Sihusiki
Hamis Kibari
JACKSON Malima, alitoka bafuni na kuangalia saa yake iliyomwonesha kwamba ilikuwa inaelekea saa mbili usiku. Akiwa bado amejifunga taulo, aliamua kuangalia taarifa ya habari kabla ya kutoka kama alivyokuwa amepanga.
Kwa takribani siku sita alizokuwa Tanga, alikuwa hajaangalia taarifa ya habari ya usiku kama ilivyo kawaida yake anapokuwa nyumbani kwake Dar es Salaam kutokana na kubanwa na ratiba.
Alipokuwa akitoka kwenye semina jioni, alilazimika ama kuandaa kile atakachowasilisha kesho kwenye semina au kwenda kutafuta chakula cha usiku alikotumia muda huo kubadilishana mawazo na wenzake.
Alishagundua kwamba pale kwenye klabu alipokuwa akienda kupata chakula cha usiku, mbali na kukosa utulivu hata kama angeomba wahusika waweke taarifa ya habari wasingemwelewa kwani kilichokuwa kinapendelewa zaidi na wengi ni mpira wa miguu au muziki.
Aliwasha seti ya runinga katika chumba chake alimofikia katika nyumba ya kulala wageni ya Twiga Executive Lodge na kuketi kitandani.
Taarifa ya habari ilimkaliza chumbani humo hadi saa tatu kasorobo alipozima runinga. Alivaa suruali ya michezo, tisheti ya rangi ya maziwa na raba kisha akatoka baada ya kuhakikisha kwamba hajasahau kuchukua fedha kidogo kwa ajili ya matumizi ya usiku huo.
“Binti, natoka kidogo,” alisema akikabidhi funguo za chumba chake kilichokuwa kimepewa jina la Kigoma kwa binti aliyekuwa mapokezi. Akaondoka.
Nyumba ya kulala wageni aliyofikia, kama zilivyo nyingine nyingi mjini Tanga, ilikuwa haiandai chakula cha mchana wala usiku zaidi ya kifungua kinywa asubuhi. Wateja walikuwa wakielekezwa kwenda kutafuta chakula katika hoteli, klabu au migahawa ya karibu.
Chakula cha mchana, Jackson na wanasemina wenzake walikuwa wakikipata katika Hoteli ya Kitalii ya Mkonge walikokuwa wakifanyia semina yao ya wiki moja ambayo sasa ilikuwa inaelekea ukingoni, huku yeye na wenzake wakilazimika kujitafutia chakula cha usiku.
Jackson alikuwa ameamua kukaa katika nyumba hiyo ya wageni kutokana na kuwa eneo tulivu huku wenzake wanne aliotoka nao ofisi moja wakiamua kukaa katika nyumba za wageni zilizoko katikati ya jiji la Tanga.
Hao wenzake walikuwa wanywaji wa pombe na wapenda wanawake lakini yeye alikuwa akijitahidi sana kujitenga na mambo hayo, hali iliyofanya apachikwe na baadhi ya wafanyakazi wenzie jina la Baba Mchungaji.
Hata hivyo, baada ya semina mara nyingi alikuwa anakutana na wenzake hao pamoja na wanasemina kutoka taasisi zingine zilizokuwa zinashiriki kwenye semina hiyo usiku katika klabu ya Tanga Raha ambayo haikuwa mbali sana na alikokuwa amefikia.
Klabu hiyo ilikuwa inachangamka sana, hasa nyakati za usiku kutokana na kuandaa vyakula vya aina mbalimbali pamoja na vinywaji.
Lakini kitu kilichokuwa kinavutia wateja wengi hususani wanaume ni uwepo wa wasichana warembo, wengi wakiwa ni wale waliojaaliwa kuwa na maumbo halisi ya Kiafrika.
Wasichana vimbaumbau pia walikuwepo wachache lakini wengi walikuwa ni wale ambao utadhani meneja wa klabu hiyo alikuwa akipita nchi nzima akisaka mabinti warefu, wenye sura za kuvutia na makalio makubwa. Ilikuwa wastani wa takribani dakika nane kutembea kwa miguu kutoka nyumba ya wageni alimofikia Jackson hadi Tanga Raha Club kama bango lake lilivyokuwa linasomeka.
Wakati Jackson anafika kwenye klabu hiyo usiku huo, nje kulikuwa na magari mengi kiasi kwamba yeyote aliyekuwa akija kwa gari muda huo alilazimika kwenda mbali kidogo kuegesha gari lake.
Ndani pia palikuwa tayari pamejaa watu kiasi kwamba upatikanaji wa viti ulianza kuwa wa shida.
Jackson alisimama pembeni karibu na mlango mkubwa akiangaza mahala ambapo anaweza kuona kiti aende kukaa. Kwa kawaida mwanga wa ndani ya klabu hiyo ambayo mchana ukipita unaweza kudhani ni godauni au gereji, ulikuwa si mkubwa sana. Wakati mwingine mpaka umkaribie mtu ndipo unamtambua.
Aliangaza huku na kule akitafuta pia kuwaona wanasemina au wafanyakazi wenzake katika Tume ya Teknolojia na Mawasiliano (TTM) ili kuungana nao lakini hakuona yeyote, labda kutokana na mwanga hafifu wa mahala pale.
Alikuwa hana hakika pia kama mfanyakazi mwenziye na rafiki yake wa karibu, Andrew Mambo, alikuwa ameshawasili ama la. Alisogea pembeni na kupiga simu yake lakini hakupokea.
Mara aliona wanasemina wawili wakiongozana na walipofika pale alipokuwa amesimama karibu na mlango, wakamsalimia na kusema wanahamia kwingine. Alipoangalia mahala walipotokea, akaona watu wengine wakiwahi viti walivyoviacha. Ilikuwa ni sehemu ambayo wapenzi wa mpira wakikaa wanaona vizuri kutokana na skrini kubwa iliyokuwa mahala hapo.
Wakati bado anaangaza macho huku na kule, msichana mmoja, mhudumu wa klabu hiyo, alimfuata na kumshika mkono.
“Habari kaka… Twende nikuoneshe mahala pa kukaa.”
Jackson aliandamana naye, hiyo ikiwa ni mara ya tatu au zaidi kuhudumiwa naye na sasa bila shaka kila mmoja wao alikuwa ameshamkariri sura mwenzake.
Ni msichana ambaye kwa mtazamo wake alikuwa mrembo kupita wote katika klabu hiyo. Hata siku ya kwanza alipomwita amhudumie, binti huyo maji ya kunde ‘alimtikisa’ vilivyo Jackson lakini akaheshimu maadili aliyojiwekea.
Ukiwa ni mwaka wa 15 tangu afunge ndoa, Jackson alikuwa hajawahi kwenda nje ya ndoa yake. Mbali ya kumwogopa Mwenyezi Mungu anayewakataza viumbe wake kuzini katika vitabu vyake vyote, Bibilia na Kurani, Jackson alikuwa hafikirii kwamba kuna siku atamsaliti mkewe mpenzi, Salome Bakunda. Ni mwanamke aliyempenda na kumridhisha kwa kila hali na hivyo hakuona sababu ya kuchepuka kama alivyokuwa akiona kwa wenzake akiwemo rafiki yake, Andrew.
Isitoshe, yeye alikuwa mshauri mkubwa wa wafanyakazi wenzake, hususani vijana waliokuwa wakianza kazi katika ofisi yao kuhusu kuzingatia maadili bora ya kazi, kujiheshimu, kuacha zinaa na kufanya yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
“Kaka, inaonekana wewe hunywi lakini nadhani leo utanipa offer ya bia moja tu, yaani nina kiu sana kaka yangu… Nakuomba,” alisema yule binti baada ya kumpeleka kwenye meza moja iliyokuwa kwenye kona, upande wa kulia wa klabu hiyo kutoka lango kuu la kuingilia.Katika meza hiyo kulikuwa na viti vingine viwili vitupu lakini kule eneo la kuingilia alikokuwa amesimama awali alikuwa hawezi kupaona.
“Bia moja tu mdogo wangu, haya, nitakununulia…”
“Asante sana kaka… Enhe, nikuletee nini?”
“Nitapata kuku nusu wa kienyeji wa kuchoma na ndizi mzuzu mbili za kuchoma pamoja na mbogamboga?”
“Bila shaka kaka,” alijibu yule msichana akiachia tabasamu pana lililoanza kumgusa Jackson.
Alitoa Sh 20,000 na kumuuliza kama kiasi hicho cha fedha kinatosha chakula alichoagiza na bia aliyoomba. Alijibu kwa bashasha kwamba kinatosha sana.
“Je, nikitaka soda pia ili niwe navutia muda wakati nasubiri kuku wangu, pesa inatosha?”
“Bado inatosha na chenji inarudi.”
“Basi niletee soda ya moto,” alisema kisha msichana yule ambaye muda wote alikuwa amesimama, akageuka na kuondoka.
Sasa Jackson, Mwanasheria Mkuu wa Tume ya Teknolojia na Mawasiliano (TTM), alipata wasaa mzuri wa kumtazama kwa nyuma na kung’amua kwamba uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ulikuwa umekamilika vilivyo kwa kiumbe wake huyo.
Aliendelea kumsindikiza kwa macho hadi alipopotelea katika eneo la jiko na hivyo akabaki anajiuliza inakuwaje msichana mrembo kiasi kile alikuwa akifanya kazi ile ambayo yeye aliiona dhalili. Kwa mtazamo wake aliona kwamba msichana huyo alipaswa awe ametulia kwa mumewe au akifanya kazi yenye staha zaidi.
“Hivi wazazi wa hawa wasichana walio humu klabu wanaweza kuwa akina nani hasa? Wamewasomesha kiasi gani watoto wao? Je, wameridhia kuona mabinti zao warembo kama huyu wanafanya kazi hii ya kibaamedi?” Alijiuliza lakini akajijibu pia kwamba kimsingi kazi ni kazi tu na katika mgawanyo wa maisha lazima pia kuwe na mgawanyo wa kazi na kwamba kimsingi hakuna kazi dhalili.
Aliuonya pia moyo wake uache kudharau kazi za wengine huku akijiuliza hali ingekuwaje kama kusingekuwa na wahudumu kama huyo binti na wenzake katika klabu hiyo?
Pamoja na kukiri kwamba hakuna kazi bora kuliko nyingine bado, hakutaka siku moja watoto wake wawili, wote wa kike, Hellen na mdogo wake Hilda, wafanye kazi ya baa.
Wakati bado akiwaza kuhusu binti huyo na wenzake kwenye klabu hiyo, alimwona akirejea na kisha akaweka chupa ya soda mezani. Akamfungulia soda, akamkaribisha kunywa.
“Naitwa Eggy… Agness kama utanihitaji… Nitaleta chakula ulichoagiza kikiwa tayari punde, karibu kaka na asante sana.”
“Nilidhani unakuja na wewe kunywea bia yako hapa?” Alijikuta akiuliza neno ambalo wala hakulitegemea na haikuwa kawaida yake.
“Sasa hivi meneja haturuhusu kukaa. Nitakuja tu baadaye kaka, asante sana kwa bia,” alisema Eggy na kumpa chenji iliyobaki, kisha akaondoka. Kama kawaida, Jackson alijikuta tena akiwa na kibarua cha kumsindikiza kwa macho kutokana na kuvutiwa na umbo lake hadi alipoitwa kwenye meza nyingine kwa ajili ya kutoa huduma.
Dakika chache baadaye, Jackson alimwona Mhandisi Mkuu wa TTM, Bruno Mapunda, akipita karibu yake akiwa na mkoba kama vile anatafuta mtu au mahala pa kukaa. Ilionekana kwamba hajafika hotelini alikokuwa amefikia tangu kumalizika kwa semina jioni.
Bruno alimkaribia kabisa lakini akageuka na kwenda uelekeo mwingine bila kumwona au alimwona bila kumtambua. Jackson akashukuru kwa sababu hakutaka kukaa naye kama ilivyokuwa imetokea jana yake ambapo Bruno alilazimisha kwenda kukaa naye.
Wawili hao hawakuwa na uhusiano mzuri kazini na hasa kutokana na kila mara Jackson kusikia Bruno akimsema vibaya na kukejeli kila alichokuwa akikifanya.
Baada ya dakika takribani 25 za kusubiri huku muda mwingi akisoma mitandao ya kijamii hususani Facebook na Whatsapp, Jackson alishituliwa na Eggy aliyekuwa akiweka sahani ya nyama ya kuku wa kuchoma kwenye meza aliyokuwa ameketi.
“Nikuletee maji ya kunawa au utakwenda pale kunawa?”
“Nitakwenda mwenyewe. Usiwe na wasiwasi,” alijibu Jackson akinyanyuka kwenda kunawa huku Eggy akibaki akilinda chakula kile.
“Uliomba bia, lakini vipi kuhusu chakula, wewe tayari?” Alihoji Jackson wakati aliporejea na kuketi.
“Sijala na nitashukuru sana kama utanipa offer nyingine ya chakula kaka’ngu,” alijibu Eggy.
“Utapenda kula nini?”
“Mchemsho wa kuku.”
“Basi agiza,” alisema huku akimpa yule msichana noti ya shilingi 10,000 na kumuuliza kama kiasi kile kilikuwa kinatosha. Eggy alijibu kwa kichwa kuashiria kwamba kiasi kile kilikuwa kinatosha.
Wakati akiendelea kula, Eggy alikuja pale mezani kwake akiwa na bakuli la mchemsho wa kuku na kuketi kisha akaanza kula.
“Wakati ule ulisema huwezi kukaa kwa sababu meneja anawazuia imekuwaje sasa umekaa?”
“Meneja mwenyewe yuko kule anakula. Ngoja nile haraka haraka kabla hajaniona.”
“Kwani nyinyi wahudumu mnakula saa ngapi?”
“Tunakula baada ya kazi, mara nyingi kwenye saa sita usiku… Unadhani tunakula basi, tunalambalamba tu kwani mara nyingi chakula hakitoshi. Usipokula kama hivi ndio unajikuta wakati mwingine unalalia mchuzi wa makongoro na kipande cha ndizi.”
“Wewe unaishi wapi?”
“Nimepanga chumba hapo mtaani, mimi na mwenzangu ambaye tunafanya kazi naye hapa.”
“Ni mwenyeji wa wapi?”
“Mimi ni mwenyeji wa hapa hapa Tanga, Mdigo. Asili yetu ni kule Chongoleani, si mbali sana kutoka hapa mjini.”
“Wazazi wako wapo?”
“Hapana, wazazi wangu walikufa nikiwa mdogo na sehemu kubwa nimelelewa na bibi yangu.”
“Pole sana,” alisema Jackson na sasa maswali yake kuhusu kinachoweza kuwa kimemsibu msichana huyo mrembo kuhusu maendeleo yake kielimu yakianza kupata majibu.
Alimwomba Mungu ampe maisha marefu ili asomeshe watoto wake, mkubwa wakati huo akiwa darasa la nne na mdogo darasa la kwanza, hadi kiwango cha chuo kikuu.
“Una mchumba Eggy?”
“Hapana, niliwahi kuishi na bwana mmoja lakini nikaona hana mwelekeo. Nikaamua kuachana naye.”
“Ukisema alikuwa hana mwelekeo unamaanisha nini?”
“Alikuwa amesoma lakini mvivu, hafikirii maisha na anataka tuendelee kuishi kwao. Nikaona ananipotezea muda wangu bure.”
“Ulizaa naye mtoto?”
“Hapana, lakini ninaye mtoto ambaye nilizaa na bwana mwingine kabla ya kukutana na huyo jamaa.”
“Vipi mtu akianzisha kitu kama mgahawa Dar es Salaam, kisha akakuchukua ukafanye kazi huko unaweza kuja?”
“Kwa nini nisije kama maslahi ni mazuri kuliko hapa? Isitoshe nimeshachoka na maisha ya Tanga.”
“Ninao mpango wa kufungua mgahawa Dar. Nikifikia hatua hiyo nitakutafuta ingawa sijui mke wangu atafikiria nini kuhusu msichana mrembo kama wewe, lakini ananiamini. Hana mashaka na mimi.”
“Mimi niko tayari hata kesho… Naona bosi keshamaliza kula. Ngoja nimalizie kuku wangu haraka haraka niondoke.”
“Ratiba yako ya leo baada ya kazi ikoje?”
“Hapa tunamaliza kazi kati ya saa tano na nusu na saa sita usiku… Wewe umefikia wapi?”
“Mimi niko hapo Twiga Executive Lodge.”
“Nitakuja baada ya kazi. Uko chumba gani?”
“Chumba kimoja kinaitwa Kigoma.”
“Aha, Kigoma mwisho wa reli! Basi nitakuja… baadaye nitakuletea namba yangu ya simu au unaweza kuinakili harakaharaka?”
“Nitajie.” Agnes alimtajia namba zake za simu kisha Jackson alipozinakili, akambipu na msichana huyo akahifadhi za kwake pia.
Alinyanyuka na kuondoka bila kumalizia chakula chake sawasawa baada ya kumwona bosi wao aliyekuwa amesimama katikati mwa ukumbi wa klabu hiyo akiangaza huku na kule.
Jackson aliendelea kula chakula chake taratibu huku akianza kujilaumu kwa kufanya jambo ambalo siyo sahihi sana, la kuwa karibu na msichana yule hadi kupeana ahadi ya kukutana baadaye.
“Hivi nimekuwaje leo, au ndio nimeshalishwa limbwata la Tanga?” Alijiuliza. Akapanga kwamba baadaye atarekebisha kile alichopotoka kwa maana ya kumzuia msichana huyo kwenda chumbani kwake.
Wakati anamaliza kula, mchezo wa mpira wa miguu uliokuwa unasubiriwa usiku huo wa vilabu mahasimu nchini Hispania, Real Madrid na Barcelona ulikuwa ndio unaanza huku skrini kubwa sita ndani ya klabu hiyo zikiuonesha. Yeye alikuwa jirani na skrini moja wapo na hivyo hakuwa na sababu ya kugeuka au kuhama kama alivyoona kwa baadhi ya wapenzi wengine wa mpira.
Toka jana usiku walipokuwa kwenye klabu hiyo na Andrew pamoja na Bruno aliyelazimisha kwenda kukaa nao, walipanga kwamba wangekuja kutazamia hapo mchezo huo na siyo vyumbani.
Kilichokuwa kinampa jeuri zaidi kuchelewa kwenda kulala hata kama angelikaa hadi klabu hiyo kufungwa ni asubuhi yake, siku ya Ijumaa ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya semina yao, kutokuwa mmoja wa wawasilishaji wa mada.
Semina hiyo ambayo ilikuwa imeandaliwa na ofisi yao kwa ajili ya taasisi na wadau kadhaa wanaofanya kazi kwa karibu na TTM yakiwemo makampuni ya simu, ilihusu mambo mbalimbali ya maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Duniani (Tehama) na jinsi nchi inavyoweza kunufaika zaidi na teknolojia hiyo.
Yeye kama mwanasheria wa tume, alikuwa na kazi kubwa ya kuelezea sheria za nchi na za kimataifa zinazohusiana na suala zima la matumizi ya Tehama. Pia alikuwa akitoa elimu, kuhusu sheria ya makosa ya mitandaoni na ya vyombo vya habari, hususani vya kielektroniki.
Wakati akiendelea kutazama mpira huku kelele ukumbini zikiwa zimeongezeka kutokana na ubishi au kutambiana baina ya wapenzi wa vilabu hivyo, alikuwa pia akimwangaza Eggy. Alipomwona alimwita kwa ishara na alipofika akamwagiza amletee juisi ya embe.
Kabla Eggy hajaondoka kwenye meza yake kumfuatia juisi, Bruno alikuwa anafika na kumzuia Eggy kuondoka.
“Usiondoke kwanza mrembo,” alisema Bruno akiketi katika kiti kilichokuwa wazi na kisha akamsalimia Jackson kwa bashasha.
“Karibu mkuu,” Jackson alimkaribisha sasa akihisi kwamba pengine Bruno alikuwa ameamua kuweka mbali hali ya uhasama baina yao, hususani katika kipindi hicho ambacho baada ya semina hiyo kulikuwa na tukio kubwa ambalo Jackson alihisi litazidi kuwafanya wahasimiane zaidi. Tukio la Mkurugenzi wa TTM kustaafu huku waliotazamiwa kukaimu nafasi yake wakiwa ni mmoja kati yao.
“Nimefurahi kugundua uko hapa Malima,” alisema Bruno kisha akamgeukia Eggy aliyekuwa amesimama akisubiri maelekezo.
“Mrembo, nifuatie bia yangu kwenye meza ile pale. Niletee na ule mkoba wangu,” Bruno alimwelekeza kwa kidole na Eggy akaiona meza moja iliyokuwa katikati ya ukumbi ambayo alibaki mwanaume mmoja akiendelea kunywa.
“Haya mheshimiwa,” alijibu Eggy na kuondoka.
Bruno, mmoja wa watu waliompokea Jackson kazini takribani miaka 12 iliyopita, aliketi na kumweleza Jackson kwamba angetamani kuona siku moja wanashirikiana katika kunywa pombe pamoja.
“Hivi starehe yako kubwa ni ipi Malima… Ina maana hujawahi kunywa pombe maishani mwako?”
“Sijawahi kunywa na wala sitarajii kunywa,” alijibu Jackson. Bado alikuwa akitafakari mabadiliko ya Bruno katika siku mbili hizo akikumbuka hali ya uhasama baina yao iliyokuwa imeongezeka kabla ya kuondoka Dar es Salaam kwa ajili ya semina hiyo.
Jackson alikuwa amesikia maneno mengi mabaya yakisemwa na Bruno juu yake baada ya kuwepo kwa uvumi kwamba Mkurugenzi wa TTM aliyekuwa anastaafu, Ibrahim Matakwali, alikuwa anafikiria kumpendekeza yeye Jackson kwenye Bodi ya Tume kukaimu nafasi yake ya ukurugenzi.
Sasa aliona hana sababu ya moyo wake kuendelea kusinyaa dhidi ya Bruno ambaye inaonekana alikuwa ameamua kukunjua moyo wake kwake.
Akiwa amevaa tisheti nyekundu kama wahudumu wenzake na suruali ya aina ya Jeans iliyombana na hivyo kuonyesha maumbile yake kwa uwazi, Eggy alileta bia aliyokuwa akinywa Bruno pale mezani na mkoba wake, kisha akaondoka kufuata juisi ambayo Bruno sasa alisema atailipia yeye.
“Hivi kesho hatuwezi kumaliza semina mapema tukaondoka na basi za jioni kurudi Dar?” Alianzisha mazungumzo Bruno akionesha kuchangamka.
“Kuwahi au kutowahi kumaliza itaanzia kwako endapo wasilisho lako halitakuwa na wachangiaji wengi na mawasilisho mengine mawili ya mwisho. Lakini kwa mtazamo wangu sioni sababu ya kuondoka kesho kurejea Dar kwa sababu wakati mwingine safari za usiku usiku si nzuri sana. Mimi nimeshaamua nitaondoka Jumamosi asubuhi.”
Eggy alileta juisi na kuiweka mezani, Bruno akamgeukia.“Mrembo, ninamjua huyu ndugu yangu ni mpenzi wa vitu vitamu, utamletea juisi nyingine, chenji utakunywa bia,” alisema Bruno akitoa noti ya shilingi elfu kumi.
“Asante sana mkuu. Hii moja inatosha,” alisema Jackson lakini Bruno akakataa, akamlazimisha Eggy kwamba akiona juisi aliyomletea Bruno inapungua amletee nyingine mara moja.
“Sawa mheshimiwa,” alijibu Eggy.
“Mkuu, soda au hizi juisi si kama bia ambazo ukikojoa inaisha mwilini. Hii ilikuwa inatosha kabisa,” alisema Jackson wakati Eggy akiondoka.
“Unadhani kwamba hadi mpira unaisha utakuwa hujaenda kujisaidia? Jana nilikuona ukienda msalani mara mbili wakati mimi ninayekunywa pombe nimeenda mara moja tu,” alisema Bruno.
Baada ya muda Eggy alirejea na bia akajiunga nao na kuendelea kunywa. Wakati wakiendelea kutazama mpira, kila mara Bruno alikuwa akimhimiza Jackson anywe juisi ili aletewe nyingine ambayo alikuwa keshailipia huku pia akifanya hivyo kwa Eggy.
Jackson alianza kuhisi kuwa Bruno keshachanganyikiwa kwa Eggy aliyekuwa akinyanyuka mara kwa mara kwenda kuhudumia wateja na kurejea.
Hata hivyo, kutokana na kukosekana kwa Andrew ambaye alihisi usiku huo alikuwa kaenda sehemu nyingine, Jackson sasa alijipangia kuondoka wakati wa mapumziko na kwenda kumalizia mtanange huo wa mpira chumbani kwake.
Kipenga cha mapumziko kilipopulizwa huku timu zote zikiwa hazijafungana, Jackson alinyanyuka kwenda kujisaidia na kumjulisha Bruno kwamba akirejea hatokaa sana.
“Mimi ninataka huyu bwana aendelee kukaa, hebu mfuatie juisi nyingine ya embe,” Bruno alimwagiza Eggy akimpa pesa na kumtaka aongeze bia nyingine mbili kwa ajili yao wawili.
Jackson alirejea kutoka msalani na kumwona Eggy akimhudumia mteja aliyekuwa jirani yao ambaye pia alionekana kumtaka msichana huyo.
Akashangaa kuona vinywaji vimeongezeka mezani huku yeye akiona ulikuwa muda mwafaka wa kuondoka ikiwezekana bila hata kumuaga Eggy.
Jackson aliamini kwamba Bruno aliyekuwa akiongea sana na kuwa tayari kumnunulia yeyote pale mezani chochote, ilikuwa ni moja ya mbinu za kumvutia kwake binti huyo mwenye haiba na umbo la kuvutia. Yeye alifurahia hilo.
“Mbona umeongeza juisi hata kabla hii haijaisha mkuu? Mimi naondoka hivyo,” aliuliza Jackson baada ya kuketi.
“Unawahi wapi na kesho huna wasilisho. Tuangalie mpira kidogo.”
“Hapana, ngoja nimalizie hii juisi niondoke. Hiyo siwezi kuinywa,” alisema na kushauri kwamba juisi ya boksi iliyoletwa ataichukua Eggy na kuinywa au kuigawa kwa sababu ilikuwa haijafunguliwa.
Wakati anapeleka mkono kuchukua juisi yake ili anywe mafunda mawili matatu kisha aondoke, kijana mmoja mlevi aliyekuwa akicheza pembeni mwa meza yao aliiangukia ile meza na kusababisha vinywaji vyote kumwagika.
Bruno alikuja juu na kumkwida shati yule kijana aliyekuwa akijitahidi kunyanyuka akimlazimisha kununua vinywaji vyao.
“Bahati mbaya father,” alisema kijana yule kwa sauti ya kilevilevi huku Bruno akiendelea kumkwida na kumtaka Eggy ambaye alikuja haraka pale mezani amwite meneja wa baa.
“Huyo kijana ni mlevi tunamfahamu hapa. Pengine hapo keshalewa gongo huko mitaani ndipo akaja hapa. Ninamjua hana uwezo wa kununua hivi vinywaji lakini akiwa hajalewa ni mkarimu sana,” alisema Eggy akimsihi Bruno amwache kwa sababu atamuua bure. Jackson pia alimsihi amwache.
“Mkuu mimi nakuacha. Lakini ngoja niwanunulie bia mimi,” alisema Jackson huku akisimama.
“Hapana acha tu… Mimi bado kidogo. Hii ndiyo sebule yetu hapa Tanga,” alisema Bruno na kumsihi sana Jackson aendelee kukaa.
Lakini alikataa akisema ataenda kumalizia dakika zilizobaki za mpira akiwa chumbani kwake
“Usiku mwema mkuu.”
“Hata hivyo, umejitahidi. Mpaka sasa bado uko hapa?” Alisema Bruno akiangalia saa yake. Ilikuwa inaelekea saa tano na robo usiku.
“Mpira ndio umenichelewesha… Haya kesho.”
“Sawa,” alijibu Bruno.
“Kaka naomba nikusindikize,” alisema Eggy akisimama.
“Binti, wewe bado uko kazini. Kaa na mkuu hapa utamsindikiza yeye.”
“Sasa hivi kazi zimepungua sana, hakuna wateja wapya wengi.”
“Ulikuwa unasemaje?”
“Ah, twende nikusindikize,” alisema Eggy akimshika mkono Jackson na kisha kuongozana naye.
Jackson alishangaa kugundua kwamba katika meza aliyokuwa ameketi awali Bruno, alikuwepo Andrew Mambo, Meneja Rasilimali Watu wa tume.
Alikuwa ameketi na msichana mwingine, mmoja wa wahudumu wa klabu hiyo.
“Vipi Andrew sikujua uko hapa. Kwa nini leo umejitenga nami… Lakini nimeshaona sababu!”
“Ah! Nipo na nilikuona wakati unaingia. Bruno alipokuja dakika mbili hivi baada ya wewe kuingia akakuulizia nikamwambia sijui ulipo ingawa nilikuona ulipokwenda kukaa na ilikuwa nikufuate. Nikaona anakutafuta lakini hakukuona, akarudi tena hapa na kukaa. Amekaa hapa akinikera mara nikaona anaamka na kisha nikaona anahamia kwako baada ya kukuona. Nadhani mambo yamekwenda vyema kuona mahasimu mnakaa tena meza moja. Nikaamua kuwaacha. Bruno kwa kweli simpendi na alipotoka hapa nikashukuru. Hata jana alinikera sana alipolazimisha kuja kukaa na sisi.”
“Naona ameamua kubadilika. Nadhani hatuna sababu ya kumtenga kama anataka ushirikiano.”
“Bruno abadilike! Labda pombe tu au anaigiza…”
“Aisee tutaonana kesho,” aliaga Jackson na kuondoka huku Eggy aliyekuwa amesimama pembeni wakati akizungumza na Andrew akijiunga naye tena kutoka nje ya ukumbi huo. Baada ya kupiga hatua kadhaa, Jackson alimgeukia Eggy na kumwambia inaonekana jamaa waliyemwacha pale mezani kwa maana ya Bruno anamtaka. Akasema yeye hana kinyongo na anamshauri kwa moyo mmoja akaungane naye.
“Ah yule bwana hana nyimbo.”
“Kwa nini unasema hana nyimbo?”
“Anapenda sana wanawake huyo mzee. Hapa anatongoza kila msichana. Mimi sipendi watu wa aina hiyo. Napenda watu wastaarabu kama wewe. Na nikipata bwana wa kunioa wa aina yako hata pombe nitaacha.”
“Kwani unamfahamu huyo bwana?”
“Nimeanza tu kumwona siku mbili tatu hizi lakini hii si mara yake ya kwanza kuja hapa klabu. Mwezi uliopita alikuwepo hapa pia.”
Jackson alijua Eggy anasema kweli kwani kipindi hicho Bruno alikuwa Tanga akishiriki semina nyingine.
“Unataka kusema hujawahi kuondoka naye?”
“Wala simtaki.”
“Acha masihara. Humtaki kwa lipi?”
“Basi tu… Yaani kila mara alikuwa ananikonyeza niondoke naye lakini nimemnong’oneza kwamba nina mtu tayari lakini yeye anang’ang’ana tu. Nimekusindikiza makusudi ili aone picha.”
“Ah! Nakushauri uondoke naye tu wala hamna shida kabisa… Ehe! Ulikuwa unasemaje?”
“Kwani wewe una mtu mwingine?”
“Hapana. Nakwenda tu kulala ila nimechoka sana.”
“Mimi nakutaka wewe na kama umechoka nitakuchangamsha… Ninaomba uniachie shilingi elfu mbili tu kwa ajili ya bodaboda nitakapokuwa ninakuja chumbani kwako.”
“Kama nilivyosema nimechoka sana na hivyo huna sababu ya kuja. Halafu hapo Twiga kama ukiamua kuja, bodaboda ya nini? Mbona mimi ninakuja hapa kwa mguu na kurejea kwa mguu?”
“We’ mwanamume. Unaijua hii mitaa usiku? Vijana wa kihuni wanaweza kunibaka.”
“Sikiliza binti, kwa hayo mazingira magumu unayosema huna sababu kabisa ya kuja. Kwa heri,” alisema na kuanza kupiga hatua.
“Haya kaka.”
Kabla hajafika mbali, yule mlevi aliyeangukia meza alimsimamisha. Inaonekana alikuwa akimfuata kwa nyuma. Jackson alishituka kidogo akihisi amekuja kwa shari, labda ni mpenzi wa Eggy na hivyo anataka kumfanyia fujo.
“Braza nilikuwa nakufuata wewe. Nimekuokoa maisha miye. Nipe pesa ya bia tu,” alisema yule kijana.
Jackson hakumwelewa, sasa akahisi huyo mlevi anataka kumtapeli, akaendelea na safari yake lakini yeye alizidi kumfuata akimsemesha.
“Mimi pale sikuanguka braza, nilijiangusha tu kwa sababu niliona mtu anaweka kitu kwenye kinywaji chako. Wewe si ulikuwa unakunywa juisi halafu ukaondoka kidogo?”
Jackson aliona anamsumbua bure. Akashika mfukoni na kumpa noti ya shilingi elfu mbili.
“Haya kaka, lakini ungejua nimekuokoa, ungenipa hata laki,” alisema yule kijana akikimbia kisogo chake kwani alishageuka kuondoka.
Jackson aliingia chumbani huku roho yake ikimuuma sana kwa kitendo chake cha kuwa karibu na yule msichana hadi kumkaribisha kwake. Alishukuru kwamba alimudu kumnyima pesa ya bodaboda na kumshauri asiende chumbani kwake.
“Bila shaka amenielewa kwamba simhitaji,” alijisemea huku akijaribu kuvaa viatu vya mkewe. Kwamba atajisikiaje siku akisikia kuna mtu anatembea na mkewe?
“Bila shaka nitajisikia vibaya sana. Vivyo hivyo na yeye ataumia sana akisikia mimi mumewe kipenzi ninatumia nafasi hii ya kuwa mbali naye kulala na mwanamke mwingine. Ewe Mwenyezi Mungu nisamehe na shetani huyu aliyekuwa ananishawishi kuwa karibu na huyo msichana. Mwondoe kwangu, ashindwe na alegee,” alizidi kujisemea.
Alivua nguo na kuvaa ya kulalia, akakaa kidogo kumwomba Mwenyezi Mungu kwa kumhifadhi mchana huo, kisha akajitupa kitandani kutafuta usingizi.
ILIKUWA haijapita muda mrefu tangu usingizi umchukue wakati simu yake ilipoita. Alishtuka na kuangalia anayepiga simu muda ule alikuwa nani. Alipoangalia kwenye skrini ya simu akaona namba ngeni.
“Halo,” aliita.
“Halo, kaka mimi Eggy niko hapa nje hotelini kwako, mlinzi keshanifungulia. Umesema uko chumbani gani?”
“Eggy, mbona umekuja. Si nilikwambia huna sababu ya kuja? Nikakwambia nimechoka?”
“Ina maana umechukua msichana mwingine, siyo? Kumbe wewe na yule mzee malaya sana eh!”
“Hapana Eggy, niko peke yangu lakini sikujua kama utakuja baada ya kukwambia vile. Naomba urudi tu na samahani sana kwa usumbufu.”
“Muda huu nirudi wapi?”
“Ngoja basi nikuletee pesa uchukue bodaboda.”
“Mimi ndio nilishamuaga mwenzangu tunayeishi naye na sasa hivi watakuwa wamefunga nyumba, siwezi kufunguliwa. Unadhani nitalala wapi?”
“Duh! Sasa itakuwaje?”
“Kaka, si umesema huna mtu, sasa kwa nini unanifanyia hivi?”
“Basi mwambie huyo mlinzi akulete Kigoma,” alisema Jackson.
Mwanaume huyo aliketi kitandani akijilaumu ni kwa nini alikuwa amefanya kilichosababisha msichana huyo kuja kwake.
Hata hivyo, sasa aliapa kwamba pamoja na kumkaribisha chumbani kwake, katu asingemgusa.
Alisikia hodi ikigongwa na mlinzi na alipokwenda kufungua akamkuta mlinzi huyo akiwa na Eggy.
Jackson alilazimika kumkaribisha msichana huyo ambaye alikuwa ameshikilia mkoba wake na bia mkononi.
“Karibu. Duh! Umekuja na bia huku?”
“Kanilazimisha yule mzee, rafiki yako,” alisema Eggy akiweka ile bia juu ya meza pale chumbani.
“Kwa hiyo ulikuwa unakuja barabarani unakunywa, siyo?”
“Hapana, kwa nini unaniuliza hivyo?”
“Si ninaona umeshaifungua.”
“Yule mshenzi ndiye kanipa hii bia, alikuwa ameshaifungua anywe yeye kisha akaamua kuniachia.”
“Sasa unachukuaje kinywaji kilichofunguliwa na mtu mwingine?”
“Haina shida… Hata kama alishatia mdomo wake sijali. Leo nina hamu sana na bia hasa ukizingatia kwamba karibu wiki nilikuwa naumwa na hivyo kujitenga na kinywaji. Tena mimi nikimaliza hii bia nitakuwa nimefika ninakopataka na nitakufurahisha zaidi leo, amini usiamini.”
Yule binti, alianza kunywa bia yake akiwa ameketi kwenye kochi pembeni mwa kitanda huku Jackson akitafuta maneno ya kumwambia ili wasifanye chochote.
Huku bado akiwaza atafanya nini kumkwepa Agnes ndani ya chumba kimoja walimokuwa, Jackson alimwona akimaliza kunywa bia yake na kunyanyuka. Akavua blauzi na suruali yake ya kubana na kuzitundika nyuma ya mlango na kuanza kuvuta hatua kuelekea bafuni kuoga akiwa kabaki na nguo ya ndani pekee.
Maumbile ya msichana huyo yalimsisimua vilivyo Jackson, akaanza kufikiria kubadili uamuzi wake lakini alipokumbuka kwamba alishaapa kutosaliti ndoa yake akajiapiza tena kwamba asingefanya lolote. Alitakiwa amshinde shetani kadiri inavyowezekana.
Baada ya muda msichana yule alirejea na kujilaza pembeni mwake. Jackson akaamua kutoka kitandani na kwenda kulala kwenye kochi moja lililokuwa kwenye chumba hicho.
“Vipi kaka, mbona sikuelewi?”
“Licha ya uchovu, lakini nimegundua kwamba nimesahau kuchukua kinga, kwa hiyo wewe lala tu. Mambo mengine tutajiandaa kesho.”
Yule msichana, huku sasa akiwa hana nguo yoyote mwilini na Jackson akijitahidi kukwepa kumtazama, alikwenda kwenye pochi yake aliyokuwa ameiacha kwenye meza na kutoa kinga, kisha akamtupia Jackson pale kwenye kochi alipokuwa amejilaza.
“Sikiliza Eggy, natamani kushiriki na wewe haya mambo ukiwa huna ulevi. Nashauri tulale halafu mambo mengine tufanya asubuhi pombe zikishakutoka, sawa?” Alisema Jackson.
Msichana huyo alimfuata pale kwenye kochi na kuanza kumshika shika akimtaka waende kitandani kulala lakini Jackson alimsihi amwache.
“Binti, ninakuomba kwa hisani yako. Wewe lala.”
“Haiwezekani. Nimekuja hapa kwa ajili yako… Kwani una tatizo lolote kaka? Sikuelewi!”
“Ndio, kwa sasa nina tatizo na ndio maana ninakwambia mambo yote kesho.”
“Hapana baby. Wala sikuelewi. Njoo tulale, unataka kunifanyia mambo gani wewe?” Aliuliza huku akiendelea kupeleka mikono yake kwenye sehemu hatarishi za Jackson ambaye muda huo alikuwa kavaa kaptula nyepesi ambayo alikuwa akiitumia kwa kulalia.
Taratibu, hali ya Jackson ilianza kubadilika, uvumilivu ulianza kumshinda. “Haya tangulia kitandani nakuja,” alisema akipapasa pale kwenye kochi kutafuta kinga.
Wakati akipambana na hisia na sasa akihema kwa nguvu, ghafla alimsikia yule binti akigumia kwa maumivu. “Ah mbona tumbo linanisokota hivi?”
“Tumbo linakusokota?” Akauliza Jackson.
“Sana, limenianza tu ghafla nilipomaliza kunywa hiyo bia. Lakini litapoa tu. Nadhani nimekula kitu kibaya.”
“Kitu gani?”
“Wala sijui… Hebu kwanza nijisikilizie,” alisema Eggy.
Jackson alishukuru Mungu na kurejea kwenye kochi lakini baada ya ukimya wa kama dakika tatu hivi, yule msichana alimwita akimwambia tumbo halipoi na badala yake anajisikia tumbo linazidi kumkata sana na kwamba ameanza kusikia kizunguzungu na kichefu chefu.
“Nasikia hata nguvu zinaniishia.”
“Binti, umekula kitu kibaya?”
“Sijui… Nasikia hali inazidi kuwa mbaya,” alizidi kulalamika, hali iliyomfanya Jackson kunyanyuka. Msichana yule ambaye alikuwa mtupu pale kwenye kitanda kipana alikuwa akigaragara huku akiwa ameshikilia tumbo.
“Vipi, nikupeleke hospitali?”
“Hapana, nadhani hali hii itatulia tu. Ni kawaida nikila kitu kibaya kufikwa na hali hii. Niwashie feni,” alisema.
Jackson aliwasha kiyoyozi kisha akamwona yule msichana akinyanyuka kwenda chooni ambako alimsikia akitapika.
Alipotoka chooni alijitupa kitandani na Jackson alipomuuliza anajisikiaje akamwambia baada ya kutapika anajisikia afueni kidogo lakini tumbo bado linamkata na mwili unaishiwa nguvu.
“Jilaze, hali itatulia. Hebu jaribu kunywa maji,” alisema Jackson na kufungua chupa ndogo ya maji na kumpa.
Alirudi kwenye kochi na kujilaza na sasa alikuwa anahisi usingizi mzito. Baada ya utulivu wa takribani dakika tano, Jackson alishikwa na usingizi mzito pale kwenye kochi.
Alishituka usingizini na kuhisi kama kuna kitu kilikuwa kinakoroma mule chumbani. Alisimama haraka na kuelekea kitandani na kumkuta binti yule akikoroma. Alipojaribu kumsemesha akagundua kwamba binti huyo alikuwa amepoteza fahamu huku povu likimtoka mdomoni.
Alikuwa keshatapika pale kitandani na sasa alikuwa kalalia matapishi yake bila kujitambua. Hali ile ilimtisha sana huku akimwonea huruma msichana yule mrembo. Akatamani kwenda kuwaamsha wahusika wa nyumba hiyo ya kulala wageni ili kumwahisha hospitali kuokoa maisha yake.
“Mbona amefikia hali hii bila kuniamsha?” Alijiuliza.
Kwa vile mkojo ulikuwa umembana kutokana na kunywa soda na juisi, Jackson aliingia bafuni kujisaidia huku akipanga kwamba ilikuwa ni lazima achukue hatua za haraka za kumwahisha Eggy hospitali. Hali ile ilikuwa si ya kawaida.
“Atakuwa kala nini huyu binti?” Alijiuliza tena bila kupata majibu.
Alitoka bafuni akipanga kumvalisha nguo haraka haraka, kumfuta matapishi na kisha kuomba msaada wa kumpeleka hospitali.
Lakini aliporejea pale kitandani, hali ile ya kukoroma ilikuwa imekatika. Alimkuta akiwa sasa ametulia tuli huku akiwa kaachama kiasi. Hali ile ilizidi kumtisha na moyo kumwenda mbio. Alipomgusa maeneo ya moyo, aligundua kwamba, ingawa mwili wake ulikuwa wa moto, hakukuwa na mapigo yoyote anayoyasikia. Aliweka pia kidole kwenye pua yake lakini hakusikia upepo wa kupumua.
Wasiwasi na uwoga ulizidi kumfunika asiamini kwamba mrembo yule ambaye alikuwa akitoa huduma pale Tanga Raha Club saa chache zilizopita, akiwa mzima na buheri wa afya, anaweza akawa kapoteza maisha.
“Haiwezekani,” alijisemea akianza kumtikisa ili kumwamsha kwani alihisi atakuwa amezirai tu, lakini hakushituka.
Kwa vile aliwahi kupata mafunzo ya huduma ya kwanza ikiwa ni pamoja na kuamsha moyo au kumzindua mtu aliyezirai (Cardiopulmonary Resuscitation – CPR), aliona afanye jaribio hilo. Bado aliamini kwamba binti yule alikuwa amezirai tu.
Alimlaza chali, akaweka kiganja cha mkono wake wa kushoto kwenye kifua chake. Akaweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto na kubana vidole. Akaanza kukandamiza kwenye kifua chake ili kushitua mapigo ya moyo.
Alimwacha kidogo, akapanua pua na kupuliza ili kufungua njia ya hewa na kurudia tena kumkandamiza kama mwanzo lakini msichana yule hakushituka.
Hali hiyo ilizidi kumtisha kwani ilikuwa inamthibitishia kwamba roho ya binti huyo ilikuwa tayari imeachana na mwili wake. Hakuwa hai. Alirejea kuketi kwenye lile kochi huku kijasho chembamba kikitanda usoni mwake. Aliwaza na kujiuliza afanye nini na hali ile? Je, kulikuwa na haja ya kuwaamsha wahusika wa nyumba hiyo ya kulala wageni? Atawaambia nini? Alijiuliza. Aliangalia saa yake. Ilikuwa inaelekea saa tisa usiku.
Aliona kwamba pengine jambo la msingi la kufanya kwa wakati ule ni kuwapigia simu polisi. Alichukua simu yake akijiuliza kama anakumbuka namba ya simu ya dharura ya polisi. Alijitahidi kukumbuka bila mafanikio. Akajilaumu sana kwa sababu aliamini huo ni uzembe mkubwa kwani kila mtu alitakiwa kuwa na namba hiyo pamoja na ya kikosi cha zimamoto.
Alisimama ili kwenda kuulizia namba ya polisi kwa wenyeji na pia kuwaeleza kadhia iliyompata.
Kabla hajatoka nje akapata wazo la kumpigia simu Andrew Mambo kumweleza tukio lililompata na kama anaweza kuwa na namba ya polisi ya dharura. Aliona lilikuwa ni wazo zuri zaidi kumshirikisha kadhia hiyo ili pia kama ana ushauri mzuri wa ziada ampe.
Aliamini Andrew, tofauti na Bruno ambaye pia alipata wazo la kumshirikisha lakini akalifuta, alikuwa mtu mkarimu na muungwana. Hakuwa na ugomvi naye na alikuwa na ushauri mzuri. Hata wafanyakazi wengi walikuwa wakimpenda Andrew kama walivyokuwa wakimpenda yeye. Simu ya Andrew ilipoita akashukuru kwamba ilikuwa hewani.
“Malima, kuna nini. Nilidhani kumekucha lakini naangalia saa naona bado ni usiku mzito,” alihoji Andrew baada ya kupokea simu sauti yake ikionesha wazi kwamba alikuwa katika usingizi mzito.
“Aisee kuna jambo la ajabu na hatari limenitokea. Una mtu hapo chumbani?”
“Hapana niko peke yangu.”
“Nilidhani umeondoka na yule msichana niliyekuacha naye.”
“Hapana, niko peke yangu.” Kwa majibu yake, Jackson alianza kumsimulia kisa na mkasa na kisha akamwomba namba za simu za polisi za dharura kama anazo.
Andrew alishitushwa sana na masimulizi ya Jackson na usingizi ukampaa. Kimsingi naye alishangaa alipomwona akiandamana na msichana wakati anatoka kwa sababu wameshakuwa naye katika safari nyingi na hata tabia zake ofisini anamjua Jackson kama mwanamume asiyejihusisha kabisa na mahusiano nje ya ndoa yake.
Yeye binafsi alikuwa akitamani aishi kama Jackson lakini alikuwa anashindwa. Hata siku hiyo alikuwa amepania kuondoka na msichana aliyekuwa naye lakini mwishoni baada ya kunywa bia zake kadhaa akadai kwamba alikuwa anahisi kuingia katika siku zake, jambo lililomkasirisha sana Andrew.
“Sikiliza Malima. Mimi nashauri hili jambo usiwashirikishe polisi wasije wakakung’ang’ania kwa kukutuhumu kwa chochote. Mpaka watakapokuja kukuachia baada ya kujua ukweli wa mambo utakuwa umeshateseka.”
“Sasa unashauri nifanyeje?”
“Wewe ondoka hapo kimya kimya kisha uje huku.”
“Hapa kuna mlinzi. Nitaondokaje usiku kama huu na anajua nina msichana chumbani? Bila shaka atapatwa na wasiwasi.”
“Basi fanya jambo moja, subiri kidogo ikifika alfajiri, ondoka na kila kitu chako na mlinzi mwambie kuna binti humo kalala, ataamka kwa wakati wake.”
“Mh! Siyo kwamba nitajichongea kwa sababu jina langu wanalo hapa kwenye kitabu cha wageni.”
“Fanya kitu kimoja. Kama unaweza kuongea na mhusika. Mpe hata pesa afute jina lako kwenye hicho kitabu. Ikiwezekana anyofoe kabisa karatasi zenye jina lako.”
“Mh! Hilo ni gumu, si rahisi kumshawishi akanielewa haraka haraka. Suala la mtu kufia kwenye gesti yao halafu akubali kufuta majina yangu, si rahisi.”
“Basi jaribu kuiba hicho kitabu kama utaweza.”
“Hilo nalo gumu… Lakini ngoja nijaribu.”
“Hebu jaribu hilo na tafadhali usimwambia mtu yeyote. Ibaki siri yangu na yako. Na hakikisha Bruno hafahamu hili.”
“Kwa nini umemtaja Bruno?”
“Ninamjua, si mtu mzuri, hasa kwako. Ninajua jinsi alivyohamanika kusikia kwamba huenda wewe ndiye utakaimu ukurugenzi. Ninajua anavyohangaika kuhakikisha anachukua nafasi hiyo. Hata wewe unajua hilo na unajua kwamba kwa hulka yake Bruno ni mtu mshari sana.”
“Asante sana Andrew. Nitafanyia kazi ushauri wako.”
Jackson, akiwa amevaa nguo ya kulalia, alitoka taratibu kwa kunyata hadi ofisi ya mapokezi. Mhudumu wa zamu alikuwa kalala kwenye ofisi hiyo hiyo, ambayo kulikuwa na kochi, kiti na kitanda.
Alichungulia na kugundua kwamba kitabu cha wageni kilikuwa kwenye kaunta na yule binti, mhudumu wa zamu, alikuwa amelala fofofo.
Alitaka kuchukua kitabu chote na kuondoka nacho lakini akahisi hilo linaweza kumshtua yule msichana akiamka na kuona kitabu hakipo.
Kwa kutumia mwanga hafifu wa nje uliokuwa unaingia mahala pale, alikifungua taratibu kitabu hicho cha wageni na kunyofoa karatasi alizoamini zilikuwa na jina lake. Wakati anakunja hizo karatasi mkononi, alisikia yule msichana wa kaunta anauliza.
“Nani… nani, mwizi?”
“Hapana ni mimi.”
“Nani, na unafanya nini hapa?” Alihoji yule msichana na kuwasha taa iliyojaza mwanga katika eneo hilo.
Huku akikunja zile karatasi na kuzishia kiganjani mwake, Jackson alimtuliza na kumjulisha kwamba alikuwa anataka kumwamsha ili amuuzie maji kwa sababu anasikia kiu lakini akawa anasita na kwamba alikuwa ameshaamua kuondoka na kujaribu kulala na kiu yake.
“Kama unaweza kunisaidia nitashukuru. Nisamehe kwa usumbufu,” alisema Jackson akihakikisha yule msichana hagundui alichokuwa amefumbata kwenye mkono wake wa kulia.
Yule msichana alinyanyuka kwenda kumchukilia maji kwenye friji na yeye haraka haraka akasokomeza zile karatasi kwenye mifuko ya nguo yake ya kulalia.
“Nadhani unakumbuka nilibakiza chenji yangu kwako. Kama sivyo nitakulipa asubuhi.”
“Yes, nakumbuka kuna chenji yako kaka.”
“Haya usiku mwema na samahani sana kwa usumbufu.”
“Hamna taabu kaka. Haya ndio majukumu yetu,” alisema na kurudi kulala, kisha akazima taa.
Jackson aliporudi chumbani kwake, alimpigia simu tena Andrew na kumweleza hatua aliyofikia.
“Basi wewe, subiri. Ikifika kwenye saa kumi na moja kasorobo hivi alfajiri wewe aga. Njoo hapa chumbani kwangu. Tutaondokea hapa kwenda kwenye semina. Bado kama saa mbili tu hivi.”
“Asante sana kwa ushauri wako.”
“Lakini nimekumbuka lingine. Usiache simu ya huyo marehemu. Ichukue kwa sababu ukiiacha polisi wataanzia hapo kusaka watu aliowasiliana nao na bila shaka wewe ndiye mtu wa mwisho kuwasiliana naye. Na kuanzia sasa jitahidi kila unachogusa uwe umevaa kitambaa ili usiendelee kuacha alama zako za vidole.”
“Aisee nimefanya vyema kukupigia simu. Hilo sikuwa ninalifikiria pamoja na mimi kuwa mwanasheria, yaani nimeshachanganyikiwa,” alisema.
Baada ya kukata simu, Jackson alijikuta na kibarua kizito cha kukaa chumbani mule na maiti hadi muda utakaofaa yeye kuondoka.
Mawazo mengi yalizidi kumwandama hasa kama mpango wake wa kukimbia maiti ile utagundulika. Kuna wakati alikuwa anaona kama wazo la Andrew linaweza kumtia matatani zaidi kuliko kuwajulisha polisi lakini akajiuliza kama tayari alikuwa ameondoa ushahidi kwamba alilala kwenye nyumba hiyo, nini kitamhusisha na kifo kile?
Kingine kilichokuwa kinamtisha kuwajulisha polisi ni endapo watamkamata kwa kufanya uchunguzi na kisha suala hilo likawafikia waandishi wa habari na hatimaye mkewe. Itakuwa ni aibu na fedheha kubwa sana kwake kwamba alichukua changudoa na kumfia chumbani!
Aliona ni vyema aendelee kufanyia kazi ushauri wa Andrew. Alivaa kitambaa akachukua simu ya yule binti, akaizima na kuiweka kwenye sanduku lake dogo la safari, kisha akakagua mkoba wa yule binti ambapo hakuona cha maana kinachoweza kuwapa polisi ushahidi dhidi yake.
Alianza kupanga nguo zake kwenye begi na kuchukua kila kilicho chake akihakikisha haachi zile karatasi alizonyofoa kwenye kitabu cha wageni. Kisha akavaa nguo alizodhamiria kuvaa siku hiyo, akamfunika yule binti shuka kiasi cha kuonekana kama aliyelala tu. Akaketi kwenye kochi kusubiri alfajiri ifike, aondoke.
* * *
Saa 11 kasorobo, Jackson alikuwa anashuka kwenye boda boda na kugonga hodi kwenye nyumba ya kulala wageni ya Tanga Kunani aliyofikia Andrew.
Alimkuta nje akimsubiri baada ya kumpigia simu, akachukua begi lake na kuongozana naye hadi chumbani kwake.
“Aisee pole sana.”
“Yaani sijui ni mkosi gani huu ambao umenikuta. Yule binti alikuwa mzima kabisa tulipokuwa naye pale baa. Yaani nashangaa sana.”
“Binadamu huwa tunatembea na magonjwa. Nadhani alikuwa anaumwa.”
“Yaani nilisita sana kuondoka naye kama nilivyokueleza kwenye simu. Na nilijilaumu sana kumpa namba yangu ya simu. Na hata alipokuja nilijaribu kumtaka arudi lakini akasema hawezi kurudi muda ule… Yaani nashangaa sana ndugu yangu.”
“Mimi huwa ninachukua sana wanawake kama hawa hasa ninapokuwa safarini, nadhani hata wewe unajua lakini sijawahi kutokewa na kitu kama hiki. Hata usiku huu nilitaka kuondoka na yule binti uliyenikuta ninaongea naye pale lakini ndio akanitapeli kwamba mambo yamemharibikia. Hili lako limenifundisha mengi.”
“Siku ya leo kwa kweli sitaisahau maishani mwangu.”
“Usijali. Matatizo tumeumbiwa wanaume. Tuombe Mungu kwamba hili suala lipite salama na nina matumaini kwamba litapita, lakini chonde chonde usimwambie mtu mwingine,” alisema Andrew.
“Unategemea nimwambie mtu mwingine? Haiwezekani Andrew,” alisema Jackson.
ANITA Msuya alimaliza kufanya usafi vyumba vyote kasoro kimoja cha Kigoma ambacho mteja aliyekuwemo aliaga kukirudisha lakini akasema kuna mgeni wake bado amelala na kwamba akiamka ataondoka.
Kwa kuwa ilikuwa inaelekea saa nne asubuhi na chumba hicho kilitakiwa kutayarishwa kwa ajili ya mgeni mwingine, aliona ni wakati mwafaka wa kumgongea mtu huyo ili akitayarishe na kama kuna mpango wa kuendelea kukitumia pia ajue.
Akiwa na vifaa vya usafi, ndoo na brashi ya kudekia, Anita alisimama mbele ya chumba hicho akitazamana na maandishi yaliyoandikwa mlangoni, Kigoma, na kuanza kugonga.
Aligonga mara nne bila kuitikiwa, akahisi kwamba huenda mtu aliyekuwemo ndani aliondoka kimya kimya bila kuaga wakati yeye akifanya usafi katika vyumba vingine. Hilo lilikuwa jambo la kawaida kutokea.
Alijaribu kufungua mlango ukafunguka. Alipopepesa macho akagundua kwamba mgeni wa mteja wake ambaye alikuwa anajua kwa asilimia 100 ni mwanamke mwenzake alikuwa bado kalala. Mtu huyo, pale kitandani alikuwa amejifunika gubigubi.
Kama mteja aliyekuwa kwenye chumba hicho wakati anaondoka alfajiri asingesema kwamba anarudisha chumba, Anita angemwacha na kurudi zake lakini ilitakiwa amwamshe.
“Dada, dada,” Anita alijaribu kumwita akahisi alikuwa na usingizi mzito. Alizingatia muda aliokuja ambao kimsingi ilikuwa imeshaingia siku nyingine, yaani siku hiyo na akahisi pia kilichomleta humo kilimfanya achelewe kulala na ndio maana mwanaume aliyekuwa naye akamwacha akiwa kalala. Alisogea kitandani na kumshika bega kisha kumtikisa.
“Dada, dada… kumekucha, dada amka,” alijaribu kumwamsha lakini bado mtu yule hakuamka.
Aliongeza nguvu ya kumtikisa lakini hakuamka. Akapata wasiwasi na kumfunua uso. Alishituka sana alivyotafakari uso ule aliokuwa akiuangalia. Kuna kitu kilimwambia kuna tatizo, akalazimika kutoka nje haraka kumfuata mhudumu mwenzake wa kiume.
Mhudumu huyo, Ramadhani Wakati, alikuwa akifanya usafi nje pamoja na kumwagilia maua yaliyokuwa yakizunguka nyumba hiyo ya wageni. Kijana huyo aliyekuwa akija asubuhi na kuondoka jioni huku pia akiwa na undugu na mmiliki wa nyumba hiyo ya wageni alikuwa pia akifanya kazi kama mlinzi wa mchana.
Anita alimjulisha kwamba ana mashaka na hali ya mtu aliyelala chumba cha Kigoma. Ramadhani, aliongozana na Anita hadi chumba cha Kigoma na alipomchunguza msichana yule kwa sekunde kadhaa ikiwa ni pamoja na kuweka kidole kwenye pua yake na kisha kusikiliza mapigo ya moyo akamgeukia Anita.
“Huyu si mzima. Kafa. Tumpigie simu uncle,” alisema akimaanisha wamwite mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni.
“Unasema kweli Rama?”
“Naona hivyo. Kafariki huyu,” alisisitiza.
Dakika chache baadaye, mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni, Muhidin Mbwana, alifika na gari lake dogo na yeye alipomchunguza msichana yule aliyesuka rasta pale kitandani, akagundua kwamba hakuwa hai.
Mara moja akataka kujua jina la mtu aliyekuwa amepanga chumba hicho na taarifa zake zote kama zinavyonakiliwa kwenye kitabu cha wageni ili awasiliane na polisi. Anita alipoleta kitabu cha wageni, waligundua kwamba karatasi za mbele zilizokuwa na jina na taarifa za mteja huyo zilikuwa zimenyofolewa.
Anita akakumbuka namna mteja huyo alivyomshitua usingizini usiku wa manane akidai alitaka maji na yeye kulazimika kumhudumia.
“Unajua niliposhituka nilihisi kama kuna mtu anachana karatasi lakini nikadhani nilikuwa naota. Kumbe ndio alikuwa akinyofoa hizi karatasi,” alisema.
“Huyu mtu ni criminal. Kamuua binti wa watu halafu kaondoka,” alisema mmiliki wa gesti hiyo, Mbwana.
Alipiga simu polisi walioahidi kufika baada ya muda mfupi. Dakika chache baadaye askari watatu walifika, wawili wakiwa wamevaa nguo za kiraia na mmoja sare za polisi na kuanza uchunguzi wao.
Askari hao walimhoji Anita na kisha wakataka pia kumhoji mlinzi aliyekuwepo kwani Anita alisema mlinzi huyo ndiye alimpokea marehemu alipokuja usiku na alisikia wakiongea mawili matatu nje.
“Binti, huyo mteja aliyekuwa chumba mnachokiita Kigoma ukimwona utamtambua?” Askari aliyejitambulisha kwa jina la Sajini Omar alimuuliza Anita wakati wakimsubiri mlinzi kuja baada ya kupigiwa simu.
“Ingawa nilianza zamu juzi lakini nina hakika nikimwona namfahamu. Ni baba mmoja anaonekana mstaarabu sana,” alisema.
“Unaweza kukumbuka kitabuni aliandika anatokea wapi na kazi yake ni ipi?” Akauliza tena huyo askari.
“Sikumbuki kazi yake lakini anatokea Dar es Salaam. Jana alikuwa ananiambia kwamba angeliondoka Jumamosi lakini alfajiri akaniambia ataondoka leo kurudi Dar es Salaam na ndio maana akarejesha chumba.”
“Je, unaweza kufahamu hapa Tanga amekuja kufanya nini?”
“Sifahamu kwa kweli,” alijibu Anita. Kabla hawajaendelea kumhoji zaidi, mlinzi aliyekuwa zamu usiku huo, Abdallah Sharif, alifika kwa usafiri bodaboda.
Mlinzi huyo alieleza kwamba binti huyo alipofika kwenye saa sita karibu na nusu usiku alitaka kwenda moja kwa moja chumba cha Kigoma lakini yeye akamzuia.
“Mimi nilimzuia nikamtaka kama ana simu ampigie kwanza mwenyeji wake kwa sababu hakuniambia kuna mgeni wake angelikuja. Alipompigia nikamwambia aweke loud speaker ili nami nisikie. Nilimsikia mwenyeji wake akimshauri arudi anakotoka lakini binti akalazimisha kulala na ndipo akamwambia aniombe nimpeleke chumbani kwake. Nikampeleka.”
“Huyu binti ulishawahi kumwona?” Alihoji askari mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Koplo Burhani.
“Namfahamu, ni baamedi wa pale Tanga Raha Club.”
“Una uhakika?” Aliuliza tena yule askari.
“Nina uhakika asilimia mia moja na hapa alishakuja siyo mara moja wala mbili na wanaume. Vyumba vyote humu ukimtajia; Musoma, Arusha, Lindi, Geita na vinginevyo anavijua,” alisema.
“Huyo bwana aliyekuwa Kigoma, ukimwona utamfahamu?” Alizidi kuhoji Koplo Burhani.
“Hata gizani ninaweza kumfahamu.”
“Unaweza kujua hapa Tanga alikuja kufanya nini?”
“Alikuja kwenye semina Mkonge Hotel. Kwa sababu siku ya kwanza mimi ndiye nilimtafutia usafiri wa kwenda Mkonge.”
“Alfajiri alipoondoka alikuaga?”
“Ndiyo.”
“Alisema anakwenda wapi?”
“Nilipomwona na begi nikamuuliza vipi, semina imeisha?”
“Akasema imeisha.”
“Alisema anaondoka muda ule kurejea Dar es Salaam?”
“Hapana, alisema tu semina imeisha.” Baada ya maelezo hayo, askari wakaona kuna haja ya kwenda Mkonge Hotel kunusa labda wanaweza kujua lolote kama kuna semina imeisha.
“Inawezekana semina ikawa inaisha leo na huyo jamaa amepanga kuondoka leo,” alisema askari Burhan kumweleza mwenziye ambaye alikubaliana naye.
Waliona hata kama kuna semina itakuwa imeisha jana yake, wanaweza wakapata majina ya wahusika na kuanza kufuatilia jina moja baada ya lingine.
Baadaye waliuliza kama kuna mwenye namba ya meneja au mmiliki wa Tanga Raha Club. Hakuna aliyekuwa nayo.
Lakini Mbwana, mmiliki wa gesti hiyo, alisema anaweza kuipata. Alimpigia simu mtu mmoja ambaye alimpa namba mbili za mmiliki na meneja wa klabu hiyo.
Mara moja askari wale walimpigia meneja na kumweleza kwamba kuna binti kafia Twiga Executive Lodge anayeaminika kuwa mmoja wa wahudumu katika klabu hiyo maarufu. Mara moja wakamtaka aje pale kumtambua marehemu.
Meneja huyo alifika baada ya dakika tano na alipomwangalia yule binti kitandani alimtambua.
“Ndio, huyu ni Agnes Makata. Ni mhudumu wetu na jana alikuwa kazini.”
“Alipokuwa kazini alikuwa anaumwa?” Alihoji Sajini Omar.
“Hapana, alikuwa mzima. Lakini kiasi cha siku nne hivi alikuwa akisumbuliwa na malaria. Tangu majuzi ni mzima na anakuja kazini kama kawaida.”
“Unamjua mtu aliyeondoka naye baada ya kazi usiku wa kuamkia leo?”
“Hapana. Baadhi ya wasichana tulio nao klabu wako palepale ghetto lakini Agnes na mwenzake anaitwa Mariamu wamepanga chumba mtaani,” alijibu Meneja yule, Hashim Thomas maarufu kama Makilikili.
“Tutamhitaji huyo Mariamu baadaye,” alisema Sajini Omar na kuongeza: “Sasa nyinyi wawili; wewe mtu wa mapokezi na wewe Mlinzi tutaondoka nanyi kwenda Mkonge Hotel kama tunaweza kumwona huyu mtuhumiwa au kujua chochote. Lakini kwanza ngoja tushughulikie mwili wa marehemu ukahifadhiwe hospitalini Bombo.”
Askari wale waliokuja na gari ya polisi aina ya Land Rover, walimwita dereva na kisha wakashirikiana kubeba maiti ile hadi kwenye gari lao.
Kisha wakatoa maagizo kwamba chumba kile kisiguswe hadi wataalamu wa alama za vidole watakapokuja.
“Tunapeleka maiti kwenye chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini, tutarudi kwa ajili ya kuwachukua nyinyi mkaandike maelezo na kisha tutakwenda Mkonge Hotel,” alitoa maagizo Sajini Omar kuwaambia Anita na Abdallah.
“Samahani afande, huyu bwana inawezekana ameondoka kurudi Dar es Salaam. Tutaenda Mkonge kufanya nini?” Alihoji bwana Abdallah.
Sajini Omar akamgeukia: “Lakini hukusema kwa asilimia mia moja kama semina anayoshiriki imeisha, na huyu mwenzio, anasema huyo bwana aliwahi kumwambia atakuwepo hapa hadi kesho Jumamosi. Kama hakuna semina iliyomalizika leo, tutajaribu kupita semina zote zinazoendelea pale na wahusika watatueleza pia kama kuna semina iliisha jana, sawa?”
“Sawa afande.”
* * *
“Tumepata taarifa sasa hivi kwamba chakula tayari. Kwa hiyo tutaendelea baada ya chakula kwa ajili ya mjadala wa mada iliyoko mbele yenu. Sasa hivi ni saa saba na nusu. Naomba saa nane na nusu tuwe hapa,” alisema mwasilishaji wa mada ya mwisho katika semina hiyo akiangalia saa yake. Akaongeza:
“Nadhani saa moja itatutosha kwa mjadala na kufunga semina saa tisa na nusu. Nimesikia basi la mwisho kwenda Dar linaondoka saa 11 na nusu kwa hiyo watakaokuwa tayari kusafiri muda huo ruksa.”
Wanasemina walifunga vifaa vyao na kusimama kuondoka. Hatua ile ya watu kuondoka ndiyo iliyomshtua Jackson aliyekuwa anasinzia.
Tangu aingie kwenye semina hiyo iliyokuwa inaanza saa tatu kamili, mawazo yake yalikuwa mbali sana. Alikuwepo pale kimwili lakini si kifikra.
Alikuwa anaendelea kujiuliza sababu hasa za kifo cha yule msichana na alitamani kubaki Tanga ili kujua madaktari wangesema nini kuhusu chanzo cha kifo chake lakini ni jambo ambalo lilikuwa haliwezekani yeye kulifuatilia.
Aliendelea kujilaumu kwa nini alijiingiza katika masuala ya wanawake, jambo ambalo huwa analipiga vita na kuwa mshauri wa vijana wengi huku akihimiza watu kushika ibada na wakati mwingine kuwasomea baadhi ya vifungu vya Biblia hadi kupachikwa jina la Baba Mchungaji.
Hakuwa amesikia tangazo la chakula lakini hali ile ya watu kuamka ghafla alijua ni wakati wa chakula. Wakati ananyanyuka akiwa wa mwisho kutoka kwenye chumba cha semina, Bruno alimsubiri na alipomfikia alimgeukia.
“Malima, vipi? Naona hauko nasi kwenye semina. Kuna shida yoyote?”
“Hamna shida yoyote mkuu isipokuwa uchovu tu.”
“Au umeserebuka sana na yule binti. Kumbe baba mchungaji umo ma’nake jana ulinizidi ujanja.”
“Wala si kwa sababu hiyo. Kwanza sikuwa naye.”
“Usinidanganye Malima, alikuja chumbani kwako kwa sababu wanafunga klabu yao mimi nipo pale na aliniaga.”
“Alikuaga kwamba anakuja kwangu?”
“Ndio, aliniambia ninakwenda kwa rafiki yako, yaani kwako. Wala hakuficha.”
“Wala sikumwona… Samahani, napitia maliwatoni kidogo,” alisema Jackson na kuachana na Bruno. Licha ya kwamba alikuwa anasikia haja ndogo, lakini hakutaka kuendelea kuzungumzia suala la msichana huyo na Bruno.
Alipotoka maliwatoni alirudi tena chumba cha semina baada ya kugundua amesahau miwani yake. Baada ya kuichukua akatoka nje kuelekea kwenye eneo la chakula.
Kulikuwa na semina nne zilizokuwa zinaendeshwa kwa wiki hiyo katika hoteli hiyo na watu wote walikuwa wakitoka kwa pamoja kwenda kwenye eneo la chakula.
Kule kwenye ukumbi wa chakula kulikuwa na bufee mbili na meza za wahusika wa kila semina ziliwekwa majina ya semina husika na bufee watakayotumia. Wakati anakaribia kuingia kwenye eneo la chakula kuna watu wanne walikuwa mbele yake, msichana na wanaume watatu.
Alipoangalia vizuri akagundua kwamba msichana yule, japo alikuwa amemtega kisogo ni yule mhudumu wa Twiga Executive Lodge na mmoja wa wale wanaume ni yule kijana mlinzi. Aligeuka mara moja na kurudi nyuma. Alirudi tena chooni haraka huku moyo ukimwenda mbio.
Alihisi kwamba wale wanaume wawili waliovaa kiraia wanaweza kuwa askari polisi na pengine walitaka kutumia mwanya huo wa chakula kumnasa mpangaji aliyekuwa chumba cha Kigoma.
“Labda nimewafananisha,” alijisemea na kwa vile eneo la chakula lilikuwa ufukweni aliamua kutoka nje na kupitia njia nyingine kama anaweza kuwaangalia kwa vizuri zaidi. Alipotoka nje akaona Land Rover ya Polisi na mule ndani kukiwa na askari wawili waliokuwa wamevaa sare.
“Naona kumekucha. Lazima niondoke sasa hivi katika hili eneo,” alijisemea na kurudi kwenye chumba cha semina hotelini hapo. Hakuwa na haja tena ya kwenda kuhakikisha sura za watu wale. Pale kwenye semina alimkuta mhudumu aliyekuwa akilinda mizigo na vifaa vya wanasemina.
“Dada, nadhani unanifahamu vyema eh?”
“Wewe tena, ninakufahamu mkuu.”
“Sasa ninajisikia vibaya na hata chakula nimeacha. Nimerudia njiani. Ngoja nikapumzike hotelini.”
“Na kweli nilipokuja kuleta taarifa ya chai na hata ya chakula nilikuona umelela ukiwa umeegemea meza.”
“Kweli ninaumwa. Nimerudia mkoba wangu. Naondoka.”
“Sawa kaka, chukua tu.”
Jackson alichukua mkoba wake na kuondoka. Pale nje ya hoteli alichukua teksi na kuelekea hotelini alikofikia Andrew.
Alipofika, alisimama nje ya hoteli na kumpigia simu Andrew na kumweleza kilichotokea.
“Aisee unasema kweli, kwa sababu hata sisi tunashangaa hapa tulipokuwa kwenye foleni ya chakula, tuliona watu wanapita kama wanamwangalia kila mtu usoni. Na hivi ninavyoongea wamehamia kwenye mstari wa bufee nyingine,” alisema Andrew.
“Sasa mimi naona niondoke sasa hivi kwenda stendi nirejee Dar es Salaam. Sasa hawa watu watanipa funguo kweli nichukue sanduku langu?”
“Kuna huyo mhudumu wa mapokezi nina namba yake ngoja nijaribu kumpigia, uko hapo mapokezi?”
“Hapana, ngoja niende.”
“Basi nitapiga simu hapo baada ya dakika mbili.”
“Sawa.”
“Nimemwambia Katibu Mkuu ukweli kwamba tunadhani kwamba Bwana Malima ana uwezo mkubwa wa kuongoza Tume kuliko mtu mwingine,” Profesa Aboubakar Mwinchumu, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Teknolojia na Mawasiliano, alimwambia makamu wake, Josiah Mafumu.
Profesa Mwinchumu ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, alikuwa akiteta na makamu wake akiwa ofisini kwake.
“Tuseme Katibu Mkuu alikuwa anataka nini, Profesa?” Alihoji Mafumu.
“Alitaka tu kujua mpango tulio nao kuhusu mrithi wa Bw. Matakwali lakini ninajua hizi zote ni kampeni za Bruno. Kwa hiyo Bruno anahaha kuhakikisha anachukua hii nafasi wakati hana uwezo.”
“Ni kweli, halali usingizi. Anajaribu kuweka mazingira kwamba anayepaswa kuongoza Tume ni muhimu awe mhandisi kama yeye. Hizi ni dhana za ovyo kwa sababu tunataka mtu wa kuongoza na siyo mtu wa kwenda field. Katibu Mkuu ameelewa kweli?”
“Nadhani ameelewa. Na nimemtaka amwambie Waziri kwamba endapo Mheshimiwa Rais atataka jina la atakayempitisha rasmi kuchukua nafasi ya Bw. Matakwali basi ni Malima. Lakini yeye ameshauri huyo tutakayempendekeza ni bora akaimu kwanza tuone uwezo wake. Nina hakika Tume itakuwa imepata mtu sahihi na atakayeleta mafanikio makubwa ndani ya uongozi wake,” alisema Profesa Mwinchumu.
“Ninajua Malima ni mtu makini sana na ndio maana hata Matakwali anampendekeza yeye na siyo Mapunda .”
“Ni kweli, Mapunda ni mzoefu kwenye Tume lakini mbambaishaji sana. Matakwali anakiri kwamba alichelewa sana kugundua vipaji vya uongozi kwa Malima na anasema kama unaona mabadiliko yoyote chanya kwa sasa kwenye Tume basi ni ushauri wa Malima. Isitoshe ni mtu mwadilifu sana, mchapakazi na anayeendana sawia na falsafa ya uadilifu ya Rais wetu. Kwa hiyo tutakapokutana na wajumbe wote wa bodi itabidi tuweke hadharani CV za hawa watu wawili.”
“Lakini Mapunda anafanya kampeni za kufa mtu. Isije ikawa wajumbe wote keshawakamata kwa sababu hata mimi juzi kanirushia laki moja na nusu akanitumia na ujumbe kwamba hicho ni kianzio. Labda ni wewe tu anayekuogopa pengine na mkurugenzi anayestaafu, Matakwali, kwa sababu ameshajua hayuko upande wake. Tutafanyaje hapo?”
“Hiyo pesa yake umeila?”
“Nitaila lakini simpendekezi abadani.”
“Hata mimi alinipigia simu na kuniambia eti kama kulionekana mapungufu huko nyuma niwe na uhakika atayasawazisha kwa kutumia uzoefu wake. Akasema maneno mengi ya kujaribu kuonesha kwamba Jackson bado haijui tume sawasawa. Mimi nikamwambia maneno machache tu kwamba kiongozi anawekwa na Mungu na sisi ndiye atatuongoza kumpata mtu safi. Nikamwambia mtu huyo anaweza kuwa yeye au mwingine. Nilitaka kumwambia maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba uongozi ni mzigo na kwamba mtu safi kabisa haukimbilii lakini nikaona nisimkatishe tamaa bure.”
“Sasa wajumbe wengi wakimpendekeza itakuwaje na kama unavyoona hata katibu mkuu amefikia kukuhoji mtazamo wako?”
“Watu wenye kura ya turufu pale ni sisi; mimi, wewe na Matakwali. Hana ujanja. Kupita kwake ni sawa na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.”
“Sawa mwenyekiti lakini wiki iliyopita nilikuwa ninaongea na Andrew Mambo, yule Meneja Rasilimali Watu, unajua yule nilimwacha Form One, ananiambia Mapunda amefikia hata hatua ya kwenda kwa waganga. Anasema Jumapili moja hivi karibuni walinzi walimuona na mtu anayeaminika kuwa ni mganga wa jadi usiku wa manane pale ofisi za tume wakiwanga.”
“Duh! Bado katika karne hii huyu bwana anategemea matunguri?”
“Andrew unajua tunaongea naye sana. Ananiambia hata huko Tanga waliko kwenye semina Mapunda ana kazi moja tu ya kuhangaika kuhakikisha anakaimu yeye ukurugenzi. Yaani ni balaa.”
“Mwalimu Nyerere alisema kweli. Kwamba ukiona mtu anatafuta madaraka, tena kwa kuhonga honga pesa, mtu huyo ni wa kuogopa kama ukoma.”
* * *
Alikuwa mezani akimsaidia mwanae, Hellen kufanya kazi za shule alizopewa kufanyia nyumbani. Msichana wa kazi alikuwa anaandaa meza kwa ajili ya chakula cha usiku.
Mkewe, Salome Bakunda, ambaye ni ofisa uraghbishi katika asasi ya kiraia ya Mwanamke Lulu, inayopigania haki za mwanamke dhidi ya mfumo dume, alikuwa ametoka jikoni na kuketi sebuleni kujiandaa kuangalia taarifa ya habari.
Kama mwanaharakati na mwanasheria, mwanamke huyo alikuwa mpenzi sana wa kusikiliza taarifa za habari, kusoma magazeti na hata kuchangia maoni mbalimbali kwenye vyombo vya habari linapokuja suala la kutetea haki za wanawake.
Alikuwa na mwaka mmoja sasa tangu alipofanikiwa kuapishwa kama wakili wa Mahakama Kuu baada ya kufaulu mafunzo husika lakini alikuwa hajaanza kufanya kazi za uwakili kutokana na kubanwa na shughuli za uanaharakati katika asasi yao isiyo ya kiserikali ambayo ilikuwa inapata misaada mingi kutoka kwa wahisani.
Salome alikutana na Jackson Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati akiwa mwaka wa kwanza na Jackson akiwa mwaka wa mwisho.
Walifunga ndoa siku chache baada ya Salome kuhitimu masomo hata kabla Jackson hajapata kazi.
Wakati muhtasari wa taarifa ya habari ya saa mbili ulipoanza katika kituo cha televisheni cha taifa, Jackson hakuwa anazingatia kinachoendelea ingawa alikuwa anasikia. Lakini aliposikia mtangazaji akisema kwamba miongoni mwa habari walizonazo Jumamosi hiyo usiku ni pamoja na ya baamedi kuuliwa kwa sumu na mpenzi wake wakiwa gesti mjini Tanga na kisha mwanaume huyo kutoweka, kulimfanya aondoke mezani ili kusikiliza taarifa ya habari.
“Hellen, endelea mama, ngoja kwanza nisikilize taarifa ya habari,” alisema akinyanyuka kwenda kukaa kwenye kochi.
Moyo ulimdunda na mapigo ya moyo yakabadilika, jasho jembamba likaanza kumtoka na akatamani kuongeza kasi ya feni lililokuwa linazunguka juu ya kichwa chake pale sebuleni.
“Vipi, mbona hivyo, kuna shida yoyote?” Alihoji mkewe ambaye aligundua kwamba kuna kitu hakikuwa sawa kwa mumewe.
“Moyo umeshituka tu… Sasa nataka niache kunywa soda na vyakula vya wanga. Naona karibu nikumbwe na shinikizo la damu,” alilazimika kuongopa.
Waliendelea kufuatilia habari na hata mwanae alipomfuata pale kwenye kochi kumuuliza swali, alimtaka asubiri kwanza taarifa ya habari iishe.
“Ngoja taarifa ya habari iishe. Hata hivyo utaendelea na mama yako, mimi ninajisikia vibaya,” alimjibu mwanae.
Baadaye ikafika habari aliyokuwa anaisubiri Jackson na ingawa mapigo ya moyo yaliongezeka tena lakini akajitahidi kuisikiliza kwa makini.
Kwa vile ilikuwa ni habari iliyohusisha masuala ya ukatili wa kijinsia, mwanaume kumuua mpenzi wake, Salome naye alikaa mkao wa kuisikiliza kwa makini huku akitamani kuchukua kalamu na karatasi. Akaamua kuirekodi kwa simu yake.
Mtangazaji alirudia ule muhtasari kisha akamwachia ripota wao kutoka Tanga kuendelea na habari ile.
Mwandishi huyo, alimkariri Mkuu wa Jeshi la Polisi la mkoa wa Tanga, Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi Joel Kambi, akitaarifu kutokea kwa mauaji katika nyumba ya kulala wageni ya Twiga Executive Lodge iliyoko maeneo ya Sabasaba. Alisema msichana ambaye ni mhudumu wa baa alikutwa amekufa huku mwanaume aliyekuwa naye katika nyumba hiyo ya kulala wageni akitoweka na kunyofoa taarifa zake kwenye kitabu cha wageni.
Huku picha ya marehemu ikioneshwa kwenye skrini na kumfanya Salome aseme kwamba marehemu alikuwa mrembo na umri mdogo, mkuu huyo wa polisi alisema uchunguzi wa madaktari ulionesha kwamba marehemu alikuwa amenyweshwa sumu aina ya aconite.
Akasema kwamba sumu hiyo pia ilionekana kwenye chupa ya bia iliyokutwa chumbani humo.
Mwandishi pia alimhoji daktari mmoja akaeleza kwamba kutegemea na wingi wa dozi sumu ya aconite inaweza kuua hapo hapo au baada ya saa kadhaa.
“Hii ni sumu ambayo hutumiwa zaidi na wafugaji wa mbwa. Mbwa wanapopata ugonjwa kama wa kichaa cha mbwa, ni sumu nzuri ya kuwaua lakini mwanadamu akitiliwa kwenye kinywaji humuua pia,” alisema daktari katika taarifa hiyo.
Mmiliki wa Twiga Executive Lodge naye alihojiwa akieleza kilichotokea na jinsi mtuhumiwa alivyofanikiwa kutoroka huku akinyofoa taarifa zake kwenye kitabu cha wageni pamoja na kuondoka na simu ya marehemu ili kupoteza ushahidi.
“Taarifa zilizopo ni kwamba mtuhumiwa ni mkazi wa Dar es Salaam aliyekuwa akishiriki kwenye semina hapa Tanga,” alisema mtu huyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Tanga Raha Club alimwelezea marehemu kama mtu mcheshi na mchapa kazi hodari na kwamba siku ya tukio alikuwa buheri wa afya.
“Baa kadhaa za jirani zilishajaribu kumwiba Agnes kutoka kwetu lakini anakataa. Ni msichana tuliyekuwa tunamtegemea sana kwa kweli. Niseme tu ukweli kama wangeondoka wasichana watano nikabaki na Agnes wala nisingejali,” alisema Meneja huyo.
Meneja huyo aliendelea kumsifu Agnes Makata akisema ni msichana aliyesaidia sana kuwaunganisha wasichana wenzake katika klabu yake.
“Kama ni shuleni tunasema alikuwa ndiye dada mkuu. Mpaka leo kazi zimeshindwa kufanyika hapa klabuni tangu wenzake waliposikia kwamba Agnes hatunaye tena duniani na hasa tuhuma kwamba kauliwa na mtu aliyeondoka kwenda kupitisha naye usiku huo,” alisema Meneja huyo na kuanza kulia hadi mwandishi wa habari alipoanza kumbembeleza anyamaze.
Hata hivyo, Meneja huyo alipoulizwa baada ya kutulia kama anamjua mpenzi wa marehemu, alisema aliwahi kuwa na mchumba dereva teksi lakini waliachana.
Lakini akasema alipowahoji wafanyakazi wenzake wakaonesha kwamba siku ya tukio aliondoka na mtu ambaye alionekana mgeni kwenye klabu yake.
Akasema kwamba siku hiyo inasemekana alionekana na wanaume wawili muda mrefu waliokuwa wameketi meza moja ambao pia si wenyeji wa Tanga na kwamba aliondoka na mmoja wao.
Pia msichana aliyekuwa amepanga naye chumba kimoja, Mariamu Hafidh, alihojiwa akasema maneno ambayo hayakutofautiana sana na ya bosi wake, Meneja Makilikili.
“Tulipomaliza kazi Eggy aliniaga kwamba amepata buzi anakwenda kulichuna. Mimi nilisepa zangu lakini huyo mwanaume hakuwahi hata kunitajia jina lake,” alisema na kuongeza kwamba anaamini hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza kwa Agnes kuondoka na mwanaume huyo.
Alipoulizwa kama akimwona mwanaume huyo anaweza kumfahamu alijibu pengine anaweza kumtambua kwa sababu alimwona Agnes akiwa naye hadi walipokuwa wanakaribia kufunga huduma.
Mariamu alipoulizwa kuhusu familia ya marehemu, akajibu:
“Eggy ana mtoto mmoja anayelelewa na bibi yake. Hilo lilikuwa linamuuma sana marehemu na alikuwa keshajifunza ususi wa nywele akiwa mbioni kufungua saluni yake ili aachane na kazi ya baa. Alikuwa anasema kazi ya baa, licha ya kipato kuwa kidogo itamnyima muda wa kutosha wa kukaa na mwanawe endapo atamchukua. Ukiingia chumbani kwetu utadhani saluni kwani Eggy keshanunua takribani kila kitu kinachofaa kwa ajili ya saluni. Hata mabaamedi wote pale kazini tulishaacha kwenda saluni zingine. Yeye ndiye anatutengeneza nywele na alishakuwa mzuri sana katika hilo,” alisema Mariamu.
“Yaani wanaume! Huu ukatili wa kijinsia utakwisha lini?” Alisema Salome kwa hasira baada ya habari ile ya baamedi kumalizika na kuingia taarifa nyingine.
Akaongeza “Yaani wanawake tunauliwa tu kama kuku pale mpenzi anapojisikia. Ni lazima tuzidishe elimu na vita dhidi ya mfumo dume.”
“Hizi tulizosikia ni tuhuma tu, hupaswi kuzichukulia kama kweli.”Alidakia Jackson
“Tuhuma? Unasemaje ni tuhuma wakati kila kitu kiko wazi? Tena huyu mwanaume aliyekuwa na huyu binti wa watu anaonekana ni mhalifu mzoefu. Kampa sumu binti wa watu, kisha akanyofoa taarifa kwenye kitabu cha wageni. Kinachonisikitisha ni jinsi ambavyo huyu binti alivyokuwa na mipango mizuri ya kulea mwanae lakini mwanaume mmoja mshenzi, kwa ukatili na ushetani wake anamuua hivi hivi tu. Dunia haiwezi kuendelea kulea vitu kama hivi,” alisema Salome akionekana mwenye hasira maneno yaliyomchoma sana Jackson. Alibaki kimya akitafakari.
Mkewe akazidi kuongea:“Kesho nitamwambia Mkurugenzi kuhusu hii kesi. Kama mhalifu atapatikana ofisi yetu itajitolea kutoa msaada wa kisheria mahakamani ili haki itendeke. Hii inaweza kuwa kazi yangu ya kwanza kama wakili kusimama mahakamani kumkaanga huyu mshenzi. Lazima huyu criminal alipie dhambi zake. Wanawake tumechoka.”
“Lakini unapandisha hasira bure kwa kusikia upande mmoja. Unaweza kusikia upande mwingine ukashangaa. Pengine huyo dada akawa kafa natural death.”Alizidi kutetea Jackson
“Hivi ulikuwa unasikiliza vizuri? Hapo imetajwa hadi sumu aliyowekewa na huyo mwanaume mshenzi… Yaani wanaume wote ni walewale tu. Na huyu mshenzi kama ulivyosikia alikuwa mwanasemina mwenzenu huko Tanga, isije hata ikawa mnatoka naye ofisi moja. Jumatatu ipeleke hii hoja ofisini kwenu,” alisema mkewe. Jackson alizidi kujisikia vibaya, akanyanyuka kwenda chumbani.
Alijitupa kitandani na kujikuta katika mawazo makali. Alikumbuka jana yake Ijumaa alipokuwa kwenye basi, Andrew alipimpigia simu na kumjulisha tena kwamba askari na watu anaoamini wanatoka Twiga Executive Lodge walipita tena kwenye vyumba vya semina kwa kushitukiza kutafuta waliyekuwa wakimtafuta.
“Itakuwaje siku nikigundulika? Itakuwaje siku mke wangu akisikia kwamba mtu anayetuhumiwa kuua ni mimi. Hivi, mimi kama mwanasheria kwa nini nimejiweka katika mtego mbaya? Kwa nini sikutoa taarifa polisi baada ya kifo cha yule binti pengine tusingefika huku.”
Aliitwa kula chakula cha usiku na mwanae mdogo, Hilda, lakini akasema bado moyo unamwenda mbio na hana hamu ya kula. Tumbo lilikuwa limejaa ghafla na alikuwa hasikii hamu ya kula. Mkewe alimfuata na kumshauri waende hospitali kama anajisikia vibaya lakini alikataa.
Usiku huo usingizi wake ulikuwa mgumu sana kupatikana. Muda mwingi alibaki macho akiwaza na pale alipopata usingizi ndoto na jinamizi la Eggy lilikuwa likimtokea na kujikuta akishtuka ghafla huku jasho likimtoka hadi mkewe akamuuliza kulikoni.
* * *
Saa tatu na dakika 10 siku ya Jumanne, wajumbe wote kasoro wawili waliokuwa na udhuru walikuwa wameshawasili kwenye Ukumbi wa Bodi, ulioko katika ofisi za TTM.
Dakika tano baadaye, yaani saa tatu na robo, kikao cha dharura cha Bodi kilifunguliwa na Mwenyekiti wake, Profesa Aboubakar Mwinchumu kwa kuwashukuru wajumbe waliofika akisema kulikuwa na ajenda kuu moja tu ya kujadili na ambayo alisema anaamini isingechukua muda mrefu.
“Katibu wetu anayemaliza muda wake atakapotusomea muhtasari wa kikao kilichopita, tutakuwa na agenda moja tu. Nayo ni ya kupitisha mtu atakayekaimu nafasi ya ukurugenzi wa tume kabla Rais hajateua mkurugenzi mwingine. Na huyu tunayempitisha leo, kama mnavyojua ndiye atakuwa katibu wetu wa muda katika vikao vijavyo,” alisema Profesa Mwinchumu.
Akaendelea:“Sasa hivi ni saa tatu na dakika… inaelekea 16 hivi. Sitegemei kama saa tano itatukuta hatujamaliza hii ajenda na kuendelea na shughuli zetu zingine. Kama mambo yatakwenda kama ninavyotarajia huenda hata saa nne na nusu isitukute hapa.”
Aliendelea kusema kwamba mchana huo, saa sita kamili, wafanyakazi wote wa tume hapo makao makuu wanatakiwa pia kukutana katika ukumbi huo huo kuagana na bosi wao, Matakwali na kutajiwa kaimu mkurugenzi wao.
“Wafanyakazi wameshatangaziwa hilo na hivyo ni muhimu sana sisi kikao hiki tukimalize mapema,” alisisitiza Mwenyekiti.
Alipomaliza kusema hayo alimkaribisha Mkurugenzi wa Tume, Ibrahim Matakwali, ambaye kwa nafasi yake alikuwa Katibu wa Bodi, kusoma muhtasari wa kikao kilichopita.
Siku hiyo ndiyo Matakwali alitazamiwa kustaafu kutokana na umri baada ya kutumikia tume kwa miaka 18 akiwa Mkurugenzi mwanzilishi. Na hiyo ilikuwa ni baada ya kuongezewa miaka mitano na Rais ambayo sasa ilikuwa imekamilika. Yeye mwenyewe alikuwa ameshachoka kazi akitaka kuendeleza miradi yake binafsi bila kuongeza siku hata moja.
Kama kawaida, muhtasari huo ulisomwa, wajumbe wote wakaafiki kwamba yote yaliyosomwa ni sahihi. Mwenyekiti alipouliza kama kuna yatokanayo hakuna aliyenyoosha mkono. Wengi walikuwa wanataka kwenda kwenye ajenda ya siku hiyo na kisha waondoke zao.
Mwenyekiti alisimama na kumpongeza Mkurugenzi aliyekuwa akimaliza muda wake, akimwelezea kama mtu mwenye weledi, mwaminifu, mbunifu, mtiifu, mwadilifu na aliyeiongoza Tume kwa mafanikio na umahiri mkubwa.
“Kama mtakumbuka mwenzetu ilikuwa astaafu miaka mitano iliyopita lakini Rais akamwongezea muda kwa sababu ya kazi yake nzuri. Tumejaribu sana kumshawishi abaki hata kwa mwaka mmoja mwingine baada ya Rais kukubali pia lakini mwenzetu anasema ni vyema akalee wajukuu.
“Kwa hiyo hatuna namna nyingine isipokuwa kumwachia akapumzike. Alikoitoa Tume kama Mkurugenzi mwanzilishi hadi sasa inafanya makubwa kwa kweli ataendelea kukumbukwa daima kwa mchango wake na utumishi uliotukuka,” alisema mwenyekiti wa bodi.
Baada ya maelezo hayo mafupi, mwenyekiti alimkaribisha Matakwali kuwaaga wajumbe wa bodi kabla ya kuingia kwenye ajenda ya kuchagua na kupitisha jina la mtu ambaye angekaimu nafasi yake.
Matakwali aliwashukuru wajumbe wa bodi kwa ushirikiano waliompa na maelekezo mazuri aliyokuwa akipata kutoka kwao ambayo alisema ndiyo hasa msingi wa kile kinachoonekana kama ni ufanisi wake.
Alikiri kwamba bodi ya sasa inayoongozwa na Profesa Mwinchumu ilikuwa ndio bodi bora na makini zaidi kuwahi kutokea kulinganisha na bodi zilizotangulia. Akasema ndio maana mwaka uliokuwa umepita, Rais alikuwa ameamua kuiacha yote na kuiongezea tena muda wa miaka mitano.
“Kwa umakini wenu huo, ninaamini pia mtapitisha mtu makini ambaye atakaimu ukurugenzi na kuongoza menejimenti kwa umahiri mkubwa pengine kuliko hata mimi. Mimi kwa kweli sikuwa ninajua kila kitu. Nilikuwa nina mapungufu mengi tu lakini niliwatumia vizuri wasaidizi wangu ambao wengine ninakiri kwamba wana uwezo mkubwa wa uongozi kuliko hata mimi,” alisema Mhandisi Matakwali.
Baada ya shukrani hizo aliketi na ndipo ajenda ya kuchagua jina la mtu atakayekaimu ukurugenzi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na wajumbe wa bodi ikawadia.
Mwenyekiti alirusha tena mpira kwa Matakwali akisema kwamba kwa vile yeye amekuwa mkurugenzi mwanzilishi na anawajua watu wake vizuri, ni vyema akamtaja mtu anayeona anafaa kukaimu nafasi yake na kama bodi itakubaliana naye basi itampitisha.
“Kwa bahati nzuri, katika kipindi hiki ambacho tumekuwa wajumbe wa hii bodi na kisha kuongezewa muda na Mheshimiwa Rais, tunawajua pia baadhi ya wasaidizi wako. Tunatazamia utatutajia jina ambalo kila mmoja wetu ataridhika nalo. Kama hatutaridhika nalo hatutakubali,” alisisitiza Mwenyekiti.
Matakwali aliposimama, akamtaja Jackson Malima, Mwanasheria Mkuu wa Tume, kwamba alikuwa na sifa zote, siyo tu za kukaimu, bali hata kuwa mkurugenzi kamili wa TTM.
“Ni mtu makini, mchapakazi, mwadilifu na mkweli na anayejifunza haraka sana. Yeye kitaaluma ni mwanasheria lakini huwezi kuamini, amejifunza haraka sana kivyake vyake teknolojia ya habari na mawasiliano na hivyo sasa anaweza kuwa mahiri kuliko hata baadhi ya wahandisi tulio nao hapa kwa nadharia.
Mimi huwa ninamwambia anatakiwa kwenda tu chuoni kupewa cheti siyo kusoma kwa sababu huwezi kumdanganya kitu. Niliwahi kupata dharura wakati nikitakiwa kuwasilisha mada kwenye moja ya semina muhimu huku mhandisi mwenzangu, Bruno Mapunda akiwa pia ana dharura, huwezi kuamini namna alivyoiwasilisha vizuri kwa niaba yangu pengine vizuri zaidi kuliko ambavyo mimi ningeliiwasilisha.
“Mwenyekiti amenisifia hapa kama mbunifu, basi huyu ndiye mbunifu halisi. Mengi ambayo ninasifiwa kwamba nimebuni na kuifanya tume kila siku ionekane inapiga hatua ni ushauri wake kwangu kwa asilimia 70. Zilizobaki 30 ndizo ninazoshauriwa na watu wengine,” alisema.
Baada ya kusema hivyo aliketi na mwenyekiti akataka kusikia wajumbe wanasemaje kuhusu pendekezo hilo.
Mjumbe wa kwanza alisimama na kutaka kukumbushwa ni mtu gani ambaye amekuwa mara kwa mara akikaimu nafasi ya ukurugenzi pale Matakwali anapokuwa hayupo, yaani pale anapokuwa yuko safari au likizo.
Matakwali alisimama na kujibu kwamba huko nyuma aliyekuwa akikaimu nafasi yake anapokuwa hayuko ofisini alikuwa Mhandisi Hassan Majura ambaye alihamishiwa wizarani na kwamba katika siku za karibuni aliyekuwa akikaimu zaidi ni Mhandisi Bruno Mapunda na kwamba Jackson Malima naye alishamkaimisha nafasi hiyo mara kadhaa.
Baada ya jibu hilo mjumbe huyo alisimama tena na kuhoji: “Kama Bwana Mapunda ndiye amekuwa akikaimu mara nyingi nafasi ya ukurugenzi, kwa nini asiendelee kukaimu wakati huu hadi hapo mkurugenzi mpya atakapoteuliwa na Mheshimiwa Rais, iwe ni yeye Mapunda, Malima au mtu mwingine kutoka nje ya TTM?”
Matakwali alisimama na kujibu kwamba amekuwa akimwachia Mapunda ofisi anapokuwa hayupo kwa sababu ya uwepo wake wa muda mrefu kwenye tume na siyo uwezo.
“Naweza kusema hizo mara chache nilizomkaimisha Bwana Malima, alifanya vizuri zaidi,” alijibu Matakwali.
Mjumbe mwingine alisimama na kuzidi kumpinga Matakwali akimtaka Mapunda kwa madai kwamba kwa vile kampuni ile inahusiana na masuala ya teknolojia ya mawasiliano ilitakiwa mkurugenzi awe mwenye taaluma hiyo kwa maana ya Mhandisi Mapunda kama ilivyo kwa Matakwali kuliko kuweka mtu mwenye taaluma nyingine tofauti.
“Tumeambiwa hapa kwamba huyo anayependekezwa ni mwanasheria ingawa tumeambiwa pia kwamba masuala haya ya kiteknolojia pia anajifunza, lakini huyu hawezi kuwa sawa na mhandisi halisi kama Mr Mapunda,” alisisitiza mjumbe huyo.
Matakwali alisimama tena kujibu hoja hiyo akisema kwamba uongozi wa tume ulikuwa haumhitaji mtalaamu wa masuala ya teknolojia bali uwezo wa kuongoza, kutoa maelekezo sahihi, kubuni miradi, umakini, uchapa kazi na uadilifu.
“Sisemi kwamba Bw. Mapunda hana sifa hizo, lakini kwa kuwalinganisha, Bw. Malima anafaa zaidi. Isitoshe, kama nilivyodokeza awali, Bw. Malima ni mtu wa kujifunza sana, humdanganyi kitu,” alisisitiza Matakwali.
Mjumbe mwingine alisimama na kusema yeye anaungana na wanaotaka nafasi hiyo ikaimiwe na Bruno kwa maelezo kwamba ana uzoefu kuliko Jackson.
“Siku zote uzoefu ni mwalimu mzuri sana. Nashangaa kwa nini tuache mzoefu, tena mhandisi kitaaluma, halafu tuchukue mtu asiye na uzoefu wa kutosha na ambaye taaluma yake siyo inayohusiana na core business ya tume,” alifafanua mjumbe huyo.
Mjumbe mwingine tena alisimama na kuunga mkono Bruno ndiye akabidhiwe madaraka ya kukaimu akidai hoja za wale wanaoona kwamba anafaa yeye kupewa nafasi hiyo zina nguvu kuliko mkurugenzi anayestaafu kwa kumpendekeza Jackson kisha akataka ipigwe kura.
Huku akijua kwamba wajumbe wale, wengi wao kama si wote walikuwa bila shaka wameshanunuliwa na Bruno, Mwenyekiti alisimama na kusema hakukuwa na sababu za kupiga kura isipokuwa kuzingatia nguvu ya hoja.
“Tukubaliane kwamba kama kuna mtu anawajua vizuri watu hawa wawili ni Matakwali. Tukubaliane pia kwamba tuko hapa kwa sababu ya kushauri na kuhakikisha Tume inafanya vyema zaidi na siyo vinginevyo.”
Mwenyekiti akakohoa kidogo kusafisha koo lake, akaendelea: “Mkurugenzi amejitahidi sana kumwelezea vizuri Malima. Binafsi pia nimefanya utafiti wangu kwa siku mbili hizi kuona ni nani atatufaa na hivyo ninaungana na Mkurugenzi moja kwa moja kwa mapendekezo yake.
“Ngoja nisimung’unye maneno kwa kusema ukweli kwamba katika utafiti wangu unaonesha kwamba Mapunda si mwadilifu sana. Mimi amenitafuta sana ili nimuunge mkono katika hili lakini ninajua hafai. Na waswahili wanasema kweli kwamba kibaya chajitembeza lakini kizuri chajiuza.
“Isije ikawa pia kapitapita huko kwenu wajumbe wenzangu. Tuambizane tu ukweli kwa faida ya tume. Rais ametubakiza hapa ili tuisaidie tume na siyo vinginevyo…, Naona makamu wangu naye anataka kusema kitu,” alisema akimwangalia makamu wake, Josiah Mafumu, aliyekuwa kanyoosha mkono.
Makamu huyo mwenyekiti aliposimama akaunga mkono mapendekezo ya Matakwali na ya Mwenyekiti akisema kulikuwa wala hakuna sababu ya kupiga kura kwani kinachotafutwa si uwakilishi wa watu bali kuangalia sifa ya anayefaa kuongoza tume kwa muda kabla Rais hajafanya uteuzi wake.
“Profesa alijipa kibarua cha kuchunguza ni nani anaweza kuvaa viatu vya Mhandisi Matakwali katika kuipeleka mbele Tume na mimi pia nimefanya kazi hiyo. Nimehoji wafanyakazi bila wao kujua ninachokitafuta na mwisho wa yote nikagundua kwamba hata kama tulizoea kuona Bw. Mapunda akikaimu ofisi lakini katika hili si Mnyamwezi tunayemtafuta. Kwa sababu Waswahili wanasema mzigo mzito mpe Mnyamwezi basi ninawahakikishieni wajumbe wenzangu kwamba hapa Mnyamwezi anayeweza kubeba huu mzigo ni Malima.”
JACKSON Malima alikuwa ofisini kwake akiendelea na kazi huku tukio la Tanga likiendelea kumsumbua kisaikolojia. Kilichomharibia siku yake mapema asubuhi hiyo ya Jumanne ni habari katika moja ya magazeti yaliyokuwa mezani kwake.
Alijilaumu hata ni kwa nini alikimbilia kusoma magazeti ya siku hiyo baada ya kuwekwa mezani kwake na mhudumu. Katika gazeti hilo kulikuwa na mwendelezo wa habari ya ‘Baamedi wa Tanga Raha Club’ aliyedaiwa kuuliwa na mpenzi wake kwa kunyweshwa sumu.
Ndani ya habari hiyo mwandishi aliwakariri polisi wakisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba wanakaribia kabisa kumkamata muuaji. Jackson alijiuliza sana kuhusu dhana ya sumu na dhana ya kukaribia kumkamata muuaji zilimaanisha nini.
Kwanza hakuamini tuhuma za sumu. Alihisi kwamba ama polisi wanadanganya au daktari aliyemfanyia uchunguzi hakupima sawasawa. Yeye aliamini kwamba Eggy aliumwa ghafla. Alijilaumu sana kwa nini hakuchukua hatua haraka ya kumkimbiza hospitali pale msichana huyo alipoanza kulalamikia tumbo.
Wakati akiendelea kutafakari tukio hilo lililomwachia maswali mengi, Andrew Mambo aliingia ofisini kwake na mara moja aligundua kwamba Jackson hakuwa sawa.
“Vipi Malima, unaumwa au bado unasumbuliwa na tukio la yule binti?” Aliuliza Andrew.
“Kwa nini unasema hivyo?”Jackson naye aliachia swali
“Ninakuona tu. Uso wako hauna bashasha. Yaani mtu yeyote anayekufahamu akiingia hapa ofisini kwako anajua hauko sawa.” Andrew alimfafanulia vizuri huku akimtazama
“Kwa kweli ndugu yangu, tukio la kifo cha yule msichana linanikosesha raha sana. Yaani ninajiona kama muuaji. Laiti ningelimwahisha hospitali, haya yote yasingetokea. Nina hakika yule binti alikuwa anaumwa lakini nashangaa wanavyosema alinyweshwa sumu,” alisema Jackson akimsukumia gazeti.
“Nitaisoma hiyo habari baadaye lakini nimekuja kukupa nyepesi nyepesi kwamba kikao cha bodi kinaendelea na Makamu Mwenyekiti amenijulisha mapema asubuhi hii kwamba Mapunda keshahonga wajumbe karibu wote ili wampitishe.”
“Mimi sioni shida kama wakimpitisha, lakini ninachoomba ni awe mwepesi tu kupokea ushauri wowote mzuri kutoka kwetu kwa ajili ya maendeleo ya tume, basi,” alisema Jackson.
“Hiyo ndio shida kubwa ya Mapunda. Huwa anadhani kwamba anajua kila kitu. Yaani kumkabidhi Mapunda kuendesha taasisi ni sawa kumkabidhi fisi mwenye njaa akulindiye ndama. Ni fisadi, hasidi na mtu mwenye roho mbaya kweli kweli. Ninajua hata wafanyakazi wengi watasikitika sana akipewa yeye uongozi wa tume.”
“Ninajua hilo… Lakini Makamu Mwenyekiti kakuambia yeye anaonaje?”
“Ameniambia kwamba wameshaweka msimamo na Mwenyekiti kwamba hawawezi kukubali kumpitisha Bruno.”
“Kama wajumbe wengi watamtaka Bruno, wataweza kuzuia?” Kabla Andrew hajajibu swali lile, askari wawili wakiwa wamevaa sare za polisi waliingia ofisini pale.
“Hamjambo mabwana?” Alisalimia mmoja wao.
“Hatujambo,” alijibu Jackson akishangaa askari wale walipitaje mapokezi hadi ofisini kwake bila hata kupigiwa simu na karani wa mapokezi. Huo haukuwa utaratibu wa kawaida.
“Tuwasaidie nini ndugu?” Akauliza Jackson.
“Bila shaka wewe ndiye Jackson Jorwa Malima?” Aliuliza askari mmojawapo akimwelekea Jackson.
“Ndio mimi, niwasaidie nini?” Alijibu huku moyo wake ukimlipuka. Akakumbuka habari ya kwenye gazeti ambayo Kamanda wa polisi alikaririwa akisema wanakaribia kabisa kumkata muuaji.
“Sisi ni askari polisi kutoka kituo kikuu hapa Dar es Salaam. Kuanzia sasa uko chini ya ulinzi. Unahitajika kituoni.”
“Ninaweza kuona vitambulisho vyenu?”
“Kwani haya mavazi hayakutoshi?” Alihoji askari yule kwa hasira.
“Ndio, wakati mwingine hata majambazi wanavaa sare,” Jackson alijitahidi kujibu kwa upole huku hofu ikizidi kutanda moyoni mwake. Yule askari alitoa kitambulisho na kuonesha.
“Haya, kosa langu ni nini?”
“Utajua mbele.”
“Yaani hata katika zama hizi bado kuna askari wanakamata watu bila kuwaambia makosa yao? Tafadhali nijulisheni kosa langu. Hiyo ni haki yangu,” alijibu kwa upole Jackson.
“Inaonekana unajifanya mjuaji… Haya unatuhumiwa kumuua changudoa Tanga. Nadhani unajua,” alijibu.
“Kwa hiyo mnataka nini kwa sababu hilo unalosema sihusiki?”
“Tunakuheshimu ndugu. Tumeshakwambia uko chini ya ulinzi na umetaka tukuambie kosa. Sasa tunakuomba unyanyuke twende kituoni.”
Wakati akinyanyuka kwa sababu hakutaka kufanya ubishi, Jackson alikuwa anajiuliza haraka haraka ni nini hasa kiliwaongoza askari hao kuja kwake. Wale askari walitaka kumtia pingu baada ya kunyanyuka lakini akawaambia.
“Ndugu zangu, mmesema ninyanyuke, nimenyanyuka. Sasa kupigana pingu kwa sababu gani tena?” Alihoji Jackson. Andrew naye akaamua kuingilia kati akisema anaamini wamekuja kumkamata kama walivyodai na si kumfedhehesha.
“Huyu ni mtu anayejiheshimu na siyo kibaka. Chonde ninawaomba mabwana acheni kumfunga pingu,” alisema na wale askari wakaamua kumwacha bila kumtia pingu.
“Andrew, nadhani umeshuhudia kila kitu, basi utatoa taarifa kwa wengine kwamba nimekamatwa. Sipendi niwe wa kwanza kumjulisha mke wangu kuhusu hili. Naomba umjulishe wewe,” alisema kisha akamtajia namba za simu za mke wake baada ya Andrew kusema alizipoteza baada ya simu yake ya awali kuharibika na kununua simu mpya na hivyo kupoteza namba nyingi ikiwemo ya mkewe Jackson.
* * *
Salome Bakunda au Salome Malima kama alivyojulikana zaidi kazini kwake kutokana na jina la mumewe huku wengine wakimwita Mama Malima, alimaliza kusoma habari ya mauaji ya baamedi wa Tanga Raha Club na kuzidi kupata hasira.
Alishukuru gazeti hilo kumkumbusha habari ambayo mpaka anafika ofisini siku hiyo ya Jumanne alikuwa hajaanza kuandaa mpango kazi wa namna ya kushughulikia tukio hilo.
Sasa alidhamiria kuacha shughuli zake za siku hiyo alizokuwa anafanya ili kwanza kujikita katika suala hilo na hatimaye kumshawishi bosi wake ili ofisi yao ianze kulifuatilia mara moja.
Alipomfikiria mtoto wa marehemu, aliwakumbuka pia wanawe. Akajiuliza ingekuwaje ni yeye ndiye kauawa na kuwaacha wanawe bila mama.
Maelezo ya binti aliyekuwa akiishi na marehemu ndio yaliyomtia huzuni zaidi na hasira kila alipofikiria namna ndoto za Agnes zilivyokatishwa kinyama na mwanaume aliyemuua kwa sumu.
“Mshenzi mmoja anakatisha maisha ya binti wa watu aliyekuwa na ndoto nyingi za maisha kwa sababu tu yeye ni mwanaume. Anasababisha mtoto wa marehemu ambaye mama yake alianza kujiandaa kuboresha maisha yake kuendelea kulelewa na bibi ambaye pia pengine anatakiwa kulelewa… ni mbaya sana,” alijisemea.
Kutokana na gazeti alilosoma kuonesha kwamba ulikuwa ni mwendelezo wa habari ya jana yake, aliona umuhimu wa kutafuta gazeti la Jumatatu ili kujua mengi zaidi kuhusu mkasa huo.
Salome alimpigia wakala wa magazeti akimuuliza kama anaweza kupata gazeti lolote la Jumatatu lililokuwa na mkasa wa Baamedi wa Tanga Raha Club kwa kina.
“Mama, ungechelewa kidogo tu usingelipata kwa sababu ndio nilikuwa ninapanga kurejesha mabaki ya magazeti ya jana,” alisema wakala huyo wa magazeti aliyekuwa akiwaletea nakala za baadhi ya magazeti ofisini kwao.
Kwa kuwa ofisi yao haikuwa mbali sana na mahala wakala huyo alikokuwa akifanyia shughuli zake za kusambaza magazeti, maeneo ya Kariakoo, baada ya dakika kumi Salome alikuwa anakabidhiwa gazeti alilokuwa akilihitaji.
Alikuwa anataka kuchukua maelezo zaidi ili apate pa kuanzia kwa sababu alidhamiria ofisi yao ifuatilie kwa karibu suala hilo hadi mwisho na kutoa msaada wa kisheria utakaohitajika ili kuhakikisha kwamba mhusika wa mauaji hayo analipia uhalifu wake.
Kitu kizuri ni kwamba mfadhili wa asasi yao ya kiraia alikuwa ameshatoa fedha za kutosha kwa ajili ya masuala ya aina hiyo na hakukuwa na sababu yoyote ambayo ingekwamisha taasisi yao kushindwa kufuatilia.
Baada ya kusoma magazeti yote mawili, alichukua daftari lake dogo na kuanza kuandika mambo muhimu kuhusu sakata hilo.
Aliandika jina la msichana aliyeuawa kwa sumu, umri wake, klabu aliyokuwa akifanya kazi, sumu inayodaiwa kumuua ambayo kwa mujibu wa habari alizosoma ilionekana pia kwenye chupa ya bia iliyokutwa chumbani alimokuwa na jina la nyumba ya kulala wageni alimofia.
Alichukua pia majina ya watu ambao wanaweza kuwa mashahidi muhimu katika kesi hiyo ambao ni pamoja na mlinzi katika nyumba ya wageni alimofia Agnes, mhudumu wa mapokezi, rafiki aliyekuwa akiishi na marehemu pamoja na meneja wa klabu ya Tanga Raha.
Maswali ambayo yalitakiwa kujibiwa ni nani alifanya uhalifu huo na sababu za kufanya hivyo. Ingawa sababu zilikuwa hazijatajwa lakini kutokana na uzoefu wake, kwa asilimia zaidi ya 70 alihisi zitakuwa zinatokana na masuala ya mapenzi.
Alihisi kwamba huenda mwanaume aliyekuwa na baamedi huyo ni mpenzi wake wa siku nyingi na huenda alitaka kumbinafsisha lakini msichana huyo mrembo ambaye picha yake ilikuwa kwenye gazeti akawa mgumu kukubaliana naye.
Alihisi pia kwamba huenda mwanaume aliyemuua ndiye alizaa naye mtoto wake wa kwanza na pengine akawa anataka warejeane lakini msichana huyo akawa hataki.
“Kama waandishi hawa wangekuwa makini wangelimtafuta huyu baba wa mtoto wake au pengine wanamtafuta. Anaweza kuwasaidia,” alijisemea.
Ofisi yao ilikuwa pia imewahi kushughulikia matukio ya akina dada kuuawa na watu waliozaa nao au wapenzi wao wa zamani waliokuwa wanalazimisha kuwaoa au kuwamiliki tena bila mafanikio na ndio maana akapata hisia hizo.
Lakini pia miongoni mwa kesi walizowahi kuzifuatilia ni za mtu mmoja ambaye alikuwa akichukizwa na uwepo wa machangudoa mitaani. Mtu huyo akadhamiria kuwamaliza kwa kuwaua ambapo alikuwa anawachukua kama mteja na kwenda nao kwenye nyumba za kulala wageni ambako aliwaua kwa kuwanyonga, wengine kwa sumu na wengine kuwachoma visu kutegemea na mazingira.
Mtu huyo kila alipokuwa akiua aliacha ujumbe usemao ‘Makahaba mjiandae’. Hata hivyo, mtu huyo aliwekewa mtego na kukamatwa akijiandaa kuua msichana wa saba.
Jambo moja lililokuwa limemtia faraja Salome katika gazeti la siku hiyo ni kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani Tanga kwamba jeshi lake linakaribia kabisa kumnasa muuaji. Lakini pia alihisi hayo yanaweza kuwa maneno tu ya kuwatia moyo wasomaji na wananchi ili walione jeshi kwamba liko kazini na siku ipite!
Baada ya kuandika mambo muhimu kuhusu kesi hiyo, Salome alinyanyuka kuelekea ofisini kwa bosi wake, Dk Jumanne Marijani. Huyu udaktari wake haukuwa wa uzamivu (PhD) bali udaktari bingwa wa tiba za binadamu, hususani magonjwa ya akina mama.
Alimkuta pia akisoma gazeti na Salome alihisi bila shaka atakuwa anasoma habari hiyo hiyo ya Baamedi wa Tanga Raha Club. Kutokana na shughuli zao zilizojielekeza katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa akina mama na watoto, kila aliyekuwa akishika gazeti anaanza kwanza kutafuta habari za aina hiyo kabla hata ya kusoma habari inayoongoza kwa siku hiyo.
“Bosi, bila shaka unasoma habari ya mauaji ya msichana wa Tanga,” aliuliza Salome baada ya kumjulia hali bosi wake ambaye walikuwa hawajakutana asubuhi hiyo.
“Ndio. Salome, inasikitisha sana. Ninaifuatilia tangu Jumamosi nilipoiona ikitangazwa kwenye runinga,” alijibu Dk Marijani.
“Kilichonileta ni habari hiyo hiyo. Jana nilitingwa na shughuli nikasahau kuizungumzia. Ninataka tuifuatilie kwa karibu na huyu mtuhumiwa atakapokamatwa tuongeze nguvu za kisheria. Ninataka ikiwezekana hii iwe kesi yangu ya kwanza kusimama mahakamani kama wakili wa marehemu na kwa mantiki hiyo kusaidiana na Serikali ili kukomesha haya mauaji. Ninataka huyu mwanaume aliyefanya haya tumshikishe adabu,” alisema Salome aliyekuwa akiongea kwa hisia kali akijitahidi kuzuia machozi.
“Bila shaka Mama Malima. Hata wakati ninasoma hii habari nilikuwa ninafikiria wapi sisi tunaweza kuingilia ili kutoa mchango wetu katika kukomesha mauaji ya wasichana wasio na hatia,” alisema.
“Ninashukuru bosi kwa hilo. Kwa hiyo mimi ninaanza kufuatilia. Nataka kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Tanga kujua maendeleo ya hii kesi na kisha nimweleze nia yetu ya kulisaidia jeshi la polisi.”
“Utaniandalia tu mpango kazi wako na bajeti. Kama utataka kusafiri kwenda Tanga utaonesha kwenye mpango kazi wako. Lakini nadhani mpango mzima utaanza baada ya mtuhumiwa kukamatwa na hapa nimeona askari wakijigamba kwamba wanakaribia kumkamata.”
“Ndio Bosi. Ndio maana nimesema nitakuwa ninawasiliana na polisi Tanga.”
“Ninakutakia kila heri Mama Malima. Kama kesi hii utaisimamia vyema hadi mwisho kwa kushirikiana na mawakili wa Serikali na mhusika kupewa adhabu anayostahili, wafadhili wetu watafurahi sana. Usisahau kuwashirikisha waandishi wa habari hasa wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake kwa kila hatua utakayochukua.”
“Sawa bosi.”
* * *
Wakati vuta nikuvute ikiendelea ndani ya kikao cha Bodi huku wajumbe wakikubali kwa shingo upande msisitizo wa Mwenyekiti kwamba mtu atakayevaa viatu vya Matakwali ni Jackson Malima, karani wa Matakwali aliingia kwenye chumba cha mkutano ghafla na kumfuata mezani alikokuwa amekaa bosi wake.
Alipofika akamnong’oneza kwamba Jackson alikuwa amekamatwa muda ule na polisi.“Wameshuka naye sasa hivi na pengine watakuwa getini,” alisema karani yule.
“Inakuwaje mtu anakuja kukamatwa hapa ofisini bila mimi kutaarifiwa?” Alihoji kwa hamaki Matakwali.
“Walianzia ofisini kwa bosi Mapunda. Nadhani bosi Mapunda, aliona kwa kuwa upo kwenye kikao kizito ndio akaamuru waendelee na kazi yao. Ndiye pia kanituma nikuletee huu ujumbe,” alijibu yule karani.
“Kama hao askari hawajaondoka naye kawaambie wanisuburi. Fanya haraka. Ondoka,” alisema Matakwali aliyeonekana kushitushwa na habari hizo. Wakati karani anaondoka, Matakwali alisimama na kuwaambia wajumbe wa bodi alichoambiwa na karani wake.
“Tafadhali mnisubiri mara moja niongee na hawa askari, ninakuja mara moja,” alisema Matakwali akinyanyuka na kutoka haraka.
Alishuka ngazi kutoka ghorofa ya tatu walikokuwa kwenye ukumbi wa mikutano kueleka chini haraka na kukuta askari wale wakiomba wafunguliwe geti waondoke kwa sababu walikuwa hawana sababu ya kusubiri mtu huku karani aliyetumwa na Matakwali akiwaambia askari wa getini wasifungue kwanza hadi Mkurugenzi afike.
Matakwali alipofika alikwenda hadi kwenye gari lao na kuwasalimia kisha akajitambulisha.“Ndugu zangu, mnafika kwa mtu, mnachukua familia yake bila kujitambulisha kwake?” Alihoji.
“Kuna bosi mmoja alishatupokea na kutupa baraka zote. Isitoshe sisi tukija kukamata mhalifu si lazima tupate ruhusu ya mtu,” alijibu mmoja wao mwenye cheo cha sajini.
“Haya niambieni, mmemkamata ofisa wangu mwandamizi kwa kosa gani?”
“Mtuhimiwa anajua lakini kwa faida yako ni kwamba kaua baamedi aliyekuwa naye gesti kule Tanga Ijumaa iliyopita.”
“Haiwezekani,” alisema na kumwangalia Jackson aliyekuwa ameketi kiti cha nyuma cha gari lile ambayo alipochunguza vizuri lilikuwa gari la kiraia. “Hawa wanasema nini Malima, mbona siwaelewi?”
“Wananituhumu hivyo bosi, lakini nakuhakikishia sihusiki abadani na hilo. Nakushauri wewe kachape kazi, niache nao lakini Mwenyezi Mungu akipenda ukweli wa hili utajulikana,” alisema Jackson kwa utulivu.
Mkurugenzi Matakwali aliondoka kwa masikitiko kurudi chumba cha mikutano cha bodi huku akiwaza namna atakavyowaambia wajumbe.
Alipofika, huku akionekana mnyonge, Matakwali aliwajulisha wajumbe wa bodi kilichotokea na kuwataka wajadili la kufanya. Mwenyekiti wa Bodi alionelea kwamba waahirishe kikao wakisubiri mustakabali wa Jackson.
Ushauri huo ulipingwa na wajumbe ambao walisema kama Jackson anatuhumiwa kwa mauaji, kesi inaweza kumaliza miaka hata mitano, kitu ambacho hawawezi kuendelea kusubiri na Tume haiwezi kuendeshwa bila kuwa na kaimu mkurugenzi.
“Malima ninayemfahamu mimi hawezi kufanya kitu kama hicho, lakini na mimi naungana na mjumbe kwamba tuangalie tunafanyeje ili ikiwezekana kesho awepo mtu wa kukaimu,” alisema Matakwali.
“Makamu mwenyekiti alisimama: Mimi nilikuwa nafikiria kwamba kikao hiki kimpitishe, Andrew Mambo ambaye ni Ofisa Rasilimali Watu, akaimu haya madaraka bila kupitishwa na bodi, yaani iwe kama kaachiwa tu ofisi na Mkurugenzi hadi tutakapokutana tena na kuona kama tumpitishe yeye au mtu mwingine. Pengine Malima atakuwa keshamalizana na polisi muda huo.”
Wazo hilo liliungwa mkono na Matakwali lakini wajumbe wengine walilipinga vikali. Wakahoji ni kwa nini meza kuu ilikuwa haimtaki Bruno hata katika mazingira kama hayo?
“Kwani Mapunda kawafanyia nini kibaya? Hapa tulikuwa tuna majina mawili tunayoyajadili, Mapunda na Jackson. Kama Mwenyezi Mungu ametuonesha mbele ya macho yetu kwamba huyo mnayemtaka kumkabidhi ofisi hafai kwa nini tusimpe huyu mwingine? Kwa nini makamu aje na jina lingine?” Alihoji mjumbe mmoja wapo.
Matakwali alijibu hoja hiyo akisema jina la mtu aliyependekezwa, kwa mtazamo wake alikuwa anafaa kuliko Bruno na kujaribu kueleza wasifu wake lakini wajumbe wakampinga. Mwenyekiti kwa kuhisi ataonekana ana lake jambo kuendelea kumpinga Bruno, akajikuta anakosa hoja na kukubaliana na wajumbe wengi kumpitisha Bruno kukaimu nafasi ya Matakwali.
Hata hivyo, moyoni aliapa kwamba angeharakisha kujadiliana na Waziri pamoja na Rais kumpata mkurugenzi mpya ambaye si Bruno hata kama anatoka nje ya taasisi kama Jackson ataendelea kung’ang’aniwa na polisi.
* * *
Jackson alifikishwa kituo kikuu cha polisi na kutakiwa kuandika maelezo. Aliwaambia askari waliomkamata kwamba asingeandika maelezo hayo kabla ya kukutana na wakili wake na hivyo akaomba awasiliane naye kwanza.
Askari hao bila shaka walidhani mtuhumiwa yule mbele yao ni mtu wa ‘kusukumwa sukumwa’ tu. Wakataka kumshurutisha kuandika maelezo kwa nguvu lakini akawaambia yeye ni mwanasheria kwa hiyo anachokiomba ana haki nacho kisheria na kikatiba.
Akaonya kwamba anaweza kuandika kwa kushurutishwa lakini askari hao pia wajiandae kwa kile atakachowarejeshea kisheria.“Madhali niko mikononi mwenu hampaswi kuwa na haraka yoyote, tekelezeni tu yale ambayo nina haki nayo.”
Akaendelea:“Nitafanya mtakachonilazimisha mkitaka lakini nina matumaini kwamba mtanipa haki yangu ya kuwakilishwa kwenye shauri hili. Kwanza mliponikamata mlitakiwa kunieleza kituo mnachonipeleka na muda huo ningeshampigia wakili wangu. Lakini nilikuwa sijui mnanipeleka wapi, hivyo mtalazimika kusubiri aje. ”
Wale askari walikubali kuchukua ushauri wake na kumpa wasaa wa kumwita wakili wake. Alimpigia simu Wakili Hussein Magabhanya, mtu aliyesoma naye sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye wakati huo alikuwa wakili maarufu katika jiji la Dar es Salaam. Mbali na kusoma pamoja, chuoni walikuwa wakilala chumba kimoja na kushirikiana mambo mengi.
Baada ya kuongea naye, Jackson aliwajulisha askari wale kwamba wakili wake alikuwa na kesi kadhaa mahakamani mchana huo na kwamba angekuwa na nafasi ya kuja pale kituoni baada ya saa 9:00 alasiri. Askari mmoja aliona kama huo ni muda mrefu kwa sababu maelezo yake yalikuwa yanahitajika mapema.
“Maelezo yangu yanahitajika mapema kivipi na nani anayeyahitaji? Kama sikosei muda wenu wa kusubiri kisheria ni saa nane na kama muda huo ukipita nitakuwa hiari kuandika maelezo bila wakili wangu. Hili ni shauri ambalo haki inapaswa itendeke pande zote, kwa mimi ninayeshtakiwa na anayenishtaki kwa maana ya Jamhuri mnayoiwakilisha. Natumaini busara itawatuma msubiri tu hadi muda huo ambao umeelezwa na sheria.”
“Wewe shauri lako liko Tanga. Unatakiwa baadaye usafirishwe kwenda Tanga na hatujui itakuwa lini lakini inabidi utakapohitajiwa maelezo yako yawe tayari. Kwani huwezi kupata wakili mwingine? Wewe si mwanasheria, unawajua wengi?”
“Kumbe kama ni Tanga basi hata huko ninaweza kuandika maelezo. Ninaweza kuwa ninawajua mawakili wengi lakini si mawakili wangu. Katika hili mtapaswa tu kusubiri huo muda wa kisheria uliowekwa,” alisema Jackson ambaye kutokana na kutoshughulikia kwa muda mrefu masuala ya kesi za jinai, alikuwa hakumbuki vyema mambo mengi ya kipolisi ikiwa ni pamoja na muda ambao mtuhumiwa anaweza kupewa kuwasiliana na wakili wake kabla ya kuandika maelezo.
Maofisa wale wa polisi ambao inaonekana, walikuwa hawafanyi kazi waliyofundishwa chuoni isipokuwa ubabe na kutumia udhaifu wa wananchi kutojua sheria kufanya wanayotaka, wakakubali kusubiri kwa shingo upande.
* * *
Saa sita mchana wafanyakazi walianza kuingia kwenye ukumbi wa mikutano wa bodi. Dakika saba baadaye ukumbi ulikuwa umejaa wafanyakazi wa Tume ya Teknolojia na Mawasiliano, baadhi wakilazimika kusimama kwa kukosa viti.
Takribani wote walikuwa wanajua ajenda ya kikao kile kwamba ilikuwa ni kuagana na bosi wao, Ibrahim Matakwali ambaye wao walizoea kumwita ‘Mzee’.Ukisikia mfanyakazi anasema ‘Mzee anakuita’, ‘Mzee kasema hivi’ na kadhalika basi ujue walimaanisha Mhandisi Ibrahim Matakwali.
Lakini hamu yao kubwa ilikuwa ni kujua ni nani atakayekaimu nafasi yake au kama tayari Rais alikuwa keshateua mkurugenzi mpya. Kutokana na malalamiko mengi ambayo walikuwa wakiyatoa dhidi ya Bruno, mtu ambaye kwa nafasi na uzoefu wake alipaswa kukaimu madaraka hayo, walikuwa wanajua fika kwamba ‘Mzee’ asingefanya kosa la kumwachia ofisi yake kama Rais alikuwa hajachagua mkurugenzi mwingine kutoka nje ya tume.
Kwa muda wa wiki nzima, kulikuwa na uvumi kwamba Jackson ndiye alikuwa anatazamiwa kukaimu madaraka hayo ingawa hakukuwa na mfanyakazi hata mmoja aliyekuwa amethibitisha habari hizo.
Kwao zilikuwa habari njema kutokana na mahusiano mazuri aliyokuwa nayo na wafanyakazi wenziye na uadilifu wake. Mara chache alizoachiwa ofisi, Jackson alionekana kuwa msaada mkubwa kwa wafanyakazi wenzake, akishughulikia hata matatizo yao binafsi na wengine kuwatembelea majumbani.
Kuanzia kipindi hicho, Matakwali alikuwa akimtegemea sana hata katika kusuluhisha migogoro ya baadhi ya wafanyakazi na wenzi wao. Kwa mfano, kuna huyu aliyekuwa ameitelekeza familia yake na kuhamia kwa hawara huku muda mwingi akishinda kwenye mabaa. Jackson alikwenda naye taratibu, wakati mwingine akimshirikisha mkewe, Salome, hadi akafanikiwa kumrejesha nyumbani kwake na kuachana na hawara na kuanza kuihudumia familia yake ipasavyo.
Ukaribu wake na Andrew uliongezeka baada ya kusaidia kuokoa ndoa yake iliyokuwa inaelekea kusambaratika.
Wengi ambacho hawakujua ni kwamba elimu ya ushauri-malezi alikuwa anaipata kutoka kwa mkewe, Salome, ambaye asasi aliyokuwa akiifanyia kazi iliwahi kumpeleka nchini Uingereza kwenda kusomea masuala hayo kwa kipindi cha miezi mitatu. Mkewe pia alikuwa ameshiriki semina kadhaa ndani na nje ya nchi kuhusu masuala ya jinsia, afya ya uzazi, malezi na saikolojia ya mahusiano.
Baadhi ya wafanyakazi wa kike ndio walifurahia zaidi uvumi huo kwa sababu walikuwa na hofu sana na Bruno ambaye alikuwa akijulikana pia kwa kupenda kila mwanamke anayepita mbele yake. Kulikuwa na tuhuma kwamba mwanamke anayemkataa alikuwa hata yuko radhi ‘kumkomesha’ kwa kumnyanyasa na hata kumpa vitisho vya kufukuzwa kazi.
Pia alituhumiwa kwa uchoyo wa safari za kikazi katika mikoa mbalimbali ya nchi ambazo zilisaidia kuwaongezea kipato wafanyakazi na hasa kwa vile nyingi zilitokea ofisini kwake akiwa kama Mhandisi Mkuu wa Tume.
Mara nyingi mambo kama hayo yenye maslahi alitaka aende yeye mwenyewe, na kama sivyo basi alimpendelea mfanyakazi mmoja waliyekuwa na undugu naye au msichana mmoja kwenye idara yake ambaye ilisemekana ana uhusiano naye wa kimapenzi.
Hata hivyo, asubuhi hiyo kulikuwa kumezuka uvumi mwingine kwamba ‘Baba Mchungaji’ Jackson, alikuwa amekamatwa na polisi. Baada ya kusikia uvumi huo, Andrew aliamua kutoka ofisini kwake na kupita akiukanusha kwa nguvu zake zote ili kulinda heshima ya Jackson katika kipindi hicho ambacho alikuwa anaamini kwamba jina ambalo lingetangazwa ili kukaimu nafasi ya ukurugenzi wa tume ni la Jackson.
Aliyekuwa amevujisha uvumi huo ni karani wa Bruno, huyo aliyekuwa akituhumiwa kutembea naye huku akiwathibitishia wafanyakazi kwamba alimwona akiwa kapigwa pingu. Ukanushaji uliofanywa na Andrew uliungwa mkono na wafanyakazi wachache ambao walikutana na Jackson kwenye korido akiongozana na askari waliokuwa kwenye sare huku akiwa hana pingu zozote.
Wakati wafanyakazi wanasubiri, hamu yao kubwa ikiwa ni kujua atakayekaimu au kuchukua moja kwa moja nafasi ya ‘Mzee’, muda waliousubiri ukawadia. Akaingia Matakwali pale ukumbini akiwa ameandamana na menejimenti yake pamoja na Mwenyekiti wa Bodi na makamu wake.
Miongoni mwa wajumbe wa menejimenti alikuwepo Mhandisi Mkuu wa Tume (Bruno), Ofisa Raslimali Watu (Andrew), Meneja wa Fedha na Meneja wa Majengo. Kidogo wafanyakazi walishituka kwa kutomwona pale Mwanasheria wa Tume, Jackson Malima.
Baada ya kuketi, mwenyekiti wa kikao hicho, Matakwali, alisimama kuwasalimia wafanyakazi, kisha akatoa hotuba yake ndefu kuhusu namna walivyopewa jukumu la kuanzisha tume hiyo na Serikali, magumu aliyopitia, mafanikio na changamoto alizopambana nazo na zinazoendelea. Matakwali pia aliwashukuru wafanyakazi wote kwa kumuunga mkono muda wote aliokuwa ofisini na kuwaomba radhi wale aliowakosea.
“Kwanza niseme, kama alivyowahi kusema Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel Arap Moi, kwamba wale wote walionikosea nimewasamehe kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwangu. Lakini kwa vile mimi kama mwanadamu nina upungufu mwingi na udhaifu, ninaomba wote niliowakosea kwa kujua au kutojua mnisamehe,” alisema.
Hatua hiyo ililipua sauti kubwa miongoni mwa wafakanyakazi zaidi ya 100 waliokuwa wamejumuika siku hiyo ikisema ‘tumekusamehe Mzee’. Matakwali aliendelea kueleza mengi kuhusu jinsi anavyoiacha taasisi, kisha akamkaribisha Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Mwinchumu ili kutaja jina la mtu atakayekaimu nafasi ya ukurugenzi hadi hapo Rais atakapoteua mkurugenzi mwingine.
Profesa Mwinchumu alianza kwa kuwashukuru wafanyakazi wote kwa juhudi zao za kila siku na akawataka kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na juhudi ili kuzidi kuboresha shughuli za tume ambayo alisema ni chombo muhimu katika maendeleo ya kisasa yanayoletwa na matumizi ya Tehama. Na kwamba ni chombo chenye jukumu adhimu la kusaidia Serikali katika kujenga uchumi unaotegemea viwanda. Kikubwa aliwataka kutoa ushirikiano mkubwa kwa kaimu mkurugenzi ambaye ataiongoza tume hadi Rais atakapochagua mkurugenzi mpya.
Baada ya maelezo hayo, akasema kwa sasa atakayekaimu nafasi ya ukurugenzi si mwingine bali Mhandisi wa Tume, Bruno James Mapunda. Kulitokea miguno ya chini chini baada ya jina hilo kutajwa hadi Matakwali, mtu ambaye wafanyakazi walikuwa wakimheshimu sana kulazimika kusimama na kuonya tabia hiyo kwamba haikubaliki na pia akaonya kwamba mtu anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu katika mazingira kama hayo.
Baada ya utulivu kurejea, Profesa Mwinchumu alimwelezea Bruno kama mkongwe pia kwenye Tume tangu inaanzishwa na kwamba ametoa mchango mkubwa katika kuifikisha mahala ilipo. Hata hivyo, alitumia nafasi hiyo kumtaka Bruno kuvaa viatu vya Matakwali kisawasawa kwani vikimpwaya bodi haitakaa hivi hivi.
Akamtaka awe mwadilifu, mtiifu na mnyoofu kwa wafanyakazi wenzake ili kuhakikisha tume inapiga hatua zaidi, ikiwezekana kuliko hata alizoita zama za Matakwali. Baadaye alimkaribisha Bruno kuzungumza na wafanyakazi wenzake na aliposimama tu miguno ikarudi tena hadi ‘Mzee’ aliposimama tena kuwatuliza.
Hali ilipotulia na Bruno alianza kuwaeleza wafanyakazi wenzake kwamba atajitahidi kuwa mwadilifu na kujali maslahi yao na ya kampuni na kuomba ushirikiano.
Hata hivyo, wakati akizungumza baadhi ya wafanyakazi walianza kutoka nje kama vile wanakwenda kujisaidia wakionekana kukerwa na hatua ya bodi kumpa madaraka hayo Bruno. Hadi Bruno anamaliza kuzungumza na wafanyakazi kama alivyoombwa takribani robo moja ya wafanyakazi walikuwa wametoka nje na wengi kuanzisha vikundi vya kushangaa uamuzi wa kumpitisha Bruno kukaimu nafasi hiyo kwenye korido.
Wengi waliendelea kujiuliza ni kwa nini Jackson ambaye awali uvumi ulionesha kwamba ndiye angeshika nafasi hiyo na kuonekana kuwakosha wafanyakazi wengi ameachwa. Hawakupata majibu.
* * *
Akiwa ameketi kwenye sakafu na watuhumiwa wenzake kadhaa katika kituo kikuu cha polisi, Jackson alijiuliza maswali mengi kuhusu kukamatwa kwake. Swali lililokuwa likimjia mara kwa mara ni namna polisi walivyopata habari zake kwamba anatuhumiwa kwa kosa hilo.
“Kwa nini hawa polisi wamekuja moja kwa moja kwangu? Kule Mkonge Hotel nilifanikiwa kuwakimbia lakini kumbe haikusaidia kitu. Kwa nini waseme wanakaribia kumkamata mtuhumiwa na mara wanakuja moja kwa moja kwangu?” Alijiuliza.
Alifikiria tena namna alivyofanikiwa kutoka kwenye ile nyumba ya wageni ya Twiga bila mtu kumtilia mashaka hadi chumbani kwa Andrew huku akiwa ameaga kurudisha chumba siku hiyo.
Akajiuliza ilikuwaje askari polisi wakajaribu kumsaka pale Mkonge Hotel. Je, kuna mtu aliwaambia yuko pale? Lakini akakumbuka kwamba mlinzi wa nyumba ile ya wageni alikuwa anajua kwamba yuko kwenye semina pale Mkonge Hotel na akakumbuka kumwambia kwamba semina yao ingelimalizika Ijumaa.
“Huyu anaweza kuwa sababu ya polisi kujaribu kunisaka Mkonge Hotel,” akajisemea. Lakini swali likabaki kwamba yule mlinzi wala mtu mwingine yeyote hakuna aliyekuwa anajua anafanya kazi wapi.
Akakumbuka kwamba hata kwenye kitabu cha wageni hakuandika ofisi yake zaidi ya jina lake, mahala anakotoka ambako ni Dar es Salaam, anakokwenda ambako ni Tanga na kisha akaandika kazi yake ambayo ni Mwanasheria. Hayo ndio maswali pakee yalikuwa yakiulizwa kwenye lile daftari kubwa la wageni.
Pale hakukuwa na kitu kama jina na ofisi anayofanya kazi. Sasa ni kwa nini polisi waje kumkamata moja kwa moja ofisini kwake? Alizidi kujiuliza. Aliamini kwamba mtu pekee aliyekuwa akijua undani wa tukio hilo ni Andrew. Je, inaweza ikawa ni yeye ndiye anayemsaliti kwa kuwasiliana na polisi? Kama ni yeye anafanya hivyo kwa maslahi gani? Pamoja na kutoamini haraka haraka kwamba Andrew anaweza kumsaliti, lakini hakuona mtu mwingine anayeweza kufanya hivyo zaidi yake. Sasa alianza kupata hisia kwamba huenda Andrew alimsaliti kwa kujua au kutojua.
“Isije ikawa alimwambia mtu akidhani ni siri lakini mtu huyo akaamua kunikaanga. Au anajifanya yuko upande wangu lakini kumbe anatumiwa na Bruno kunimaliza kwa sababu ya cheo,” aliendelea kujiuliza.
Lakini kwamba Andrew anaweza kushirikiana na Bruno ingawa hawakuwa na uhasama wa wazi wazi lilikuwa ni jambo ambalo pia lilikataa kuingia kwenye akili yake.
“Lakini siku ile pale klabu Bruno alipokuja kuungana na mimi alitokea kwenye meza yake na yeye akabaki pale hadi nilipokuwa ninaondoka. Je, walikuwa wamepanga nini? Tangu lini Bruno akawa karibu na Andrew au na mimi?”
Jackson aliendelea kujiuliza na kadiri alivyojiuliza ndipo alizidi kumtuhumu Andrew kuwa nyuma ya mpango mzima wa polisi kumkamata. Sasa alianza pia kujilaumu ni kwa nini alimwachia Andrew jukumu la kumtaarifu mkewe suala la kukamatwa kwake hasa kama atakuwa na ajenda ya siri.
Wakati bado akiwaza, alitolewa ndani ya selo kwamba alikuwa na wageni na kupelekwa selo nyingine ambayo ingeruhusu kuongea na wageni wake.Alihisi ni mwanasheria wake kaja, pengine akiwa na mtu mwingine kwani aliambiwa ana wageni na siyo mgeni. Alipofika akakuta waliokuwa wamekuja kumtembelea ni Mhandisi Ibrahim Matakwali akiwa ameandamana na Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Aboubakar Mwinchumu na makamu wake, Josiah Mafumu.
Kutokana na kesi aliyokuwa akituhumiwa nayo kuwa ya aibu alijikuta pia akihisi aibu kukabiliana na mabosi wake hao.“Malima, pole sana. Tumelazimika kuja baada ya kumaliza kikao na wafanyakazi kujua hasa kilichokusibu. Maneno tunayosikia ni kweli?” Aliuliza Profesa Mwinchumu.
Lilikuwa ni swali gumu kujibu. Je, alitakiwa kueleza ukweli kwamba alikuwa na msichana huyo chumbani lakini si yeye aliyemuua au kukana? “Kwa kweli sihusiki abadani,” hatimaye alijibu baada ya kufikiri kidogo na akawa anajiuliza kama swali likija lingine la kumtaka aeleze anachokijua yeye atajibu nini.
“Hata mimi ninaamini hivyo. Niliposikia tu hizi habari nikajua ni suala la mistaken identity. Kijana wangu ninayemjua hawezi kuua mtu, achilia mbali hata kuchukua baamedi kwenda naye chumbani,” alisema Mhandisi Matakwali.
“Ni kweli bosi… Lakini ninaamini ni suala la muda tu, ukweli utajulikana muda si mrefu. Sihusiki kabisa na hili jambo,” alisema huku akijipa matumaini.
“Kwani ilikuwaje hadi ukatuhumiwa na hili?” Akauliza Profesa Mwinchumu.
“Wala sielewi chochote. Ninadaiwa kuua mtu ambaye wala simfahamu,” alijibu Jackson.
“Kwa hiyo umejipangaje katika kushughulikia hii kesi?” Akauliza Matakwali.
“Nimeshawasiliana na mwanasheria wangu na ninamsubiri. Hata nilipoambiwa nina wageni nilidhani ni yeye.”
“Lakini usiwe na wasiwasi. Kwa sababu jambo hili limekupata ulipokuwa ukifanya kazi ya kuwakilisha kampuni, tulikuwa tunajadili na Mwenyekiti hapa wa Bodi kwamba ikiwezekana kampuni igharimie gharama za wakili. Mimi sina wasiwasi pia na hii kesi kwa sababu wewe mwenyewe ni mwanasheria,” alisema Matakwali.
“Nitashukuru sana kwa hilo bosi.”
“Usiendelee kuniita bosi. Hivi nimekuja kukuaga rasmi kwa sababu muda mfupi uliopita nimekabidhi ofisi kwa Mapunda. Kwa kifupi tukio hili limetuharibia sana mimi na mwenyekiti wangu hapa kwani ofisi tulidhamiria kukukabidhi wewe.”
“Mambo yote hupangwa na Mungu na hivyo Mwenyezi Mungu alipenda Bwana Mapunda ndiye awe Mkurugenzi wetu na mimi ninamtakia kila heri na kumwombea mazuri. Hata Waswahili wanasema kisicho riziki hakiliki.”
Profesa Mwinchumu aliingilia kati: “Lakini kuanzia sasa jiandae pia kwani tutaanza harakati za kumshawishi Waziri na hatimaye Rais kuhusu wewe. Jiandae hata kisaikolojia tu kuja kuwa Mkurugenzi mpya labda kama wawili hao (Rais na Waziri) watakuwa na mtu mwingine watakayeona anafaa zaidi. Lakini mimi kama Mwenyekiti mapendekezo yangu ni wewe.”
“Ninashukuru sana Mwenyekiti kwa kuweka imani yako kwangu. Ninakushukuru sana.”
“Tuna habari zako kwamba unafaa sana. Nikueleze tu kwamba hatua ya kumkabidhi ofisi Mapunda hata imewaudhi wafanyakazi wenziyo. Karibu wanizomee nilipotaja jina lake na Mhandisi hapa ndiye kaniokoa. Nitajitahidi sana mchakato wa kumpata mkurugenzi mpya wa tume ufanywe haraka. Lakini hili tafadhali ibaki kuwa siri yako na litategemea kadri kesi hii itakapomalizika mapema. Lakini kwa bahati mbaya hii ni kesi ya mauaji, inaweza kuchukua siku nyingi,” alisema Profesa Mwinchumu.
“Hamna taabu Mwenyekiti. Hili hutolisikia kwa mtu yeyote hata mke wangu. Binafsi ninaamini polisi wataniachia muda si mrefu baada ya kufanya uchunguzi wao. Nina hakika kuna mahala wamekosea,” alisema Jackson.
“Hata mimi ninaamini hivyo…” akasema Matakwali.
“Kama alivyokwambia Mkurugenzi… Bado mimi namwita hivyo, kesho nitamwagiza Bruno ashughulikie malipo ya wakili wako. Tutajadili zaidi namna ya kuliweka hili ili isije ikaonekana ni jambo binafsi. Tutajitahidi lionekane ni la tume pia,” alisema Mwenyekiti.
Kabla hawajaondoka, Wakili wake, Hussein Magabhanya aliwasili na hivyo wakamuaga kuondoka.
“Kabla ya kuja kwako tumeongea na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (MUM) ambaye ameniahidi kwamba utapatiwa huduma zote za msingi kisheria. Huyo MUM alikuwa mwanafunzi wangu wakati nafundisha sekondari kabla sijarudi shule kusoma,” alisema Profesa Mwinchumu ambaye mbali na kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TTM, ni mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wakati wanaanza kuondoka, MUM alifika eneo hilo na kumsalimia Jackson na kumpa pole. Akaagiza askari waliokuwepo kumwangalia mtuhumiwa huyo kwa jicho tofauti, jambo ambalo lilizidi kumpa faraja Jackson ambaye kabla ya hapo alikuwa katika hali kama ya kuchanganyikiwa.
Safari hii, Jackson hakupata upinzani mkali alipoomba kukaa faragha na wakili wake. Alimsimulia kila kitu kilichotokea na hivyo akataka kusikia ushauri wake kabla ya kuandika maelezo.
“Kabla sijakushauri, labda tuyapime haya mambo mawili. Kukubali kwamba ni kweli ulikuwa na huyu binti chumbani au kukana. Ukikana najua polisi watafanya gwaride la utambuzi na hawa wahudumu wa gesti ulimokuwa watakutambua na ukikubali itakuwa vigumu kuthibitisha kwamba huyu binti alikufa kwa ugonjwa kwa sababu kuna maelezo ya daktari kwamba alitiliwa sumu kwenye bia,” alisema Wakili.
Akaendelea: “Halikadhalika, kitendo cha kukubali kuwa na huyu binti chumbani, hatua ulizochukuwa za kutelekeza mwili wa marehemu na kunyofoa taarifa zako kwenye kitabu cha wageni zitaonesha kwamba ulikuwa na nia ovu. Hapo tuangalie linaloweza kutusaidia.”
“Binafsi natamani kusema ukweli tu kwamba nilikuwa naye. Siku zote huwa ninaamini kwamba ukweli humuacha mtu huru. Hata jambo hili ninaamini limekuwa gumu kwa sababu nilipindisha ukweli. Nadhani sikutakiwa kufanyia kazi ushauri wa Mambo.
Lakini tatizo linalonitisha ni hayo uliyoyasema kusababisha ugumu kama nitakubali, ingawa kubwa zaidi namhofia mke wangu. Ile hali tu ya kujua kwamba nilifikia hatua ya kuwa chumbani na msichana huyu itamwathiri sana kisaikolojia na kuondoa uaminifu wake kwangu.
Itakuwa mbaya zaidi kama hatoniamini kwamba sikuhusika abadani na kifo chake. Hilo linanisumbua sana. Hawezi kuniamini kwamba nilimwachia kitanda, nikalala kwenye kiti mithili ya mtu anayekaribisha mgeni aliyepotea njia usiku wa manane huku mvua ikinyesha. Niko tayari hata kufungwa lakini siyo mke wangu kuwa na mashaka na uaminifu wangu kwake kama ambavyo mimi namwamini kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo nishauri nifanyeje,” alisema huku akikumbuka pia kwamba wakati anamtaka Andrew kumjulisha mkewe kukamatwa kwake hakumzuia asimwambie sababu za kukamatwa kwake.
“Kama mkeo anakuamini ukimwambia ukweli kama ulivyoniambia atakuamini tu kama mimi nilivyokuamini. Hofu yangu bado ni vipi tutajinasua na nia ovu iliyokufanya ukimbie na kuondoa kitabuni details zako. Halafu kama daktari kasema marehemu alikufa kwa sumu tutakuwa na ushahidi gani wa kumpinga?”Alihoji wakili Hussein.
“Kwa hiyo unashaurije?”
“Mimi nashauri ukane halafu mahakamani tutajitahidi wasiweze kuthibitisha kesi yao kwa sababu wao watategemea zaidi ushahidi wa wahudumu ambao wewe utawakana. Huku ninaona njia ya kutokea katika hii kesi ni nyepesi kuliko upande ule mwingine.”
“Nikitakiwa kuthibitisha mahala ambako siku zote nilizokuwa kwenye semina Tanga nilikuwa ninalala, hapo nitafanyaje?”
Wakili Hussein Magabhanya alibaki kimya kwa muda kisha akasema:”Hapo pagumu kidogo lakini pia tunaweza tukapata mbinu. Kuna mteja wangu mmoja Tanga anamiliki nyumba za kulala wageni mbili au tatu. Ni mjanja mjanja hivi, pengine anaweza kutusaidia. Katika hili tutamwomba ionekane kwamba ulilala muda wote kwenye moja ya gesti zake. Kufoji kitabu kikiwa na jina lako sidhani kama itakuwa shida kwake alimradi tumhakikishie malipo kwa ajili hiyo. Mimi nashauri tufanye hivyo. Wewe tumetoka mbali na kama hukumbuki ulichangia sana mimi kupata shahada yangu. Nitapigana kuhakikisha unatoka salama.”
Jackson ambaye moja ya vitu anavyochukia sana ni kusema au kuambiwa ni uongo alibaki kimya kwa muda. Wazo la wakili wake aliona limekaa vyema lakini tatizo ni kwamba ni suala la kusema uongo!
“Aisee Hussein, naogopa sana uongo. Unaweza kunisumbua zaidi.”
“Lakini katika hili uongo ndio utakaokuokoa Jackie… Halafu katika maelezo yako ulionesha unashangaa namna polisi walivyokujua na kukukamata, mimi sitaki kumung’unya maneno, huyu jamaa anayejua kila hatua yako atakuwa ni yeye anayekusaliti. Na kuanzia sasa nakushauri jitenge naye. Usimwambie chochote.”
“Bila shaka atakuwa ni yeye. Napata hisia hizo pia na kwamba alikuja kukaa na mimi muda ule ofisini kwangu ili polisi wakinikamata nisimshuku. Alikuwa ni mtu wangu wa karibu sana ambaye katu sikumtazamia anitendee haya kama kweli yeye ndiye anayenichoma.”
“Usiamini sana watu, pengine atakuwa na sababu zake za kufanya haya. Inatokea sana kwamba yule unayemwamini ndiye anayekusaliti.”
“Unajua nimeshawaza sana kiasi kwamba kichwa changu kimefikia ukomo na hivyo naomba ushauri wako. Unadhani mke wangu atakapokuja kuniona nimwambie nini? Kumbuka hata yeye, kama angekuwa mtu baki, angeweza kuwa wakili wangu pia na anaweza kukusaidia katika hili.”
“Kutokana na ulivyonieleza mwanzo nafikiri ungekana pia kwake kwamba huyu msichana hukuwa naye chumbani kwako na kama baadaye itabidi mimi wakili wako ndiye nitamwambia ukweli wa mambo,” alisema wakili huyo ambaye pia anamfahamu vyema Salome tangu wakiwa chuo.
Hatua ya Jackson kumtuhumu kwamba ndiye aliyemsaliti hadi kukamatwa ilimfanya usiku huo asipate usingizi mzuri. Kila mara alikuwa anakumbuka maneno makali ya Jackson dhidi yake na kujikuta akinyong’onyea.
Hata hivyo, alikuwa anajaribu kufikiria cha kufanya ili kurudisha imani yake kwa Jackson, mtu ambaye alikuwa akimheshimu sana.
Siyo tu kwa sababu ya urafiki wao uliokuwa ukijengeka siku hata siku bali kwa jinsi alivyokaa imara mithili ya ndugu wa karibu sana katika kuokoa ndoa yake.
Aliendelea kuamini kwamba mahala alikokuwa akilala Jackson kulikuwa na kamera za CCTV, vinginevyo Jackson asingekamatwa mapema kiasi kile.
Sasa alifikiria ikiwezekana aombe wiki moja ya dharura ya kutokuwa kazini itakayokatwa kwenye likizo yake ya mwaka, kisha atumie mwanya huo kusafiri kwenda Tanga kufanya uchunguzi wake binafsi.
Aliona ni muhimu afanye hivyo na ikiwezekana ajaribu kuhakikisha kile alichoambiwa na Jackson kwamba usiku ule wa kuamkia Ijumaa, alikuwa amemgomea msichana huyo kwenda chumbani kwake lakini akasema hana mahala pengine pa kulala usiku huo.
“Ndio, alisema msichana huyo alikuwa na mlinzi wakati anakuja chumbani kwake. Huyu nikimpata atanieleza ukweli wa kilichojiri na pengine huyu mlinzi au mtu wa mapokezi wanaweza kuwa ndio chanzo cha Malima kukamatwa. Bila shaka itanisaidia kujua pia namna ya kumwokoa Malima” Alijisemea.
Lakini alijiuliza ataanzia wapi kufanya upelelezi wake na wahudumu wa Twiga Executive Lodge? Je, watakuwa tayari kumpa ushirikiano? Atajitambulishaje? Aliendelea kujiuliza maswali lakini akaona ni lazima aende na kwamba mambo ya kufanya ili afanikiwe katika uchunguzi wake atajua huko huko.
Pamoja na Jackson kumtuhumu kwa usaliti na kumfukuza, aliamua Jumatano hiyo aende tena kumwona polisi ili kumweleza kwa viapo kwamba hajamsaliti. Aliamini Jackson alikuwa amechanganyikiwa baada ya kukamatwa na hivyo kuwa rahisi kumshuku yeyote. Alihisi pengine usiku huo, atakuwa amejifikiria upya, hasira akiziweka pembeni na kukubali kuzungumza naye.
Jackson anayemfahamu ni tofauti na huyu aliyegeuka kuwa mkali na asiyetaka hata kusikiliza hoja zake. Kwa kawaida Jackson ni mtu muungwana, mkarimu na anayefikiria sana kabla ya kutamka neno. Ni mtu wa subira ambaye kila jambo hulichunguza na kujihakikishia ukweli wake kabla ya kutoa uamuzi.
“Bila shaka mkewe, mama Hellen alikwenda jana kumwona. Ngoja nimpigie simu kusikia anasema nini halafu nitakwenda polisi,” alijisema akichukua simu yake ya mkononi ambayo baada ya kuingia ofisini aliibwaga mezani.
Alihisi pia mazungumzo yake na Salome yanaweza kumpa mwanga wowote kuhusu kadhia hiyo na pengine akawa kiunganishi cha kurejesha imani ya Jackson kwake.
Kimsingi, Andrew alishagundua kwamba asingemudu kufanya kazi vizuri siku hiyo bila kushughulikia kadhia ya Jackson sambamba na kutafuta jibu litakaloleta mwafaka baina yao.
Jana yake usiku alikuwa anataka kumsimulia mkewe kuhusu yaliyompata Jackson lakini akasita. Kwanza mkewe angepata hisia kwamba huenda yeye pia anapokuwa safari hutoka na wasichana wa baa. Lakini mkewe pia alikuwa si mtu wa kuchukulia mambo maanani na alikuwa na tabia ya umbea. Sakata hilo la Jackson, kama lingefika kwake, huenda lingekuwa limempa kitu cha kuchonga mdomo kwa mashoga zake mtaani!
Andrew alimpigia simu Salome kumuuliza namna alivyokutana na mumewe jana yake akitaka waungane kuona namna ya kumsaidia. Alishangaa kwa majibu makali ya mwanamke huyo akisema hana muda tena wa kuzungumzia habari ya mwanamume mzinifu, msaliti wa ndoa na mbaya zaidi muuaji.
“Shemeji, mbona umefika huko. Jackson hahusiki na hilo abadani. Ninakuhakikishia si msaliti wala muuaji…”
“Wanaume ni wale wale tu, baba yao mmoja na mama yao mmoja. Unachotaka kufanya ni kumlinda mwanaume mwenziyo kwa upuuzi wake. Uhalifu hauna rangi wala sura ya mtu.”
“Shemeji, kwani mumeo hakukueleza ukweli wa mambo? Kwa nini unamdhania mabaya?”
“Anieleze ukweli gani tena? Mimi sitaki kusikia habari zake kwa kweli shemeji.” Alisema na kukata simu.
Andrew alishikwa na butwaa. Alimpigia tena simu lakini mwanamke huyo ambaye Andrew alimjua kwamba ni mwanaharakati sana wa kupinga unyanyasaji wa kijinsia, hakupokea simu yake.
Kwa kuwa ni mwanamke huyo na mumewe waliokoa ndoa yake, aliona sasa ni zamu yake pia kuokoa ndoa ya wawili hao kwa sababu majibu ya Salome yalimwonesha picha mbaya. Alinyanyuka na kutoka nje akiwa anawaza kama alipaswa muda huo kwenda ofisini kwa Salome au kwenda polisi kuonana tena na Jackson.
Huku akiwa hajaamua aanzie wapi alitoka kwenda kumuaga bosi wake mpya, Bruno, akipanga kumweleza kwamba anakwenda polisi kumwona Jackson. Alitaka pia kuona namna bosi huyo mpya wa TTM anavyoguswa na suala la Jackson kukamatwa.
Wakati anaingia ofisini kwa Bruno ambaye alikuwa bado kwenye ofisi yake ya awali kama mhandisi mkuu wa tume, alisikia karani wake akimhadithia mfanyakazi mwingine wa kike kuhusu kukamatwa kwa Jackson.
Kwa vile walikuwa wamezama kwenye ‘mchapo’ wao, hawakujua kama kuna mtu kaingia mahala pale. Baada ya kugundua kuwa wanamsema Jackson akarudi nyuma kidogo kwa kunyata ili apate kuwasikiliza vizuri zaidi.
“Kwani dada hujaangalia gazeti la leo? Hili hapa, utaenda ukasome mwenyewe uthibitishe maneno niliyokutonya jana. Bosi (Bruno) anasema Jackson ataozea jela,” alisema Nancy Komba, katibu muhtasi wa Bruno aliyesemekana pia kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Bruno.
“Kwa hiyo ni kweli Jackson amekamatwa?” Aliuliza tena Neema Athuman, ambaye alikuwa karani mkuu wa Masijala na rafiki mkubwa wa Nancy.
“Kwani tangu jana umemwona hapa huyo baba mchungaji wenu? Wakati kikao cha Tume kinaendelea, bosi aliniambia niwapigie simu polisi, wakaja wakamkamata. Lakini shoga, hili usimwambie mtu. Chondechonde tafadhali usimwambia yeyote. Yaani ukifanya hivyo utakuwa umeniponza mwenzio.”
“Yaani siamini Nancy. Kwamba baba mchungaji anaweza kuchepuka na msichana wa baa na kisha kumuua kwa sumu, nashangaa sana. Niliwahi kusoma mahala, sikumbuki ni wapi, lakini alikuwepo mwanaume mmoja ambaye alikuwa akiwachukua wanawake wanaouza miili yao kama mteja na kuishia kuwaua. Alipokamatwa alisema anaudhika sana na uwepo wao na hivyo aliazimia kuwafuta kabisa kwenye uso wa dunia. Isije ikawa Baba Mchungaji naye alikuwa na mpango kama huo.”
“Huyu alikuwa mnafiki tu. Alikuwa anajifanya mtu wa Mungu kumbe hakuna lolote na ndio maana Mwenyezi Mungu akaamua kumuumbua…”
Kabla hawajaendelea, Nancy alihisi kuna mtu baada ya kunyanyua uso na kumwona Andrew ambaye alijifanya anasoma ujumbe kwenye simu.
“Vipi, bosi mpya yupo?” Aliuliza Andrew.
“Ndio,” alijibu akibabaika kwa hofu kama Andrew alikuwa amesikia mazungumzo yao ama la.
“Ngoja nimjulishe,” Nancy alimpigia simu Bruno kwamba Meneja Rasilimali Watu alikuwa pale akitaka kumwona. Bruno aliruhusu aingie.
“Karibu Mambo, unaendeleaje na shughuli zako?”
“Nzuri bosi. Hujahamia kwenye ofisi yako mpya?”
“Sijakabidhiwa rasmi. Nadhani itakuwa leo. Hata hivyo, nashukuru umekuja kwa sababu nitataka nibadilishiwe samani. Yale makochi pale yamezeeka, siyataki pamoja na viti vyote vya ofisi. Nitataka pia mapazia ya kisasa zaidi kuliko yaliyopo kwenye ofisi ya Mkurugenzi. Kwa hiyo utaandikia hilo kwa ofisa manunuzi haraka kadiri itakavyowezekana. Nitakwenda mwenyewe madukani kutafuta samani na mapazia ninayoyataka, sawa?”
“Itabidi uende madukani kwanza kujua bei na wakuandikie Proforma Invoice na kama gharama ya hivyo vitu ni kubwa itashindikana kwenye bajeti. Itabidi kusubiri bajeti ijayo… Lakini mbona samani zile hazijazeeka sana bosi, zina miaka miwili tu na ushei.”
“Tekeleza maagizo yangu, mimi ninajua mahala pesa zilipo. Anyway kesho nitaleta hiyo Proforma ya samani zote ninazotaka… Ehe ulikuwa unasemaje?”
“Nilikuja kukuaga kwamba kidogo ninatoka kwenda polisi kumwona Malima. Nadhani una taarifa kwamba alikamatwa jana akiwa hapa ofisini.”
“Ndio nina taarifa. Unataka kwenda kufanya nini wakati Jackson yuko katika mikono salama?”
“Nilitarajia utasema twende wote bosi ili kumpa faraja mwenzetu. Haiwezi kuleta picha nzuri mwenzetu yuko mahabusu sisi tusiende kumjulia hali na kumfariji.”
“Sihangaiki na muuaji.”
“Hapo unamhukumu, na hizi ni tuhuma tu. Tuambizane ukweli, wewe ulichepuka mara ngapi bosi tulipokuwa Tanga?”
“Mimi sijamwita mchepukaji, nimesema muuaji.”
“Hizi bado ni tuhuma tu. Tuna uthibitisho gani kwamba aliua?” Bruno alitoa gazeti na kumpa Andrew:“Soma hiyo. Kamnywesha sumu binti wa watu na kumuua bila huruma. Sijui kamkosea nini yarabi!”
“Ni tuhuma tu ambazo mimi sizimiani… Lakini huyu binti si ndiye mlikuwa mkinywa pamoja Ijumaa iliyopita na kisha Malima alikuacha naye pale mezani?”
“Heri angeondoka na mimi angelibaki salama lakini yeye alimpapatikia Malima, pengine alivutiwa na mustachi wake kumbe anakwenda kwenye mdomo wa mamba.”
“Kwani na wewe unaamini kwamba Malima alimuua kweli? Amuue kwa kisa gani?”
“Kama alikwenda kwake na kufia chumbani kwake, kisha ikagundulika kwamba alikufa kwa sumu, mimi ni nani nikatae maelezo ya daktari ambaye ametaja mpaka aina ya sumu ambayo Malima aliitumia kumuua huyu msichana? Hata mimi ninajiuliza sana kwa nini Malima akanyofoa roho ya binti wa watu bila huruma.”
“Je, kama huyu binti alidhamiria kujiua siku hiyo na huenda alikwenda tu kufia chumbani kwa baba mchungaji?”
“Hizo sasa unazosema ndizo dhana.”
“Na kama huyu binti alikufa kifo cha kawaida na daktari kakosea katika vipimo vyake!”
“Hiyo bado ni dhana tu Bw. Mambo.”
“Haya mkuu, mimi naenda kumwona.”
“Msalimie. Lakini nilitaka kukukumbusha kwamba huu ni utawala mpya, siku nyingine ukija usiseme nimekuja kukuaga, sema ninaomba ruhusa. Kama mlizoea kuaga tu na kujiondokea, basi hapa mnaomba ruhusa na ninaweza kuwaruhusu au kukataa lakini leo ninakuruhusu. Nenda.”
“Sawa bosi.”
* * *
Salome alikuwa ofisini kwa bosi wake, Dk Jumanne Marijani, akimwelezea sakata la mumewe na msichana wa Tanga Raha Club huku machozi yakimbubujika. Dk Marijani, licha ya kwamba alikuwa hajawahi kukutana na Jackson, lakini alionekana kutoamini moja kwa moja kwamba mtu wa aina ya Jackson anaweza kufanya kitu kama hicho, hususani suala la kuua.
“Hilo la kuchukua mwanamke baa na kwenda naye chumbani linawezekana. Hii nikwambie tu mama Malima ni tabia ya wanaume wengi lakini kuamua kumuua, hapo ndipo ninapata ukakasi kuamini,” alisema Dk Marijani.
“Kutojua sababu hakuondoi ukweli kwamba ndiye mtuhumiwa. Inawezekana, kama nilivyokwambia labda ndiye baba wa mtoto wa huyo binti wa watu.”
“Sasa kama ndiye baba wa mtoto, sababu ya kumuua ni nini? Bado haingii akilini.”
“Kimsingi, sisi hatujui sababu lakini kwa mujibu wa uchunguzi wa polisi, msichana alifia chumbani kwake. Ungeweza kusema kwamba huyo msichana alikufa ghafla kwa maradhi na matukio ya aina hiyo yapo lakini kwa mujibu wa taarifa zilizopo, alimtelekeza na kung’oa taarifa zake kwenye kitabu cha wageni. Huoni mume wangu alidhamiria kuua?”
“Lakini, hiyo kutekeleza mwili na kuondoa taarifa haimaanishi moja kwa moja kuua. Hata mimi nikiri kwamba nilishamsaliti mke wangu. Unadhani mwanamke niliyekuwa nachepuka naye angenifia ghafla gesti usiku ningefanyaje, ningemtelekeza tu na kukimbia!”
“Ukweli utakuja kujulikana mahakamani. Mimi ninaandaa barua za kuwaita waandishi wa habari ili kesho tuwajulishe kwamba taasisi hii itasaidiana na Serikali katika sakata hili ili kuhakikisha mhusika ananyongwa.”
“Mama Malima, utakuwa tayari kusimama dhidi ya mumeo?”
“Niko tayari kabisa, bosi. Mhalifu ni mhalifu tu hata akiwa mwanangu wa kuzaa akafanya ushenzi siwezi kumtetea.”
“Duh! Lakini hili linaacha maswali kidogo kutokana na aina ya mtuhumiwa.”
“Kwani wewe ulitaka mtuhumiwa awe wa aina gani bosi?” Kabla Dk Marijani hajaendeleza mjadala, mhudumu aligonga hodi na alipokaribishwa alisema kwamba mama Malima alikuwa na mgeni eneo la mapokezi aitwaye Andrew Mambo ambaye alikuwa anataka kumwona kwa haraka.
“Samahani, ameshasubiri muda na alitaka kuondoka. Nikaona nikujulishe pengine ana jambo la muhimu kwako.” Alisema yule mhudumu.
“Kamwambie tumeshaongea kwenye simu inatosha.” Alijibu Salome.
“Huyo mgeni ni nani. Kama mmeongea kwenye simu bado akaona kuna haja ya kukuona kwa nini usimsikilize?” Alihoji Dk Marijani ambaye alikuwa anahimiza sana kila mwenye hitaji katika taasisi yao kuhakikisha anasikilizwa.
“Anafanya kazi na mume wangu na wote walikuwa huko Tanga. Ninaona amekuja tu kumkingia kifua mzinifu mwenziye.”
“Hapana, msikilize.” Alihimiza Dk Marijani akimwita mhudumu ambaye alikuwa ameshatoka nje lakini akiwa hajafika mbali. “Kamwambie huyo mgeni aje hapa ofisini kwangu.”
“Sawa bosi,” aliitikia mhudumu na kutoka nje.
Dakika chache baadaye Andrew aliingia ofisini kwa Dk Marijani ambaye alimkaribisha na kuketi katika moja ya viti katika ofisi hiyo finyu kidogo kulinganisha na ya kwake.
“Karibu ndugu, naitwa Dk Marijani. Mkurugenzi wa taasisi hii ya Mwanamke Lulu ambayo kimsingi ni mtandao wa kupambana na ukatili wa kijinsia nchini.”
“Naitwa Andrew Mambo… Mwanamke Lulu, kwa hiyo mwanaume ni nini? Takataka?”
“Hilo ni jina tu la usajili Bw. Mambo, kimsingi linalotakiwa kuzingatiwa ni shughuli zetu kwa mujibu wa katiba yetu. Tunaangalia haki za wanaume, wanawake na watoto, hususani makundi ambayo tunaita ya pembezoni, the marginalized.”
“Nashukuru kukufahamu Dk Marijani. Mimi ninafanya kazi ofisi moja na mume wa mama Malima pale Tume ya Teknolojia na Mawasiliano.”
“Vizuri, karibu sana Bw. Mambo. Nilikuwa ninaelezwa hapa kwamba huyo mfanyakazi mwenziyo kakamatwa na tuhuma nzito. Na nimesikia mlikuwa naye huko Tanga, labda unaweza kutuelezea kama kuna ukweli wowote unaoujua kuhusu kadhia hii?”
Ingawa alitamani ukweli huo autoe kwa Salome peke yake, lakini aliona autoe tu kwa wawili hao pengine ikamsaidia mwanamke huyo kubadili mawazo mabaya aliyokuwa nayo juu ya mumewe.
Mazungumzo yake na Salome asubuhi hiyo yalikuwa yamemshitua sana akapata hisia kwamba mwanamke huyo anaamini kinachoandikwa kwenye magazeti.
Huku akikumbuka namna Salome aliyekuwa pembeni mwake hapo na mumewe walivyohangaikia ndoa yake, aliona pengine kwa kumweleza ukweli halisi wa kilichotokea inaweza kusaidia.
Alianza kueleza kilichotokea kwenye klabu ya Tanga Raha hadi Jackson alipoondoka kwenda kulala akimwacha binti hiyo akiendelea na kazi na huku akiwa na mfanyakazi mwenzao, Bruno Mapunda.
Akaeleza namna Eggy alipokwenda alikofikia Jackson, lakini mwanamume huyo akamsihi binti huyo aondoke lakini akalazimisha kutaka msaada wa kulala kwa kuwa hakuwa na mahala pengine pa kwenda usiku huo.
“Ninasikia kulikuwa na ngurumo za mvua, kwa hiyo Jackson akaingiwa na huruma ndio maana akaamua kumruhusu kwenda chumbani kwake,” aliamua kusema sentensi hiyo akiongozea suala la mvua ili kuweka uzito. Akaendelea:
“Malima alimwachia kitanda, yeye akaenda kulala kwenye kochi lakini Eggy akaugua ghafla na kufariki dunia. Kama kweli alikufa kwa sumu basi huenda alikuwa keshainywa au kunyweshwa kabla ya kwenda chumbani kwa Malima. Lakini mimi siamini sana hizo habari za sumu na badala yake naamini alikufa kifo cha kawaida.
Kuna vifo vingi ambavyo watu hufa ghafla na hata kuna mmoja kafa ghafla juzi pale mtaani kwangu. Alikuwa dukani akinunua mahitaji mara akajisikia vibaya na kuomba msaada. Wakati wanahangaika kumkimbiza hospitali akakata roho,” alisimulia Andrew.
Wakati wakitafakari maelezo yake, Andrew akazidi kuendelea:“Ninazidi kusisitiza kwamba yule binti alikufa kwa ugonjwa tu na hili suala la sumu pengine polisi wamechomekea tu kama ambavyo huwa inatokea katika baadhi ya matukio kuwabambika watu kesi.”
Andrew akazidi kueleza namna Jackson alivyompigia simu usiku huo huku akitaka kuwaita polisi lakini yeye ndiye akamshauri kuutelekeza ule mwili, kunyofoa taarifa zake kwenye kitabu cha wageni na ilipofika asubuhi Jackson akaondoka hotelini kwake na akaenda chumbani kwake yeye Andrew.
“Ninaapa haki ya Mungu tulibishana sana na Bwana Malima kuhusu suala la kutowataarifu polisi na yeye kuondoka bila kumwambia mtu yeyote kilichotokea chumbani mwake. Hata hatua ya kunyofoa taarifa zake kwenye kitabu cha wageni nilimshauri mimi. Kama ningelijua haya yangetokea, ningerekodi mazungumzo yangu na yeye kwenye simu.
Narudia tena, yeye hakutaka kabisa na pengine ndio maana amenikasirikia sana ingawa pia anatuhumu kwamba huenda mimi ndiye nimewataarifu polisi hadi yeye kukamatwa kwa sababu mimi na yeye ndiye tulikuwa tunayajua haya, jambo ambalo siwezi kuthubutu kufanya abadani,” alisema Andrew.
“Mimi kwa upande wangu, kama nilikuwa na mashaka kama mume wangu anahusika na kifo cha huyu binti ndio umeyaondoa kabisa,” alisema Salome. Akaendelea kusema huku Andrew na Dk Marijani wamemtumbulia macho:
“Kwanza umekiri kwamba huyu binti aliingia chumbani kwa baba Hellen. Suala kwamba alilazimisha mwenyewe kwenda kwake, sijui vikapanda vikashuka, huna uhakika navyo bali mume wangu alikueleza tu ili umwone kama mtu mwema. Halafu suala la huyu binti kufa kwa sumu hawajasema polisi, bali kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari waliogundua sababu ya kifo kuwa ni sumu ni madaktari.” Kama kawaida, Salome alikuwa akizungumza huku akifuta machozi na macho yake kuzidi kuwa mekundu.
“Ndugu zangu, tangu nimemjua Bwana Malima, takribani miaka kumi sasa, sijawahi kusikia anasema uongo. Kama kuna watu wakweli duniani basi ni huyu bwana na ndio maana usiku ule nilifanya kazi sana kumshauri asiwashirikishe polisi na hivyo kuficha ukweli wa jambo hili. Nilijua kadhia hii itaisha tu… Niseme tu kwamba mimi ninamwamini Bw. Malima kwa kusema ukweli kwa asilimia mia moja. Nimaamini hata wewe mkewe ambaye umeishi naye kwa miaka mingi unalijua hilo pia.”
“Shemeji, kuna mambo ya kuamini na kutilia shaka,” alidakia Salome.“Kwa mfano, ni kwa nini huyu msichana akamfuata hadi chumbani kama walikuwa hawajakubaliana? Yaani mtu anamfuata mtu hivi hivi tu? Alijuaje kwamba yuko hapo kwenye hiyo gesti kama hakukuwa na mawasiliano?” Alizidi kuhoji Salome.
“Ninachofahamu ni kwamba, kwa sababu ya kula pale klabu kila siku usiku, huyu msichana alitokea tu kumzoea na nadhani Malima alimtajia alikofikia kwa nia njema tu au kwa ajili ya kuwa anampigia simu kumwandalia chakula kwa sababu ile klabu unaweza kusubiri muda mrefu chakula.
Kingine ninachojua ni kwamba aliyekuwa akimtaka huyu mwanamke ni Mapunda ambaye ndiye ana tabia hiyo lakini huyu msichana alikuwa hamtaki na Mapunda aliendelea kuwa naye akimnunulia bia hadi baa ilipofungwa kwa sababu hata mimi nilikuwepo,” alijibu Andrew.
“Hayo ni maneno tu. Naona umepania sana kumsafisha mwenzako katika hii kadhia. Yaani unayosema wala hayaniingii akilini. Kikubwa yameniongezea uhakika kwamba baba Hellen ndiye mhusika wa mauaji… Mkuu, mimi ninaendelea na taratibu za kuongea na waandishi wa habari kesho,” alisema Salome akimgeukia bosi wake, Dk Marijani.
“Hapana mama Malima. Ngoja kwanza tufanyie kazi maneno ya Bw. Mambo. Mimi kama yananiingia akilini kidogo. Natamani nikajaribu kuongea na Bw. Malima kwanza nimsikie. Mimi nina kipaji cha kuzaliwa kwamba mtu anayeongea ukweli huwa ninamjua. Kwa mfano huyu brother hapa anaongea ukweli kabisa kadiri ya anavyoelewa sakata zima. Nilitamani hata mimi kumsikia huyu mheshimiwa (Jackson),” alisema Dk. Marijani.
“Yaani naona hii ni kesi ya wizi wa mahindi inayomkabili nyani ambayo sasa ngedere mmoja anaileta kwa ngedere mwenziye. Wanaume ni wale wale kumbe na ndio maana itachukua miongo mingi kuondoa mfumo dume katika nchi yetu. Yaani mnaamua kutetea uovu?” Alihoji Salome akionekana ameghadhabika na kusimama akijiandaa kutoka nje ya ofisi ya bosi wake.
“Mama Malima, kaa kwanza. Hasira za nini? Mtazamo wako kwamba hata mimi namtetea mumeo kwa kuwa ni mwanaume mwenzangu nadhani si sahihi,” Dk Marijani alikiambia kisogo chake kwani alishapiga hatua na kuondoka ofisini hapo.
“Bw. Mambo, huyu mama Malima ni mwanaharakati kweli kweli. Ni wanawake wachache wanaweza kuwa tayari kumwangamiza baba wa watoto wake hata kama kweli kafanya hivyo. Mimi from the beginning alivyomtaja mumewe na kunisimulia alichoambiwa na polisi nilikuwa nina doubt kuhusu uhusika wa mumewe,” alisema Dk Marijani.
“Mimi mwenyewe ninamshangaa sana shemeji yangu. Ingawa sikuwemo chumbani kwake, mimi nina uhakika kwamba Bw. Malima hakumuua huyu binti kwa sababu hakukuwa na sababu yoyote ya kufanya hivyo.”
“Lakini, kwa jinsi ulivyosimulia, isingekuwa rahisi kwa polisi kumfahamu haraka namna hii. Ingeweza hata kuchukua muda mrefu kidogo na wewe umesema hata Bw. Malima pia anakutuhumu. Unadhani kwa nini imekuwa hivi?”
“Hili, hata mimi limenisumbua sana na pia ndilo limemsumbua Bw. Malima mwenyewe kiasi cha kumfanya anituhumu mimi kwamba huenda nimemsaliti. Lakini mimi ninahisi kwamba Malima amekamatwa mapema kutokana na sababu mbili: Mosi, inawezekana pale kwenye hoteli kuna kamera za CCTV na hivyo alionekana na ikawa rahisi kumtafuta. Lakini sasa kwa asilimia nyingi nahisi mtu mmoja anaitwa Bruno Mapunda ndiye kasuka mpango mzima wa kukamatwa kwake lakini sijui alijuaje kuhusu kadhia nzima,” alisema Andrew na kusimulia kwa kifupi jinsi Bruno alivyokuwa akiwania nafasi ya kukaimu ukurugenzi huku kikwazo kikiwa ni Bw. Malima.
“Unataka kusema huyu Mapunda anaweza akawa ndiye kamuua huyu binti kwa sumu akiwa chumbani kwa Bw. Malima?”
“Hapo ndipo kuna kitendawili. Nilichogundua ni kwamba Mapunda ndiye aliwaita polisi kama nilivyosikia karani wake akisema? Kama polisi walikuwa hawajamjulisha kabla kuhusu kumtafuta Jackson na yeye kuwahakikishia kwamba yupo ofisini muda ule, ninajikuta nikimtilia sana shaka.”
“Kwani kama polisi wangekuwa wanatafuta mtumishi katika Tume yenu ili kumkamata, unadhani yeye ndiye mtu wa kujulishwa?”
“Inawezekana kwa sababu wakati Jackson anakamatwa, kulikuwa na kikao cha bodi kinaendelea na bosi aliyepaswa kujulishwa alikuwa kikaoni na mara nyingi Mapunda alionekana kama mtu wa pili kwenye tume baada ya bosi Matakwali ambaye amestaafu. Lakini mtu sahihi kujulishwa na polisi nilikuwa mimi ambaye ndiye meneja rasilimali watu wa tume lakini sikuwa na habari.”
“Je, haiwezekani kwamba Mapunda alitumia taarifa za gazeti kuwasiliana na polisi?”
“Hilo nalo linawezekana na ndio maana nikasema huenda pale kulikuwa na kamera za CCTV. Lakini pamoja na hayo, Mapunda alijuaje kuwa anayetuhumiwa kwenye gazeti ni Bw Malima? Jina la Malima limetajwa leo kwenye vyombo vya habari na kama ni watu tuliokuwa kwenye semina kutokea Dar es Salaam tulikuwa zaidi ya 10. Kwa nini nisituhumiwe mimi au mwingine?”
“Hapo kweli kunahitajika uchunguzi makini. Bila shaka kuna haja ya kumchunguza huyu Mapunda Lakini natamani kwanza nikaongee na Bw. Malima.”
“Mimi ndiko ninakoelekea polisi. Jana alinikasirikia hadi akanifukuza kuongea naye kutokana na kunituhumu kwamba mimi ndiye nimemsaliti. Na kweli katika mazingira yalivyo wala simlaumu sana ingawa ninaweza kumlaumu kwa kukataa kunisikiliza,” alisema Andrew.
“Kama una muda kama wa dakika tano hivi ninaomba unisubiri hapo nje nipange mambo yangu hapa kisha twende sote,” alisema Dk Marijani.
“Haya ninakusubiri,” alisema Andrew akisimama na kutoka nje ya ofisi ya Dk Marijani.