Miss Tz

Hussein Tuwa

Bishkuku

Mtaa wa Aggrey, Kariakoo, Jijini Dar es Salaam – Wakati uliopo:

Binti wa urembo namba tatu Afrika Mashariki wa mwaka 79 aliyependa na aliyezoeleka kutambulika kwa jina moja tu la Bishkuku, alikuwa amefura kwa hasira wakati akitazama pilika pilika za jiji zilizokuwa zikiendelea nje ya nyumba ya msajili iliyokuwa eneo lile lenye harakati lukuki jijini Dar.

Akiwa kwenye ghorofa ya nne ya jengo lile la msajili, aliweza kuona eneo kubwa sana la jiji, lakini yote aliyoyaona kule nje hayakuleta maana yoyote akilini mwake, na hayakuleta maana kutokana na ukweli kwamba akili yake ilikuwa ikichambua jambo moja tu wakati ule.

Lakini kadiri alivyozidi kulichambua ili angalau limwingie akilini, ndivyo jambo lile lilivyozidi kuivuruga akili yake!

Jambo lililokuwa likimvuruga akili asubuhi ile lilikuwa nyuma yake wakati ule, ameligeuzia mgongo, na lilikuwa likijidhihirisha katika namna ya binti mmoja mrembo na mwenye uelewa wa hali ya juu, ambaye alikuwa anafanya jambo lisiloendana kabisa na uelewa wake.Na kwa sababu hiyo Bishkuku alikuwa amechukia vibaya sana.

Alitoa sauti ya kukereka na kutupa mikono yake hewani huku akigeuka kutoka pale dirishani na kumtazama yule binti aliyeketi kwa pozi la kuvutia kwenye moja ya makochi yake pale sebuleni.

“Tunis…! Kwa nini lakini Tunis, eenh?” Alimuuliza kwa hasira iliyofungamana na kushangazwa, na hicho ambacho yule kiumbe mwenye urembo wa sura na maumbile aliyekuwa pamoja naye mle ndani alikuwa anataka kukifanya.

“Ah…Si nd’o ka’a hivyo n’livyokwambia Bishkuku…” Tunisizye Mwakabaga, au ‘Tunis’, kama warembo wenzake walivyozoea na kupenda kumwita, alimjibu huku akibadili mkao pale kwenye kochi, na akimtazama kwa macho ya pozi.

“Khah! Eti Si nd’o ka’a hivyo n’livyokwambia Bishkuku…’” Bishkuku alimwigiza yule binti huku akibana pua yake kwa vidole vyake, na kuifanya sauti yake itoke kwa wembamba uliozidihuku akimtikisia kichwa yule binti, kisha akaacha kuibana ile pua na kuendelea kwa sauti yake ya kawaida, “…hivi we’ unataka kunifanya mi’ majinuni eenh?”

“Sio hivyo bwana…”

“Nani bwana’ako hapa? Yaani mi’ nikutoe kusikojulikana mpaka nikufikishe hapo ulipo halafu unakuja kuniambia eti,” akabana tena pua yake na kuigiza sauti nyembamba na ya deko ya yule binti, “…nimepata mdhamini mwingine!’” Akaacha kuibana ile pua yake na kuendelea kwa sauti yake ya kawaida, “…mdhamini mwingine?” (akasonya)

“Ye’ huyo mdhamini mwingine alikuwa wapi wakati mi’ nakutoa huko machokoani na kukupa mafunzo na kukugharamia mpaka leo unaonekana mrembo miongoni mwa warembo hapa mjini, eenh?”

Tunis alibetua midomo yake kwa kiburi na kugeukia pembeni.

“Mi’ hukunitoa machokoani bwana!”

“Mi’ s’o bwana’ako wewe…umes’kia hiyo?Alla!”

“Sasa kwani ni nini lakini anti Bishi jamani?!” Tunis alilalama huku akimtazama kwa macho ya huzuni yule mwanamama aliyekuwa mbele yake mle ndani.

Bishkuku alimtazama kwa muda yule msichana ambaye sasa alikuwa akimwona kuwa ni mjinga kuliko alivyotarajia na msaliti kuliko Yuda.

“Ina maana huelewi ni nini kinachotokea hapa Tunis?” Alimuuliza kwa sauti iliyojaa utulivu wa kulazimisha, kwani hakika utulivu ulikuwa ni mgumu sana kwake muda ule.

Tunis alimtazama, kisha akamjibu huku akiinamisha chini uso wake.

“Wewe hunimiliki mimi kama huyo paka wako wa ndani bwana…mi’ n’na uhuru wa kufanya maamuzi ninayoona kuwa ni ya msingi kwa maisha yangu, anti Bishi!”

Na hata wakati akisema maneno yale, paka mnene wa Bishkuku, mwenye mkia wenye manyoya mengi ya kupendeza,alipiga mwayo na kuunguruma kidogo kutokea kwenye kochi lingine pale sebuleni. Kana kwamba alikuwa akimlaumu yule binti kwa aidha, kumtaja kwenye mjadala wao usiomhusu, au kwa kumtolea majibu ya jeuri yule bosi wake amdekezaye.

“Maamuzi unayoona Tunis? Au maamuzi unayoshawishiwa kuyaona na huyo ‘mdhamini’ uliyempata?” Bishkuku alimuuliza kwa jazba, na hapo hapo, kabla Tunis hajajibu, aliunganisha kwa swali lingine, “na huyo mdhamini mwenyewe ni nani khaswa, enh?”

I doesn’t matter Bishi…mi’ nimeshafanya maamuzi na nimeshakubaliana naye. Hapa nimekuja kukupa taarifa tu.”

Bishkuku alitikisa kichwa kwa kuchanganyikiwa.

“Na unadhani kuwa huyo…huyo…mdhamini uliyempata…atakuwezesha kutwaa taji la u-miss hapa nchini!”

Halikuwa swali, bali ilikuwa ni kauli iliyodhihirisha wazi kuwa yule binti alikuwa akijidanganya.

“Sio wa hapa nchini tu Bishi…hata u-miss wa dunia! Huyu mtu ana pesa na uwezo wa kutosha…inatakiwa nawe ufurahie maendeleo yangu anti          Bishi, lakini kama hutaki kuniunga mkono sawa tu. Mi’ nimeshakubaliana naye na hapa nimekuja kukuaga rasmi…”

“Lakini sio haki namna hii binti! Sio baada ya muda, nguvu na gharama nilizopoteza kwako Tunis…na definitely sio wakati huu ambapo mashindano ya Miss Tanzania tuliyokuwa tukijiandaa nayo siku zote hizo, yako miezi mitano tu mbele!” Bishkuku alisema kwa fadhaa kubwa, huku akimsogelea yule binti na kumshika mabega, akimtazama usoni kwa macho ya kuomboleza.

“Gharama zako atakurejeshea…” Tunis alisema huku akijichomoa kutoka mikononi mwa yule mwanamama.Alianza kupekua mkoba wake aliokuwa ameupakata juu ya mapaja yake ya mviringo.

“Khah!” Bishkuku alimaka, “Sasa atawezaje kunirejeshea gharama zangu? Vipi na muda niliopoteza? Vipi na ujuzi wangu niliokupatia… mafunzo niliyokupa? Navyo atarejesha? Kivipi khaswa, hebu nijuze tafadhali kisura wangu!”

Tunis alitoa hawala ya fedha kutoka kwenye ulemkoba wake na kumkabidhi.

“Ameniagiza nikuletee hii cheki kufidia gharama zako zote…” Alimwambia huku akimtazama.

Jicho alilokutana nalo lilimfanya ainamishe macho yake pasina kupenda, huku bado akiwa amemnyooshea ule mkono uliokamata ile hawala ya fedha.

Bishkuku alishusha macho yake na kuitazama ile hawala ya fedha iliyokuwa mkononi kwa yule binti, lakini hakufanya bidii yoyote kuipokea. Alimtazama yule msichana kwa dharau kubwa huku akiwa amebetua midomo.

“Milioni mbili!” Alisema kwa kutoamini, “ yaani nawe unaamini kabisa kuwa thamani yako ni milioni mbili? Unajiuza sasa Tunisizye, eenh? Huyo mdhamini wako sijui, mfadhili wako…anakununua kutoka kwangu kwa milioni mbili?” Alimuuliza kwa uchungu na dharau.

“Anti Bishi!” Tunis alimaka, “yaani unaniambia mi’ najiuza kweli?” Alimuuliza kwa sauti iliyoonesha kuumia.

“Bado nina jingine la kukwambia mrembo…” Bishkuku alimjibu kwa hasira, “…hutafika mbali katika fani hii mwanangu. Sio kwa mfumo huu uliouanzisha…na utakuja kunikumbuka sana baadaye!”

Tunis alimtazama kwa huzuni.Alitaka kusema kitu, akakosa la kusema. Akabaki akimkodolea macho ya aibu huku machozi yakimlenga, na ile hawala ya fedha bado ikiwa mkononi mwake.

“Sasa toka nyumbani kwangu bi mdogo,” Bishkuku alimwambia huku akimtazama kwa macho makavu, “toka…! Ondoka na nisikuone tena ndani ya nyumba yangu, mwana mjaa laana usiye na hata chembe ya shukurani we!”

“Anti Bishi…”

“Tena ondoka na hicho kijicheki chako, sina shida na vijisenti vyenu. Kamwambie huyo mrubuni wako kuwa amefanya kosa kubwa sana kuniingilia kwenye anga zangu!”

“Ah, jamani anti Bishi! Sasa—”

“TOKAAAA!” Bishkuku alifoka kwa sauti huku akiwa amemtumbulia macho ya ghadhabu.

Tunis na yule paka mnene wa Bishkuku waliruka kwa pamoja kutoka kwenye makochi waliyokuwa wamekalia, paka akitoa mlio wa woga na kukimbilia jikoni, ilhali Tunis akibweka kama mbwa aliyeshtushwa ghafla wakati akijisaidia. Alitoka mbio hadi mlangoni, ambako alisimama kibwege akiwa ameshikilia mkoba wake kwa mkono mmoja, na ile hawala ya fedha kwa mkono mwingine. Alibaki akimtazama yule mkufunzi na mfadhili wake mkubwa kwa macho yaliyojaa woga na kutatizika kukubwa kabisa, midomo ikimcheza.

“Hebu n’tokee mimi hapa wewe!” Bishkuku alimfokea tena huku macho yakiwa yamemuiva,huku akipiga hatua kumfuata pale alipokuwa amesimama.

Yowe lingine la woga lilimchomoka Tunis huku akigeuka na kutoka mbio nje ya sebule na nyumba ile, akiitupa chini ile hawala ya fedha.

Dakika tano baadaye, Bishkuku alimwona yule binti mrefu akitoka kwa mwendo wa haraka nje ya jengo lile alilokuwa akiishi, na kwenda moja kwa moja hadi kwenye gari moja la kifahari lililokuwa limeegeshwa upande wa pili wa barabara mbele ya jengo lile.

Nje ya gari lile alikuwa amesimama mwanadada mmoja mwenye asili ya ushombeshombe aliyekuwa amevaa mavazi ya kileo.

Kutokea dirishani kwake kule ghorofani, Bishkuku alimwona yule mwanadada akimkumbatia Tunis na kumhoji kitu fulani, kisha akainua uso wake kutazama kule juu ambako dirisha la Bishkuku lilikuwepo.

Ah! Kumbe ni huyu…? Huyu ndiye mdhamini mpya wa Tunis!

Bishkuku alimfahamu fika yule mwanadada aliyekuwa na Tunis kule chini, na alikubali kuwa kama yeye ndiye huyo mdhamini wake mpya, basi hakika alikuwa ana fedha ya kutosha.

Lakini u-miss haupatikani kwa fedha, Tunis!

Kule chini, yule mwanadada shombeshombe aligeuka na kumfungulia mlango wa gari Tunis ambaye aliingia, kisha naye akazunguka na kuingia upande wa dereva.

Lile gari likaondoka eneo lile.

Bishkuku alibaki akikodoa macho kutazama kule chini, huku akitiririkwa na machozi ya fadhaa.

 

***

Alibaki akiwa amesimama pale nyuma ya dirisha lake kwa dakika zipatazo kumi zaidi, sasa akili yake haikuwa ikimzunguka tena, bali ilikuwa imeganda. Haikumpa mwongozo wowote juu ya hatua gani ifuate baada ya usaliti ule wa Tunis. Hatimaye alijizindua na kupangusa machozi yaliyokuwa yakimbubujika bila hata ya yeye kujitambua.

“Mtoto mjinga sana yule!” Alijisemea peke yake, kisha akasonya huku akirudi na kuketi kwenye moja ya makochi ya pale sebuleni.

“Yaani baada ya maandalizi yote niliyofanya kwake! Na mafunzo niliyompa…! Anathubutu kweli kunitosa namna hii mimi? Tena katika dakika za mwishomwisho kiasi hiki?” Alizidi kujisemea peke yake, safari hii ikiwa ni kwa hasira zaidi kuliko fadhaa.

Mara paka wake mnene alirudi pale sebuleni na kumrukia mapajani huku akitoa sauti za deko.

“Haya nini tena na wewe? Unataka kunitosa pia? Eenh?” Alimsemesha yule paka wake huku akimpapasa kichwani.

Paka alitoa milio ya kuliwazwa na mipapaso ya mmiliki wake huku akifumba macho.

“Yaa, hata mimi najua kuwa huwezi kunitosa rafiki yangu…” Alimjibisha yule paka huku akili yake ikiwa mbali kimawazo, na akiendelea kumpapasa kichwani paka wake mtiifu.

Lazima nitafute ufumbuzi juu ya swala hili…lazima niingize binti kwenye mashindano ya Miss Tanzania mwaka huu…lazima! Hii ni nadhiri yangu…na ni lazima niitimize! Tunis alikuwa tegemeo kubwa sana kwangu lakini sasa…Dah!

Mara alipata wazo.

Aliinuka kutoka pale kochini, akimsahau paka aliyekuwa amejikunyata mapajani mwake, na hivyo kumwangusha huku paka naye akitoa mlio wa kulalamikia kitendo kile.

Alichukua simu yake na kuanza kupiga namba ya mtu ambaye alijua angeweza kumsaidia katika tatizo lile.

Simu ya huyo mtu ilikuwa haipatikani.

“Aaaargh, Sheeeeyiiit! Mambo gani tena haya sasa…? Ah!” Alibwata kwa kuchanganyikiwa huku akiruka juu na kutupa mikono yake hewani.

Paka aliachia mlio wa woga huku akitimua mbio na kupotelea jikoni.

“Na we’ acha woga wa kijinga bwana, ebbo!” Alimfokea yule paka wake ambaye tayari alikuwa ameshapotelea chini ya uvungu wa moja ya makabati yaliyokuwa kule jikoni.

Bishkuku alijibweteka tena kochini kwa hasira.

Kokos Wandiba

Wakati Bishkuku akibishana na Tunis, Mwalimu Kokos Wandiba, p.a.k.(pia akijulikana kama) ‘Ticha’, tayari alishakuwa katika ari mbaya sana kwa siku ile. Kisirani kilikuwa kimemjaa, na matusi yalikuwa yamemfura kichwani.

Akiwa ni mwanasheria kijana wa kujitegemea aliyenyang’anywa kibali cha kufanya kazi ile ya uwakili mahala popote nchini na baraza la sheria la taifa, wakili Kokos alijikuta akirejea katika fani ile ya ualimu, ambayo pia aliisomea na kuifanya kabla ya kuingia kwenye uanasheria, kama njia tu ya kujipatia pesa za kujikimu.

Sasa kitendo cha mkuu wa shule ile binafsi alipokuwa akifundisha masomo ya kiingereza na historia kumtaka atoe maelezo ya kina juu ya mambo yaliyo nje ya uwezo wake, kilimkera sana.

Eti ajieleze ni kwa nini wanafunzi wengi wamefeli kwenye masomo yake katika mtihani wa taifa wa majaribio, au mock, kidato cha pili! Tena atoe maelezo yale kwa maandishi na ayawasilishe kwa mkuu yule wa shule kabla ya muda wa kwenda nyumbani siku ile ile!

Ebbo!

“Hivi huyu anadhani mi’ ni mwalimu wa kubabaisha eenh? Mitoto yenyewe mitundu kama nini! Haielewi na wala haitaki kueleweshwa…kazi kutongozana tu darasani bloody fools! Halafu eti mi’ nitoe maelezo kwa nini wamefeli!” Kokos alijisemea huku akiwa amejikunja mezani kwake kwenye ofisi ya walimu akiandika ‘maelezo’ aliyotakiwa kuyawasilisha kwa yule mkuu wa shule mjinga.

Akilini mwake alikumbuka majibizano yaliyopita baina yake na yule mkuu wa shule majinuni.

“Hivi unaelewa lakini kama mimi nimekaa na wanafunzi hawa kwa miezi minne tu kabla hawajafanya mtihani wa taifa?” Alimuuliza yule mkuu wa shule, ambaye alikuwa ni mama mmoja mnene sana na mwenye kipaji cha kuvaa nguo zisizompendeza siku zote.

Yule mama alimbetulia midomo.

“Kwa hiyo…?”

Kokos alimtazama kwa mshangao, kisha akaamua kumkumbusha zaidi.

“Pia si unakumbuka kuwa kabla ya mimi kuanza kuwafundisha hawa watoto, tayari walikuwa wameshakaa bila mwalimu wa historia wala kiingereza kwa miezi mingine mitatu?”

“Hivyo vyote ni visingizio tu vya kuziba utendaji wako mbovu na uwezo wako duni mwalimu!”

“Uwezo duni…? Uwezo wangu duni mimi?”

“We’ ulijua kabisa kuwa watoto wale hawakuwa na walimu wa masomo hayo kwa muda mrefu, na bado ulikubali kuwafundisha na kutuchaji mshahara mkubwa…”

“Anha! Kwa hiyo tatizo hapa ni mshahara mnaonilipa, sio?”

“…sasa leo umetufelishia watoto! Nataka maelezo ya kina, tena nataka maelezo haraka sana…by close of business today, mwalimu, ama sivyo…” Mkuu wa shule alifoka kwa hasira, na Kokos akamjia juu.

“Ama sivyo nini mama, eenh? Ama sivyo nini?” Alimuuliza huku akimtolea macho.

“Maelezo by close of business today mwalimu! Huu mjadala umekwisha!” Mkuu wa shule alimkatisha kwa ukali.

Kokos alitoka mle ofisini kwa mkuu wa shule akiwa amefura kwa hasira.

“Mwalimu…”

Alishtushwa kutoka kwenye kumbukumbu ile na kuinua uso wake kumtazama yule mwanafunzi aliyemsimamia mbele yake pale ofisini.

“Nini?” Alimuuliza kwa kisirani, kalamu yake ikielea juu ya ile karatasi aliyokuwa akiiandika hapo awali.

“Mu…muda wa kipindi umefika mwalimu…” Mwanafunzi alimwambia huku akimtazama kwa woga.

Kokos alimkodolea macho yule mwanafunzi.

“Kipindi gani?”

“Historia mwalimu…”

“Kwa hiyo…?”

“Ah, nimekuja kukukumbusha tu mwalimu…dakika kumi zimeshapita!”

Kokos alimtazama yule mwanafunzi kana kwamba alikuwa mwehu, kisha akazungusha macho yake na kuona kuwa walimu wengine waliokuwamo mle ofisini nao walikuwa wakifuatilia mjadala ule.

“Sasa wewe ndio umekuja kunikumbushaukiwa kama nani?” Alimgeukia yule mwanafunzi na kumuuliza kwa utulivu, akiweka kalamu yake juu ya ile karatasi iliyokuwa mbele yake, huku akijiegemeza vizuri kitini na kufumbata mikono kifuani kwake.

“Amm, mi’ nd’o kaka wa darasa mwalimu…class monitor…”

“Ooow, class monitor…kiranja sio?” Kokos alisema huku akitikisa kichwa taratibu kuonesha kuwa alikuwa ameelewa.Kijana akaafiki kwa kichwa kuwa hakika yeye ni kiranja, na Kokos akaendelea, “…kwa hiyo, umekuja kunikumbusha kutokana na kuujua sana wajibu wako kama class monitor, au kwa kuwa wenzako wamekutuma?”

“Ah, wameniagiza nije kukuita mwalimu…” Kaka wa darasa alijibu. Mwalimu Kokos alitikisa tena kichwa taratibu kuashiria kuzidi kumwelewa yule mwanafunzi. Alibaki akitikisa kichwa namna ile huku akiwa ameinamisha kichwa chake, kisha akainua uso na kumtazama moja kwa moja usoni yule mwanafunzi.Akamweleza kwa ufasaha sana ili kuhakikisha kuwa maneno yake yanaeleweka vizuri sana kwa yule mwanafunzi, na kwa wale walimu wenzake waliokuwa wakifuatilia ule mjadala pale ofisini.

“Sasa nakwambia hivi…” Alianza, “…wewe mwenyewe kwanza (akamtukania mama yake)…” Jicho lilimtoka pima yule mwanafunzi, na walimu wenzake wakaachia miguno ya mshangao na kutoamini mle ofisini.

Kokos akaendelea kwa utulivu na kwa ufasaha ule ule, “…na hao wanafunzi wenzako waliokutuma nao pia (akawatukania mama zao)… na huyo mkuu wenu wa shule naye pia (akamtukania mama yake)! Sasa TOKA MBELE YA USO WANGU NYAU WEE!!!”

Mwanafunzi alitoka mbio mle ofisini, akiparamia meza mbili, kabla ya kuufikia mlango na kutoweka.

Kokos aliwageukia walimu wenzake mle ofisini waliobaki wakimkodolea macho ya kutoamini, ilhali wengine wakiwa vinywa wazi.

What?” Aliwauliza huku akiwatazama mmoja baada ya mwingine, “Na nyi’ mnataka niwape zenu?” Aliwauliza.

Walimu wote pale ofisini wakainamia meza zao, kila mmoja akiwa bize ghafla kuandika anayoyajua mwenyewe.

“Good!” Kokos alisema, kisha akamalizia kuisaini ile karatasi aliyokuwa akiiandika kabla ya ujio wa yule mwanafunzi.

Alikusanya vitu vyake vichache na kutoka nje ya ofisi ile, akiiacha ile barua yake ya kuacha kazi ndani ya saa ishirini na nne pale mezani, ikiwa imekandamizwa na mashine nzito ya kutobolea karatasi.

 

***

 

Siku ile ile, maeneo ya Manzese ndani ya Jiji la Dar es Salaam, binti mmoja alikuwa katika wakati mgumu sana maishani mwake. Sio kwamba ile ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kujikuta katika wakati mgumu, la hasha!Alishakuwa kwenye nyakati ngumu mara kadhaa kabla ya hapo, ila hili lililokuwa likimkabili safari hii lilikuwa la aina yake.

Ugumu wa jambo lililokuwa likimkabili wakati ule, ulimfanya awe amejiinamia akiwa ameketi juu ya kitanda kidogo na kichafu, huku akili ikimzunguka.

“Sasa ndio itakuwaje…ndio au hapana?” Binti mwingine aliyekuwa pamoja naye mle ndani ya chumba kile kidogo cha kupanga, alimuuliza kwa nongwa. Huyu alikuwa amesimama mbele yake huku ameegemea ukuta wa kile chumba, mikono yake akiwa ameifumbata kifuani, na mwilini akiwa hana nguo hata moja.

“Mi’ siwezi bwana!” Binti alimjibu yule mwenzake huku bado akiwa amejiinamia.Kwa jibu lile, yule binti mwingine alipiga makofi mara moja kwa viganja vya mikono yake na kuhamishia uzito wa mwili wake kutoka mguu mmoja kwenda mwingine, akajishika kiuno.

“Sasa hapo ndipo utakapokuwa kwenye tatizo kubwa sana shoga, kwa sababu itakubidi uweze tu ndugu yangu…vinginevyo utafute pa kwenda.Upo?”

“Lakini mi’ sijawahi kufanya mambo hayo Jackie…sipendi  kwanza!” Binti wa kwanza alizidi kupinga.

Cheko la bezo lilimtoka yule binti aliyeitwa Jackie, ambaye alikuwa mwembamba, mrefu, na mwenye sura iliyoonesha ukomavu wa kimaisha kuliko umri wake halisi.

“Kwa taarifa yako hakuna anayefanya mambo haya kwa kupenda bibi, upo? Ni ugumu wa maisha tu mdogo wangu. Sasa kama mi’ najiuza na naweza kumudu maisha yangu na kukuhifadhi na wewe kwa siku mbili tatu hizi, kwa nini na wewe usiingie sokoni ukaanza kujikimu mwenyewe?”

“Da’ Jackie!”

“Da Jackie nini bwana? Kwanza we’ una sura nzuri sana. Shepu yako bomba kweli kweli… mwonekano wako ni baab kubwa! Kwa nini uendelee kuninyonya kama kupe wakati una kila rasilimali ya kukuweka matawi ya juu hapa mjini, eenh?” Yule binti asiye nguo alimwambia mwenzake.

“Najua kuwa maisha ni magumu dada, lakini mi’ siwezi…” Binti alizidi kujitetea.

“Candy sikiliza eenh! Tena sikiliza vizuri bibi wewe!”

Yule binti aliyeitwa Candy aliinua uso kumtazama mwenzake kwa simanzi.

“Mi’ n’shaweka mambo hadharani, upo?” Aliambiwa, “Aidha uchukue kilicho chako utafute uelekeo, au leo jioni tutoke sote kuelekea viwanja. Uamuzi ni wako. Sasa hebu nipishe mi’ nilale huko!” Jackie alimalizia huku akijilaza pale kitandani na kumsukuma yule binti asiyejua mambo kwa mguu wake.

Kwa unyonge yule binti aliyeitwa Candy alijisogeza pembeni kumpa nafasi, kisha akaendelea kukaa kwenye pembe ya kitanda kile ilhali bado amejiinamia.Muda si muda, alimsikia Jackie, ambaye ndiyo alikuwa amerudi asubuhi ile kutoka ‘viwanja’ alipokesha usiku kucha, akikoroma kwa usingizi mzito. Alimtazama yule mwanadada aliyelala akiwa uchi wa mnyama kwa muda mrefu, na mwili ukamsisimka alipojifikiria na yeye kuwa katika hali kama ile.

Alianza kulia…

 

***

 

Kokos Wandiba alikuwa ameshalewa kiasi cha kutosha, na kadiri alivyozidi kumfikiria yule mama mwenye sura iliyokosa mvuto aliyepachikwa cheo cha mkuu wa shule, ndivyo alivyozidi kubugia kinywaji.

Hali ile haikusaidiwa kabisa na kitendo cha akili yake kuendelea kumrudisha katika wakati alipokuwa akiitumikia fani yake ya uanasheria na jinsi ambavyo aliweza kuwaweka watu kama lile jimama linene livaalo nguo zisizompendeza, mahala panapowastahili.

Na kadiri alivyoikumbuka enzi hiyo iliyozimika ghafla mwaka mmoja uliopita, ndivyo alivyozidi kujisokomeza kilevi.

Baada ya kutoka pale shuleni mchana ule, kituo kilichofuata kilikuwa ni kwenye ile baa aliyoizoea na kuanza kukata ulabu huku akiutafakari mporomoko wa mfumo mzima wa maisha yake.

Mara simu yake ilianza kuita, na alipobaini kuwa ilikuwa ni namba ya yule mkuu wa ile shule aliyokwisha ifuta kutoka kwenye sehemu ya maisha yake, aliizima ile simu na kurudia kushambulia kilevi kwa ari, kasi na nguvu mpya. Kutokea hapo alipoteza kabisa kumbukumbu ya muda, na pale alipokumbuka kutazama saa yake tayari ilikuwa imetimia saa moja usiku.

“Unajua nini faza…?” Alimwambia kilevi yule muuza vinywaji pale kaunta.

“Sijui nini Ticha…hebu nijulishe nini basi!” Yule muuza vinywaji, ambaye alimfahamu vizuri, alimjibu kwa masihara huku akimcheka jinsi alivyolewa.

Wweeery good! Basi subiri nikujulishe…”  Kokos alimwambia kilevi huku akicheka kibwege, “…ni kwamba sasa nahitaji kujipatia kimwana kimoja matata sana, unasikia bwana? Na hapo siku yangu itakuwa imekamilika kaabbb-bisa!” Kokos alisema kilevi huku akipigapiga uso wa ile kaunta kwa kiganja cha mkono wake.

Yule jamaa wa kaunta alimcheka.

 “Haya na ukishampata huyo kimwana mmoja matata sana unamfanya nini, Ticha?”

Sasa ilikuwa zamu ya Kokos kumcheka.

“Unauliza majawabu eenh…? Unataka kuniigilizia, eenh?” Alimwambia huku akiweka pesa juu ya ile kaunta na kuanza kuondoka huku akiyumbayumba kidogo.

“Oyaa, subiri chenji yako basi!” Jamaa wa kaunta alimpigia kelele.

Keep the change, kimwana!”

Nje ya ile baa aliingia kwenye gari lake aina ya Suzuki Escudo, likiwa ni matunda ya kile kipindi alichokuwa akiitumikia ile fani yake ya uanasheria kama wakili wa kujitegemea. Alipiga stata huku mbwewe za kilevi zikimtoka.

Sifa moja ya Kokos Wandiba ni kwamba huwa halewi kiasi cha kushindwa kuendesha gari, au kiasi cha kupotea nyumbani kwake, hivyo aliliingiza barabarani lile gari na kushika uelekeo wa nyumbani kwake Mbezi Beach, akichukua njia ya Kinondoni makaburini kutokea pale kwenye ile baa iliyokuwa katikati ya jiji.

 

***

 

Jackie alimtazama Candy kwa jicho la kuchuja lilichokuwa likikiona, kabla ya kutikisa kichwa kuafiki kile alichokiona.

“Hapo uko bomba mwanangu…yaani si mchezo!” Alimwambia huku akimpandisha juu kijisketi kifupi cha jeans alichokuwa amemvika, ambacho Candy alikuwa akikivuta chini kila dakika.

Walikuwa ‘viwanja’, na Candy alikuwa amevaa nywele za bandia kichwani kwake na uso wake ulikuwa umekolea poda na nakshi za kilimbwende, midomo yake ikiwa imekolezwa rangi nyekundu, ilhali machoni alikuwa amepakwa wanja kwa mtindo wa Kimisri.

Hakika alionekana mrembo maradufu, na moyo wake ulikuwa ukimpiga kuliko ulivyowahi kumpiga maishani mwake.

“Acha kushusha hiyo sketi sasa bwana, we’ vipi? Lazima uoneshe mapaja yakohayo ili uvutie wateja!” Jackie alimkemea.

“Ah, lakini mi’ sitaweza mambo haya Jackie…sijawahi!” Candy alilalama huku akiivuta tena chini ile sketi.

“Tulishamaliza mjadala huo Candy…na kumbuka…ukiwa viwanja wewe sio Candy tena. Wewe ni Judy, okay? Na…lazima uhakikishe kuwa kondomu inatumika, si unazo kwenye pochi yako humo?”

“Ndiyo. Lakini…”

Good, hakuna cha lakini tena hapo. Kondomu ni muhimu, bado hujafikia kiwango cha kwenda kavu kavu wewe! Na kama n’livyokwambia…nitajitahidi twende pamoja kwenye kazi yako ya kwanza, lakini kama mteja akikataa itabidi tuachane, kila mmoja awe kivyake…tutakutana maskani.” Jackie alimwambia kwa msisitizo, na muda huo gari moja lilisimama kando ya barabara na kupiga honi.

Haraka Jackie alimshika Candy mkono na kumvuta huku akilikimbilia lile gari, wakiwashinda akina dada poa wengine wawili waliokuwa wakijaribu kuliwahi. Aliinama kishawishi, akiegesha viwiko vya mikono yake kwenye ukingo wa dirisha la lile gari na kumchungulia dereva.

Hello lover boy, unataka raha?” Alimuuliza yule dereva kwa sauti ya kuchombeza huku bado akiwa amemkamata Candy kwa mkono wake mmoja.

Candy alikuwa akimtupia jicho la woga yule dereva huku akigeuka huku na huko, moyo ukimwenda mbio.

Kokos Wandiba alimtazama Jackie na hakuvutiwa na alichokiona.

“Raha naitaka, tena usiku kucha…lakini sio na wewe. Hebu msogeze huyo mwenzako naye nimwone vizuri!” Alimjibu kilevi, akimtupia Jackieharufu ya pombe kutoka kinywani mwake.

Jackie alifinya uso na kupunga kiganja chake mbele ya pua yake.

“Ai! Mtu mwenyewe umelewa hivyo? Basi tutakuja sote wawili…mi’ na mwenzangu na tutakupa raha mpaka uchanganyikiwe…ushawahi kupewa mapigo ya chuma mboga we? Basi twende tukakupe mambo lover boy! Elfu thelathini tu mpaka majogoo, unasemaje?”

“Toka ‘uko! Elfu thelathini unaniuzia nini? Mi’ sitaki wawili! Hebu msogeze huyo mwenzio kwanza naye nimwone…” Kokos alimwambia kihuni.

Jackie alimvuta Candy pale dirishani.

“Judy hebu msalimie mteja wetu basi, ana hamu ya kukusalimu huyo…! Na anataraji raha usiku kucha…”

“Shhk…Sh’kamoo!” Candy aliamkia kwa woga.

Jackie alimfinya kwa nguvu kwenye makalio. “Aaah, sasa shikamoo ndio salamu gani tena maeneo haya na wewe?” Alimnong’oneza kwa hasira.

Kokos aliinamia upande wa lile dirisha ili amwone vizuri zaidi yule dada poa wa pili.

“Ewaaa! Wewe ndiye haswa ninayekutaka! Ingia twende mtoto…!” Alisema huku akimfungulia mlango.

Uso ulimsawajika Candy na akamgeukia Jackie kwa woga, akimtazama kwa macho ya kuomboleza. Haraka Jackie alimvutia pembeni kabla hajasema neno lolote la kuharibu biashara.

“Sikiliza wewe! Huyu jamaa kalewa, kwa hiyo hatokupa tabu…mwepesi sana huyu, na bila shaka hataweza kufanya lolote. We’ mchezee-chezee tu kama nilivyokuonesha kule nyumbani, mpaka alale. Cha msingi ukifika tu dai pesa yako kabisa, asubuhi unaondoka tu…nimemwambia elfu thelathini kajitia kugoma, lakini we komaa humo humo…n’tajaribu kuingia nawe kwenye gari, ila akizidi kugoma basi ujue habari ndiyo hiyo!”

Kokos alipiga honi.

“Vipi tena nyie…mnaringa?”

Jackie alimvuta Candy mpaka pale kwenye gari.

Don’t worry honey, tuko tayari…” Alimwambia mteja wao huku akimsukumia Candy ndani ya lile gari naye akianza kufungua mlango wa nyuma.

“We’ unaenda wapi? Nimesema sitaki wawili bwana…huyu mwenzako anatosha sana!” Kokos alimkemea.

Jackie aliteremka na kuubamiza mlango kwa hasira.

Candy alimgeukia Kokos.

“Twe…twende naye tu, kaka…” Alimwambia kwa sauti ya kuomboleza.

Kokos aliliondoa lile gari taratibu kutoka eneo lile.

“Hakuna haja ya kuja wawili mrembo wangu…we’ mbona watosha sana tu, my pretty, eenh? Unataka kunichanganyia biriyani na ugali saa hizi?” Alimjibu kilevi huku akitabasamu.

Candy alihisi mwili ukimyong’onyea na meno yakigongana kinywani mwake.

“Unaitwa nani wewe…mbona unaonekana mwoga mwoga sana, vipi?” Kokos alimuuliza huku akimpapasa paja lake kwa mkono wake wa kushoto.

“Judy…naitwa Judy.” Candy alijibu, machozi yakimlengalenga, moyo ukimbamiza vibaya sana ndani ya kifua chake huku akijilazimisha kutokwepesha mapaja yake.

Eeh Mungu wangu, balaa gani hili unaloniletea sasa lakini…? Sifanyi kwa kupenda Mungu wangu, ila sioni namna nyingine kwa sasa…nisamehe mola wangu…nisamehe!

Safari ya kwenda kusikojulikana ilikuwa imeanza, na kadiri walivyozidi kukata mitaa, ndivyo Candy alivyozidi kukaribia kwenye tukio lililokuja kubadili kabisa maisha yake.

 

***

 

Vishindo vya mlango wake wa mbele ukigongwa kwa pupa na vurugu vilimshitua Kokos Wandiba kutoka kwenye usingizi mzito uliokolezwa na kilevi. Alijigeuza pale kitandani huku akisonya na kuzamisha kichwa chake chini ya mto aliokuwa amelalia. Akazidi kujikunja pale kitandani huku akifinya macho yake ili ule usingizi wake mzito usikatishwe na vishindo vile.

Lakini wapi!Vishindo vilizidi.

“Aaaaah! Nani tena huyu saa hizi jamani!!” Alimaka peke yake na kuinuka kutoka pale kitandani huku akifikicha macho.

Aliitupia macho saa ya mezani iliyokuwa juu ya mtoto wa meza aliyekuwa kando ya kitanda, na kuona kuwa muda ulikuwa ni saa kumi na mbili kasorobo asubuhi.

“Ama! Hii nini sasa! Huu ni muda wa kugongea watu majumbani mwao kweli?” Kokos alilaani huku akitembea kwa kupepesuka kuelekea nje ya chumba chake cha kulala, akipita kwenye sebule yake ghali iliyoenea kila kitakiwacho kwenye sebule. Aliufikia mlango wa mbele wa nyumba yake akiwa na bukta tu, akilini akijiuliza ni vipi mlinzi wake huko nje ameweza kuruhusu hali ile itokee.

Nje ya mlango ule, mgongaji alikuwa akizidi kugonga.

“Nani wewe lakini?” Kokos aliuliza kwa ukali.

“Hebu fungua mlango huo wewe!” Sauti ambayo aliitambua mara moja ilimkemea kutokea kule nje.

Kokos alizungusha juu mboni za macho yake na kutupa mikono yake hewani kwa kukata tamaa. Alifungua mlango na kubaki akimkodolea macho yule mgongaji, ambaye bila ya salamu alipita moja kwa moja ndani ya nyumba ile na kwenda kuketi kwenye moja ya makochi mazuri sana yaliyoipamba ile sebule ghali.

Kokos alibaki akiwa ameshikilia mlango huku akimtazama kwa mshangao, yule mgeni aliyeingia mle ndani.

“Hivi unajua ni saa ngapi saa hizi lakini Bishkuku?” Hatimaye alimuuliza kwa hisia kali huku bado akiwa ameshikilia mlango wake.

“Hebu nijie hapa mimi, sio unasimama tu hapo mlangoni kama askari kea! Hutaki kujua nimepatwa na nini hata nikaja kwenye hili kasri lako la kifakhari lukwili namna hii? We’ unachojua ni kuniuliza saa hizi ni saa ngapi?” Bishkuku alimjibu kwa ufedhuli huku akikunja nne pale kwenye kochi.

Kokos alimtazama kwa muda, kisha akatikisa kichwa kwa masikitiko na kuufunga ule mlango. Alirudi pale sebuleni na kukalia mkono wa moja ya makochi yaliyotapakaa eneo lile huku akiachia mwayo mrefu, kisha akabaki akimtazama kwa macho ya kuuliza.

Walibaki wakitazamana kwa muda, lakini Bishkuku alipoona haulizwi kilichompeleka pale muda ule, akaanza kuongea.

“Haya kisa cha kuzima simu jana kutwa nzima ni nini?” Alimuuliza, na kabla Kokos hajajibu, akaendelea,“…halafu ulikuwa umelewa wewe, mtizame kwanza!”

“Ni nini kilichokuleta kwangu saa hizi Bishi?” Kokos alimuuliza huku akibana mwayo mwingine, akipuuzia zile shutuma za Bishkuku. Bishkuku alimtazama kwa muda, kisha uso wake ukabadilika na kuwa makini.

“Tunis kanitosa.” Alisema kwa uchungu.

Kokos alibaki akimtazama kwa mshangao.

What do you mean, Tunis kakutosa…?” Alimuuliza kwa mshangao.

“Namaanisha kanitosa Kokos…kachukuliwa na mtu mwingine!” Bishkuku alisema kwa uchungu.

Kokos alimtazama kwa mshangao mkubwa sana, kana kwamba ni muda ule ndio alikuwa anagundua kitu ambacho siku zote hakuwa amekigundua kwa mwanamama yule aliyekuwa mbele yake, kisha kana kwamba aliyeshukiwa na uwelewa wa kile alichokigundua kwa mara ya kwanza, alimwambia huku macho yake yakionesha kuumia sana.

“Ah! Bishi! Yaani…ah! Yaani unataka kuniambia kuwa wewe na Tunis…mlikuwa mna uhusiano wa ki…mlikuwa mnasagana? Alikuwa mpenzi wako? Na sasa kachukuliwa na mpenzi mwingine, amekutosa? Mungu wangu, nyie wanawake wa siku hizi! Sasa hicho ndicho kilichokuleta huku saa hi—”

“Kokos!” Bishkuku alimaka kwa hasira huku akiinuka kutoka kwenye kochi alilokuwa amekalia, “sio hivyo unavyofikiria wewe, alla! Sina maana hiyo kabisa!”

“Ish!”

“Nina maana kuwa Tunis sasa kaamua kuungana na msimamizi mwingine katika maandalizi yake ya kugombea taji la Miss Tanzania, we vipi? Mi’ msagaji tangu lini? Una wazimu nini?” Bishkuku alimjia juu.

“Dah, afadhali! Sasa we’ umeanza vibaya hayo maelezo yako bwana!”

“Achana na hayo! Jambo langu mi ndiyo hilo! Tunis kanikimbia!”

“Khah! Sasa hiyo itawezekana vipi? We’ si nd’o uliyemfikisha hapo, yule?” Kokos alionesha kushangazwa na hali ile.

“Sa’ si nd’o maana nimechanganyikiwa? Yaani Tunis amenisaliti vibaya sana…”

“Pesa, muda na mafunzo yote yale uliyompa?” Kokos naye aliongea kwa mshangao.

“Sasa unaona ni jinsi gani nilivyohamanika?”

“Mambo haya yametokea lini lakini?” Kokos aliuliza.

“Jana. Na nikawa nakupigia simu hupatikani, nikaja kule kazini kwako nikaambiwa kuwa umeondoka katika mazingira yasiyo mwafaka kabisa…umetukana kuanzia wanafunzi hadi mkuu wa shule!”

Kokos alitabasamu kidogo alipokumbuka jinsi yule mwanafunzi alivyotoka mbio pale ofisini, na jinsi wale walimu wenzake walivyoangusha midomo kwa mshangao.

“Ah, wale nimeshaachana nao…” Alisema, sasa akiwa makini zaidi ya alivyokuwa hapo awali, “sasa…kwa hiyo sasa huyo mrembo wako amekwenda kushirikiana na nani?” Aliuliza.

Bishkuku alibetua midomo na kukunja uso kwa hasira kabla ya kumjibu.

“Sanura Kashogi.” 

Sasa ilikuwa zamu ya Kokos kuacha kinywa wazi.

“Sanura Kashogi!”

“Mnhu!”

“Huyu mwanamitindo mkubwa jijini?” Kokos alimuuliza tena.

“Ndiye haswa!” Bishkuku alijibu tena, na hapo wote wawili walisikia kishindo kizito pale sebuleni.

Waligeuka kwa pamoja kule kilipotokea kile kishindo.

Walibaki vinywa wazi…

Candy Gamasala

Akiwa ndani ya lile jumba la kifahari aliloingizwa usiku uliopita, Candy naye alishitushwa na vile vishindo vilivyomshitua Kokos kutoka kwenye usingizi mzito.

Baada ya kufika ndani ya jumba lile usiku uliopita, alijikuta kwenye wakati mgumu kweli kweli, kwani yule bwana aliyemwopoa hakuwa mchovu kwa ulevi kama jinsi ambavyo Jackie alivyomwambia kuwa angekuwa.

Jamaa alikuwa ana nia kweli kweli ya kutimiziwa haja zake za kimwili usiku ule, na Candy alishindwa kabisa kumdhibiti. Jamaa alianza kumshikashika na kumtomasatomasa huku akijaribu kumbusu na mara akijaribu kumbeba na kumwingiza chumbani kwake.

Candy alijitahidi kumkwepa na kumpumbaza ili angalau achoke kutokana na ulevi ule na hatimaye alale usingizi, lakini wapi!

Jamaa alikuwa ana nguvu na nia ile ile, pamoja na kulewa kwake. Mwishowe, Candy alizidiwa kabisa, na alipoona hali imekuwa ngumu ilibidi aangue kilio huku akimwomba jamaa msamaha, akijieleza kuwa yeye hakuwa amewahi kufanya jambo lile hata siku moja, na kwamba ni shinikizo tu la yule mwenzake ndiyo lililomfikisha pale. Alimwahidi kuwa hatochukua malipo yoyote kutoka kwake ili yule bwana amsamehe na asimshurutishe kufanya kitendo kile.

La haula!

Acha Jamaa aje mbogo!

Alimchachamalia huku akimtukana matusi mazito mazito na kumfukuza kutoka mle ndani. Candy alizidi kulia na kuomboleza. Angeondokaje usiku ule nayeye mgeni jijini? Alimwomba amsitiri tu mpaka asubuhi naye ataondoka na hatotaka malipo yoyote.

“Hebu niletee kinywaji kule kwenye friji upesi, kabla sijakubaka bure hapa saa hizi, ebbo!” Hatimaye jamaa alimfokea kilevi, na Candy alikimbia hadi kwenye jokofu, ambamo alikuta kumesheheni vinywaji vya kila aina.

Alitaka kumuuliza ampelekee kinywaji gani lakini jamaa alimfokea kwa ukali, naye akanyakua chupa moja ya pombe kali na kumpelekea.

Jamaa alimkamata mkono na kumwambia kilevi, “Sasa lazima ufanye kazi hapa sio ukae bure bure tu ndani mwangu, umesikia?”

Candy aliafiki kwa pupa.

“Nenda pale kabatini uchukue gilasi kubwa kuliko zote uje nayo hapa…” Jamaa alimwamuru kilevi, “…halafu utakuwa unanimiminia hii pombe kwenye gilasi nami nakunywa…mpaka nikwambie basi, sawasawa?”

Doh, maneno yale yalikuwa kama wimbo mzuri sana masikioni mwake. Alikimbia haraka na kuleta gilasi kubwa iliyokuwa katika lile kabati zuri na ghali, na kuanza kummiminia kinywaji yule bwana.

Mara moja jamaa alijimwagia kinywaji kwenye suruali na kumkemea kwa hasira, na Candy akanywea kwa woga.

“Ole wako unimwagie tena…nakubaka hapa hapa, shwaini we!” Alimkemea, na Candy akaendelea kummiminia kinywaji kwa umakini mpaka alipoelemewa na kilevi na kuchapa usingizi mzito.

Ndipo alipoanza kuivinjari ile nyumba kutoka chumba mpaka chumba, na akajionea jinsi yule mtu alivyokuwa ameenea kiuwezo.

Hatimaye alirudi pale kwenye kochi alipokuwa amelala yule ‘mteja’ wake na kuanza kumburura kwa taabu hadi kwenye chumba ambacho kufikia muda ule alijua kuwa ndicho kilikuwa chumba chake cha kulala.Akamlaza kwa taabu kitandani.

Akiwa amemlaza chali pale kitandani, Candy alimvua viatu na soksi yule bwana. Kisha akamvua nguo kwa woga na taabu na kumwacha na bukta ya ndani tu.

Akamwacha aendelee kulala naye akaingia chumba kimojawapo mle ndani na kujifungia, akijaribu kutafuta usingizi, akilini akijifikiria itakuwaje pindi kukicha na atakapokutana tena na yule bwana…

 

***

 

Baada ya kushtushwa na vile vishindo vya kugongwa mlango wa nyumba ile, Candy alitoka taratibu nje ya kile chumba alimokuwa amejifungia. Alinyata kuelekea sebuleni ambako alisikia sauti zikitokea, na aliposikia sauti ya kike mara moja moyo ukampaa.

Mama yangu…! Mkewe kafika! Nitasema nini leo mimi masikini ya mungu jamani!

Huku moyo ukimpiga alizidi kusogea kule sebuleni taratibu ili asikie yale yaliyokuwa yakiongewa huko. Hakuziona kandambili zilizokuwa zimevuliwa nje ya mlango ule naye akazivamia kiasi cha kumfanya apepesuke kidogo, akinyoosha mikono yake ili awahi kujishikilia ukutani. Badala yake mikono yake ikauparamia ule mlango, ambao ulifunguka naye akajikuta akipitiliza nao mpaka kule sebuleni kwa mweleka mzito.

Ayyaa! Nimegundulika!

Alijiinua haraka na kubaki akiwa ametumbua macho akiwatazama wale watu wawili waliokuwa pale sebuleni. Kokos Wandiba alimtumbulia macho yule mrembo aliyeibuka ghafla sebuleni kwake. Alifinya na kufinyua macho mara tatu mfululizo, kabla hajagundua kuwa alikuwa ameacha kinywa wazi. Akakifumba haraka.

Hakuwa amepata kumwona hata siku moja yule mrembo aliyesimama mbele ya macho yake, na akili yake ilikuwa ikijaribu kuvuta matukio ya siku iliyopita apate kujua ilikuwaje hata mrembo yule akawa ndani mwake muda ule.

Bishkuku naye alibaki akimkodolea macho ya mastaajabu yule binti aliyesimama kibwege hatua chache kutoka pale mlangoni. Alizitazama zile nguo alizovaa yule binti, na kubaki kwenye kile kijisketi kifupi alichokuwa amekivaa.Akamgeukia Kokos kwa macho ya kuuliza.

“Shhk…sh’kamooni…!” Candy alijikuta akitupa salamu huku akiviringaviringa vidole vya mikono yake kwa woga.

“We…wewe nani…?” Kokos alimuuliza kwa mastaajabu makubwa, na Candy akapigwa na butwaa.

Bishkuku akazidi kumtazama Kokos kwa mshangao.

“Unajifanya humjui? Hujui kafikaje humu ndani huyu wewe?” Alimuuliza kwa hasira, kisha akamgeukia yule binti aliyesimama mbele yao, na Candy akahisi moyo wake ukipiga tikitaka ndani ya kifua chake.

“Nakuuliza wewe binti…” Kokos alizidi kumuuliza Candy kwa ukali, “…umefikaje humu…na unataka nini?”

Na Bishkuku alimjia juu Kokos.

“Toka hapa wewe! Mtu unaona kabisa kuwa huyu ni changudoa uliyemwopoa huko majiani halafu sasa unajitia humjui?”

“Mi’ s’o Changudoa!” Candy alijikuta akimaka kwa ukali.

Bishkuku alimtulizia macho kwa muda, kisha alianza kumsogelea taratibu. Candy alitamani kukimbia, lakini alijikaza na kujipa ujasiri wa kuendelea kusimama palepale huku akimtazama yule mwanamke aliyekuwa akimjongelea huku akimtazama kwa namna ambayo hakuweza kuielewa mara moja.

Kokos alibaki akimkodolea macho yule binti huku akili ikimzunguka. Bado hakuwa na kumbukumbu kabisa ya jinsi yule msichana mrembo alivyoweza kufika ndani mwake.

Bishkuku alimfikia Candy na kumtazama moja kwa moja machoni. Candy naye alijitutumua na kumrejeshea mtazamo huku akiwa amevimbisha midomo tayari kwa makabiliano.

“Sasa kama we’ si changudoa ni nani basi?” Bishkuku alimuuliza huku bado akimtazama kwa makini, nyuso zao zikiwa zimekaribiana sana.

“Mi’ naitwa Candy, na—”

“Na ulifikaje humu ndani? Maana hata mwenye nyumba anakushangaa!” Bishkuku alimkatisha kwa swali lingine, na hapo Kokos naye akaingilia kati.

“Sio bwana! Jina lake…Jina lake ni Judy huyu…au Julia…au Ju-kitu fulani hivi, lakini sio Candy, nimeshakumbuka sasa!” Alibwata, akiilazimisha akili yake kukumbuka zaidi matukio ya usiku uliopita.

Sasa Candy alikuwa amechanganyikiwa, hakujua ajibu hoja ya nani kati ya wale watu wawili.

Bishkuku alimgeukia Kokos.

“Kwa hiyo kumbe ni wewe mwenyewe ndiye uliyemleta humu ndani huyu binti, sio?”

Kokos alimtazama na kujikuna kichwa kizembe.

Yeah…nadhani ni hivyo. Nilikuwa nimelewa sana hata hivyo, na—”

“Na hata hujui kama ulitumia kondomu au la?” Bishkuku alimuuliza kwa ukali na shutuma.

“Aan-aah, nakuhakikishia anti hakuna chochote kilichofanyika baina yetu!” Candy alidakia kwa kiherehere, na Bishkuku akamtulizia macho ya kuuliza.

“Ni kweli dada! Huyu kaka…sijui mumeo, au mpenzi wako…alinileta hapa, lakini nilimwomba tusifanye mambo hayo—” Candy aliendelea kujieleza haraka haraka, lakini kufikia hapo Bishkuku aliangua kicheko kikubwa.

Candy akapigwa butwaa.

“Mume wangu…? Mpenzi wangu…? We’ binti usiwe mjinga!” Bishkuku alimwambia huku akicheka na akirudi kuketi kwenye moja ya makochi pale sebuleni.

“Kwa…kwani sio mumeo?” Candy aliuliza kwa mshangao, akitembeza macho kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine.

“Huyu ni dada’angu,” Kokos alimwambia, “na hana mamlaka ya kuingilia maisha yangu binafsi!”

Akabakia akimtazama dada yake kwa jicho kali. Bishkuku alimrejeshea jicho kali mdogo wake, kisha akamgeukia Candy.

“Kwa hiyo binti sasa unakiri kuwa we’ ni changudoa uliyeopolewa na mdogo wangu jana?”

Candy hakuwa na jibu, akainamisha uso.

“Sawa…nilichukua changudoa. Na sawa… najua kuwa siku zote huwa unanikanya kuhusu suala hilo. Lakini hilo ni suala la maisha yangu, si la kwako. Tuongee kilichokuleta halafu uniache nikamalizie usingizi wangu!” Kokos aliingilia kati.

Candy alitembeza macho kutoka kwa kaka kwenda kwa dada, na kuyarudisha tena kwa kaka.

“Ba…basi mi’ naomba niende tu kakaangu, nashukuru kwa yote…”

“Hapana!”

“Usiondoke!”

Kokos na Bishkuku walisema kwa pamoja.

Candy akashangaa.

“Ni…nisiondoke? Kwa nini…?”

“Wewe na mimi bado tuna mambo ya kuwekana sawa mrembo,” Kokos alimwambia, “…jana nilikuwa nimelewa sana, na huenda nilikosa adabu kwa kiasi fulani, ila leo niko safi kiasi. Naomba usubiri kidogo…tupate chai, kisha utaondoka kama utapenda, okay? Kwa sasa nina maongezi kidogo na dada’angu hapa, akiondoka nitaongea na wewe.”

Candy na Bishkuku walimtazama kwa mshangao, kila mmoja kwa sababu yake. Candy alitaka kusema neno, akaghairi. Aligeuka na kurudi kule chumbani alikokuwa amejifungia usiku uliopita, akilini akijiuliza ni maongezi gani ambayo yule jamaa alitaka kuongea naye.

Mara baada ya Candy kuondoka, Bishkuku alimgeukia Kokos kwa wahka.

“Umeona jinsi binti alivyoumbika yule? Umeona?”

Kokos akamshangaa.

“Una maana gani, mbona sikuelewi? Umekuja kuongelea juu ya Tunis na jinsi alivyokusaliti…haya ya huyu binti kuumbika yanakujaje tena?”

“Ah, yaani huelewi? Ni kwamba tangu Tunis anisaliti nimekuwa nikijisemesha kuwa ni lazima niingize mrembo kwenye Miss Tanzania ya mwaka huu!”

“So?”

“Na nilikuja kwako nikitegemea kupata ushauri juu ya hatua gani za kisheria nimchukulie Tunis na huyo mtu aliyemrubuni—” Bishkuku alimjibu, na hapo hapo Kokos alimkatisha.

“Aa-aa, hapo hapo Bishkuku, hapo hapo!”

Dada yake akamkodolea macho.

“Nilikubali kukuunga mkono kwenye hizo harakati zako tangu ulipoanza na Tunis, na nilikushauri kuwa umsainishe mkataba yule mtoto mbele ya mwanasheria, we’ ukapuuza. Ona alivyokufanya sasa!”

“Ni kweli uliniambia Kokos, na hilo ni moja ya sababu za ujio wangu kwako asubuhi hii… sababu nyingine ikiwa ni kukuomba msaada wa kifedha. Lakini sasa naona kumbe nimeshapata na mrembo wangu mpya hapa hapa.

“Sina tena haja ya kumshtaki Tunis, kwani nitapoteza muda bure… ila nataka kumwonesha kuwa hawezi kunisaliti halafu akapata taji la urembo nchini. Na huyu binti ndiye atakayeniwezesha kutimiza azma hiyo!” Bishkuku alimweleza kwa hamasa kubwa.

Kokos alimshangaa kupita kiasi.

“Khah, Bishi! Hivi we’ unamjua huyu binti kiundani kweli? Unajua katoka wapi?Unajua historia yake…? Mi’ nimemwopoa kwenye uwanja wa machangudoa jana! Hivi unaelewa maana yake hiyo? Hiyo maana yake ni kwamba huwezi kumwingiza mtu wa aina hiyo kwenye mashindano yenye hadhi na heshima kama hayo…!”

“Ila kuingiliana naye kimwili bila kinga ni sawa, sio?”

“Awww come on, Bishi! Hii sio kuhusu mimi na matamanio binafsi ya mwili wangu bwana! Hii ni kuhusu wewe kujiaibisha kwa kuingiza mtu mwenye historia ya uchangudoa, kwenye mashindano makubwa kama hayo Bishi!

“Wewe unatarajia huyu binti atwae taji, na hivyo awe kioo cha jamii wakati yeye mwenyewe ni mchafu… unaona mkanganyiko huo?”

“Sasa kama mchafu mbona ulitaka kulala naye?” Bishkuku alimjia juu.

“Akh, nimeshakwambia kuwa ni mchafu kumuweka kwenye mambo ya u-miss Bishi. Huko alipo ni sawa kumtoa na akaendelea na maisha kwa njia nyingine, lakini sio kwenye u-miss!”

“Kwa nini?”

Crystal clear mbona… ? Kule sio pa kupeleka watu wenye historia chafu chafu Bishi, nawe’unalijua hilo!”

“Mnhu! Laiti ungejua machafu waliyonayo hao waliokuwamo kwenye mashindano hayo wala usingesema hivyo mdogo wangu… hata hivyo, sijui ilikuwaje tu hata huyu binti akaangukia huko ulipomwopoa, ila naamini kuwa anaweza kurekebishwa Kokos!”

Aaaa come on, Bishi… come on!

“Nipe huyu binti nimfunde Kokos!Na nakuhakikishia Tunis atausikia u-miss Tanzania kwenye bomba, na taji la huo u-miss ataishia kuliona kichwani kwa huyo binti aliyemo ndani mwako hivi sasa!”

Ukiandika

Tunahariri

(+225) 715 001 818 | 787 001 819

info@uhariri.com