Mkaanga Sauti
Hussein Tuwa
ILIKUWA ni nafasi nyeti na iliyowapasa kuijaza haraka sana. Kifo cha ghafla cha mtaalamu wao wa takwimu za miradi kilisababisha nafasi ile ibaki wazi.
Kazi ilitangazwa, na kati ya waombaji 35, ni sita tu walionekana kukidhi sifa za kuitwa kwenye usaili.
“Hii ni nafasi adimu sana Mary,” Mkurugenzi mkuu wa shirika alimwambia mkuu wa kitengo cha rasilimali watu , wa shirika, “hivyo ningependa wewe mwenyewe uingie kwenye chumba cha usaili kusimamia mchakato mzima wa kumpata mtaalamu mpya wa takwimu.”
“Sawa, boss… will do.” Mary Komunte, mkuu wa kitengo cha rasilimali watu, alijibu. Kiukweli, alikubali kwa shingo upande tu, kwani yeyote kati ya wasaidizi wake watatu kwenye kile kitengo anachokiongoza angeweza kuusimamia vilivyo usaili ule. Ni kama vile nafsi ilitaka kumnusu na lililokuwa likimsubiri kwenye chumba cha usaili.
Kutokana na nchi kuwa kwenye janga kubwa la UVIKO-19, wafanyakazi wote wa shirika lao walikuwa wakifanyia kazi majumbani mwao, wakitumia mitandao kutimiza majukumu yao. Kuingia kwenye jengo la shirika kuliruhusiwa kwa vibali maalumu na kwa idadi maalumu tu ya watu, pindi kukiwa kuna ulazima wa kufanya hivyo.
Akamwagiza mmoja wa wasaidizi wake, awasiliane na wale waombaji sita na awapangie tarehe ya kuwafanyia usaili.
Hilo likafanyika.
Usaili ulipangwa kufanyika kwa njia ya simu, ambapo wasaili walipaswa kuwasiliana na wasailiwa, kwa njia ya mikutano ya kimtandao kwa kutumia simu maalumu zilizokuwa kwenye kila chumba cha mikutano cha shirika lile, kwa madhumuni hayo.
Kamati ya usaili iliundwa na watu watatu. Wawili kutoka idara inayohusika na kazi iliyotangazwa, mmoja kutoka idara nyingine ndani ya shirika, ili kuondoa maamuzi ya upande mmoja kwenye uteuzi wa msailiwa atakayepitishwa.
Mary, kama mkuu wa kitengo cha rasilimali watu hakuwa akihusika kwenye maamuzi, ila alipaswa kuwemo kwenye chumba cha usaili kuhakikisha kuwa wasailiwa wote wanaulizwa maswali sawa, na hakuna anayepewa upendeleo dhidi ya wengine; na kujibu maswali ya wasailiwa kuhusu mikataba ya ajira, matarajio ya shirika kutoka kwao kama wataajiriwa, na vitu kama hivyo.
Kwa unyeti wa ile nafasi, iliamuliwa kuwa wajumbe wa kamati wafike ofisini na waendeshe usaili ule kwa kuwapigia simu wasailiwa, ilhali wao wote wakiwa kwenye chumba kimoja ndani ya jengo la shirika. Wasailiwa wataongea nao kwa simu wakiwa majumbani kwao. Wakiwa mle ndani ya jengo la shirika, wanakamati walipaswa kuzingatia kanuni zote za kujikinga dhidi ya UVIKO-19 – kuvaa barakoa, kutokukaribiana, na kuhakikisha wananawa mikono kila mara, wakati wamo ndani ya jengo la shirika.
Kila kitu kilikaa kwenye mstari. Hatimaye, nafasi ile muhimu shirikani, ilikuwa inaelekea kujazwa.
***
USAILI ulipangwa kufanywa kwa siku mbili. Siku ya kwanza kamati ingeongea na wasailiwa watatu, na ya pili halikadhalika.
Kutokea kwenye chumba cha usaili, wajumbe wa kamati waliwapigia simu wasailiwa na kuongea nao kwa simu maalumu kwa mikutano ya aina ile, ambapo sauti za wasailiwa ziliweza kusikika na wote kwenye kile chumba.
Siku ya kwanza ya usaili ilienda salama.
Siku ya pili iliharibika mara tu msailiwa wa tano kati ya wale sita, alipoanza kuongea.
Kimsingi, siku ilibadilika hata kabla msailiwa yule wa pili kwa siku ile, hajamaliza kujibu swali la kwanza la jopo la usaili.
Lile swali lilimtaka msailiwa alieleze jopo, ni kwa nini anadhani yeye anastahili kupewa kazi ile, na kwa nini anataka kufanya kazi kwenye shirika lile. Lengo la swali lilikuwa ni kumpima msailiwa uwezo wa kujieleza kwa lugha ya Kkiingereza, ambayo ndiyo ilikuwa lugha rasmi ya mawasiliano ndani ya shirika.
Mary Komunte alimpomsikia tu yule mtu akiongea moyo ukamlipuka. Ukaanza kumwenda mbio, na pumzi zikayaelemea mapafu yake.
“Oh my God!” Alitweta huku akiikodolea macho ile simu iliyokuwa ikiwatawanyia mawimbi ya sauti ya msailiwa wao, mle chumbani.
Jamaa aliendelea kujieleza simuni, na Mary akazidi kuhemewa na ile sauti iliyokuwa ikiwasukumizia maelezo ya msailiwa wao.
No! It can’t be! Hai, haiwezekani!
Mary alijikuta akiinuka kutoka kitini.
“Ah! Huy-AAh!” Alishindwa kuyapanga maneno, akajihisi kizunguzungu.
“Mary! Umekuwaje!” Mmoja wa wanakamati alimhoji.
“Er, excuse me?” Kutokea kwenye simu, msailiwa wao alihoji.
Mary akapiga mweleka, bahati akaangukia makalio kwenye kile kile kiti chake. Mtafauruku ukastafidi kwenye kile chumba cha mikutano.
“Er, Hebu subiri kidogo Mista Kitambi… tuna mwenzetu hayuko sawa hapa!” Mwenyekiti wa jopo alimwambia msaliwa wao, kwa Kkizungu.
“Oh? Okay…” Sauti ya msaliwa iliwajibu kwa mashaka, kutokea upande wa pili.
Mary alikuwa kwenye wakati mgumu. Wenzake walimzonga pale kitini
“Mary! Una nini? Uko sawa?” Mmoja alimuuliza.
“Of course hayuko sawa bwana, si unamwona alivyo?” Mwingine akamrekebisha yule wa kwanza.
Mwenyekiti wa kamati akabonyeza kitufe kwenye ile simu yao, na kubana sauti zao zisisikike kule kwa msailiwa wao.
Uso wa Mary ulikuwa umepauka ghafla. Pumzi zilikuwa zikimwelemea. Akili ilimzunguka vibaya sana. Kitisho alichokumbana nacho miezi kadhaa iliyopita kilimrudia upya akiwa pale ofisini… baada ya kuwa kikimrudia mara kadhaa akiwa usingizini, kwa njia ya ndoto za kutisha.
Sasa leo… ofisini? Laivu?
“Sih, siko vizuri… siko, Oh!” Alibwabwaja huku akijishika paji la uso.
Mwenyekiti wa kamati ambaye alikuwa Mmzungu, alifyatua kitufe cha sauti kwenye ile simu yao.
“Er, Mista Kitambi, samahani sana. Tunaomba tuahirishe usaili huu kwa leo. Mwenzetu ameumwa ghafla…”
“Oh, poleni sana. Ha, haina shida. Naelewa.”
“Aam, watu wetu wa kitengo cha rasilimali watu watakupigia kupanga tarehe nyingine ya usaili huu, okay?”
“Yes Madam, ni sawa. Ahsante, na… poleni sana!” Msailiwa Kitambi alimjibu kwa sauti yake ya upole na iliyoishia kwenye mkoromo hafifu kila aongeapo.
Simu ikakatwa.
“Un, unadhani ni… Korona?” Mmoja wa wanakamati aliuliza kwa mashaka.
“Hapana. Sote humu ofisini tumepigwa chanjo, so uwezekano wa kuambukizwa kwa kiwango kama hiki ni mdogo san-“
“Not Corona! ” Mary alidakia kwa tweto, “ni, ni kitu kingine tu… niitieni uber niende home… siwezi kuendesha kabisa!”
“No, nakupeleka hospitali kwanza…” Mwenyekiti wa kamati alidakia, “kisha kutokea hapo nd’o itajulikana kama uende home au la!”
Mary Komunte hakuwa na nguvu ya kubishana.
***
ILICHUKUA siku tatu kabla Baiyu Kitambi hajapokea simu kutoka kwa mmoja wa watendaji wa kitengo cha rasilimali watu wa lile shirika kubwa kabisa la kimataifa nchini.
Ile simu ilimtaka ahudhurie usaili wa uso kwa uso na wajumbe wa kamati ya usaili.
“Oh? Nilidhani tutaendelea kufanya interview kwa simu?” Aliuliza.
“Hapana, tutafanya uso kwa uso safari hii. Ndiyo maana hatutafanyia kwenye jengo la ofisi yetu bali kwenye ofisi ya mmoja wa washirika wetu, aam… kule Masaki.” Alijibiwa.
“Oh?”
“Ndiyo. Eer, au… una tatizo na hilo mista Kitambi?”
“Ah, hapana… iko sawa tu hiyo!” Alimjibu.
Ile kazi alikuwa anaitaka sana. Kwa mujibu wa tangazo la kazi ile, mshahara ulikuwa ni zaidi ya mara mbili na nusu, ya ule anaoupata kwa mwajiri wake wa sasa.
Akapewa maelekezo ya namna ya kufika mahala ambako usaili ule wa uso kwa uso utafanyika, na kuombwa afike eneo la tukio kesho yake, saa nne asubuhi.
Hakudhamiria kukosa.
***
CHUMBA cha usaili kilikuwa kizuri na cha kisasa, kama jinsi jengo lililohifadhi ofisi ile lilivyokuwa.
Alikuta akina dada watatu wakimsubiri, wa nne mwanaume, ndiye aliyempokea na kumwongozea ndani ya chumba kile.
Alielekezwa aketi kwenye kiti kilichokuwa peke yake upande mmoja wa meza, ilhali upande mwingine wa meza ile, kulikuwa kuna viti vinne.
Mary Komunte aliyekuwa ameketi kwenye kiti kilichokuwa kikitazamana moja kwa moja na kile alichokalia bwana Kitambi, alimtazama kwa makini yule msailiwa wao.
Mwonekano wake uliendana na umri wake wa miaka 45 alioubainisha kwenye taarifa zake za maombi ya kazi. Alikuwa amejengeka kimazoezi na alikuwa nadhifu.
Baiyu Kitambi aliwatazama wajumbe wa ile kamati ya usaili waliokuwa mbele yake. Wanawake watatu, mwanaume mmoja. Alikumbuka vyema kuwa kwenye ule usaili wa simu ulioahirishwa, mmoja wa wasaili wale alikuwa na lafudhi ya Kkizungu. Hawa waliokuwa mle ndani pamoja naye wote walikuwa Wwaswahili, na mmoja wa wake wanawake, alikuwa mjamzito.
“Er, poleni sana kwa dharura iliyotokea mara ya mwisho tulipoongea kwa simu…” Aliwaambia kwa sauti yake nzito, ya upole, na iliyomalizikia kwenye mkoromo hafifu kila aongeapo.
Mary akamtupia jicho yule mwenzake mwenye ujauzito mle ndani. Akaona kuwa naye amekisikia kile ambacho yeye alikisikia.
Akamgeukia msailiwa wao.
“Ahsante sana bwana Kitambi… aam, naitwa Mary Komunte. Ni mkuu wa kitengo cha rasilimali watu wa shirika, na ndiye niliyepatwa na tatizo wakati ule.” Alimwambia huku akimpa mkono kumsalimia.
“Oh? Pole sana, na nafurahi kuona uko salama sasa.” Jamaa alimjibu huku akiupokea ule mkono. Mary akahisi kovu baya nyuma ya kiganja cha kulia cha yule msailiwa wao, na mwili ukamsisimka.
Kila mjumbe alimpa mkono huku akijitambulisha. Wakaketi na kufunua makabrasha yaliyokuwa mbele yao.
“Sawa bwana Kitambi, tunaweza kuanza usaili wetu sasa?” Yule mwanamama mjamzito ambaye ndiye alijitambulisha kuwa ndiye mwenyekiti wa ile kamati, alimuuliza.
“Bila shaka, madam Fatma!” Bwana Kitambi alimjibu.
Mary akamuuliza lile swali la kwanza ambalo hakuwahi kumaliza kulijibu kwenye simu, siku tatu nyuma.
Baiyu Kitambi akajieleza vizuri sana, huku wale wajumbe wakimsikiliza na wakiandika andika kwenye fomu maalumu walizokuwa nazo pale mezani.
“Ahsante sana mista Kitambi, aaam, swal’ la pili litatoka kwangu,” mMwenyekiti wa kamati alimwambia baada ya kukamilisha jibu lake.
“Please go ahead, ma’am.” Baiyu Kitambi akamwambia kwa nidhamu sahihi na Kkizungu nyoofu.
“Tarehe 14 Februari, siku ya wapendanao, saa tano usiku… ulikuwa wapi?” Aliulizwa.
“Whaaat?” Baiyu aling’aka huku akimkodolea macho ya kutoamini yule mwanadada mjamzito, aliyejitambulisha kwake kwa jina la Fatma Suluja.
Akakutana na macho makavu yenye kiu ya jibu.
Akafyatua cheko la mashaka, na kutoelewa. Akamgeukia aAfisa rasilimali watu wa lile shirika kwa macho ya kuuliza. Akakutana na macho yenye uchu wa jibu, na kitu kingine ambacho hakutaka kuamini kuwa ndicho alichokiona.
Hasira?
Alishindwa kuelewa. Akamgeukia yule mwanakamati wa kiume. Akakutana na macho makavu tu.
“Aam, sielewi msingi wa hili swali… linahusika vipi na hii interview?” Alimuuliza yule mwenyekiti wa kKamati.
“Oh, linahusika sana bwana Kitambi, so naomba ujibu ili tuokoe muda.” Mwenyekiti wa kamati Fatma alimwambia.
Baiyu akatikisa kichwa.
“Mn-Mnh! Hili sio swali sahihi,” Baiyu alisema, na kumgeukia Mary, “na we’ unajua hilo!”
“Hilo ni swali na linahitaji jibu,” alijibiwa “ulikuwa wapi usiku wa wapendanao mwaka huu, saa tano usiku, bwana Kitambi?” Akarudishiwa swali.
Akakunja uso kwa mshangao, kwani safari hii, sauti ya yule mwenyekiti wa kKamati ilimbadilikia na kuwa ya mamlaka sana.
Alichanganyikiwa.
“Ah, okay… tuseme nijitahidi kuwaridhisha tu na kulijibu,” alisema kwa mashaka, “sikumbuki!”
Wajumbe wa kamati ya usaili wakamtazama wakiwa kimya kwa muda.
Vipele vya jasho vilionekana kumea kwenye paji lake la uso, pamoja na kiyoyozi kilichokuwamo.
“Sawa, nalo pia ni jibu,” yule mjumbe mwingine alisema hatimaye, kisha akaendelea, “swali linalofuata litatoka kwangu, na hili liko kwenye mfumo wa chemsha bongo.”
Safari hii Baiyu wala hakuwa na nguvu ya kumjibu, alibaki akimtazama tu huku akihisi makwapa yakimlowa ndani ya koti alilovaa juu ya shati lake ghali.
“Naomba utusomee kwa sauti, kilichoandikwa hapo.” Yule mjumbe wa tatu alimwambia huku akimsukumia karatasi iliyoandikwa kwa kompyuta.
Baiyu aliitazama huku akiisoma ile karatasi, lakini badala ya kutamka kwa sauti alichokisoma, alitumbua macho na kuuma mdomo kwa hasira. Akainua uso kumtazama yule mjumbe aliyempa ile karatasi.
“What… what is this?” Alihoji kwa Kkiingereza.
“Wrong answer!” Alifyatuliwa jibu kwa Kkiingereza vilevile, ” si jibu sahihi hilo!” Fatma alidakia.
“Soma kwa sauti kilichoandikwa!” Mjumbe mwenye swali lake, naye akamchachamalia.
“AH!” Baiyu alimbweta, “mbo, mbona si, siele-”
“Unakujaje klabu wakati oili inavuja malaya wewe? Leo utan’piga bloojob ‘apa’apa!” Mary aliropoka kwa sauti yenye hasira.
“Eh!” Baiyu aligutuka kwa mshangao na woga mkubwa, huku akimgekia Mary.
Hasira aliyoiona machoni kwa yule afisa rasilimali watu iliikidhi ile aliyoisikia kwenye sauti iliyomtamkia maneno yale tata, sekunde tu iliyopita.
Macho yao yakaumana.
“Si ndicho kilichoandikwa hapo?” Mary alimtemea swali, kwa ukali.
Baiyu Kitambi alikuwa ni taswira halisi ya ndege mjanja kabisa, aliyenaswa kwenye tundu bovu kabisa.
“Unajua ni nani alimtamkia nani maneno hayo, saa tano ya usiku wa siku ya wapendanao mwaka huu?” Mary alimfokea.
Tusi la nguoni likamtoka Baiyu huku akikurupuka kutoka pale kitini.
“Mna wazimu nyote!” Alibwata huku akiuwahi mlango wa kutokea nje ya chumba kile. Aliuvuta kwa nguvu ule mlango kwa lengo la kutoka na kuondoka mahala pale.
Patupu.
Mlango ulikuwa umekomewa kwa ndani.
“AAAKH!” Alimaka kwa fadhaa huku akiwageukia wale wajumbe wa kamati ya usaili.
Akaganda.
Mwanadada aliyejitambulisha kwake kwa jina la Fatma, alikuwa ameshika bastola, wakati yule aliyempa ile karatasi yenye yale maneno aliyolazimishwa kuyasoma kwa sauti, alikuwa ameshika pingu.
Heh!
Akamgeukia afisa rasilimali watu Mary Komunte. Akakutana na macho yenye ghadhabu iliyopigiwa mstari kwa machozi yaliyokuwa yakimbubujika bila kizuizi mashavuni mwake.
“Samahani, sikuwa nimejitambulisha vyema hapo mwanzo mwana Baiyu,” Mwenyekiti wa Kamati ya usaili alimwambia, “mimi ni Inspekta Fatma Suluja kutoka Kkituo Kkikuu cha Ppolisi, na sasa uko chini ya ulinzi kwa makosa matati ya ubakaji na moja la kujaribu kubaka na kutishia uhai.”
Miguu ikamlegea Baiyu Kitambi, akajishitukia ameketi sakafuni.
“Ah, kumbe hapa sio…?”
“Kwenye usaili? No way! Umeingia kwenye mtego wetu kiulaini sana, baada ya kulisumbua jeshi la polisi kwa mwaka mzima, shwaini, wewe.” Inspekta Fatma alimwambia huku akimsogelea.
“Lakini, lakini… mmejuaje, yaani… kivi-“
“Ni sauti yako ndiyo iliyokukamatisha, Mr. Vvoice fry!” Inspekta Fatma mjamzito alimwambia.
Kitambi akamtupia Mary macho ya viulizo vilivyotatizika, uelewa wa kilichomponza ukimzama akilini kwa mkito mzito.
Huku midomo ikimtetemeka, Mary Komunte alimtazama mbakaji Baiyu Kitambi akiangua kilio cha fadhaa wakati akifungwa pingu.
***
SIKU mbili baadaye kamati halisi ya usaili ilikuwa imekutana tena.
“Sasa tumeshawasaili waombaji wote kasoro yule mmoja…” Mwenyekiti halisi wa ile kamati, mama wa Kkizungu alisema.
“Yah, Baiyu Kitambi!” Mjumbe mwingine alidakia.
Kabla mjadala haujasonga, mlango ukagongwa, kisha ukasukumwa ndani. Mmoja wa wasaidizi wa afisa rasilimali watu aliingia.
“Er, samahani… msailiwa wa mwisho, Baiyu Kitambi? Bado hapatikani kwenye simu mpaka sasa.” Msaidizi aliripoti kile ambacho Mary alishakijua. Atapokeaje simu wakati yuko mahabusu anasubiri mashitaka?
Mary aliwatazama wajumbe wa kamati kwa utulivu. Wao wakamgeukia yeye.
“Ah, sasa tunafanye kwenye hali kama hii, Mary? Tunahitaji kumaliza hili suala ili tuingie hatua nyingine…”
Mary akatabasamu. Alishajua kuwa ingefikia pale.
“The guy’s a no show,” alisema kwa utulivu, akimaanisha kuwa jamaa ameshindwa kutokea kwenye usaili, “amepewa nafasi akapotea hewani. Nashauri kamati iendelee kufanya maamuzi kwa kuwaangalia hawa ambao tumeshawasaili mpaka sasa.”
“Oh? Okay… na Mista Kitambi?” Mwenyekiti alihoji.
“Ah, kimsingi ni kwamba amejitoa mwenyewe kwenye usaili kwa kutopatikana hewani. There’s no way tungemfuata nyumbani kwake sisi. Huu usaili umekamilikia hapa!”
“Safi sana Mary. Hayo ndiyo maamuzi!” Mwenyekiti wa kamati alimpongeza.
Mary akaachia tabasamu la upande mmoja.
“Good. Mi’ naondoka sasa. Nataraji kupata memo ya mapendekezo ya mtu gani aliyepita kwenye usaili huu very soon, right?” Alisema huku akiinuka.
“Oh, yes!” Mwenyekiti na mjumbe mwingine mmoja walimjibu kwa pamoja.
***
USIKU WA WAPENDANAO, MIEZI MINNE ILIYOPITA.
Alikuwa amedhamiria kulienzi penzi lake, kwa kufanya kile ambacho mpenzi wake alichokuwa akipenda wakifanye pamoja, kila ifikapo siku ya wapendanao.
Hakutaka kuruhusu majonzi yawe sehemu ya kumbukizi ya hayati mpenzi wake.
Hivyo, pamoja na kuwa “Valentine Day” hii hatokuwa na mpenzi wa moyo wake, alienda klabu na kujirusha kama ambavyo wangefanya, kama mpenziwe angekuwepo.
Na alijirudha sana usiku ule. Akiwa peke yake. Alicheza muziki, akanywa kinywaji akipendacho yeye, “Strawberry Mojito”, na kile akipendacho marehemu mpenzi wake, mvinyo ghali wa “Cabernet Sauvignon.”
Saa tano usiku aliamua kuondoka. Aliliendea gari lake ghali, Rav 4 Station Wagon modeli mpya kabisa, alilokuwa ameliegesha kwenye kona kabisa ya eneo la maegesho ya ile klabu iliyofurika mno usiku ule. Ilikuwa ni siku iliyosadifu mfuriko ule. Maegesho yalikuwa adimu na alijiona mwenye bahati japo kupata nafasi ya kupaki pale upenuni kabisa mwa maegesho yale.
Alikaa nyuma ya usukani na akaruka kwa mshituko huku kiyowe kikimponyoka kwa woga, pale kioo cha dirisha lake kilipogongwa ghafla. Alikigeukia kioo na kuona kijana mtanashati akiwa amesimama nje ya dirisha lile huku akitabasamu. Alikuwa akimwashiria kitu kwa kidole chake, lakini hakumwelewa.
“What?” Alimuuliza baada ya kushusha kioo.
“Pole, nilikuwa nakwambia kuwa una pancha tairi lako la upande huo….” Jamaa aliwambia huku akioneshea upande wa kiti cha abiria.
“Ah, kweli? Oh, shit… imetokeaje hii?” Alimaka na kulaani.
“Aam…una jeki labda… ? Na tairi la akiba nikusaidie fasta?” Jamaa alimuuliza.
Akateremka na kuzunguikia ule upande ambao aliambiwa tairi limepata pancha , akizisikia hatua za yule jamaa zikimfuata nyuma yake.
Hakukuwa na pancha.
“Hah? Mbona-”
“Kimya wewe!” Yule jamaa alimkoromea na wakati huo huo akimkaba kutokea nyuma. Alimwekea kisu kooni.
Oh, My God, naporwa gari?
“Un, Unataka ni-?”
Aligongwa kwa nguvu nyuma ya goti, na akaenda chini bila kupenda. Jamaa akawa ameshamlalia juu yake.
“Kimya! Laa sivyo nakutoa uhai!” Alimkoromea.
Mungu wangu!
Alikuwa amebananishwa pale chini, ubavuni mwa gari lake kwa upande mmoja, ilhali upande mwingine kulikuwa kuna ukuta wa uzio wa lile eneo la maegesho. Walikuwa wamegubikwa na kiza kutokana na kuwa upenuni kabisa mwa eneo lile.
“Uh, unataka ni-”
Alianza kuuliza kwa woga lakini hapo, aliuhisi mkono mmoja wa yule mtu ukazama ndani ya sketi yake fupi.
Ananibaka??
Alijikukurusha, lakini akadidimizwa kisu shingoni hadi akahisi mchirizi wa damu.
“Tulia!” Jamaa alimkemea kwa kunong’ona, kwa mara ya kwanza uajabu wa sauti ya yule mtu ukimzama akilini.
Woga uliomgubika haukuwa kama aliowahi kuuhisi kabla, maishani mwake.
Alianza kulia kwa uchungu wakati akiuhisi mkono wa yule mvamizi ukimpapasa ndani ya mapaja yake huku akimhemea kwa tweto nyuma ya shingo yake.
Kwa kitendo cha pupa, jamaa aliivuta na kuiachanilia mbali chupi yake, akiikwapua na ile taulo ya hedhi aliyokuwa amejipachika mahala pake.
“Aarggh! Unablidi??” Jamaa alimkemea kwa mnong’ono wa ghadhabu.
“Oh, we’e kaka niachie tafadh-”
“Unakujaje klabu wakati oili inavuja malaya wewe?” Alikemewa huku akigongwa kwa nguvu kisogoni, kwa kichwa cha yule mvamizi wake.
“Oh, we kaka please-”
“Sasa leo utan’piga bloojob ‘apa’apa (akamtukania mama yake)!”
Hah!
Jamaa alimgeuza kimabavu na kumnlaza chali pale chini, kisha hapo hapo akamdidizia tena kisu kooni.
“Piga kelele nikuchinje, malaya we!” Jamaa alimlalia kifuani huku bado amemdidimizia makali ya kisu kooni. Mary alilazimika kutulia kwa kukihofia kisu. Akawa analia kimya kimya.
“Kimya weweee! Unadhani s’jakuona ulivyokuwa unajichetua kule klabu nyau wewe?” Jamaa alimtemea maneno huku bado akihangaika kufungua zipu ya suruali yake kwa ule mkono wake mwingine.
Oh, My love! Hivi kweli mi’ nabakwa kwenye kumbukizi ya penzi letu??
Ghafla aliukamata ule mkono wake wenye kisu wa yule jamaa na kuudidimiza meno kwa nguvu zake zote nyuma ya kiganja.
“YAAAALLAAA-AYYA YAY-YYAAKH!” Jamaa alipiga ulelele wa uchungu. Yeye alizidi kumng’ata kwa nguvu huku ameushika ule mkono kama anayemega muwa mgumu.
Jamaa akaachia kisu kikimwanguka na akamzaba kofi kali la uso kwa ule mkono wake mwingine. Japo lile kofi lilimtembezea nyota usoni, hakuyang’atua meno yake kutoka kwenye nyama ya kiganja cha hasimu wake hata kidogo, tena sasa alikuwa akiunguruma kama mbwa mkali aliyeng’ang’ania nofu tamu la nyama.
Jamaa alipiga ukelele mkubwa zaidi kwa maumivu, na hapo hapo akamtwanga ngumi kali ya upande wa kichwa. Mary akatupwa pembeni kwa nguvu na kujibamiza vibaya kichwa chake kwenye ringi la tairi la mbele la gari lake.
Fahamu zilimwelea. Akahisi kiza juu ya kile kilichotanda usiku ule.
Hapo alisikia mayowe mapya na vishindo vya miguu vikikimbilia pale walipokuwa.
Akagoma kuzirai.
Msaada jamaniii!
Hakujua kama ni kweli aliyatamka yale maneno au yalikuwa akilini mwake tu, maana hata sauti yake yenyewe hakuisikia. Alijitutumua na kujiinua kwa kujishikiza kwenye gari lake huku bado akiwa amemng’ata mkono yule jamaa.
“Nini ‘apa? Kulikoni?” Sauti yenye wahka ilimsemesha. Sio ile ya ajabu ya yule mbakaji. Alitumbua macho. Alikuwa ni mlinzi wa pale klabu.
Eenh?
Aligeuka huku na huko. Yule jamaa aliyemshambulia, hakuwepo.
Atakuwa ameondokaje na mi’i bado nimemng’ata hapa?
“Anti! Una damu! Um, umekutwa na nini?” Mlinzi alimhoji tena.
Akatutumua macho. Kweli mvamizi wake hakuwepo.
Inakuwaje?
“Anti!!”
Akafunua kinywa kumjibu, na kipande cha nyama kikaanguka kutoka kinywani kwake. Na ndipo kwa mara ya kwanza alipoihisi ladha ya damu kinywani mwake.
“Oh, My God! Alijaribu kunibaka!” Aliropoka huku akitema mate yenye damu ya mbakaji.
***
Nusu saa baadaye alikuwa Kkituo Kkikuu cha Ppolisi, na ndipo alipokutana na Inspekta Fatma kwa mara ya kwanza. Wakati huo ujauzito wake haukuwa ukionekana vyema.
Inspekta alishangaa kuona akiwekewa kipande cha nyama ya binadamu mezani kwake, kikiwa kimefungwa kwenye hanchifu iliyolowa damu.
“Alijaribu kunibaka! Nikamng’ata… akakimbia… nyama yake hiyo!” Mary aliongea kwa kiwewe. Inspekta Fatma na mwenzake walitazamana, kisha wakamtazama kwa udadisi.
Jinsi alivyofika pale kituoni ilikuwa kama muwujiza tu kwake.
Hakuzubaa sana pale klabu. Walinzi walimzonga kwa maswali yasiyo mantiki. Alikishika kisu cha mbakaji kwa kitambaa na kukitupia kwenye kiti cha nyuma ndani ya gari lake. Kisha ndio akakiokota kile kipande cha nyama kwa kukiviringa kwenye ile hanchifu.
Akaingia garini na kuongoza kituoni huku akilia na akitetemeka kwa woga na hasira. Alihisi kudhalilika vibaya.
“Ulipata kumwona sura yake?” Inspekta Fatma alimuuliza baada ya kumtuliza na kupata maelezo yake ya awali.
“Ah, sio vizuri… s’kumwona vuzuri. Kulikuwa kuna giza.”
“Okay kuna kitu gani unachoweza kukumbuka kuhusu huyo mvamizi?” Aliulizwa tena. Akakunja uso.
“Ah, sijui… labda pafyumu? Alikuwa ananukia pafyumu f’lani hivi ya kiume… ila, ila siwezi kuitambua ni aina gani!”
Wale askari waliokuwa naye kwenye chumba cha mahojiano walitazamana. Namna walivyotazamana, ilimfanya Mary ahisi walikuwa wanalo wanalolijua kuhusu kile kilichomkuta. Akamakinika.
“Ee, ku, kuna nini? Anything I should know?” Aliuliza iwapo kuna alilopaswa kulijua, huku akiwatazama kwa zamu wale askari.
Inspekta Fatma akajikohoza kidogo.
“Ah, tunajaribu kuelewa mazingira ya jaribio hilo… huwezi kukumbuka chochote zaidi kuhusu huyo mtu? Namna yake ya kutembea labda… lafudhi yake, au labd-”
“Sauti!” Mary aliropoka huku akimwoneshea kidole yule Inspekta, na kabla Inspekta hajaomba ufafanuzi wa ile kauli yake, yeye akaendelea, “alikuwa ana, ana, ana…,” alitafuna neno mwafaka, akalikosa, “ah! A voice fry!”
“A voice Fry?” Inspekta Fatma alimuuliza kwa umakini mpya. Mary akaafiki kwa kichwa huku akimtazmaa kwa matarajio.
“AH!” Inspekta alimaka huku akiinuka kitini na akipiga kiganja chake mezani, “ni yeye!” Alisema kwa kiherehere huku akimgeukia yule askari mwenzake wa kiume.
“Kabisa!” Mwenzake akaafiki.
Mary alibutwaika.
“Sasa inaleta maana, manake-”
“Mna maana gani ni yeye?” Mary alimkatisha kwa wahka, “ina maana mnamjua huyo jamaa? Alishabaka mwingine before?”
Wale askari walimtazama.
“Alishabaka watu watatu kabla yako.”
“Eeenh?”
“Yes! Mmoja kwenye fiesta, mwingine muunza muuza mihogo kando ya barabara aliyejitia kumpa lifti usiku… na wa mwisho hapa juzi juzi baada ya mechi ya Ssimba na Yyanga. Mmoja wa akina dada waliokuwa wakishangilia mabarabarani usiku baada ya ile mechi!”
“Duh!”
“Tumekuwa tukimsaka kwa muda mrefu huyu mjinga!”
“Kwa hiyo kama nisingekuwa kwenye siku zangu leo… mi’i ningekuwa namba nne?”
“Yap!”
Mary alichanganyikiwa.
“Sasa ni kipi kilichowajuza kuwa ni yeye… ni sauti yake?” Alihoji.
Inspekta Fatma akaguna.
“Wote hao waliobakwa hawakufanikiwa kumwona kama wewe, lakini the common denominator kwenye maelezo yao wote ilikuwa ni sauti ya mbakaji…” Alimwambia, akimaanisha kuwa kitu kilichofanana kwenye maelezo ya wale wahanga wote waliotangulia kilikuwa ni sauti ya mbakaji.
“Kivipi?”
“Wote walisema kuwa alikuwa ana namna ya kuongea ambayo iliifaya sauti yake iwe tofauti,” Inspekta Fatma alimwambia, “mmoja alisema sauti yake huwa inaishia kwenye mkoromo. Mwingine akasema akiongea sauti yake ilikuwa inaingia msinzio.”
“Eh?”
“Yes. Na mwingine akasema alikuwa ana sauti ya kuchombeza.”
“Ish!”
“Hatukuweza kuwaelewa wakati ule, lakini leo ndio umetufumbua macho!”
“Kwa, kwa kusema kuwa alikuwa ana voice fry?”
“Yes! Hiyo sasa ndiyo ianleta inaleta maana ya namna wale wengine walivyokuwa wanajaribu kutwelezea kuhusu sauti ya mbakaji wetu… kumbe ana kilema cha kukaanga sauti kila aongeapo!”
“Mbakaji wetu ni mkaanga sauti.” Yule askari mwingine alihitimisha.
Mary alishusha pumzi za mshangao.
“Sasa kulijua hilo kutawawezesha kumpata?” Alihoji.
“Tutaendelea kumsaka. Umetupa vitu vitatu muhimu, leo bi Mary… kisu chake ambacho kina alama zake za vidole, namna yake ya kuongea, na kwamba atakuwa ana kovu baya kwenye mgongo wa kiganja cha mkono wake wa kulia… kitendawili kimezidi kuwa chepesi sasa.” Inspekta Fatma alimwambia kwa kirefu.
Mary alishushahs apumzi za ahueni.
“Doh afadhali. Naombea mumpate haraka sana, mshenzi mkubwa!” Alisema.
“Hilo tutalifanya. We’ tuzidi kuwasiliana tu, dada.” Inspekta Fatma alimwambia.
Tangu siku ile njozi mbaya za tukio lile zilimwandama. Sauti mbaya ya yule mbakaji, ikazitawala fahamu zake kila anapokuwa usingizini.
Lakini, mbakaji hakupatikana.
Mpaka alipokuja kuisikia sauti yake kwenye chumba cha usaili, miezi minne baadaye.
Hussein Tuwa
Goba, Dar es Salaam.
Julai 22, 2021
#riwayandozetu