Mwimbula

Frank Masai

Katika kutunza mila na desturi za Mwafrika na utamaduni wake, ilitupasa kujifunza na kupitia mafunzo machache ambayo yalikuwepo tangu enzi za babu na bibi zetu. Mafunzo kama jando na unyago, ni tamaduni ambazo kila kaya kwenye jamii nyingi za Kiafrika zilipitia kwa njia tofauti. Wapo waliofanya haya kwa wanawake wakubwa. Na wapo waliofanya kwa wanawake wadogo ambao ndio kwanza walikuwa wanavunja ungo. Hata kwa wanaume ilikuwa vivyo hivyo. Jando ilifanyika kwa wanaume wakubwa na wadogo ambao tayari walikuwa wamepevuka kiakili.
 

Tofauti na maisha ya sasa, yanayoendana na kasi ya ukuaji wa Sayansi na Teknolojia pamoja na Dini. Maisha yamebadilika na tamaduni zetu zimefunikwa na mabadiliko haya ya dunia. Jando na Unyago ni desturi ambazo zimeanza kuzikwa kwenye kivuli cha Sayansi na Teknolojia. Kumekuwa na sababu nyingi za kufifia kwa tamaduni hizi, ikiwepo vitisho, dini na kwenda na wakati.

Sehemu ya vitisho hivyo ni pamoja na maambukizo ya magonjwa na kutengana kwa familia. Kwamba, mtoto wa kiume asipofanyiwa tohara akiwa mdogo, kuna uwezekano mkubwa wa kukumbwa na magonjwa. Ama la! Asipofanyiwa tohara, basi kuna uwezekano mkubwa wa mtoto kubaki hivyo kama familia yake; baba na mama watatengana.

Pia unyago  unaweza kusababisha magonjwa ya maambukizo. Mfano magonjwa ya ngozi. Huku wengine wakidai ni maadili potofu.  Sababu kama hizi zinapelekea kufa kwa mila nyingi za Kiafrika. Ama kama si kufa, basi kupoteza mvuto wake.

Pia dini tunazoziamini, zimekuwa chanzo kikubwa kingine cha kufunika tamaduni za Mwafrika. Katika suala hili la dini ambalo linaweza kuongelewa kiundani zaidi kwenye makala zinazoandaliwa na wataalam.Naomba kwenye kazi hii nisigusie sana kwa sababu hii ni imani na si vema kuingilia imani ya mtu. Ila kwa kifupi, babu zetu hawakukosea pale walipokuwa wanaamini na kuzitukuza tamaduni zao. Nimeandika haya kwa sababu yupo bwana mmoja mlowezi wa dini, aliwahi kuniambia kuwa, babu zetu hawakuwa sahihi kwenye kuamini tamaduni zao.

Imekuwa nadra kwa watoto wa mjini kuwekwa ndani na kupatiwa mafunzo yaliyokuwa yanatolewa jandoni na unyagoni. Kwanza atatoka wapi wa kutoa mafunzo hayo? Hali imebadilika na watoa mafunzo nao wamepotea.

Hata kama alikuwa ni mkufunzi mzuri hapo kale, siku ukikutana naye, anaweza kujikataa. Yote ni kwa sababu ya mabadiliko ya dunia kwenye Sayansi na Teknolojia. Mabadiliko yamekandamiza hadi akili zetu. Tunajikuta tunajikataa sisi ni wakina nani.

Tunauita UTANDAWAZI. Ambao ukiingia ndani yake kwa kina, utagundua kuwa ni sehemu ya ukoloni. Kwamba mtu mweupe kaamua kututawala kwa akili yake hadi tunaweka pembeni akili zetu. Anatuendesha atakavyo kupitia teknolojia. Na ukute anafahamu fika kuwa tunachokiamini sisi ni sahihi kuliko aaminicho. Lakini kwa kuwa tayari ni mweupe, na sisi ni weusi, yeye yupo sahihi. Inafika kipindi mtu mweusi haamini anachoelezwa na mweusi mwenzake.

Sitoona ajabu hata haya maandishi kuna watu wataishia kuyasoma na kuyaona kama upotoshaji. Yote kwa sababu yapo kinyume na mawazo ya mtu mweupe.

Imani ya mtu mweupe kichwani mwa mtu mweusi, ni kwamba: BAADA YA MUNGU NI MZUNGU. Hivyo ukienda kinyume na mtu mweupe, kuna baadhi ya watu weusi, watakuona unamkosea MUNGU. Si kweli.

Licha ya mabadiliko ambayo kila siku yanaendelea kuichukua Dunia, zipo sehemu ambazo hazijaingiliwa na mwamvuli wa utandawazi. Sehemu hizo bado zinaamini mila na desturi za Kiafrika zinapaswa kuzingatiwa na kutunzwa.

Hata mijini, kuna wazee ambao wanarithisha tamaduni hizo kama wao walivyorithishwa na vizazi vya nyuma. Sehemu za tamaduni ambazo hurithishwa kizazi na kizazi ni pamoja na suala la kutoa mahari pale unapotaka kuoa.

Katika vitu ambavyo vinaendelea kuwepo katika jamii zetu nyingi, ukiachana na jando na unyago, ni suala la mahari. Humwambii  kitu Mwafrika kuhusu utamaduni huo. Huko tumepatunza kwakuwa kuna manufaa kwenye baadhi ya familia. Na ninapozungumzia mahari, simaanishi ‘mamilioni’ ya fedha na vitu ambavyo havimaanishi chochote kwenye maisha ya ndoa ambayo mwanadamu anakwenda kuyaanza.

Katika jamii zetu hizi za kisasa, unakuta familia ina kila kitu ambacho hata anayekwenda kuoa hana. Lakini familia hiyohiyo, inakutajia vitu ambavyo unapaswa kuvipeleka ili umuoe binti yao. Vinaitwa vitu vya kimila.

Mahari hupangwa, lakini kwenye sehemu hiyo ya mahari, kuna hivyo vitu. Ni kheri usipeleke mahari ya mamilioni kuliko usipeleke vitu vya kimila.

Vitu hivyo ndivyo vinathibitisha kuwa utamaduni wa mtu mweusi bado unaendelea kuchukua nafasi katika jamii nyingi.

Kwa mfano: Yapo makabila ambayo yatahitaji upinde na mkuki ambavyo hudaiwa na kaka mkubwa. Kwa muoaji, hii umaanisha shukrani kaka kwa kunilindia mke. Kuna vitenge kwa mashangazi na mama ikiwa kama ahsante kwa kumlea mke. Aliwachafua utotoni, sasa chukueni vitenge hivi kujifuta.

Tofauti       ya vitu hivyo na mahari ya pesa, ni kwamba: kiasi kikubwa cha mahari hupewa mwali. Na mara nyingi hutolewa kutokana na mila za kabila hilo.

Mfano: Ukienda kuoa kwenye kabila la Wasukuma, watahitaji ng’ombe kwa sababu wao ni wafugaji. Ukienda kuoa kwa Wafipa, watahitaji majembe na maksai kwa sababu wao ni wakulima. Ukienda Uchagani watadai ndizi na mbege. Na makabila mengine.

Vitu hivi huletwa na upande wa mwanaume. Na mara nyingi, unaweza kubadili mahari na kuwa pesa tasilimu. Pesa hizo zinaenda kununua vile vilivyohitajika.

Hiyo ndio tofauti. Kwamba vile vitu vya kimila, havibadiliki. Ni lazima uvilete kama vilivyo. Kama mkuki, uwe mkuki. Kama mshale, uwe kweli mshale. Wakati huo mahari ya kawaida, huweza kuwa kiasi cha fedha. Pia unaweza kuomba kupunguziwa.

Katika jamii za sasa za utandawazi, mahari huwaponza wanawake. Wanawake walioolewa wanaumizwa kwa sababu ya mahari. Wanakuwa watumwa kwenye ndoa zao. Maisha mazuri waliyoyategemea yanageuka na kuwa huzuni. Mtoa mahari anamhesabu mke wake kama bidhaa aliyoinunua kwa wazazi na ndugu zake. Na hapo ndipo ubaya unapoanzia. Visasi, hasira na kila aina ya kadhia, vyote vinamvamia.

****

“Nilifunzwa mambo mengi yahusuyo kuhudumia ndoa. Mambo ambayo si wanawake wote wanaoyapitia. Naweza kuwa uzao wa mwisho kuyajua mambo haya.”

Sikumjua hapo mwanzo. Sikumjua yeye ni nani na alikuwa na masahibu gani. Lakini taarifa zenye mvuto juu ya maisha yake, ndizo zilizonivuta na mimi nikavutika. Nikajikuta nataka kujua mengine ambayo wengine walikuwa hawayajui.

“Kwani unaitwa nani?”  siku ya kwanza kukutana naye nilijikuta namuuliza swali hilo baada ya kujitambulisha kwake.

Alinitazama kwa sekunde kadhaa kama mwenye kutaka uhakika wa swali langu, ama mwenye kutaka kuuliza kwa nini nataka kujua jina lake? 

“Ah! Usijali dada yangu,” nikajikuta naanza kujitetea kwakuwa macho yake yaligota usoni kwangu kwa muda kidogo bila kunena jambo. “Siwezi kukuandika jina lako kwenye kazi zangu. Na wala sitawatuma watu waje kukuona.” Nikajitetea.

“Sasa jina langu la nini?” aliniuliza.

Nilimtazama vema machoni. Hakuwa kama siku niliyokutana naye kwa mara ya kwanza. Siku ile alikuwa na macho mekundu na yalitengeneza umande wa machozi ndani yake. Lakini siku hii macho yake yalikuwa meupe, na mboni  zilikuwa za kahawia iliyoiva. Chini na juu ya kope zake alipaka wanja.  Kope alizinakshi kwa rangi nyeusi na kuzifanya zisimame. Nyusi hakuziacha nyuma, alizisiriba kwa wanja mkali ambao ulizidi kumfanya aonekane mrembo mwenye mvuto wa kipekee.

“Okay…” alinitoa mawazoni kwa sauti yake. “naitwa Mwimbula,” alijitambulisha lakini hakuwa kamaliza, “sidhani kama unahitaji kujua ubini wangu na mengine ya ndani ya familia yetu.”

“Hapana. Jina pekee linatosha dada yangu,” nilimjibu kwa upole ili nisije kumpeperusha kiumbe huyu ambaye nilisota kumuweka karibu yangu.

Ilichukua mwezi mmoja hadi kukubali kukaa naye na kunipa historia ya maisha yake. Historia ambayo ilikuwa mateso kusimulika na kusikilizika pia.

“Sawa.” Alikubali.

Hiyo ndio siku ya kwanza kukaa naye na kuongea kwa kirefu. Siku ambayo ilibadili mwelekeo wa maisha yangu. Labda na wa kwake.

Kwa jina naitwa Sam; Samwel Timbe. Ni mwenyeji wa Iringa. Nilizaliwa na kukulia huko. Nikasomeshwa elimu ya msingi hadi chuo, huko huko. Ajira zilipotoka, kituo cha kazi kikawa Lindi.

Ajira yangu niliipata kwa shida hasa kwa sababu ya jinsia yangu. Kipaumbele cha pale nilipoomba, walikuwa wanataka wanawake kuliko wanaume. Naweza kusema nilibahatika kuipata.

Nilipata kazi kwenye shirika moja la kuhudumia Wanawake na Watoto. Nikafanya kazi hiyo kwa miaka miwili na ndipo nikaamua kutafuta changamoto mpya za maisha. Nikaomba kazi ustawi wa jamii. Nao walipendezwa na wasifu wangu, wakanipangia Mbeya. Safari yangu ilianzia hapo.

Miaka miwili ya kufanya kazi Mbeya, nilikutana na kesi nyingi za wakina mama. Kesi ambazo zilikuwa zinahusu unyanyasaji wa kijinsia toka kwa mwanaume kwenda kwa mwanamke. Mimi na wenzangu tuliyoajiriwa, tulipigana kufa na kupona ili kuzipatia ufumbuzi kesi hizo.

Baada ya mwaka wa mafanikio makubwa kupita, uliingia mwaka wa neema kwa baadhi ya wafanyakazi. Tulichaguliwa wafanyakazi watano pekee, mimi nikiwa mmojawapo. Tulitakiwa kufanya kitu ambacho kitavutia wengi hasa wale watakaokipitia.

Kwa ufupi, walitaka kitu hicho kiwe ndani ya kazi zetu za kila siku. Mwisho wa siku, ni mfanyakazi mmoja pekee ambaye angechukuliwa na Umoja wa Mataifa kwenda kuwa Balozi wao nchini Uswisi.

Tulipewa kila kitu kwenye kazi ambayo walitaka tuifanye kwa miezi sita. Nasema tena, tuligharamikiwa kila kitu. Kazi ikabaki kwetu.

Nina mpenzi pia. Nampenda na ananipenda; tunapendana. Anaitwa Siha. Yeye  alisomea mambo ya fedha na alibahatika kupata kazi kwenye benki fulani kubwa ya hapa Tanzania.

Siha; mpenzi wangu. Nilijuana naye kitambo sana. Kwanza alikuwa jirani yangu kule Iringa. Mama yangu na familia yake walijuana. Mara kwa mara walitembeleana kwa ajili ya kujuliana hali. Baba yangu pia alikuwa na urafiki na Baba wa Siha. Lakini hawakuwa wanatembeleana mara kwa mara kwa sababu ya safari za baba yangu.

Wakati mimi nina miaka nane, Siha alikuwa na miaka sita. Wazazi wangu na wake, walikuwa wanapenda kututania kuwa ni wachumba. Kuna muda tulinuna labda sababu ya utoto, ila haikuwa sababu ya wao kuacha huo utani.

Baada ya kumaliza shule ya msingi, tulianza kusoma katika shule tofauti. Mwenzangu alisoma shule ya bweni huko Mbeya, na mimi nikabaki Iringa kwenye shule ya kutwa. Lakini tulipofika chuoni, tukajikuta tupo pamoja na hapo ndipo mahusiano yetu yakaanza rasmi.

 

****

 

Siha ndiye alikuwa mtu wa kwanza kujua kile ambacho kilinitazama mbele yangu. Baada ya mambo ya hapa na pale kama wapenzi, nikamweleza kinagaubaga juu ya kile ambacho kitaenda kutokea kama nitafanikiwa kushinda.

Nilimwambia kama mpenzi wangu na pia nilitaka ushauri wake wa nini cha kufanya. Lakini baada ya kumaliza maelezo yangu, mwenzangu hakuwa na mawazo kama ambayo niliyafikiria. Sikuyaona macho yake kwa kuwa ilikuwa ni usiku na tena tulikuwa kitandani tumejipumzisha huku taa zimezimwa

Zikapita siku tatu bila kuongea na Siha. Alikuwa kanuna na hataki kuongea na mimi suala lolote. Sikudhani kama angefikia ile hatua pale nilipomwelezea yaliyojiri kwenye maisha yetu. Sikuyajua mawazo ya mwenzangu. Muda ukawa unakwenda na kazi nilipaswa kuianza haraka.

 “Kwa hiyo ukienda huko, mimi nitabaki na nani?” ni swali ambalo aliliuliza baada ya kutoa maelezo yangu kuhusu tuliyotumwa na Umoja wa Mataifa.

“Kwenda wapi jamani D?” nilimuuliza kwa uchungu hasa baada ya kugundua hakuwa akisikiliza yale niliyomwambia na badala yake alitengeneza uzio moyoni mwake. Uzio ambao uliunda wivu.

Nilipenda kumwita D, nikimaanisha Dear. Yeye alipenda kuniita Sam.

“Huko Ulaya. Unadhani mi’ sijui mambo ya Ulaya? Hao watakutafutia hadi mke ili mzae mtoto mwenye akili kama zako,” nikazidi kumshangaa.

“Lakini D,” nikakwama, “sikiliza Siha…” nilimuita jina lake halisi ili ajue sikuwa katika bembelezo wala masihara. “Hii ni kazi mama yangu…” licha ya kutoa masihara na bembelezo, ungeisikia hiyo mama yangu nilivyoitamka, hata angekuwa nani angelainika. “Haimaanishi kuwa nakwenda kula na kulala bure. Ni kazini kule. Ninachotaka ni baraka zako na kunipa ushauri.”

“Hakuna baraka wala ushauri Sam,” aliongea huku anageukia upande wa pili. Alinipa mgongo.

Nikavuta pumzi na kuishusha taratibu. Nikawaza na kuwazua ni nini nifanye. Sikuwa nimefunga naye ndoa, hata kwao sikutambulika. Wasifu wangu kazini ulikuwa ni single. Hata wake. Nitajiteteaje?

Nilipotaka kufungua mdomo wangu, nikajikuta nakwama. Siwezi weka neno lolote. Ilibidi na mimi nimpe mgongo. Ikawa hivyo hadi siku tatu. Ya nne tukawa tunasalimiana na kufanya hiki na kile pamoja, lakini Siha hakutaka habari za kazi yetu. Ilipita wiki bila yeye kunishauri lolote.

Sixbert,

Huyu alikuwa ni rafiki yangu nambari moja duniani. Rafiki ambaye kasuluhisha mengi kwenye mahusiano yetu. Mengine kwa kutukutanisha na mengine kwa kunielekeza cha kufanya. Huyu akawa kimbilio langu la mwisho kabla sijalikimbiza kwenye familia yangu. Nikamweleza kila kitu.

“AhBrother…” alianza kwa kulaumu huku pia akinogesha kwa tabasamu. Nilipoona hizo ishara, nikajua hilo si tatizo kubwa kwake.

Namjua.

Mara nyingi likiwa tatizo kubwa, huguna na kuinamisha kichwa chini. “bado hujaelewa hila za watoto wa kike?” aliniuliza na mimi nilionyesha ukinda wangu kwenye hizo nyanja. Sikutaka kujifanya mjuaji kila mahali licha ya kujua vichache ambavyo vilinisaidia kutunza penzi langu.

“Kaka…” nilimuita, “wiki sasa sijui hata nifanye nini. Natamani kuwaambia wale Wazungu waniondoe lakini roho inasita. Nisaidie kwa huyu Siha,” nakumbuka maneno haya yalinichomoka.

“Ila hata mimi nawashangaa ni vipi mnaweza kukaa pamoja bila hata kutambulika kwenye familia zenu?” aliniuliza.
Nilitulia kidogo nikitafakari maneno yake.

Nikakumbuka ni Siha huyu huyu ndiye aliyenitumia tangazo la watu kuhitajika kwenye ustawi wa jamii kila mkoa. Kipindi hicho yeye alikuwa anafanya kazi kama Muhasibu wa Mahakama Kuu ya Mkoa wa Iringa. Alitaka nitoke Lindi kwa sababu hali ya hewa ya kule, haikuendana na mwili wake. Ndipo nikaomba ile kazi na kubahatika kupangiwa Mbeya. Na yeye haraka akaomba kazi kwenye benki; akapata. Wote tukakutana Mbeya. Tukaanza kuishi kama mume na mke.

“Hapo anajua wazi kuwa utaenda na kuoa huko. Hata kama usipooa basi kukuona itakuwa mara tatu kwa mwaka. Mwanamke mwenye mapenzi ya kweli, hawezi kuvumilia hayo,” Six akaongea maneno ambayo hata mimi nilikuwa nayajua wazi.

“Sasa nifanyaje?” nilimuuliza.

“Muoe yeye…” aliniambia bila kupepesa.

Nikatulia kwa muda. “Kama utamuoa, halafu hiyo kazi mliyotumwa ukabahatika kushinda wewe, utakuwa na uwezo wa kuondoka na mkeo hadi huko utakapoitwa kufanya kazi,” safari hii nikakaa na kupunguza makunyanzi yaliyokuwa yameshiba usoni kwangu.

Nilimwelewa.

Aliendelea kunipa haya na yale hadi nikaiva. Na mimi baada ya kutoka hapo,  nikiwa na imani mpya, nilipitia pete kwa ajili ya Siha.

Furaha ikarudi tena baada ya mimi kwenda kutambulika kwao na kufanya kila kitu walichohitaji. Ila kwenye kufunga ndoa nikaomba kwanza nikamalize kazi ambayo ilikuwa inanitazama kwa sababu tayari ilikuwa mikononi mwangu na baadhi ya wenzangu walikuwa wamekwishaianza.

****

 

“Sam…” usiku mmoja Siha aliniita. Na mimi niligeuka na kumsikiliza nikiwa naye kitandani, “umepata cha kwenda kufanya?” aliniuliza na mimi nilimjibu hapana. Hapo ndipo akanipa habari za mwanadada anayepatikana Mkoa wa Mpanda.

Siha alipewa taarifa na rafiki yake kuhusu mwanadada fulani huko kwao Mpanda alipokwenda kujifungua. Alikutana na hadithi za mwanamke ambaye ndiye alijitambulisha mbele yangu kwa jina la Mwimbula.

Sikutaka kuchoma nauli yangu bila kujua ni hadithi gani ambayo alikuwa nayo huyo mwanamke. Nikamtaka Siha anikutanishe na huyo rafiki yake. Naye hakuwa na hiana. Siku mbili mbele, nilikutana na rafiki wa mpenzi wangu.

“Shem hata kuja kumwangalia mtoto…” nilijikuna kichwa kwa kauli hiyo na kujikuta nacheka kama zezeta. Nilikosa jibu.

Sikuwa na urafiki naye wa karibu na sikumjua hata kidogo. Lakini ni kama alinilaumu kwa kutokwenda kumuona mtoto wake.

“Ni huyu mke wangu bwana. Hata hajawahi kuniambia tuje kwako…” nilijitetea na hapo nikamuona anacheka kidogo na kusikitika.

Rafiki wa mke wangu anasali Kanisa la Mashahidi wa Yehova. Watu hawa nawaogopa sana kwenye kuchambua Neno la MUNGU. Wana vifungu vingi vya Biblia. Ni ngumu kupambana nao kimaandiko kama hujawahi hata kuangalia filamu za dini.

“Usisikitike Shem. Huu ndio mwanzo wa kujuana. Wikiendi hii nitakuja kumuona Kamanda wetu,” nilijiongelesha.

“Sisikitiki kwa kuwa mkeo hajakuambia, ila nasikitika kwa jibu ambalo umenipa,” nilitulia.Niliomba MUNGU Siha aje haraka maana alikwenda kuchukua bili  baada kujipatia chakula kwenye mgahawa mmoja uliopo karibu na benki wanayofanyia kazi. Waliupenda mgahawa huo kwa sababu ya mazingira pamoja na chakula cha nadra wanachokipika. Hata mimi nilitokea kupapenda.

“…jibu lako ni kama jibu la wanaume wote waliowahi kuishi kwenye hii dunia. Na tena jibu hilo mmerithishwa na baba yenu,” aliendelea huku ananitazama machoni.

“Sasa baba gani huyo. Shem bwana,” niliuliza na kujichekesha kibwege.

“Baba yenu Adam,” alijibu, “baada ya kula tunda la kujua mema na mabaya, wakajikuta wapo uchi. Ile MUNGU anakuja kuwaona, baba yenu badala ya kumuitikia MUNGU, yeye akasema ni huyu mwanamke,” nikawa namtazama Shemeji yangu huku nikijuta kumsingizia Siha. “MUNGU akamuuliza, kwani kafanyaje? Baba yenu akajibu kama wewe hivyo.”

“Kwani ni baba yangu peke yangu au hata wewe?” nilimuuliza huku nikijifanya kupamba tabasamu kuonyesha kuwa nafurahia yale maongezi. Ila moyoni nilitamani kumwambia, ebu acha ujinga, niambie kuhusu huyo mwanamke uliyemsikia huko kwenu.

“Baba yenu nyie. Umesikia sisi tumebebeshwa majukumu yenu?” sikutaka kuendelea kubishana naye kwa sababu angeanza kumwaga maandiko mengine wakati mimi sikuenda pale kupewa maandiko.

“Haya bwana. Samahani kama nimekosea. Ila nakuahidi, nitakuja wikiendi hii.” Akawa hana ujanja tena.

Akavuta maji yake yaliyokuwa kwenye kopo la lita moja na nusu. Akayamimina kwenye bilauri ya kioo na kuyagida.

“Mke wangu aliniambia kuna mtu huko kijijini kwenu ana matatizo sana na ana historia ya kugusa mioyo ya watu,” nilitupa karata ya kwanza baada ya kumaliza mchezo wa kutomuona mtoto na habari za Adam na Eva.

Yeah. Kweli Shem. Nilisikia juujuu historia ya huyo dada. Mama alikuwa ananihadithia habari zake. Zilikuwa za kusikitisha sana. Na mimi kwa kuwa nilikwenda kujifungua, sikutaka kuzifuatilia sana maana zilikuwa kama mateso kwenye moyo wangu,” aliongea na kunifanya nivutike na kutaka kujua zaidi.

“Unadhani historia yake inaweza kukamata mioyo ya watu?” nilimuuliza.

“Yawezekana roho yangu ya Kilokole ndio imenisukuma kusema haya. Lakini naamini hata uwe na roho ya namna gani, huwezi kuacha kusononeka,” alinijibu na kuendelea kunifanya nitamani kuifanya hiyo kazi.

Kweli. Niliingia kazini kwa ajili ya kutafuta kitu cha kuwavutia wale waliotuchagua. Na nilipofuatilia wenzangu, nao walikuwa wameanza kuifanya kazi tuliyotumwa. Niliingia kazini baada ya wiki mbili na nusu za kujiandaa. Ukijumlisha na mwezi mzima niliotumia kumrudisha Siha na kumvisha pete, mwezi na nusu ulikatika.

Nilipokwenda huko, napo nikapata mwezi mmoja wa kumfuatilia huyo dada ili anihadithie historia yake.

“Nilibahatika kupitia unyago. Nilifundwa mambo kadha wa kadha kuhusu mila na desturi zetu,” aliendelea kunihadithia taratibu huku redio ndogo iwezayo kunakili ikiwa mezani ikimeza sauti yake. “Familia yetu haikuwa masikini. Na haijawahi kuwa masikini. Lakini ni familia ambayo ilikataa kusahau tamaduni na mila zao licha ya baba na mama kuwa wasomi,” akameza mate, “…nilipovunja ungo, mama yangu alichukua likizo fupi na kunileta kwa bibi yangu. Huko niliwekwa ndani na kupigwa msasa wa maana kuhusu maisha ya kidunia na mambo ya kike.”

“Ulipenda kuwekwa ndani?” nikamuuliza kabla ya kuendelea.

“Ndio. Nilipenda. Lakini sikujua kama yale mafunzo yangekuwa silaha ya mimi kuteseka na kuhangaika namna hii,” akafunua sehemu ya mkono wake.

Nikasisimka.

“Ni nini hii?” nikamuuliza huku nikitaka kushika mkono wake. Akarudisha haraka na kuufunika kwa vazi lake la kitenge.

“Unajua…” akanitazama usoni. Nami niliyatazama macho yake. Alitamani kulia. Niliona. “…licha ya tamaduni zetu kugeuka silaha, lakini najihisi bado natamani kuzifuata. Si rahisi kwa mimi kukubali kushikwa mwili wangu na mwanaume mwingine ambaye simjui.”

“Lakini sijataka kukushika kwa matamanio,” nikajitetea.

“Najuaje?” akaniuliza. Na hakutaka nimjibu, “…au unajuaje kama sitakutamani baada ya kunishika?” nikabaki kimya. “…ndivyo nilivyofunzwa,” akaongeza, “kwani kuniuliza bila kunishika ungekuwa hujaniuliza?”

“Yaishe dada. Sikujua. Ila umenipa somo lingine,” nikamtaka radhi. Akaonyesha kukubaliana na mimi.

“Nini kilikutokea?” nikamuuliza kuhusu kile nilichokiona kwenye mkono wake.

“Unajua…” nilijikuta naanza kupenda jinsi anavyotaka kuanza kusimulia. Mara tatu au nne alikuwa anaanza na neno unajua.

Alikuwa na sauti nzito kiasi, halafu kwa mbali imekauka. Kama ningepata nafasi ya kumchagulia kufanya kazi, basi ningemshauri aende kwenye vituo vya matangazo kama redioni au kwenye luninga. Tena angependeza kwenye kusimulia makala.

“…mimi ni mwanamke. Si mwanamke kwa sababu ya viungo vyangu ama mwonekano na mavazi yangu. Mimi ni mwanamke kwa sababu nina mtoto na nina mume. Nawatazama bila kuchoka. Huwezi kuniweka kwenye kundi la wakinadada au wanawake wengine ambao hawayajui haya majukumu. Hicho ndicho kimeniponza. Kujifanya mwanamke.”

Nini kimekutokea Mwimbula? Mbona unaiweka roho yangu juu? Nikajikuta nawaza na kutamani kujua nini sababu ya mkono wake kuwa na kidonda kikubwa namna ile. Kidonda ambacho ni wazi kilikosa tiba, kikawa kinajiponea chenyewe.

Kilianzia sehemu ambayo saa hukaa hadi kwenye kiwiko. Ni kama mtu alichukua kisu na kuikwangua ngozi ya sehemu hiyo. Palikuwa pekundu na palitisha.

“…hawahawa ambao tunawaita mawifi. Wanaocheza kwa mbwembwe kwenye harusi za kaka zao, ndio wamenipa hichi kidonda,” akaongea,“sasa ni heri ingekuwa bahati mbaya kaka yangu…” sauti yake ikaanza kubadilika na kuwa yenye mchanganyiko wa kilio. “…heri ingekuwa bahati mbaya…  Lakini walifanya makusudi kabisa. Walifanya kwa kudhamiria,” akaanza kulia.

Nilitamani nisimame na kwenda pale alipokaa na kumpooza.  Nikakumbuka maneno yake pale nilipotaka kuushika mkono wake. Nikanywea na kubaki namtazama.

“Pole dada,” maumivu yaliukamata moyo wangu na kuuchanachana kwa simanzi. Moyo ukachubuka kwa maumivu ya Mwimbula.

Tamaa ya kutaka kuujua ukweli, nilihisi imetonesha jeraha la huyu mwanamke. Taratibu nilianza kujilaumu na kujiona mkosaji. Labda machozi yalishaanza kuondoka maishani mwake, mimi na ufukuzi wangu nayarudisha. Nikavuta kile kinasa sauti na kutaka kukizima.

“Usizime,” akanikanya huku anajipangusa, “utazima nikimaliza,” akaongeza huku akinitazama kwa macho yake yenye unyevu wa machozi. Kamasi nyepesi nazo hazikuwa na aibu, zikamtoka na kudondokea kifuani; juu ya vazi lake la kitenge. Nikawahi haraka kumpatia kitambaa changu ambacho sikuwa nimekutumia.

“Ahsante,” Akashukuru na kujifuta. “Watu watatu; wale ninaowaheshimu…” akaendelea baada ya kukaa sawa. “…ninaowaheshimu na ambao hata bibi alinielekeza kuwa niwaheshimu hao kuliko hata wazazi wangu. Walinikamata na kuchukua mafuta niliyokaangia samaki, wakanimwagia mkononi,” nilimeza funda moja la mate na kujikuta najiuliza maswali lukuki.

“Ngoja kwanza…” niliongea kwa pupa, “ngoja dada yangu…” japo alikuwa kweli ananingoja, ila bado nikamsihi asiendelee kusimulia. Nilikuwa na kihoro. “Yaani mafuta ya kukaangia samaki, wakakumwagia…” nikakwama kidogo, “wewe?” nilimuuliza huku nimemnyooshea kidole.

“Nayaona maumivu yako kaka. Lakini huo ndio ukweli,” alijibu kinyonge.

“Kumbe haya mambo yapo?” nikajiuliza kwa sauti ya chini.

Nimefanya kazi ustawi wa jamii. Kesi nyingi nilizokumbana nazo ni za madai ya wakina mama kutaka matumizi ya watoto toka kwa wanaume waliowazalisha. Kesi zingine ni za kudai kugawana mali za mwanaume na nyingine za madai kama hayo. Lakini hili la Mwimbula, mbona ni zito? Na wangapi hawaji kushtaki mambo kama haya?

“Yapo. Na mimi ndio mfano wake…” alinitoa katika mawazo. “…nachoshukuru walishindwa kunimwagia hadi kwenye kiganja cha mkono kwa sababu wifi mwingine alikuwa kakamata sehemu hiyo. Hivyo mmwagiaji aliona atammwagia na dada yake. Wakaishia hapa…” akaonyesha tena mkono wake, “yalikuwa ni mafuta ambayo bado yanachemka kwenye jiko la gesi. Walichofanya ni kuyachota kwa kijiko kikubwa chamboga na kuanza kunimwagia,” akaongeza.

Mkono wake ulitisha hata kwa kuutazama. Ni wazi kidonda kilikosa huduma. Kilivimba na kupasuka chenyewe. Kisha ngozi yake ilibanduka na kilichoonekana ni hiyo nyama nyekundu. Nilimtazama kwa makini machoni wakati bado kafunua nguo yake sehemu ya mkononi.

Nikavuta kamasi ndani. Nilihisi machozi yanataka kutoka. “Twende hospitali,” nilizima kinasa sauti na kusimama. Sikutaka mjadala wowote juu ya maamuzi niliyoyaamua. Licha ya kwamba nilikuja kuchukua historia, pia nilikuja kama binadamu mwenye utu.

“Kaka siwezi kwenda hospitali,” aliniambia huku akianza kuomboleza.

“Kwa nini?” nilimuuliza kwa sauti iliyojaa ukali kwa mbali.

“Wakijua kuwa nimeenda hospitali watanipa kidonda kingine halafu mume wangu atateseka,” alinijibu.

Nikakaa kwenye kiti; Kiti cha Ofisi ya Mtendaji wa Kata.

“Mumeo yupo?” nikamuuliza. Akajibu kwa kichwa kukubali. “Anakutetea?”

“Yupo kitandani…” akaanza kulia kwa uchungu. Alilia kwa sauti ya kwikwi. “Mu.. me… waa…nguu,” alilia kwa sauti na kunifanya hata mimi kuumia. Nikatulia na kumwacha aendelee kuitoa nyongo ya maumivu kwa kutumia kilio.

Nikakumbuka maneno ya Shemeji; Rafiki wa Siha. “Kuna watu wana matatizo Shem. Tena wakitembea mtaani hutoyaona hadi wakae na kukuhadithia ama uone mwenyewe wanavyoteseka,” ni maneno ya Mama Daddy. Alimpa mtoto wake jina la Daddy.

Hakuishia kunieleza hayo pekee, “Mama anasema huyo dada huku mgongoni ana alama za kuchanjwa kama si kwa kisu, basi ni wembe. Halafu anayemfanyia hayo sasa…” sauti ya Mama Daddy bado iliendelea kujiri kichwani mwangu. “Ni mume wake. Mume ambaye nasikia alimtoa mbali balaa,” maneno ya Mama Daddy na kilio cha Mwimbula, vilinipa mshangao.

Nini kimekutokea Mwimbula? nilijiuliza moyoni wakati mwenyewe akiwa anaendelea kulia kwa sauti ya chini. Mumeo kakuchanja hovyo mwilini. Ila kwa sasa unalia ukisema mumeo anateseka. Nini kimetokea? macho yangu yalimtazama Mwimbula, lakini kichwa kilijaa mawazo mengine ya mbali kabisa.  Hata alipomaliza kulia na kuniongelesha, sikusikia.

“Kaka…” aliniita na ndipo nikashtuka na kuminya macho kidogo. Machozi yakanitoka. Nikawahi kuyafuta haraka. Inawezekana ni machozi ya uchungu ama machozi yaliyotokana na kumtazama Mwimbula muda mrefu bila kufumba macho. “Sijui umenisikia?” akaniuliza kwa upole.

“Sijasikia. Umesemaje dada?” nikamuuliza baada ya kukaa sawa kitini na kiakili.

“Naomba nikuhadithie. Haya mengine unayoyataka, sidhani kama ni nafasi yake,” akaniambia.

“Sikiliza dada. Naomba usikilize nachokwambia…” akamakinika, “sijaja kama mnyama au mdudu. Nimekuja kama binadamu mwenye roho yenye kila sababu ya kuitwa utu. Nitakuwa wa ajabu kukuacha uendelee kuumia kwa maumivu ya hicho kidonda. Yaani muda wote nitakaokaa na wewe, niwe navumilia kuona hicho kidonda? Aisee nitakuwa chizi mimi,” niliona macho yake yalivyokuwa na mengi ya kuniambia. Lakini sikuwa na uhitaji wa kuyajua, nilichohitaji ni yeye kutibiwa kwanza. Mengine yangefuata.

Akapumua pumzi moja ndefu. Akakaa mkao wa kufikiri jambo. “Utatibu madonda mangapi?” akaniuliza, “huu si mwanzo wala mwisho wa mimi kuumia. Nikiumia tena au kupata vidonda, nani atanitibu?”

“Haijalishi dada. Kwa kuwa tayari nipo hapa na ninaona vidonda vyako, sina sababu ya kutovifanyia mpango wa matibabu,” nikamwambia. Niliona ahueni machoni kwake. “Naomba twende hospitali.” Tulinyanyuka na kutoka nje.

Nilipewa gari la ustawi wa jamii kwa Mkoa wa Mpanda kwa ajili shughuli zangu. Kazi yangu ilikuwa ni kujaza mafuta na kufanya safari nizitakazo. Tukapanda na kwenda hospitali ya Wilaya.

“Naomba baada ya kutoka hospitali nirudi kwanza nyumbani,” aliniambia na sikuwa na pingamizi kwa sababu tayari muda ulikuwa umekimbia na tena aliniambia kuwa ana mtoto na mumewe ni mgonjwa.

Hospitali alishughulikiwa ipasavyo. Akaoshwa kidonda na kupewa dawa za kukikausha. Akafungwa bendeji na kupewa kalenda ya kwenda kuoshwa. Tukatoka hapo.

Safari iliyofuata ilikuwa ni kwenda sokoni na kununua hiki na kile kwa ajili ya nyumbani. Nilijitahidi kumnunulia vitu vya muhimu ambavyo vitamsukuma kwa muda mrefu. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kushukuru. Ilifika muda nikaboreka na shukrani zake. Sikupenda anavyonishukuru.

“Unajua…” alianza tena wakati tunaanza kuondoka sokoni. Tulikuwa tayari ndani ya gari. “Kuna muda unaweza kuona kila kiumbe kilichokuwa mbele yako ni Shetani. Unaweza kuchukia hata Malaika. Ule ung’avu wake, kwako ukaona kama rangi nyeusi ikerayo na kutisha,” aliongea lakini sikujua maana yake. Akaendelea, “hata huyu mume wangu ambaye sasa yupo kitandani hajiwezi, alikuwa kama Malaika. Aling’aa usoni kwangu. Sikuwahi kuwaza kama atageuka na kuwa Shetani. Sitaki kuingia kwenye ule mtego tena.”

“Una maana gani?” nilimuuliza kwa utulivu huku safari ya kumpeleka kwake ikiwa imechukua nafasi.

Akanitazama usoni. Mimi sikumwangalia. Nilikuwa naendesha gari.

“Nahisi nimekutana tena na Malaika. Kwa jina la….” akawa kwenye hali ya kutaka kukumbuka jina langu, “sijui waitwa nani?” nilihisi kisu kikali kikichana moyo wangu.

Ina maana na mimi ananiona kama Malaika mng’aavu halafu badaye nitakuwa Shetani ama ananiona Shetani moja kwa moja? nilijiuliza kichwani na wakati huo huo nikamjibu. “Naitwa Sam.”

“… nimekutana na Malaika kwa jina la Sam. Ambaye ananisaidia kwa kila hali. Lakini najua baadaye naye nahisi atageuka na kuwa Shetani. Just like others did,” nikatulia kwa muda.

“Just like others did…” kauli hiyo ikanipa swali ambalo sikujua jibu lake ni lipi.  Wakina nani? Kwa nini? nikajiuliza.

Nikamtazama Mwimbula. Alikuwa kaegamia kioo cha gari na macho yake yalikuwa yanatazama nje. Sikujua kama ni kweli yalikuwa nje ama alikuwa anawaza. Mara nyingi hata mimi nikiwa na mawazo ndani ya gari, huwa naegamia kioo namna ile. Mwisho wake huwa napitiwa na usingizi.

“Unaweza kuchukulia wanaume wote kama Shetani.Ni halali yako hasa kwa yaliyokukuta. Lakini nashukuru umenipa nafasi mimi. Unaweza kuniona kama Shetani au vyovyote, lakini mwisho wa haya, ndio utatoa majibu. Uniite Shetani ama Malaika. Zote ni sifa, japo moja ni sifa chafu na nyingine ya kuvutia,” nilimwambia. Nikasikia anacheka kicheko kidogo.

“As usual,” akaweka kauli hiyo ya Kiingereza. Nikamshangaa.

“Una maana gani?” nikamuuliza.

“Nasema ni kawaida ya wanaume wote. Mna kauli zinazofanana…” nikaanza kucheka. Nikacheka kwa muda. “Unaona? Hata wewe unakubaliana na mimi.”

“Hapana…” nilimkatalia, “umenikumbusha shemeji yangu mmoja. Ni rafiki wa mke wangu…” nikaona kainuka ghafla na kunitazama.

“Umeoa?” akaniuliza kwa hamaki.

“Sijaoa. Ila nimemchumbia mpenzi wangu juzi tu! Kabla sijaja huku,” nikamjibu.

“He!” nikaona tabasamu lake. Nilimtazama mara moja na kuhamishia macho yangu barabarani.

Mwimbula alikuwa mzuri.

Lile tabasamu naweza kulipa namba mbili kwa uzuri. Au labda si la pili. Kama Siha asingekuwepo maishani mwangu; lile tabasamu lingekuwa la pili. Ila nalipa namba tatu. La kwanza ni la mama yangu, la pili la Siha na la tatu ndilo hili nililoliona kwa Mwimbula.

“Basi nilitaka kukusema hovyo jamani. Unisamehe mimi,” nilimsikia Mwimbula akiomba msamaha.

“It’s okay. You have to.”

“No. It’s not okay. Am wrong.”

“No one is perfect in this life. Hakuna aliye sawa dada,” nikamtoa wasiwasi.

“Unajua…” Dah! Angejua jinsi anavyoniua wakati anavyoanza kwa hiyo kauli. Ananifanya nitake kumsikiliza kila mara. “…hata kama hakuna aliyekamilika kwenye hii dunia, lakini kuna idara atakuwa kakamilika. Mimi pia sijakamilika Sam; Sikatai. Lakini kuonyesha kuwa sijakamilika, yapaswa niombe msamaha. Msamaha pekee ndio unaonyesha kutokamilika kwa binadamu. Hakuna msamaha kwa mtu ambaye anajiona kakamilika,” aliniambia lakini maelezo yake yalikuwa magumu kuyaelewa. Labda kwa sababu akili nyingine ilikuwa kwenye kuendesha gari.

“Una maana gani?”

“Mtu ambaye anajiona kakamilika kwa kila kitu, huwa haombi msamaha kwa kuwa anajua kuwa kafanya kilicho sahihi,” hapo nikamwelewa. “Najijua kuwa sijakamilika na ndio maana nikaropoka bila kujua. Na nimejigundua kuwa nimeropoka, nimekuomba msamaha. Only sorry can define someone isn’t perfect,” akamaliza kwa lugha ya ughaibuni.

“I forgive you,” nikamwambia ili kuepuka kuombwa msamaha bila sababu za msingi toka kwake. Sikutaka awe ananiomba msamaha ama kunishukuru kila nukta. Sikupenda hiyo tabia.

“Thanks…” moyo wangu ukachubuka kwa ahsante yake. Nilitamani kumwambia asiwe anashukuru. Ila nikanyamaza.

“Ehee! Shemeji yako alikwambia nini?” akanirudisha nyuma. Nikamtazama tena na kugundua kuwa alikuwa yupo kwenye hali ambayo labda aliikosa kwa muda mrefu kwenye maisha yake. Waingereza wanasema ‘she is comfortable and happier’. Yaani hali ya moyo kutulia na furaha.

“Aliniambia wanaume tumerithi tabia za baba yetu,” nikamjibu na kucheka kidogo. Nikakumbuka siku zilizopita nikiwa na mama Daddy baada ya kumsingizia Siha kuwa hakunipeleka kumtazama mwanaye.

“Baba yenu ni nani?” Mwimbula akauliza.

“Adam…” nikamjibu na kucheka tena, “unajua Adam baada ya kula tunda la mti wa kati akajigundua kuwa hakuwa sawa. Yeye na Eva. MUNGU alipowatembelea na kumuita jina lake, cha kwanza Adam kujibu,  alisema ni huyu mwanamke. Badala ya kuitika, yeye akatupa lawama. MUNGU akamuuliza kafanyaje? Jamaa akajibu kanidanganya nikala tunda…” nikaanza kucheka kwa ile hadithi. “Sasa hiyo tabia, Shemeji yangu anasema kila mwanaume anayo. Na wewe umeongea suala lilelile kwamba wanaume wote tuna kauli zilizo sawa,” Mwimbula naye akacheka.

“Yawezekana…” akaongeza, “naishi nyumba inayofuata,” akanielekeza na mimi nikanyoosha hadi kwenye hiyo nyumba.

Haikuwa nyumba haba. Ilipendeza na ilikuwa yenye mwonekano wa kuishi mtu ambaye hana shida. Swali likawa linaelea kichwani. Iweje Mwimbula alalamike namna ile hadi hatua ya kumwaga machozi? Wakati nawaza hayo, nikakumbuka alinihadithia kuhusu wifi zake. Mwili ukasisimka na kutaka hata kuondoka, nirudi kazini nikamshughulikie Mwimbula na hao wifi zake watokomezwe.

“Wifi zako wapo?” nikamuuliza wakati anataka kushuka.

“Hawapo. Huwa wanakuja mara mojamoja na wakija ujue siku hiyo ni taabu tupu,” akaniambia kwa upole.

Ahueni ikaja. Nikasaidiana naye kushusha baadhi ya mizigo. Geti lake likafunguliwa, akatoka kijana mmoja ambaye alinisalimu na kuanza kuingiza mizigo ndani. Mimi sikutaka kuingia. Nikabaki naweka mizigo pale getini na wao wanaingiza ndani.

“Huyo ni mtoto wangu. Ndiye anamsaidia baba yake kwa kila kitu. Hakuna anayemgusa mume wangu zaidi ya huyu na mimi. Hata wadogo zake ambao yeye ndiye aliwatoa kimaisha, hawajawahi kumgusa. Wakija hapa wanakaa dakika mbili na kuondoka. Utawaona tena baada ya miezi mitatu.”

“Kwani mumeo ana shida gani?” ikabidi nimuulize.

Akanitazama kwa muda usoni. Uso wake ulisawajika kwa lile swali. Akasikitika na kuangalia chini.

“Ana virusi vya UKIMWI,” nikakumbwa na taharuki ya ghafla. Sikujua hata nataka kuongea nini. Lakini nilifadhaika kwa mfadhaiko ulioonekana wazi.

“Naona maswali yalivyokujaa kaka yangu. Lakini usijali, kwa kuwa leo ndio mwanzo, basi nina imani hautokuwa mwisho wetu. Nitakueleza kila unachotaka kukijua,” aliniambia baada ya muda kidogo wa mimi kutulia.

Nikamtazama usoni kwa umakini huku nikiwa sijui nataka kusema nini. Ila akilini picha kadhaa za Mwimbula ziliendelea kuzagaa. Sikuelewa ni picha za nini lakini zilijijenga na kuniumiza moyo. Akatazama pembeni kwa aibu za kike.

Nikajishtukia. Nilikuwa namwangalia hadi akahisi mengine.

“Kesho nije kukuchukua ama utakuja mwenyewe pale ofisini?” nikamuuliza baada ya hitilafu za hapa na pale za kifikra.

“Nitakuja mwenyewe. Siyo mbali sana pale,” akanijibu na mimi kwa haraka nikatoa pochi yangu na kumpatia kiasi kidogo cha fedha.

Akanitazama usoni mara moja bila kuzichukua. Nikaelewa nia yake; kuzikataa.

“Sikuhongi na wewe,” nikaongea kwa utani huku natabasamu. Naye akatabasamu zaidi na meno yake yakaonekana. Akazichukua zile hela na kunishukuru.

Nikaingia garini tayari kwa kuondoka. Yeye alibaki anarudishia geti. Baada ya kumaliza, alifungua mlango mdogo wa geti na kunipungia mkono. Nami nikafanya vivyo hivyo. Nikaondoka eneo lile huku moyo wangu ukiwa na amani.

Akili yangu ikawa inawaza kusikiliza tena kazi nzima ambayo tuliifanya na Mwimbula. Na kama itawezekana, basi nianze kuiandika.

 

****

 

Nilifika ninapoishi muda wa jioni.  Ilinibidi nipite tena sokoni na kununua mahitaji haya na yale kwa ajili ya kupeleka pale napoishi. Nilipokelewa na mama aliyenipa chumba kwa ajili ya kuishi. Huyu ni mama mzazi wa mama Daddy; Shemeji yangu.

Wakati nakwenda Mpanda, alinipa mawasiliano ya mama yake ili nikifika huko iwe rahisi kwangu kumpata Mwimbula. Yule mama alinipokea vema.

Kulikuwa na chumba cha nje ambacho hakikuwa na watu. Akanipa niwe nalala huko. Japo nilimkatalia, lakini hakunielewa. Hakutaka niende kupangisha nyumba za wageni angali kwake kuna chumba na ndani yake kuna kila kitu.

Baada ya kushusha mazaga niliyowanunulia pale nyumbani, nilifunga gari na kuingia chumbani kwangu nikiwa na mkoba wa kuweka kompyuta na vifaa vingine vidogo kama kile cha kinasa sauti, kalamu na daftari dogo la kutunzia kumbukumbu.

Nikatupia mkoba wangu kitandani, kisha na mimi nikajitupia pembeni yake. Nikawa nimelala chali; natazama paa. Mawazo yangu yakahama na kuanza kufikiria hili na lile kuhusu maisha. Nikalikumbuka tabasamu la Mwimbula kwenye gari pale nilipomwambia kuwa nina mke. Nikakumbuka na pale nilipompa fedha na utani ndani yake. Nikakumbuka alivyoniaga. Nikajikuta natabasamu na kucheka kicheko kidogo kilichopaa hadi nje.

“Mwanangu kazi imeendaje?” nilisikia sauti ya mama aliyenipokea ikiniuliza. Nikasimama na kwenda mlangoni.

“Imeenda salama. Nashukuru MUNGU,” nilimjibu kinyenyekevu.

“Naona tu! Maana umecheka hadi huku nje nimesikia…” Nikajikuta natabasamu na aibu fulani ikinichukua. “…jitahidi umalize naye salama tu!” aliongea huku anaondoka.

Nilielewa maana yake. Na mimi nikajikanya moyoni. Nikamkumbuka na Siha wangu. Nikarudi ndani na kuchukua simu yangu; nikampigia.

 

 

 “Saa tatu asubuhi, nilikuwa nimekwishajiandaa na kuvaa vema mavazi yangu. Sikuhitaji kioo kujitazama nilivyovaa lakini niliamini kuwa nipo sawa. Nikaweka vema nywele zangu na kukusanya vitu ambavyo nilivitoa kwenye mkoba wangu, ikiwemo kompyuta na kinasa sauti. Nikaviweka ndani ya mkoba na kutoka nje huku nikifunga mlango. Nilimuaga mama mwenye nyumba aliyekuwa anatwanga ulezi. Nikaingia garini na kuanza kuelekea kwenye ofisi  niliyokuwa nimeomba kwa ajili ya kufanya mahojiano na Mwimbula; Kwa Mtendaji.

Niliingia ofisini kwa madaha na kusalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa serikalini. Sikuwa na maongezi mengi, nilinyoosha hadi kwenye ofisi niliyopewa. Nikafungua taratibu na kuingia. Macho yangu yakagongana na Mwimbula.

Surprise…” aliongea huku akichanua tabasamu.

Nikamrudishia tabasamu huku nafunga mlango.

“Umefika saa ngapi?” nilimuuliza huku nakwenda upande wa pili wa meza ambapo ndipo kulikuwa na kiti changu. Nikavua mkoba wangu na kuuweka juu ya meza.

“Si muda mrefu sana. It’s like…”akaangalia saa ya ukutani, “… saa mbili au tatu kamili,” akanijibu na mimi nikaangalia saa yangu. Ilikuwa ni saa tatu na dakika arobaini na mbili.

“Umewahi mwenyewe…” nikamtania. Sikumpa nafasi ya kurudisha utani, “umekunywa chai?” nikamuuliza.

“Huwa sipendelei chai asubuhi.”

“Unapenda ugali sio?” nikamtania huku nasimama kwenda mlangoni.

“Acha utani basi,” akaongea huku anacheka.

Tayari nilikuwa nimefungua mlango na kumuita dada mmoja ambaye alijulikana pale ofisini kama msaidizi.

“Naomba utuletee uji wa ulezi kwenye chupa na maziwa fresh,” niliongea huku nampatia noti moja ya elfu kumi.

Akataka kuondoka ,nikakumbuka kitu,“dada…” nilimwita, “utaleta na chapati za maji kama za juzi pamoja na mayai ya kukaanga,” nikamwelekeza na mwanadada akakubaliana nami; akaondoka.

Nilirudi kwenye kiti changu na kukaa. Mwimbula alikuwa kimya na mimi sikutaka kumghasi wakati huo. Nilitoa kompyuta yangu pamoja na kifaa chake cha kuingizia umeme. Nikaviunga na kupachika kwenye swichi ya ukutani. Nikawasha na kuisogeza pembeni. Nikatoa kinasa sauti na daftari langu. Mwimbula bado alikuwa kimya.

“Mbona kimya?” hatimaye nikamuuliza.

Akaniangalia usoni. Na mimi niliendelea kumwangalia.

“Kuna muda huwa najiuliza kama nikiamua kuwaua walionifanyia unyama, nitaua wangapi?” nikashangaa swali lake.

Nikajiuliza zaidi baada ya kugundua kimya chake alikuwa anawaza mauaji.

“Kwa nini unawaza hayo?” nikamuuliza.

“Sasa kama mtu anakuua kwa upanga, kwa nini we’ ulemae?” nikatabasamu kidogo.

“Unasahau kuwa mtu akikunyang’anya shati, mpatie na suruali?”

“Na wewe unasahau kuwa haki ya mtu haidhulumiwi?” kimya kikatanda kwa sekunde kadhaa, “au hujui?” akaondoa ukimya. “Hujui kuwa unatetea haki za watu kama sisi? Umewahi kuwaambia wakinyang’anywa mashati wawape hadi suruali zao?”

“Sawa. Lakini suala la kuua limetoka wapi?” kimya kingine kikaikumba ofisi yangu.

“Unajua…” akaanza.

Nikashusha pumzi huku moyo wangu ukienda kwa kasi. Sikujua sababu ya moyo kuwa vile. Lakini alivyoanza tu! Nikajua kuna kitu muhimu anataka kukiongea. Nikawahi kuwasha kinasa sauti nilichokuja nacho.

“Watu wamebarikiwa mioyo ya kikatili pamoja na usahaulifu. Watu wanasahau ni wapi wametoka na wapi ulipita nao. Wanakuja kukusaliti kipumbavu sana. Kuna muda nilitamani kugeuka hata kuwa Iddi Amin au Hilter. Msaliti nimuondoe duniani…”

“Lakini hukufanya hivyo…” nikamuwahi.

“Sikufanya hivyo, ndio.”

“Unajua ni kwa nini hukufanya?”

“Labda kutokana na mafunzo ambayo nilipewa kabla sijaingia kwenye ndoa.”

“Hapana. Si mafunzo pekee bali wewe si muuaji, hata kama utajivisha vazi la kiuaji…” nikamwambia na yeye akawa katulia asijue aseme nini.

Ikawa nafasi yangu ya kujitanua kimaongezi, “kuna uso unaweza ukawa nao, lakini haukutafsiri wewe ni nani bali kilicho ndani yako ndicho kinakuelezea sifa zako…” nikatulia nukta chache nikiwaza mfano wa kutoa.

Nikaupata.

“Hata chura, kwenye kuzaliwa kwake. Huzaliwa ndani ya maji kwa kutotolewa akiwa na uso kama wa samaki. Na ukimtoa ndani ya maji. Hufa. Lakini kuna daraja akifika, anatoka ndani ya maji na kuja nchi kavu. Na kutembea kwake huwa kwa kurukaruka sababu ndivyo alivyoumbwa. Pia akiamua, anarudi tena majini. Na huko hutembea kwa kuogelea.”

“Unataka kumaanisha nini?”

“Hapa na maana kwamba, unaweza kuishi maisha ya aina moja kwa muda fulani lakini huwezi kuishi hivyo daima. Utaingia kwenye shida na kwenye raha pia. Sasa kama kwenye raha unakuwa na mawazo mazuri, kwa nini ukiingia kwenye shida ufikie hatua ya uovu? Pambana kama chura. Akitoka ndani ya maji, atatumia njia ya kuruka ili afike mahali fulani. Na akiingia kwenye maji, huongelea…” nikamshauri kwa utulivu, “upo kwenye shida. Toka kwenye hizo shida. Tena anza kwa kuondoa mawazo maovu.”

“Mgh!” akaguna.

“Umewahi kuona sehemu ambayo kipepeo anawekwa na mamaye kabla hajazaliwa?”

“Ndio….” akajibu haraka, “huwa anaitwa katapila au lava kama sikosei,” akaongeza.

“Mwonekano wake upoje?” nikamuuliza.

“Kama mnyoo mweusi…”alijibu, “au funza… Ehee! Kama funza wale wa Dar ambao mvua ikinyesha wanatokea.”

“Wabayaaa,” nikaongezea.

“Sitakagi hata kuwaona.”

“Lakini vipi baada ya kuzaliwa?”

Beautiful,” akajibu.

“Very beautiful,” nikaongezea.

Akatikisa kichwa kukubaliana na mimi.“Lakini vipi tungemuhukumu kipepeo yule kwa mwonekano wake kabla hajatotolewa?” hakuwa na jibu. “Look inside you,” kidole changu kikasonta kwenye kifua changu, upande wa kushoto,“who are you? That’s what matter and not how you look. Wewe si muuaji,” alinitazama.

Alikuwa kapendeza kama jana yake.

“I wish ningekujua mapema. Labda ningekuwa na furaha nusu na karaha nusu.”

“Raha na karaha, vyote vimeumbwa kwa ajili yetu. Unaweza kuwa na raha kila siku, ila ukija wakati wa karaha, utatamani ardhi ipasuke na kukumeza.”

“Same to me,” akajibu, “mwanzoni sikuwa nazijua shida. Nilikuwa napata kila ambacho nilikihitaji kwa muda mwafaka. Baba na mama yangu walinipenda. Walikuwa wapo tayari walale njaa ili mimi nipate hitaji langu,” alihadithia kwa sauti ya chini.

Nilimtizama usoni wakati anahadithia. “Mambo yalikuja kubadilika baada ya Step kuja maishani mwetu. Damn…” neno la Kiingereza alilinong’ona, “sikuwahi kuwaza kuwa nitakuwa kichaa wa mapenzi namna ile. Mapenzi yalivuruga mtindo mzima wa maisha yangu. Licha ya mengi ambayo nilimtendea huyu mwanaume, lakini bado hakuona thamani ya upendo wangu,” Mwimbula aliongea kwa masikitiko.

Hakujua tamaa yangu juu ya kile ambacho anakihadithia. Nilitamani nijue kilichomkuta, lakini na yeye hakuenda moja kwa moja. Nikabaki kwenye koma.“Upendo wangu aliugeuza ng’ombe wa sherehe. Akauchinja bila huruma, kisha akauchuna ngozi yake na kuubakiza nyama pekee. Napo hakuridhika. Akaupasua upendo huo na kuusambaza kama ambavyo anasambaza ng’ombe huyo. Utumbo huko, miguu kule, mbavu hapa, maini kule. Ndivyo upendo wangu nao ulivyothaminiwa. Nilimchukia Step.”

“Popote penye chuki, palianza kwa upendo. Huwezi kumchukia mtu ambaye hukuwahi kumpenda,” alinitazama usoni kwa maneno niliyomwambia.

Akatabasamu na kutaka kuongea lakini mlango wa ofisini uligongwa. Kabla sijaitika, ulifunguliwa.

Alikuwa ni yule mwanadada niliyemuagiza chakula. Alikuwa kabeba kikapu kidogo na mkono mwingine alikuwa kabeba chupa ya kuhifadhi chai. Nikasimamisha kinasa sauti na wakati huo Mwimbula alinyanyuka haraka na kumpokea chupa.Yule dada aliweka kikapu mezani na kunirudishia pesa iliyobaki.

“Hiyo kaa nayo. Nitakuongezea nyingine baadaye utuletee chakula cha mchana,” nilimwambia na yeye akazirudisha zile hela kwenye pochi ndogo aliyokuwa nayo.

Akatoka ndani ya ofisi na mimi niliinuka na kuanza kutoa vilivyomo kwenye kikapu. Punde tukawa tunafungua kimya; mimi na Mwimbula.

 

****

 “Hakuna kishangazacho kama mapenzi,” baada ya kupata kifungua kinywa, tuliendelea na maongezi yetu.

Niliruhusu kinasa sauti kiendelee kuchukua sauti zetu. Mwimbula ndiye aliyeanzisha.“Watu wanapenda lakini baadaye wanaumizwa. Wanapenda tena na kuumizwa tena. Wanapenda na kuumizwa, wanapenda na kuumizwa hadi inafikia muda wanatazama juu. Mawinguni. Kisha wanamuuliza MUNGU kwa nini umeyaumba haya mapenzi? Ni kweli umeyaumba yaje yatutese namna hii?” macho yangu hayakukwama kwenye uso wake wakati anajaribu kunielezea. “Lakini licha ya kutoa kauli hizo za kukata tamaa, wakitokea watu wengine ama walewale waliyowaumiza, wanapenda tena,” akasindikiza kwa cheko.

Sikujua maana ya cheko lake. Furaha ama maneno yake yalimchekesha. Nilichofanya ni kumuunga mkono kwenye cheko lake.

“Love is like magic,” nilimwambia.

Yeah. That’s true kaka,” naye akajibu kwa kukubaliana na kauli yangu. “I was proved that to Step,” akanitazama.

“Nini kilikutokea kwa Step?” ilibidi nimuulize baada ya kuona anazunguka sana kutaka kuniambia.

Akanitazama machoni kama kawaida yake. Nami sikupindisha macho yangu kwa kutazama kwingine. Niliendelea kumtazama. Tukawa tunatazamana.“Nakuhadithia alivyonihadithia yeye. Since his life hadi tukakutana,” nikakubali.

Nikakaa mkao mzuri wa kusikiliza simulizi yake na Step.

                                      

MOROGORO.

MIAKA THELATHINI ILIYOPITA.

Yalikuwa ni majira ya masika. Mvua zilikuwa zinaendelea kunyesha mikoa karibu yote ya Tanzania. Moja ya mkoa ambao ulipata bahati ya kushushiwa mvua, ulikuwa ni huu wa Morogoro. Mvua zilinyesha kwa nguvu na kuleta furaha kwa wakulima huku wale wenye nyumba ambazo hazikuhimili mvua kubwa, wakiwa na wasiwasi juu ya makazi yao.

Katika Wilaya ya Kilosa, Wilaya ambayo ipo mbali kidogo na Morogoro Mjini, ndipo alipatikana kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Stepeda Sekisengo. Alikuwa anahitimu darasa la saba wakati huo akiwa na miaka kumi na mitatu.

Wazazi wake ambao walitegemea kilimo cha nyanya na mahindi kumsomesha na kumpa mahitaji mengine, walikuwa wenye furaha walipokuwa kwenye mahafali ya darasa la saba yaliyofanyika katika shule aliyokuwa anasoma Stepeda. Kila mara walipambwa na tabasamu pale walipoona mwana wao anafurahia uwepo wao.

Hali ya hewa haikuwa kama siku zote. Ilianza kwa jua kali muda wa mchana. Muda ulivyokuwa unasonga, hali nayo ikaendelea kubadilika na kuwa tayari kwa mvua kunyesha. Mshereheshaji wa mahafali, alimaliza haraka kazi yake ili wazazi pamoja na wanafunzi ambao walikuja kushiriki kwa ukaribu sherehe zile, warudi kwao.

“Hongera mwanangu,” mama mzazi wa Stepeda alitoa pongezi huku akimpatia kiasi cha pesa mkononi.

Stepeda aliielewa hali yao ya umasikini wao. Hata ile pesa alipoiona, hakuwa na haja ya kuipokea. Aliona anapunguza bajeti ya pale nyumbani. “Chukua Step. Ni hiki nilichonacho. Tafadhali naomba usikikatae,” mama yake alisisitiza baada ya kuona dalili ya Stepeda kukataa.

“Take it son,” baba baye alisisitiza.

Kijana hakuona sababu ya kukataa. Akaichukua na kuiweka mfukoni. “Tuiwahi hii mvua kabla haijaanza kushuka,” baba wa Stepeda aliongea na kuanza kuondoka eneo lile na familia yake ikimfuata.

Umbali kutoka shule aliyomaliza Stepeda, hadi makazi yao, ilikuwa ni kilometa zipatazo saba. Walitembea kwa mguu na kwa kasi ili mvua isiwakute. Mama akiwa na mwana nyuma, baba alitangulia mbele huku akiwa na mashaka tele hasa kwa wingu jeusi ambalo lilitanda kila upande. Kila mara aligeuka nyuma na kuwahimiza Stepeda na mkewe watembee kwa kasi kwa kuwa hawajui litakalotokea endapo mvua itanyesha.

“Lile daraja likijaa maji, basi tutalala porini au tutarudi kuomba hifadhi shuleni,” maneno hayo yakawafanya mama na mwana kukaza mwendo.

Wakalivuka daraja kabla mvua haijaanza kunyesha. Zikabaki kilometa mbili ili wafike kwao. Tayari ilikwishatimu saa kumi na moja jioni.

 

****

Saa moja usiku, familia ya mzee Sekisengo ilikuwa mezani ikijipatia chakula cha usiku. Tayari manyunyu na radi vilikwishaanza kushamiri sehemu mbalimbali pale kijijini. Eneo waliloishi wao lilikuwa mbali kidogo na makazi ya watu wengine.

Nyumba yao ilitosha  kuelezea umasikini ambao ulikuwa umetanda kwenye maisha yao. Mabati mabovu. Choo cha nyasi. Ukuta wa udongo ambao mtu wa nje anaweza kumuona wa ndani kupitia matobo, vilitosha kutishia amani ya maisha yao.

Hofu ziliwakumba pale mvua zilipokuwa zinanyesha bila kukoma. Imani yao ilibaki kukimbilia kanisani endapo nyumba hiyo haitoweza kuwasitiri. Kanisa lenyewe lipo umbali wa kilometa zipatazo mbili au zaidi.

“Tule haraka kisha tufukie msingi wa nyumba kwa mchanga. Baada ya hapo tutakuwa salama kidogo,” aliongea mzee Sekisengo.

“Mimi tayari nimeshiba baba,” Stepeda aliongea akiwa kakamata kiazi kitamu nusu pamoja na kikombe cha uji wa moto.

“Sawa,” baba yake akakubali na wote wawili wakatoka nje tayari kwa kujaza mchanga maeneo yote ambayo walihisi maji yatapita na kuleta mtafaruku.

Mama yake Stepeda alibaki ndani akipanga vyombo na kuandaa malazi. Mvua iliendelea kunyesha taratibu.

Saa sita usiku, Stepeda alishtuka toka usingizini baada ya maji yaliyokuwa yanadondoka kutoka juu ya bati kumwagikia usoni. Alitulia kwa muda kabla hajafanya lolote na ndipo aliposikia sauti ya mama na baba yake wakiwa nje wanapambana. Akainuka haraka na kutoka.

“Rudi ndani Stepeda,” mama yake alimwambia lakini kijana yule hakutaka kufanya hivyo kwa kuwa hali ya mama yake ilikuwa mbaya.

Alikuwa kalowa chapachapa kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inazidi kunyesha. Mikononi alikuwa kakamata ndoo ambayo aliitumia kuchota maji yaliyokuwa yanaingia ndani na kuyamwaga nje.

“Baba yupo wapi?” akauliza Stepeda.

“Nimekwambia rudi ndani ukalale,” mama mtu akasisitiza lakini Stepeda alihisi kaambiwa toka nje kamsaidie baba yako.

Naye akafanya vile alivyohisi kasikia. Akatoka nje.

Huko alimkuta baba yake akiwa na chepe akichimba mchanga na kujaza kwenye ndoo kisha anaubeba na kwenda kufukia pembezoni mwa nyumba yake. Naye alilowa sawa na mama yake.

Stepeda alipagawa.

Bila kusita naye akajitoma mvuani na kuanza kumsaidia baba yake. Mvua nayo haikuwa na dogo wala macho, iliendelea kupamba moto huku radi na mingurumo ikizidi kurindima kila upande. Hali iliogopesha.

Ndani ya saa moja, familia ile ilikuwa inapambana kuikoa nyumba yao kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inaendelea kunyesha. Hakuna mafanikio yaliyokuwa yanaonekana licha ya mapambano yaliyokuwa yanaendelea.

Udongo na mchanga ambao ulikuwa unachimbwa na mzee Sekisengo, ulichimbwa hadi ukaisha. Akahama sehemu mbalimbali na kutengeneza mashimo kadhaa, lakini bado hali ya mvua iliendelea kudhoofisha nyumba yao.

Mara ikadondoka upande mmoja. Mzee Sekisengo akabaki kakamata kiuno huku kaduwaa. Aliishiwa maamuzi akabaki na akili ya kukimbilia kanisani.

Mzee Sekisengo; baba wa Stepeda, alitazama njia ya kuelekea kanisani. Ilishonwa na miti mikubwa pamoja na pori moja lililotisha hasa nyakati za usiku. Miti ilipuyanga na kulia kwa nguvu kutokana na upepo mkali ambao uliendelea kuvuma kwa bidii.

“Hali ni mbaya mwanangu,” Sekisengo aliongea akiwa kakata tamaa, “lolote litakalonitokea, hakikisha mama yako unamlinda na kumtunza. Usimwache wala kumtenga,” alimuhasa mwanaye ambaye alikuwa kasimama naye sawia, “ngoja niende kanisani kuona kama nitapata msaada wowote toka kwa watumishi. Nitakuja nao haraka sana,” aliongea na kugeuka tayari kwa kuondoka.

“Kwa nini tusiende wote?” Stepeda alimuuliza baba yake.

“Tazama kule,” akamwonyesha kwa kidole kule kwenye njia ya kuelekea kanisani.

Giza lilitanda na pia uwepo wa pori lenye miti mikubwa, ulitosha kuongeza hofu. Stepeda alielewa maana ya baba yake. “Kwa mfano miti ile ikatudondokea wote, huoni kama ni hatari kwenu? Bora niende mimi kwanza, kama nitachelewa ndani ya nusu saa basi tambueni nitakuwa nimeingia hatarini. Msijaribu kuja. Tafuteni njia nyingine ya kujikomboa. Msifuate nyayo zangu. Ni hatari mwanangu. Hatari sana.”

“Nimekuelewa,” akajibu Stepeda.

Baba yake alianza kuondoka kwa kasi baada ya kukubaliana na mwanaye.

Stepeda akarudi ndani ambako mama yake aliendelea kupambana kwa kuchota maji na kuyamwaga  nje.

“Baba yako yuko wapi?” ndilo swali la kwanza ambalo mama Stepeda alimuuliza baada ya kumwona mwanaye na chepe pamoja na ndoo.

“Kaenda kanisani,” mama Stepeda alisimama wima akiwa haamini kile ambacho amekisikia toka kwa mwanaye.

“Unasema?” akauliza tena.

“Amekwenda Kanisani,” Stepeda akajibu huku akiwa kakata tamaa pia.

“Baba Step. Kwa nini?” mwanamama alijiuliza kwa uchungu, “…unajua ni hatari gani ambayo ilikuwa katikati ya ule msitu hasa nyakati za usiku. Kwa nini baba?” hapo ndipo uchungu wa mke ulipoonekana.

“Kasema kama atachelewa ndani ya nusu saa, basi tutafute njia nyingine ya kujiokoa,” akaongeza Stepeda.

“Haiwezekani Stepeda. Baba yako anajitoa sadaka. Na siwezi kusubiri hilo litokee,” mama mtu hakusubiri kweli.

Akachomoka toka mule ndani na kuanza kukimbilia ile njia ambayo mumewe alielekea. Stepeda  naye hakuwa na jinsi. Alichomoka na kuanza kumfuata mama yake kule alipokuwa anaelekea.

Kasi ya mama ilikuwa kubwa  kuliko ya mwana. Mtoto alizidiwa hatua zipatazo thelathini. Stepeda hakukata tamaa. Aliendelea kumkimbiza mama yake huku akijaribu kumwita na kuongea maneno ambayo baba yake alimwambia.

Mvua ikiwa inaendelea na wakati huo si Stepeda wala mama yake walikuwa wanaona kila kitu mbele yao. Radi zilipokuwa zinapiga,  ndipo nao waliweza kuona waendako.

Mama akapinda upande wa kushoto ambao ndipo palikuwa na njia ya kuelekea kanisani. Mwana naye aliyekuwa anakimbia kwa kasi, alikata maeneo hayo hayo lakini ilikuwa si bahati kwake.

Kibao cha mbao ambacho kilipandwa pembezoni mwa njia hiyo, kilikuwa kimeng’oka na misumari iliyotumika kukigongelea, ilikuwa imesimama wima. Stepeda akavamia njia lakini pia aliivamia misumari hiyo kwa kuikanyaga kwa mguu wake wa kulia. Misumari miwili ikatokeza juu ya mguu. Alipiga ukelele mkali ambao ulimfanya mama yake asimame na kutazama nyuma. Stepeda alikuwa na wakati mbaya, lakini mama yake alikuwa na bahati mbaya.

Maumivu ya misumari miwili iliyotokeza juu ya mguu wake, yalimfanya kijana yule akae bila kupenda. Lakini bado hakuwa mwenye bahati usiku ule. Stepeda alikalia  misumari mingine. Hali ikazidi kuwa mbaya kwake.

Wakati hayo yanaendelea kwa Stepeda, mama yake alikuwa kwenye hatari kubwa zaidi. Chatu mkubwa ambaye ilisemekana alikuwa katika msitu huo, alikuwa anaacha windo lake alilolipata dakika chache zilizopita na kuanza kummendea yule mama ambaye alikuwa kasimama hajielewi aende mbele au amrudie mwanaye.

Akiwa katika mawazo hayo, alijikuta yupo chini baada ya kupigwa ngwara nzito kwa mkia wa chatu. Mama mtu alipojaribu kujitetea kwa kuinuka, tayari yule chatu alikuwa amekwishamfikia na kumrudisha tena chini.

Sauti ya kuomba msaada ilisikika toka kinywani mwa yule mama lakini hakuna msaada ambao alikuwa anautegemea. Stepeda alikuwa anamsikia vema lakini hakuwa na uwezo wa kujinasua na kwenda kumtetea mama yake. Hali ilikuwa mbaya mno.

“Stepeda nakufa mama yako. Chatu ananiua Stepeda…” sauti ya kukwamakwama ya yule mama ilisikika huku yule chatu ambaye hakuelewa lolote lile, aliendelea kumviringisha mwili wake na kisha kumbana vema.

“Nakufa Stepeda. Baki salama,” sauti ndogo ilimtoka mama Stepeda.

Sauti ambayo haikufika popote pale kwa sababu ya kelele za mvua. Radi zilipopiga, ndipo Stepeda alipomuona mama yake akivurugwa vibaya na chatu. Alibiringishwa na kubanwa hadi akapoteza uhai. Chatu akabaki katulia kwa muda palepale kama mwenye kusubiria windo lingine lijitokeze ili alivamie. Stepeda alikuwa katulia tuli. Aliamua kuvumilia bila kupiga kelele. Aliogopa kufuatwa na yule chatu ambaye ni wazi aliondoa wazazi wake wote wawili. Bado mvua iliendelea kunya.

 

***

 

 

SURA YA SITA

Asubuhi ya saa moja, wanakijiji pamoja na wananchi wengine walitembea huku na huko kuangalia athari iliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku uliopita. Katika matembezi hayo, ndipo wakakutana na mwili wa Stepeda ambao ulipoteza ahueni kabisa. Alipumua kwa mbali mno. Damu ziliendelea kumtoka taratibu maeneo yote ambayo yalipenya misumari.

Hali ilikuwa tete kwa yule kijana ambaye alikuwa kabadilika na kuwa mweupe kutokana na baridi kali pamoja na mzunguko wa damu kuwa mdogo.

Wasamaria wema walimtoa kwenye ile kasumba na kumkimbiza haraka kwenye hospitali ya Wilaya. Huko alipokelewa na kuanza kupewa huduma ya kwanza. Hakuonyesha dalili yoyote ya kuweza kupona. Hali ilikuwa mbaya sana kwa Stepeda. Ikashauriwa aondoshwe pale na kupelekwa hospitali ya Mkoa kwa ajili ya huduma bora zaidi.

Katika siku ambayo si Stepeda wala familia yake waliitegemea, ilikuwa ni siku ya ile mvua kubwa.  Ilianza kwa furaha kwa kijana  kumaliza darasa la saba. Kisha ukaja wakati mgumu mno katika maisha yake. Akapoteza familia yake baada ya chatu mkubwa ambaye inasemekana huonekana kwa nadra sana katika ule msitu.

Wanakijiji pamoja na wenyeji wa hapo, wanasema chatu huyo hupatikana hasa nyakati za baridi pamoja na mvua kubwa. Hukimbia makazi yake halisi na kuja kujificha katika miti mikubwa inayopatikana maeneo hayo. Wazazi wa Stepeda walilitambua hilo lakini hawakuwa na jinsi zaidi ya kukimbilia huko kwa ajili ya kuomba msaada.

Hapo ndipo mambo mazito yalipowakumba. Wote wawili wakageuzwa chakula ndani ya usiku mmoja. Naye  Stepeda aligeuka jina na kuitwa yatima. Kila mmoja aliyesikia simulizi ile, hakusita kusikitika.

****

Mwezi ukatimia kwa Stepeda kuwepo hospitali. Mguu ambao ulichomwa kwamisumari ulikuwa ukioshwa mara mbili kwa wiki na kuendelea kufungwa bendeji. Hakupewa huduma bora kwa kuwa hakuwa na mtu wa karibu wa kutoa pesa ili yule kijana apate huduma kama hizo.

Kwa mdomo wake, Stepeda alikubali kuwa mguu wake unapoteza mawasiliano. Alipoguswa kwa vyuma maalumu, hakusikia maumivu wala miguso hiyo. Wauguzi pamoja na matabibu, walielewa wazi kuwa mguu huo unaoza. Wasipouwahi kuukata mapema, unaweza kufika mbali na kuleta shida zaidi. Ikabidi wampe taarifa maalumu kwa ajili ya kukatwa mguu wake.

Hakuna siku nyingine mbaya hapa duniani kama ile ambayo aliipokea kwa ajili ya kuondolewa mguu wake.

Aliumia mno. Na akalia sana.

Akaomboleza huku na huko ili apate msaada ambao ungesaidia kutokatwa mguu wake. Hakukuwa na jipya. Alipangiwa kukatwa mguu siku mbili zijazo na kisha baadaye angeondolewa hospitali maana muda wa kukaa bure ulikuwa umekwisha.

Stepeda akabaki hana wa kumkimbilia zaidi ya MUNGU ambaye hakuna ambaye haamini uwepo wake. Na hujibu kwa wakati.

Naam. Ukafika wakati wa MUNGU kujibu maombi ya Stepeda. Aliyajibu wakati anatolewa wodi aliyolazwa tayari kwa kupelekwa chumba cha upasuaji. Alikuwa analia kwa nguvu kila alipokuwa anafikiria tendo ambalo alikuwa anakwenda kufanyiwa baada ya muda mchache. Kilio kilikuwa kikubwa na kilivuta hisia za wengi mule hospitali.

Moja ya watu ambao waliguswa na kile kilio, alikuwa ni Sasha Majige. Sasha ni mwanamama mwenye mtoto wa kike usawa wa Stepeda. Aliitwa Faraja Majige. Sasha pamoja na mwanaye waliongozana kuja hospitali na Mzee Majige; baba wa Faraja na mume wa Sasha. Ilikuwa ni kawaida yao kutembelea hospitali na kutoa sadaka.

Waliamini utajiri wao haukuwa kitu kama wataacha kutoa sadaka kwenye madhehebu ya dini pamoja na kusaidia wasiojiweza ambao wanapatikana kila mahali.

Siku hii walitembelea hospitali na kukutana na kisanga cha Stepeda. Mwanamama Sasha roho ya imani ikamkumba. Si huyo tu! Mwanaye Faraja naye alikuwa kachanganyikiwa kwa huzuni wakati Stepeda anapelekwa chumba cha upasuaji.

“Baba Faraja,” ilimbidi Sasha aongee na mumewe kuhusu suala la kumsaidia yule kijana abaki na mguu wake.

Alionekana bado anauhitaji sana. “Tumsaidie huyu kijana.”

“Lakini tayari tumekwishasaidia mke wangu,” mzee Majige hakuonyesha nia ya kutaka kufanya hivyo licha ya kupewa simulizi ya kusisimua kuhusu Stepeda.

“Sidhani kama tutakuwa tumetoa sadaka iliyokubalika kwa MUNGU kwa miaka yote tunayofanya hivyo endapo hatutamsaidia huyu kijana,” mumewe akatulia kwa muda.

Akamtazama Faraja; mwanaye kipenzi. Machozi yalikuwa yanambubujika kama mvua ituayo batini.

“Sawa,” mzee Majige hakuwa na haja ya kupambana na ushawishi wa mkewe.

Mkewe alimwelewa kwenye ushawishi wa kufanya jambo. Lakini macho ya Faraja ndio yalimsukuma kumsaidia Stepeda.

Wakafanya linalowezekana na zoezi la kukatwa mguu likazima. Wakalipa gharama kadhaa za kuoshwa tena mguu wa Stepeda. Baada ya hapo wakamuhamisha hospitali na kumpeleka hospitali binafsi inayomilikiwa na Wahindi.

Kama maumivu ndio tiba, basi Stepeda alikuwa tayari kukumbana na maumivu hayo ili apate tiba kamili ya mguu pamoja na makalio.

Ndani ya ile hospitali hakukuwa na mambo ya kuangalia utoto wala ukubwa. Stepeda alitakiwa kurudishwa katika hali yake ya mwanzo. Na ili lifanikiwe, ilibidi atolewe usaha uliotunga kwenye mguu wake pamoja na nyama ambazo zilikuwa zimeozea. Suala hilo halikuhitaji ganzi wala nusu kaputi. Lilifanyika huku kijana yule akiliona kwa macho yake.

Mguu ulichanwa kwa kisu kikali. Yule kijana hakuhisi maumivu yoyote wakati wa hilo tendo. Usaha ukamwagika wa kutosha. Mguu ukaendelea kukamuliwa na wauguzi maalumu. Nyama zikaanza kutolewa kwa makini.

Ndani ya dakika kumi, hali ya Stepeda ilianza kubadilika. Aliyahisi maumivu makali wakati tendo la kukamuliwa likiendelea. Na huo ndio wakati ambapo usaha ulikoma na damu kuchukua nafasi. Alijitahidi kuvumilia mwanzoni, lakini pale wauguzi walipoanza kuosha kwa dawa maalum ndani ya mguu wake, hakuona kama kuna maana ya kuvumilia.

Akaanza kulia. Hakuna ambaye alimsikia.

Alikupuruka mwili na mikono, lakini miguu haikufanya hivyo kwa kuwa ilibanwa vema na vifaa maalum. Stepeda alikuwa anapitia kiama kingine kwenye maisha yake. Aliumia, lakini hiyo ndio tiba. Mwisho wa yote hayo ilikuwa ni yeye kupoteza fahamu kutokana na maumivu.

Wauguzi waliangalia mapigo yake ya moyo, hawakuona lolote ambalo lingezuia kuendelea zoezi lao. Wakafanya kile walichoamini ni kuokoa mguu wa yule kijana.

Wakafanikiwa kuokoa mguu wa Stepeda. Kutoka usawa wa goti, hadi kulipochomwa misumari kulikuwa kumepoteza uwezo wake wa kufanya kazi. Wauguzi wakaosha kidonda na kuondoa upuuzi wote ulioleta lile tatizo.

 

****

Baada ya saa nne, Stepeda alirudiwa na fahamu na kujikuta ndani ya wodi maalum akiwa kafungwa kidonda chake. Aliyahisi maumivu kwenye mguu wake. Alishukuru hata kwa hilo kwa kuwa hakuwahi kuyahisi maumivu kama yale kwa wiki mbili mfululizo. Hivyo ile ilikuwa ahueni.

Akakaa ndani ya ile hospitali mwezi mzima. Aliendelea kuoshwa kidonda chake kwa mtindo uleule.

Alilia lakini hakuwa na jinsi.

Kila alipokuwa anafanyiwa lile tendo, aliona mabadiliko kwenye mguu wake. Mwisho wake hakuwa anayahisi yale maumivu ambayo alikuwa anayapata mara ya kwanza. Alianza kupona na mguu wake ulionekana wazi unarudi kwenye hali yake. Nyama zilirudi na kidonda kilianza kufunga.

Hatimaye akarudishwa nyumbani akiwa na gongo maalum kwa ajili ya kutembelea. Bado mguu wake haukuweza kutembea wala kupewa shuruba za namna yoyote. Sasha alichukua jukumu la kumlea Stepeda kwa kuwa hakuwa na sehemu yoyote ya kwenda zaidi ya kijijini kwao ambapo hakuwa na sehemu ya kuishi baada ya nyumba yao kubebwa na maji yaliyotokana na mvua zilizoendelea kunyesha.

Kila wiki alipelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi na mazoezi madogo ambayo yangemsaidia kuweza kutembea kama zamani.

Binti wa Majige; Faraja. Ambaye alikuwa darasa la tano. Alimpenda Stepeda na alimchukulia kama kaka yake. Kila mara alikaa naye sebuleni na kuongea naye mengi huku wakicheka. Kuna muda Stepeda alimfundisha Faraja masomo ya darasani na hilo ndilo ambalo lilizidi kuwapa imani wazazi wa Faraja. Waliona kuna kitu ndani ya Stepeda. Hawakutaka kitu hicho kipotee kama moshi upoteavyo ufikapo angani.

Mwaka mmoja ukapita tangu masahibu yale yamkute Stepeda. Tayari alikuwa karudi katika hali yake na aliishi ndani ya familia ya Majige. Alifurahi kuwa sehemu ya ile familia.

Alipewa jukumu la kuyatunza mazingira ya nje. Alihakikisha yapo safi na salama. Mifugo mbalimbali ambayo ilifugwa na ile familia, ilikuwa chini ya uangalizi wake.

Stepeda hakuwa mkaidi. Fadhila pekee ambazo alipaswa kuzirudisha kwa ile familia, ilikuwa ni kufanya zile kazi ambazo wala hazikumuumiza. Alizifanya kwa moyo wake wote na aliaminika sana na ile familia.

Faraja aliendelea kusoma hadi akamaliza darasa la saba. Akafaulu vema sana. Alichaguliwa shule fulani nje ya Mkoa wa Morogoro lakini alikataa kwenda kusoma huko. Alitaka awe karibu na familia yake. Wazazi wake wakaamua kumtafutia shule nyingine palepale Morogoro.

Hawakuwa na jinsi.

Ikabidi pia wampeleke na Stepeda chuo cha ufundi stadi. Huko kijana akachukua mambo ya ufundi uashi na baadaye akaomba asomee na ufugaji.

Miaka miwili mbele, mabadiliko ya kimwili kwa Faraja yalianza kuonekana. Mwili wake ulichipuka kwa kasi na ulianza kunona kama umepakwa mafuta ya kupikia. Uzuri wake ambao hapo kabla ulifichwa kwa utoto, safari hii ulionekana bila kificho machoni mwa watu.

Wanaume wakware pamoja na vijana aliokuwa anasoma nao, walianza kumtolea macho ya tamaa. Usumbufu nao ulianza kuchukua nafasi yake. Wanaume wakajipanga mstari. Nia yao ilikuwa moja tu! Kulala naye.

Mabadiliko haya hayakuwa kwa Faraja pekee. Stepeda naye hakuwa nyuma kukumbwa na balehe. Sauti, kifua na ndevu rasharasha, vilitosha kusema kijana amebalehe. Wazazi wa Faraja wakaongeza umakini dhidi ya wawili hawa. Hawakutaka waharibikiwe mapema kwa kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi.

Mzee Majige aliamua kukaa na Stepeda. Huku Sasha akikaa na Faraja. Wakatoa masomo muhimu ya ujana. Wakawahasa sana kuhusu dunia ya kisasa. Wakawaambia kuhusu magonjwa na ulaghai ambao unapatikana nje ya nyumba yao.

Kwa upande wa Stepeda, somo liliisha. Ilikuwa ni kazi kwake kufuata ushauri wa mzee Majige. Ila kwa upande wa Faraja, somo bado liliendelea. Akiwa kwenye likizo, alipelekwa huko Stalike mkoani Mpanda ambapo ndipo chimbuko la wazazi wake.

Huko akakabidhiwa kwa bibi yake kwa ajili ya unyago. Faraja akawekwa ndani na kufunzwa haya na yale. Alifunzwa mengi hasa heshima na hekima.

“Faraja mjukuu wangu,” nyanya wake alimuita wakati anamfunda.

Faraja akamtazama machoni bibi yake, “ukibahatika kuolewa, usiwe mwanamke wa kuongea sana. Hakuna mwanaume anayependa kidomodomo. Msikilize mumeo. Na si kusikiliza tu! Liingie kichwani mwako. Si kuingia shoto kisha limwagikie lia. Nakukanya mjukuu wangu, usifanye hivyo,” Faraja akatazama chini, “umenielewa?”

“Nimekuelewa bibi.”

Licha ya udogo wake, lakini kuna baadhi ya mambo aliyofundishwa, hayakuendana na umri wake. Lakini hakuwa na jinsi. Alikubaliana na yote na hakutaka kuleta pingamizi lolote. Inawezekana ndio iliyomjenga na kumfanya awe imara baada ya kuolewa.

“Asikudanganye mtu yeyote yule kuwa mumeo si bora bali elimu yako ndio. Asikudanganye yeyote yule. Katika ndoa yako, kwanza mumeo kisha dada na kaka zake. Usisahau wazazi wake. Mengine yanafuata. Ukiwadharau mawifi na mashemeji zako, jua umemdharau mumeo moja kwa moja,” aliendelea kupewa somo. “Narudia tena. Ukiwadharau mawifi na mashemeji zako…” akarudia maneno aliyomwambia. “Umenielewa?”

“Nimekuelewa bibi,” akajibu huku macho yake yakiwa yanatizama chini.

“Haya ni nini mjukuu wangu?” Faraja akatazama alichoulizwa.

“Hayo ni mafiga bibi,” akajibu alichokiona.

“Yapo mangapi?”

“Matatu.”Bibi akachukua chungu na kukiweka juu ya yale mafiga.

“Je? Chungu hichi kimekaa au hakijakaa?” akamuuliza.

“Kimekaa bibi.”

“Vipi nikifanya hivi?” akamuuliza huku anavuta figa moja na chungu kile kikadondoka.

“Kimedondoka.”

“Ndivyo ilivyo,” akamwambia,“haya mafiga matatu. Moja ni mumeo, lingine ni mashemeji na lingine ni mawifi. Na hichi chungu ni wewe. Endapo mmoja kati ya hawa akatokea kutokuelewa, basi ni lazima utadondoka. Tena hapa shukuru chungu hakina chochote ndani na chini hakuna moto. Shukuru hili kwa leo. Lakini nataka nikwambie kuwa, wewe ni chungu. Ndani yako umebeba eidha chakula cha familia yako au mboga au maji. Kwa kifupi wewe ndiye muhimu sana kwenye mji ambao mumeo kakupatia. Ndoa yako, ipo ndani yako wewe,” Faraja alikuwa kimya.

Macho aliyarudisha chini lakini bibi yake alimtazama moja kwa moja.“Endapo figa moja litaacha kukubeba. Amini nakwambia, utamwaga uliyoyabeba na utayamwagia motoni. Hakuna ambaye atavumilia. Mumeo pia atajiondoa kwenye kukubeba,” Faraja akamtazama kwa mshtuko bibi yake.“Usiache mbachao kwa msahala upitao. Kamwe usibabaike kwa maneno ya watu, ukayaona hayo ndio yanafaa na kuikacha ndoa yako hata kama ndoa hiyo ni sawa na kuzimu. Nakwambia tena, usiache mbachao…” akaurudia msemo uleule. “Maneno yao ni maneno tu! Siku ndoa yako ikiharibika, ni haohao ambao watakuja kukucheka. Hakuna anayependa kukuona unadumu ndani ya ndoa yako. Iwe wifi, iwe shemeji, iwe jirani au rafiki. Ni wazazi na nduguzo pekee ndio wanahitaji ndoa yako idumu. Sasa ukiacha ndoa yako kisa maneno ya kupita, jua unaunguza nyumba yako. Hakuna atakayevumilia.”

Mafunzo yalikuwa mengi kwenye unyago. Lakini kubwa zaidi, Faraja alifundwa kuhusu usafi, wanaume, mume, hekima, heshima na mambo yote muhimu ambayo yangesaidia  kuukomboa ujana na ndoa yake.

“Tayari umepata mwanaume?” siku moja bibi yake alimuuliza.

“Hapana bibi. Hapana…” Faraja alijibu haraka huku anaona aibu.

“Anaona aibu huyoo…” bibi yake akamtania huku anafinya mashavu laini ya mjukuu wake.

“Bibi bwana sitaki…” Faraja akadeka.

“Naona kuna mtu unampenda. Lakini bado si mwanaume wako…” Faraja akazidi kuona aibu.“Sitaki kumjua. Lakini kwa sasa, rudi nyumbani. Soma kama wazazi wako wanavyotaka usome. Usijiingize kwenye mambo yoyote yatakayowavunja moyo wazazi wako. Achana kabisa na mapenzi. We soma tu,” kama kuna maneno ambayo Faraja aliyashika, yalikuwa ni haya.

Miaka mitano mbele, Faraja alikuwa anasomea Sheria chuo cha Mzumbe, bado hakuwa katika mahusiano ya kimapenzi.

Stepeda alirudi kwenye makazi aliyowahi kuishi na wazazi wake. Huko alikuta kiwanja cha baba yake kikiwa salama kabisa. Alipewa taarifa kuwa baadhi ya ndugu wa baba zake, walikilipia na kukipatia hati maalumu. Alipofika, alikabidhiwa hati hiyo na serikali ya kijiji.

Kwa pesa ambayo alipewa na Mzee Majige, Stepeda alijenga nyumba ya kawaida kwa ajili ya kuishi. Akajenga na mabanda kadhaa ambapo alianza ufugaji wa kuku wa mayai na nyama. Pia alijenga sehemu maalum kwa ajili ya kufanya ufundi. Yote hayo ni katika kufanya maisha yake yasonge mbele bila kutegemea vya jirani. Mambo yakasonga namna hiyo.

 

****

Uzuri wa Faraja, ukawa gumzo kila sehemu aliyokatiza. Weusi wake, pamoja na hekima alizozibeba, kila mmoja alitamani kumwangalia na kumsikiliza.

Licha ya kusoma sharia na elimu zingine za kidunia. lakini bado alikuwa kasimama kwenye misimamo ya mila na desturi za Kiafrika. Alipingana kwa hoja na baadhi ya marafiki zake ambao kutokana na usomi wao, waliamini Mila na Desturi za Kiafrika, zimepitwa na wakati.

Kivipi zimepitwa na wakati? Hilo ndilo swali ambalo Faraja alikuwa anajiuliza kila siku.

Waliompa majibu walisimama kwenye jinsi ya kuabudu na mafunzo ya jando na unyago ambayo wao walisema yanatolewa kwa vijana wadogo ambao ni kama wanavurugwa. Wasomi wenzake waliamini vijana hao walibebeshwa mizigo mizito angali ni wadogo.

Hawakujua msomi mwenzao aliwekwa ndani miezi kadhaa akipewa hili na lile na bibi yake. Na ndio huyo ambaye ana misimamo thabiti kwenye mahusiano kuliko wao.

“Hivi ngojeni niwaulize,” siku moja Faraja aliamua kuvalia njuga suala la mila na desturi mbovu za Kiafrika.

Wote wakiwa wanamtazama kwa macho ya kutaka kujua swali lake, akawauliza. “Ni nani kati yenu hajawahi kulala na mwanaume au mwanamke?” kwenye huo mdahalo kulikuwa na wanaume wanne na wanawake wanne. Jumla walikuwa nane.

Baada ya swali hilo wote walikaa kimya wakimtazama. “Nani ambaye hajawahi kufanya mapenzi kati yenu?” akauliza tena.

Wote walikuwa kimya. “Doris…” akataka jibu toka kwa rafiki yake.

“Mii nimewahi bwana. Kwa nini nidanganye?” Doris akajibu na kusababisha wengine wacheke.

“Hakuna haja ya kucheka hapa,” akawaambia,“ambaye hajawahi kufanya mapenzi anyooshe mkono wake juu,” akajikuta ni yeye peke yake ndiye kanyoosha. “Sijawahi kufanya mapenzi na sina mpango huo. Lakini nimepitia unyago nikiwa na miaka kumi na sita. Na nazijua mila na desturi za kabila letu. Kila mwaka nakwenda kijijini kwetu kujifunza,” akawaambia wenzake.

Wote wakabaki wanamtazama.“Nawashangaa nyie ambao tayari mmejua jinsi ya kufanya ngono, mnasema mila na desturi za Kiafrika zinaharibu kizazi chetu. How? Mbona nyie hamjazipitia lakini tayari mmeshaingia huko kwenye kuharibikiwa? Tena ukute wengine hapa wameanza wakiwa na miaka kumi na mbili au tano. Na hadi sasa wengine mmelala na wapenzi zaidi ya wanne,” kimya kikatanda. “Mimba ngapi zinatolewa huko nje? Wangapi huko wadogo kwa wakubwa wanaua watoto kwa kuchoropoa mimba? Na nyie wanaume mnawasaidia wangapi kwenye kuua? Je? Hayo yote ni kwa sababu ya mila na desturi zetu?”

“Dada mkubwa basi bwana,” jamaa mmoja aliongea kukubali usahihi wa Faraja.

“Sio basi Zeko. Bila sisi kupambania mila na desturi zetu, tutaumizwa sana na Uzungu. Mbona mila zetu kulikuwa hakuna kutoa mimba wala nyota sijui ya rangi gani huko. Sasa hivi tunaua utadhani mimba ni mende au panya. Kwamba utakapoona wadudu hawa, wewe ua tu! Ni uchafu,” pumzi zikawashuka. “Tunadanganywa na rangi nyeupe na kuiona yenyewe ndio sahihi. Lakini ukweli ni kwamba, rangi nyeusi ndio tupo sahihi.”

“Hapana Sister,” jamaa mwingine akadakia, “unataka kuniambia tupo sahihi sisi? Mbona tulikuwa tukizaa albino tunaenda kuwatupa maporini kwa kudai kuwa ni mikosi?” akawatazama kwa zamu.

“Na mbona hizohizo mila walisema mwanamke akila mayai akiwa na mimba, anazaa mtoto ambaye hana nywele?” Zeko akakazia swali.

“Na tena walidai firigisi za kuku au ndege yeyote yule, anatakiwa kula mwanaume na si mwanamke?” Doris akaongeza swali.

“Hapo swali kauliza Kundi tu! Kuhusu suala la Maalbino. Haya mambo ya mayai na firigisi sioni kama yana uzito. Wewe kutokula firigisi kunakupunguzia nini? Au usipokula mayai kipindi una mimba, kunakupotezea nini? Na tena mayai yenyewe si ndio haya ya kisasa? Tena mengine yana viini viwili. Kwamba ukiamua kutotolesha, yai moja linaleta vifaranga wawili,” wote wakacheka.“Kuhusu albino, hizo ndizo mila ambazo tulipaswa kuzipiga vita na kuzisimamia kidete. Wale ni wenzetu pia. Na hawapo Afrika pekee. Hata Wazungu wapo huko. Kwa nini sisi tuwabague na tufikie hatua hadi kuhitaji viungo vyao? Hii si halali. Na kwenye kabila letu, haya mambo yalikuwepo zamani huko. Lakini tuliyaacha baada ya kuona ni uonevu usio na tija.”

“Sasa kwa nini useme sisi ndio tupo sahihi kuliko Wazungu?” akauliza Kundi; jamaa aliyeuliza kuhusu albino.

“Kwani yule Adolf Hilter alikuwa mweusi? Mbona aliwachoma Wazungu wenzake?” akauliza Faraja.

“Ah! Ile usifananishe na mila na desturi za jamii fulani. Yule alikuwa na chuki zake,” akajibu Kundi.

“Eti chuki zake,” akaongeza na cheko, “na vipi Mfalme Leopard? Aliyeua Wakongo zaidi ya milioni kadhaa na bado leo hii hasemwi ubaya wake kama Hilter. Hii nayo vipi? Kwa nini Hilter azungumzwe sana kuliko Leopard?”

“Ah! Sasa hapo sijui. Na nitasimamia kuwa hiyo ipo nje ya mada,” akajibu tena Kundi.

“Nje ya mada wapi Kundi? Hawa weupe wanajitanguliza sana wao. Yaani wanataka tuamini wao wapo sahihi na ndio maana kuua Waafrika kwao si jambo la maana kama kuuwawa kwa wenzao. Angalia hata huko Amerika pale mweusi anapomuua mweupe mambo yanavyokuwa. Ni tofauti na akiuawa mweusi. Upo wapi Kundi? Hizi ni kama desturi zao Bro,” alimwambia huku anapigapiga karatasi kwa kalamu. “Halafu nikurudishe tena kwa swali bro Kundi. Ipi ni mila na desturi sahihi kwako kati ya hizi?” akameza mate kabla hajaendelea. “Wanaume kuoa wanawake idadi waitakayo au wanaume kwa wanaume kuoana.” Wote wakamtazama Kundi.

“Duh!” akaguna, “aisee bora hiyo kuoa wanawake kibao kuliko dume kwa dume,” akajibu.

“Kwa upande wa ndoa. Mila ya nani ipo sahihi kati ya Mzungu na Mwafrika?” akauliza Faraja.

“Hapo Mwafrika lakini bado Mzungu yupo sahihi kuliko sisi kwenye vingi,” akaongeza.

“Vingi vipi brother Kundi? Kwenye kuabudu sisi tulikuwa tupo sahihi na ndio maana tuliomba mvua zikanyesha. Tuliomba mazao yapatikane, na ikawa. Kulikuwa hakuna operesheni wakati wa mama kujifungua, lakini sasa hivi operesheni kibao. Nguvu za kiume ni tatizo kwa taifa sababu ya vyakula vyao. Watoto wanazaliwa na ulemavu wa kudumu. Yote haya yameanza kutokea vipindi hivi ambavyo mila na desturi zetu zinadidimia. Bro. Wake up. They are wrong and we are right,” mdahalo ukaendelea na kila mmoja akavutia kwake.

Faraja alikuwa ana ushawishi mkubwa kwa kuwa alizielewa mila na desturi kutoka kwenye kabila lake. Wale waliojaa utandawazi, hawakutaka kuamini anacho amini.

Miaka iliyofuata, Faraja alimaliza chuo na alifaulu vema. Akaenda kusoma tena shule ya sheria (School of LAW). Hii ni shule ambayo inakuandaa kuwa mwanasheria kamili. Akasoma mwaka mmoja na baada ya hapo akaapishwa na kuwa mwanasheria. Kazi ikabaki kwake eidha kuajiriwa au kujiajri. Akaamua kusimamia mali za wazazi wake ambao nao umri ulikuwa umewatupa mkono.

Kila mara Stepeda aliitembelea familia ya Majige. Walimpenda yule kijana kwa kuwa hakuwatupa katika maisha yao. Stepeda alikuwa kafanikiwa kwenye shughuli zake kwa kiasi kikubwa. Tayari alikuwa kawapata ndugu zake ambao kwake aliwachukulia ndio kaka na dada zake. Baadhi aliwasomesha na wengine aliwapa mitaji ambayo ilisogeza mbele ya maisha yao.

****

 

 

 

 

SURA YA NANE

K

atika kila hangaiko la maisha, kuna suala moja ambalo linakutanisha akili moja na nyingine na kuunda mapenzi. Kuna msemo unasema;upendo ni mmea uwezao kuchipua mahali popote pale katika moyo. Na popote penye mmea huo, hakuna ambaye anaweza kuingilia na kuharibu.

Naam.

Stepeda na Faraja waliangukia kwenye mahaba. Wakapendana kama utani. Ile kuonana mara kwa mara, kukatengeneza mmea uliomea mioyoni mwao. Wakapendana na kujikuta wakianza mahusiano ya kimapenzi.

Muda nao haukutaka kuficha jambo.Habari zikafika kwa wazazi pamoja na walezi wao. Japo ilikuwa ngumu kwa upande wa wazazi wa Faraja lakini walipogundua kuwa Stepeda si damu yao pia wanamfahamu vema kuliko vijana wengine.

Hawakuwa na jinsi.

Wakabariki yale mahusiano. Na huo ndio ukawa mwanzo wa safari mpya ya Faraja. Ndio ukawa mwanzo wa kuitwa Mwimbula badala ya Faraja.

Baraka zilipotolewa, ukawadia ule wakati kutaka kuoana kabisa. Mambo yalikimbia kama sekunde.Kulikuwa hakuna haja ya kuchunguzana. Wachunguzane nini wakati walikua pamoja? Walililewa pamoja na walikaa nyumba moja. Mambo yakaenda kwa kasi ya usiku kutafuta pambazuko.

Hatimaye akaitwa Stepeda na ndugu zake pamoja na mshenga kwa ajili ya kupangiwa mahari. Siku hiyo Mzee Majige ndiye aliyesimamia kila jambo.

“Vyote mnaweza kuvibadili na kuwa fedha,” Mzee Majige aliongea baada ya kutaja mahari na vitu vingine vya kuleta. “Lakini upinde na mishale yake, jembe, vitenge na mwimbula, hivi ni lazima vije kama vilivyo. Havibadilishwi. Bora hata mkikosa hiyo mishale au jembe lakini si MWIMBULA.”

“Umesema huyu mwimbula ni nini?” mshenga akauliza huku akiwa anaandika kwenye daftari lake.

“Embu shangazi mtu elezea,” mzee Majige akampa kazi dada yake ambaye ndiye shangazi wa Faraja.

“Mwimbula anaweza kuwa ng’ombe au mbuzi. Ila kwetu sisi, tunahitaji zaidi ng’ombe kwa sababu ni ishara kubwa na hata mababu zetu tunaamini wataridhika zaidi akiwa ng’ombe. Hayo ni mambo ya kimila zaidi. Na mwimbula huyo ni lazima aje kama alivyo kwa sababu ndiye atachinjwa siku ya kugawa mahari ya binti yetu,” akatulia kidogo. Kisha akaendelea kutoa elimu, “kama mnavyojua, mahari ni ya pande tatu. Upande wetu sisi kama baba. Upande wa mama. Na upande wa binti. Hivyo wakati wa kugawa mahari hiyo, mwimbula atakuwa sehemu ya mahari hiyo na pia kabla ya hapo tutafanya jambo la kimila kuomba ridhaa kwa mababu zetu tufanikishe tukio hilo. Na mwimbula ndiye atahusika kuomba ridhaa hiyo kupitia damu yake,” akawatazama wageni waliokuja kusikiliza mahari ya kuozeshwa binti wa mzee Majige. “Ni lazima mwimbula aje kama alivyo. Hata kama hamtoleta mahari, kwa maana Stepeda ni kama mtoto wetu pia. Ila mwimbula awepo kwa ajili ya wazee wetu,” akasisitiza.

“Tumekuelewa.” Maneno ya mshenga yakamaliza kila kitu.

Na yale ambayo yalipaswa kufanyika, yakafanyika haraka mno.

Mwimbula akaletwa. Akachinjwa. Akafanywa sadaka kwa damu yake kunyweka na wazee mbalimbali wa kimila. Nyama ikachemshwa na kugaiwa pande zote. Iliyobaki ikaliwa na waalikwa wengine pamoja pombe ya kimila iliyopikwa na jopo la wakinamama. Kila aliyehudhuria, alikiri kuwa amefurahia pombe pamoja na nyama.

Walikenua siku nzima huku wakitoa nyama kwenye meno kwa vijiti na wengine kwa vidole.

Baada ya kuunganishwa na kuwa mume na mke, Stepeda na Faraja wakaamua kujenga nyumba kwenye kiwanja alichopewa Faraja huko Stalike. Marehemu bibi yake; yule aliyemfunda alimpa kiwanja hicho zamani mno. Na  yeye akaona ni vema wakajenga huko na kwenda kuishi. Hakutaka mumewe aendelee kukumbuka kadhia ambazo aliwahi kuzipitia huko Morogoro.

Morogoro akawekwa mtu ambaye atasimamia ile miradi ya kuku na ufundi. Wao wakaenda kuishi Mpanda ambapo pia kulikuwa na kampuni aliyoimiliki Mzee Majige. Faraja alikuwa Mwanasheria wa makampuni ya baba yake.

Miaka miwili ya ndoa yao, mimba ikatungwa na wakati huo Stepeda akasukumwa na mkewe afanye muziki kwa kuwa ndicho kitu alichokipenda. Faraja akamsaidia kila kitu hadi mumewe akawa msanii maarufu Tanzania kutokana na uwezo wake kuimba.

Stepeda Sekisengo almaarufu kama Step Sex, alikuwa kipenzi cha watu. Alialikwa kwenye matamasha mbalimbali nchini. Akapata umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi. Kila wimbo alioutoa, ulikamata na kukonga nyoyo za watu. Aliposema natoa wimbo siku fulani, kila shabiki alisubiri kwa hamu wimbo huo.

Step Sex hakuwa msanii wa kusimamishwa na wasanii wengine. Hata matamasha yake aliyafanya kwa malipo ghali mno. Kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ni yeye ndiye aliyeongoza kwa kulipwa pesa nyingi pale alipokuwa anaitwa kufanya matamasha.

Umaarufu ni gunia la misumari unalotakiwa kujitwika kichwani na kutembea nalo kila mahali. Stepeda alilitambua hilo lakini hakujali. Akaanza kuutumia umaarufu wake vibaya. Akajaa kichwa na kujisahau. Akasahau alipotoka na anapoelekea. Akasahau kuwa ana ndoa na ana mtoto.

Pesa zikamchanganya. Usaliti ukaukumba moyo wake. Pombe nazo zikaanza kumlevya. Zilikuwa nyingi kiasi cha kuona zingine kazi yake ni kuwahonga wanawake ili alale nao. Zingine alizimwaga hewani akiwa baa au sehemu zenye mikusanyiko. Mitandao ya kijamii ikawa inaweka matukio kedekede kuhusu yeye. Wanawake anaolala nao na wale ambao wanahitaji kulala naye.

Yote hayo Faraja aliyapata kupitia dunia kiganjani; Utandawazi. Ilimuuma na saa zingine alijuta kwa nini alimruhusu mumewe afanye muziki. Lakini maji yakisha mwagika, achana nayo kwa hayazoleki.

Mambo yalianza kama utani. Kupuuzia kwa Faraja, ndiko kukaleta kujiamini kwa Stepeda. Akaanza kuvuka mipaka. Akawa si yule wa zamani ambaye alirudi nyumbani mapema na kama angelikuwa anachelewa, angelitoa taarifa.

Huyu wa sasa alianza kuchelewa kurudi. Na aliporudi alikuwa kalewa chakari. Alipoulizwa kwa nini umechelewa, alijibu kwa nyodo. Akiambiwa kuhusu kunywa pombe, basi kipigo kinafuata. Mkewe akawa mhusika mkuu wa matendo yote.

Hakuwa na pa kukimbilia. Kila alipokwenda kuomba msaada, iwe kwa wazazi, mshenga au kwa rafikize, walimwambia avumilie. Na tena aliambiwa hakuna ndoa rahisi. Kila ndoa ina mapungufu yake. Kwa hiyo kukwazana ndani ya ndoa, ni jambo la kawaida. Wakaendelea kumpa mifano, hata vikombe kabatini vinagongana, sembuse binadamu? Mambo yakapita namna hiyo.

Siku zote maisha yamejaa mitihani pamoja na kasumba zisizo na hodi. Pale zinapoingia katika maisha yako, huwa hazikupi taarifa. Huja kwa nguvu na kwa mfululizo. Hichi ndicho kilichotokea kwa Faraja. Wakati anaendelea kupambana  na ndoa yake, mara baba na mama yake wanapatwa na mkasa ambao unachukua maisha yao.

Jioni moja wakiwa nyumbani kwao wamejipumzisha, majambazi wenye silaha za moto wanawavamia na kuwatoa uhai bila huruma.  Ikashangaza, hawakubeba chochote kile. Ilikuwa wazi waliagizwa kuua pekee. Na hilo wanalifanikisha na kuondoka kifua mbele.

Majonzi yanatawala kila mahali. Mzee Majige alijulikana kwa kuendesha makampuni makubwa yaliyotapakaa nusu ya nchi ya Tanzania. Ajira alizozimwaga zinakuwa sababu ya watu wengi kulia na kusikitika sana kutokana na kifo chake.

Kwa Faraja hilo lilikuwa ni pigo zito mno moyoni mwake. Ni kama mpigaji alikuwa anajua apige wapi. Naye akapiga palepale. Hakuna wakati ambao ulimfanya Faraja ajisikie kufa kama huo. Ni kweli matatizo yalikuwa sehemu ya maisha ya kila siku, lakini vifo vya wazazi wake, havikuwa sehemu ya fikra zake. Vilitokea mapema sana.

Polisi walileta taarifa za vifo vile baada ya uchunguzi. Ni kweli waliuawa lakini hakukuwa na maana yoyote kwani muuaji hakupatikana na wala mtumaji wa wauaji hakujulikana. Kuipa familia Mzee Majige moyo, wakasema upelelezi bado unaendelea.

Kesi ikawa imekwisha namna hiyo. Hakuna aliyekuja kutoa taarifa wala ndugu wa mrehemu kufuatilia mauaji ya ndugu zao. Ni Faraja pekee ndiye aliyekuwa anahangaika. Lakini angehangaika mpaka lini? Huku ana mtoto, kule ana lawama za mumewe. Na vipigo  navyo vikawa sehemu ya maisha yake. Angemudu vipi?

Angemudu vipi kwenda kituo cha polisi na majeraha? Angeulizwa alipoyapata, angejibu nini?

Licha ya kuchukia matendo ya mumewe, lakini bado alikuwa anamuhitaji, anamuheshimu na pia anamjali kama mwanaume pekee aliyewahi kuwa naye maishani. Mwanaume wa kwanza kuujua mwili wake. Sababu hizi zikamrudisha nyuma na kuamua kutulia huku akisubiri lolote kutokea.

Likizo ya kuhani msiba wa wazazi wake ilipokwisha, alirudi kazini na kukuta umiliki mpya wa makampuni ya wazazi wake. Nyaraka mbalimbali zilibadilishwa na baadhi ya ndugu zake.

Hakujulikana tena kama mwanasheria wa kampuni. Waliwekwa wanasheria wengine ambao hata alipofuatilia mahakamani na sehemu zingine za sheria, bado wale waliowekwa, walionekana ni halali na  si yeye.

Kampuni moja pekee ndio ambayo ilishindwa kuchukuliwa. Nyingine tano ziliobebwa kirahisi mno. Na ni afadhali labda zingekuwa kampuni pekee. Nyumba na mali zingine nyingi zilipewa umiliki wa ndugu hao. Faraja akabakizwa mchache kwenye umiliki wa mali za wazazi wake. Akabaki na nyumba anayoishi ambayo nayo ilikuwa na jina la mumewe na la kwake.

Pia kulikuwa na kampuni moja ambayo mama yake aliipa umiliki wa Faraja. Hiyo ndio pekee ikabaki pamoja na nyumba nyingine ambayo si mumewe wala nduguze wengine waliifahamu. Ilikuwa ni yeye na wazazi wake. Mara kwa mara alipelekwa kwenye nyumba hiyo kwa ajili ya kufurahi na kuondoa mawazo. Hiyo ikabaki ni siri yake. Na hakutaka kuifichua wakati huo.

 

****