Muda wa Uhariri
Waandishi wengi hupenda kufahamu muda ambao mhariri anaweza kuutumia kukamilisha uhariri wa miswada yao kama wakimkabidhi. Huu ni ufafanuzi mfupi kuhusiana na suala hilo.
Muda ambao mhariri huweza kuutumia kukamilisha uhariri wa kazi yako huweza kuwa muda mrefu au mfupi kutokana na sababu nyingi, zifuatazo ni miongoni mwa sababu hizo
1. Ratiba ya mhariri
Baadhi ya wahariri makini huwa na miswada mingi ya kuihariri, hivyo basi mhariri anaweza kupokea mswada wako na kuuweka kwenye foleni. Atakapomaliza kuishughulikia miswada iliyotangulia ndiyo aanze kushughulikia mswada wako. Suala hili huumiza sana waandishi huru kwani lengo la mwandishi huwa kupokea kazi yake kutoka kwa mhariri mapema ili aendelee na michakato mingine ya uchapishaji.
2. Ugumu wa kazi husika
Mswada ambao umekuwa na makosa mengi sana huchukua muda mwingi kwa mhariri kuyapitia kwa umakini na kuyaweka sawa, kazi za namna hii pia muda mwingine husababisha mhariri kupunguza kasi ya kusoma ili abaini makosa na kuyasahihisha. Kadri kazi inavyokuwa nyepesi kuhariri ndivyo inavyochukua muda mfupi kuihariri.
3. Aina ya kazi inayohaririwa
Mhariri ambaye maisha yake yote amekuwa akihariri magazeti huchukua muda mfupi kuhariri gazeti au jarida kuliko kuhariri mswada wa riwaya ya kifalsafa au kijasusi. Hivyo ni vyema kwa mwandishi kumbaini mhariri ambaye anaweza kuhariri kazi ambazo zipo katika mwegamo wa mkondo wa mswada husika. Mhariri ambaye amezoea kuhariri kazi ngumu, huweza kuhariri kwa muda mfupi kazi ambazo hazina urefu wa mfungamano wa mambo.
4. Uchipukizi au ukongwe wa mwandishi
Mara nyingi waandishi chipukizi miswada yao hukaa muda mrefu kwa wahariri, ukilinganisha na waandishi wakongwe wanaojua kaida za uandishi na kuzifuata. Waandishi chipukizi huhitaji msaada mkubwa wa kuboresha kazi zao kuliko waandishi wakongwe.
5. Ukubwa wa kazi
Kazi ambayo ina maneno mengi, huchukua muda mrefu kuhaririwa kuliko kazi yenye idadi ndogo ya maneno.
6. Wapi umepeleka kazi yako ihaririwe
Mswada uliopelekwa katika kampuni fulani kwa ajili ya kuhaririwa, huweza kuchukua muda mrefu kuhaririwa kutokana na mlolongo mrefu ulioko kwenye kampuni za uhariri na uchapishaji, ila kazi iliyopelekwa kwa mhariri binafsi huweza kuchukua muda mfupi kwa sababu aghalabu maamuzi huwa ya mtu mmoja au wawili.
Kwa huduma bora ya uhariri ndani ya muda mfupi usisite kuwasiliana nasi.