Sarafu ya Gavana
Wilbard Makene
Boniphace alikunja mkono na kisha kuuelekeza upande wa kushoto wa kichwa. Spika ya simu alilengesha vizuri sikioni. Alimeza mate kulainisha koromeo lake, kisha akasema, “Ameshafika ila amekuta mlango wa mbele umetiwa kufuli. Amegonga kengele bila mafanikio.”
Kabla hajajibiwa simuni, Boniphace alichungulia nje ili kuhakikisha hakuna anayemsikia wala kumwona. Alipojiridhisha, akarudisha uso ndani. Makwapa yake yalilowa jasho kwa hofu, moyo ulimwenda mbio, miguu iliyokuwa imeachia breki za gari ilikuwa ikitetemeka kama mcheza kiduku.
Kiyoyozi cha gari hakikufua dafu kuzituliza tezi za jasho kutoa taka. Boniphace alijitahidi kuficha kilichoendelea ndani ya akili yake, lakini mwili ulimsaliti; kila kiungo cha mwili, kuanzia utosini hadi kidole cha mwisho cha mguuni, vilidhihirisha wazi kile kilichokuwa kikiendelea kichwani mwake.
“Sina hakika na usalama eneo hili,” Boniphace alindelea kuongea huku akimwangalia bosi wake, Gavana wa Benki Kuu ya Weusi Kusini.
Boniphace alikuwa amemaliza kumshusha kwenye gari Gavana aliyekuwa ametoka kazini. Kiutaratibu na kulingana na mafunzo aliyopewa, Boniphace alitakiwa kuhakikisha bosi wake anaingia ndani akiwa salama kabla ya yeye kuondoa gari. Aliendelea kumtazama Gavana akitembea hadi alipoufikia mlango. Gavana aligonga kengele mara kadhaa bila kufunguliwa.
Boniphace, akiwa yu-ndani ya gari na simu sikioni, aliendelea kuzungumza, “Mimi mwenyewe sina hakika na usalama wangu mahali hapa.”
Mtu aliyekuwa akizungumza naye simuni akajibu, “Acha woga, endelea kufanya kazi. Kila kitu kitakuwa sawia. Maelekezo mengine nitakupa baadaye.”
Simu ikakatwa.
Boniphace alitoa mkono sikioni, na kuuelekeza mfuko wake wambele. Aliiachia simu itulie iserereke kuelekea ukingo wa mfuko.
Baada ya Boniphace kuuondoa mkono wenye simu sikioni, na kuiweka simu kwenye mfuko wa suruali yake, alirudisha macho kule mlangoni alikosimama Gavana. Bado mlango ulikuwa haujafunguliwa.
Hali hiyo ilimtatiza Boniphace, hakujua kama ni hali ya kawaida tu hivyo anaweza kuondoka. Ni hali tatanishi hivyo anapaswa kwenda kutoa msaada.
Laiti angelijua, asingeliendelea kupoteza muda kwenye gari.
….
Boniphace ni kijana wa makamo, mcheshi na asiyependa makuu. Alikulia katika familia duni kijijini Iyovu, mkoani Iringa. Alipata elimu ya msingi, na kuhitimu elimu ya sekondari kwa kupata daraja la tatu. Alimaliza elimu ya sekondari miaka ya tisini. Ni katika kipindi hicho, Serikali ilikuwa na shule chache. Ufaulu daraja la kwanza na la pili ndiyo uliopewa kipaumbele. Hilo lilisababisha ashindwe kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita. Hata hivyo, aliweza kujiunga na shule za maarifa ya jamii. Alichukua fani ya udereva. Alipohitimu aliajiriwa serikalini. Akiwa kazini, alijiendeleza katika fani hiyo ya udereva. Akapata daraja la umahiri na kuajiriwa na Benki Kuu. Tofauti na vijana wenziye wengi hapo kazini, walioendekeza anasa,
Boniphace alikuwa na nidhamu ya pesa. Kiasi kidogo alichopata kwa mshahara, alikitumia kwa mahitaji ya msingi, pamoja na kuwatunza wazazi wake. Mara zote alizowatumia pesa wazazi wake, alitumia muda huo pia kuwajulia hali. Wazazi walimpenda sana na kumwombea dua kila uchao.
Mbali na kuwasaidia wazazi wake, pia alikuwa akiwasomesha wadogo zake. Majukumu mazito ya kifamilia yalimfanya kuwa makini na mwenye nidhamu kwenye maisha. Hakutaka kabisa kuwa sababu ya kuwaangamiza wazazi na nduguze. Lakini kuna mzigo wa siri, alioubeba kwa muda mrefu, akihofia kuutoa kwa kuchelea kuangamia yeye na familia yake, ulimsumbua sana kichwa kiasi cha kuanza kukata tamaa.
Alifanikisha kuificha siri hiyo kama mwanaume kubeba ujauzito. Tofauti ni kwamba, ujauzito unaonekana kwa wote lakini siri haionekani kwa macho, na mara nyingi, ujazito huleta neema ufikiapo tamati, walakini siri huleta madhara kwa mtunzaji endapo itatoka nje.
Mara chache, Boniphace alipojaribu kuwashirikisha watu wake wa karibu, aliishia kupigiwa simu zikitoa onyo kwake kuacha mara moja tabia hiyo. Ujanja wake wa mjini pamoja na mwili wake uliojengeka kimazoezi havikumfanya athubutu kukabiliana na genge hilo lililomsakama. Nguvu zake binafsi dhidi ya genge hilo ilikuwa ni sawa na tone la maji katika bahari.
*****
Annakova Boris alikuwa amejilaza kizembe kwenye kochi wakati simu ya mezani ilipoita. Alijiinua na kwenda kupokea. “Hallo,” alisema baada ya kuinua mkonga na kuubandika sikioni.
“Naweza kuzungumza na Anna?” Sauti kavu ilijibu upande wa pili wa simu.
“Ndiye anayeongea hivi sasa,” Anna alisema kwa utulivu. “Nani mwenzangu?”
“Good,” sauti ile upande wa pili ilisikika tena. “Napiga simu toka Ikulu ya Kremlim!”
Kimya kikatanda.
Kupokea simu kutoka Ikulu ya Kremlim lilikuwa jambo zito sana. Anna alijua wazi kuna tatizo sehemu.
Kabla hajajua ajibu nini, sauti ile ikaendelea, “Unahitajika Kremlim haraka iwezekavyo, Okay? Sihitaji kurudia mara mbili kwamba ni haraka!”
Simu ikakatwa.
Anna alirudisha mkonga wa simu mahala pake. Akarudi kochini na kujibwaga. Haikuchukua hata dakika moja, akasimama tena na kuelekea bafuni kwa ajili ya kujisafi mwili, tayari kuanza safari ya Kremlim.
Annakova Boris, almaarufu kama “Mwanamke wa Chuma” ni mwanamke shupavu asiyemithilika. Alipigana Vita Vikuu vya Pili vya dunia, baadaye alikwenda kutumikia jeshi kama shushushu. Aliaminika na viongozi wengi kwa namna alivyokuwa tayari muda wote kutekeleza amri kutoka kwa wakuu. Katika mapambano ya Vita Vikuu vya Pili ya dunia. Alipoteza figo moja ili kuokoa maisha ya askari mwenzake aliyejeruhiwa vibaya na figo zake zote kuharibika. Serikali ya Urusi ilimpeleka nchini Cuba kusomea masomo ya Kemia, na hatimaye kuhitimu shahada ya uzamivu. Huko alijifunza masuala muhimu ya uchanganyaji kemikali kwa matumizi mbalimbali ya kiusalama. Baadaye alirudi Urusi kuendelea na kazi zake za ushushushu jeshini.
Akiwa bafuni anaendelea kujisafi mwili, Anna alisikia sauti toka sebuleni. Mlango wa sebuleni uligongwa. Alitupa dodoki chini na kufungua maji yatiririke kwenye mwili wake kuondoa povu. Kisha alijifunga taulo haraka na kukimbilia sebuleni.
Alipofika sebuleni, alisikia tena mlango ukigongwa.
“Nakuja,” alijibu huku akikimbia chumbani kujisitiri mwili na kujiweka tayari. Kwa haraka alivalia fulana nyeupe na jinzi ya bluu. Kisha, alianza kupiga hatua kuelekea sebuleni. Alipoufikia mlango, kabla hajafungua wala kumfahamu mtu aliyekuwa mlangoni, akasema, “Samahani kwa kukuweka mlangoni muda mrefu!”
Hakujibiwa.
Hilo lilimshitua kidogo. Hivyo, kabla hajafungua mlango, alihoji, “Nani mwenzangu?”
Kimya!
“Hallo!” aliita tena.
Kimya tena.
Mlango ulikuwa na tundu lililowezesha kuchungulia nje. Alisogeza kichwa chake. Kisha, kupitia tundu hilo, alichungulia nje. Mlio mkubwa ulisikika mlangoni. Vipande vya mbao vilivyokuwa vimezunguka sehemu ya tundu la kuangalizia nje vilisambaa na kuacha tundu kubwa. Kwa bahati, Anna alikwishagundua hila za mvamizi wake, na akawahi kuruka pembeni. Kisha, kwa umakini mkubwa, aliamka na kusogea kuelekea ulipokuwa mlango huku akiwa na bastola mkononi.
Alipoufika mlango na kuangalia nje kupitia tundu kubwa lililotengenezwa, aliliona gari aina na Mercedes Benz lililokuwa sehemu ya maegesho–upande wa pili wa barabara, likirudi nyuma na kuondoka kwa kasi.
Ni akina nani hawa na kwa nini wadhamirie kunidhuru? Anna aliwaza, huku akijaribu kulihusianisha tukio hilo na ile simu toka Kremlim aliyotoka kupokea muda mfupi nyuma.
*****
Baxter aliinuka toka kitini. Akajongea kuelekea meza iliyokuwa pembeni. Meza ilikuwa ndogo, tofauti na iliyotumika kufanya mazungumzo. Alipofika, akafungua chupa ya chai na kisha kuiinamisha.
Maji moto yalitiririka katika kikombe kidogo kilichokuwa chini ya chupa. Kilipojaa, akarudisha chupa wima na kuifunga. Akaweka kijiko kimoja cha kahawa na kingine cha sukari, akakoroga na kisha akabeba kikombe kidogo mkono wa kulia na kijiko mkono wa kushoto. Alipofika alipokuwa amekaa rafikiye wa siku nyingi, Alister, alisimama. Akashusha kikombe cha chai mezani, mbele ya Alister, huku akisema, “Karibu sana.”
Baxter alijongea sehemu yake ya kuketi na kisha kuketi huku akimwangalia Alister. “Benki ya Ulaya imepata ombi kutoka kwa Rais Bonge wa Jamhuri ya Weusi Kusini,” Baxter alinza mazungumzo.
“Mhhh..” Alister aliitikia.
“Anahitaji mkopo wa dola za Marekani bilioni moja ili kuongeza nguvu kwenye vita.”
“Sijasikia kama ana vita!” Alister alibisha.
“Si vita yake; ni ile anayowasaidia nchi ya Matoke, Kaskazini-
Magharibi mwa nchi yake,” Baxter aliongeza, “Endapo akishinda, Bonge atakuwa amejiongezea ushawishi katika kanda ya maziwa makuu na hata nchi za Kusini mwa Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa ujumla.”
Baxter aliendelea, “Kuna uasi umezuka nchini Matoke, na hivyo Bonge anajitahidi kadri iwezekanavyo kushirikiana na Rais wa Matoke, kuzima uasi. Lakini ajenda kubwa ya Bonge ni kuleta amani eneo la maziwa makuu, kwa namna hiyo atakuwa ameongeza ushawishi wake.”
“Unadhani mkopo utalipika?” Alister aliuliza. “Na kama utalipika, tunatumia mbinu gani kuwaeleza bodi ya wakurugenzi kwamba, mkopo kwa Rais Bonge utalipika?” Alister alisisitiza.
“Hilo niachie mimi,” Baxter alijigamba.