Uhuru wa Wahusika

Unapoumba wahusika wa hadithi yako usisahau jambo hili muhimu, waache huru wahusika wako usiwafanye kuwa wafungwa au watumwa wako. Athari za mwandishi zinapaswa kuwa za wastani kwa wahusika wake, usiwavike wahusika wako wote mambo yanayofanana kana kwamba ni wa kufu moja.
 
Waache huru wahusika wako kwa kutowafungamanisha na;
 
a) Athari za kilahaja
Matumizi ya lugha hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine, kama kazi yako imejikita katika muktadha wenye watu kutoka jamii mbalimbali, ni vyema kutokuwafanya wahusika wako kuwa wafungwa au watumwa wa lahaja yako, iwe ni kimvita, kiunguja au kiamu.
 
Kazi ihusuyo watu kutoka jamii mbalimbali iwe na vionjo walau kidogo kutoka katika jamii mbalimbali.
 
b) Dini
Usiwafanye wahusika wako kuwa watakatifu kuzidi utakatifu wenyewe, mtume Mussa (Mosses) alikuwa ni mtume wa Mwenyezi Mungu ila aliua kwa bahati mbaya, usiwafanye wahusika wako kuwa watumwa wa imani yako hadi ukapitiliza kwenye uhalisia wenyewe.
 
Hata mitume wa Mwenyezi Mungu walifanya makosa sikwambii kwa wahusika wa bunilizi yako. Wahusika wa kazi yako ni muhimu wafanye makosa, iwe kwa bahati mbaya au makusudi. 
 
c) Umri
Waache huru wahusika wako wafanye au wanene kulingana na umri wao. Mtoto mdogo mwache afanye vitendo vya kitoto, hata kama mtoto huyo awe ni mtoto wa rais, mwache ajisaidie kitandani.
 
d) Ujuzi wako wa lugha
Usiwafanye wahusika wako wote wakawa watumwa wa ujuzi wako wa lugha kama vile ujuzi wa misemo, nahau na mafumbo, ujuzi wa lugha ya Kiingereza n.k. 
 
Chagua wahusika wachache wabebeshe ladha hiyo ya mafumbo au lugha ya kigeni, wahusika wako wengine waache huru.
 
e) Waache huru na kabila lako.
Kama kitabu chako hakihusu jamii moja, usiwafungamanishe wahusika wako na majina ya watu kutoka kabila lako iwe wewe ni Mhaya,  Mmatengo au Mnyamwezi wa soko mjinga.
 
Kumbuka:
Kabla ya kuwafanya wahusika wako kuwa wafungwa, fikiri mara tatu kama kuna ulazima wa kufanya hivyo.
 
Kalunga Matovolwa,
Dar es Salaam,
03.01.2020