake tu.
 
Mainda alishakuta meseji za mapenzi kwenye simu yake, si chini ya mara kumi. Aliishia kulia tu kimyakimya, huku akimwonesha zile meseji zake za aibu.
 
Badala ya kujutia, yeye akawa ni wa kumgombeza na kumsimanga dhidi ya tabia yake ya kupekua simu yake.
“Tena ukome kabisa tabia hii nakwambia. Ni dharau kubwa hii… siyo adabu kabisa hii. Lazima uheshimu faragha yangu, Mainda! Utapekuaje simu yangu kila unapojisikia tu bwana?” Aliwahi kumfokea kwenye moja ya matukio yale. Akamgeuzia kosa. Mkosa akawa Mainda, mkosewa akawa yeye.
 
“Ni sawa mume wangu, lakini elewa kuwa wewe ndiyo faragha yangu… aibu yako ni yangu baba Nsaji!” Mainda aliwahi kumjibu hivyo siku moja.
Huwa akimwita kwa jina la mtoto wao kwa kwanza, yaani ‘baba Nsaji’, ni kwamba Mainda amechukia. Lakini pamoja na kuchukizwa kwake, bado Mainda alimwambia maneno yale kwa upole, huku akimtazama kwa macho yake mazuri, makubwa, yaliyokuwa yakibubujikwa machozi.
 
Yeye hakujali.
Wala asiishie hapo. Akamletea mtoto wa nje ya ndoa. Na hapo ndipo kwa mara ya kwanza akajihisi woga mkubwa. Alimwogopa Mainda kwa mara ya kwanza, kwani alijua sasa, ndoa yake ndiyo ilikuwa imevunjika. Ikamshukia wazi kuwa hiki ni kitu ambacho anakiogopa kuliko vyote – ndoa yake kuvunjika.
 
Angewaeleza nini watoto wao waliokuwa vyuoni wakisoma? Ni nani atakayeweza kumjali na kumvumilia, kama Mainda?
Aliogopa.
Lakini pamoja na misukosuko yote iliyofuatia kadhia ile, Mainda alimsamehe.
 
Kimwaga aliishiwa namna.
 
Hivi huyu mwanamke anawezaje kuendelea kunipenda namna hii, pamoja na yote haya ninayomfanyia?
Hakupata jibu.
 
Hivi ndivyo alivyokuwa akimfanyia mkewe, masikini.
Kamwe hakuwahi kujutia tabia hiyo…
 
Mpaka leo.
Leo alikuwa siyo tu anayajutia yote hayo aliyowahi kumfanyia mkewe, bali pia, alijichukia kwayo. Na sasa, aliinua uso wake na kumtazama Mainda wake.
Aliuona upendo wa dhati usoni na machoni kwa mkewe.
 
“Una simanzi mume wangu, lakini haya yameshaisha sasa. Si tumeshasameheana?” Mainda alimwambia kwa kujali. Macho yake, yalionesha huruma na kujali kukubwa, juu ya ule upendo uliofanya makazi ya kudumu kwenye macho yale.
“Ah, binti Shomvi! Hivi kweli unasema tumesameheana?” Kimwaga alimuuliza kwa hisia, “unapaswa useme umeshanisamehe kwa mara nyingine, siyo tumesameheana… kuna nini cha mimi kukusamehe wewe mke wangu?”
Mara chache anapouhisi upendo wake wa dhati kwa mkewe, hupenda kumwita kwa ubini wake, yaani ‘binti Shomvi.’
Mainda alijipangusa kijichozi.
 
“Ooh, b’ba Nsaji wangu… usinifanye nilie upya, baby… yameisha haya. Kosa lako ni langu na langu ni lako, si ndiyo?”
Kimwaga alibaki akimtazama pasi na jawabu.
Maida aliinuka na kumbusu kwenye paji la uso.
 
“Wacha nikaandae chajio tule mume wangu… tukalale!” Alimnong’oneza huku sauti ikimvunjika kwa kwikwi ya kilio cha uficho, na Kimwaga alilihisi fukuto la chozi la mkewe lililomdondokea shavuni kwake.
Kisha Maida akageuka haraka na kuelekea jikoni, “Leo ni supu ya ulimi kwa ndizi za kuchemsha!” Mainda alisema huku akipotelea jikoni na akijipangusa chozi kwa kiganja cha mkono wake.
 
Wakati akimtazama mkewe akielekea jikoni namna ile, Kimwaga alihisi donge gumu kooni na myeyuko wa fukuto moyoni.
 
Ule ni mlo aupendao sana, na mkewe hulazimika kuamka alfajiri sana kuwahi ulimi wa ng’ombe buchani, kila anapotaka kumpikia mlo ule.
 
Ama hakika huyu mwanamke ni wa ajabu sana.
 
Na hapa Kimwaga akapigia mstari nia yake ya kubadilika. Anabadilika rasmi kuanzia usiku ule. Ataacha umalaya wake wote. Atapiga chini vimichepuko vyote. Atavifungia vioo vidangaji vyote. Yeye na Mainda tu sasa. Yeye na mama Nsaji wake. Yeye na binti Shomvi, binti Shomvi na yeye. Siyo kwa upendo huu. Siyo kwa kujaliwa huku. Alikuwa mjinga sana siku zote hizo, lakini sasa ameerevuka.
 
Anatulia ndoani.
Wakati akiwa amejibweteka kinyonge pale sebuleni akisubiri mlo wake aupendao, akili yake ikamrudisha kwenye mjadala aliotoka kuushiriki yapata saa moja tu iliyopita, baina yake na bwana Hamduni, rafiki yao mkubwa na mshenga wake.
 
Ulikuwa ni mjadala mchungu sana maishani mwake, kwani ulikuja baada ya yeye kufanya kosa kubwa kabisa dhidi ya Mainda, ambalo kwalo, Mainda mwenye upendo aliapa kutomsamehe.
Alifumaniwa akiwa na shemeji yake, mdogo wa mkewe… toka n’toke!
***
Alichokiona machoni kwa Mainda baada ya fumanizi lile kilimtisha. Kilikuwa kipya kabisa, kwani badala ya kulalama huku akilia kama afanyavyo siku zote, Mainda alibaki akimtazama huku ameilaza shingo yake upande hali akibubujikwa machozi kimya kimya. Kuna kitu kwenye macho yake hakuwahi kukiona hata siku moja, na hakuweza kukijua ni kitu gani – ila kilimtisha sana.
 
“Kwa hili sitokusamehe, b’ba Nsaji!” Hatimaye Mainda alimwambia kwa simanzi kubwa kabisa.
“Ah, Ma, Mainda-”
Mainda alimnyamazisha kwa kumwinulia kiganja cha mkono, naye akajikuta ananyamaza pasi kupenda. Wakatazamana. Alichokiona kwenye macho ya Mainda, kilimtembezea buibui kwenye uti wa mgongo.
Oh, Mungu wangu… ataniacha huyu!
 
“Mainda…”
Mwenzake aligeuka kwa hasira na kwenda kujifungia chumbani.
Juhudi za kumsihi afungue mlango ziligonga mwamba. Kila alivyoita na kujieleza na kujiapiza nje ya ule mlango, hakupokea jibu hata moja kutoka kwa Mainda.
 
Tafsiri mpya ya kile alichokiona machoni mwa Mainda ambacho kilimtisha sana, ikajijenga akilini mwake.
Mainda amejiua!
Oh, Mungu wangu!
 
Akaanza kuvunja mlango.
“Hebu toka hapo malaya koko wewe!” Sauti ya Mainda iliyojaa ghadhabu ilimfikia kutoka nyuma ya ule mlango.
Oh, angalau hajajiua!
 
Ndipo akampigia simu bwana Hamduni. Akamsihi afike pale haraka. Kwa kuwa hakuwa akiishi mbali nao, bwana Hamduni alifika haraka na kumkuta akiwa nje ya mlango wa chumba chao, akimbembeleza Maida amfungulie.
Bwana Hamduni akamtaka amjuze kulikoni, na Kimwaga akamweleza. Jicho alilokatwa na rafikiye lilitosha kumjuza kuwa alikuwa peke yake kwenye kadhia ile.
 
“Kwa hiyo umeniitia nini hapa mimi, Kimwaga?” Hamduni alimuuliza kwa hasira, na Kimwaga akalia mbele yake. Alimwambia kuwa hakutaka kumpoteza Mainda. Alimjuza kuwa ameshajua makosa yake na sasa anataka kubaki mtulivu kwa mkewe. Akamwomba amsihi Mainda asichukue maamuzi ya kujitenga naye. Hatorudia, ametubu.
Bwana Hamduni naye hakumbakisha. Alimsema vilivyo. Alimfokea na kumkemea. Alimsonya na kumpiga masingi. Kimwaga alimchefua na yeye akamchefukia.
 
Hatimaye, bwana Hamduni, ambaye siku zote huwa ana nafasi laini moyoni kwa Mainda, alimsihi shemejiye afungue mlango wayaongee.
 
“Shemeji nitatoka kwa heshima yako tu, lakini huyo bazazi sitaki kabisa nimkute hapo!” Mainda alimtupia jibu kutokea nyuma ya mlango.
 
Kimwaga akatoka nje. Akaiacha hatima ya ndoa yake mikononi kwa rafiki yake, bwana Hamduni.
Alipoitwa tena ndani nusu saa baadaye, aliingia pale sebuleni kwake akiwa ameelemewa na uzito wa mabega yake.
Bwana Hamduni alimwambia kuwa amemweleza mkewe yale ambayo yeye alimweleza kabla hajatolewa nje, kisha akamweleza kuwa amesikia upande wa Mainda kuhusu tukio lile baya alilolifanya, akishirikiana na mdogo wa mkewe.
 
“Lakini pamoja na yote haya, hususan hili la leo hili…” Bwana Hamduni alimwambia na kuweka kituo huku akiwa amemkazia macho, “ Mainda, shemeji yangu aliyefundwa akafundika, amekubali kukusamehe, Kimwaga.” Alimalizia na Kimwaga aliyekuwa amejiinamia kwa fadhaa, aibu na majuto, akainua kichwa kumtazama kwa mshangao.
 
“Naam Kimwaga… amekusamehe mkeo.”
“Oh, Mainda!” Kimwaga alikurupuka na kumfuata mkewe akiwa amechanua mikono tayari kumkumbatia, lakini Mainda alijikumbatia yeye mwenyewe. Hakutaka kukumbatiwa naye.
Kimwaga akagwaya. Alimtazama Mainda kwa macho yaliyotatizika, akakutana na macho yaliyokwazika.
 
“Ongea na shemeji Hamduni kwanza…” Mainda alimwambia, kisha akainuka na kuingia chumbani, akimwacha Kimwaga na bwana Hamduni pale sebuleni.
Ndipo alipojikuta akikabiliwa na makemeo makali kabisa kutoka kwa rafiki yake.
“Kimwaga inabidi ukuwe sasa rafiki yangu! Hivi unajua ni wangapi wanatamani kupata mke kama Mainda wewe? Hebu tazama umri wetu basi kaka! Siye siyo tena wale tuliokuwa tunavaa mapekosi na kunengua kwenye kumbi za dansi bwana!”
 
“Aah, Hamduni, miye sipo tena huko sasa, kaka! Si nimeshakwambia?”
“Hata kama! Usije ukaniita tena hapa kwa maujinga yako mimi nakwambia! Huyu mama ameumia sana leo… alikuwa anaelekea kubaya huyu! Shukuru Mungu amekubali kukusamehe Kimwaga, maana nakuhakikishia akitoka na virago vyake nje ya huo mlango…?” Bwana Hamduni alimfokea na kumning’inizia kauli huku akiuoneshea mlango wa nyumba yao, “watu watamnyakua fasta, nakwambia!” alimalizia, na Kimwaga akahisi mchomo mkali moyoni.
 
“Doh! Sitaki aniache aisee…!” Kimwaga alisema kwa kitetemeshi.
“Na kwa maelezo yake, hatokuacha Kimwaga… kwa sasa. Amesema hili ni kosa lako la mwisho Kimwaga. Anataka ubadilike na umwahidi mbele yangu kuwa utabadilika… na ikiwa unaona hutaweza kabisa kubadilika, basi amesema ombi lake ni moja tu. Mpe siku mbili apokee hela yake ya mchezo, asepe!”
 
“Mweh!”
“Sio ng’weee… hali ndiyo hiyo! Na usitake kutumia urafiki wetu kuniweka upande wako. Kwenye hili siko na wewe Kimwaga…”
“Nimekuelewa sana Hamduni.”
“Shemeji yako! Mdogo wa mkeo! Kweli?! Aah, ama kweli wee Fisi Maji aisee!”
Maneno hayo yalimchoma sana Kimwaga. Soni ikamjaa. Nafsi ikamnyanyapaa.
 
“Basi kaka, basi. Nimeelewa ndugu yangu … haya mambo mimi sasa basi. Huku nilipokuwa naelekea hakika ni kubaya.”
“Usiniletee ngonjera Kimwaga… unaahidi kuacha hii michezo?”
“Naahidi Hamduni. Naahidi.”
Walitazamana kwa muda. Hamduni aliiona dhamira ya kweli machoni kwa rafikiye.
 
Akaguna.
“Nakuamini… natumai hutaitusi imani yangu kwako, Kimwaga.”
“Siivunji na sikuvunji, Hamduni. Natulia na Mainda kaka. Imetosha. Uhuni sasa basi,” Kimwaga aliahidi, udhati wa alichokuwa akikisema ukimwagikia kwenye sauti yake.
“Uhuni wapi, ulimbukeni tu huo, Kimwaga?” Hamduni alimsuta.
“Sawa Hamduni…yote sawa. Naachana na hayo yote mimi!”
 
Bwana Hamduni akamwita Mainda. Kimwaga akaahidi kubadilika mbele ya mkewe, huku bwana Hamduni akiwa shahidi. Akamthibitishia kwa maneno yake mwenyewe kuwa hakika, lile ndiyo lilikuwa kosa lake la mwisho kumfanyia. 
 
Hatomtenda tena.
Mke na mume wakakumbatiana, na kufutana machozi.
Bwana Hamduni akaaga.
***
“Haya b’ba Nsaji, njoo tule sasa mume wangu!” Sauti ya Mainda ilimgutua Kimwaga kutoka kwenye kumbukumbu ile iliyokuwa ikijirudia mawazoni mwake.
 
Naam, supu ya ulimi ilikuwa ikinukia vizuri. Na Kimwaga, ambaye hata hakujiamini kuwa angeweza kula chochote kutokana na msukosuko aliosukuliwa nao usiku ule, akapata hamu ya kula.
 
Akasogea mezani na kwenda kuketi kwenye kiti kilichokuwa usawa wa bakuli lake. Bakuli lake siku zote huwa ni lile lile, na hakuna yeyote mwingine aliyeruhusiwa kula kutokea kwenye bakuli hilo.
 
Yeye si ndo baba mwenye nyumba?
Twaba’an. Mke na mume wakakaa mezani, wakitazamana huku mabakuli ya supu yakiwa mbele yao, na vijiko vikiwa kwenye mikono mlio.
 
Kimwaga akamtazama tena mkewe, na akaona jinsi Mainda alivyokuwa akimtazama kwa mchanganyiko wa upendo mkubwa na simanzi nzito, huku ameshika kijiko cha kunywea supu.
 
Akajawa hisia msuto.
“Mainda mke wangu… kiukweli kabisa-”
“Ah Kimwaga… yaache hayo tena sasa! Hebu tule tukalale mume wangu… au unataka tuanze kulizana upya saa hizi?” Mainda alimkatisha huku akijifuta kijichozi na wakati huo huo akijilazimisha kutabasamu.
Moyo wa Kimwaga ukamyeyukia mkewe.
 
“Sawa mke wangu…” Alimjibu huku akiliinamia bakuli lake la supu.
Kama kawaida yake, aliinusa ile harufu aipendayo bila shaka kuliko hata ile ladha ya supu yenyewe.
Ghafla, kiza kikatamalaki.
 
“AAAAH, TANESKOOO!” Mainda alipayuka kwa fadhaa na chembechembe za hasira baada ya giza kutanda ghafla. Kimwaga alibaki ameliduwaia bakuli lake la supu, gizani.
“B’ba Nsaji! Kan’letee kiberiti haraka niwashe mishumaa! Kiko pale sebuleni kwenye kijimeza kidogo pale!” Mainda alimwambia mumewe kwa wahka.
 
Kimwaga aliinuka taratibu huku bado akiwa analikodolea macho bakuli lake la supu gizani. Alienda kule alipoelekezwa na mkewe, kwa kunyata, akiihisi miguu yake ikiwa mizito ghafla. Yeyote ambaye angemwona alivyokuwa akitembea, angehisi alikuwa akihofia kujikwaa kwenye samani nyingine za mle ndani.
Huku nyuma mkewe akawasha tochi ya simu yake na mwanga ukapatikana.
 
“Ah, hiki ‘apa!” Alimsikia mkewe akisema nyuma yake, na muda huo huo akasikia mkwaruzo wa ujiti wa kiberiti kwenye ganda la kiberiti. Mwanga wa tochi ukachanganyika na ule wa mishumaa.
Alipogeuka, alimwona Mainda akiihamishia pale mezani, mishumaa miwili ambayo siku zote huwa inakaa kwenye kijimeza kidogo na chembamba, maarufu kama “console”, kilichokuwa kando ya meza yao ya chakula.
 
“Haya, njoo tule basi, tukalale… Ah, hawa Tanesko hawa!” Mainda alisema, sauti yake ikitoa mtetemo hafifu.
Kimwaga akajibweteka kwenye kochi pale sebuleni.
“Ah, hamu ya kula imeshaniisha tena, mke wangu… naona nilale tu.” Kimwaga alimwambia.
“Ah, sasa jamani… yaani nimekutengenezea supu uipendayo b’ba Nsaji!” Mainda alilalama.
“Na n’nakushukuru sana kwa hilo, mke wangu… ila kiukweli sikuwa na hamu ya kula tangu mwanzo… hawa Tanesko ndio wamenikata stimu kabisa, yaani!” Kimwaga alijitetea.
 
“Akh, sasa kwa nini, lakini?” Mainda aliuliza kwa mashaka makubwa.
Kimwaga akaguna na kupiga kimya. Alishukuru kuwa mwanga hafifu wa mle ndani haukumwezesha mkewe kuona jinsi alivyokunja uso kwa tafakuri nzito.
“Nimekukosea sana mke wangu, bado nafsi yangu inaumia kwa haya niliyokufanyia.”
“Eh, si tumeshayamaliza lakini?”
“Najua, na n’nakushukuru sana kwa hilo… ila naomba leo nilale tu, nikijutia makosa yangu Mainda. Labda kesho nitakuwa vyema?”
 
Mainda alipiga kimya huku akiyatazama yale mabakuli ya supu.
“Ah, sawa. Na mimi umeshanikata stimu ya kula!” alisema huku akiyarudisha jikoni yale mabakuli ya supu.
Wakalala.
Kulipokucha, Kimwaga akampa mkewe talaka.
***
“Hivi Kimwaga ni wewe kweli ndiye uliyemo kwenye hilo jumba bovu lako hapo juu, au umewaachia wapangaji tu humo?” Bwana Hamduni alimkoromea bila hata ya salamu, huku akikioneshea kichwa cha rafikiye alichokimithilisha na jumba bovu.
 
Kimwaga aliinuka na kwenda kuufunga mlango wa ofisi yake ili kuzuia wasaidizi wake kusikia maongezi yao.
“Tulia basi Hamduni… tulia kwanza. Hebu kaa kwenye kochi basi…” alimwambia kwa upole huku akimwelekeza kwenye moja ya makochi yaliyokuwa hatua kadhaa mbele ya meza yake ya kufanyia kazi.
 
Hamduni hakuketi.
“Hii nini hii, Kimwaga?” alimuuliza kwa hisia, huku akimtikisia nakala ya talaka aliyoiandika usiku wa manane wakati Mainda amelala, na kumkabidhi asubuhi kulipopambazuka.
“Najua haiingii akilini Hamduni, lakin-”
 
“Of Course haiingii! Mtu jana usiku tu nimetoka kuwapatanisha, halafu leo asubuhi naambiwa eti umempa talaka mkeo?” Hamduni alimjia juu.
“Ndiyo maana nakutaka utulie kwanza ili-”
 
“Demmit, Kimwaga! Hivi unajua wa kudai talaka alikuwa ni Mainda, na siyo wewe?”
“Miye sijadai talaka Hamduni… nimetoa talaka!”
“Basi nimeamini mwenye nyumba hayumo humo!” Hamduni alikishambulia tena kichwa cha rafiki yake.
Kimwaga akajibweteka kochini na kujiinamia kwa kukata tamaa.
“Unajitia kujuta sasa, siyo? Hivi umekuwaje laki-”
“Alitaka kuniua jana.”
“Eenh?”
 
Kimwaga akainua uso wake na kumtazama rafikiye kwa simanzi ya wazi.
“Kabisa ndugu yangu… hakika, talaka haikuwa kabisa akilini mwangu baada ya wewe kuondoka ile jana, na kabla Tanesko hawajakata umeme… lakini baada ya umeme kukatika? Kila kitu kikabadilika,” alimwambia kwa masikitiko makubwa na ya kweli, kiasi Hamduni akagwaya. Akaketi kochini kando yake.
 
“Hivi unajisikia unachoongea, kaka?” alimuuliza.
Kimwaga akamtikisia kichwa taratibu kukiri kuwa anajisikia.
“Na kinakuingia akilini kabisa?” alihoji zaidi.
“Hapana Hamduni, hakitakiwi kiniingie mimi akilini… kinatoka akilini mwangu hiki. Wewe ndiye unayepaswa kukiingiza akilini mwako rafiki yangu,” alijibu kwa unyonge mkubwa.
Hamdunu akajikuta anafumba mdomo, pasi kukumbika aliuacha wazi kipindi gani na ulibaki wazi kwa muda gani.
“Breaking News, kaka… hakiniingi akilini mimi!” Hatimaye alisema kwa kejeli ya ghadhabu, mara alipojaaliwa kuufunua tena mdomo wake.
 
Kimwaga aliguna tu na kutikisa kichwa kusi-kaskazi, kwa masikitiko.
“Tanesko inahusika vipi na hiki ulichokifanya, Kimwaga? Na hii habari ya kuwa eti Mainda alitaka kukuua… inatokea wapi hii? Nimemwuliza kama mligombana, amen’ambia hakukuwa na kitu kama hicho kabisa. Sasa hebu nieleweshe ndugu yangu, ni nini hiki?” Bwana Hamduni alimwambia rafiki yake wa tangu utoto.
“Hamduni, kuna methali inayosema Sumu mpe paka…?” Kimwaga alimwambia na kuiachia hewani ile methali.
“Mbuzi utamwonea,” Hamduni akajikuta anaimalizia ile methali huku akimtazama kwa kutoelewa.
 
“Exactly!” Kimwaga alidakia kumuunga mkono, “basi jana usiku Mainda alitaka kuiweka kwenye matendo hiyo methali, dhidi yangu kaka.”
“Sikuelewi na nimeshachoshwa na hii kombolela yako ya maneno, Kimwaga!”
Kimwaga alitikisa kichwa taratibu kukubaliana na hali ile. Akamtazama kwa huzuni kubwa rafiki yake.
“Nadhani unaelewa kuwa kabla ya kufungua hii kampuni yangu ya kusambaza kemikali za viwandani, nilikuwa mwalimu wa kemia, Hamduni… kwa hiyo haya nitakayokwambia ni mambo ninayoaelewa kiundani sana.” Alimwambia, na bwana Hamduni alimtazama tu bila kumjibu ingawa macho yake yalibainisha kuwa anamsikiliza ili aelewe zaidi.
“Aidha, unajua fika kuwa Mainda alikuwa mwanafunzi wangu wa kemia, kabla sijamwoa… na kuwa naye, ana ufahamu mzuri wa masuala haya.”
“Ndiyo, kwa hiyo?”
“Jana aliniwekea sumu hatari sana kwenye supu Hamduni…”
 
“Mainda?”
“Yes, kaka. Fosiforasi ya njano… elemental yellow phosphorus, kwa ufasaha zaidi.”
“Akh, kwa nini? Yaani, una ushahidi gani juu ya hilo? Na… kama ni hivyo, mbona bado uko hai?”
“Kwa nini…? Jibu lake liko wazi sana… ”
“Ambalo?”
 
“Akh, unajua nimelifikiria sana hili jambo jana usiku Hamduni,” Kimwaga alisema kwa fadhaa, akionekana kuchoka sana, kisha akaendelea, “chukulia kuwa mimi ni paka, na mdogo wake na vimada wangu wengine wote, ni mbuzi… mdogo wake na vimada wangu angeweza kuwamudu kwa njia rahisi sana iwapo akiamua, kama jinsi ilivyo rahisi kwa mtu kumkamata na kumdhibiti mbuzi. Lakini paka miye? Jana Mainda alijithibitishia kuwa paka miye hatoweza kunimudu wala kunidhibiti asilani… ”
 
“Ndiyo atake kukuua, kama unavyodai?” Bwana Hamduni alimuuliza huku amemkodolea macho sio tu ya kutoelewa, bali pia ya kutoamini.
 
“Sumu mpe paka, Hamduni… mbuzi utamwonea. Unakumbuka hiyo?” Kimwaga alikazia hoja yake ya awali.
“Una ushahidi gani juu ya hilo? Hiyo ni shutuma nzito sana!”
Kabla ya kumjibu, Kimwaga aliguna kwanza. “Ulinisimanga sana nilipoamua kuchukua mkondo wa sayansi shuleni, wakati wewe unakwenda kwenye masomo yako ya Arts, lakini jana usiku, uamuzi ule wa miaka ile mingi iliyopita ndiyo uliookoa maisha yangu.”
 
“Kivipi?”
“Sifa kubwa ya hii kemikali niliyokutajia, elemental yellow phosphorus, ni kwamba inakuwa highly luminous, yaani inang’aa sana, pindi ikichemshwa na ikiwa kizani…”
“So?”
“So, Tanesko walipokata umeme ghafla ile jana wakati mimi ndiyo nimeliinamia bakuli langu la supu tayari kuila, mng’ao niliouona kwenye supu yangu pale kizani, ulinirudisha moja kwa moja kwenye enzi zile nafanya practical za kemia na wanafunzi wangu darasani…”
 
“Ah!”
“Ndiyo! Siwezi kuupotea mng’ao wa kemikali ile hata uniamshe usingizini! Mainda alinijazia kiwango kikubwa sana cha kemikali ile kwenye supu kaka. Alinichoka Mainda. Aliona bora aniondoe duniani. Kutembea na mdogo wake lingekuwa ndilo kosa langu la mwisho kumfanyia!” Kimwaga alifafanua kwa kirefu.
Bwana Hamduni aliishiwa nguvu.
 
“Lah, kwa hiyo kukosa Tanesko kukata umeme…”
“Leo mngekuwa mnaniandalia maziko.”
“Sub-haana Llaah!”
Kimya kikatanda. Kimwaga aligeuka pembeni na kujifuta chozi kwa kujiibia.
“Sasa?” Hatimaye bwana Hamduni alihoji.
Kimwaga alishusha pumzi ndefu.
 
“Sasa ndiyo nikaamua kumpa talaka, kaka. Ni kwa kuwa nampenda sana Mainda. Sikutaka aje aishi na dhambi ya kifo changu, kwa makosa niliyomfanyia. Pia na mimi nijinusuru maisha yangu.”
“Doh!” Bwana Hamduni aliishia kuguna tu.
“Naomba unielewe, sitaki watoto wetu wajue kuhusu sababu ya hii talaka. Kamwambie Mainda haya niliyokwambia. Mwambie nilijua alichotaka kunifanyia ndio maana nimeamua hivi.”
“Halafu?”
“Halafu basi. Sitaki alete shida tu ya kuubishia uamuzi wangu. Najua hatobisha akijua kuwa nimejua alichotaka kunifanya ile jana. Ila mwambie kuwa mimi sitalisema popote hili, na wewe nakutaka hili liwe siri yako,” Kimwaga alisema huku akiinuka.
Akaenda mezani kwake, akavuta droo ya ile meza. Akatoa mfuko wa nailoni, ndani yake kukiwa kuna bakuli.
Akamwonesha.
 
“Hili ndilo bakuli langu la supu. Nilienda kulifuata jikoni jana usiku wakati yeye amelala. Kuna kiasi kidogo cha supu aliyoniwekea humu. Nalishikilia hili bakuli na supu yake kama ushahidi, ikiwa atataka kuniletea shida. Airidhie hiyo talaka, na asiwaambie wanetu sababu halisi ya mimi kumtaliki.”
 
Bwana Hamduni akapigwa butwaa.
 
“Sasa awaambie nini?” alimuuliza.
Kimwaga akatabasamu kwa fadhaa.
“Kila mtu anajua kuwa mimi ni Fisi Maji, bwana. Hiyo ni sababu tosha sana,” alimjibu, na Hamduni akatikisa kichwa kwa mastaajabu.
 
“Nenda kamweleweshe Mainda rafiki yangu, nina mkutano muda si mrefu hapa ofisini,” Kimwaga alimwambia.
Bwana Hamduni aliufuata mlango wa kutokea nje ya ofisi ya rafikiye huku akiwa amezongwa na mawazo. Alipofika mlangoni, akageuka.
 
“Lakini… nyie mnapendana hakika. Kama yeye ameshakusamehe makosa chungu mzima, kwa nini na wewe usimsamehe hili mkaishi kwa upendo tu?” alimwambia rafikiye kwa kuomboleza.
Kimwaga alimtazama rafiki yake kwa muda.
 
“Ni kweli Hamduni… nilipoahidi kuwa la jana lilikuwa ndiyo kosa langu la mwisho? Nilidhamiria iwe hivyo, hakika. Lakini kumbe Mainda naye alilidhamiria hilo kwa maana yake binafisi… alilikusudia lile liwe kosa langu la mwisho kabisa hapa duniani, kwa kuniondoa duniani!” Alimwambia kwa huzuni.
 
“Dah, ni kweli kaka. Lakini, hiyo ndo imeshakuwa sasa… haimaanishi kuwa msisameheane… usimsamehe! Naamini, ukimsamehe kwa hili na ukaishi naye kwa uaminifu kama ulivyoahidi, Mainda hatakuwa tena na sababu ya kufanya tena kitu kama hiki!”
Hamduni alisimamia ushauri wake, kwa rafiki yake.
Kimwaga alimtazama kwa muda huku akiwa kimya, akionekana kuyatafakari maneno ya rafiki yake. Kisha sura yake ikachanua kwa tabasamu la fadhaa.
“Ni kweli kuwa mimi ni Fisi Maji Hamduni, lakini hakika siyo kichwa maji. Mara nyingine Tanesko wanaweza wasizime umeme kwa wakati.”
*Mwisho*
 
Hussein Tuwa
Goba, Dar es Salaam
Machi 15, 2021